Sehemu ya Kwanza

Abubakar As Siddique  (Radhiya Llaahu ‘anhu)
Khalifa wa kwanza aliyeongoka

Akiutafuta ukweli


Kabla ya kuja kwa Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hapakuwa na wanaomuabudu Allah isipokuwa watu wachache sana wakiwemo wafuatao;
Qussa ibn Saaida,
Zaid ibn Amr,
Waraqa Ibn Noufel (aliyekuwa akifuata dini ya Kimasihi)
na Abi Qays ibn Anas.
Hawa walikuwa wakisema wazi wazi kuwa wao wanamuabudu Mungu wa kweli Mola wa Ibrahim (Alayhis salaam).
Makureshi hawakuwadhuru watu hao kwa sababu hawakuwa wakiitukana miungu yao, na pia kwa sababu walikuwa na wafuasi wachache sana waliokuwa wakiwaendea na kuwasikiliza.

Alikuwa akihudhuria vikao vyao na kuwasikiliza wakizungumza juu ya Mungu wa kweli aliyekuwa akiabudiwa na Ibrahim na Ismail (Alayhis salaam), na juu ya Mtume ambaye wakati wa kuja kwake umekwishawadia, na kwamba Mtume huyu ndiye atakayewarudisha watu katika ibada ya Mungu mmoja wa kweli.
Vikao hivyo ndivyo vilivyomsaidia Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuiona nuru ya Utume kwa haraka, akawa anajitayarisha na kuisubiri.

Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mfanya biashara marufu sana mwenye kujulikana kwa uaminifu wake hapo Makkah, heshima yake ilikuwa kubwa sana baina ya Makureshi, na alikuwa mtu mwenye elimu kubwa ya kuhifadhi nasaba za makabila na mataifa ya kiarabu, na kwa ajili hiyo alipewa yeye jukumu la kushughulikia mambo ya fidia panapotokea matatizo hayo baina ya makabila..

Safari ya Sham

Aliposafiri kwenda Sham (Syria) akifuatana na wafanya biashara wenzake, Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyakuta yale yale yaliyoko Makkah.
Watu na akili zao, mashujaa, wafasihi wa lugha, washairi wakubwa, walikuwa wakiyaporomokea masanamu na kuyasujudia. Na hali hii ndiyo ilivyokuwa Bara ya Arabuni kote.
Na huko Sham pia walikuwepo wachache waliokuwa wakizungumza juu ya dini ya Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) na juu ya kumuabudu Mungu wa kweli asiye na mshirika.

Akiwaendea na kusikiliza maneno ya Imani

Walikuwepo wengine waliokuwa wakisoma Taurati na Injili mfano wa Waraka bin Noufel kule Makkah. Hawa walikuwa wakizungumza juu ya dini mpya ambayo muda wake umeshakaribia na juu ya Mtume mpya ambaye wakati wa kuja kwake umeshawadia, na kwamba Mtume huyo atatokea katika nchi ambayo Nabii Ibrahim aliijenga Al Kaaba.
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa anawaza;
Ni kweli Mtume atatokea katika nchi ile iliyojaa watu wanaoabudu masanamu, walevi, wacheza kamari na wauwaji wa watoto wachanga wa kike? Hivyo Kweli anaweza akatokea mtume mahali kama pale penye watu wenye tabia ovu kama zile? 
Alikuwa akijiuliza hivyo nafsini mwake kisha akijijibu mwenywe;
Na kwa nini asitokee Mtume wakati daktari haitwi mpaka pawepo na mgonjwa?
Isitoshe, watu wa Makkah juu ya kuwa na mabaya yote hayo, lakini walikuwa na sifa nyingi njema.
Walikuwa maarufu kuwa ni wasema kweli, na uwongo kwao ulikuwa ni aibu kubwa sana. Ukarimu ulikuwa ni moja ya sifa zao, walikuwa wakiwaambia watumwa wao;
"Atakayeweza kuniletea wageni wengi nitampa uhuru wake".
Watu wenye tabia kama hizi kwa nini asitokee Mtume miongoni mwao?"
Akawa anaikumbuka siku ile Qussa bin Saaida alipoingia ndani ya msikiti wa Al Kaaba bila ya kuwaogopa washrikina huku akisema;
"Labayka Mola wa kweli, Labayka Mola wa kweli, najikinga kwa yule aliyejikinga kwake Ibrahim".
Yote haya yaliyokuwa yakimpitikia akilini mwake alipokuwa huko Sham yaliujaza moyo wake shauku kubwa ya kumsubiri Mtume huyu mpya atakayeujaza ulimwengu Nuru ya dini ya Haki na kuwaondolea Makureshi na watu wote balaa hili la kuwasujudia masanamu.

Ikiwa yeye amesema hivyo basi mimi namsadiki


Siku zikapita kwa haraka sana, na safari ya kurudi Makkah ikawadia, na usiku kabla ya safari yake, Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliota ndoto ya ajabu sana. Aliota kuwa mwezi umepasuka na vipande vya nuru yake vimeanguka, vikapukutika na kuingia ndani ya kila nyumba ya Makkah.
Asubuhi yake akawaendea wale wacha Mungu aliokuwa akihudhuria darsi zao na kuwauliza juu ya tafsiri ya ndoto yake hiyo, na wote wakamwambia kuwa inaleta bishara njema.
Safari ikaiva. Ngamia wakaanza kuondoka kuelekea Makkah, na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akiielezea safari hiyo alisema:
"Ngamia siku hiyo walikuwa wakitoa sauti za furaha kama kwamba  wanasherehekea sikukuu."
Mara baada ya kuwasili Makkah, wafanya biashara na wanunuzi wa kawaida wakawa wanausogelea msafara huo kwa ajili ya kununua bidhaa zitokazo nchi ya Sham. Wengine walikuwa wakipatana na wengine wakizungumza, wote walikuwa wakipaza sauti zao, na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwasikia baadhi yao wakizungumza juu ya Mtume mpya aliyedhihiri hapo Makka na namna anavyodai kuwa anapata habari za mbinguni.
Alipounyanyua uso wake akamuona Abu Jahal (Amr ibn Hisham) akimsogelea na kumvamia kwa masuali:
"Umesikia juu ya rafiki yako Muhammad ewe Atiq?" (Atiq lilikuwa jina la kubandikwa la Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Abubakar  : "Amepatwa na jambo gani?"
Abu Jahal : "Muhammad anadai kwamba eti yeye ni Mtume na kwamba eti anapata habari kutoka mbinguni" .
Abubakar :  "Nani anayemletea habari hizo?"
Abu Jahal : "Anasema eti Malaika aitwaye Jibril."
Abubakar :  "Yeye mwenyewe amesema hivyo?"
Abu Jahal : "Ndiyo! nimemsikia kwa sikio langu."
Abubakar : "Ikiwa yeye mwenyewe ametamka hivyo basi mimi namsadiki."
Abu Jahal hakuweza kustahamili msituko huo na miguu yake ikaaanza kutetemeka, akakaa chini.
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaona bora kwanza aende nyumbani akawaone watu wake na kuitua mizigo yake, kisha ende nyumbani kwa sahibu yake Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kumsikiliza.

Mkweli mwaminifu


Alipokuwa akielekea nyumbani, Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa anaikumbuka siku ilee jiwe jeusi lilipoanguka kutoka mahali pake baada ya kunyesha mvua kali, dhoruba na upepo na mafuriko makubwa, na sehemu kubwa ya msikiti kubomoka.
Makureshi walikubaliana kuujenga upya msikiti huo, lakini mgogoro mkubwa ukazuka wakati wa kulirudisha jiwe jeusi mahali pake, kwani kila kabila lilitaka heshima ya kulirudisha jiwe hilo.
Akawa anakumbuka namna Makureshi walivyokuwa tayari kupigana, pata shika panga mkononi, na mgogoro huo uliendelea muda wa siku tano bila kupatikana suluhisho, mpaka pale aliposimama Aba Umayya Ibn Al Mughira Al Makhzumy na kutoa shauri lake maarufu aliposema;
"Wa mwanzo kuingia msikitini kupitia mlango huu ndiye atakayehukumu baina yetu". 
Makureshi wote kwa pamoja wakalikubali shauri hilo.

Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa anakumbuka namna gani Makureshi walivyokaa kimya siku ile wakingoja na kusubiri kwa hamu kubwa nani atakayeingia mwanzo kupitia mlango ule atakayeweza kutoa hukumu itakayowatoa katika janga hilo la kuuwana na kumwaga damu.
Ghafla! Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akatokeza baada ya kuingia kupitia mlango huo, na Makureshi wote kwa pamoja wakapiga ukelele wa furaha huku wakisema;
"Al-Saadiq Al-Amiin" (Msema kweli Mwaminifu),  Sote tuko radhi juu ya uamuzi atakautoa Mkweli Muaminifu".

Akawa anaikumbuka miaka 40 alioishi naye akiwa sahibu yake mpenzi, Msema kweli, asiyepata kumsikia hata siku moja akitamka neno la uongo. Hata katika mzaha alikuwa akisema kweli tupu. Kisha akawa anajisemesha nafsini mwake;
"Leo mtu huyu aje aseme uongo, tena juu ya Mwenyezi Mungu? La, haiwezekani kabisa.
Wakati vijana wenzake walipokuwa wakenda ngomani na kuhudhuria sherehe mbali mbali, Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwa akijishughulisha na mambo hayo, bali alikuwa akisema kuwa yeye hakuumbwa kwa ajili ya mchezo".

Anazitamka shahada mbili


Yote haya yalikuwa yakimpitia Abubakar akilini mwake huku akielekea nyumbani kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) baada ya kutua mizigo yake, na baada ya kusalimiana na watu wake.
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposikia mlango unagongwa akamtaka mkewe Bibi Khadija (Radhiya Llaahu ‘anha) akatizame nani aliye mlangoni.
Bibi Khadija (Radhiya Llaahu ‘anha) akasema; "Abubakar huyo"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):  "Mfungulie".
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaingia, na baada ya kusalimiana akaanza kuuliza;
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu):   "Ni kweli wanayosema juu yako?"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):  "Wanasema nini?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu):   "Wanasema kuwa wewe unasema umepata Utume na kwamba unapata habari kutoka mbinguni."
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam): "Na wewe uliwajibu nini?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu):   "Niliwaambia; Ikiwa kweli umesema hivyo basi mimi nasadiki."
Furaha ilimjaa Bwana Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na machozi kumlengalenga. Akamkumbatia Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kukibusu kipaji cha uso wake, kisha akakaa na kuanza kumhadithia namna alivyojiwa na Jibrili katika Pango la Hiraa na jinsi alivyobanwa na Malaika huyo na kumtaka asome aya tano za mwanzo za Suratul Alaq:
"Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Aliyemuumba mwanadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako mkarimu sana. Ambaye amemfundisha (binadamu ilimu zote hizi kwa msaada) wa kalamu. Amemfundisha mwanadamu (chungu ya) mambo ambayo alikuwa hayajuwi ."
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa akiyasikiliza yote hayo kwa utulivu mkubwa, akatizama chini kwa khushuu, kisha akatamka;
"Ash- hadu al laa ilaha Illa Allah wa ash- hadu annaka rasulu llah".
(Nashuhudia kuwa hapana Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah, na nashuhudia kuwa wewe ni mjumbe wa Allah).
Hivi ndivyo alivyosilimu Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu).

Anaanza kazi ya kuwasilimisha watu


Siku ya pili yake Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwasilimisha watano katika mabwana wa kabila la Kikureshi, nao ni Othman bin Affan, Al Zubeir bin Awam, Abdurahman bin Auf, Saad bin Abi Waqas na Talha bin Ubaidullah; akaja nao mpaka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na wote hawa ni katika wale kumi waliokwisha bashiriwa Pepo .
Siku iliyofuata aliwasilimisha vigogo wengine wanne na kuja nao mbele ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), nao ni Uthman bin Madha-un, Abi Ubaidah Aamir bin Al Jarrah, Abi Salama na Al Arqam bin Abi Al Arqam.
Nguvu ya Uislamu ikaongezeka, na Abubakar aliitumia mali yake yote katika kuunusuru Uislam na pia nguvu zake na daraja lake mbele ya Makureshi, na vyote hivi vilisaidia sana katika kuujenga na kuuendeleza Uislamu, hata watu wakawa wanasema;
"Wasingeshikamana wawili hawa kama hivi, kwa jambo la upotovu" .

Nasaba yake


Jina lake ni Abdullah bin Othman bin Amer bin Amru bin Kaab bin Saad bin Tayim bin Murrah bin Kaab bi Luay Al Kurashiy Al Taymiy, na uhusiano wake na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) unakutana kwa Murrah bin Kaab, kwani jina la Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni Muhammad bin Abdillah bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdu Manaf  bin Qusay bin Kilab bin Murrah bin Kaab.
Jina la baba yake ni Othman, lakini alikuwa maarufu kwa jina la Abu Quhafah, kwa hivyo Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akijulikana kwa jina Ibni Abi Quhafah, yaani mwana wa Abu Quhafah.
Mama yake ni Ummu l Khayr – Salma binti Sakhar bin Amer bin Kaab bin Saad bin Tayim bin Murrah bin Kaab na alikuwa binti ammi yake Abu Quhafah.

Watu wote wa nyumba yake walisilimu


Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni sahaba wa pekee ambaye watu wake wote kuanzia wazee wake na jamii yake yote pamoja na watoto wake waliingia katika Uislamu..

Wakeze na wanawe


Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alioa wake wanne;
Wakati wa ujahilia (kabla ya kuja kwa Uislamu) alimuoa Qutailah binti Saad na akazaa naye Abdullah na Asmaa (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Abdullahi aliingia katika Uislamu tokea siku za mwanzo na alifariki wakati wa ukhalifa wa baba yake.
Asmaa (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni maarufu kwa jina la 'Dhaat nitwaqayn', na alipewa jina hilo baada ya kukata 'Nitaaq' mkanda wa kitambaa kinachofungiwa nguo kiunoni na kukifunika chombo kilichotiwa chakula alichokuwa akipelekewa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) walipokuwa pangoni wakati wa kuhajir kwenda Madina, na alikuwa mkubwa kwa umri kuliko Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha).
Aliolewa na Al Zubeir (Radhiya Llaahu ‘anhu) walipokuwa Makkah na alizaa naye watoto wengi mpaka alipomuacha akawa anaishi kwa mwanawe Abdullah bin Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyeuliwa Makkah.
Bibi Asmaa (Radhiya Llaahu ‘anha) aliishi miaka mia, na mwisho wa maisha yake alikuwa kipofu.

Wakati wa ujahilia Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimuoa pia Umm Rumaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyezaa naye Abdul Rahman na Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) mke wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na alifariki dunia wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyeteremka kaburini kwake siku ya maziko na kumuombea maghfira.
Abdul Rahman alipigana vita vya Badr na vita vya Uhud akiwa upande wa makafiri, na kabla ya kuanza vita vya Badr aliita kwa sauti kubwa akitaka mtu yeyote upande wa Waislamu aje kupambana naye na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipotaka kutoka na kupambana na mwanawe huyo, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimzuwia na kumwambia;
"Tuache tukufaidi.".
Abdul Rahman alikuwa shujaa na mtupa mshale mwenye shabaha aliyesilimu baada ya mapatano ya Hudaibia (Sulhul Hudaibiah), akawa Muislamu mwema aliyepigana vita mbali mbali akiwa upande wa Waislamu, alishiriki katika vita vya Al Yamamah chini ya uongozi wa Khalid bin Waliyd (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakati majeshi ya Waislamu yalipopambana na majeshi ya Musailimah al Kadhaab (Mtume wa uongo), na yeye ndiye mkubwa wa watoto wa Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na alifariki dunia ghafla mahali panapoitwa Hibsh karibu na mji wa Makka katika mwaka wa 53 H.
Kitabu cha 'Abubakar al Siddiq – Muhammad Ridha
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimuoa pia Asmaa binti Umais (Radhiya Llaahu ‘anhu) baada ya kuuliwa kwa mumewe wa mwanzo Jaafar bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu), wakapata mtoto waliyempa jina la Muhammad bin Abubakar.
Abubakar alipofariki dunia, Asmaa aliolewa na Ali bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu) akazaa naye mtoto waliyempa jina la Al Qasem.

Wakati wa Uislamu Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimuoa pia Habibah binti Kharijah bin Zeid bin Abi Zuhair Al Khazraji wakapata mtoto waliyempa jina la Aishat Ummu Kulthum aliyeolewa na Talha bin Ubeidullah (Radhiya Llaahu ‘anhu).

Baadhi ya sifa alizopewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)


Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimpa Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) sifa nyingi sana, na zifuatazo ni baadhi chache sana ya sifa hizo;

HAKUSITA WALA HAKURUDI NYUMA
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisema;
"Mikono yote iliyotunyoshea tushailipa, isipokuwa wa Abubakar, msaada alioutowa ni Mwenyezi Mungu tu ndiye atakayemlipa".
"Wote niliowaita katika Uislamu walisita kwanza isipokuwa Abubakar, yeye hakusita wala kurudi nyuma, hapo hapo alisilimu."
Al-Hakim.

USIPONIKUTA MWENDEE ABUBAKAR
Mwanamke mmoja alimwendea Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa na shida fulani, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyekuwa na shughuli nyingi sana wakati ule akamwambia;
"Nenda urudi siku nyingine".
Yule bibi akamuuliza;
"Nisipokukuta je?"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia;
"Mwendee Abubakar'.
Bukhari

MILANGO YOTE ILIYOELEKEA MSIKITINI IFUNGWE ISIPOKUWA WA ABUBAKAR
Siku moja Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipanda juu ya membari na baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumpwekesha akasema;
"Mwenyezi Mungu alimshauri mja wake achaguwe iwapo anaitaka dunia au anataka yaliyo kwa Mola wake (anataka kwenda kwa Mola wake), na mja huyo akachagua yaliyo kwa Mola wake."
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliposikia maneno hayo akalia sana huku akisema;
" Kwa baba yangu na mama yangu nakufidia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu".
Masahaba waliohudhuria walishangazwa na kilio chake hicho wakawa wanasema;
'Vipi mtu huyu! Kipi kinachomliza wakati Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anatuhadithia juu ya mja aliyeshauriwa achague baina ya dunia na baina yaliyo kwa Mola wake na akachagua yaliyo kwa Mola wake?'
Hawakuwa wakijua kuwa aliyeshauriwa ni Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na kwamba alitakiwa achague baina ya kwenda kwa Mola wake au abaki nao duniani, na kwamba Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amechagua kwenda kwa Mola wake.
Ndipo Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema;
"Katika watu walonisaidia sana kwa hali na mali ni Abubakar, ingelikuwa naweza kumchagua Khalil (rafiki), basi angekuwa Abubakar, lakini ni undugu katika Uislamu na kupendana. Milango yote iliyoelekea msikitini ifungwe isipokuwa wa Abubakar".
Bukhari na Muslim

HIZI NI SIFA ZA WATU WA PEPONI
Siku moja Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliuliza;
"Yupi kati yenu asubuhi ya leo amefunga?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Mimi".
Kisha akauliza tena;
"Yupi katika yenu aliyehudhuria mazishi siku ya leo?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Mimi."
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akauliza tena;
"Yupi kati yenu aliyemlisha masikini siku ya leo?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Mimi."
Akauliza tena;
"Yupi katika yenu aliyemtembelea mgonjwa?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Mimi."
Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
"Hayajumuiki yote haya kwa mtu, isipokuwa ataingia Peponi."
Muslim

WEWE NI SAHIBU YANGU PENYE HODHI NA WA PANGONI
Kutoka kwa Abdullah bin Omar kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimwambia Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Wewe ni sahibu yangu penye Hodhi na sahibu yangu wa Pangoni."
Attirmidhiy

NANI ALIYE BORA BAADA YA MTUME (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
Siku moja Muhammad ibn Hanafiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye ni Mtoto wa Sayiduna Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu), alimuuliza babake;
"Nani aliye bora baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ?"
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu ; Abubakar
Akauliza tena ;     Kisha nani
Akajibu ;               Kisha Umar
Bukhari

LEO MNATAKA KUMUACHA MKONO SAHIBU YANGU
Siku moja Abubakar na Omar (Radhia llahu Anhum) walijadiliana wakakhitalifiana, na Abubakar alimkasirisha Omar (R.Anhum) kwa kumwambia maneno yasiyomridhisha. Abubakar alimtaka msamaha Omar, lakini Omar alikataa Kumsamehe, kisha Abubakar akenda kumsikitikia Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Mwenyezi Mungu keshakusamehe ewe Abubakar".
Wakati huo huo Omar(Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyejuta kwa kutomsamehe sahibu yake, alikuwa akimtafuta ili amtake yeye msamaha na akatokea wakati Abubakar(Radhiya Llaahu ‘anhu) amekaa pamoja na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyekuwa amekasirika alipiga magoti mara baada ya kumuona Omar, lakini Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipomuona Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) katika hali ile akamwambia;;
"Mimi ndiye niliyemkosea ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu."
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema (kumwambia Omar(Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Mwenyezi Mungu alinituma kwenu nyote, na nyote mlinikadhibisha hapo mwanzo isipokuwa Abubakar. Yeye alisema " Sadakta", basi leo mnataka kumwacha mkono Sahibu yangu?"
Anasema Omar bin Khattab (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Tokea siku ile hapana mtu aliyethubutu kumkasirikia Abubakar(Radhiya Llaahu ‘anhu)".
Bukhari
TULIA EWE UHUD
Siku moja Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipanda juu ya Jabali Uhud na jabali likatingishika. Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akauweka mkono wake mtukufu juu ya jabali hilo huku akiliambia;
"Tulia ewe Uhud! Kwa hakika juu yako yupo Mtume, na Aliyesadiki (Abubakar al Siddiq (Radhiya Llaahu ‘anhu)), na mashahidi wawili (Omar na Othman(Radhiya Llaahu ‘anhu)" .
Bukhari.
(Omar na Othman (R-Anhum), wote walikufa  mashahidi).

NA AMCHAE MWENYEZI MUNGU ATAEPUSHWA NA MOTO
Mwenyezi Mungu anasema;   
 “Na amchaye (Mwenyezi Mungu) ataepushwa nao (Moto).
Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa.
Na hali ya kuwa hakuna yeyote aliyemfanyia ihsani ili awe anamlipa.
Isipokuwa (anafanya haya) kwa kutaka radhi ya Mola wake Mtukufu.
Basi atapata la kumridhisha.”
Al Layl – 16 – 21
Maulamaa wa tafsiri wamekubaliana kuwa katika aya hizi Mwenyezi Mungu anamsifia Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa sababu sifa zote zilizotajwa zinakwenda sambamba na mwenendo na tabia zake;
Mwenyezi Mungu anasema;
“NA AMCHAYE (MWENYEZI MUNGU) ATAEPUSHWA NAO (MOTO).”
Hapana shaka kuwa Masahaba wote ni wacha Mungu, lakini ukiendelea kuzisoma na kuzichunguza vizuri zaidi aya zilizofuatilia utaona kuwa Mwenyezi Mungu ameongeza sifa nyingine inayomuelezea zaidi Sahaba huyu mtukufu (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Mwenyezi Mungu anasema;
“AMBAYE HUTOA MALI YAKE KWA AJILI YA KUJITAKASA.
NA HALI YA KUWA HAKUNA YEYOTE ALIYEMFANYIA IHSANI ILI AWE ANAMLIPA.”
Wasfu huu unakubaliana na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) kupita mwengine yeyote kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akitoa mali yake yote kwa ajili ya kuwalisha na kuwavisha masikini pamoja na kuwakomboa Waislam waliokuwa watumwa na kuwaachia huru, yote haya kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu. Na kisa cha kumkomboa Bilal (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni maarufu sana.

SITOSHINDANA NAYE TENA
Omar bin Khatab(Radhiya Llaahu ‘anhu) anasema;
“Siku moja Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alituamrisha tutoe Sadaka, na siku hiyo nilikuwa na Mali (pesa nyingi), Nikasema leo nitamshinda AbuBakar, nikampelekea Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) nusu ya Mali niliyokuwa nayo.
Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaniuliza:
“Ahli yako umewabakishia nini?”.
Nikamjibu;
“Nimewabakishia kima kama hiki cha mali (yaani nusu yake)”.
Akaja Abubakar na mali yote aliyokuwa nayo,  Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamuuliza;
“Umewabakishia nini ahli yako ewe Abubakar”.
Abubakar akasema;
“Nimewabakishia Mwenyezi Mungu na Mtume wake”.
Nikajisemea moyoni mwangu;
“Sitoshindana naye tena”.
Abu Daud na Ibni Majah
OH! MTAMUUA MTU KWA SABABU ANASEMA MOLA WANGU NI ALLAH?
Katika kuifasiri kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo;
“Na akasema mtu mmoja Mwislamu aliyekuwa mmoja wa watu wa Firauni afichaye Uislamu wake; Oh! Mtamwua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu? Na kwa yakini yeye amekujieni kwa dalili wazi wazi zitokazo kwa Mola wenu!”
AL MUUMIN (GHAFIR) – 28

Katika kuifasiri aya hii anasema Imam Al Qurtuby;
Imepokelewa na Imam Bukhari na Muslim kuwa, Urwa bin Al Zubeir, amesema;
“Nilimuuliza Abdullahi bin Amr bin Anas (Radhiya Llaahu ‘anhu); Hebu nihadithiye juu ya kubwa kabisa lililomkuta Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kutoka kwa Mushrikina, akasema;
“Siku moja Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa nje ya Al Kaaba, akamtokelea Uqba bin Abi Muit na kumshika mabega yake, kisha akamzungushia nguo shingoni pake na kumbana kwa nguvu kabisa, akatokea Abubakar na kumshika mabega yake (Uqba) na kumsukumilia mbali na Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kisha akasema;
“Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu?”

Hivi ndivyo alivyosimulia Bukhari


Ama hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Attirmidhiy inasema;
“Kutoka kwa Jaafar bin Muhammad, kutoka kwa babake, kuwa Ali(Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema;
“Baada ya kufa kwa Abi Talib, Makureshi walikusanyika na kutaka kumuuwa Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), wakamvamia, huyu akimburura na huyu akimsukuma, Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawa anaomba  msaada, hapana aliyethubutu kusogea isipokuwa Abubakar, aliwaendea akamvuta huyu na kumsukuma yule huku akipiga kelele na kusema;
“Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allah? Wallahi huyu ni Mtume wake”.
(Ataq tuluna rajulan an yaquula rabbiya Llah? Wallahi innahu la Rasuluhu)

Imepokelewa kutoka kwa Al Bazaar katika Musnad yake kuwa Muhammad Bin Aqeel (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema kuwa Ali(Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akihutubu akasema;
“Enyi watu! Nani shujaa kupita wote?”
Wakasema;
“Wewe ewe Amiri wa Waislam”
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Ama mimi kila niliyepambana naye nimemshinda, lakini (shujaa kupita wote) ni Abubakar. Siku moja tulimjengea Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hema kisha tukaulizana; ‘Nani atakayebaki na kumlinda Mtume(SA) ili asije akatokea mmoja katika Mushrikina na kumshambulia, basi Wallahi hapana aliyeingia isipokuwa Abubakar akiunyanyua upanga wake juu ya kichwa cha Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kila kafiri aliyejaribu kumsogelea Abubakar alikuwa akimrukia (na kumkabili, huyu ni shujaa kupita wote.
Na siku hiyo nilimuona pale alipochukuliwa Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na Makureshi, huyu akimvuta na huyu akimsukuma, hapana aliyesogea siku hiyo isipokuwa Abubakar, alisogea akiwapiga na kuwasukuma, huku akisema;
“Ole wenu  Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu? Wallahi huyu ni Mtume wake”.
(Waylukum! Ataq tuluna rajulan an yaquula rabiya Llah?) Wallahi innahu la Rasuluhu))”
Kisha Ali(Radhiya Llaahu ‘anhu) akalinyanyua guo alilokuwa amejifunika nalo na kuanza kulia mpaka ndevu zake zikaroa machozi.

Isra na Miraji


Mara baada ya kurudi katika safari ya Miraji aliyopelekwa ndani yake mpaka mbingu ya saba, kisha akasogezwa mahali panapoitwa ‘Sidratul muntaha na kuzungumza na Mola wake Subhahanu wa Taala, kisha akarudishwa ardhini katika usiku huo mmoja, na kabla ya kumhadithia mtu yeyote juu ya safari yake hiyo adhimu, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa amekaa kimya nje ya msikiti wa Al Kaaba, na Abu Jahal alipomuona katika hali ile akamuendea na kuanza kumkejeli huku akimuuliza.
"Enhe! Vipi pana habari yo yote mpya kutoka mbinguni leo?"
Kwa utulivu na upole Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamjibu: "Ndiyo, nilipelekwa usiku wa leo mpaka Baitul Maqdis (Palestina)."
Abu Jahal:            "Na asubuhi hii ukarudi Makkah?"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):  "Naam, na nilisali na ndugu zangu Manabii huko."
Abu Jahal akapiga ukelele kama mwenda wazimu na kuwaita jamaa zake.
"He! Amma leo Muhammad ametia fora"
Akaanza kuwahadithia yale aliyoyasikia kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), jambo lililowafanya hata baadhi ya waliosilimu karibuni wastushwe na habari hizo na kurudi nyuma kidogo.
Washirikina wa Kikureshi wakaona kuwa leo ndiyo siku ya kumfedhehesha Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kumtenganisha na sahibu yake Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu), wakaanza kusemezana;
"Abubakar anajua kuwa inachukua miezi mingi kusafiri kutoka Makkah hadi Sham, mahali ulipo msikiti huo wa Baytul Maqdis, maana kesha safiri kwenda huko mara nyingi, na leo Muhammad anasema eti amesafiri hadi huko ndani usiku mmoja tu"
Wakenda mpaka nyumbani kwa Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumgongea mlango huku wakimwita kwa sauti kubwa: "Abubakar!",
Abubakar  (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza:      " Kuna nini tena?"
Makureshi:                    "Rafiki yako Muhammad …",
Abubakar  (Radhiya Llaahu ‘anhu):           " Amefikiwa na jambo lolote ?" .
Makureshi:"                            "Eti anasema kuwa amesafiri usiku wa leo kutoka Makkah hadi Baytul Maqdis na kurudi ."
Abubakar  (Radhiya Llaahu ‘anhu):            "Ni yeye Mwenyewe aliyesema hayo?"
Makureshi:                    " Ndiyo! Tena tumemsikia kwa masikio yetu!"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu):             "Ikiwa Yeye Mwenyewe amesema hivyo, basi mimi namsadiki. Mimi namsadiki kwa mambo makubwa kupita hayo. Nasadiki kuwa anapata Wahyi unaotoka mbinguni, basi nisimsadiki juu ya kwenda hapo Baytul Maqdis?"
Hii ndiyo Imani ya Abubakar(Radhiya Llaahu ‘anhu) ambayo ikiwekwa upande mmoja wa mizani na zikiwekwa Imani za watu wote upande wa pili, basi imani ya Abubakar(Radhiya Llaahu ‘anhu) itazidi uzito.
Abubakar(Radhiya Llaahu ‘anhu) akavaa nguo zake, akatoka na kwenda kumtafuta Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), aliyemkuta amekaa kimya peke yake nje ya Al Kaaba, akamsogelea na kumkabili, kisha kwa utulivu na khushuu akamkumbatia na kumwambia;
"Wallahi wewe husemi uwongo na mimi nakusadiki , Wallahi nakusadiki."

Kuhajir pamoja na Sahibu yake


Juu ya kuwa hapana uamuzi mzito kuliko mtu kuamua kuihama nchi yake, kuwaacha watu wake pamoja na nyumba aliyozaliwa ndani yake, na kuyaacha nyuma yote yanayomkumbusha utoto wake, sahibu zake wa utotoni pamoja na kuwa mbali na ardhi aliyocheza na kugaragara juu yake, lakini Waislamu iliwabidi wafanye hivyo baada ya washirikina wa Makkah kuwaonjesha kila aina ya adhabu na kuwazuwia wasiifanye kazi waliyokabidhiwa na Mola wao ya kuilingania dini Yake, dini ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.
Iliwabidi watafute ardhi nyengine, ardhi madhubuti itakayowawezesha kusimama imara juu yake kwa ajili ya kuifikisha kwa watu amana waliyopewa na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala na pia kuwawezesha kujilinda kutokana na maadui wa Mwenyezi Mungu. Mahali watakapoweza kujitayarisha kwa ajili ya kupigana Jihadi.
Kwa ajili ya lengo hilo adhimu, watu wa Madina walikuwa wakiwasubiri kwa hamu kubwa sana ndugu zao kutoka Makkah, kwani wao ndio waliokuja mahali panapoitwa Mina kwa ajili ya kufungamana na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) katika Mafungamano mawili yaliyokuja kujulikana kwa jina la 'Fungamano la Aqaba' la kwanza na la pili na kumtaka Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ahamie kwao na kumuahidi kuwa watamlinda na kumsaidia katika kuilingania dini hii kwa hali na mali.
Wakati wa kuhama ulipowadia, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), alimwendea Sahibu yake Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumtaka wafuatane pamoja kuelekea Madina, akamwambia;
"(Assuhba ya Ababakar)”.
Kabla ya hapo Makureshi walikwisha amua kumuuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), wakihofia kuwa akifanikiwa kuhamia Madina itakuwa rahisi kwake kujijenga na kuineza dini aliyokuja nayo na kuipiga vita dini yao iliyo batil.
Kwa kusudi hilo, wakatuma vijana kutoka matumbo mbali mbali ya kabila lao na kuwataka wote kwa pamoja wamchome Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa panga zao ili damu yake ichanganyike baina ya matumbo yote hayo, jambo litakalowazuwia jamaa zake wasiweze kudai kulipa kisasi cha mtu wao, na itawabidi waridhike  kwa kulipwa fidia tu.
Jibril (Alayhis salaam) alimjulisha Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) yote hayo na akamtaka aondoke usiku huo huo kuelekea Madina.
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwita Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwakilisha jukumu la kurudisha amana za watu, akamtaka pia alale juu ya kitanda chake, kisha akatoka huku akiwasomea wale vijana waliokuja kumuwa waliokuwa wakimsubiri nje ya nyumba yake baadhi ya aya za Surat Yaasin, huku akiwanyunyizia mchanga juu ya vichwa vyao na kuwaacha hapo wakiwa wamelala usingizi mzito.

Alitoka na kwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Abubakar Al Siddiq (Radhiya Llaahu ‘anhu), na baada ya kumgongea mlango huku akiwa amejifunika uso wake, sahibu yake akatoka, wakaondoka wote kwa pamoja na kuelekea Madina kupitia njia ya pwani pwani kwa ajili ya kuwababaisha makafiri, kwa sababu njia hiyo kwa kawaida haikuwa ikitumiwa na wasafiri wanaokwenda Madina.
Walipowasili penye pango linaloitwa ‘Ghari Thour’ wakaingia humo kwa ajili ya kujipumzisha.
Alipokuwa akilichunguza pango hilo, Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akagundua mashimo mengi ndani yake ambayo nyoka, nge au wadudu wabaya wangeweza kupenya kupitia humo. Akachana nguo zake za kujifunikia na kuanza kuyaziba matundu hayo, isipokuwa moja alishindwa kuliziba baada kuishiwa na nguo za kuchana, akakaa karibu yake na kuliziba kwa mguu wake haidhuri adhurike yeye, lakini chochote kisipitie humo na kumdhuru Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alitaka kupumzika, akalala karibu na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akiwa ameuweka uso wake mtukufu juu ya paja la Sahibu yake huyo, na haukupita muda wakaanza kusikia sauti za Makureshi waliokuwa wakiwatafuta.
Sauti zikawa zinakaribia, na Abubakar(Radhiya Llaahu ‘anhu), alipoinama na kutizama nje aliweza kuona namna gani maadui hao walivyo karibu nao, akamwambia Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam);
"Mmoja wao akiinama tu, atatuona ."
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia;
"Usihuzunike ewe Abubakar, Mwenyezi Mungu yupo pamoja nasi, Unaonaje ikiwa wawili, watatu wao ni Allah?"

Mwenyezi Mungu anasema:
"Ikiwa nyinyi hamtamnusuru (Mtume), basi Mwenyezi Mungu alikwisha mnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wapili katika wawili walipokuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: ‘Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi’. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima."

Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatafunwa na n'ge, katika mguu wake ule aliouweka juu ya tundu pale alipoishiwa na vitambaa vya kuzibia. Maumivu yakawa yanazidi, lakini alihiari kunyamaza na kustahamili asije akamshughulisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ingawaje alikuwa akijua kuwa sumu inatembea ndani ya damu yake na huenda ikamuua.
Maumivu yalikuwa makali sana hata chozi likamdondoka na kuanguka juu ya uso wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), aliyestuka na kuuliza:
"Kuna nini Abubakar, mbona unalia ?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Nimetafunwa na n'ge ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu" .
 Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akainuka na kuushika mguu pale ulipotafunwa, na kumuomba Mwenyezi Mungu na hapo hapo sumu hiyo ikatoweka na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akapona .