Sehemu ya Pili

Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Llahu ‘anhu)  
Khalifa wa tatu wa tatu aliyeongoka

‘Uthmaan na vita


‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mtu asiyependa vita wala umwagaji wa damu wa aina yoyote ile. Hata hivyo pale inapobidi alikuwa msitari wa mbele kuitikia mwito wa jihadi dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu kwa hali na mali.
Hakupigana vita vya Badr ingawaje alikuwa miongoni mwa wachache waliotoka kwenda kushiriki, na hii ni kwa sababu walipokuwa wakielekea Badr, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimtaka ‘Uthmaan arudi nyumbani kwake Madiynah kwa ajili ya kumuuguza mkewe Bibi Ruqayyah (Radhiya Llaahu ‘anha) ambaye hali yake ilikuwa mbaya sana, na hatimaye akafariki dunia siku ile zilipowafikia habari za ushindi wa Waislamu katika vita hivyo.
Katika vita vya Uhud, ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alishiriki, akapigana, lakini alirudi nyuma pamoja na wenzake pale majeshi ya makafiri yalipofanikiwa kuwazunguka na kuupanda mlima Uhud na kuanza kuwarushia mishale na kusababisha kuuliwa kwa Waislamu wengi.
Katika vita hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwaweka juu ya jabali Uhud watu hamsini waliokuwa mahodari wa kutupa mishale wapate kuwalinda wenzao wanaopigana chini, akawataka wasiondoke hapo iwe itakavyokuwa ili baada ya kumalizika vita hivyo majeshi ya washirikina yasiweze kuwazunguka na kuwashambulia kwa nyuma .
Lakini watupa mishale hao walikwenda kinyume na amri hiyo mara baada ya kuwaona wenzao walioshinda wakianza kuwaendesha mbio washirikina huku wakikusanya ngawira. Baadhi yao isipokuwa watu kumi na nne tu walikhalifu amri hii, wakateremka na kwenda kuwasaidia wenzao katika kuwateka washirikina na katika kukusanya ngawira.
Baadhi ya majemadari wa jeshi la washirikina waliokuwa wakirudi nyuma, walipowaona Waislamu wakiliteremka jabali, wakageuza njia na kulizunguka kwa nyuma, wakalipanda na kuanza kuwashambulia Waislamu kwa kuwamiminia mishale.
Waislamu wengi walikufa na wengine kujeruhiwa, na wengi wengine akiwemo ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakarudi nyuma kwa msituko wa walipoona wenzao wanapukutika, na Mwenyezi Mungu akateremsha kauli yake ya kuwasamehe wale waliorudi nyuma siku hiyo akasema;
"…..Naye sasa amekusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ihsani nyingi juu ya wanaoamini."
Aali Imran - 152
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alishiriki katika vita vyote vilivyobaki walivyopigana Waislamu. Alishiriki katika vita vya Khaybar, vita vya kuuteka mji wa Makkah, vita vya Taif, Howazin, Tabuk na vingi vinginevyo.
Siku ya Hudaybiyah kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa yeye ndiye aliyepewa jukumu la hatari, pale alipochaguliwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwenda Makkah akajadiliane na washirikina, naye akalikubali jukumu hilo kwa ushujaa mkubwa, yakatokea yaliyotokea, na kwa ajili yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwataka Waislamu wafungamane naye chini ya mti, na kwa ajili yake siku hiyo Mwenyezi Mungu aliteremsha aya ya kuridhika na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliofungamana na Mtume wake mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Khalifa wa tatu


Alipokuwa akivuta pumzi zake za mwisho, ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikataa kumchagua Khalifa atakayeongoza baada yake juu ya kuwa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) walimshikilia afanye hivyo; ‘Umar aliwaambia;
"Mzigo wenu nimeubeba nikiwa hai, na baada ya kufa kwangu mnanitaka nikubebeeni pia? Ikiwa kuchagua basi amekwisha chagua aliyekuwa bora kuliko mimi - Abu Bakr , na ikiwa ni kuacha basi aliacha kuchagua aliyekuwa bora kuliko mimi - Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na Mwenyezi Mungu ataihifadhi dini yake".
Lakini ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwaita Maswahaba sita; Ali, ‘Uthmaan, Twalha, Al Zubayr, Saad na ‘Abdur-Rahmaan bin Al-’Awf (Radhiya Llaahu ‘anhum) na kuwaambia;
"Nimetazama na nikakuoneni kuwa nyinyi ndio mnaostahiki kuwa viongozi, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipofariki dunia alikuwa radhi nanyi nyote. Mimi sikuogopeeni watu iwapo mtasimama katika njia ya haki, basi nitakapokufa mushauriane muda wa siku tatu, na siku ya nne ikiingia muwe mumekwishamchagua kiongozi kati yenu. Na ahudhurie pamoja nanyi ‘Abdullaah bin ‘Umar akiwa kama ni mshauri tu, lakini yeye hana haki yoyote ya kuchaguliwa kuwa kiongozi".
Twalha hakuwepo Madiynah siku walipokutana, na ‘Abdur-Rahmaan bin Al-’Awf(Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwashauri Maswahaba waliohudhuria kuwa itakuwa bora iwapo mmoja wao atajitoa ili pawezekane kuchaguliwa Khalifa kwa urahisi. Kisha yeye mwenyewe akajitoa, kisha Al Zubeir (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajitoa na Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) pia akajitoa. Wakabaki wawili, nao ni ‘Uthmaan na Ali (Radhiya Llaahu ‘anhumaa), na ‘Abdur-Rahmaan bin Al-’Awf akapewa jukumu la kumchaguwa mmoja kati yao.
Ibni Al-’Awf (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa na kazi kubwa ya kuwashauri Maswahaba wote waliopo Madiynah kwa muda wa siku tatu tu ili aweze kutoa uamuzi wake muhimu.
Anasema Ibni Kathir katika kitabu cha 'Al Bidaya wa Nnihaya';
"‘Abdur-Rahmaan alikuwa na kazi kubwa katika siku tatu hizo ya kuupitia mji wote wa Madiynah na kuwagongea milango watu akiwashauri na kusikiliza rai zao.
Aliwauliza Maswahaba waliokuwa maarufu, watu wa kawaida, wanawake, na ilimbidi wakati mweingine awaulize hata watoto wadogo na wasafiri waliokuwa wakiwasili Madiynah katika siku hizo."
Ibni Kathir anaendelea kusema;
"Kisha ‘Abdur-Rahmaan bin Al-’Awf akawaita ‘Uthmaan na Ali, wakamjia, na yeye akawakabili na kuwaambia;
"Nimewauliza watu wote juu yenu na sikumpata hata mmoja anayekufadhilisheni baina yenu wawili, kwani wote wanataka mmoja wenu awe Khalifa wao."
Kisha ‘Abdur-Rahmaan akawataka watoe ahadi kuwa yeyote kati yao atakayechaguliwa kuwa Khalifa atahukumu kwa uadilifu na yule asiyechaguliwa atatii.
Kisha akatoka pamoja nao na kuelekea msikitini, ‘Abdur-Rahmaan akiwa amevaa kilemba alichopewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) huku akiwa ameufunga upanga wake kiunoni, na alipowasili msikitini akawataka watu wote wakusanyike. Kisha pakanadiwa; "Assalaatu Jaamia", watu wakamiminika msikitini mpaka msikiti ukajaa na kufurika hata ‘Uthmaan hakupata mahali pa kukaa isipokuwa mwisho wa safu, na alikuwa mtu mwenye kuona haya sana.
Kisha ‘Abdur-Rahmaan akapanda juu ya membari ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuomba dua ndefu sana, kisha akasema;
"Enyi watu! Mimi nilikuulizeni kwa siri na kwa dhahiri na sikumpata hata mmoja katika yenu anayemtaka mwengine isipokuwa Ali au ‘Uthmaan. Inuka njoo kwangu ewe Ali".
Ali akainuka na kumwendea, na ‘Abdur-Rahmaan akaushika mkono wake na kumuuliza;
"Je! Upo tayari kufungamana nami kufuatana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake na matendo ya Abu Bakr  na ‘Umar?"
‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Kufuatana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake na Ijtihadi kwa rai yangu".
Kisha akasema;
"Inuka njoo kwangu ewe ‘Uthmaan".
‘Uthmaan akainuka na kumwendea, na ‘Abdur-Rahmaan akaushika mkono wake na kumuuliza;
"Je! Upo tayari kufungamana nami kufuatana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake na matendo ya Abu Bakr  na ‘Umar?"
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Allahumma Ndiyo, nimekubali".
‘Abdur-Rahmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaunyanyua uso wake juu na kutizama juu ya sakafu ya msikiti huku mkono wake ukiwa ndani ya mkono wa ‘Uthmaan kisha akasema;
"Ewe Mola wangu sikia na ushuhudie, mimi nimeitua amana iliyokuwa juu ya shingo yangu na kuiweka juu ya shingo ya ‘Uthmaan".
Watu wakaanza kumkimbilia ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ili wafungamane naye, na mkono wa mwanzo uliofungamana naye ulikuwa mkono wa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu), kisha Waislamu wote waliobaki wakafungamana naye.
Na hivi ndivyo ‘Uthmaan alivyopewa Ukhalifa akiwa na umri unaokaribia miaka sabini".

Hotuba yake ya mwanzo


‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa msemaji hodari, lakini siku ile alipopanda juu ya membari kutoa hotuba yake ya mwanzo, alishindwa kusema maneno mengi, na badala yake alitamka maneno machache yafuatayo;
"Hakika dunia imejaa ghururi, basi yasikudanganyeni maisha ya dunia wala asikudanganyeni yule mdanganyi mkubwa (Iblisi) katika (mambo ya) Mwenyezi Mungu. Dunia itupeni mbali kama vile Mwenyezi Mungu alivyoitupa na itafuteni akhera yenu, kwani Mwenyezi Mungu ameipigia mfano dunia Akasema;
"Na wapigie mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tunayoyateremsha kutoka mawinguni; kisha huchanganyika nayo mimea ya ardhi kisha ikawa majani makavu yaliyokatikakatika ambayo upepo huyarusha huku na huko. Na Mwenyezi Mungu Ana uweza juu ya kila kitu.
"Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia. Na vitendo vizuri vibakiavyo ndivyo bora mbele ya Mola wako kwa malipo na tumaini bora (kuliko hayo mali na watoto)".
Al Kahf - 45 - 46

Anasema Ibni Kathir katika Al Bidaya wal Nihaya;
"‘Uthmaan ameianza kazi yake ya ukhalifa kwa kuwaandikia wakuu wa mikoa mbali mbali, washika hazina pamoja na majemadari wake akiwanasihi pamoja na kuwaamrisha mema na kuwakataza maovu na akawataka wafuate mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuacha kuzusha mambo mepya katika dini.
Katika utawala wake nyumba ya Hazina ya Waislamu (Baytul Mal), ilijaa mali nyingi, akawaongezea watu mishahara na kuhusisha kiwango maalum cha mali kwa ajili ya kuwalipa na kuwalisha wanaokesha wakifanya ibada na kutafuta elimu misikitini ".

Uasi


Mara baada ya ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kukamata hatamu za kuongoza umma, Warumi na baadhi ya Wafursi wakaanza kuvunja mikataba iliyokuwa baina yao na dola ya Kiislamu. Uasi ulianza katika nchi za Azarbeijan na Armenia, na Warumi wakajaribu kuuvamia mji wa Alexandria na Palestine, na moto wa uasi ukaendelea kuwaka mpaka ukafika sehemu za Khurasan na Karman na kwengineko.
Waasi hawakuwa watu wa kawaida wa miji ile, kwani watu wa miji hiyo baada ya kukombolewa na Waislamu kutokana na utawala wa Kirumi na wa Kifursi waliridhika na utawala wa viongozi waadilifu wa Kiislamu. Lakini uasi huo ulitokana na nguvu iliyokuwa ikitawala kabla ya Uislamu, nguvu iliyopoteza ufalme na utawala wake, nguvu iliyokula hasara ya kila kitu baada ya kushindwa na Majeshi ya Kiislamu.
Nguvu hiyo ilipoona kuwa Khalifa mwenye nguvu ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) ameuliwa na kafiri mwenzao, na kwamba Khalifa mzee mwenye umri unaokaribia miaka sabini ndiye aliyetawala, tamaa ikawaingia, wakaona hii ndiyo fursa nzuri ya kuurudisha utawala wao.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwa akijulikana kama ni mtu wa vita kama vile Khalid bin Walid au Sa’ad bin Abi Waqaasau ‘Aliy bin Abi Twaalib(Radhiya Llaahu ‘anhum) na wengineo, bali umaarufu wake ulikuwa juu ya ukarimu na wingi wa kuona haya, na kwa ajili hiyo tamaa ikaingia katika nafsi za waasi, wakadhani kuwa fursa imewadia ya kuurudisha utawala wao.
Lakini mzee huyu anayekaribia umri wa miaka sabini akaona ni vizuri awaoneshe makafiri hawa kuwa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hawapimwi kwa umri wao wala hawakisiwi kwa miili yao, bali vipimo vyao ni Imani iliyojaa nyoyoni mwao, imani yao juu ya Dini yao, juu ya Mola wao na juu ya Mtume wao mtukufu Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoa amri ya kuuzima moto huo wa uasi kwa haraka sana kama ulivyoanza. Si hivyo tu, bali aliyapa majeshi yake amri ya kusonga mbele na kuiteka miji mingine ya Warumi ili wasiipate kwa wepesi fursa nyengine ya kuanzisha uasi kama huo karibu na dola ya Kiislamu.
‘Uthmaan mwenyewe (Radhiya Llaahu ‘anhu) ndiye aliyewachagua wakuu wa majeshi yatakayoifanya kazi hiyo. Jambo la ajabu ni kuwa hapana hata jeshi moja katika majeshi ya ‘Uthmaan yaliyoshindwa katika mapambano hayo isipokuwa katika pambano moja tu.
‘Uthmaan alikuwa akipanga, akifikiri, akikisia kama kwamba amerejeshewa tena ujana wake Radhiyallahu anhu. Na alipoona kuwa ipo haja ya kuunda jeshi la baharia, akaliunda. ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), juu ya ushujaa wake hakujaribu kuchukua hatua kama hiyo ambayo ni ngeni na ingehatarisha usalama wa majeshi ya Kiislamu.
Waislamu walipomuona Khalifa wao akiwa na hamasa, imani pamoja na moyo ule wa kishujaa, wao pia imani yao ikaongezeka nguvu. Wakawa wajasiri zaidi na wenye moyo thabiti.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaanza kwa kutoa amri ya kuushambulia mji wa Azerbeijan, kisha Armenia, ile miji iliyovunja ahadi. Akamchagua Al Walid bin ‘Uqbah (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa mkuu wa majeshi yatakayokwenda huko, na baada ya kuwashinda akafanikiwa kuwafanya waasi hao watie saini (sahihi) mkataba mwingine kama ule waliouvunja.
Walipokuwa wakirudi mji wa Al Kuufa baada ya kuwashinda waasi hao, Al Walid na majeshi yake wakapata habari kuwa majeshi ya Warumi yameanza uchokozi katika miji ya Sham. Ikamfikia amri kutoka kwa Khalifa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa atayarishe jeshi la watu elfu kumi sharti liongozwe na mtu mwaminifu tena mkarimu.
Al Walid (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamchagua mtu mmoja aitwae Habib bin Maslamah al Fahariy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuliongoza jeshi hilo. Habib akaondoka na jeshi lake lisilozidi watu elfu kumi na kupambana na majeshi ya Warumi pamoja na Waturki yasiyopungua watu elfu themanini.
Mke wa Habib alikuwa miongoni mwa wanajeshi hao, na alipomuuliza mumewe kabla ya kuanza vita;
"Tutaonana wapi ikiwa vita vitapamba moto na majeshi kutawanyika?"
Akamjibu;
"Katika hema la mkuu wa majeshi ya Kirumi au Peponi".
Majeshi mawili hayo yakakutana katika mapambano makali, na Habib aliyashinda majeshi ya Warumi na Waturuki kwa pamoja, kisha hakusimama hapo, bali alisonga mbele kuelekea nchi za Warumi huku akizivunja ngome zao moja baada ya moja.

Habari nyengine zikamfikia Khalifa wa Waislamu kuwa majeshi ya baharia ya Warumi yanauvamia mji wa Alexandria huko Misri na kwamba majeshi mengine zaidi yanakuja kutoka Roma kuelekea huko.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuamrisha ‘Amr bin Al-‘Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa Gavana wa nchi ya Misri apeleke jeshi lake Alexandria na ayaangamize majeshi ya Kirumi. Wakati huo huo Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akiuteka mji wa Qansarin, na Majemadari wengine walikuwa wakizima moto ya uasi katika sehemu mbali mbali.
Khalifa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akayaamrisha majeshi yake kwenda Afrika ya Kaskazini chini ya uongozi wa Abdullah bin Saad pamoja na Abdullaah bin ‘Amr na Abdullaah bin Zubayr (Radhiya Llaahu ‘anhu), na baada ya mapambano makali majeshi hayo yakawashinda majeshi ya wabarbari ya Afrika ya Kaskazini.
Jeshi la baharia la Warumi lilokuwepo Cyprus, lilikuwa katika hali ambayo lingeweza kusababisha hatari kwa nchi za Kiislamu, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaona ni bora ahatarishe na kupeleka jeshi la baharia la Waislamu kupambana nalo.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamchagua Muawiya bin Abi Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu), kuwa kiongozi wa jeshi la kuiteka nchi ya Cyprus na akampelekea jeshi lingine likongozwa na Saeed bin Abu Sarh (Radhiya Llaahu ‘anhu) ili washirikiane katika jukumu hilo. Majeshi mawili hayo makubwa yakapambana na hatimaye jeshi la Warumi likasalimu amri na kutia saini (sahihi) mkataba wa sulhu uliowekewa masharti na Waislamu.

Vita hivyo vikafuatiliwa na vita vya Sawariy. Vita ambavyo Constantine, mfalme wa Roma alitayarisha jeshi kubwa sana lisilopata kutayarishwa mfano wake kwa ajili ya kupambana na majeshi ya Kiislamu. Akalipeleka jeshi hilo Morocco pamoja na merikebu mia tano za kivita, na mapambano makali yakatokea huko na hatimaye majeshi ya Kiislamu yakawashinda Warumi katika vita hivi ambavyo watu wengi sana kutoka pande zote mbili walikufa.
Hivi ndivyo ilivyokuwa, mara baada ya kutawala ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu). Majeshi ya Kiislamu yalisonga mbele kila upande na kuyashinda majeshi ya Warumi na ya Wafursi na kufanikiwa kuiteka miji mbali mbali kama vile Constantinople, Karman na kwengineko, na hatimaye kufanikiwa kuuzima moto huo wa uasi.
Yule waliyemdhania kuwa ni mzee na wangeweza kumchezea, aligeuka kuwa simba mshambuliaji.

Msahafu Mmoja


Inajulikana kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiteremshiwa Qur-aan kidogo kidogo kutokana na sababu na matukio mbali mbali, na wakati mwingine bila hata sababu wala matukio, wala hakuteremshiwa yote kwa pamoja.
Tunaelewa pia kuwa Qur-aan tukufu imeteremshwa kwa lugha (lahja) ya Ki-Quraysh, na kwamba pale Madiynah yalikuwepo makabila mengine yasiyokuwa ya Ki-Quraysh, na kwa ajili ya kuwarahisishia usomaji wa Qur-aan, Mtume wa mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimuomba Mola wake awaruhusu kuisoma na kuiandika kwa lahja zao mbali mbali. Idadi ya lahja hizo zilikuwa saba, na inaeleweka pia kuwa baadhi ya wale walioandika Qur-aan kwa lahja zao hizo waliieneza kila pembe ya nchi za Kiislamu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa kila anapoteremshiwa Wahyi akiwaamrisha waandishi wake kuandika Wahyi huo mbele yake. Kwa hivyo Qur-aan iliandikwa wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na mbele yake ndani ya sehemu mbali mbali za kuandikia za wakati huo kama vile magamba ya miti, mbao, makozi nk. Na baada ya kuandikwa ikawa inawekwa nyumbani kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) nao pia waliihifadhi Qur-aan kwa moyo na kuisoma majumbani mwao na katika sala zao, na waliokuwa wakijua kuandika waliiandika katika sehemu mbali mbali na kuzihifadhi majumbani mwao pia.
Kwa hivyo Qur-aan iliandikwa tokea wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuhifadhiwa na Maswahaba wengi (Radhiya Llaahu ‘anhum), lakini haikuwa katika kitabu kimoja, bali iliandikwa katika sehemu mbali mbali zilizowarahisikia kuandika.
Alipotawala Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu), alishauriwa na ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aikusanye ile Qur-aan iliyoandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuilinganisha na ile iliyoandikwa na Maswahaba wengine na ile iliyohifadhiwa vifuani mwa waandishi wa wahyi pamoja na Maswahaba wengine wengi (Radhiya Llaahu ‘anhum), na kuijumuisha katika kitabu kimoja.
Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) hapo mwanzo hakupendelea kufanya jambo kama hilo ambalo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakulifanya, lakini hatimaye alilikubali pendekezo hilo la ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumpa Zayd bin Thabit (Radhiya Llaahu ‘anhu) jukumu la kuisimamia kazi hiyo akishirikiana na Maswahaba wenzake kama vile Saeed bin ‘Aas, ‘Abdullaah bin Zubayr, ‘Abdur-Rahmaan bin Al-Haarith na wengineo waliokuwa wakiuandika wahyi huo mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pale ulipokuwa ukiteremshwa.
Alimpa jukumu hilo Zayd (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa sababu yeye ndiye aliyeandika wahyi zaidi kuliko Maswahaba wengine, na alikuwa pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa muda mrefu zaidi kuliko waandishi wa wahyi wenzake.
Baada ya juhudi kubwa sana, Zayd pamoja na wenzake (Radhiya Llaahu ‘anhum) wakafanikiwa kuikusanya Qur-aan na kuiandika yote katika msahafu mmoja, na kuanzia siku hiyo ile Qur-aan iliyoandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) katika sehemu mbali mbali na kuhifadhiwa vifuani mwa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) ikawa imekusanywa na kuandikwa katika msahafu mmoja tu uliopangwa sura zake na aya zake kama alivyowapangia Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Kisha msahafu huo ukawekwa na kuhifadhiwa nyumbani kwa Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu), na baada ya kufa kwake ukawa nyumbani kwa ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye kabla ya kufa kwake alimkabidhi binti yake Hafswa (Radhiya Llaahu ‘anha), mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Wakati huo huo ile misahafu ya mwanzo iliyoandikwa kwa lahja zile saba ilienea na kusomwa na watu katika nchi mbali mbali za Kiislamu, na inajulikana kuwa alipotawala ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) dini ya Kiislamu ilipata nguvu zaidi, na majeshi yao yaliweza kuzishinda nchi mbali mbali na kusonga mbele hadi kufikia Azarbeijan na Armenia na Cyprus, na kuweza pia kuziteka nchi mbali mbali za Asia na za Ulaya na Afrika.
Baadhi ya Maswahaba kama vile ‘Hudhaiyfa (Radhiya Llaahu ‘anhu) walikuwa wakiona mambo ya kiajabu kila wanaposonga mbele kuziteka nchi hizo. Katika nchi ya Syria na Misri kwa mfano, Waislamu walikuwa wakigombana na kushindana kwa kutamba katika usomaji wao wa Qur-aan kila mmoja kwa lahaja yake, kila mmoja akisema kuwa usomaji wake wa Qur-aan ni bora kuliko wa mwenzake na kufikia hadi kukufurishana.
Zilizpomfikia habari hizo, ‘Uthmaan akashauriana na Maswahaba wenzake (Radhiya Llaahu ‘anhum) na wote wakaona kuwa ipo haja kubwa ya kuwaunganisha Waislamu wote wawe wanaisoma Qur-aan kwa msomo mmoja tu na kwa kutumia Lahaja moja tu.
Wakakubaliana wauchukue ule Msahafu uliokusanywa na kuandikwa wakati wa Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kuunukuu kwa kuuandika tena katika misahafu mingine mingi, na wakakubaliana kuwa itumike lugha ya ki Quraysh iliyoteremshiwa Qur-aan, kisha waisambaze misahafu hiyo katika nchi za Kiislamu na kuichoma moto misahafu yote iliyobaki iliyoandikwa kwa misomo na lahaja tofauti ili kuukata mizizi ya fitna kuanzia chanzo chake, mizizi ambayo kama ingeachwa basi mwisho wake usingekuwa mwema.
Ikachaguliwa tume ya waliohifadhi Qur-aan pamoja na wajuzi wa lugha ya kiarabu, wote wakiwa ni wale waandishi wa wahyi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), pamoja na wale walioihifadhi mbele yake, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawaambia;
‘Itakapotokea khitilafu yoyote kati yenu katika usomaji basi andikeni kwa lahja ya ki Quraysh’.
Baada ya kukamilika kazi hiyo, akaurudisha ule msahafu wa Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) nyumbani kwa Bi Hafswa (Radhiya Llaahu ‘anha), na Waislamu wakaanza kunukuu kutoka katika msahafu huo ulioandikwa mbele ya Maswahaba wote (Radhiya Llaahu ‘anhum) na kuisambaza duniani kote. Haya yalifanywa baada ya kupatikana makubaliano baina ya Maswahaba wote (Radhiya Llaahu ‘anhum) ya kuwepo haja kubwa ya kuifanya kazi hiyo.
Sayyidna ‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipowasikia baadhi ya watu wakimlaumu ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa ameichoma moto misahafu, aliwaambia;
“Mcheni Mola wenu enyi watu! Msipindukie mipaka katika kumlaumu ‘Uthmaan na kusema kuwa eti yeye ni mchomaji wa misahafu, kwani Wallahi misahafu imechomwa mbele ya Maswahaba wote na baada ya sote kukubaliana. Na mimi ningelikuwa Khalifa basi ningefanya kama alivyofanya”.
Kwa hivyo Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu) akihofia Qur-aan isije ikapotea baada ya kufa kwa waliohifadhi aliikusanya na kuiandika mahala pamoja, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliiandika katika kitabu kimoja na kuichoma iliyobaki kwa kuogopa mtafaruko.
Lakini Qur-aan aliyoiandika ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni ile ile aliyoiandika Abu Bakr  (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliyoinukuu kutoka katika ile iliyoandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuhifadhiwa nyumbani kwake.
Katika hadithi iliyosimuliwa na Imam Ahmad, Ibni Majah, At-Tirmidhiy na kwa njia nyingi, anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam);
"Yule kati yenu atakayeishi (miaka mingi), atakuja kuona hitilafu nyingi sana, basi (mtakapoona hitilafu hizo) mzifuate (msiziache) Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waongofu watakaokuja baada yangu. Zikamateni kwa magego yenu".
Na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni katika hao Makhalifa waongofu (Radhiya Llaahu ‘anhum) ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anatutaka tufuate mafundisho yao na mwenendo wao.

Miaka Migumu


Baada ya kushindwa katika mapambano ya uso kwa uso, ile nguvu ya shari ya kikafiri ikiongozwa na wafalme wa Fursi pamoja na Warumi ikaingia katika mapambano ya siri na ya hila dhidi ya Khalifa wa Waislamu.
Mayahudi nao hawakutaka kubaki wawe washangiliaji tu, kwani wao pia walitolewa na kufukuzwa nje ya Madiynah na kupoteza vyote walivyomiliki baada ya kufanya hiana yao katika vita vya Khandaq.
Wote hawa walikuwa wakiungulika kila wanapoona na kusikia juu ya kusonga mbele kwa majeshi ya Kiislamu, na namna Waislamu walivyokuwa wakiteka nchi baada ya nchi huku wakiwatoa watu kutoka katika kiza cha kufru na kuwaingiza katika nuru ya Uislamu.
Warumi na Wafursi walifanya mbinu zao kwa nje, na Mayahudi wakafanya mbinu zao na hila zao kwa ndani, na halikuwa jambo la sudfa pale alipokuja kutoka nchi ya Yemen myahudi aitwaye ‘Abdullaah bin Saba-a na kudai kuwa eti amesoma juu ya dini ya Kiislamu na akaipenda, na kwamba anataka kuingia katika dini hii na kuchukua nafasi yake anayostahiki katika kuuongoza umma huo.
Myahudi huyo aliyekuwa akijifanya mcha Mungu sana alikuwa mwingi wa hila, na akafanikiwa kiasi kikubwa katika kuwagombanisha Waislamu.
Alianza kuingiza fitna zake kidogo kidogo kwa kumtuhumu Khalifa wa Waislamu ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa amejichukulia uongozi kwa nguvu na kwamba amemdhulumu ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu). Na katika tuhuma zake hizo alikuwa akizitumilia hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) zinazozungumza juu ya sifa mbali mbali za Sayiduna ‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) kama vile;
"Anayenipenda mimi ampende Ali ".
na;
"Mola wangu mnusuru atakayemnusuru na uwe dhidi ya atakayekuwa dhidi yake".
Alizitumilia hadithi kama hizi ili kuonesha kuwa wote waliokuwa Makhalifa kabla yake walikuwa maadui wa ‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kwamba hawakuwa wakimpenda, bali hawakuwa wakifuata hata maamrisho ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akichukizwa na maneno hayo ya ‘Abdullaah bin Saba-a na mara nyingi alimjulisha juu ya kuchukizwa kwake huko na kuwatahadharisha Waislamu juu ya ubaya wake, lakini juu ya yote hayo Ibni Saba-a huyu alifanikiwa kuieneza chuki yake hiyo katika nyoyo za baadhi ya Waislamu.
Alikuwa akisafiri nchi mbali mbali kuanzia mji wa Al-Kuufah (Iraq), kisha nchi ya Sham, kisha akaelekea Misri na kukaa huko muda mrefu akijifanya kama ni mtu anayependa kuamrisha mema na kukataza maovu huku akiieneza sumu yake hiyo na kuwataka watu wainuke na kupigana kwa ajili ya kuirudisha haki hiyo kwa wanaoistahiki, na kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ameusia juu ya Ukhalifa wa ‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu).
‘Abdullaah bin Saba-a alifanikiwa kuyatumilia baadhi ya makosa yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya magavana wa Kiislamu wakati ule kwa ajili ya kuifanikisha fitna yake hiyo.

Bora damu yangu imwagike


Habari za njama hizo pamoja na matayarisho ya uasi yaliyokuwa yakifanyika huko Misri, Basra na Al-Kuufah zilimfikia ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), lakini kila anaposhauriwa kutumia nguvu kuzivunja njama hizo, alikuwa akikataa huku akisema;
"Iwapo damu lazima imwagike, basi bora imwagike damu yangu badala ya kumwagika damu ya Waislamu.".
Alikuwa akisema pia;
"Sipendi nikutane na Allah na juu ya shingo yangu ipo hata tone ya damu ya Mwislamu".
Wafuasi wa ‘Abdullaah bin Saba-a walifanikiwa kujipenyeza na kuingia Madiynah kwa makundi na wakati mwengine mmoja mmoja bila ya kuonesha nia yao hiyo ovu, wakidai kwamba wamekuja kwa ajili ya kujitayarisha kwenda Makkah kwa ajili ya Hija. Wengine walidai kuwa wamekuja Madiynah kutafuta elimu.
Wakafanikiwa kuingiza hofu pale Madiynah baada ya kutambua kuwa wengi kati ya Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hawakuwepo Madiynah wakati huo, kwani wengi wao walikuwa nje kwa ajili ya kupigana Jihadi na wengine walikuwa Makkah kwa ajili ya Hija.
Haukupita muda waasi hao wakataka kukutana na Khalifa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wapate kumjulisha juu ya nia yao ya kutaka kusahihisha baadhi ya makosa yaliyokuwa yakitendwa na baadhi ya magavana wake, na ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu) alifanikiwa kuleta makubaliano kuwa maombi yao yaangaliwe sharti wao warudi katika nchi zao kwanza.

Hali ya mambo ilizidi kuwa mbaya, na waasi hao ambao wengi wao walitoka nchi ya Misri walitishia kufanya uasi mkubwa na kumuuwa Khalifa wa Waislamu, na Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwandikia ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akimtaka ende Sham mahali alipo yeye Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) mpaka mambo yatakapotulia, lakini ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikataa akamwambia;
"Mimi sikubali kuhamia mahali pengine nikawa mbali na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)".
Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) akashauri kumpelekea jeshi kubwa liuzunguke mji wa Madiynah na kumlinda na waasi hao, lakini ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu;
"Naogopa wasije wakafanya zahma katika mji wa Madiynah na kuwadhiki Maswahaba wa Mtume katika Muhajirin na Ansar".
Muawiya akamuandikia kuwa;
"Waasi hao wanaweza kukuuwa"
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu;
"Hasbiya Llahu wa neema l wakiyl"
(Mwenyezi Mungu ananitosha Naye ni mlinzi bora kabisa).
Asubuhi moja watu wa Madiynah walipoamka walistukia mji wao umezungukwa na maelfu ya watu wenye silaha waliotanda barabarani na kuanza kufanya zogo na kutaka kukutana na ‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu).
‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawaambia;
"Rudini katika nchi zenu".
Wakakataa halafu wakaanza kumuamrisha ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) awaachishe kazi baadhi ya magavana na wakataka wapewe Marwan bin Al Hakam wamhukumu, jambo lisilowezekana kwani ikiwa leo wamemtaka huyu na kesho watamtaka mwengine. ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamtaka ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu) amsaidie kulitatua tatizo hili na kumuomba ende kuzungumza na waasi hao na kuwataka warudishe silaha ndani ya ala zake na kurudi katika nchi zao, na akatoa ahadi kuwa iwapo watafanya hivyo atamuondoa Al Hakam katika kazi yake na pia baadhi ya magavana wanaotuhumiwa.

‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoka kwenda kwenye kambi ya waasi akifuatana na Muhammad bin Maslamah pamoja na Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Llaahu ‘anhumaa), na baada ya majadiliano marefu waasi hao wakakubali kurudi makwao iwapo masharti yao yatatimizwa, na ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawapa ahadi kuwa masharti yatatimizwa.

Waasi warudi tena


Hazikupita siku chache waasi wakarudi tena mjini, wakatanda barabarani na vichochoroni na kuizunguka nyumba ya Khalifa wa Waislamu. ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoka na kuwaendea kwanza wale waasi waliotoka Misri na kuwauliza ni jambo gani lililowafanya wavunje ahadi na kurudi baada ya makubaliano?
Wakamwambia;
"Tumemkamata mtu aliyebeba barua iliyopigwa mhuri wa Khalifa, inayomtaka gavana wa Misri atukamate na kutuuwa mara baada ya kuwasili kwetu huko. Na tulipomuuliza nani aliyempa barua hiyo, akasema kuwa amepewa na Marwan".
Kisha ‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawaendea waasi waliotoka mji wa Al-Kuufah na kuwauliza suali hilo hilo;
"Nini kilichokurudisheni wakati tumeshakubaliana?"
Wakamjibu kuwa wao wamekuja kuwasaidia wenzao wa Misri.
Kisha akawaendea watu wa Basra na kuwauliza;
"Na nyinyi kipi kilichokurudisheni baada ya makubaliano kumalizika?"
Akapata jibu lile lile kuwa wao wamekuja kuwasaidia wenzao waliotoka Misri.
‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawauliza;
"Lakini nyinyi mlipoondoka hapa, kila mmoja alipita njia yake. Mlipita njia mbali mbali, mmezipataje nyote habari za barua hii?"
Hawakuwa na jawabu, na ndipo ilipojulikana kuwa tokea mwanzo nia yao hasa ilikuwa ni kutaka kumuondoa Khalifa, na kwamba hawakuwa na nia ya kuondoka na kurudi makwao, na kwamba sababu iliyowafanya warudi tena Madiynah ni kile walichokijia hapo mwanzo nayo ni kutaka kumuangusha au kumuuwa Khalifa wa Waislamu.

Ukweli juu ya barua


Anasema Dr. Khalid Mohammed Khalid;
"‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikula kiapo kuwa yeye hakuiandika barua hiyo wala hakutoa amri ya kuandikwa. Na bila shaka yoyote ile ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) hasemi uongo, kwani yeye ni mkweli anayejulikana kwa kupenda ukweli. Kisha vipi atoe amri ya kuuliwa jeshi zima la waasi wakati alikwisha kataa ombi la Muawiya la kumpelekea jeshi kubwa kwa ajili ya kumlinda akahiari imwagike damu yake kuliko kumwagika damu ya Waislamu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe?
Ama Marwan naye pia haiwezekani afanye hivyo, kwani alikuwa akijulikana kuwa ni mtu anayemuogopa Mwenyezi Mungu na mwenye kumpenda Khalifa wake, na alikuwa mtu mwenye hekima sana, na kwa hivyo anajua kuwa jambo kama hilo lingeharibu sifa ya Khalifa huyo mkarimu anayempenda.
Kwa hivyo hapana aliyebaki wa kuweza kutuhumiwa kwa jambo kama hilo isipokuwa viongozi wa waasi hao. Na hii ndiyo sababu baada ya uasi huo kusababisha vita vikubwa baina ya Waislamu na hatimaye kuuliwa kwa ‘Uthmaan na Ali (Radhiya Llaahu ‘anhumaa).
Viongozi wa waasi hao walikamatwa na barua nyengine za uongo walizoziandika wenyewe, zilizojulikana baadaye kuwa ni 'barua za fitna' iliyosababisha vita hivyo, na waasi hao kama kawaida yao walikanusha tena na kudai kuwa si wao walioziandika, na kuwatuhumu Mama wa Waislamu ‘Aaishah na Talha na Az-Zubayr (Radhiya Llaahu ‘anhum) kuwa eti wao ndio walioziandika.
Nia ya waasi hao ikajulikana vizuri pale walipotoa masharti yao ya mwisho waliposema kuwa;
"Ama Khalifa ajiuzulu, au tutamuuwa".
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikataa kujiuzulu, na hii ni kwa sababu angekubali kufanya hivyo atakuwa amewakubalia waasi hao matamanio yao, na kwa ajili hiyo heshima pamoja na haiba ya dola ya Kiislamu itaondoka kwa sababu siku za mbele kila asiyeridhika na Khalifa atakusanya makundi ya watu na kulazimisha matakwa yake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kumwambia ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu):
"Ewe ‘Uthmaan! Mwenyezi Mungu atakapokuvalisha joho kisha wakaja wanafiki kukutaka ulivue, usikubali kulivua".
Imam Ahmad bin Hanbal – Al-Haakim na Sunan za Abu Daawuud
Na joho alilokusudia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni ukhalifa.
Baadhi ya watu walidhania kuwa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikataa kujiuzulu kwa sababu ya kupenda ukubwa. Lakini ukweli ni kwamba alikataa kwa sababu alikuwa akiona mbali, alikuwa akiona yale wenzake hawakuwa wakiyaona, na hii ndio sababu ya kutowachukulia hatua kali waasi hao, pamoja na kustahamili adha zao na kuhiari kufa iwapo hapana budi, badala ya kusababisha vita baina ya Waislamu.
Siku moja aliposimama juu ya membari ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwahutubia Waislamu, alisema;
"Baadhi ya watu wamefanya pupa kuukimbilia uasi na kutamani nife haraka. Lakini wallahi wakiniuwa watatamani ningeishi zaidi kila siku moja mfano wa mwaka, na hii ni pale watakapoiona damu ikimwagika kwa wingi.
Enyi watu! Wallahi mimi nia yangu ni kutengeneza, iwapo nitakosea au nitasibu. Na nikiuliwa basi mjuwe kuwa hamtopendana tena na wala hamtosali pamoja tena na hamtoweza kuteka miji mingine tena baada yangu".
"Kuona kwake mbali huko", anaendelea kusema Dr. Khalid Mohammed Khalid; "Kulionekana baada ya kufa kwake, kwani maana mara baada ya Khalifa huyo mtukufu kuuliwa, chuki ikaenea na umma ukatawanyika na kugawanyika, na wala hawakuweza kukubaliana juu ya Khalifa mmoja tena mpaka siku ya leo".

Ananyimwa hata maji ya kunywa


Waasi wakaizunguka nyumba ya Khalifa kwa muda wa siku nyingi na hawakumruhusu kutoka nje. Hata maji ya kunywa yalipomalizika, hawakumruhusu kwenda kuchota, wakasahau kuwa siku ile Waislamu walipokuwa hawana maji ya kunywa, ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ndiye aliyekinunua kisima cha Roma kwa pesa zake binafsi na kuwaacha Waislamu wachote bila malipo yoyote, na mpaka siku hiyo walikuwa bado wanaendelea kuchota kutoka kisima hicho, lakini leo wanakataa kumruhusu yeye na ahli yake waliokuwa nyumbani kwenda kuchota.
Hapana aliyetegemea kuwa waovu hao watafikia daraja hii ya ukatili hasa kutokana na sababu zifuatazo;
Kwanza  - ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakati huo alikuwa na umri upatao miaka themanini.
Pili - Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika dini ya Kiislamu.
Tatu – ‘Uthmaan ameoa mabinti wawili wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Nne - Alikuwa Khalifa wa Waislamu.
Tano – Amebashiriwa mara nyingi na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuingia Peponi.
Tano - Yeye ndiye aliyetayarisha kwa pesa zake jeshi la wakati wa dhiki lililotoka kwenda kupambana na Warumi.
Sita - Na yeye ndiye aliyekuwa akitoa mali yake bila hesabu kwa ajili ya kuwasaidia Waislamu na kwa ajili ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu.
Yote haya na mengi mengineyo hayakutiwa maanani hata kidogo na waasi hao.

‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawataka baadhi ya vijana waende kuizunguka nyumba ya Khalifa kwa ajili ya kumlinda. Akawachagua Al-Hasan, Al-Husayn, (wanawe), Abdullaah bin Zubayr, Abdullaah bin ‘Umar bin Al-Khattwwaab na Maswahaba wachache (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliokuwepo Madiynah wakati ule na kuwapa jukumu hilo.
Anasema Ibni Taimiya katika kitabu chake kiitwacho 'Minhaji Sunnah' kuwa;
"Hapana hata mmoja katika Maswahaba watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum) aliyesimama pamoja na waasi hao, isipokuwa Muhammad bin Abu Bakr aliyethubutu kuingia ndani ya nyumba ya ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumshika ndevu zake na kuzivuta kwa nguvu, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
"Baba yako alikuwa akiziheshimu ndevu hizi na laiti angekuona katika hali hii basi angeona haya kwa haya unayoyatenda".
Baada ya kuambiwa maneno hayo Muhammad akatoka mbio nje ya nyumba huku akiwa analia na mikono yake ikimtetemeka".
(Mwisho wa maneno ya Ibn Taymiyyah).

Waasi wanajaribu ndani ya nyumba ya Khalifa


Waasi, wengi wao wakiwa watu waliotoka nchi ya Misri walijaribu kuuvamia mlango wa nyumba ya Khalifa na kuingia kwa nguvu, lakini Maswahaba wachache waliokuwepo nje ya nyumba h iyo kwa ajili ya kuilinda walifanikiwa kuwazuwia na kuwarudisha nyuma.
‘Abdullaah bin Salaam (Radhiya Llaahu ‘anhu)[1] alikuja pia na akajaribu kuwazuwia huku akiwaambia;
"Msizisalitishe panga za Mwenyezi Mungu baina yenu, kwani Wallahi mkizisalitisha hamtoweza tena kuuzima moto wake, na mji wenu huu umezungukwa na Malaika, Wallahi mkimuuwa basi Malaika wataondoka na  kukuacheni."
Wakamwambia;
"Ondoka ewe mwana wa kiyahudi".
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Omair (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa; ‘Abdullaah bin Salaam aliingia nyumbani kwa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), lakini ‘Uthmaan ambaye hakuwa akitaka kulindwa na mtu yeyote akamwambia:
"Kwangu mimi bora uwe nje kuliko ndani humu".
‘Abdullaah akatoka na kuwahutubia tena waasi hao akawaambia;
"Enyi watu! Jina langu wakati wa Ujahilia lilikuwa fulani, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akanipa jina la ‘Abdullaah, na kwa ajili yangu ikateremshwa aya ya kumi katika Suratul Ah-qaf isemayo;
"Sema; "Mnaonaje kikiwa (kitabu hiki) kimetoka kwa Mwenyezi Mungu; nanyi mumekikanusha na mashahidi MIONGONI MWA WANA WA ISRAILI, (Mayahudi waliosilimu) walishuhudia juu ya mfano wa haya na wakaamini haya na nyinyi mnafanya kiburi. Kwa yakini Mwenyezi Mungu hawaokoi watu madhalimu".
Na pia imeteremshwa juu yangu aya ya 43 ya Suratul Raad isemayo;
"Na wanasema waliokufuru "Wewe si Mtume", sema; "Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na baina yenu (kuwa mimi ni Mtume) na (pia) yule MWENYE ILIMU YA KITABU.[2]"
Nakuusieni msije mkazisalitisha panga zenu baina yenu kwani mji huu umejaa Malaika na mtakapomuuwa Khalifa wa Waislamu basi Malaika watakuhameni".
Waasi wote kwa pamoj wakasema; "Muuweni Myahudi huyu"
Anasema Ibni Kathiyr (Rahimahu Allaahu);
"Tizameni tofauti kubwa iliyopo baina ya ‘Abdullaah bin Salaam (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyesilimu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na ambaye aya nyingi zimeteremka juu yake zikimsifia, vipi alivyokuwa akimtetea Khalifa wa Waislamu, na ‘Abdullaah bin Saba-a Myahudi aliyesilimu kwa unafiki aliyekuwa akiwachochea watu wamuuwe Khalifa huyo".

Kuuliwa kwa  ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu)


Wakati nje ya nyumba waasi wanajibizana na Maswahaba, huko ndani ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliuchukua msahafu wake na kuanza kusoma mpaka usingizi ulipomchukua, na alipokuwa amelala akamuota Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akimwambia;
"Njoo ule futari pamoja nasi leo". Na ‘Uthmaan siku hiyo alikuwa amefunga. Alipozindukana alifurahi sana, akawa akijisemesha moyoni mwake; 'Nimemuota Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na amenialika nile futari pamoja naye! Subhanallah!", Akainuka na kwenda kuwaeleza watu wa nyumba yake juu ya ndoto ile, kisha akaingia chumbani kwake na kuendelea kusoma Qur-aan.
Waasi baada ya kushindwa kuingia kupitia mlangoni kutokana na ulinzi mkali uliopo nje, wakaamua baadhi yao waondoke kwa siri na kujaribu kuingia kwa njia ya uwani.
Wakafanikiwa kuubomoa ukuta wa uwa na kuingia bila ya walinzi walioko mbele ya nyumba kuwa na habari, wakenda moja kwa moja mpaka chumbani kwa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumsimamia mbele yake huku yeye akiwa anaendelea kusoma Qur-aan bila kuwajali, na wakati huo alikuwa ameifikia aya 173 ya Suratul Imran, pale Mwenyezi Mungu Anaposema;
"Wale ambao watu waliwaambia; "Watu wamekukusanyikieni. Kwa hivyo waogopeni". Lakini (maneno hayo) yakawazidisha imani wakasema; "Mwenyezi Mungu anatutosha. Naye Mlinzi bora ".
Mmoja wa waasi hao aitwaye Saudan bin Hamran alinyanyua chuma alichokuwa amekibeba na kumpiga nacho ‘Uthmaan mkononi kwa nguvu zake zote, na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakupiga kelele wala kujitetea, bali alistahamili huku akiwaambia;
"Huu ni mkono wa mwanzo ulioandika Qur-aan".[3]
‘Uthmaan akataka kuukumbatia msahafu, na khabithi yule akaupiga teke ili asiweze kuukumbatia, lakini msahafu ulikataa kutengana na yule aliyefanya juhudi ya kuuandika katika kitabu kimoja, ukazunguka na kubaki mikononi mwake.
‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaufunga msahafu akihofia asije akauchafua kwa damu iliyokuwa ikimtoka kwa wingi, lakini mnafiki yule aliendelea kumpiga kwa chuma tumboni na kila sehemu aliyoweza kuifikia huku akitumia nguvu zake zote na alikuwa akisaidiwa na mnafiki mwengine aitwae Al Ghafiqiy aliyeunyanyua upanga wake juu na kuuteremsha kwa nguvu zake zote ili ampige nao ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumuuwa, lakini mke wa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliupeleka mkono wake kumkinga mumemwe, na upanga wa khabithi yule ukaangukia mkononi mwake na kukikata kiganja pamoja na vidole vya mkono wake, kisha akaunyayua tena upanga wake juu na kumchoma ‘Uthmaan kwenye tumbo mara tisa mpaka akamuuwa, na baada ya kumuuwa akasema kwa kujisifu;
"Nimemchoma mara tisa, tatu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na mara sita kwa ajili ya yaliyokuwa moyoni mwangu".
Amesema uongo mnafiki yule, kwani angelisema;
"Nimemchoma mara tisa kwa ajili ya yaliyomo moyoni mwangu", hapo angekuwa amesema kweli.
Kisha wanafiki hao wakasema;
"Kwa vile damu yake ni halali kwetu, kwa hivyo hata mali yake ni halali kwetu pia".
Wakaanza kuchukua kila kilichokuwemo ndani ya nyumba, na mwisho wakamvua mke wa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) hata kitambaa alichokuwa amejifunikia, na baada ya kufanya dhulma yao hiyo wakaondoka na kumuacha Khalifa wa Waislamu akiwa keshafariki dunia na mkewe waliyemkata mkono akiwa taabani huku damu ikimtoka kwa wingi.

Maziko Yake


Ulipita muda kidogo kabla ya watu waliopo nje kutanabahi juu ya yaliyotendeka ndani ya nyumba ya Khalifa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu). Walipoingia walimkuta akiwa keshairudisha roho yake kwa Mola wake. Wakaichukua maiti yake na kuikosha, wakamsalia, kisha wakaenda nayo Al Baqiy-i kwa ajili ya kumzika. Lakini waasi wakafanya zogo kubwa sana na kuzuwia asizikwe humo, na badala yake akazikwa nje ya ukuta wa makaburi ya Al Baqiy-i, mahala panapoitwa 'Hishil kaukab', lakini wakati wa utawala wa Muawiya bin Abi Sufyan Radhiyallahu anhu, akaamrisha ukuta wa Al Baqiy-i uvunjwe na eneo lake kuongezwa ili kaburi la ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) liwemo ndani ya eneo la Al Baqiy-i.

"Wewe Ndiye Rafiki Yangu Peponi ewe ‘Uthmaan"


Katika Mujamma al Zawaida kitabu cha Manaqib, anasema Al Haythamiy;
"Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisema kuwaambia Maswahaba wake (Radhiya Llaahu ‘anhu):
"Leo nimeoneshwa daraja zenu Peponi", kisha akamsogelea Abu Bakr (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Pana mtu ninayemjua jina lake na jina la baba yake na la mama yake. Mtu huyu mlango wowote wa Peponi atakaoupitia atakuwa akiambiwa;
'Marhaban Marhaban (karibu karibu)".
Salman (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza;
"Bila shaka mtu huyu shani yake ni kubwa sana?"
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
"Mtu huyo ni Abu Bakr  bin Abi Quhafa" (Jina halisi la Abu Bakr Asw-Swiddiyq)
Kisha akamuelekea ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Ewe ‘Umar, nimeoneshwa kasri iliyojengwa kwa lulu nyeupe na kupambwa kwa Yakuti, nikauliza:
'Kasri ya nani hii?'
Nikaambiwa kuwa ni ya kijana wa Ki-Quraysh. Nikadhania ni yangu, na nilipotaka kuingia ndani, nikaambiwa; 'Muhammad, hii ni kasri ya ‘Umar, na hakuna kilichonizuwia nisiingie isipokuwa nilipokumbuka wivu wako".
‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akalia sana, kisha akamwambia;
"Nakufidia kwa baba na mama yangu. Nikuonee wivu wewe ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwendea ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Kila Mtume ana rafiki yake Peponi na wewe ndiye rafiki yangu Peponi (Ewe ‘Uthmaan)",
Kisha akauchukua mkono wa ‘Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Ewe ‘Aliy! hutoridhika ikiwa nyumba yako Peponi imekabiliana na nyumba yangu?"
Ali Akamwambia;
"Nakufidia kwa baba yangu na mama yangu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu".
Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia;
"Basi nyumba yako imeelekezana na nyumba yangu Peponi…"







[1] Huyu alikuwa Myahudi aliyesilimu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na aya nyingi katika Qurani ziliteremshwa kumsifia
[2] Ambaye ni Abdullahi bin Salaam (Radhiya Llahu anhu)
[3] Uthmaan (Radhiya Llahu ‘anhu) ndiye aliyeiandika Sura za mwanzo za Qurani,  Suratul Fatiha, Suratul Naas na Suratul Falaq.