Abu Hurayrah-mpokezi wa hadithi
“An ‘Abi Hurayrata radhiya
llah annhu qaal, Qaala rasulullah salla llahu alayhi wassalam….”
Mamilioni ya waislam tokea mwanzo
mwanzo mwa historia ya kiislam hadi hii leo wanaisoma kauli hii ‘kutoka kwa
Bwana Abu Hurayrah radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie amesema, mjumbe wa Mwenyezi
Mungu amesema…….”
Katika khutba, mihadhara, darsa
kwenye vitabu vya hadithi, sira na fiqh, Abu Hurayrah hutajwa mara kwa mara.
Kwa jitihada yake, hadithi nyingi za
Mtume (SAW) zimeweza kuwafika kizazi baada ya kizazi baada yake kufikia hadi
hata mtoto mdogo wa miaka mitatu/mine akiwa bado hayuko chekechea anamtaja Abu
Hurayrah.
Abu Hurayrah alisilimu mikononi mwa
At-tufail ibn Amr ambaye alikuwa mkuu wa kabila la Dhaws. Wadhaws
waliishi katika eneo la Tihamah ufukweni mwa bahari nyekundu kusini mwa bara la
Arab.
At-tufayl aliporudi kijijini kwake
baada ya kukutana na Mtume (SAW) na kusilimu mwanzoni mwazo mwa uislam, Abu
Hurayrah alikuwa wa mwanzo kuitikia wito. Alisilimu na kuwa tofauti na
wadhaws wengi ambao walikataa kusilimu na kuendelea na imani zao potofu.
Pia pale At-tufayl alipofanya tena
safari kwenda Makka, Abu Hurayrah akafuatana naye. Hapo akapata heshima
ya kukutana na Mtume (SAW) ambaye alimuuliza:
“Nani jina lako?”
Akajibu Abu Hurayrah, “Abdu Shams.”
“Kuanzia leo utakuwa Abdulrahman,”
akasema Mtume (SAW)
“Naam, Abdulrahman ewe mjumbe wa
Mwenyezi Mungu.”
Mtume (SAW) ilibidi alibadilishe
jina lake kwani kwa muislam kuitwa Abdu Shams, mja wa jua ni kinyume na kuwa
kama juo ndio mungu wake. Hivyo, akampa jina la Abdulrahman mja wa mwenye
kurehemu. Hata hivyo, jina lake la utani ‘Abu Hurayrah’ likiwa na maana
ya (baba wa paka) lilikuwa ndio maarufu zaidi kwani alipenda sana kufuga paka
tokea utotoni kwake.
Abu Hurayrah muda wote alikuwa
Tihamah mpaka mwanzoni mwa mwaka wa saba hijiriya ndipo alipowasili Madina
akiwa pamoja na baadhi ya watu wa kabila lake. Kipindi hicho Mtume (SAW)
alikuwa vitani Khaybar. Aliishi msikitini pamoja na Ahlu Suffa – wasiokuwa na
uwezo. Alikuwa bado kuoa na wala hana mtoto.
Hata hivyo, aliambatana na mama yake
ambaye wakati huo alikuwa bado kusilimu. Abu Hurayrah alikuwa akiomba na
kutamani mama yake asilimu lakini alikuwa mkaidi. Siku moja alimlingania
kuamini mungu mmoja na kumfuata Mtume (SAW) lakini mama yake alitamka maneno
kuhusu Mtume (SAW) ambayo yalimsikitisha sana, huku akitokwa na machozi
alielewa kwa Bwana Mtume (SAW) . Mtume Muhammad alipomuona na hali ile
akamuuliza:
“Nini kilichokufanya
ulie?”
“Ninajitahidi kumlingania mama yangu
uislam na kila siku ananikatalia, leo nilimlingania tena na nimesikia maneno
kutoka kwake na sikuyapenda. Hivyo, muombee dua kwa Mwenyezi Mungu aulainishe
moyo wake na kuingia uislam.”
Mtume akamkubalia na kumwombea dua,
Abu Hurayrah anasema:-
Nikaenda nyumbani na kukuta mlango
umefungwa nikasikia maji yakichuruzika kama mtu anaoga na nilipotaka kuingia
mama yangu akasema;
“Nisubiri hapo hapo, Abu Hurayrah,
alipomaliza na kuvaa nguo zake akaniruhusu niingie. Nilipoingia tu
akaanza kutamka kalima: “Ash-hadu anlaa ilaha ill allah waa-sh hadu anna
Muhammadan abduhu waraasuluhu.”
“Nikarudi mbio kwa Mtume (SAW) huku
nikitokwa machozi ya furaha ikiwa ni muda mfupi tu kabla yake nilitokwa machozi
ya huzuni na kumwambia Mtume (SAW), nina habari njema, ewe mjumbe wa Mwenyezi
Mungu. Mwenyezi Mungu (SW) ameitikia dua yako na kumuongoza mama wa Abu
Hurayrah kwenye uislam.”
Alipofika tu Madina, Abu Hurayrah
aliazimia kusoma. Zayd ibn Thabit (RA) anasema: “Wakati mimi Abu Hurayrah
na mmoja wa marafiki zangu tupo msikitini tukiomba na kufanya dhikr Mtume (SAW)
alitokezea na akaja kujumuika nasi. Tukanyamaza Mtume (SAW) akasema,
‘endeleeni na mlikuwa mkifanya’.
Hivyo mimi na rafiki yangu tukaomba
kwa Mwenyezi Mungu kabla ya Abu hurayrah na Mtume (SAW) akawa anaitikia Amin.
Kisha Abu Hurayrah akaomba kwa
kusema “Ewe Mola ninakuomba kwa ajili ya yale ambayo masahaba hawa wenzangu
wamekuomba na ninakuomba elimu ambayo haitosahauliwa.”
Mtume (SAW) akasema, ‘Amin’.
Na sisi tukasoma pia, “Tunakuomba
mola wetu elimu isiyosahaulika” Mtume (SAW) akajibu: “Kijana huyu wa kidhaws
tayari ameshaliomba hilo kabla yenu”
Akiwa na hifadhi madhubuti Abu Hurayrah
aliweza kuhifadhi katika kipindi cha miaka mine aliokaa na Mtume (SAW), hazina
ya busara iliyokuwa ikitoka midomoni mwake. Aliweza kugundua kwamba ana
kipaji cha kuhifadhi hiyo kipaji hiki alikitumia vyema katika kuuhudumia
uislam.
Abu Hurayrah hakuwa kama walivyokuwa
wengi wa Muhajirin wakijishughulisha na biashara. Wala hakuwa kama wa
ansari kwani hakuwa na shamba la kulima na wala vipando vya
kuvishughulikia. Alikaa sana na Mtume (SAW) na kufuatana naye kwenye
misafara yake.
Hata masahaba walishangazwa sana na
wingi wa hadithi alizozihifadhi na mara kwa mara humuuliza wakati alipozisikia
na katika mazingira gani. Mara moja Marwan Al – Hakam alitaka kumjaribu
Abu Hurayrah na kuona uwezo wake wa kuhifadhi. Alikaa naye kwenye chumba
na nyuma ya pazia kulikuwa na mwandishi ambaye aliagizwa aandike kila
atakachokisikia kutoka kwa Abu Hurayrah. Haya yote yanafanyika, Abu
Hurayrah hana habari.
Mwaka mmoja baadaye, Marwan akamwita
Abu Hurayarah na kumuuliza tena hadithi ile ile ambayo yule mwandishi
aliinukuu. Abu Hurayrah akaitamka vile vile bila ya kuongeza wala
kupunguza kitu.
Licha ya kuwa na kipaji cha
kuhifadhi. Abu Hurayrah alikuwa pia na hima ya kuwafundisha waislam
hadithi na dini kwa ujumla. Inasemekana siku moja alipita soko kuu la
Madina na kama kawaida ya sokoni aliwaona watu walivyoshughulika na
biashara. Alikaa na kuwatazama kwa muda kasha akawambia:
“Mbona mmelala hivi, watu wa
Madina?”
Wakamuuliza, “Umeona kitu gani kwetu
Abu Hurayrah mpaka kutwambia tumelala?”
“Mirathi ya Mtume (SAW) inagawiwa na
nyinyi mko hapa. Hamwendi kuchukua sehemu yenu?” aliwajibu.
“Wapi huko Abu Hurayrah?”
Akawajibu, “Msikitini”
Wakatoka mbio kuelekea msikitini,
Abu Hurayrah akawasubiri mpaka waliporudi.
“Vipi Abu Hurayrah? Mbona tumekwenda
msikitini na kuingia hadi ndani lakini hatukuona kitu chochote kinachogawiwa?”
Akawauliza, “Hamkumuona mtu yoyote
msikitini?”
“Eee ndio, tuliona baadhi ya watu
wanasali, wengine wanasoma Quran na wengine wanajadiliana kipi ni halali na
kipi haramu.” Wakamjibu.
“Ole wenu, yale ndio mirathi ya
Mtume (SAW)”.
Kwa kuwa Abu Hurayrah aliamua moja
kwa moja kujifunga na kutafuta elimu, hakupata muda wa kujishughulisha na kazi
au biashara na hivyo kuyafanya maisha yake kuwa duni na ya hali ya chini
kabisa. Mara nyingi alikuwa hana hata chakula na anaeleza:
“Nikiwa na njaa hujidai kwenda kwa
sahaba yoyote yule na kumuuliza aya fulani ya Quran na hukaa hapo kujifunza
ili tukimaliza tunakwenda pamoja kula.
Siku moja nilishikwa na njaa kali
sana mpaka nikaweka kijiwe juu ya tumbo langu, nikakaa pembezoni mwa ujia
wapitao masahaba. Akapita Abubakar na kama kawaida yangu nikamuuliza aya
ya Quran lakini hakunialika nyumbani kwake kisha alipita Umar naye pia
hakunialika. Akapita Mtume (SAW) ma aliponiona tu alijua kwamba nina njaa
akaniita, “Abu Hurayrah”
“Labbayka” nikamjibu na nikamfuata
mpaka nyumbani kwake. Akakuta bakuli la maziwa na akauliza ahli
yake: Mmeyapata haya?
Akajibiwa, “Kuna mtu kaleta hapa kwa
ajili yako”
Mtume (SAW) akaniambia, “ewe Abu
Hurayrah, nenda kwa Ahlu Suffah kawaalike”
Abu Hurayrah akafanya kama
alivyoagizwa na wote wakanywa maziwa yale.
Ukaja muda ambao waislam
wakabarikiwa na mali na utajiri aina kwa aina. Abu Hurayrah naye
akabahatika kupata sehemu yake. Akawa na nyumba mke na kujaaliwa
mtoto. Hata hivyo, utajiri haukumbadilisha kiti chochote wala hakusahau
siku za umasikini wake muda woke mwingi aliuutuma kwa ajili ya ibada kusimama
na kusali sala za usiku kwake ilikuwa ada na pia kwa familia yake.
Huanza yeye thuluthi ya usiku kisha humuamsha mkewe thuluthi ya pili na
thuluthi ya mwisho himalizia binti yao. Kwa utaratibu huu nyumba ya Abu
Hurayrah usiku mzima ni ibada, dhikr na sala.
Enzi za ukhalifa wa Umar, Abu
Hurayrah alichaguliwa kuwa Amir wa Bahrain. Umar aliwatahadharisha sana
ma-amir wake kutojishughulisha sana na kupata mali hata ikiwa ni kwa njia za
halali. Aliwaasa waishi maisha yasiyokuwa na fahari wale kuwa na anasa
kupindukia.
Wakati Abu Hurayrah yupo Bahrain
akabahatika kuwa tajiri mkubwa, Umar aliposikia haraka akamwita aje Madina.
Alipofika, Umar akataka apewe habari
vipi na wapi alipata mali zake. Abu Hurayrah akajibu,
“kutoka katika biashara yangu ya
kupandishia farasi na zawadi nilizokuwa nikiletewa”
“Zikabidhi zote Baytul Maal,”
akaamrisha Umar.
Abu Hurayrah akafanya kama
alivyoagizwa na akanyanyua mikono yake na kuomba, “Ewe mola msamaha Amirul
Muuminiin.” Baadaye Umar akamtaka tena Abu Hurayrah awe Amir lakini
alikataa na alipoulizwa kwa nini anakataa?.
Abu Hurayrah akajibu, “Ili heshima
yangu isiingie doa, utajiri wangu kuchukuliwa na mgongoni kwangu kusemwa.”
Akaongeza, “Naogopa kuhukumu bila ya
elimu na kuongea bila ya hekima.”
Maisha yake yote Abu Hurayrah
alikuwa mkarimu sana na mama yake. Anapotaka kutoka nyumbani huenda hadi
mlango wa chumba chake na kusema:
“Assalam Aleykum, Ya Ummatah,
warahamatullahi wabarakatuh.”
Na mama yake humjibu, “Waalykas
salaam, ya Bunayyah, warahmatullah wakarakatu.”
Kisha Abu Hurayrah husema pia, “Mwenyezi
Mungu akurehemu kwani ulinilea na kunienzi nilipokuwa mdogo.”
“Mwenyezi Mungu akurehemu kwani
umenitoa kwenye makosa nilipokuwa mzee,” mama humjibu.
Ilikuwa ni tabia yake Abu Hurayrah
kuwahimiza waislam kuwatendea wema wazazi wao.
Siku moja aliwaona watu wawili
wakitembea kwa pamoja. Mmoja alikuwa mkubwa wa umri kuliko mwenzake.
Akamuuliza yule aliyeonekana kuwa kijana:
“Huyu ni nani wako.”
Akajibu, “ni baba yangu.”
“Usimwite kwa jina lake, usitembee
ukawa uko mbele yake na usikae kabla yake.”Abu Hurayrah alimpa nasaha yule
kijana.
Waislam wana deni kubwa la heshima
kwa Abu Hurayrah hasa kwa kuweza kusaidia kuzihifadhi na kuzitunza hadithi za
Mtume Muhammad (SAW) na ambao ni msingi mkuu wa pili katika sheria baada ya
Quran. Alifariki mwa 59 Hijriya akiwa na umri wa miaka sabini na
nane.