12. SURAT YUSUF

  يُوسُفْ

12. SURAT YUSUF

(Imeteremka Makka)


Sura hii ni ya Makka, na Aya zake ni mia na kumi na moja. Ndani yake Mwenyezi Mungu amesimulia hadithi ya Yusuf katika Aya tisiini na nane, na ameitangulizia kwa Aya tatu alizo taja ndani yake huu ufunuo alio mteremshia Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zishuke juu yake.  Na ameuita ufunuo huu katika Aya ya kwanza: Kitabu kinacho bainisha. Na katika Aya ya pili akauiita: Qur'ani kwa Kiarabu, kuwa ni kuashiria kwamba ni haki yake uhifadhiwe kwa maandishi na katika vifua vya watu vile vile.  Kisha katika Aya ya tatu akataja kuwa ufunuo huu umekusanya simulizi nzuri kabisa, na ukataja kuwa Nabii Muhammad hakuwa akiyajua hayo kabla hakuteremshiwa huo Wahyi (ufunuo). Na hiyo ni dalili kuwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kisa hichi na Sura hii imemalizikia kwa kutilia mkazo yaliyo anzia. Na akamuelekeza Nabii mnamo Aya kumi azingatie kuwa masimulizi haya ni katika khabari za ghaibu, ambazo yeye Nabii, Salla Llahu alayhi wasallama, hakuwa akizijua, na kuzijua ukweli wake zilivyo, kabla ya kuteremshiwa Wahyi. Wala yeye hakuwa pamoja na hao ndugu zake Yusuf walipo kuwa wakipanga mipango yao, na wakiunda njama zao za shari kumuundia ndugu yao kwa baba. Kisha Qur'ani inamwambia Mtume kuwa inda na husda huwapelekea watu wengi kuingia ukafirini. Na kwamba pupa yake Mtume s.a.w. kuwa waamini wengi wao haitomfalia kitu, lakini Qur'ani inampoza kwa hayo kwa kuwa yeye hataki ujira, ila ni kuwa yeye anawaletea Qur'ani iwe ni uwongofu na ukumbusho kwa watu wote. Na mwisho wa Sura inaashiria Mitume ambao hadithi zao zimesimuliwa, na ukasimuliwa msimamo wa kaumu zao, na vipi mwishoe walivyo washinda makafiri wakosefu. Na katika hadithi hizi za Manabii pana mazingatio kwa wenye akili. Hakika hii Qur'ani inayo simulia masimulio haya na mengineyo si kitu cha kutungwa tu na kuzuliwa kuwa kinatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa uwongo. Hakika hii ni haki na kweli tupu, na hichi ni Kitabu kinacho sadikisha Vitabu sahihi vilivyo toka mbinguni, na ni uwongofu, na rehema kwa watu wanao zingatia na wakaamini.
Linalo onekana wazi katika sifa za Sura hii ni kuwa kimesimuliwa kisa cha Yusuf kwa ukamilifu wake. Na pia imeonekana kuwa katika ule ule ukoo mmoja upo uhasidi ulio enea na pia katika baadhi yao yapo mapenzi. Husda ya wana wa Yaaqub iliwapelekea kumtumbukiza ndugu yao kisimani. Lakini Mwenyezi Mungu alimlinda na vitimbi vyao, kama alivyo mkinga na matamanio ya mke wa Mheshimiwa pale Yusuf alipo fikilia utuuzima nyumbani kwa Mheshimiwa. Mwenyezi Mungu akamweka vizuri katika nchi ya Misri, na akamjaalia kuwa nchi hiyo iwe makimbilio (mategemeo) ya wale walio mpangia njama za kumdhuru.  Basi ni hivyo shani yake Subhanahu wa Taa'la kwa Manabii wake na vipenzi vyake. Huwanusuru dhidi ya maadui zao, na huwathibitisha na kuwaweka vyema katika ardhi maadamu wanaishika Haki na wanaiamini, na wanaishikilia kamba ya Mwenyezi Mungu.
 



بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

الر ۚ تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿١﴾
1. Alif Laam Raa. Hizo ni Aayaat za Kitabu kinachobainisha.


إِنَّا أَنزَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٢﴾
2. Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan kwa (lugha ya) Kiarabu ili mpate kutia akilini (muifahamu vyema).


نَحْنُ نَقُصُّ عَلَيْكَ أَحْسَنَ الْقَصَصِ بِمَا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ هَـٰذَا الْقُرْآنَ وَإِن كُنتَ مِن قَبْلِهِ لَمِنَ الْغَافِلِينَ ﴿٣﴾
3. Sisi Tunakusimulia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) simulizi nzuri kabisa kwa kukufunulia Wahy hii Qur-aan. Na hakika kabla ya (kukuteremshia Qur-aan) ulikuwa miongoni mwa walioghafilika.


إِذْ قَالَ يُوسُفُ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ إِنِّي رَأَيْتُ أَحَدَ عَشَرَ كَوْكَبًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ رَأَيْتُهُمْ لِي سَاجِدِينَ ﴿٤﴾
4. (Katika simulizi hizo, taja) Pale Yuwsuf alipomwambia baba yake: “Ee baba yangu! Hakika mimi nimeona (katika ndoto) nyota kumi na moja na jua na mwezi; nimeziona zikinisujudia.”


قَالَ يَا بُنَيَّ لَا تَقْصُصْ رُؤْيَاكَ عَلَىٰ إِخْوَتِكَ فَيَكِيدُوا لَكَ كَيْدًا ۖ إِنَّ الشَّيْطَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوٌّ مُّبِينٌ﴿٥﴾
5. (Baba yake) Akasema: “Ee mwanangu! Usisimulie ndoto yako (hii) kwa kaka zako watakupangia njama. Hakika shaytwaan kwa insani ni adui bayana.”


وَكَذَٰلِكَ يَجْتَبِيكَ رَبُّكَ وَيُعَلِّمُكَ مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ وَيُتِمُّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكَ وَعَلَىٰ آلِ يَعْقُوبَ كَمَا أَتَمَّهَا عَلَىٰ أَبَوَيْكَ مِن قَبْلُ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ عَلِيمٌ حَكِيمٌ﴿٦﴾
6. Na hivyo ndivyo Atakuteua Rabb (Mola) wako na Atakufunza tafsiri za al-ahaadiyth (masimulizi) na Atakutimizia Neema Yake juu yako, na juu ya kizazi cha Ya’quwb, kama Alivyoitimiza kabla juu ya baba zako; Ibraahiym na Is-haaq. Hakika Rabb wako ni ‘Aliymun-Hakiym (Mjuzi wa yote – Mwenye hikmah wa yote).


لَّقَدْ كَانَ فِي يُوسُفَ وَإِخْوَتِهِ آيَاتٌ لِّلسَّائِلِينَ﴿٧﴾
7. Kwa yakini imekuwa katika (kisa cha) Yuwsuf na kaka zake Aayaat (ishara,
dalili, zingatio) kwa waulizao.


إِذْ قَالُوا لَيُوسُفُ وَأَخُوهُ أَحَبُّ إِلَىٰ أَبِينَا مِنَّا وَنَحْنُ عُصْبَةٌ إِنَّ أَبَانَا لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ﴿٨﴾
8. (Kumbuka pale kaka zake) Waliposema: “Bila shaka Yuwsuf na ndugu yake (wa baba na mama mmoja) ni vipenzi zaidi kwa baba yetu kuliko sisi, na hali sisi (wa mama wengine) ni kundi lenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu bayana.”


اقْتُلُوا يُوسُفَ أَوِ اطْرَحُوهُ أَرْضًا يَخْلُ لَكُمْ وَجْهُ أَبِيكُمْ وَتَكُونُوا مِن بَعْدِهِ قَوْمًا صَالِحِينَ﴿٩﴾
9. “Muueni Yuwsuf, au mtupilieni mbali katika nchi ya mbali ili uso wa baba yenu ukuelekeeni nyinyi (akupendeni) na muwe baada ya hapo Swalihina.”


قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ لَا تَقْتُلُوا يُوسُفَ وَأَلْقُوهُ فِي غَيَابَتِ الْجُبِّ يَلْتَقِطْهُ بَعْضُ السَّيَّارَةِ إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ﴿١٠﴾
10. Akasema msemaji miongoni wao: “Msimuue Yuwsuf, (lakini) mtupeni katika kisima kirefu watamwokota baadhi ya misafara, ikiwa nyinyi ni wenye (kuazimia) kufanya.”


قَالُوا يَا أَبَانَا مَا لَكَ لَا تَأْمَنَّا عَلَىٰ يُوسُفَ وَإِنَّا لَهُ لَنَاصِحُونَ﴿١١﴾
11. (Baada ya kuwafikiana) Wakasema: “Ee baba yetu! Una nini, hutuamini juu ya Yuwsuf, na hakika sisi kwake ni wenye kumnasihi?” 


أَرْسِلْهُ مَعَنَا غَدًا يَرْتَعْ وَيَلْعَبْ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ﴿١٢﴾
12. “Mpeleke pamoja nasi kesho, ale atakacho na acheze na sisi tutamhifadhi.” 



قَالَ إِنِّي لَيَحْزُنُنِي أَن تَذْهَبُوا بِهِ وَأَخَافُ أَن يَأْكُلَهُ الذِّئْبُ وَأَنتُمْ عَنْهُ غَافِلُونَ﴿١٣﴾
13. (Baba yao) Akasema: “Hakika mimi inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na nakhofu (kuja) kuliwa na mbwa mwitu; nanyi muwe mmeghafilika naye.” 


قَالُوا لَئِنْ أَكَلَهُ الذِّئْبُ وَنَحْنُ عُصْبَةٌ إِنَّا إِذًا لَّخَاسِرُونَ﴿١٤﴾
14. Wakasema: “Ikiwa mbwa mwitu atamla na hali sisi ni kundi lenye nguvu (la kumlinda); hakika sisi hapo bila shaka tutakuwa wenye kukhasirika.”


فَلَمَّا ذَهَبُوا بِهِ وَأَجْمَعُوا أَن يَجْعَلُوهُ فِي غَيَابَتِ الْجُبِّ ۚ وَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ لَتُنَبِّئَنَّهُم بِأَمْرِهِمْ هَـٰذَا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ﴿١٥﴾
15. Basi walipokwenda naye, na wakakubaliana wamtie katika kisima kirefu. Tukamtia ilhamu (Yuwsuf) kwamba bila shaka (iko siku) utakuja kuwajulisha jambo lao hili; na (hali) wao hawahisi.


وَجَاءُوا أَبَاهُمْ عِشَاءً يَبْكُونَ﴿١٦﴾
16.  Wakaja kwa baba yao usiku wakilia.


قَالُوا يَا أَبَانَا إِنَّا ذَهَبْنَا نَسْتَبِقُ وَتَرَكْنَا يُوسُفَ عِندَ مَتَاعِنَا فَأَكَلَهُ الذِّئْبُ ۖ وَمَا أَنتَ بِمُؤْمِنٍ لَّنَا وَلَوْ كُنَّا صَادِقِينَ﴿١٧﴾
17. Wakasema: “Ee baba yetu! Hakika sisi tulikwenda (tukawa) tunashindana mbio na tulimwacha Yuwsuf kwenye vitu vyetu; basi (akatokea) mbwa mwitu akamla. Nawe hutotuamini japo tukiwa niwakweli.”


وَجَاءُوا عَلَىٰ قَمِيصِهِ بِدَمٍ كَذِبٍ ۚ قَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنفُسُكُمْ أَمْرًا ۖ فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ وَاللَّـهُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ﴿١٨﴾
18.  Na walikuja (huku wameweka) juu ya shati lake damu ya uongo. (Baba yao) Akasema: “Bali zimekushawishini nafsi zenu jambo. Basi subira njema, na Allaah Al-Musta’aanu (Aombwaye msaada) juu ya (hayo) mnayoelezea.”


وَجَاءَتْ سَيَّارَةٌ فَأَرْسَلُوا وَارِدَهُمْ فَأَدْلَىٰ دَلْوَهُ ۖ قَالَ يَا بُشْرَىٰ هَـٰذَا غُلَامٌ ۚ وَأَسَرُّوهُ بِضَاعَةً ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَعْمَلُونَ﴿١٩﴾
19.  Ukaja msafara wakamtuma mtekaji maji wao, naye akatumbukiza ndoo yake. Akasema: “Ee bishara njema! Huyu ni ghulamu!” na wakamficha (wakadai kuwa) ni (miongoni mwa) bidhaa (zao). Na Allaah ni ‘Aliym (Mjuzi) kwa yale wanayoyatenda. 


وَشَرَوْهُ بِثَمَنٍ بَخْسٍ دَرَاهِمَ مَعْدُودَةٍ وَكَانُوا فِيهِ مِنَ الزَّاهِدِينَ﴿٢٠﴾
20. Wakamuuza kwa thamani pungufu (kidogo tu) ya dirham za kuhesabika; na walikuwa ni wenye kuridhika na kidogo.


وَقَالَ الَّذِي اشْتَرَاهُ مِن مِّصْرَ لِامْرَأَتِهِ أَكْرِمِي مَثْوَاهُ عَسَىٰ أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا ۚ وَكَذَٰلِكَ مَكَّنَّا لِيُوسُفَ فِي الْأَرْضِ وَلِنُعَلِّمَهُ مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ ۚ وَاللَّـهُ غَالِبٌ عَلَىٰ أَمْرِهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴿٢١﴾
21. Na yule aliyemnunua huko Misri alimwamrisha mke wake (kwa kusema): “Mkirimu makazi yake, huenda akatufaa au tutamchukua kama ni waladi (wetu).” Na hivyo ndivyo Tulivyommakinisha Yuwsuf katika ardhi na ili Tumfunzetafsiri za al-ahaadiyth (matukio). Na Allaah ni Mwenye kushinda juu ya jambo Lake, lakini watu wengi hawajui.


وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ﴿٢٢﴾
22. Na (Yuwsuf) alipobaleghe kufikia umri wa kupevuka, Tulimpa hukumu na elimu. Na hivyo ndivyo Tunavyowalipa wafanyao ihsaan.


وَرَاوَدَتْهُ الَّتِي هُوَ فِي بَيْتِهَا عَن نَّفْسِهِ وَغَلَّقَتِ الْأَبْوَابَ وَقَالَتْ هَيْتَ لَكَ ۚ قَالَ مَعَاذَ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ رَبِّي أَحْسَنَ مَثْوَايَ ۖ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ﴿٢٣﴾
23. Na (yule mwanamke) ambaye (Yuwsuf) alikuwa katika nyumba yake akamtongoza kinyume na nafsi yake (Yuwsuf); na akafunga milango, na akasema: “Haya njoo!” (Yuwsuf) Akasema: “Najikinga kwa Allaah! Hakika yeye bwana wangu amenifanyia makazi mazuri. Hakika madhalimu hawafaulu.”


وَلَقَدْ هَمَّتْ بِهِ ۖ وَهَمَّ بِهَا لَوْلَا أَن رَّأَىٰ بُرْهَانَ رَبِّهِ ۚ كَذَٰلِكَ لِنَصْرِفَ عَنْهُ السُّوءَ وَالْفَحْشَاءَ ۚ إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُخْلَصِينَ﴿٢٤﴾
24. Na kwa yakini aliingiwa hima naye (kumtamani Yuwsuf) na (Yuwsuf) angeliingiwa na hima kama asingeliona buruhani kutoka kwa Rabb (Mola) wake. Hivyo ndivyo Tunavyomwepusha na uovu na machafu. Hakika yeye ni miongoni mwa waja Wetu al-mukhlaswiyna (waliochaguliwa na kutakaswa).


وَاسْتَبَقَا الْبَابَ وَقَدَّتْ قَمِيصَهُ مِن دُبُرٍ وَأَلْفَيَا سَيِّدَهَا لَدَى الْبَابِ ۚ قَالَتْ مَا جَزَاءُ مَنْ أَرَادَ بِأَهْلِكَ سُوءًا إِلَّا أَن يُسْجَنَ أَوْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٢٥﴾
25. Wakakimbilia mlangoni wote wawili na (yule mwanamke) akairarua kanzu (ya Yuwsuf) yake kwa nyuma, na wakamkuta bwana wake mlangoni. (Mke wa al-‘Aziyz) Akasema: “Hakuna jazaa ya anayemtakia uovu ahli (mke) wako isipokuwa kufungwa jela au (apewe) adhabu iumizayo.”


قَالَ هِيَ رَاوَدَتْنِي عَن نَّفْسِي ۚ وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِّنْ أَهْلِهَا إِن كَانَ قَمِيصُهُ قُدَّ مِن قُبُلٍ فَصَدَقَتْ وَهُوَ مِنَ الْكَاذِبِينَ﴿٢٦﴾
26.  (Yuwsuf) Akasema: “Yeye ndiye aliyenitaka kinyume na nafsi yangu.” Na akashuhudia shahidi miongoni mwa ahli zake (mwanamke kwa kusema): “Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele, basi mwanamke (atakuwa) amesema kweli; naye (Yuwsuf) ni miongoni mwa waongo.


وَإِن كَانَ قَمِيصُهُ قُدَّ مِن دُبُرٍ فَكَذَبَتْ وَهُوَ مِنَ الصَّادِقِينَ﴿٢٧﴾
27. Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma, basi mwanamke (atakuwa) amesema uongo; naye (Yuwsuf) ni miongoni mwa wakweli.


فَلَمَّا رَأَىٰ قَمِيصَهُ قُدَّ مِن دُبُرٍ قَالَ إِنَّهُ مِن كَيْدِكُنَّ ۖ إِنَّ كَيْدَكُنَّ عَظِيمٌ﴿٢٨﴾
28. Basi (yule mume) alipoona kanzu yake imechanwa nyuma; alisema: “Hakika hii ni katika vitimbi vyenu wanawake. Hakika vitimbi vyenu wanawake ni vikuu.”


يُوسُفُ أَعْرِضْ عَنْ هَـٰذَا ۚ وَاسْتَغْفِرِي لِذَنبِكِ ۖ إِنَّكِ كُنتِ مِنَ الْخَاطِئِينَ﴿٢٩﴾
29. “Yuwsuf yaachilie mbali haya. Na (wewe mwanamke) omba maghfirah kwa dhambi lako. Hakika wewe ulikuwa miongoni mwa wakosao.”



وَقَالَ نِسْوَةٌ فِي الْمَدِينَةِ امْرَأَتُ الْعَزِيزِ تُرَاوِدُ فَتَاهَا عَن نَّفْسِهِ ۖ قَدْ شَغَفَهَا حُبًّا ۖ إِنَّا لَنَرَاهَا فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ﴿٣٠﴾
30. Na wanawake katika mji ule wakasema: “mke wa al-Aziyz anataka kumtongoza kijana (mtumishi) wake kinyume na nafsi yake.” Kwa yakini amemuathiri kwa mapenzi. Hakika sisi tunamuona (mke wa al-Aziyz) yumo katika upotofu bayana.”


فَلَمَّا سَمِعَتْ بِمَكْرِهِنَّ أَرْسَلَتْ إِلَيْهِنَّ وَأَعْتَدَتْ لَهُنَّ مُتَّكَأً وَآتَتْ كُلَّ وَاحِدَةٍ مِّنْهُنَّ سِكِّينًا وَقَالَتِ اخْرُجْ عَلَيْهِنَّ ۖ فَلَمَّا رَأَيْنَهُ أَكْبَرْنَهُ وَقَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ وَقُلْنَ حَاشَ لِلَّـهِ مَا هَـٰذَا بَشَرًا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا مَلَكٌ كَرِيمٌ﴿٣١﴾
31. Basi (mke wa al-Aziyz) aliposikia vitimbi vyao, aliwapelekea (mwaliko) na akawaandalia karamu na akampa kila mmoja wao kisu. Kisha akasema (kumwambia Yuwsuf): “Tokeza mbele yao.” Basi walipomuona walimtukuza (kwa uzuri wake), na wakajikatakata mikono yao (bila ya kujitambua), na wakasema: “Haasha liLLaah!  Huyu si mtu! Huyu si yeyote ila ni Malaika mtukufu.”


قَالَتْ فَذَٰلِكُنَّ الَّذِي لُمْتُنَّنِي فِيهِ ۖ وَلَقَدْ رَاوَدتُّهُ عَن نَّفْسِهِ فَاسْتَعْصَمَ ۖ وَلَئِن لَّمْ يَفْعَلْ مَا آمُرُهُ لَيُسْجَنَنَّ وَلَيَكُونًا مِّنَ الصَّاغِرِينَ﴿٣٢﴾
32. (Mke wa al-‘Aziyz) akasema: “Basi huyo ndiye (kijana) mliyekuwa mkinilaumia. Na kwa yakini nilimtamani kinyume na nafsi yake, akajilinda. Na kama hatofanya ninalomuamrisha, basi bila shaka atafungwa jela, na bila shaka atakuwa miongoni mwa waliodunishwa (dhalili).”


قَالَ رَبِّ السِّجْنُ أَحَبُّ إِلَيَّ مِمَّا يَدْعُونَنِي إِلَيْهِ ۖ وَإِلَّا تَصْرِفْ عَنِّي كَيْدَهُنَّ أَصْبُ إِلَيْهِنَّ وَأَكُن مِّنَ الْجَاهِلِينَ﴿٣٣﴾
33. (Yuwsuf) Akasema (akiomba du’aa): “Ee Rabb (Mola) wangu!  Nastahabu zaidi (kufungwa) jela kwangu kuliko yale wanayoniitia. Na Usiponiepusha na vitimbi vyao nitaelemea kwao na nitakuwa miongoni mwa majahili.”


فَاسْتَجَابَ لَهُ رَبُّهُ فَصَرَفَ عَنْهُ كَيْدَهُنَّ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٣٤﴾
34. Basi Rabb (Mola) wake Akamuitikia (du’aa yake); Akamuepusha na vitimbi vyao. Hakika Yeye ni As-Samiy’ul-‘Aliym (Mwenye kusikia yote – Mjuzi wa yote).


ثُمَّ بَدَا لَهُم مِّن بَعْدِ مَا رَأَوُا الْآيَاتِ لَيَسْجُنُنَّهُ حَتَّى حِينٍ﴿٣٥﴾
35. Kisha ikawadhihirikia (kwa al-‘Aziyz na watu wake) baada ya kuona Aayaat (dalili) (za utakaso wa Nabiy Yuwsuf), kuwa wamfunge jela kwa muda kidogo.


وَدَخَلَ مَعَهُ السِّجْنَ فَتَيَانِ ۖ قَالَ أَحَدُهُمَا إِنِّي أَرَانِي أَعْصِرُ خَمْرًا ۖ وَقَالَ الْآخَرُ إِنِّي أَرَانِي أَحْمِلُ فَوْقَ رَأْسِي خُبْزًا تَأْكُلُ الطَّيْرُ مِنْهُ ۖ نَبِّئْنَا بِتَأْوِيلِهِ ۖ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ﴿٣٦﴾
36.  Wakaingia pamoja naye jela vijana wawili.  Mmoja wao akasema: “Hakika mimi nimejiona (ndotoni) kuwa nakamua mvinyo.” Na mwengine akasema: “Hakika mimi nimejiona (ndotoni) nabeba juu ya kichwa changu mikate wanaila ndege humo.” (Wakasema) “Tujulishe tafsiri yake, hakika sisi tunakuona (wewe) ni miongoni mwa watu wa ihsaan”.


قَالَ لَا يَأْتِيكُمَا طَعَامٌ تُرْزَقَانِهِ إِلَّا نَبَّأْتُكُمَا بِتَأْوِيلِهِ قَبْلَ أَن يَأْتِيَكُمَا ۚ ذَٰلِكُمَا مِمَّا عَلَّمَنِي رَبِّي ۚ إِنِّي تَرَكْتُ مِلَّةَ قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ﴿٣٧﴾
37. (Yuwsuf) Akasema: “Hakitakufikieni chakula chochote mtakachoruzukiwa isipokuwa nitakujulisheni tafsiri yake kabla havijakufikieni. Haya ni katika Aliyonifunza Rabb (Mola) wangu. Hakika mimi nimeacha millah (dini) ya watu wasiomwamini Allaah na wao kwa Aakhirah wenye kuikanusha.


وَاتَّبَعْتُ مِلَّةَ آبَائِي إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۚ مَا كَانَ لَنَا أَن نُّشْرِكَ بِاللَّـهِ مِن شَيْءٍ ۚ ذَٰلِكَ مِن فَضْلِ اللَّـهِ عَلَيْنَا وَعَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ﴿٣٨﴾
38. “Na nimefuata millah ya baba zangu; Ibraahiym, na Is-haaq na Ya’quwb. Haikutupasa kumshirikisha Allaah na kitu chochote. Hiyo ni katika fadhila za Allaah juu yetu na juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.”


يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ﴿٣٩﴾
39. “Enyi masahibu wangu wawili wa jela. Je, waungu wengi wanaofarakana ni bora (kuabudiwa) au Allaah (ambaye ni) Al-Waahidul-Qahhaar (Mmoja Pekee - Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Mshindi, Asiyepingika.”)


مَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا أَسْمَاءً سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ ۚ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ ۚ أَمَرَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴿٤٠﴾
40. “Hamuabudu pasi Naye (Allaah) isipokuwa majina (ya masanamu) mmeyaita nyinyi na baba zenu, Hakuyateremshia Allaah kwayo ushahidi (au amri) yoyote. Hakuna hukumu isipokuwa ya Allaah. Ameamrisha kwamba msimwabudu (yeyote au chochote) isipokuwa Yeye Pekee. Hiyo ndio Dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui.”


يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَمَّا أَحَدُكُمَا فَيَسْقِي رَبَّهُ خَمْرًا ۖ وَأَمَّا الْآخَرُ فَيُصْلَبُ فَتَأْكُلُ الطَّيْرُ مِن رَّأْسِهِ ۚ قُضِيَ الْأَمْرُ الَّذِي فِيهِ تَسْتَفْتِيَانِ﴿٤١﴾
41. “Enyi masahibu wangu wawili wa jela! Ama mmoja wenu atamnywesha bwana wake mvinyo. Na ama mwengine atasulubiwa, na ndege watakula kutoka kichwani mwake. Imeshahukumiwa jambo ambalo mkiliulizia.”


وَقَالَ لِلَّذِي ظَنَّ أَنَّهُ نَاجٍ مِّنْهُمَا اذْكُرْنِي عِندَ رَبِّكَ فَأَنسَاهُ الشَّيْطَانُ ذِكْرَ رَبِّهِ فَلَبِثَ فِي السِّجْنِ بِضْعَ سِنِينَ﴿٤٢﴾
42. (Na Yuwsuf) Akasema kumwambia yule aliyejua kuwa ataokoka miongoni mwa wale wawili: “Nikimbuke mbele ya bwana wako.” Lakini shaytwaan alimsahaulisha kumkumbuka kwa bwana wake. Basi (Yuwsuf) akabakia jela miaka kadhaa.



وَقَالَ الْمَلِكُ إِنِّي أَرَىٰ سَبْعَ بَقَرَاتٍ سِمَانٍ يَأْكُلُهُنَّ سَبْعٌ عِجَافٌ وَسَبْعَ سُنبُلَاتٍ خُضْرٍ وَأُخَرَ يَابِسَاتٍ ۖ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَفْتُونِي فِي رُؤْيَايَ إِن كُنتُمْ لِلرُّؤْيَا تَعْبُرُونَ﴿٤٣﴾
43. Na (siku moja) mfalme akasema: “Hakika mimi naona (ndotoni) ng’ombe saba wanene wanaliwa na ng’ombe saba waliokonda, na (pia) mashuke saba ya kijani na mengineyo (saba) yabisi (makavu). Enyi wakuu (na washauri wangu)! Nifutuni (tafsiri) katika ndoto yangu, mkiwa ni wenye kuagua ndoto”.


قَالُوا أَضْغَاثُ أَحْلَامٍ ۖ وَمَا نَحْنُ بِتَأْوِيلِ الْأَحْلَامِ بِعَالِمِينَ﴿٤٤﴾
44.  (Wakuu) Wakasema: “Ndoto za mparaganyiko (hizo); nasi si wenye kuelewa kufasiri ndoto.”


وَقَالَ الَّذِي نَجَا مِنْهُمَا وَادَّكَرَ بَعْدَ أُمَّةٍ أَنَا أُنَبِّئُكُم بِتَأْوِيلِهِ فَأَرْسِلُونِ﴿٤٥﴾
45. (Hapo ndipo) Aliposema yule aliyeokoka kati ya wale (masahibu wa jela), na akakumbuka baada ya muda (maagizo ya Yuwsuf): “Mimi nitakujulisheni kuhusu tafsiri yake. Basi, nitumeni (kwa Yuwsuf).”


يُوسُفُ أَيُّهَا الصِّدِّيقُ أَفْتِنَا فِي سَبْعِ بَقَرَاتٍ سِمَانٍ يَأْكُلُهُنَّ سَبْعٌ عِجَافٌ وَسَبْعِ سُنبُلَاتٍ خُضْرٍ وَأُخَرَ يَابِسَاتٍ لَّعَلِّي أَرْجِعُ إِلَى النَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَعْلَمُونَ﴿٤٦﴾
46. “Yuwsuf! Ee mkweli! Tufutu katika (ndoto ya) ng’ombe saba wanene wanaliwa na ng’ombe saba waliokonda, na mashuke saba ya kijani na mengineyo (saba) yabisi; ili nirejee kwa watu ili wapate kujua.”


قَالَ تَزْرَعُونَ سَبْعَ سِنِينَ دَأَبًا فَمَا حَصَدتُّمْ فَذَرُوهُ فِي سُنبُلِهِ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّا تَأْكُلُونَ﴿٤٧﴾
47.  (Yuwsuf) Akasema: “Mtalima miaka saba mfululizo. Mtakachokivuna kiacheni katika mashuke yake isipokuwa kichache mtakachokula


ثُمَّ يَأْتِي مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ سَبْعٌ شِدَادٌ يَأْكُلْنَ مَا قَدَّمْتُمْ لَهُنَّ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّا تُحْصِنُونَ﴿٤٨﴾
48. “Kisha itakuja baada ya hapo (miaka) saba ya shida itakayokula vile mlivyovitanguliza kuviweka kwa ajili yao isipokuwa kidogo katika vile mtakavyovihifadhi (kama akiba).


ثُمَّ يَأْتِي مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ عَامٌ فِيهِ يُغَاثُ النَّاسُ وَفِيهِ يَعْصِرُونَ﴿٤٩﴾
49. “Kisha utakuja baada ya hapo mwaka (ambao) humo watu watasaidiwa kwa kunyweshewa mvua na humo watakamua (vya kukamuliwa).”


وَقَالَ الْمَلِكُ ائْتُونِي بِهِ ۖ فَلَمَّا جَاءَهُ الرَّسُولُ قَالَ ارْجِعْ إِلَىٰ رَبِّكَ فَاسْأَلْهُ مَا بَالُ النِّسْوَةِ اللَّاتِي قَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ ۚ إِنَّ رَبِّي بِكَيْدِهِنَّ عَلِيمٌ﴿٥٠﴾
50.  Mfalme akasema:  “Nileteeni (Yuwsuf).” Basi (Yuwsuf) alipojiwa na mjumbe (wa mfalme) alisema: “Rejea kwa bwana wako umuulize nini mkasa wa wanawake waliojikatakata mikono yao. Hakika Rabb (Mola) wangu kwa vitimbi vyao ni ‘Aliym (Mjuzi).”


قَالَ مَا خَطْبُكُنَّ إِذْ رَاوَدتُّنَّ يُوسُفَ عَن نَّفْسِهِ ۚ قُلْنَ حَاشَ لِلَّـهِ مَا عَلِمْنَا عَلَيْهِ مِن سُوءٍ ۚ قَالَتِ امْرَأَتُ الْعَزِيزِ الْآنَ حَصْحَصَ الْحَقُّ أَنَا رَاوَدتُّهُ عَن نَّفْسِهِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ﴿٥١﴾
51. (Mfalme akawauliza wanawake): “Nini jambo lenu lilikuwa mlipomtaka Yuwsuf kinyume na nafsi yake?” Wakasema: “Haasha liLLaah! Hatukujua uovu wowote kwake.” Mke wa al-Aziyz (akakiri) akasema: “Hivi sasa umefichuka ukweli! Mimi nilimtongoza (Yuwsuf) kinyume na nafsi yake. Na hakika yeye bila shaka ni miongoni mwa wakweli”.


ذَٰلِكَ لِيَعْلَمَ أَنِّي لَمْ أَخُنْهُ بِالْغَيْبِ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي كَيْدَ الْخَائِنِينَ﴿٥٢﴾
52. (Mke wa al-Aziyz au Yuwusuf akasema: Nimeuliza) “Hivyo ili (al-Aziyz) apate kujua kwamba mimi sikumfanyia khiyana nyuma yake; na kwamba Allaah Haongozi hila za makhaini.”


وَمَا أُبَرِّئُ نَفْسِي ۚ إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ إِلَّا مَا رَحِمَ رَبِّي ۚ إِنَّ رَبِّي غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥٣﴾
53. Na siitoi hatiani nafsi yangu. Hakika nafsi ni yenye kuamrisha maovu isipokuwa (ile) ambayo Rabb (Mola) wangu Ameirehemu.  Hakika Rabb wangu ni Ghafuwrur-Rahiym (Mwingi wa kughufuria - Mwenye kurehemu).

وَقَالَ الْمَلِكُ ائْتُونِي بِهِ أَسْتَخْلِصْهُ لِنَفْسِي ۖ فَلَمَّا كَلَّمَهُ قَالَ إِنَّكَ الْيَوْمَ لَدَيْنَا مَكِينٌ أَمِينٌ ﴿٥٤﴾
54. Na mfalme akasema: “Nileteeni (Yuwsuf) nimchague awe wangu khaswa.” Basi aliposema naye, akasema: “Hakika wewe leo kwetu umetamakani kwa cheo na umekuwa muaminiwa.”


قَالَ اجْعَلْنِي عَلَىٰ خَزَائِنِ الْأَرْضِ ۖ إِنِّي حَفِيظٌ عَلِيمٌ ﴿٥٥﴾
55.  (Yuwsuf) Akasema: “Niweke katika kusimamia hazina ya nchi; hakika mimi ni mhifadhi mjuzi.”

وَكَذَٰلِكَ مَكَّنَّا لِيُوسُفَ فِي الْأَرْضِ يَتَبَوَّأُ مِنْهَا حَيْثُ يَشَاءُ ۚ نُصِيبُ بِرَحْمَتِنَا مَن نَّشَاءُ ۖ وَلَا نُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾
56. Na hivyo ndivyo Tulivyommakinisha Yuwsuf katika ardhi; anakaa humo popote atakapo. Tunamfikishia Rahmah Yetu Tumtakaye, na wala Hatupotezi ujira wa watendao ihsaan.


وَلَأَجْرُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ ﴿٥٧﴾
57. Na bila shaka ujira wa Aakhirah ni bora zaidi kwa wale walioamini na wakawa na taqwa.


وَجَاءَ إِخْوَةُ يُوسُفَ فَدَخَلُوا عَلَيْهِ فَعَرَفَهُمْ وَهُمْ لَهُ مُنكِرُونَ ﴿٥٨﴾
58. Wakaja kaka zake Yuwsuf (kutafuta chakula); wakaingia kwake, basi yeye akawatambua, lakini wao hawakumtambua.


وَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ قَالَ ائْتُونِي بِأَخٍ لَّكُم مِّنْ أَبِيكُمْ ۚ أَلَا تَرَوْنَ أَنِّي أُوفِي الْكَيْلَ وَأَنَا خَيْرُ الْمُنزِلِينَ﴿٥٩﴾
59. Na alipowatayarishia mahitaji yao (ya chakula, Yuwsuf) akasema: “Njooni na ndugu yenu kutoka kwa baba yenu. Je, hamuoni kwamba hakika mimi natimiza kikamilifu kipimo nami ni mbora wa wenye kukaribisha (na kukirimu)?


فَإِن لَّمْ تَأْتُونِي بِهِ فَلَا كَيْلَ لَكُمْ عِندِي وَلَا تَقْرَبُونِ ﴿٦٠﴾
60. “Msiponijia naye, basi hamtokuwa na kipimo kwangu (cha chakula) wala msinikurubie.”


قَالُوا سَنُرَاوِدُ عَنْهُ أَبَاهُ وَإِنَّا لَفَاعِلُونَ ﴿٦١﴾
61.  Wakasema: “Tutambembeleza baba yake na bila shaka tutafanya.”



وَقَالَ لِفِتْيَانِهِ اجْعَلُوا بِضَاعَتَهُمْ فِي رِحَالِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَعْرِفُونَهَا إِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٦٢﴾
62. (Yuwsuf) Akawaambia watumishi wake: “Wekeni bidhaa zao (thamani walizonunulia chakula) katika mizigo yao, huenda wakazitambua watakaporudi kwa ahli zao, huenda wakarejea (tena).”



فَلَمَّا رَجَعُوا إِلَىٰ أَبِيهِمْ قَالُوا يَا أَبَانَا مُنِعَ مِنَّا الْكَيْلُ فَأَرْسِلْ مَعَنَا أَخَانَا نَكْتَلْ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ﴿٦٣﴾
63. Basi waliporejea kwa baba yao, walisema: “Ee baba yetu! Tumenyimwa kipimo (cha chakula) basi mpeleke pamoja nasi ndugu yetu, tupate kupimiwa; na sisi bila shaka tutamhifadhi.”


قَالَ هَلْ آمَنُكُمْ عَلَيْهِ إِلَّا كَمَا أَمِنتُكُمْ عَلَىٰ أَخِيهِ مِن قَبْلُ ۖ فَاللَّـهُ خَيْرٌ حَافِظًا ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٦٤﴾
64.  (Baba yao) Akasema: “Je, nimwaminishe kwenu isipokuwa kama nilivyokuaminini juu ya kaka yake (Yuwsuf) kabla? Basi Allaah ni Mbora wa wenye kuhifadhi. Naye ni Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”.


وَلَمَّا فَتَحُوا مَتَاعَهُمْ وَجَدُوا بِضَاعَتَهُمْ رُدَّتْ إِلَيْهِمْ ۖ قَالُوا يَا أَبَانَا مَا نَبْغِي ۖ هَـٰذِهِ بِضَاعَتُنَا رُدَّتْ إِلَيْنَا ۖ وَنَمِيرُ أَهْلَنَا وَنَحْفَظُ أَخَانَا وَنَزْدَادُ كَيْلَ بَعِيرٍ ۖ ذَٰلِكَ كَيْلٌ يَسِيرٌ ﴿٦٥﴾
65.  Walipofungua mizigo yao, wakakuta bidhaa zao zimerudishwa kwao. Wakasema: “Ee baba yetu! Tunataka nini zaidi? Hizi (ni) bidhaa zetu zimerudishwa kwetu, na tutawaletea chakula ahli zetu, na tutamhifadhi ndugu yetu, na tutapata ziada ya kipimo cha ngamia (cha chakula). Hicho ni kipimo chepesi.”


قَالَ لَنْ أُرْسِلَهُ مَعَكُمْ حَتَّىٰ تُؤْتُونِ مَوْثِقًا مِّنَ اللَّـهِ لَتَأْتُنَّنِي بِهِ إِلَّا أَن يُحَاطَ بِكُمْ ۖ فَلَمَّا آتَوْهُ مَوْثِقَهُمْ قَالَ اللَّـهُ عَلَىٰ مَا نَقُولُ وَكِيلٌ ﴿٦٦﴾
66. (Baba yao) Akasema: “Sitampeleka pamoja nanyi mpaka mnipe ahadi ya Allaah kwamba; bila shaka mtamrudisha kwangu isipokuwa ikiwa mmezungukwa (na maadui).” Basi walipompa ahadi yao, akasema: “Allaah kwa tuyasemayo ni Wakiyl (Mdhamini Anayetegemewa kwa yote).”


وَقَالَ يَا بَنِيَّ لَا تَدْخُلُوا مِن بَابٍ وَاحِدٍ وَادْخُلُوا مِنْ أَبْوَابٍ مُّتَفَرِّقَةٍ ۖ وَمَا أُغْنِي عَنكُم مِّنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ ۖ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ ۖ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ ۖوَعَلَيْهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُتَوَكِّلُونَ ﴿٦٧﴾
67. Na akasema: “Enyi wanangu! Msiingie kwa (kupitia) mlango mmoja, bali ingieni kwa milango tofauti. Na wala siwezi kukufaeni chochote mbele ya (majaaliwa ya) Allaah. Hapana hukumu isipokuwa kwa Allaah. Kwake natawakali. Na Kwake watawakali wanaotawakali.”


وَلَمَّا دَخَلُوا مِنْ حَيْثُ أَمَرَهُمْ أَبُوهُم مَّا كَانَ يُغْنِي عَنْهُم مِّنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ إِلَّا حَاجَةً فِي نَفْسِ يَعْقُوبَ قَضَاهَا ۚ وَإِنَّهُ لَذُو عِلْمٍ لِّمَا عَلَّمْنَاهُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٦٨﴾
68. Na walipoingia kwa namna alivyowaamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Allaah isipokuwa haja iliyokuwa katika nafsi ya Ya’quwb aliyoitimiza. Na hakika yeye alikuwa mwenye elimu Tuliyomfunza, lakini watu wengi hawajui.


وَلَمَّا دَخَلُوا عَلَىٰ يُوسُفَ آوَىٰ إِلَيْهِ أَخَاهُ ۖ قَالَ إِنِّي أَنَا أَخُوكَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٦٩﴾
69. Na walipoingia kwa Yuwsuf, alimuweka ndugu yake kwake (akamkumbatia). Akasema: “Hakika mimi ni kaka yako, basi usisikitike kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.”


فَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ جَعَلَ السِّقَايَةَ فِي رَحْلِ أَخِيهِ ثُمَّ أَذَّنَ مُؤَذِّنٌ أَيَّتُهَا الْعِيرُ إِنَّكُمْ لَسَارِقُونَ﴿٧٠﴾
70. Na alipowatayarishia mahitaji yao (ya chakula), alikitia kikopo cha kunywea katika mzigo wa ndugu yake, kisha mwenye kunadi akanadi: “Enyi wasafiri! Hakika nyinyi ni wezi!”


قَالُوا وَأَقْبَلُوا عَلَيْهِم مَّاذَا تَفْقِدُونَ ﴿٧١﴾
71. Wakasema na huku wamewakabili: “Mmepoteza nini?”


قَالُوا نَفْقِدُ صُوَاعَ الْمَلِكِ وَلِمَن جَاءَ بِهِ حِمْلُ بَعِيرٍ وَأَنَا بِهِ زَعِيمٌ ﴿٧٢﴾
72. Wakasema: “Tumepoteza pishi ya mfalme. Na atakayekuja nayo atapewa shehena ya ngamia;” (na mwenye kunadi akasema): “Nami kwa hayo ni mdhamini.”


قَالُوا تَاللَّـهِ لَقَدْ عَلِمْتُم مَّا جِئْنَا لِنُفْسِدَ فِي الْأَرْضِ وَمَا كُنَّا سَارِقِينَ ﴿٧٣﴾
73.  Wakasema: “Ta-Allaahi (tunaapa kwa Jina la Allaah) mmekwishajua (kwamba) hatukuja kufanya ufisadi katika ardhi, na hatukuwa wezi.”



قَالُوا فَمَا جَزَاؤُهُ إِن كُنتُمْ كَاذِبِينَ ﴿٧٤﴾
74. Wakasema: “Basi nini jazaa yake, mkiwa ni waongo?” 


قَالُوا جَزَاؤُهُ مَن وُجِدَ فِي رَحْلِهِ فَهُوَ جَزَاؤُهُ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ ﴿٧٥﴾
75. Wakasema: “Jazaa yake ni (kuwa) yule ambaye itapatikana (pishi ya mfalme) kwenye mzigo wake; basi yeye ndiye jazaa yake. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.”


فَبَدَأَ بِأَوْعِيَتِهِمْ قَبْلَ وِعَاءِ أَخِيهِ ثُمَّ اسْتَخْرَجَهَا مِن وِعَاءِ أَخِيهِ ۚ كَذَٰلِكَ كِدْنَا لِيُوسُفَ ۖ مَا كَانَ لِيَأْخُذَ أَخَاهُ فِي دِينِ الْمَلِكِ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ نَرْفَعُ دَرَجَاتٍ مَّن نَّشَاءُ ۗ وَفَوْقَ كُلِّ ذِي عِلْمٍ عَلِيمٌ ﴿٧٦﴾
76. Basi (Yuwsuf) alianza (kutafuta) katika mizigo yao kabla ya mzigo wa ndugu yake. Kisha akaitoa (pishi) kutoka mzigo wa ndugu yake. Hivyo ndivyo Tulivyompangia Yuwsuf. Hakuweza kumchukua ndugu yake (kumzuia) katika sheria ya mfalme isipokuwa Atake Allaah. Tunampandisha vyeo Tumtakaye. Na juu ya kila mwenye elimu yuko mwenye elimu (zaidi).



قَالُوا إِن يَسْرِقْ فَقَدْ سَرَقَ أَخٌ لَّهُ مِن قَبْلُ ۚ فَأَسَرَّهَا يُوسُفُ فِي نَفْسِهِ وَلَمْ يُبْدِهَا لَهُمْ ۚ قَالَ أَنتُمْ شَرٌّ مَّكَانًا ۖ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا تَصِفُونَ ﴿٧٧﴾
77. Wakasema: “Ikiwa ameiba, basi amekwishaiba kaka yake kabla!” Yuwsuf aliyaweka siri katika nafsi yake na wala hakuwadhihirishia. Akasema: “Nyinyi mna hali mbaya; na Allaah Anajua zaidi yale mnayoyaelezea.”


قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ إِنَّ لَهُ أَبًا شَيْخًا كَبِيرًا فَخُذْ أَحَدَنَا مَكَانَهُ ۖ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٧٨﴾
78. Wakasema: “Ee al-‘Aziyz! Hakika yeye ana baba mkongwe, basi chukua mmoja wetu mahali pake. Hakika sisi tunakuona ni miongoni mwa wafanyao ihsaan.”


قَالَ مَعَاذَ اللَّـهِ أَن نَّأْخُذَ إِلَّا مَن وَجَدْنَا مَتَاعَنَا عِندَهُ إِنَّا إِذًا لَّظَالِمُونَ﴿٧٩﴾
79. Akasema: “Tunajikinga kwa Allaah kumchukua isipokuwa yule tuliyekuta vifaa vyetu kwake, (tukimchukua mwengine) basi hapo sisi bila shaka tutakuwa madhalimu.”



فَلَمَّا اسْتَيْأَسُوا مِنْهُ خَلَصُوا نَجِيًّا ۖ قَالَ كَبِيرُهُمْ أَلَمْ تَعْلَمُوا أَنَّ أَبَاكُمْ قَدْ أَخَذَ عَلَيْكُم مَّوْثِقًا مِّنَ اللَّـهِ وَمِن قَبْلُ مَا فَرَّطتُمْ فِي يُوسُفَ ۖ فَلَنْ أَبْرَحَ الْأَرْضَ حَتَّىٰ يَأْذَنَ لِي أَبِي أَوْ يَحْكُمَ اللَّـهُ لِي ۖ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ ﴿٨٠﴾
80. Basi walipokata tamaa; wakajitenga kando kushauriana kisiri.  Mkubwa wao akasema: “Je, hamjui kwamba baba yenu amekwishachukua kwenu ahadi kutoka kwa Allaah, na kabla (hapo) yale mlokusuru kuhusu Yuwsuf? Basi sitaondoka ardhi hii mpaka anipe idhini baba yangu, au Allaah Anihukumie. Naye ni Mbora wa wenye kuhukumu.”


ارْجِعُوا إِلَىٰ أَبِيكُمْ فَقُولُوا يَا أَبَانَا إِنَّ ابْنَكَ سَرَقَ وَمَا شَهِدْنَا إِلَّا بِمَا عَلِمْنَا وَمَا كُنَّا لِلْغَيْبِ حَافِظِينَ ﴿٨١﴾
81. “Rejeeni kwa baba yenu, na semeni: “Ee baba yetu! Hakika mwanao ameiba; nasi hatushuhudii isipokuwa kwa yale tunayoyajua; na hatukuwa wenye kuhifadhi (mambo ya) ghayb.”


وَاسْأَلِ الْقَرْيَةَ الَّتِي كُنَّا فِيهَا وَالْعِيرَ الَّتِي أَقْبَلْنَا فِيهَا ۖ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٨٢﴾
82. “Na uliza (watu wa) mji ambao tulikuwa humo, na msafara ambao tumekuja nao, na hakika sisi ni wakweli.”


قَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنفُسُكُمْ أَمْرًا ۖ فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ عَسَى اللَّـهُ أَن يَأْتِيَنِي بِهِمْ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٨٣﴾
83. (Baba yao) Akasema: “Bali nafsi zenu zimekushawishini (kufanya) jambo. Basi subira ni njema. ’Asaa Allaah Aniletee wote (wawili) pamoja. Hakika Yeye Ndiye Al-‘Aliymul-Hakiym (Mjuzi wa yote - Mwenye hikmah wa yote).”


وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ ﴿٨٤﴾
84. Na akajitenga nao, na akasema: “Ee majonzi yangu juu ya Yuwsuf.” Na macho yake yakageuka meupe kutokana na huzuni, naye huku akiwa amezuia ghaidhi (na huzuni).


قَالُوا تَاللَّـهِ تَفْتَأُ تَذْكُرُ يُوسُفَ حَتَّىٰ تَكُونَ حَرَضًا أَوْ تَكُونَ مِنَ الْهَالِكِينَ ﴿٨٥﴾
85. Wakasema: “Ta-Allaahi (Tunaapa kwa Jina la Allaah) hutoacha kumkumbuka Yuwsuf mpaka uwe mgonjwa mahtuti, au uwe miongoni mwa wanaohiliki.”


قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٨٦﴾
86. Akasema: “Hakika mimi nashitakia dhiki (ya majonzi) yangu na huzuni zangu kwa Allaah. Na najuwa kutoka kwa Allaah yale msiyoyajua.”


يَا بَنِيَّ اذْهَبُوا فَتَحَسَّسُوا مِن يُوسُفَ وَأَخِيهِ وَلَا تَيْأَسُوا مِن رَّوْحِ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾
87. “Ee wanangu! Nendeni mkamtafute Yuwsuf na ndugu yake; na wala msikate tamaa na faraja ya Allaah; hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri.”


فَلَمَّا دَخَلُوا عَلَيْهِ قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ مَسَّنَا وَأَهْلَنَا الضُّرُّ وَجِئْنَا بِبِضَاعَةٍ مُّزْجَاةٍ فَأَوْفِ لَنَا الْكَيْلَ وَتَصَدَّقْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يَجْزِي الْمُتَصَدِّقِينَ ﴿٨٨﴾
88. (Wakarudi kwa Yuwsuf). Walipoingia kwake wakasema: “Ee al-‘Aziyz!  Dhara imetugusa pamoja na ahli zetu, na tumekuja na bidhaa duni, basi tutimizie kipimo, na tupe swadaqah. Hakika Allaah Anawalipa watoao swadaqah.”


قَالَ هَلْ عَلِمْتُم مَّا فَعَلْتُم بِيُوسُفَ وَأَخِيهِ إِذْ أَنتُمْ جَاهِلُونَ ﴿٨٩﴾
89. Akasema: “Je, mmejua yale mliyomfanyia Yuwsuf na ndugu yake mlipokuwa majahili?”


قَالُوا أَإِنَّكَ لَأَنتَ يُوسُفُ ۖ قَالَ أَنَا يُوسُفُ وَهَـٰذَا أَخِي ۖ قَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا ۖ إِنَّهُ مَن يَتَّقِ وَيَصْبِرْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٩٠﴾
90.  Wakasema: “Je, kwani wewe ndio Yuwsuf?” Akasema: “Mimi ni Yuwsuf, na huyu ni ndugu yangu. Kwa yakini Allaah Ametufanyia ihsaan. Hakika mwenye kuwa na taqwa na akasubiri, basi hakika Allaah Hapotezi ujira wa watendao ihsaan.”


قَالُوا تَاللَّـهِ لَقَدْ آثَرَكَ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَإِن كُنَّا لَخَاطِئِينَ ﴿٩١﴾
91. Wakasema: “Ta-Allaahi (Tunaapa kwa Jina la Allaah) Kwa yakini Allaah Amekufadhilisha juu yetu, nasi bila shaka tulikuwa wakosa.”


قَالَ لَا تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ ۖ يَغْفِرُ اللَّـهُ لَكُمْ ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٩٢﴾
92. Akasema: “Hakuna lawama juu yenu leo. Allaah Atakughufurieni. Naye ni Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”


اذْهَبُوا بِقَمِيصِي هَـٰذَا فَأَلْقُوهُ عَلَىٰ وَجْهِ أَبِي يَأْتِ بَصِيرًا وَأْتُونِي بِأَهْلِكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٣﴾
93. “Nendeni na kanzu yangu hii, na litupeni kwenye uso wa baba yangu, atakuwa mwenye kuona; na nijieni na ahli zenu nyote pamoja.”

وَلَمَّا فَصَلَتِ الْعِيرُ قَالَ أَبُوهُمْ إِنِّي لَأَجِدُ رِيحَ يُوسُفَ ۖ لَوْلَا أَن تُفَنِّدُونِ ﴿٩٤﴾
94. Na ulipoondoka msafara (kutoka Misr) baba yao (akiwa Shaam) alisema: “Hakika mimi nasikia harufu ya Yuwsuf, ikiwa hamkunidhania nachanganyikiwa akili (kutokana na uzee).”


قَالُوا تَاللَّـهِ إِنَّكَ لَفِي ضَلَالِكَ الْقَدِيمِ ﴿٩٥﴾
95. Wakasema: “Ta-Allaahi (Tunaapa kwa Jina la Allaah) Hakika wewe umo katika upotofu wako wa zamani (wa kumpenda Yuwsuf mno).”


فَلَمَّا أَن جَاءَ الْبَشِيرُ أَلْقَاهُ عَلَىٰ وَجْهِهِ فَارْتَدَّ بَصِيرًا ۖ قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ إِنِّي أَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٩٦﴾
96. Basi alipokuja mtoaji bishara akaiweka (kanzu) juu ya uso wake (tahamaki) alirudi kuona. Akasema: “Je, sikukuambieni (kwamba) hakika mimi najua kutoka kwa Allaah yale msiyoyajua?”


قَالُوا يَا أَبَانَا اسْتَغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا إِنَّا كُنَّا خَاطِئِينَ ﴿٩٧﴾
97. Wakasema: “Ee baba yetu! Tuombee maghfirah madhambi yetu; hakika sisi tulikuwa wakosa.”


قَالَ سَوْفَ أَسْتَغْفِرُ لَكُمْ رَبِّي ۖ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٩٨﴾
98. Akasema: “Nitakuombeeni maghfirah kwa Rabb (Mola) wangu. Hakika Yeye Ndiye Al-Ghafuwrur-Rahiym (Mwingi wa kughufuria -  Mwenye kurehemu).”


فَلَمَّا دَخَلُوا عَلَىٰ يُوسُفَ آوَىٰ إِلَيْهِ أَبَوَيْهِ وَقَالَ ادْخُلُوا مِصْرَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ ﴿٩٩﴾
99.  Na walipoingia kwa Yuwsuf akawaweka (aliwakumbatia) wazazi wake kwake. Na akasema: “Ingieni Misri In Shaa Allaah mkiwa mmo katika amani.”


وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى الْعَرْشِ وَخَرُّوا لَهُ سُجَّدًا ۖ وَقَالَ يَا أَبَتِ هَـٰذَا تَأْوِيلُ رُؤْيَايَ مِن قَبْلُ قَدْ جَعَلَهَا رَبِّي حَقًّا ۖ وَقَدْ أَحْسَنَ بِي إِذْ أَخْرَجَنِي مِنَ السِّجْنِ وَجَاءَ بِكُم مِّنَ الْبَدْوِ مِن بَعْدِ أَن نَّزَغَ الشَّيْطَانُ بَيْنِي وَبَيْنَ إِخْوَتِي ۚ إِنَّ رَبِّي لَطِيفٌ لِّمَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿١٠٠﴾
100. Aliwainua wazazi wake wawili juu ya kiti cha ufalme; wakaporomoka wote kumsujudia. Na (Yuwsuf) akasema: “Ee baba yangu! Hii ni tafsiri ya (ile) ndoto yangu hapo kabla, Rabb (Mola) wangu Ameijaalia kweli. Na Amenifanyia ihsaan Aliponitoa kutoka jela, na Akakuleteni kutoka jangwani baada ya shaytwaan kuchochea baina yangu na baina ya kaka zangu. Hakika Rabb wangu ni Latwiyf (Latifu, Anadabiri mambo kwa uficho) kwa lile Alitakalo. Hakika Yeye Ndiye Al-’Aliymul-Hakiym (Mjuzi wa yote - Mwenye hikmah wa yote).”


رَبِّ قَدْ آتَيْتَنِي مِنَ الْمُلْكِ وَعَلَّمْتَنِي مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ ۚ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَنتَ وَلِيِّي فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿١٠١﴾
101. “Rabb (Mola) wangu kwa yakini Umenipa katika utawala, na Umenifunza katika tafsiri za al-ahaadiyth (matukio). Muanzilishi wa mbingu na ardhi. Wewe ni Waliyyi (Mtawalia, Mlinzi) wangu duniani na Aakhirah. Nifishe (hali ya kuwa) Muislamu na Unikutanishe na Swalihina.”


ذَٰلِكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ ۖ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ أَجْمَعُوا أَمْرَهُمْ وَهُمْ يَمْكُرُونَ ﴿١٠٢﴾
102. Hizo ni baadhi ya habari za ghayb Tunakufunulia Wahy kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na hukuwa pamoja nao (pale) walipokubaliana jambo lao, nao wakifanya mbinu.


وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾
103. Na wengi wa watu hawatoamini japokuwa utatilia hima.



وَمَا تَسْأَلُهُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٤﴾
104. Na huwaombi kwa haya ujira wowote (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Hii (Qur-aan) si chochote isipokuwa ni ukumbusho kwa walimwengu.


وَكَأَيِّن مِّنْ آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ ﴿١٠٥﴾
105. Na Aayah (ishara, dalili) ngapi (za kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah) katika mbingu na ardhi wanazipitia na huku wao wanazipuuza.


وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ ﴿١٠٦﴾
106. Na wengi kati yao hawamwamini Allaah isipokuwa wao ni wenye kufanya shirki


أَفَأَمِنُوا أَن تَأْتِيَهُمْ غَاشِيَةٌ مِّنْ عَذَابِ اللَّـهِ أَوْ تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١٠٧﴾
107. Je, wanaaminisha kuwa haitowafikia adhabu ya Allaah ya kuwagubika au itawafikia Saa (Qiyaamah) kwa ghafla nao hawahisi?


قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٨﴾
108. Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya baswiyrah (nuru ya elimu, ujuzi, umaizi) mimi na anayenifuata. Na Subhaana-Allaah (Utakasifu ni wa Allaah), nami si miongoni mwa washirikina.”


وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِم مِّنْ أَهْلِ الْقُرَىٰ ۗ أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۗ وَلَدَارُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ اتَّقَوْا ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿١٠٩﴾
109. Na Hatukutuma kabla yako (Rasuli) isipokuwa wanaume Tuliowafunulia Wahy katika watu wa miji; Je, basi hawatembei katika ardhi wakatazama vipi ilikuwa hatima ya wale kabla yao? Na bila shaka nyumba ya Aakhirah ni bora kwa wale waliokuwa na taqwa. Je, basi hawatii akilini?


حَتَّىٰ إِذَا اسْتَيْأَسَ الرُّسُلُ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ قَدْ كُذِبُوا جَاءَهُمْ نَصْرُنَا فَنُجِّيَ مَن نَّشَاءُ ۖ وَلَا يُرَدُّ بَأْسُنَا عَنِ الْقَوْمِ الْمُجْرِمِينَ ﴿١١٠﴾
110. (Wakaendelea kulingania Dini) Mpaka walipokata tamaa Rasuli na wakadhani kwamba wao kwa yakini wamekadhibishwa (na watu wao) ikawajia nusra Yetu; na wakaokolewa Tuwatakao. Na wala hairudishwi nyuma adhabu Yetu kwa watu wahalifu.


لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَىٰ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١١١﴾
111. Kwa yakini katika visa vyao kuna zingatio (na mawaidha) kwa wenye akili. Haikuwa (Qur-aan) hadiyth inayozushwa, lakini ni ya kusadikisha (vitabu vilivyoitangulia) vya kabla yake na tafsili ya kila kitu, na ni Mwongozo na Rahmah kwa watu wanaoamini.


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com