021 - Hadiyth Ya 21: Kumpendelea Kheri Ndugu Yako Muislamu Kama Unavyojipendelea Nafsi Yako


 
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يُحِبَّ لإِخِيهِ مَا يُحِبُّ لِنَفْسِهِ)) متفق عليه
 
Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه)   kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye anayojipendelea nafsi yake)).[1]
 
 
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
 
  1. Uislamu unasisitiza Waumini kupendana na kuungana, na unapendelea ummah uwe mmoja wenye nguvu. [Aal-‘Imraan 3: 200].
 
  1. Iymaan zinatofautiana kwa daraja, Waumini wengineo Iymaan zao ni kubwa kabisa kiasi cha kumpendelea mwenziwe anayojipendelea nafsi yake. Nayo si sifa nyepesi kuimiliki.
 
 
 لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٩٢﴾
 
Hamtoweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachotoa basi hakika Allaah kwacho ni ‘Aliym (Mjuzi wa yote daima)[2]
 
  1. Waumini wapendeleane kheri daima, wakirimiane na waoneane huruma.
 
  1. Muumin daima awe ni mwenye kumnufaisha mwenziwe na jambo lao liwe moja katika kumtii Allaah (سبحانه وتعالى). [At-Tawbah 9: 71]. [Rejea Hadiyth namba 21, 22].
 
  1. Muumin ayachukie maovu kumfikia mwenziwe kama anavyochukia kumfikia mwenyewe.
 
  1. Muumin asiwe na sifa ya uchoyo, bali ajikhini nafsi yake kwa ajili ya nduguye. [Al-Hashr 59: 9].
 
  1. Sifa ya kumpendelea mwenzio imesawazishwa na Iymaan kwa maana kuwa ikiwa Muislamu hatompendelea nduguye anachokipendelea yeye, basi Iymaan yake itakuwa na utata.



[1]  Al-Bukhaariy na Muslim.
[2]  Aal-‘Imraan (3: 92).