Sehemu ya Kwanza

Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Llahu ‘anhu)
Khalifa wa tatu wa tatu aliyeongoka

Jina na Nasaba yake


Jina lake ni ‘Uthmaan bin ‘Affaan bin Abi l Aas bin Umayyah bin Abdul Shams bin Abdu Manaf (Radhiya Llaahu ‘anhu). Anatokana na kabila la Quraysh, naye ni Khalifa wa tatu mwongofu wa Waislamu. Uhusiano wake na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) unakutana katika babu yake wa pili Abdu Manaf.
Alizaliwa mji wa Taif katika mwaka wa sita baada ya mwaka wa Tembo. (Mwaka ule As-habul fiyl walipokwenda Makkah pamoja na tembo wao wakitaka kuibomoa Al Kaaba, na Mwenyezi Mungu akawaangamiza).
Baba yake ni Affan bin Abi l Aas aliyefariki dunia kabla ya kupewa utume Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Kwa hivyo hakuwahi kusilimu. Mama yake ni Arwa binti Kurayz bin Rabia bin Habib bin Abdul Shams bin Abdi Manaf.
Mama yake ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alisilimu, akahajir kwenda Madiynah, akafungamana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Aliishi Madiynah mpaka alipofariki dunia wakati wa Ukhalifa wa mwanawe ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Ama bibi yake, (mama wa mamake), anaitwa Um Hakim bint Abdul Muttalib, huyu anakuwa shangazi lake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alisilimishwa na Abu Bakr  Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu) tokea siku ya mwanzo. Siku ile aliposilimu Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) kisha akamwendea ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumjulisha juu ya dini hii tukufu, na  Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakupata taabu kumsadikisha ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na wote kwa pamoja  wakamwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuzitamka shahada mbili mbele yake.

‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mcha Mungu sana, na mtoaji katika njia ya Mwenyezi Mungu bila kiasi, na alikuwa mwingi wa haya. Akijulikana pia kwa jina la ‘Dhu Nnuraiyn’ na maana yake ni Mwenye Nuru mbili, kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimuwozesha binti zake wawili; Mabibi Ruqayya na Ummu Kulthum (Radhiya Llaahu ‘anhumaa), mmoja baada ya mwengine, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alihuzunika sana baada ya kufariki mkewe wa pili Bibi Ummu Kulthum (Radhiya Llaahu ‘anha) na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akipita alimuona akilia kwa huzuni kubwa, akamuuliza;
"Kipi kinachokuliza ewe ‘Uthmaan?"
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu;
"Nalia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa sababu kumekatika kunasibiana kwangu na wewe."
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia;
"Usilie ewe ‘Uthmaan, naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, lau kama nina mabinti mia wanakufa mmoja baada ya mmoja, basi ningekuozesha nao mpaka wasibaki katika mia hao hata mmoja."
Attabarani na wengine
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ameoa nuru mbili, amehajiri Hijra mbili, (ya kwanza alipokwenda Uhabeshi na ya pili Madiynah), na amesali kuelekea kibla mbili.
Mwenyezi Mungu Anasema;
“Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye mahala anapouweka ujumbe wake.”
Mwenyezi Mungu Subahanahu wa Taala amemchagua kipenzi chake na mbora wa viumbe vyake Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa Mtume wake wa mwisho, akawachagua Maswahaba watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum) kuwa Maswahibu wake watakaosimama naye tokea siku za mwanzo na kuuendeleza ujumbe wake baada ya kufa kwake.
Mwenyezi Mungu Anasema;
“Na kumbukeni (enyi Waislamu) mlipokuwa wachache, mkionekana madhaifu katika ardhi, mkawa mnaogopa watu wasikunyakueni, akakupeni mahali pazuri pa kukaa (Napo ni hapa Madiynah) na akakutieni nguvu kwa nusura yake, na akakupeni riziki nzuri ili mupate kushukuru”
Al Anfal - 26
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa miongoni mwa wachache hao waliotangulia kumsadiki na kumfuata Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kusimama naye na kumsaidia kwa hali na mali. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamvisha nishani Swahaba wake huyu si kwa kumuozesha binti zake wawili tu, bali mara nyingi alikuwa akimsifia kwa sifa njema mbali mbali.

Malaika wanamsitahi


Anasema Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anha);
“Siku moja Abu Bakr  alitaka ruhusa ya kuingia nyumbani, na wakati huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa amekaa huku akiwa ameegemea ukuta na nguo yake ilikuwa imepanda kidogo juu ya goti lake, akamruhusu Abu Bakr  aingie. Akazungumza naye. Kisha Abu Bakr  akatoka lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakujishughulisha na kujifunika goti lake.
Haukupita muda ‘Umar bin Al-Khattwwaab naye akataka ruhusa, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamruhusu aingie. Akazungumza naye kisha akatoka. Lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu aliendelea kukaa mkao ule ule huku akiwa ameegemea ukutani wala hakujishughulisha kuiweka nguo yake vizuri.
Haukupita muda ‘Uthmaan naye akagonga mlango na kutaka ruhusa ya kuingia. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikaa vizuri kwanza, akaiteremsha nguo yake na kulifunika goti lake vizuri, kisha akamruhusu ‘Uthmaan aingie”.
Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anha) akiendela kuhadithia anasema:
“Nikashangazwa na yale aliyotenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuiweka nguo yake vizuri na kulifunika goti lake pale alipoingia ‘Uthmaan, wakati walipoingia Abu Bakr  na ‘Umar hata hakushughulika. Nilipomuuliza sababu ya kufanya vile, akanijibu;
“Hakika ‘Uthmaan ni mwingi wa kuona haya, na kama ningelikaa vile vile bila kulifunika goti langu basi asingeingia. Na hata kama angeingia angeshindwa kunielezea haja yake. Ewe ‘Aaishah kwa nini nisimsitahi mtu ambaye hata Malaika wanamsitahi?”
Ahmad bin Hanbal na Abu Is- haq
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) angeliondoka duniani akiwa na sifa hiyo tu ya kusitahiwa na Malaika pamoja na kusitahiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), basi zingelimtosha, lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amemtunukia sifa nyingi sana pamoja na kumbashiria Pepo ya Mwenyezi Mungu.

Bishara ya kuingia Peponi


Anasema Abu Musa Al Asha-ary;
“Siku moja nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiingia penye bustani iliyozungushiwa ukuta na ndani ya bustani hiyo pana kisima. Nikasema; 'Leo mimi nitakuwa mlinzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Nikamuona akielekea kisimani, akakidhi haja kisha akakaa juu ya kisima huku akining’iniza miguu yake.
Akaja Abu Bakr  na kutaka ruhusa ya kuingia, nikamwambia; “Hapo hapo ulipo. Ngoja kwanza nikakuombee ruhusa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu”.
Nikamwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia;
“Abu Bakr  anataka ruhusa ya kuingia”,
Akaniambia;
“Mwache aingie na umpe bishara kuwa ataingia Peponi”.
Nikafanya hivyo.Akaingia na kukaa juu ya kisima kuliani kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) huku akining’iniza miguu yake kama alivyofanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Mlango ukagongwa tena. Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu.
Nikauliza;
“Nani?”
“‘Umar bin Al-Khattwwaab”,
Nikamwambia;
“Hapo hapo ulipo. Usiingie mpaka kwanza nimjulishe Mtume wa Mwenyezi Mungu”.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaniambia;
“Mruhusu aingie na mpe bishara kuwa ataingia Peponi”.
Nikafanya hivyo, na ‘Umar naye akaingia na kukaa juu ya kisima kushotoni kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaning’iniza miguu yake kama walivyofanya wenzake.
Haujapita muda, mlango ukagongwa tena; Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu.
“Nani?”
“‘Uthmaan bin ‘Affaan”.
Nikamwambia; “Hapo hapo ulipo. Usiingie mpaka kwanza nimjulishe Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)”.
Nilipomjulisha, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akanyamaza  muda kidogo, kisha akaniambia;
“Mruhusu aingie na mpe bishara kuwa ataingia Peponi lakini baada ya kupambana na mtihani mkubwa”.
Nilipomwambia hivyo, ‘Uthmaan akasema;
“Allaahul Mustaan”, (na katika riwaya nyengine alisema; “Tutakuwa na subira InshaAllaah”), kisha akaingia, lakini ‘Uthmaan hakupata pa kukaa, akenda upande wa pili akakaa akiwa amekabiliana nao."
Anasema Abu Musa (Radhiya Llaahu ‘anhu);
“Nikahisi kama hivi ndivyo makaburi yao yatakavyokuwa, na nikatamani ndugu yangu naye aje”.
Al-Bukhaariy

Anabashiriwa kufa Shahidi


Katika hadithi iliyosimuliwa na Sahal bin Saad (Radhiya Llaahu ‘anhu), anasema;
“Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa juu ya Jabali Uhud pamoja na Abu Bakr  na ‘Umar na ‘Uthmaan, jabali likatikisika, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawa analigusa jabali huku akiliambia;
“Tulia ewe Uhud, kwani juu yako yupo Mtume na Asw-Swiddiyq, na Mashahidi wawili (Watu wawili watakaokufa shahid).”
Imam Ahmad
Na hapa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anawabashiria Swahaba zake wawili ‘Umar na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhumaa) kuwa watakufa vifo vya shahidi.

Kisima cha Roma


Walipohamia Madiynah, Waislamu walikabiliwa na tatizo kubwa sana la maji ya kunywa, kwani hapakuwa na maji ya kutosha, na kisima cha pekee chenye maji mazuri na mengi kilichokuwa kikijulikana kwa jina la Kisima cha Roma, kilikuwa kikimilikiwa na Myahudi mmoja aliyekuwa akiwauzia Waislamu maji hayo kiriba kimoja kwa gao la ngano au kwa nafaka yoyote nyengine.
Waislamu waliohamia Madiynah na kuacha mali zao zote huko Makkah wengi wao hawakuwa na uwezo wa kuyapata maji hayo kwa sababu hawakuwa wakimiliki hata ngano ya kula. Kwa ajili hiyo wakawa katika taabu na mashaka makubwa sana.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
“Atakayekinunua kisima cha Roma na kuwaruhusu Waislamu kunywa maji yake bila malipo yoyote, ataingia Peponi”.
Al-Bukhaariy
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwendea Myahudi yule na kumtaka amuuzie kisima hicho, Myahudi akakubali kwa sharti kuwa anunue nusu ya kisima na wawe wakichota kwa zamu, siku moja zamu ya ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na siku moja zamu ya Myahudi.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akakubali na kukinunua kisima hicho kwa Dirham elfu kumi na mbili. Ikisha akawapa Waislamu wachote maji bure. Wakawa katika siku ya zamu yao wanachota maji ya kuwatosha muda wa siku mbili, na kwa ajili hiyo siku ya zamu ya Myahudi hapakuwa na mnunuzi wa maji yake.
Myahudi alipoona kuwa maji yake hayanunuliwi tena, na alipotambua kuwa amewezwa, akakubali kumuuzia ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) nusu yake (sehemu yake) kwa Dirham elfu nane, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akakinunua kisima chote na kuwaachia Waislamu wachote maji watakavyo bila ya malipo yoyote.
Hakuwa akipata malipo yoyote kwa hesabu za kidunia, lakini bila shaka kwa Mwenyezi Mungu ujira wake ni mkubwa sana.

Upanuzi wa Msikiti


Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipotamani kuupanua msikiti wake baada ya kuona idadi ya wanaosali inaongezeka, akauliza;
“Nani atakayeupanua msikiti wetu?”
Kama kawaida ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajitokeza na kukinunua kipande cha ardhi jirani na msikiti na kukiunganisha na msikiti huo.

Fungamano la chini ya Mti


Katika mwaka wa sita wa Al Hijra, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliondoka Madiynah kuelekea Makkah akiwa pamoja na Maswahaba wengi (Radhiya Llaahu ‘anhum) kwa ajili ya kufanya ibada ya Umra.
Maquraysh walituma wajumbe kumtahadharisha asiingie Makkah, lakini kwa vile nia yake ilikuwa ni kufanya Umra na si kupigana vita, hakuona sababu yoyote ya kumzuwia asikamilishe safari yake hiyo.
Maquraysh wakamtuma mjumbe wao Urwa bin Mas’uud amuonye Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa mara ya mwisho kuwa asiporudi alikotoka atapigwa vita, lakini baada ya kuonana naye na kuwaona namna gani Swahaba zake (Radhiya Llaahu ‘anhu) wanavyompenda na kumlinda, Urwa alirudi Makkahh na kuwaambia wenzake:
 “Nimemuona Muhammad akiwa na Sahibu zake nikazungumza nao. Wallahi Muhammad anapendwa na sahibu zake kupita kiasi. Anapotawadha wanafanya kila njia ili wata wadhe kama yeye. Anaposema, wote wananyamaza kumsikiliza, tena hawamkodolei macho kwa kumtizama moja kwa moja (bali wanamtazama kwa heshima kubwa). Watu wa aina gani hawa! Wallahi nishawahi kuwatembelea wafalme na nishamtembelea Qaysar (mfalme wa Warumi) na Kisraa (mfalme wa Fursi - Iran) na Annajashi (mfalme wa Uhabeshi), Wallahi sikumuona hata mfalme mmoja anayeheshimiwa kama anavyoheshimiwa Muhammad na Sahibu zake. Sidhani kama watu wake wanaweza kumuasi abadan. Kwa hivyo fanyeni vile mnavyoona sawa.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamtuma Swahaba mmoja aitwaye Khuraash Al Khuzaaiy (Radhiya Llaahu ‘anhu), akampa ngamia wake aitwaye Thaalab aende kuwaeleza Maquraysh juu ya kusudi lake na kuwa hakuja kupigana vita, lakini Maquraysh walimchinja ngamia huyo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), wakataka kumuuwa Khurash (Radhiya Llaahu ‘anhu) lakini masikini wa pale Makkah wakasaidia akaweza kukimbia na kurudi kwa wenzake.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaamua kumchagua mjumbe mwenye nguvu na hekima pamoja na uwezo mkubwa wa kuweza kujadiliana na Maquraysh. Akamwita ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
“‘Umar! Nakutaka wewe uende Makkah ukajaribu kulitatua tatizo hili.”
‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hapana aliyebaki huko Makkah katika watu wa kabila langu. Na unajua namna gani Maquraysh wanavyonichukia. Kusema kweli mimi sitofaa katika jukumu hili, lakini nitakujulisha juu ya mtu aliye bora kuliko mimi. Nitakwambia ni nani hasa anayefaa katika kazi hii muhimu ya kuleta suluhu baina yetu – Mpeleke ‘Uthmaan bin ‘Affaan”.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akalikubali shauri hilo akamtuma ‘Uthmaan kwenda Makkah, na alipokuwa akiingia mjini Makkah alikutana na mmoja katika jamaa zake aitwaye Aban bin Saeed bin Aas, akamsalimia na kufuatana naye mpaka kwa Abu Sufyan aliyekuwa mkuu wa Maquraysh wakati huo.
Alipokuwa akiingia Makkah, ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akitembea huku akiitizama Al Kaaba, na Maquraysh wakamwambia;
“Kama unataka unaweza kwenda kutufu”.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwaambia;
“Siye mimi nitakayetufu kabla ya Mtume wa Mwenyezi Mungu”.
Mazungumzo baina yake na Maquraysh yalichukuwa muda mrefu na ‘Uthmaan akachelewa kurudi kwa wenzake. Wakati huo huo uvumi ukaenea kuwa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ameuliwa.
Zilipofika habari hizi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), alisimama chini ya mti akawaita Maswahaba wake (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kuwaarifu kuwa anataka kupigana vita na Maquraysh.
Maswahaba wote (Radhiya Llaahu ‘anhum) wakafungamana naye chini ya mti huo katika fungamano la kumridhisha Mola (Bay-atul Ridhwan), lililokuja kujulikana pia kwa jina la ‘Fungamano la kifo,’ kwa sababu walifungamana naye huku wakitoa ahadi kuwa wako tayari kupigana mpaka kufa, na kwamba hawatorudi nyuma watakapopambana na adui.
Mwenyezi Mungu akalitaja tukio hilo katika Qur-aan tukufu Aliposema;
"Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waislamu walipofungamana nawe chini ya mti na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao na akawapa kushinda kwa zama za karibu".
Al Fat-h – 18
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye kwa ajili yake kufungamana huko kulitokea alikuwa Makkah wakati ule na kwa ajili hiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliunyayua juu mkono wake wa kulia kisha akauingiza ndani ya mkono wake wa kushoto huku akisema;
“Na huu ni mkono wa ‘Uthmaan.”
Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) wakasema;
“Mkono wa ‘Uthmaan ukawa mtukufu kupita mikono yetu sote”.
Haukupita muda mrefu ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akarudi, na ikajulikana kuwa ule ulikuwa ni uvumi tu.
Hata hivyo kufungamana huko pamoja na ahadi waloitoa Waislamu siku hiyo mbele ya Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuliwatisha sana Maquraysh. Wakamtuma mwenzao aitwaye Suheil bin Amr aandikiane nao mkataba wa sulhu uliokuja kujulikana kwa jina la ‘Masikilizano ya Hudaybiyah’ (Sulhul Hudaibiya).
Huyu ndiye ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), ambaye kwa ajili yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alifungamana na Waislamu Fungamano la kifo, na kwa ajili yake zikateremshwa aya zikieleza juu ya radhi za Mwenyezi Mungu alizowateremshia Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum).
Al-Bukhaariy – Muslim – At-Tirmidhiy

Jeshi la wakati wa dhiki


Katika mwaka wa tisa wa Hijri, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipata habari kuwa Mfalme wa Warumi ‘Heracleus’ akishirikiana na baadhi ya makabila ya kiarabu waliokuwa wakifuata dini ya Manasara walikuwa wakijitayarisha kuwashambulia Waislamu na kuiteka nchi ya Hijazi pamoja na kuingia Makkah na Madiynah.
Wakati huo Waislamu walikuwa katika shida kubwa sana. Hali zao hazikuwa nzuri na wengi katika wapiganaji wao hawakuwa na uwezo wa kununua wanyama wa kupanda kwa ajili ya kuwapeleka vitani, wala hawakuwa na uwezo wa kununua vifaa pamoja na silaha za kupigania vita. Isitoshe, safari ya kwenda kupambana na Warumi katika mji wa Tabuk ilikuwa ndefu sana tena katika wakati wa joto kali sana. Kwa hivyo mali nyingi ilihitajika kwa ajili ya kutayarisha jeshi kubwa la kupambana na adui.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akapanda juu ya membari ya msikiti wake na kuwajulisha Waislamu juu ya nia yake hiyo, na kuwataka Waislamu wajitayarishe, na wenye uwezo wasaidie kwa mali zao.
Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) walikimbilia kutoa misaada, kila mmoja kiasi alichoweza. Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) alitoa kila alichomiliki, ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) alitoa nusu ya mali yake, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alitoa siku hiyo mpaka Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akateremka kutoka juu ya membari na kusimama mbele yake huku akisema;
“Mola wangu uwe radhi na ‘Uthmaan, maana mimi niko radhi naye”.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alijitolea mali nyingi na wanyama wengi wa kupanda na wa kuchinja. Ikawa kama kwamba ni yeye peke yake aliyelitayarisha jeshi hilo.
Alitoa ngamia mia tisa na hamsini, farasi hamsini, kisha akaingia chumbani kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuziweka mbele yake Dinari elfu moja, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ambaye hasemi isipokuwa yale aliyofunuliwa akasema huku uso ukimeremeta kwa furaha;
“Hawezi kutenda madhara yoyote ‘Uthmaan baada ya leo”.
Na akasema;
“Kila aliyetoa mchango katika kulitayarisha jeshi la wakati wa dhiki (Jayshul ‘usra), ataingia Peponi”.
Al-Bukhaariy
Hii ndiyo daraja ya Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na huu ndio ukweli wao, imani zao, ushujaa wao, kumpenda kwao Mola wao Subhanahu wa Ta’ala, kumpenda Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kuipenda dini yao na kutokujali kwao hali zao, mali zao, watu wao wala hata roho zao mbele ya kuipigania dini ya Mola wao Subhanahu wa Ta’ala.
Walitoa mali wa hiari zao na wakajitolea nafsi zao kwa kuingia vitani tena katika wakati wa joto kali sana, wakati unaojulikana kuwa ni mzuri kwa kuvuna tende pale Madiynah.
Walisamehe kuvuna tende zao, wakasamehe kukaa majumbani mwao pamoja na watoto wao na mali zao wakiwa katika usalama mbali kabisa na kuhatarisha kukatwa vichwa vyao katika vita, wakaziona raha zote hizo kuwa ni upuuzi mbele ya Pepo ya Mola wao waliyokuwa wakiikimbilia.
Kwa ajili hii wakastahiki sifa walizopewa na Mola wao Subhanahu wa Ta’ala Aliposema;
“Wala hawatowi kinachotolewa chochote, kidogo wala kikubwa, wala hawapiti bonde lolote (katika kwenda vitani) ila wanaandikiwa ili Mwenyezi Mungu awalipe (malipo) mema ya yale (mambo) waliyokuwa wakiyatenda.”
At Tawba – 121

Biashara na Mola Wake


Wakati wa Ukhalifa wa Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) paliwahi kutokea shida na njaa iliyosababishwa na ukame, na watu walipokwenda kwa Khalifa  Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) kumshitakia hali zao akawaambia;
“Inshaallah kesho haitofika isipokuwa mtakuwa mumeshapata faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu”.
Ilipoingia asubuhi ya siku ya pili, uliwasili Madiynah msafara wa biashara wenye ngamia elfu waliobeba vyakula vingi, vyote vikiwa milki ya ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na matajiri walipomwendea kutaka kuinunuwa mali hiyo, akawauliza;
“Ngapi mtanipa”
Wakasema;
“Kwa kila kumi uliyonunulia tutakulipa kumi na mbili”.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawaambia;
“Yupo atakaenipa faida kubwa kuliko hiyo”
Wakamwambia;
“Basi kwa kila kumi tutakupa kumi na tano"
Akasema;
“Yupo atakaenipa zaidi kuliko hizo”.
Wakamwambia;
“Nani atakayekupa faida hiyo wakati wafanya biashara wa Madiynah wote ndiyo sisi hapa, hapana asiyehudhuria?”
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawaambia;
“Mwenyezi Mungu atanipa kwa kila Dirham moja mara kumi zaidi; 'Mola wangu! mali yangu yote nimejitolea kuwapa masikini wa Madiynah bila malipo yoyote”.
Huyu ndiye ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa akiwalisha watu chakula cha wafalme wakati  yeye mwenyewe alikuwa akila mkate kwa mafuta yaliyochanganywa na siki.
Anasema ‘Abdullaah bin Shaddad (Radhiya Llaahu ‘anhu)
“Nilimuona ‘Uthmaan akihutubia siku ya Ijumaa akiwa amevaa nguo yenye thamani ya Dirham nne au tano, na wakati huo yeye ndiye Khalifa wa Waislamu”.

Mhamiaji (Muhajir)


Jambo la mwanzo kufaridhishwa katika dini lilikuwa Uhamiaji, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), alistahiki kupewa sifa hiyo ya Uhamiaji, kwani alikuwa Mhamiaji kwa kila maana na sifa inayobeba jina hilo. Na hii ni kwa sababu ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwa Mhamiaji aliyehama kutoka Makkah kwenda Uhabesi na kutoka Makkah kwenda Madiynah tu, bali alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuuhama ukafiri na kujiunga na watu watano au sita wa mwanzo waliomtangulia kuingia katika dini hii tukufu. Aliuhama ukafiri juu ya kuelewa kwake kuwa ile heshima kubwa aliyokuwa nayo mbele ya Maquraysh sasa itaondoka, utajiri wake utaanza kupigwa vita, na jamaa zake hawatomuacha astarehe, bali watamtenga na kumuadhibu.
Ami yake Al Hakam bin Abil Aas ndiye aliyechukua jukumu la kumuadhibisha, alikuwa akimfunga kwa minyororo na kumtesa huku akimpigia kelele na kumwambia;
“Unaiacha dini ya baba zako na kufuata dini hii mpya? Wallahi sitokufungua iwapo bado utaendelea kuifuata dini hii”.
‘Uthmaan akawa anamjibu kwa kumwambia;
“Wallahi sitaiacha dini ya Allaah abadan”.
Akawa anaendelea kumuadhibu na yeye anaendelea kukataa, na huku Maquraysh wakimfanyia njama mbali mbali huku wakimuonyesha dharau yao juu yake apate kuhisi tofauti iliyopo baina ya pale mwanzo alipokuwa mwenzao walipokuwa wakimpa heshima kubwa, na baada ya kusilimu kwake. Lakini ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakutetereka kwa sababu heshima ya kweli ni ile atakayoipata kwa Mola wake baada ya kuifuata haki, na si heshima atakayoipata kwa Maquraysh iwapo ataiacha haki.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwaonea huruma Swahaba zake kutokana na mateso waliyokuwa wakiyapata kwa Maquraysh, akawataka wahame kwenda nchi ya Uhabeshi. Huko yupo mfalme muadilifu aliyeeneza amani katika nchi yake.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), akawa miongoni wa watu wa mwanzo kuhajiri. Akaondoka akifuatana na mkewe Bibi Ruqayyah (Radhiya Llaahu ‘anha) binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), aliyemuozesha mara baada ya kusilimu kwake, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliagana nao huku akiwatazama kwa jicho la huruma, akasema;
“Hawa ni wahamiaji wa mwanzo baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu Luut”

MchaMungu


Siku moja baada ya kughadhibishwa na mtumishi wake, ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alilikamata sikio la mtumishi huyo na kulivuta. Baada ya ghadhabu zake kutulia na kukumbuka kosa lake, ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimwendea mtumishi yule na kumuamrisha amvute na yeye sikio lake sawa kama alivyomtendea, lakini mtumishi alikimbia na kukataa.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamfuata na kumlazimisha amrudishie kwa kumvuta sikio lake kama alivyomfanyia yeye huku akimwambia;
“Vuta kwa nguvu ewe kijana, kwani kisasi cha duniani ni chepesi kuliko kisasi cha akhera”.
Alikuwa mwingi wa kusali hasa katika nyakati za usiku. Imepokelewa kutoka kwa Abu Ubaida Aamir bin Jarrah (Radhiya Llaahu ‘anhu)  kuwa mara nyengine katika nyakati hizo alikuwa akiusoma msahafu mzima katika usiku mmoja.
Abdlillahi bin ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa kila anapoisoma au kuisikia kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo;
“Je, afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama na kuogopa Akhera na kutarajia rehema ya Mola wake (ni sawa na asiyefanya hayo?) Je, wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojuwa? “ Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu”.
Az Zumar – 9
Kila anapoisikia aya hii Abdullah bin ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akisema;
"Huyo ni ‘Uthmaan".
Ibni abi Hatim

‘Uthmaan na vita

 
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mtu asiyependa vita wala umwagaji wa damu wa aina yoyote ile. Hata hivyo pale inapobidi alikuwa msitari wa mbele kuitikia mwito wa jihadi dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu kwa hali na mali.
Hakupigana vita vya Badr ingawaje alikuwa miongoni mwa wachache waliotoka kwenda kushiriki, na hii ni kwa sababu walipokuwa wakielekea Badr, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimtaka ‘Uthmaan arudi nyumbani kwake Madiynah kwa ajili ya kumuuguza mkewe Bibi Ruqayyah (Radhiya Llaahu ‘anha) ambaye hali yake ilikuwa mbaya sana, na hatimaye akafariki dunia siku ile zilipowafikia habari za ushindi wa Waislamu katika vita hivyo.
Katika vita vya Uhud, ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alishiriki, akapigana, lakini alirudi nyuma pamoja na wenzake pale majeshi ya makafiri yalipofanikiwa kuwazunguka na kuupanda mlima Uhud na kuanza kuwarushia mishale na kusababisha kuuliwa kwa Waislamu wengi.
Katika vita hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwaweka juu ya jabali Uhud watu hamsini waliokuwa mahodari wa kutupa mishale wapate kuwalinda wenzao wanaopigana chini, akawataka wasiondoke hapo iwe itakavyokuwa ili baada ya kumalizika vita hivyo majeshi ya washirikina yasiweze kuwazunguka na kuwashambulia kwa nyuma .
Lakini watupa mishale hao walikwenda kinyume na amri hiyo mara baada ya kuwaona wenzao walioshinda wakianza kuwaendesha mbio washirikina huku wakikusanya ngawira. Baadhi yao isipokuwa watu kumi na nne tu walikhalifu amri hii, wakateremka na kwenda kuwasaidia wenzao katika kuwateka washirikina na katika kukusanya ngawira.
Baadhi ya majemadari wa jeshi la washirikina waliokuwa wakirudi nyuma, walipowaona Waislamu wakiliteremka jabali, wakageuza njia na kulizunguka kwa nyuma, wakalipanda na kuanza kuwashambulia Waislamu kwa kuwamiminia mishale.
Waislamu wengi walikufa na wengine kujeruhiwa, na wengi wengine akiwemo ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakarudi nyuma kwa msituko wa walipoona wenzao wanapukutika, na Mwenyezi Mungu akateremsha kauli yake ya kuwasamehe wale waliorudi nyuma siku hiyo akasema;
"…..Naye sasa amekusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ihsani nyingi juu ya wanaoamini."
Aali Imran - 152
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alishiriki katika vita vyote vilivyobaki walivyopigana Waislamu. Alishiriki katika vita vya Khaybar, vita vya kuuteka mji wa Makkah, vita vya Taif, Howazin, Tabuk na vingi vinginevyo.
Siku ya Hudaybiyah kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa yeye ndiye aliyepewa jukumu la hatari, pale alipochaguliwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwenda Makkah akajadiliane na washirikina, naye akalikubali jukumu hilo kwa ushujaa mkubwa, yakatokea yaliyotokea, na kwa ajili yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwataka Waislamu wafungamane naye chini ya mti, na kwa ajili yake siku hiyo Mwenyezi Mungu aliteremsha aya ya kuridhika na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliofungamana na Mtume wake mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Khalifa wa tatu

 
Alipokuwa akivuta pumzi zake za mwisho, ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikataa kumchagua Khalifa atakayeongoza baada yake juu ya kuwa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) walimshikilia afanye hivyo; ‘Umar aliwaambia;
"Mzigo wenu nimeubeba nikiwa hai, na baada ya kufa kwangu mnanitaka nikubebeeni pia? Ikiwa kuchagua basi amekwisha chagua aliyekuwa bora kuliko mimi - Abu Bakr , na ikiwa ni kuacha basi aliacha kuchagua aliyekuwa bora kuliko mimi - Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na Mwenyezi Mungu ataihifadhi dini yake".
Lakini ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwaita Maswahaba sita; Ali, ‘Uthmaan, Twalha, Al Zubayr, Saad na ‘Abdur-Rahmaan bin Al-’Awf (Radhiya Llaahu ‘anhum) na kuwaambia;
"Nimetazama na nikakuoneni kuwa nyinyi ndio mnaostahiki kuwa viongozi, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipofariki dunia alikuwa radhi nanyi nyote. Mimi sikuogopeeni watu iwapo mtasimama katika njia ya haki, basi nitakapokufa mushauriane muda wa siku tatu, na siku ya nne ikiingia muwe mumekwishamchagua kiongozi kati yenu. Na ahudhurie pamoja nanyi ‘Abdullaah bin ‘Umar akiwa kama ni mshauri tu, lakini yeye hana haki yoyote ya kuchaguliwa kuwa kiongozi".
Twalha hakuwepo Madiynah siku walipokutana, na ‘Abdur-Rahmaan bin Al-’Awf(Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwashauri Maswahaba waliohudhuria kuwa itakuwa bora iwapo mmoja wao atajitoa ili pawezekane kuchaguliwa Khalifa kwa urahisi. Kisha yeye mwenyewe akajitoa, kisha Al Zubeir (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajitoa na Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) pia akajitoa. Wakabaki wawili, nao ni ‘Uthmaan na Ali (Radhiya Llaahu ‘anhumaa), na ‘Abdur-Rahmaan bin Al-’Awf akapewa jukumu la kumchaguwa mmoja kati yao.
Ibni Al-’Awf (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa na kazi kubwa ya kuwashauri Maswahaba wote waliopo Madiynah kwa muda wa siku tatu tu ili aweze kutoa uamuzi wake muhimu.
Anasema Ibni Kathir katika kitabu cha 'Al Bidaya wa Nnihaya';
"‘Abdur-Rahmaan alikuwa na kazi kubwa katika siku tatu hizo ya kuupitia mji wote wa Madiynah na kuwagongea milango watu akiwashauri na kusikiliza rai zao.
Aliwauliza Maswahaba waliokuwa maarufu, watu wa kawaida, wanawake, na ilimbidi wakati mweingine awaulize hata watoto wadogo na wasafiri waliokuwa wakiwasili Madiynah katika siku hizo."
Ibni Kathir anaendelea kusema;
"Kisha ‘Abdur-Rahmaan bin Al-’Awf akawaita ‘Uthmaan na Ali, wakamjia, na yeye akawakabili na kuwaambia;
"Nimewauliza watu wote juu yenu na sikumpata hata mmoja anayekufadhilisheni baina yenu wawili, kwani wote wanataka mmoja wenu awe Khalifa wao."
Kisha ‘Abdur-Rahmaan akawataka watoe ahadi kuwa yeyote kati yao atakayechaguliwa kuwa Khalifa atahukumu kwa uadilifu na yule asiyechaguliwa atatii.
Kisha akatoka pamoja nao na kuelekea msikitini, ‘Abdur-Rahmaan akiwa amevaa kilemba alichopewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) huku akiwa ameufunga upanga wake kiunoni, na alipowasili msikitini akawataka watu wote wakusanyike. Kisha pakanadiwa; "Assalaatu Jaamia", watu wakamiminika msikitini mpaka msikiti ukajaa na kufurika hata ‘Uthmaan hakupata mahali pa kukaa isipokuwa mwisho wa safu, na alikuwa mtu mwenye kuona haya sana.
Kisha ‘Abdur-Rahmaan akapanda juu ya membari ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuomba dua ndefu sana, kisha akasema;
"Enyi watu! Mimi nilikuulizeni kwa siri na kwa dhahiri na sikumpata hata mmoja katika yenu anayemtaka mwengine isipokuwa Ali au ‘Uthmaan. Inuka njoo kwangu ewe Ali".
Ali akainuka na kumwendea, na ‘Abdur-Rahmaan akaushika mkono wake na kumuuliza;
"Je! Upo tayari kufungamana nami kufuatana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake na matendo ya Abu Bakr  na ‘Umar?"
‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Kufuatana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake na Ijtihadi kwa rai yangu".
Kisha akasema;
"Inuka njoo kwangu ewe ‘Uthmaan".
‘Uthmaan akainuka na kumwendea, na ‘Abdur-Rahmaan akaushika mkono wake na kumuuliza;
"Je! Upo tayari kufungamana nami kufuatana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake na matendo ya Abu Bakr  na ‘Umar?"
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Allahumma Ndiyo, nimekubali".
‘Abdur-Rahmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaunyanyua uso wake juu na kutizama juu ya sakafu ya msikiti huku mkono wake ukiwa ndani ya mkono wa ‘Uthmaan kisha akasema;
"Ewe Mola wangu sikia na ushuhudie, mimi nimeitua amana iliyokuwa juu ya shingo yangu na kuiweka juu ya shingo ya ‘Uthmaan".
Watu wakaanza kumkimbilia ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ili wafungamane naye, na mkono wa mwanzo uliofungamana naye ulikuwa mkono wa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu), kisha Waislamu wote waliobaki wakafungamana naye.
Na hivi ndivyo ‘Uthmaan alivyopewa Ukhalifa akiwa na umri unaokaribia miaka sabini".

Hotuba yake ya mwanzo

 
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa msemaji hodari, lakini siku ile alipopanda juu ya membari kutoa hotuba yake ya mwanzo, alishindwa kusema maneno mengi, na badala yake alitamka maneno machache yafuatayo;
"Hakika dunia imejaa ghururi, basi yasikudanganyeni maisha ya dunia wala asikudanganyeni yule mdanganyi mkubwa (Iblisi) katika (mambo ya) Mwenyezi Mungu. Dunia itupeni mbali kama vile Mwenyezi Mungu alivyoitupa na itafuteni akhera yenu, kwani Mwenyezi Mungu ameipigia mfano dunia Akasema;
"Na wapigie mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tunayoyateremsha kutoka mawinguni; kisha huchanganyika nayo mimea ya ardhi kisha ikawa majani makavu yaliyokatikakatika ambayo upepo huyarusha huku na huko. Na Mwenyezi Mungu Ana uweza juu ya kila kitu.
"Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia. Na vitendo vizuri vibakiavyo ndivyo bora mbele ya Mola wako kwa malipo na tumaini bora (kuliko hayo mali na watoto)".
Al Kahf - 45 - 46

Anasema Ibni Kathir katika Al Bidaya wal Nihaya;
"‘Uthmaan ameianza kazi yake ya ukhalifa kwa kuwaandikia wakuu wa mikoa mbali mbali, washika hazina pamoja na majemadari wake akiwanasihi pamoja na kuwaamrisha mema na kuwakataza maovu na akawataka wafuate mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuacha kuzusha mambo mepya katika dini.
Katika utawala wake nyumba ya Hazina ya Waislamu (Baytul Mal), ilijaa mali nyingi, akawaongezea watu mishahara na kuhusisha kiwango maalum cha mali kwa ajili ya kuwalipa na kuwalisha wanaokesha wakifanya ibada na kutafuta elimu misikitini ".

Uasi

 
Mara baada ya ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kukamata hatamu za kuongoza umma, Warumi na baadhi ya Wafursi wakaanza kuvunja mikataba iliyokuwa baina yao na dola ya Kiislamu. Uasi ulianza katika nchi za Azarbeijan na Armenia, na Warumi wakajaribu kuuvamia mji wa Alexandria na Palestine, na moto wa uasi ukaendelea kuwaka mpaka ukafika sehemu za Khurasan na Karman na kwengineko.
Waasi hawakuwa watu wa kawaida wa miji ile, kwani watu wa miji hiyo baada ya kukombolewa na Waislamu kutokana na utawala wa Kirumi na wa Kifursi waliridhika na utawala wa viongozi waadilifu wa Kiislamu. Lakini uasi huo ulitokana na nguvu iliyokuwa ikitawala kabla ya Uislamu, nguvu iliyopoteza ufalme na utawala wake, nguvu iliyokula hasara ya kila kitu baada ya kushindwa na Majeshi ya Kiislamu.
Nguvu hiyo ilipoona kuwa Khalifa mwenye nguvu ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) ameuliwa na kafiri mwenzao, na kwamba Khalifa mzee mwenye umri unaokaribia miaka sabini ndiye aliyetawala, tamaa ikawaingia, wakaona hii ndiyo fursa nzuri ya kuurudisha utawala wao.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwa akijulikana kama ni mtu wa vita kama vile Khalid bin Walid au Sa’ad bin Abi Waqaasau ‘Aliy bin Abi Twaalib(Radhiya Llaahu ‘anhum) na wengineo, bali umaarufu wake ulikuwa juu ya ukarimu na wingi wa kuona haya, na kwa ajili hiyo tamaa ikaingia katika nafsi za waasi, wakadhani kuwa fursa imewadia ya kuurudisha utawala wao.
Lakini mzee huyu anayekaribia umri wa miaka sabini akaona ni vizuri awaoneshe makafiri hawa kuwa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hawapimwi kwa umri wao wala hawakisiwi kwa miili yao, bali vipimo vyao ni Imani iliyojaa nyoyoni mwao, imani yao juu ya Dini yao, juu ya Mola wao na juu ya Mtume wao mtukufu Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoa amri ya kuuzima moto huo wa uasi kwa haraka sana kama ulivyoanza. Si hivyo tu, bali aliyapa majeshi yake amri ya kusonga mbele na kuiteka miji mingine ya Warumi ili wasiipate kwa wepesi fursa nyengine ya kuanzisha uasi kama huo karibu na dola ya Kiislamu.
‘Uthmaan mwenyewe (Radhiya Llaahu ‘anhu) ndiye aliyewachagua wakuu wa majeshi yatakayoifanya kazi hiyo. Jambo la ajabu ni kuwa hapana hata jeshi moja katika majeshi ya ‘Uthmaan yaliyoshindwa katika mapambano hayo isipokuwa katika pambano moja tu.
‘Uthmaan alikuwa akipanga, akifikiri, akikisia kama kwamba amerejeshewa tena ujana wake Radhiyallahu anhu. Na alipoona kuwa ipo haja ya kuunda jeshi la baharia, akaliunda. ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), juu ya ushujaa wake hakujaribu kuchukua hatua kama hiyo ambayo ni ngeni na ingehatarisha usalama wa majeshi ya Kiislamu.
Waislamu walipomuona Khalifa wao akiwa na hamasa, imani pamoja na moyo ule wa kishujaa, wao pia imani yao ikaongezeka nguvu. Wakawa wajasiri zaidi na wenye moyo thabiti.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaanza kwa kutoa amri ya kuushambulia mji wa Azerbeijan, kisha Armenia, ile miji iliyovunja ahadi. Akamchagua Al Walid bin ‘Uqbah (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa mkuu wa majeshi yatakayokwenda huko, na baada ya kuwashinda akafanikiwa kuwafanya waasi hao watie saini (sahihi) mkataba mwingine kama ule waliouvunja.
Walipokuwa wakirudi mji wa Al Kuufa baada ya kuwashinda waasi hao, Al Walid na majeshi yake wakapata habari kuwa majeshi ya Warumi yameanza uchokozi katika miji ya Sham. Ikamfikia amri kutoka kwa Khalifa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa atayarishe jeshi la watu elfu kumi sharti liongozwe na mtu mwaminifu tena mkarimu.
Al Walid (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamchagua mtu mmoja aitwae Habib bin Maslamah al Fahariy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuliongoza jeshi hilo. Habib akaondoka na jeshi lake lisilozidi watu elfu kumi na kupambana na majeshi ya Warumi pamoja na Waturki yasiyopungua watu elfu themanini.
Mke wa Habib alikuwa miongoni mwa wanajeshi hao, na alipomuuliza mumewe kabla ya kuanza vita;
"Tutaonana wapi ikiwa vita vitapamba moto na majeshi kutawanyika?"
Akamjibu;
"Katika hema la mkuu wa majeshi ya Kirumi au Peponi".
Majeshi mawili hayo yakakutana katika mapambano makali, na Habib aliyashinda majeshi ya Warumi na Waturuki kwa pamoja, kisha hakusimama hapo, bali alisonga mbele kuelekea nchi za Warumi huku akizivunja ngome zao moja baada ya moja.

Habari nyengine zikamfikia Khalifa wa Waislamu kuwa majeshi ya baharia ya Warumi yanauvamia mji wa Alexandria huko Misri na kwamba majeshi mengine zaidi yanakuja kutoka Roma kuelekea huko.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuamrisha ‘Amr bin Al-‘Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa Gavana wa nchi ya Misri apeleke jeshi lake Alexandria na ayaangamize majeshi ya Kirumi. Wakati huo huo Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akiuteka mji wa Qansarin, na Majemadari wengine walikuwa wakizima moto ya uasi katika sehemu mbali mbali.
Khalifa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akayaamrisha majeshi yake kwenda Afrika ya Kaskazini chini ya uongozi wa Abdullah bin Saad pamoja na Abdullaah bin ‘Amr na Abdullaah bin Zubayr (Radhiya Llaahu ‘anhu), na baada ya mapambano makali majeshi hayo yakawashinda majeshi ya wabarbari ya Afrika ya Kaskazini.
Jeshi la baharia la Warumi lilokuwepo Cyprus, lilikuwa katika hali ambayo lingeweza kusababisha hatari kwa nchi za Kiislamu, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaona ni bora ahatarishe na kupeleka jeshi la baharia la Waislamu kupambana nalo.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamchagua Muawiya bin Abi Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu), kuwa kiongozi wa jeshi la kuiteka nchi ya Cyprus na akampelekea jeshi lingine likongozwa na Saeed bin Abu Sarh (Radhiya Llaahu ‘anhu) ili washirikiane katika jukumu hilo. Majeshi mawili hayo makubwa yakapambana na hatimaye jeshi la Warumi likasalimu amri na kutia saini (sahihi) mkataba wa sulhu uliowekewa masharti na Waislamu.

Vita hivyo vikafuatiliwa na vita vya Sawariy. Vita ambavyo Constantine, mfalme wa Roma alitayarisha jeshi kubwa sana lisilopata kutayarishwa mfano wake kwa ajili ya kupambana na majeshi ya Kiislamu. Akalipeleka jeshi hilo Morocco pamoja na merikebu mia tano za kivita, na mapambano makali yakatokea huko na hatimaye majeshi ya Kiislamu yakawashinda Warumi katika vita hivi ambavyo watu wengi sana kutoka pande zote mbili walikufa.
Hivi ndivyo ilivyokuwa, mara baada ya kutawala ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu). Majeshi ya Kiislamu yalisonga mbele kila upande na kuyashinda majeshi ya Warumi na ya Wafursi na kufanikiwa kuiteka miji mbali mbali kama vile Constantinople, Karman na kwengineko, na hatimaye kufanikiwa kuuzima moto huo wa uasi.
Yule waliyemdhania kuwa ni mzee na wangeweza kumchezea, aligeuka kuwa simba mshambuliaji.

Msahafu Mmoja

 
Inajulikana kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiteremshiwa Qur-aan kidogo kidogo kutokana na sababu na matukio mbali mbali, na wakati mwingine bila hata sababu wala matukio, wala hakuteremshiwa yote kwa pamoja.
Tunaelewa pia kuwa Qur-aan tukufu imeteremshwa kwa lugha (lahja) ya Ki-Quraysh, na kwamba pale Madiynah yalikuwepo makabila mengine yasiyokuwa ya Ki-Quraysh, na kwa ajili ya kuwarahisishia usomaji wa Qur-aan, Mtume wa mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimuomba Mola wake awaruhusu kuisoma na kuiandika kwa lahja zao mbali mbali. Idadi ya lahja hizo zilikuwa saba, na inaeleweka pia kuwa baadhi ya wale walioandika Qur-aan kwa lahja zao hizo waliieneza kila pembe ya nchi za Kiislamu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa kila anapoteremshiwa Wahyi akiwaamrisha waandishi wake kuandika Wahyi huo mbele yake. Kwa hivyo Qur-aan iliandikwa wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na mbele yake ndani ya sehemu mbali mbali za kuandikia za wakati huo kama vile magamba ya miti, mbao, makozi nk. Na baada ya kuandikwa ikawa inawekwa nyumbani kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) nao pia waliihifadhi Qur-aan kwa moyo na kuisoma majumbani mwao na katika sala zao, na waliokuwa wakijua kuandika waliiandika katika sehemu mbali mbali na kuzihifadhi majumbani mwao pia.
Kwa hivyo Qur-aan iliandikwa tokea wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuhifadhiwa na Maswahaba wengi (Radhiya Llaahu ‘anhum), lakini haikuwa katika kitabu kimoja, bali iliandikwa katika sehemu mbali mbali zilizowarahisikia kuandika.
Alipotawala Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu), alishauriwa na ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aikusanye ile Qur-aan iliyoandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuilinganisha na ile iliyoandikwa na Maswahaba wengine na ile iliyohifadhiwa vifuani mwa waandishi wa wahyi pamoja na Maswahaba wengine wengi (Radhiya Llaahu ‘anhum), na kuijumuisha katika kitabu kimoja.
Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) hapo mwanzo hakupendelea kufanya jambo kama hilo ambalo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakulifanya, lakini hatimaye alilikubali pendekezo hilo la ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumpa Zayd bin Thabit (Radhiya Llaahu ‘anhu) jukumu la kuisimamia kazi hiyo akishirikiana na Maswahaba wenzake kama vile Saeed bin ‘Aas, ‘Abdullaah bin Zubayr, ‘Abdur-Rahmaan bin Al-Haarith na wengineo waliokuwa wakiuandika wahyi huo mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pale ulipokuwa ukiteremshwa.
Alimpa jukumu hilo Zayd (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa sababu yeye ndiye aliyeandika wahyi zaidi kuliko Maswahaba wengine, na alikuwa pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa muda mrefu zaidi kuliko waandishi wa wahyi wenzake.
Baada ya juhudi kubwa sana, Zayd pamoja na wenzake (Radhiya Llaahu ‘anhum) wakafanikiwa kuikusanya Qur-aan na kuiandika yote katika msahafu mmoja, na kuanzia siku hiyo ile Qur-aan iliyoandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) katika sehemu mbali mbali na kuhifadhiwa vifuani mwa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) ikawa imekusanywa na kuandikwa katika msahafu mmoja tu uliopangwa sura zake na aya zake kama alivyowapangia Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Kisha msahafu huo ukawekwa na kuhifadhiwa nyumbani kwa Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu), na baada ya kufa kwake ukawa nyumbani kwa ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye kabla ya kufa kwake alimkabidhi binti yake Hafswa (Radhiya Llaahu ‘anha), mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Wakati huo huo ile misahafu ya mwanzo iliyoandikwa kwa lahja zile saba ilienea na kusomwa na watu katika nchi mbali mbali za Kiislamu, na inajulikana kuwa alipotawala ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) dini ya Kiislamu ilipata nguvu zaidi, na majeshi yao yaliweza kuzishinda nchi mbali mbali na kusonga mbele hadi kufikia Azarbeijan na Armenia na Cyprus, na kuweza pia kuziteka nchi mbali mbali za Asia na za Ulaya na Afrika.
Baadhi ya Maswahaba kama vile ‘Hudhaiyfa (Radhiya Llaahu ‘anhu) walikuwa wakiona mambo ya kiajabu kila wanaposonga mbele kuziteka nchi hizo. Katika nchi ya Syria na Misri kwa mfano, Waislamu walikuwa wakigombana na kushindana kwa kutamba katika usomaji wao wa Qur-aan kila mmoja kwa lahaja yake, kila mmoja akisema kuwa usomaji wake wa Qur-aan ni bora kuliko wa mwenzake na kufikia hadi kukufurishana.
Zilizpomfikia habari hizo, ‘Uthmaan akashauriana na Maswahaba wenzake (Radhiya Llaahu ‘anhum) na wote wakaona kuwa ipo haja kubwa ya kuwaunganisha Waislamu wote wawe wanaisoma Qur-aan kwa msomo mmoja tu na kwa kutumia Lahaja moja tu.
Wakakubaliana wauchukue ule Msahafu uliokusanywa na kuandikwa wakati wa Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kuunukuu kwa kuuandika tena katika misahafu mingine mingi, na wakakubaliana kuwa itumike lugha ya ki Quraysh iliyoteremshiwa Qur-aan, kisha waisambaze misahafu hiyo katika nchi za Kiislamu na kuichoma moto misahafu yote iliyobaki iliyoandikwa kwa misomo na lahaja tofauti ili kuukata mizizi ya fitna kuanzia chanzo chake, mizizi ambayo kama ingeachwa basi mwisho wake usingekuwa mwema.
Ikachaguliwa tume ya waliohifadhi Qur-aan pamoja na wajuzi wa lugha ya kiarabu, wote wakiwa ni wale waandishi wa wahyi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), pamoja na wale walioihifadhi mbele yake, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawaambia;
‘Itakapotokea