Abubakar As Siddique
(Radhiya Llaahu ‘anhu)
Khalifa wa kwanza aliyeongoka
Makubaliano ya Hudaibia
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikua akimfahamu na
akimuelewa vizuri sahibu yake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kupita Masahaba
wote (Radhiya Llaahu ‘anhu), na alikuwa na uhakika kuwa yote anayoyasema ni Wahyi
utokao kwa Mola wake Subhanahu wa Taala.
Katika mwaka wa tano baada ya kuhamia Madina, Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Masahaba wake (Radhiya
Llaahu ‘anhu) waliondoka Madina kuelekea Makkah kwa nia ya kufanya Umra. Wakapiga
kambi karibu na mji wa Makkah mahali panapoitwa Al Hudaibiyya, kisha wakamtuma
Othman bin Affan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ende Makkah kuwajulisha Makureshi juu
ya nia yao hiyo na kwamba hawakuja kwa nia ya kupigana vita.
Makureshi wakapeleka majeshi yao
kutaka kuwazuia, na baada ya majadiliano marefu yaliyopita baina yao, wakaamua kumtuma
mjumbe wao aitwaye Suhail bin Amr, aliyeweza kufikia makubaliano na Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam), yaliyokuja kujulikana kwa jina la Makubaliano ya Al
Hudaibiyya.
Yafuatayo ni baadhi ya shuruti za makubaliano hayo;
·
Waislamu
warudi Madina mwaka huu na wafanye Umra mwaka ufuatao.
·
Waislamu
wanalazimika kumrudisha kwa Makureish yoyote atakayeingia katika dini yao na kukimbilia Madina,
lakini Makureshi hawalazimiki kumrudisha atakayetoka katika Uislamu na
kukimbilia Makkah.
·
Wasipigane
vita kwa muda wa miaka kumi, na wawe wanaendeana watakavyo.
Kabla ya mkataba huo kutiwa sahihi (saini), Waislamu
walistukia kijana mmoja aitwae Aba Jandal aliyesilimu lakini alikuwa akiishi
Makkah akipitishwa mbele yao akiwa amefungwa minyororo shingoni huku na
kubebeshwa jiwe kubwa akipiga kelele akiwaomba Waislamu wenzake wamuokoe
kutokana na adhabu hiyo.
Kijana huyu Aba Jandal ni mwana wa Suhail, mjumbe wa
Makureish katika sulhu hiyo.
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), alimuonea
huruma kijana huyo, akamtaka Suhail amruhusu wamchukuwe kwa sababu mkataba
ulikuwa bado haukutiwa saini wala haukupigwa mhuri, lakini baba yake alikataa
na kutishia kuuvunja mkataba na kuanzisha vita ikiwa watajaribu kumchukua kwa nguvu.
Abu Jandal alikuwa akipiga kelele huku akisema;
"Enyi Waislamu wenzangu! mnaniacha nirudi kwa
washirikina hawa na mimi nataka himaya yenu?"
Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia ;
"Kuwa na subira, na Mwenyezi Mungu atakujaalia
utoke katika janga hilo".
Omar bin Khattab (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuweza
kuyastahamilia haya, akamuendea Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na
kumuuliza;
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, wewe si Mtume wa
Haki?"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamjibu;
"Ndiyo, ewe Omar".
Akauliza tena;
" Kwa nini basi tunakubali kujidhalilisha?"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia;
"Ewe Omar, mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, siwezi
kumuasi, na Yeye ndiye atakayetunusuru".
Omar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza;
"Si ulituahidi kuwa tutakwenda Makkah na tutatufu
katika nyumba kongwe?"
Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akajibu;
"Nilikwambia kuwa ni mwaka huu ewe Omar?"
Omar akajibu;
"La hukusema hivyo."
Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akasema;
"Utakwenda Makkah ewe Omar na utatufu penye
nyumba."
Omar pamoja na baadhi ya Masahaba (R.Anhum)
hawakuridhika na baadhi ya masharti yaliyokuwemo ndani ya mkataba ule, wao
waliona kuwa Waislamu wamekubali kujidhalilisha kwa kuyakubali masharti yote ya
makafiri, na hii ni kwa sababu dhahiri yake mkataba huo si mzuri juu ya
Waislamu, lakini kwa anayeona mbali mkataba huo ulikuwa ni ufunguzi mkubwa kwa
Waislamu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Suratul Fat-h aya ya mwanzo;
"Bila shaka tumekwishakupa kushinda kuliko
dhahiri"
Mwenyezi Mungu katika aya hii anatujulisha kuwa
kuukubali mkataba huo ni ushindi mkubwa kwa Waislamu, juu ya kuwa dhahiri yake
ni kukubali masharti yote ya makafiri, na hii ni inatokana na sababu zifuatazo;
1)
Kutokana
na suluhu hiyo, makafiri walifungika wasiweze kupigana vita dhidi ya Waislamu
muda wa miaka Kumi.
2)
Katika
muda wote huo Waislmu wakawa na uwezo wa kujishughulisha na kuieneza dini yao miongoni mwa makabila
mengine ya Bara arabu, pamoja na nchi za Sham.
3)
Mtume
wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alituma ujumbe kwa wafalme
mbali mbali
4)
Wale
waliosilimu wasioruhusiwa kukimbilia Madina kwa ndugu zao Waislamu, ni bora
kwao kubaki Makkah kwa ajili ya kuwalingania watu katika dini ya Kiislam huko
Makkah.
5)
Makafiri
watakaorudi Makkah iwapo watatoka katika Uislam, hawataudhuru Uislam.
Sababu hizi na nyinginezo ambazo si wasaa wake huu
kuzitaja ni dalili kuwa mkataba huo undani wake ulikuwa na manufaa makubwa kwa
Waislamu, juu ya kuwa dhahiri yake ni kusalimu amri na kukubali masharti yote
ya Makureshi.
Na hii ndiyo sababu iliyomfanya Omar (Radhiya Llaahu
‘anhu) asiridhike nao, wala asisimame hapo. Kwani alimwendea pia Abubakar Al
Siddiq (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumuuliza tena masuali yale yale;
"Ewe Abubakar, Muhammad si Mtume wa Haki?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu); "Ndiyo"
Omar (Radhiya Llaahu ‘anhu); "Tukipambana nao
makafiri hawa, si atakayekufa upande wetu ataingia Peponi na wao wanaingia
Motoni?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu); "Ndiyo".
Omar (Radhiya Llaahu ‘anhu); "Kwa nini basi
tunakubali kujidhalilisha?"
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Ewe Omar, yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na
hawezi kumuasi, na Mwenyezi Mungu ndiye atakayemnusuru, kamatana naye kwani
Wallahi yupo katika Haki".
Majibu yale yale ya Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) kayapata kwa Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu), na
Mwenyezi Mungu akawateremshia Waislamu utulivu nyoyoni mwao.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Yeye ndiye
aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waislamu ili waongezeke imani juu ya
imani yao".
Suratul Fat-h 4
Omar(Radhiya Llaahu ‘anhu)
alisema baadaye;
"Nikatambua kuwa ile
ndiyo Haki".
Mwaka wa tisa Hijri ndio mwaka ulioitwa 'Mwaka wa
Wajumbe' na hii ni kutokana na wajumbe wa makabila mbali mbali ya kiarabu
waliokuja kusilimu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam).
Vita vya Badr
Imani ya Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) ilikuwa ikijitokeza na kueneza tumaini baina ya watu kila
inapotokea shida au dhiki.
Katika vita vya Badr, jeshi
dogo sana la Waislamu liliondoka mjini Madina
kwa nia ya kuuteka msafara mdogo wa kibiashara ukiongozwa na Abu Sufyan
unaotokea Syria
na kuelekea Makkah, na Waislamu walitegemea kuwa bila shaka msafara huo utakuwa
na watu wachache waliokwishachoka baada ya safari ndefu hiyo.
Mwenyezi Mungu akawataka
Waislamu wauachilie mbali msafara huo na wende kupambana na jeshi kubwa la
Makureshi lililokwishaondoka Makkah kuelekea Madina likiwa limejitayarisha
kivita na limejizatiti barabara. Na Mwenyezi Mungu aliwaahidi Waislam kuwa
watawashinda Makureshi hao juu ya wingi wao.
Idadi ya Waislam ilikuwa mia
tatu na kidogo tu, na hawakuwa na silaha nzito isipokuwa panga zao.
Waislamu wakapiga mahema yao katika bonde la Badr
na kumtaka Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) asiondoke hemani pake iwe
itakavyokuwa.
Jeshi kubwa la makafiri
likaanza kuhujumu kwa nguvu, na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa
akihuzunika kila anapoona Muislam anauliwa, na mambo yalipozidi kuwa magumu
hata akawa anasikia sauti za panga na kelele na mayowe zikikaribia, akaamua
kutoka nje ya hema huku akinyanyua mikono yake mbinguni na kumuomba Mola wake
kwa hamasa akisema;
"Mola wangu ikiwa kundi
hili litaangamizwa, hutoabudiwa tena ardhini, Mola wangu nipe ushindi
ulioniahidi Mola……"
Aliendelea hivyo mpaka
Sayiduna Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipomwendea na kuiweka sawa nguo ya
kujifunikia ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) iliyokuwa ikimwanguka
huku akimwambia;
"Ewe Mtume wa Mwenyezi
Mungu inatosha kuomba, kwani Mola wako atakupa kile alichokuahidi".
Bila shaka Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anaamini kuwa kila alichoahidiwa na
Mola wake atakipata, bali hata kabla ya vita hivyo kuanza, yeye ndiye
aliyewaonesha Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu) mwahali watakapoanguka vigogo vya
Makureshi. Aliwaonyesha mahali gani Abu Jahal atauliwa na kuanguka, na
akawaonyesha mwahali gani watauliwa na kuanguka vigogo wengine mbali mbali wa
Kikureshi, na yote yalitokea kama alivyosema.
Lakini hisia yake juu ya
uzito wa mzigo alioubeba na hofu yake katika pambano hili la mwanzo baina ya
Imani na Kufru ndiyo iliyomfanya atoke nje ya hema lake na
kunyanyua mikono yake juu akiomba kwa hamasa namna ile.
Imani ya hali ya juu
Imani ya hali ya juu kabisa
ya Abubakar ilionekana pale alipofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) .
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) alipokuwa akiumwa maradhi yake ya mwisho, alimtaka Abubakar awe
anasalisha watu. Siku moja baada ya kuwasalisha Waislam, Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliingia
chumbani kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na baada ya kuzungumza
naye muda mrefu akamtaka ruhusa arudi nyumbani kwa ajili ya kukidhi haja zake.
Baada ya kumaliza haja zake
na alipokuwa akijitayarisha kurudi msikitini, akasikia sauti za watu
wanalizana, akazipokea habari za kufariki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu huku
anakimbia kuelekea msikitini na huku machozi yakimtoka huku akisema;
"Inna lillahi wa inna
ilayhi raaji uun".
Ndani ya nyumba ya Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) watu walikuwa mfano wa waliorukwa na akili.
Hata Omar bin Khatab (Radhiya
Llaahu ‘anhu), mwenye nguvu, shujaa, alisimama mbele ya watu panga mkononi huku
akisema:
"Wanafiki wanadai kuwa
eti Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amekufa, Mtume hajafa, bali
amekwenda kwa Mola wake kama alivyokwenda Musa
mwana wa Imran na atarudi. Sitaki kumsikia mtu akitamka kuwa Mtume amekufa.,
nikimsikia mtu anasema hivyo nitamkata kichwa chake kwa upanga wangu huu."
Ikiwa hii ni hali ya Omar,
ilikuwaje basi hali ya walio chini yake? Waislam hawakutegemea kuwa Mtume wao,
kipenzi chao, (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) siku moja atakuja kuwatoka,
msituko ulikuwa mkubwa sana.
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) aliingia moja kwa moja chumbani alipolazwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam), akamfunua uso wake na kuubusu huku akisema;
"Uso wako unapendeza
ukiwa u hai au umekufa. Ama kile kifo alichokuandikia Mola wako
kimekwishakufikia".
Akaufunika uso wake na kutoka
nje na kumkuta Omar (Radhiya Llaahu ‘anhu) angali anawasemesha watu. Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akamtaka anyamaze lakini Omar (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakunyamaza,
na alipomuona hanyamazi akawaelekea watu na kuwaambia;
"Aliyekuwa akimuabudu
Muhammad, basi Muhammad kesha kufa, ama aliyekuwa akimuabudu Allah, basi Allah
yu hai na wala hafi."
Kisha akaisoma kauli ya
Mwenyezi Mungu isemayo:
"Na hakuwa Muhammad ila
ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa). Akifa au akiuawa ndiyo
mtarudi nyuma (kwa Visigino vyenu), muwe makafiri kama
zamani? Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Mwenyezi Mungu cho
chote. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaomshukuru."
Aali Imran- 144
Alipoisikia tu aya hiyo Omar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) hakuweza kusimama, akakaa kitako mfano wa simba aliyenyeshewa
mvua. Siku zilizofuata alisema:
"Ilikuwa kama kwamba
ninaisikia aya hiyo kwa mara ya mwanzo, miguu haikuweza kunichukua nikajitupa
chini na kukaa".
Bukhari.
Ama Ibni Abbas alisema;
"Wallahi ilikuwa kama hawaijui aya hii, na mara walipomsikia Abubakar akiisoma,
watu wote waliipokea na kila aliyeisikia alikuwa akiisoma na
kuirudiarudia".
Bukhari.
Huu ndio ushujaa wa Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu), wakati kama huu, umma wote
ulipobabaika na kutetereka, akiwemo Omar bin Khatab (Radhiya Llaahu ‘anhu),
Abubakar Al Siddiq alikuwa thabiti mfano wa jabali mbele ya kimbunga
kilichouvamia umma siku hiyo, na aya aliyoisoma siku ile ikawa inarudiwarudiwa
na kila mtu;
"Aliyekuwa akimuabudu
Muhammad, basi Muhammad kesha kufa, ama aliyekuwa akimuabudu Allah, basi Allah
yu hai na wala hafi."
Neno la Tawhid, neno la
kuuamsha Umma, 'Ikiwa mnamuabudu Allah basi amkeni na muifanye bendera ya Laa
ilaaha Illa llah ipepee kila mahali. Aamkeni muyaendeleze mapambano
yaliyoanzishwa na Mtume wenu huyu mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)'.
Neno hilo liliwaamsha na kuwatanabahisha Waislamu,
wakaanza kutimiza wajibu wao, wakamuosha, wakumshughulikia na kumsalia na
kumuaga Mtume wao mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
"Je kusingekuwepo na
Abubakar, hali ingekuwaje siku hiyo?"
Siku ya Saqifa
Hii ni siku aliyofariki Mtume
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na baadhi ya watu wa Madina walijikusanya
mahali panapoitwa Saqeefat Bani Saaidah karibu na msikiti wa Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa ajili ya kufungamana na sahaba mmoja katika watu
wa Madina aitwaye Saad bin Obada (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumchagua kuwa ni
Khalifa wa Waislam.
Omar (Radhiya Llaahu ‘anhu),
alipopata habari hizo alimwendea Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumhadithia
yanayotokea, na wote kwa pamoja wakifuatana na Abu Ubeidah Amer bin Jarrah (Radhiya
Llaahu ‘anhu) wakaelekea huko.
Abubakar wala Omar hawakuwa
na tamaa ya Ukhalifa kama tutakavyoona, na hii ni kwa sababu walimsikia Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akimkatalia Ami yake Al Abbas, alipomuomba ampe
ugavana wa mkoa mmojawapo, na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akamwambia;
"Sisi Wallahi hatumpi
utawala mwenye kuuomba wala mwenye kuung'ang'ania" .
Na hii ni kwa sababu utawala,
si neema wala raha hata mtu aung'ang'anie na kuutaka. Mwenye kuung'ang'ania
utawala ni yule asiyeelewa jukumu lake,
ama sivyo asingeutaka. Na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyajua hayo
vizuri .
Wengi walibabaika baada ya
kuzipokea habari za kifo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam), na miongoni mwao ni watu wa Madina
waliojikusanya mahali hapo panapoitwa Saqeefat Bani Saaidah, wakasema
kuwa; lazima pafanywe haraka kumchagua kiongozi wa umma kabla hapajatokea
machafuko, na wakataka kiongozi huyo atoke katika watu wao (awe mtu wa Madina),
kwa sababu Madina ni mji wao, na kwa sababu ya fadhila zao nyingi katika
kuunusuru Uislamu, na kwa ajili hiyo wakaamua kumchagua sahaba huyo aitwaye
Saad bin Obada (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Mara baada ya kuwasili mahali
hapo, Omar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akataka kuuhutubia mkusanyiko huo, lakini
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu), alimvuta nyuma na kumuomba amwachie yeye
ahutubie, akajisogeza mbele na kusema;
"Enyi watu wa Madina,
hakika hapana fadhila itakayowezwa kutajwa bila ya kutajwa nyinyi ….",
akaendelea kuwapa sifa zao walizostahiki, kisha akasema.
"Lakini Khalifa wa
Waislamu atoke kwetu sisi watu wa Makkah".
Katika kitabu chake kitukufu,
Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala daima hutanguliza kuwataja watu wa Makka 'Al
Muhajirin' kabla ya watu wa Madina 'Al Ansar'
.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Na wale waliotangulia
wakawa wa kwanza katika (Uislamu) Muhajiri na Ansari…".
At Tawba-100
Mmoja katika watu wa Madina
aitwaye Al Khabbab bin Mundhir (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Kwetu atoke Amiri na kwenu
Amiri".
Akainuka sahaba mwengine
ambaye pia ni katika watu wa Madina aitwaye Bashir bin Mubarak (Radhiya Llaahu
‘anhu) na kusema;
"Enyi Al Ansar (Watu wa
Madina), ingawaje sisi tumeipigania dini hii kwa hali na mali, lakini
haijuzu kwetu kujifanya bora kuliko wenzetu, sisi tulifanya hayo kwa ajili ya
kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume wetu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam). Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anatokana na kabila la
Kikureshi, na watu wake ndio wanaostahiki kutuongoza. Mwenyezi Mungu
asinijaalie nikapingana nao. Muogopeni Mola wenu enyi watu wa Madina na
msiwaendee kinyume Al Muhajirina (watu wa Makkah)".
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu), akaunyanyua juu mkono wa Omar na
wa Abu Obaida Amir bin Jarah (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kusema;
"Huyu Omar bin Khattab
ambaye Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimuomba Mwenyezi Mungu
kutokana naye autukuze Uislamu, na huyu Abu Ubaida ambaye Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) alimsifia kuwa ni 'Mwaminifu wa Umma huu', mimi nimeridhika
(achaguliwe) mmoja kati yao, (awe Khalifa)"
Omar aliuchomoa mkono wake
kwa nguvu mfano wa mtu aliyeshika jinga la moto na Abu Ubaida akasema;
"La wallahi! Nina hiari
nikatwe kichwa changu bila ya kutenda dhambi yoyote, lakini sikubali niwe
kiongozi wa watu akiwemo Abubakar ndani yao.
Ewe Abubakar, Mtume wa Mwenyezi Mungu alikutanguliza wewe utusalishe, na katika
kila kubwa na dogo aliridhika na wewe, basi kwa nini na sisi tusiridhike na
wewe? Utandaze mkono wako tufungamane nawe, ewe Abubakar".
Akautandaza, na katika riwaya
zilizo sahihi, wa mwanzo kufungamana naye alikuwa Bashir bin Mundhir ambaye ni
mtu wa Madina, kisha Omar kisha Abu Ubaida kisha wakamvamia masahaba wote mmoja
baada ya mmoja wakifungamana naye (Radhiyallahu anhum).
Siku ya msiba mkubwa kupita
yote iliyopata kuwatokea Waislamu ilimalizika kwa amani baada ya kuweza
kuiondoa hitilafu iliyozuka baina yao, na baada ya kupata matumaini kwa kumuona
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ndiye aliyeshika hatamu, kwani Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anapokuwa anaumwa au
anapopatwa na udhuru wowote, alikuwa daima akimtanguliza Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) kusalisha watu, kuongoza misafara ya hija na kusimamia mambo
mbali mbali.
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) alipokuwa akiumwa katika maradhi yake ya mwisho, alimchagua Abubakar
(Radhiya Llaahu ‘anhu) awasalishe watu, na bibi Ayesha (Radhiya Llaahu ‘anha)
alipojaribu kumtaka Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kumpa Omar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) jukumu hilo badala ya baba yake kwa sababu Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) alikuwa mwingi wa kulia anaposalisha, Mtume(Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) alikasirika akamwambia;
"Mwambie Abubakar
asalishe watu!"
Mimi si mbora wenu
Siku ya mwanzo ya utawala
wake Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipanda juu ya membari ya msikiti wa
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwahutubia Umma aliopewa jukumu la
kuwaongoza. Baada ya kupanda ngazi mbili alishindwa kuzikamilisha ngazi zote
tatu alizokuwa akizipanda Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam), maana aliona kuwa akizikamilisha ngazi zote atakuwa amejiweka daraja
moja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Baada ya kuzipanda ngazi hizo
akaanza kuhutubia kwa kusema;
"Enyi watu!
'Mimi nimepewa uongozi juu yenu, lakini si
mbora wenu.
Nikihukumu sawa, nisaidieni.
Nikihukumu vibaya
nirakibisheni.
Hakika aliye dhaifu miongoni
mwenu, kwangu mimi ni mwenye nguvu mpaka nimpatie haki yake, na hakika mwenye
nguvu miongoni mwenu, kwangu mimi ni dhaifu mpaka niichukue haki ya watu iliyo
kwake.
Nitiini iwapo nitamtii
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ama nikiasi (amri ya Mwenyezi Mungu) basi
msinitii.
Umma unapoiacha Jihadi,
hudhalilika.
Inukeni msali, Mwenyezi Mungu
akurehemuni".
Hii ndiyo hutuba ya mwanzo ya
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu); hotuba fupi iliyoweka wazi jinsi gani
atakavyohukumu.
Alisema;
'Mimi nimepewa uongozi juu yenu,
lakini si mbora wenu'.
Aliyasema haya ili kuujulisha
Umma kuwa yeye si mfalme juu yao
bali ni kiongozi tu, na hivi ndivyo uhusiano utakavyokuwa baina yake na Umma
wake, Kiongozi, Mwalimu, Jemadari, Khalifa wao na Mwenzao.
Kwa njia hii aliwajulisha
Umma wake juu ya Dhamana aliyopewa na juu ya kiongozi mwaminifu, vipi anatakiwa
awe.
Pia alitaka kuondoa katika
fikra zao kwamba, anayehukumu, yupo juu ya sheria, na kwamba anaweza akafanya
atakavyo, na kwamba hakosi na wala hakosolewi.
Alitaka kuwajulisha kuwa
Uongozi si cheo cha kujivunia bali ni dhamana, na Ukhalifa alopewa ni kazi na
si kitu cha kujitakabaria mbele ya watu.
"Lakini si mbora
wenu"
Katika kitabu chake kiitwacho
'Khulafaa a Rrasuul' Mwandishi maarufu Khalid Muhammad Khalid (Mwenyezi Mungu
amrehemu) alisema;
"Huenda akawa Kweli si
mbora wao kwa vile yeye ni mwenye kuhukumu, lakini alikuwa mwenye hekima kupita
wao na hii ni kwa sababu yeye ni Al Siddiq, Aliyesadiki ambaye ndani yake
amekusanya Kusadiki, Imani, Uaminifu na Uongofu ulomfanya astahiki kuwa Sahibu
yake Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa pangoni.
Alikuwa mwenye hikima kwa
sababu alijua kuwa hatokuwa huru mpaka Umma wake kwanza uwe huru.
Hatokuwa na nguvu mpaka Umma
wake kwanza upate nguvu.
Hatokuwa na Amani mpaka Umma
wake kwanza upate amani"
Kupambana na waliortadi
Baadhi ya makabila yanayoishi
mbali na mji wa Madina na ambayo yaliingia karibuni tu katika Uislamu, yalianza
kufanya uasi na kurtadi mara baada ya kusikia habari za kifo cha Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Walirtadi baada ya kukataa
kumpa Khalifa mpya wa Waislamu mali
ya zaka kama walivyokuwa wakimpa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Walisema kuwa Mwenyezi Mungu
katika aya ya 103 ya Suratu Tawba anasema;
"Chukua sadaka katika mali zao,
ziwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Zaka) kuwataja kwa vizuri (mbele
yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu na Mwenyezi
Mungu ndiye asikiaye na ajuaye."
Waasi hao wakasema:
"Tulitakiwa tutoe Zaka
na kumpa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) apate kututakasa kwa ajili ya
hizo Zaka na kutuombea dua, lakini sasa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
kesha kufa na Abubakar hawezi kututakasa na kutuombea dua kama
alivyokuwa akifanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Kwa ajili hiyo hakuna tena haja ya kutoa Zaka."
Sayiduna Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akaamua kuingia vitani na waasi hao kutokana na sababu mbili;
1-
Aliona kuwa huko ni Kurtadi, kwa sababu Zaka ni nguzo ya
tatu ya Kiislamu na kukataa kuitoa ni kuikataa nguzo hiyo.
2-
Akaona pia kuwa kuyanyamazia mambo hayo kutasababisha
kutokea uasi wa aina nyingine, maana watu watakapoona kuwa pana udhaifu katika
uongozi, kila mmoja atataka kuiweka sheria mikononi mwake.
Umar bin Khatab (Radhiya
Llaahu ‘anhu) yeye aliona kuwa kwa vile watu hao wanaukubali Uislamu, bora
wasiwapige vita, lakini Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa akijulikana
kwa upole hakuikubali rai hiyo na akashikilia kupigana na waasi hao.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
akamwambia; "Vipi unapigana vita na watu wanaoikubali shahada ya "Laa
ilaaha illa llah" wakati Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisema
kuwa; atakayeikubali shahada hiyo itahifadhika mali yake na damu yake?
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akajibu;
"Lakini si alisema kuwa
ni lazima aipe haki yake (shahada hiyo)? Na Zaka ni katika haki zake."
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alisema baadaye kuwaambia watu:
"Kisha Mwenyezi Mungu
alikifungua kifua changu kuikubali rai ya Abubakar".
Jeshi la Usama
Wakati haya yakitokea,
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliona ni bora kulianzisha tena jeshi la Osama (Radhiya
Llaahu ‘anhu), jeshi lililoundwa na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
mwenyewe chini ya uongozi wa Osama bin Zeid (Radhiya Llaahu ‘anhu), na jeshi
hilo lilikuwa limekwishapiga kambi nje ya Madina likijitayarisha kwenda
kupigana na Warumi, lakini kutokana na kushtadi kwa maradhi ya Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) jeshi hilo halikuondoka.
Baada ya kifo cha Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) jeshi hilo lilirudi
tena Madina, na Waislamu wakahitilafiana juu ya kulianzisha tena jeshi hilo.
Baadhi ya Waislamu akiwemo
Omar bin Khatab (Radhiya Llaahu ‘anhu) waliona kuwa si fikra nzuri kulianzisha
tena jeshi hilo
hasa wakati huu ambapo mji wa Madina umo katika hatari ya kuvamiwa na makundi
ya waliortadi.
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akasema;
"Lianzisheni tena jeshi
la Osama, kwani Wallahi hata kama mbwa wa mwitu wataninyakua basi nitalianzisha
tena kama alivyofanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam)."
Alipoona kuwa Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) ameshikilia jambo hilo,
Omar bin Khattab (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Kwa vile Osama ni
kijana mdogo sana, basi angalau ungemweka mtu
mzima aliongoze jeshi hilo".
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) aliruka kutoka pale aliposimama na kuzishika ndevu za Omar bin Khatab (Radhiya
Llaahu ‘anhu), akamwambia;
"Ole wako ewe Ibnil
Khatab! Amepewa uongozi na Mtume wa Mwenyezi Mungu na wewe unanitaka mimi
nimuondoe?"
Ndani ya jeshi hilo
walikuwemo masahaba wakubwa kama vile Omar, Othman na wengine (R.Anhum), na
lilipokuwa likiondoka mjini Madina, Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa
analisindikiza huku akitembea kwa miguu na Osama (Radhiya Llaahu ‘anhu) akiwa
amepanda farasi.
Osama (Radhiya Llaahu ‘anhu)
ambaye umri wake haukuzidi miaka kumi na nane wakati ule akasema;
"Ewe Khalifa wa
Waislamu, bora wewe panda juu ya mnyama huyu na mimi nitakwenda kwa
miguu".
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akamjibu;
"Wallahi utabaki juu ya
farasi na mimi nitatembea kwa miguu, kwani nitakuwa nimefanya jambo kubwa sana ikiwa nitaitia miguu
yangu vumbi angalau kidogo katika njia ya Mwenyezi Mungu?."
Kwa vile Abubakar alikuwa
akiuhitajia ushauri na msaada wa Omar katika uendeshaji wa mambo ya Waislamu,
na kwa vile Omar alikuwa miongoni mwa wanajeshi chini ya uongozi wa Osama,
ilimbidi Abubakar amuombe Osama ili amruhusu Omar abaki naye Madina.
Akamnong'oneza sikioni pake na kumwambia;
"Itakuwa vizuri kama utakubali kuniachia Omar, maana namhitajia katika
kuendesha mambo ya Umma".
Osama (Radhiya Llaahu ‘anhu),
akakubali.
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) angeweza kumuamrisha Osama (Radhiya Llaahu ‘anhu) juu ya jambo hilo, lakini hakufanya hivyo kwa sababu Osama (Radhiya
Llaahu ‘anhu) alikuwa mkuu wa jeshi hilo na
mwenye haki ya kutoa ruhusa hiyo, na kama
Osama angelikataa, basi asingemlazimisha.
Na jambo hili la Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) kuliunda tena jeshi la Osama lilisaidia sana
kuyavunja nguvu makundi ya walortadi na kuingiza uoga nyoyoni mwao, maana waasi
hao walipoliona jeshi hilo
likitoka nje ya Madina kuelekea Sham, walisema:
"Wallahi ungekuwa mji wa
Madina uko katika udhaifu na hitilafu kama tunavyosikia, basi wasingeweza
kulitoa nje jeshi kubwa kama hili kupambana na
Warumi".
Baada ya kuwasindikiza mpaka
nje kidogo ya mji wa Madina, Abubakar akalihutubia jeshi hilo na kulijulisha juu ya misingi ya jeshi
la Kiislamu linavyotakiwa liwe.
Baada ya kumshukuru na
kumpwekesha Mwenyezi Mungu, akasema:
"Msifanye khiyana wala
msishambulie bila taarifa (ghadran), wala msikate kate maiti za adui, wala
msiue mtoto wala mzee wala mwanamke, wala msiunguze mtende wala msikate mti
unaotoa mazao wala msichinje mbuzi wala n'gome wala ngamia isipokuwa kwa ajili
ya kula.
Na mtakutana na watu
waliojitenga ndani ya hekalu zao kwa ajili ya ibada, basi waacheni hivyo hivyo
walivyo."
Kisha akasema: "Nendeni
kwa jina la Mwenyezi Mungu."
Haya ndiyo maamrisho ya
Kiislamu, na hivi ndivyo alivyofundishwa Abubakar na Mwalimu wake Muhammad (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam). Na hivi ndivyo majeshi ya kiislamu yalivyokuwa
yakifanya kupitia karne zote.
Na waisome historia ya
ufunguzi wa Kiislamu kama watakuta yale waliyofanya wao huko Algeria, Bosnia Kosovo, Afghanistan na
hivi sasa Palestina. Waislamu wanachinjwa kama
mbuzi na kukatwa katwa maiti zao na wengine wamezikwa wakiwa wazima, na wake
zao wameingiliwa kwa nguvu na kuharibiwa, kisha wanajidai kuwa wao ni mabingwa
wa kugombania haki za binadamu.
Alipotoka kwenda sokoni
Siku ya pili baada ya kuwa
Khalifa wa Waislamu, Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alitoka kuelekea sokoni
huku akiwa amebeba rundu la nguo.
Omar bin Khataab na Abu
Ubaida (Radhiya Llaahu ‘anhu) walipomwona katika hali hiyo wakamuuliza;
"Unakwenda wapi ewe
Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Akawajibu;
"Naelekea sokoni".
Omar akamuuliza;
"Unakwenda kufanya nini
sokoni na umepewa u Khalifa juu ya Waislamu?"
Abubakar akajibu;
"Wanangu nitawalisha nini?"
Omar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
akatoa akasema;
"Itakuwa bora kama tutashauriana na masahaba wa Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) waweze kumjaalia Khalifa wa Waislamu malipo maalum ili aweze
kujihusisha na matatizo ya Umma".
Masahaba wote wakakubali
ushauri huo.
Hali chakula cha haramu
Alikuwa akihiyari kufunga
mawe tumboni pake, yamsaidie asihisi njaa kuliko kuingiza tumboni mwake chakula
cha haramu.
Katika Sahihul Bukhari
imeelezwa kuwa;
'Abubakar(Radhiya Llaahu
‘anhu) alikuwa na mfanyakazi, kijana mdogo, na siku moja kijana huyo alikuja na
chakula na kumkaribisha Khalifa wa Waislamu (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekipokea
na kula.
Yule kijana akamuuliza
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu);
'Unajuwa kitu gani ulichokula
ewe Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)?"
Abubakar(Radhiya Llaahu
‘anhu) akauliza;
'Kitu gani?"
Yule kijana akajibu;
"Hapo zamani, zama za
ujahilia (kabla ya kuwa Muislamu), niliwahi kumtabiria mtu, na mimi sijui
chochote kuhusu utabiri wakati huo, nilimdanganya tu, na tokea siku ile
sijaonana na mtu huyo isipokuwa leo, akanipa zawadi yangu (malipo yangu),
na.'zawadi yenyewe ni hicho ulichokula."
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akaingiza mkono wake kinywani na kuanza kujitapisha kwa nguvu, na yule
kijana akamwambia;
'Mungu akurehemu! Yote haya
(unafanya) kwa sababu ya tonge moja tu?'
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akamwambia;
'Wallahi kama haiwezekani
kukitoa mpaka niitoe roho yangu basi nitafanya hivyo, maana nilimsikia Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akisema; "Sehemu yoyote
ya mwili iliyojengeka kwa mali
ya haramu basi Motoni ndipo panapostahiki kuingizwa mwili huo, na mimi naogopa
isiongezeke sehemu yoyote ya mwili wangu kwa tonge hili".
Wakati majeshi ya Waislamu
yalipokuwa yakisonga mbele kuyashinda majeshi ya Kirumi na kuteka nchi baada ya
nchi, huku mali nyingi za ngawira zikiletwa Madina, Abubakar hakuyumbishwa wala
kubabaishwa na yote hayo, bali aliendelea kuhukumu kwa uadilifu na kuishi
maisha yale yale na kuvaa nguo zile zile na kula chakula kile kile alichokuwa
akila kabla ya kuwa Khalifa.
Alipofariki dunia Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) aliwacha vitu vifuatavyo;
Ngamia aliyekuwa akimbebea
maji, chombo cha kukamulia maziwa ya mnyama, na jokho alokuwa akilivaa
anapopokea wajumbe kutoka nje, na alipoviona vitu hivyo Omar (Radhiya Llaahu
‘anhu) alilia sana
kisha akasema:
"Wallahi umekwisha wapa
taabu kubwa watakaokuja kuhukumu baada yako."
Alikuwa akisema;
Siku ile alipobashiriwa Pepo
na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) alisema;
"Wallahi siamini kuwa
nitaepukana na adhabu ya Mwenyezi Mungu, hata kama
mguu wangu mmoja utakuwa ushaingia Peponi, huenda nikawa nimemkosea huyu au
yule, kisha uje kutolewa mguu wangu Peponi na kuingizwa Motoni."
Rabia Al Aslamiy (Radhiya
Llaahu ‘anhu) anasema;
"Siku moja nilikuwa
nikijadiliana na Abubakar(Radhiya Llaahu ‘anhu), akaniambia neno
lililonichukiza, kisha akajuta na kuniambia;
'Ewe Rabia nirudishie kama nilivyokwambia, upate kulipa kisasi chako'
'Nikamwambia;
Sitofanya hivyo'
Akenda kwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na mimi nikamfuata, hata watu
wakashangaa wakasema;
'Vipi huyu mtu, yeye
anakukosea kisha anakwenda kukushitaki?"
Nikawambia, 'Huyu ni Abubakar
….'
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaniuliza;
'Ewe Rabia, kuna nini baina
yako na Abubakar?'
Nikamwambia;
'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu,
yeye aliniambia neno lililonichukiza akataka nimrudishie ili nimlipize kisasi,
nikakataa'.
Mtume akaniambia;
'Ahsante (umefanya vizuri)
ewe Rabia, usimrudishie, lakini sema;
'Mungu akusamehe ewe
Abubakar'
Nikasema, ' Mungu akusamehe
ewe Abubakar', Abubakar akaondoka huku analia".
Musnad Imam Ahmed
Khalid Mohammad Khalid katika
kitabu cha 'Khulafaa Rasuul', anasema;
"Neno moja tu ulimi
uliteleza akalitamka. Halikuwa neno ovu, kwa sababu Abubakar haiwezekani atamke
neno ovu, lakini neno hilo
lilimchukiza Rabia likamsituwa na kumhuzunisha Abubakar aliyeshikilia kuwa
lazima alipizwe kisasi.
Na kwa nini asifanye hivyo
wakati aliwahi kumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) akifanya hivyo hivyo siku ile alipokuwa akiwapanga majeshi ya Waislamu
katika vita, na kwa bahati mbaya alimpiga mtu mmoja kwa nguvu tumboni pake, na alipohisi kuwa pigo hilo limemuumiza
mtu huyo, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipandisha
nguo yake na kulifunua tumbo lake na kumtaka mtu yule amrudishie kama
alivyompiga."
Mkamuaji maziwa
Kabla ya kupewa Ukhalifa,
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akipenda kwenda kuwasaidia masikini na
wazee na vilema, akiwapikia na kuwaoshea vyombo vyao na hata kuwakamulia
maziwa.
Siku moja baada ya kuwa
Khalifa wa Waislamu, alikwenda kuwatembelea baadhi ya wale masikini aliokuwa
akiwatumikia, na mara baada ya kugonga mlango wa mojawapo ya nyumba hizo mtoto
mdogo alifungua, na alipoulizwa na mamake ;
'Nani anayegonga mlango
mwanangu?'
Mtoto akajibu;
'Mkamuaji maziwa amekuja,
mama'
Mama alipomwona Abubakar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akastuka na kusema;
'Mwanangu, sema 'Khalifa wa
Waislamu'.
Abubakar(Radhiya Llaahu
‘anhu) akasema;
'Mwache, kwani ameniita kwa
jina ninalolipenda kuliko yote'
Alikuwa akiwapenda masikini
na akipenda kuwatumikia, na alikuwa akiwapenda watumwa na aliwakomboa wengi kwa
mali
yake.
Alimkomboa Amer bin Fuhayra,
Zubeir, Um Absi na mwanawe, na wengi katika Masahaba waliokuwa wakiteswa na
makafiri wakati ule, na siku ile alipomkomboa Bilal bin Rabah (Radhiya Llaahu
‘anhu) aliambiwa na kafiri aliyekuwa akimtesa na kumuadhibu;
'Ungenambia huna isipokuwa
vijisenti kidogo tu, basi ningekuuzia'
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akamjibu;
'Wallahi ungelitaka hata
riali mia za dhahabu basi ningelikulipa'.
Huyu ndiye Abubakar(Radhiya
Llaahu ‘anhu) aliyekuwa mwingi wa huruma, mwingi wa kuona haya, hasa
anaposifiwa mbele ya watu, alikuwa akisema;
"Mola wangu nijaalie
niwe bora kuliko wanavyonifikiria na unisamehe kwa yale wasiyoyajua juu yangu
na usinihisabie kwa wanayoyasema."
Na Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) alisema juu yake;
"Mwenye huruma kupita
wote katika umma wangu Abubakar"
Imam Ahmed na Ibni Haban.
Kufariki kwake
Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) alikuwa Khalifa wa mwanzo wa Waislamu na alikuwa amiri wa mwanzo
aliyetumwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu kuongoza msafara wa Hija katika mwaka wa
tisa wa Hijri, na alikuwa wa mwanzo kuikusanya Qur-ani na kuiandika katika
kitabu kimoja baada ya hapo mwanzo kuwa iliandikwa ndani ya majani, mifupa,
vigogo vya miti nk.
Alikuwa akiruhusiwa na Mtume
wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) yeye na Omar bin Khattab (Radhiya
Llaahu ‘anhu) kutoa fatwa hata wakati wa uhai wake Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam).
Alifariki dunia siku ya
Jumatatu mwezi 13 Jamadil akher mwaka wa 13 wa Hijri mwafaka na mwezi wa Agosti
mwaka wa 634 akiwa na umri wa miaka 63, na baba yake alifariki baada yake kwa
kiasi cha miezi sita.