Tujifunze Kutoka kwa Waliofahamu Kujifunza


Hiki ni kisa kinachosimuliwa na Shaqiyq Al Bakhliy ambae siku moja alimwambia Haatim, mwanafunzi wake, kama kilivyotajwa katika kitabu cha Minhaaj Qaasidiin cha Ibnu Qudaamah/25 kwamba:

“Tumekuwa pamoja kwa muda sasa . Umejifunza nini kutoka kwangu?
Haatim akasema: “mambo manane”.

La Kwanza:

Hakika mimi kila nikiwaangalia viumbe nnamuona kila kiumbe ana mpenzi/kipenzi. Hata hivyo afikapo kaburini mpenzi hufarikiana nae. Hivyo nikayajaalia matendo yangu mema ndio kipenzi changu ili yawe nami ndani ya kaburi.

La Pili

Nikiitazama kauli ya Allah  Subhaanahu Wata'ala katika Annazia’at/40

                                                      وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَى

Na akaikataza nafsi na matamanio
Basi nikamua kupigana jihadi na nafsi yangu ili itulie katika kumtii Allah Subhaanahu Wata’ala.

La Tatu

Nimeona kila mwenye kitu chake cha thamani hukitunza na kukihifadhi vizuri. Nikaiangalia kauli ya Allah Subhaanahu Wata’ala katika Annahl/96

                                مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ وَمَا عِندَ اللّهِ بَاقٍ   
Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Allah ndivyo vitakavyobakia.
Hivyo kila nikijaaliwa kupata kitu chochote cha thamani hukielekeza kwake Allah subhaanahu Wata’ala ili kibakie huko.

La Nne

Nimeona watu hufungamana zaidi na mali, nasaba na sharafu nikaiangalia kauli ya Allah Subhaanahu Wata’ala Al Hujuraat/13

                                    إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ
Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allah ni huyo aliye mchamungu zaidi katika nyinyi

Hivyo nikajifunga zaidi na taqwa – uchamungu ili niwe karimu kwake Allah Subhaanahu Wata’ala.

La Tano

Nimeona watu wanapenda husuda na kuhusudiana wao kwa wao. Nikaiangalia kauli ya Allah Subhaanahu Wata’ala Azzukhruf/32

                     نَحْنُ قَسَمْنَا بَيْنَهُم مَّعِيشَتَهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا    
Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani

Basi hapo hapo nikaacha kuhusudu.

La Sita

Nimeona watu wanafanyiana uadui wenyewe kwa wenyewe nikaangalia kauli ya Allah Subhaanahu Wata’ala  Faatir/6

                              إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا
Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui
Hivyo nikaacha kuwafanya watu kuwa maadui na kuwa na adui mmoja tu – shetani.

La Saba

Nimeona jinsi watu wanavyojidhalilisha katika kutafuta rizki Nikaiangalia kauli ya Allah Subhaanahu Wata’ala Huud/6

                            وَمَا مِن دَآبَّةٍ فِي الأَرْضِ إِلاَّ عَلَى اللّهِ رِزْقُهَا
Na hakuna  mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Allah.
Nikajishughulisha zaidi na yale yaliyokuwa wajibu kwangu kwake Allah  na nikaiacha mali yangu kwake

La Nane

Nimeona watu muda wao mwingi wanategemea biashara zao, viwanda vyao na afya ya miili yao hivyo mimi nikawacha yote hayo na kumtegemea Allah Subhaanahu Wata’ala pekee.

Wabillahi Attawfiyq