Abu Ammaar
Elimu yetu ya dini inazidi kuenea na
kusambaa. Maendeleo ya teknolojia yamerahisisha kwa kiasi kikubwa upatikanaji
wa elimu miongoni mwa waislamu.Qur’aan kwa mfano sasa inapatikana katika mp3,
ipod, mobile phones, computers na kadhalika. Unaweza sasa ukajifunza Qur’aan
uko nyumbani ukitumia computer.Vitabu takriban vingi vya kizamani na vya
karibuni vinapatikana kwa urahisi. Televisheni na mitandao nayo haiko nyuma
katika jitihada hizi za kuielimisha dini yetu. Tuna mitandao na yenye
kutegemewa kwa lugha yetu ya Kiswahili. Wahadhiri wetu nao wanatoa mada
mbalimbali zenye manufaa kwetu nayo kuhifadhiwa katika njia za cd, mp3 na
kaseti na kuwezesha wengine kufaidika pia.Vitabu katika lugha yetu pia navyo
viko vingi na vinazidi kutolewa. Magazeti ya kiislamu pia kwa upande mwengine
yanaendeleza kazi hii ya kuelimisha.
Yote haya yanafanyika kwa jitihada
kubwa na ndugu zetu kutuwekea elimu hii kwa ajili ya manufaa yetu na
tuifahamu dini yetu wakiwa tayari wameshatekeleza wajibu wao na kututaka sisi
tutekeleze wajibu wetu katika kujifunza na kuelimika.Wajibu ambao ni fardhi
kwa kila muislamu.
Kama siku moja Khalifa ‘Umar ibnul
Abdul ‘Aziz ambae anahesabika kama ni khalifa wa tano katika makhalifa
raashiduun - walioongoka, aliwahi kumuandikia mmoja wa ma amiri wake Abubakar
ibnu Hazm na kumwambia:
انظر ما كان من حديث رسول
الله صلى الله عليه وسلم فاكتبه، فإني خفت دروس العلم وذهاب العلماء، ولا تقبل
إلا حديث النبي صلى الله عليه وسلم، ولتفشوا العلم،
ولتجلسوا حتى يعلم من لا يعلم، فإن العلم لا يهلك
حتى يكون سرا.
“Angalia katika hadithi za Mtume
na uziandike. Kwani ninachelea elimu kufichwa na maulamaa kutoweka. Na wala
usikubali kitu chengine isipokuwa hadithi ya Mtume na idhihirisheni elimu na
mkae kusomesha mpaka ajue na afahamu yule asiejua kwani elimu haipotei mpaka
ikiwa imefichwa”.
Angalia sahihi Bukhari - vipi elimu itakavyopotea
Licha ya kuwepo utajiri wote huu wa
elimu lakini wenye kuitafuta na kunufaika nayo ni wachache sana miongoni
mwetu. Ni waislamu wachache walio tayari kujitolea muda na wakati wao kusoma
dini yao ambayo hawana maarifa nayo. Ni waislamu wachache wanaothamini
michango hii inayotolewa na waislamu na kufanyia kazi kisawasawa katika
kuhakikisha wanaijua na kuifahamu vyema dini yao.
Kinachosikitisha na kuhuzunisha ni
kwa waislamu kukosa msukumo na muelekeo wa kujipa hima ya kuitafuta elimu hii
ya dini.Kwa sababu elimu ipo lakini wenye kuitafuta wameadimika, wanaotaka
kusoma hatunao, ila tuna waislamu ambao ndio wengi waliokuwa radhi kutekeleza
wajibu wao bila ya kuja au kuwa na maarifa machache tu.
Bila ya kuwa na elimu hatuwezi kujua
mfumo wa matendo ya ibada kama sala, tohara, Hajj na matendo yake na
Zakah na utekelezaji wake na kadhalika. Haya ni mambo ya kimsingi ambayo kila
muislamu anapaswa kuyafahamu vilivyo na yanahitaji maarifa na upeo ili kuweza
kuyatekeleza jinsi inavyotakikana.
Bila ya kuwa na elimu hatutokuwa na
uhakika kwamba amali tunazozitenda tumepata ujira au kutopata chochote,
tumetenda thawabu au tumefanya dhambi ikiwa ni za kujificha kama hasada,
kiburi,chuki, choyo na kadhalika. Au ni za dhahiri kama kusengenya, kutazama
yaliyoharamishwa, zinaa na kadhalika.
Bila ya kuwa na elimu hatuweza
kuifahamu itikadi yetu sahihi ambayo ni wajibu kwa kila muislamu kuifahamu
vyema aqidah yake na kuweza kumjua Allah Subhaanahu Wata’ala, kumpwekesha
(Tauhiyd) na kujua sifa na majina yake na kuyatekeleza ipasavyo.
Bila ya kuwa na elimu hatuwezi
kuzitambua tofauti zinazojitokeza katika dini yetu na kuweza kuelewa kwa
ushuhuda wa kidalili na pia kuweza kujiepusha na mambo mengi ambayo
yamezushwa katika dini yetu nasi tukijikuta kuyafuata tu bila ya kuyajua undani
wake.
Ushahidi mdogo kuonesha kwamba
kiwango cha elimu ya dini miongoni mwa waislamu ni duni tuangalie masuala na
majibu na fatawa na aina ya masuala ambayo ni mambo ya kimsingi “basic”
yanayoulizwa ambayo kisheria kila muislamu anapaswa kuyafahamu. Hiki nii
kielelezo tosha kwamba bado jitihada haijafanyika kwa upande wa wenye
kuitafuta elimu.
Hali hii ni kinyume kabisa na enzi za
Mtume, masahaba na mataabiina pamoja na watangu wema. Kipindi chao
hawakubahatika na kuwa na nyenzo kama tulizobahatika kuwa nazo lakini hamu
yao na jitihada waliyoionesha katika kuitafuta elimu ni ushahidi tosha
kuonesha jinsi walivyoitilia maanani elimu ya dini yetu ya kiislamu.
Kwa mfano enzi za uhai wa Mtume Salla
Allahu ‘Alayhi Wasallam, mmoja wa masahaba Abdullah Ibnu ‘Abbass Allah,
awawie radhi yeye na baba yake, hakuwahi kukosa vikao vya Mtume Salla Allahu
‘Alayhi Wasallam na kuhifadhi yale yote atakayoyasema na baada ya kufariki
kwake. Alijihimu kwenda kwa masahaba wengi kujifunza yale waliyofundishwa na
Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Akisikia tu! Kuna mtu anajua hadithi
ambayo yeye haijui atakwenda kwake haraka na kuiandika. Ataihakiki na
kuilinganisha na hadithi nyengine na aliwahi kwenda kwa masahaba karibu
thelathini kuhakiki jambo moja tu
Pia tunamuona mmoja wa Masahaba
alitoka Madina kwenda Damascus Syria kuithibitisha hadithi moja tu ya Mtume
Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam aliyoisikia na mtu wa kuthibitisha hayo alikuwa
ni sahaba Abu Dardaai, Allah amuwie radhi, ambae kipindi hicho
alikuwepo Syria.
Elimu yetu ya dini imepita katika
nyanja mbali mbali tokea kwa Mtume Salla Allahu Alayhi Wasallam hadi
kutufikia. Katika mtiririko huu kuna elimu ambayo imehifadhiwa kupitia kizazi
baada ya kizazi. Pia kuna elimu ambayo ndani yake imepitia tamaduni tofauti
na kuingizwa katika dini kama ni sehemu moja wapo ya elimu yetu. Pia kuna
watu ambao kwa maksudi wamejaribu kuupotosha umma wetu kwa kutumia nyanja hii
hii ya elimu kwa kuingiza yasiyokuwemo au kuongeza kwa yaliyopo kwa lengo la
kupotosha na si kuelimisha. Na pia kutia mashaka kwa yaliyopo kwamba hayana
ukweli na kadhalika.
Ndiyo maana kwa ulimwengu wetu wa leo
na hali hii tuliyonayo, kuisoma elimu ya dini itahitaji mtazamo mwengine na
mfumo tofauti na mifumo iliyokuwepo katika siku za zamani.Kwani si rahisi
kuweza kupambanua elimu iliyo sahihi na elimu isiyokuwa sahihi bila ya sisi
wenyewe kuanza kujifunza kwa mfumo wa kukabiliana na hali halisi
inayotukabili. Mazingira tayari yamebadilika na mfumo wa elimu pia itabidi
ubadilike. Ule wakati wa kupokea tu elimu bila ya kuwa na uhakika na
unachoelimishwa tayari umepita na tupo katika zama za kuisoma dini yetu
kiutaalamu na upeo tukizingatia zaidi vigezo vinavyotumika.
Imepokewa katika hadithi sahihi
kwamba miongoni mwa alama za siku ya kiama ni elimu kusomeshwa na watu
wasiokuwa na elimu. Na matokeo yake ni kupotoka kwa waliofundisha na
kupotoshwa kwa wanaofundishwa kwa mujibu wa hadithi ya Mtume Salla Allahu
‘Alayhi Wasallam:
: (إن الله لا يقبض العلم انتزاعا ينتزعه من
العباد، ولكن يقبض العلم بقبض العلماء، حتى إذا لم يبق عالما، اتخذ الناس رؤوسا
جهالا، فسئلوا، فأفتوا بغير علم، فضلوا وأضلوا).
“Hakika Allah haiondoi elimu kwa
kuindosha kutoka(vifuani) kwa watu bali huiondosha kwa kuwaondoa Maulamaa
mpaka hapatobaki msomi miongoni mwao na watu kuwachagua majahili kuwa ni
viongozi ambao watatoa fatwa bila ya kuwa na elimu na watapotea(wao wenyewe)
na kuwapoteza
watu.”
Bukhari
Haya yalitamkwa na Mtume Salla Allahu
‘Alayhi Wasallam kabla ya kufariki kwake lakini hali hii tunaishuhudia
wenyewe katika jamii zetu jinsi dini yetu inavyochezewa na watu ambao
wanawapoteza wenzi wao.Nao si miongoni mwa makafiri waliodhihirisha kufru yao
bali ni miongoni mwa waislamu ambao wamejitolea katika kuwapoteza waislamu
wenzi wao.
Elimu ya dini ya kiislamu inazidi
kusahauliwa kwa kasi ya kutisha licha ya kuwepo utajiri wote wa elimu
tulioutaja hapo juu na hasa kwa sisi ambao tuko nchi ambazo hazina chembe
chembe za kiislamu katika mfumo wa maisha tunaathirika sana kwa kukosa hata
yale mafundisho ya kivitendo ambayo hutokea katika jamii za kiislamu.
Lau
kama elimu ya ilipewa umuhimu kama ule aliousia Mtume Muhammad Salla Allahu
‘Alayhi Wasallam kama ilivyoelezwa na Abdullah Ibn Masoud, Allah amuwie
radhi.na kupokewa na Hakim katika hadithi inayofuata labda matatizo haya
yasingelikuwepo:
تعلموا القرآن و علموه
الناس و تعلمو الفرائض و علموه الناس فإني امرؤ مقبوض و أن العلم سيقبض و تظهر
الفتن حتى يختلف الإثنان في الفريضة لا يجدان من يقضي بها .
“Jifunzeni Quraan na muwafundishe
watu, na jifunzeni elimu ya Mirathi na muwafundishe watu, kwani mimi na mja
ambae nitakufa na elimu itapotea na kudhihiri fitna(majaribu) na (kufikia)
kuwatia shaka watu wawili na kutofautiana katika mirathi na wala wasipate mtu
wa kuwapatia hukumu.”
Uislamu ni dini ya elimu na aya ya
kwanza kabisa kuteremshwa katika Qur’aan inagusia kusoma ambao ndio ufunguo
wa elimu yoyote.
Wengi wetu tunalichukulia jambo la
kusoma elimu ya dini kama si lazima bali ni jambo la ziada lakini elimu
nyengine na mambo mengine huwa tunayapa kipaumbele na umuhimu kuliko
tunavyoipa umuhimu elimu yetu ya dini. Tumsikilize Mtume Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam anavyotukumbushia nini cha muhimu hasa katika elimu kama ilivyosimuliwa
na Abdullah ibn Amr bin Al Aas (Allah amuwie radhi) na kupokewa na Dar qutni
inavyobainisha:
أن رسول الله صلى الله
عليه وسلم قال : العلم ثلاثة وماسوى ذلك فهو فضل : آية محكمة ، أو سنة قائمة أو
ريضة عادلة ،
Hakika
Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema:
“Elimu ni tatu na zisizokuwa hizo ni ziada, (Elimu ya) aya (za
Quraan) zinazobainisha hukumu, au sunna (za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam) zilizosimama, au Mirathi adilifu.”
Allah Subhaanahu Wataala
anawashuhudisha wenye kuitafuta elimu na Maulamaa kwamba ni watu wenye
tauhiyd na wenye kumfahamu vyema Allah. Aal Imraan/18
شَهِدَ اللّهُ أَنَّهُ لاَ إِلَـهَ إِلاَّ
هُوَ وَالْمَلاَئِكَةُ وَأُوْلُواْ الْعِلْمِ قَآئِمَاً بِالْقِسْطِ لاَ إِلَـهَ
إِلاَّ هُوَ الْعَزِيزُ
الْحَكِيم
Allah, na Malaika, na wenye ilimu,
wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha
uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima
Moja katika malengo ya kujifunza
elimu ya dini ni kutukurubisha na kuwa karibu na muumba - Allah Subhaanahu
Wata’ala na kutaka radhi zake. Hujifunza tuweze kujua na kuelewa jinsi ya
kumuabudu inavyotakikana na kuweza kumtakasia ibada zake kwa ikhlasi
Pia kujifunza elimu ni ibada. Hivyo
ni wajibu kwa mwenye kujifunza kuitakasa ibada hii kama zilivyo ibada
nyenginezo. Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amemuweka daraja moja mwenye
kutafuta elimu na mwenye kupigana jihadi kwa njia ya Allah Subhaanahu
Wata’ala.
من خرج في طلب العلم فهو في سبيل الله حتى
يرجع))أخرجه التِّرْمِذِي وقال : حديث حسن
“Mwenye kutoka kwa ajili ya kutafuta
elimu huwa katika njia ya Allah mpaka atakaporudi.”
Attirmidhiy na amesema ni hadith hasan
Kujifunza elimu yetu ya dini si jambo
lililowekewa muda maalum. Ni kazi inayoendelea mpaka kuelekea kaburini bado
tuna mengi ya kujifunza katika dini yetu. Umri mkubwa pia si kisingizio wala
kigezo cha kukataa kujifunza. Tukiacha na kutojifunza dhimma itabaki kwetu na
kuwa na viongozi watakaotupoteza, Maustaadh watakaotoa fatwa pasipokuwa na
ujuzi wa kufanya hivyo na hatimaye umma wa kiislamu kuangamia na kula hasara.
Ni ibada muhimu kwa kila mmoja wetu
kuipigania kwani hata husuda, ingawa ni haramu kisheria, ni jambo
lililoruhusiwa kwa hili kama hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam
inavyobainisha.
: (لا حسد إلا في اثنتين: رجل آتاه الله مالا
فسلط على هلكته في الحق، ورجل آتاه الله الحكمة فهو يقضي بها
ويعلمها
“Hakuna husuda isipokuwa katika mambo
mawili: Mtu ambae Allah amempa utajiri kisha akautumia katika njia ya haki na
mtu ambae Allah amempa hekima (elimu ya dini) na akawa akitoa hukumu(sahihi)
na kuifundisha kwa wengine.”
Bukhari
Mwisho na tuzidi kuikumbuka hadithi
ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akituhimiza katika kujifunza elimu ya
dini pale aliposema kama ilivyopokewa na Bukhari:
يطلب به علما سهل الله له طريقا إلى الجنة ومن سلك طريقا …
“…Na atakaenyoosha njia kutafuta
ndani yake elimu basi Allah humuwepesishia njia ya kwenda peponi.”
Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’ala
aturudishie tena hamu ya kuisoma na kuifahamu dini yetu. Pia atuongoze katika
njia iliyonyooka.Tumuombe Allah atupe uwezo na muda wa kuweza kurudi kwake
kwa kujifunza yale yatakayokuwa na kheri kwetu katika dini, dunia na akhera
yetu. Amin Amin
Wabillahi Ttawfiyq.
|
Umuhimu Wa Kujifunza Elimu Ya Dini
Subscribe to:
Posts (Atom)