Ka'ab Ibn Malik - Ukweli Ulivyomtakasa



Ka'ab Ibn Malik - Ukweli Ulivyomtakasa

Kabla ya kusilimu kwake Ka’ab Ibn Malik alikuwa mmoja katika washairi wakubwa katika mji wa Madina. Alijaaliwa ufasaha wa lugha ya kiarabu na mashairi yake yalitumika katika vita vya Aws na Khazraj (Makabila mawili makubwa katika mji wa Madina)
Sahaba Ka’ab ibn Malik, Allah Amuwie radhi,  alishindwa kuhudhuria vita vya Tabuuk pamoja na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Baadhi ya Masahaba walidiriki kutoa visingizio tofauti na ilipofika zamu yake licha ya kuwa mfasaha wa maneno na mzuri katika kujadiliana, alimwambia Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam ukweli kwamba ulikuwa ni uvivu na ajizi tu iliyomzuia na wala hana sababu nyengine yoyote. Hata Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wassallam alisema baada ya kumsikiliza: “Ama huyu amesema ukweli simama na ungojee mpaka Allah Subhaanahu Wata’ala akuhukumie.”
Ka’ab ibn Malik alisema ukweli. Lakini madhara yake yalikuwa makubwa. Mji mzima wa Madina ulimgomea pamoja na wenzake wawili. Kwa takriban siku hamsini hakuna aliesemezana nae wala kumjulia hali. Kisa alisema ukweli mbele ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Ukweli ulimponza. Wale waliodanganya mbele ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam wakaonekana ndio waungwana. Kwa mtazamo mfupi wa kibinadamu, kumeonekana uongo ndio suluhisho.
Lakini ukweli ulikuja kuthibitika kwamba athari zake zinakwenda mbali kuliko uongo pale Allah Subhaanahu Wata’ala alipoteremsha aya kutoka kwake inayowatakasa Ka’ab ibn Malik na wenzake . Attawbah/117- 118   
لَقَد تَّابَ الله عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ إِنَّهُ بِهِمْ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ {117}
وَعَلَى الثَّلاَثَةِ الَّذِينَ خُلِّفُواْ حَتَّى إِذَا ضَاقَتْ عَلَيْهِمُ الأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ وَضَاقَتْ عَلَيْهِمْ أَنفُسُهُمْ وَظَنُّواْ أَن لاَّ مَلْجَأَ مِنَ اللّهِ إِلاَّ إِلَيْهِ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ لِيَتُوبُواْ إِنَّ اللّهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ
Allah amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari wali mfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu
Na pia wale watatu walioachwa nyuma hata dunia wakaiona dhiki juu ya ukunjufu wake, na nafsi zao zikabanika, na wakayakinika kuwa hapana pa kumkimbia Allah isipokuwa kwake Yeye. Kisha akawaelekea kwa rehema yake ili nao waendelee kutubu. Hakika Allah ndiye Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
Ka’ab alitubu akarudi kwa mola wake pamoja na wenzake. Alisema kweli na akajirudi kwa kosa lake. Athari zake ni kuteremshiwa wahy na Allah Subhaanahu Wata’ala na kuuthibitishia ulimwengu (si mji wa Madina pekee kwani Quraan inasomwa na itaendelea kusomwa mpaka siku ya kiama) kwamba toba yao imepokelewa.
Licha ya kukubalika toba yake bado hakutosheka, Ka’ab alikwenda kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam na kumwambia :
 “Katika toba yangu nilikuwa nijitakase kwa kuitoa mali yangu yote kwa ajili ya Allah Subhaanahu Wata’ala na Mtume wake Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam”
Akasema Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam : “ Baki na baadhi ya  mali yako ni kheri kwako”.
Akaendelea kusema Ka’ab : “Ewe Mjumbe wa Allah! Hakika Allah ameniokoa kwa sababu ya kuusema ukweli kwa hivyo katika toba yangu sitothubutu kusema uongo ila nitakuwa mkweli katika umri wangu uliobakia.”
Ka’ab ibn Malik anathibitisha kauli kwa kusema: “Wallahi hakuna neema kubwa  aliyonijaalia Allah Subhaanahu Wata’ala baada ya kuniongoa kwa Uislamu zaidi ya kuwa mkweli mbele ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam”
Naam ni neema gani nyengine kama kila siku katika maisha ya ulimwengu Ka’ab ibn Malik husomwa kila inaposomwa Suuratu Tawbah. Ni neema gani nyengine kuliko kuthibitishiwa kukubaliwa toba kutoka kwa Allah Subhaanahu Wata’ala. Ni aina gani ya toba ambayo licha ya kutubiwa bado Ka’ab anataka kuitoa mali yake yote kama ni sadaka kwa ajili ya Allah na Mtume wake. Ni kwa sababu ya kusema ukweli hata kama unauma, hata kama utamdhuru, hata kama atakosa la kukosa almuradi wakati wa kutakiwa kusema ukweli aliusema.
Ndio maana Allah Subhaanahu Wata’ala baada ya kutukumbusha kisa cha Ka’ab na wenzake pamoja na Waislamu walioshiriki katika vita vya Tabuuk ambao walipata taabu na misukosuko ya aina yake akaendelea kwa kusema Attawbah 119
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَكُونُواْ مَعَ الصَّادِقِينَ  
Enyi mlioamini! Mcheni Allah, na kuweni pamoja na wakweli
Imaam Ibn Kathiyr katika tafsiri yake anasema katika kuitafsiri aya hii kwamba; semeni ukweli na mjiweke katika hali ya ukweli daima kwani mtakuwa pamoja na wakweli na kuepukana na majanga  na mabalaa na hatimae Allah kukupeni faraja.
Katika hadithi nyengine Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema kama ilivyopokewa na Abdullah ibn Masoud, Allah amuwie radhi:
Juu yenu kusema ukweli kwani ukweli unakuongoza kwenye uadilifu na uadilifu unakuongoza kwenye pepo. Hubaki mja anasema ukweli na hujichunga kuusema ukweli mpaka huandikiwa mbele ya Allah kuwa ni Siddiyq – mkweli. Na ole wenu na kusema uongo  kwani uongo hukuongoza kwenye uovu na uovu hukuongoza kwenye moto. Hubaki mja anasema uongo  na kujikita katika kusema uongo mpaka huandikwa mbele ya Allah – Muongo”. Bukhari na Muslim