Faatimah bint Al Khattaab - Aliethibitisha ombi la Mtume Salla Allahu Alayhi Wasallam





Faatimah bint Al Khattaab - Aliethibitisha ombi la Mtume Salla Allahu Alayhi Wasallam

Historia ya kiislamu itamkumbuka Bi Faatimah kupitia kusilimu kwa ndugu yake ‘Umar Al Khattaab na hivyo ombi la Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kusilimu mmoja wa ‘Umar wawili lilitimia.
Historia yake inasimuliwa na mwenyewe ‘Umar anapokisimulia kisa  cha kusilimu kwake:
Nilitoka siku moja takriban baada ya siku tatu tokea kusilimu kwa Hamzah Ibn Abdul Muttalib na nikakutana na Nu’aim ibn Abdullah Al Makhzuumiy na nikamwambia:
“Umeiacha dini yako na kuingia dini ya Muhammad?”
Akasema: “Bali tayari ameshalifanya hilo ambaye ana haki kubwa juu yako!”
Nikasema: “Ni nani huyo?”
Akasema: “Dada yako Faatimah pamoja na mumewe”
Nikatoka kuelekea kwa dada yangu na nikakuta mlango umefungwa na nilisikia sauti. Ulipofunguliwa nikauliza:
 “Ni sauti gani niliyokuwa nikiisikia?”. Akasema Faatimah:
“Mimi sijaisikia”
Tukawa tunabishana mpaka nikamkamata kichwa chake kwa nguvu na kumpiga usoni. Nilifanya hayo bila ya kujijua kwa hasira mpaka nikaona damu. Nikamwachia na kusema:
“Nionesheni kitabu mlichokuwa mkikisoma!”
Akasema: “Hakika sisi tunakiogopa juu yako”
Nikasema: “Msiogope na nikaapa kwa miungu ya kisanamu kuwahakikishia”
Akasema: “Hakika hawakigusi isipokuwa walio tohara”
Nikaoga na kuanza kusoma:
طه  * مَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَى * إِلَّا تَذْكِرَةً لِّمَن يَخْشَى * تَنزِيلًا مِّمَّنْ خَلَقَ الْأَرْضَ وَالسَّمَاوَاتِ الْعُلَى
الرَّحْمَنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَى
T'aaha. Hatukukuteremshia Quraan ili upate mashaka. Bali ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea. Materemsho yatokayo kwa aliyeumba ardhi na mbingu zilizo juu. Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliyetawala juu ya Kiti cha Enzi.
Nikasema: “ni maneno mazuri na karimu”. Aliposikia Khabbaab Ibnul Arraat maneno haya alitoka alipojificha kwani alikuwa akiwasomesha Faatimah na mumewe Quraan. ‘Umar alipokuja na kwa khofu ikabidi ajifiche. Akasema Khabbaab:
 “Ewe ‘Umar! Nnatarajia kutoka kwa Allah kwamba ni wewe aliyekuchagua kwa ajili ya Da’awah ya Mtume wake. Kwani ni jana tu nilimsikia akisema:
 "اللهم أيِّد الإسلام بأبى الحكم بن هشام أو بعمر بن الخطاب" (وفى رواية: بأحد العُمَرَيْن) فاللهَ اللهَ يا عمر
 “Ewe mola upe nguvu uislamu kwa (kumsilimisha) Abul Hakam ibn Hishaam au ‘Umar ibnul Khattaab. Na katika riwaya ( ni kwa mmoja wa ‘Umar wawili). Allah Allah Ewe ‘Umar ( Fanya haraka twende kusilimu)
Nikasema: “Nipelekeni kwa Muhammad”
Nikapelekwa na Khabbaab mpaka nyumba ya Arqam ibn Abil Arqam na hapo nikatamka shahada mbele ya Mtume na Mtume Akaleta takbira masahaba wakafuatilia na kuonesha furaha yao.
Alikulia Faatimah katika nyumba ya baba yao yao Al Khattab ibn Nawfal Al Makhzuumiy na mama yao Khantamah bint Haashim Al Mughiyrah.
Faatimah alikuwa mwanamke Sahaba mwenye heshima kwani yeye na mumewe Said ibn Zayd ni miongoni mwa watu kumi waliobashiriwa pepo kwa kusilimu kwao hata kabla ya kuhamia Daawah ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wassallam katika nyumba ya Arqam. Na alikuwa kiungo muhimu wakati wa kuanza Daawah katika mji wa Makkah. Alikuwa ni mfano wa wanawake walioweza kutunza siri na kuhifadhi Uislamu wao katika mazingira ya vitisho, unyanyasaji, kudhalilishwa na mateso.
Kutoka kwa Bibi ‘Aishah, Allah Amuwie radhi amesema:
Walikutana masahaba kiasi cha thelathini na nane na Abubakar akamshauri Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasalam kwamba umefika wakati wa kuudhihirisha Uislamu. Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam hakuwafikiana na shauri hili na kusema : “Bado tuko wachache” Hata hivyo Abubakar alizidi kumnasihi Mtume mpaka siku moja wakakutana katika  Al Ka’abah na Waislamu wakajitenga kila mmoja na kabila lake. Akasimama Abubakr kuhutubia na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amekaa. Abubakr alikuwa ni wa kwanza kutoa hotuba kwa ajili ya Allah na Mtume wake, jambo lilioamsha hasira za washirikina na walighadhibika mpaka kuanza kupiga kuta za Al Kaabah na kisha kumvamia Abubakar na kumpiga kwa hasira. ‘Utbah ibn Rabi’ah akamwendea na kumpiga kwa viatu vyake usoni na kumchania nguo zake mpaka pasijulikane tumbo liko wapi na uso wapi na kutokuwa na kauli. Wakaja watu wake wa Banu Taym na kumchukua Abubakar mpaka nyumbani kwake. Kisha wakarudi Al Ka’abah na kusema” Wallahi akifariki Abubakar tutamuua ‘Utbah”
Kauli ilimrudia jioni yake na jambo la kwanza alilouliza : “Nini Alichofanywa Mtume?”. Hawakumjibu wakawa wanaendelea kumhudumia na kumlisha. Wakamuachia mama yake Abubakar,  Ummul Khayr kazi ya kumhudumia. Walipoondoka akawa anamuuliza suala lile lile:
“Nini Alichofanywa Mtume?”.
Akasema: “Wallahi mimi sijui chochote kuhusu rafiki yako”
Akasema: “Nenda kwa Ummu Jameel bint Al Khattaab na kamuulize”
Akatoka mama yake mpaka kwa Ummu Jameel na akasema:
“Abubakar anakuuliza kuhusu Muhammad ibn Abdillah”
Akasema: “ Mimi simjui Abubakar wala Muhammad ibn Abdillah na kama utapenda nitafuatana pamoja nawe kwenda kwa mwanao kumjulia hali (wakati huo mama yake Abubakar alikuwa hajasilimu)”
Akasema : “Sawa”
Wakafuatana mpaka kwa Abubakar na jinsi alivyomuona katika hali yake ya kuugua aliinama na kutoa sauti kali kwa kusema:” Wallahi hakika hawa waliokufanyia haya ni mafasiki na makafiri na ninatarajia Allah Subhaanahu Wata’ala atakulipizia kisasi juu yao”
Abubakr akarudia suala lake: : “Nini Alichofanywa Mtume?”.
Akasema Faatimah: “Huyu ni mama yako anasikia”
Akasema: “Hana matatizo kwako”
Akasema: “Yupo Salama na mzima”
Akauliza: “Yupo wapi?”
Akajibiwa: “Kwenye nyumba ya Arqam’”
Akasema: “ Wallahi sionji chakula wala kunywa maji mpaka mnipeleke kwa Mtume”
 Tukamuomba  avumilie mpaka utulivu uliporudi na watu kurudi katika hali za kawaida na tukamchukua mimi na mama yake hivyo hivyo akijikongoja mpaka kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam.
Alipofika na kukutana na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam, Mtume akamkumbatia na masahaba waliokuwepo wakaenda kumkumbatia huku wakimuonea huruma. Akasema Abubakar:
“Kwa baba na mama yangu, ewe mjumbe wa Allah. Mimi sina matatizo ila alivyonifanyia fasiki katika uso wangu, na huyu ni mama yangu ambae mwanawe hana dhimma nae, nawe ni mtu mwenye baraka hivyo mlinganie kwa ajili ya Allah na umuombee  ‘asaa atakuja kumuokoa na moto”
Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akamlingania na kumuombea nae akasilimu.
Hivyi ndivyo alivyoweza kutunza na kuhifadhi siri wakati Uislamu upo katika majaribu kwa kutokuwa na nguvu mpaka mama yake Abubakar hakuweza kumpa habari juu ya Mtume wa Allah.