Salman Al-Farisiy- mtafuta ukweli
Hiki ni kisa cha mtafuta ukweli. Na kwa
kuanzia na tumsikilize mwenyewe Salman:
“Nilikuwa Isfahan katika kijiji cah Tayyan
katika uajemi (Iran). Baba yangu alikuwa ‘Dihqan’ mkuu wa kijiji chetu na
alikuwa tajiri na alikuwa na nyumba kubwa.
Tokea utotoni baba alinipenda kuliko watoto
wake wengine na ilifika wakati mapenzi yake yalivyokuwa makubwa aliogopa kwamba
huenda nikapotea au kitu chochote kile kunifika, alinifungia ndani kama mfungwa
au kama vile wasichana wari wanavyotawishwa.”
Anaendelea kueleza, “Dini ya kimajusi
ikaniiingia kikwelikweli mpaka kufikia kupewa cheo cha mwenye kuulinda moto
tuliokuwa tukiuabudu. Kazi yangu ni kuhakikisha moto ule unawaka bila
kuzimika mchana na usiku kila siku.
Baba alikuwa na shamba kubwa ambalo
lilitoa mazao ya kutosha na mwenyewe baba alilishughulikia na kusimamia
mavuno. Siku moja ‘Dihqan’ akiwa katika kazi zake aliniambia: “Mwanangu
kama unavyoniona, nina shughuli nyingi sana leo na sitoweza kwenda shamba nendo
leo kaangalie na kulikagua.”
Nikiwa njiani, nikapita njia moja ambako kuna
kanisa na nilisikia sauti za maombi na yalinivutia. Sikujua chochote kuhusu
ukristo, wala dini nyenginezo kwani nilikuwa ‘mtawa’ na nilipozisikia zile
sauti nikaingia ndani kanisani kuona mwenyewe nini wanafanya watu hawa.
Nilipendezwa na jinsi wanavyosali na kuvutika
na dini yao, nikajisemea, “Hii ni bora kuliko yetu, sitoondoka mpaka jua
litue.”
Nilipouliza nikaambiwa dini hii asili yake ni
Sham. Lile hasa nililotumwa na baba sikulifanya kwani sikufika shamba na
ulipoingia usiku nilirudi nyumbani. Baba aliponiuliza nikamfahamisha
kukutana kwangu na wakristo na kumfahamisha jinsi nilivyovutiwa nao. Baba
akanishangaa na kuniambia, “Mwanangu hakuna chochote kizuri katika dini yao,
dini yako na wazazi wako ni bora zaidi.” Lakini mimi nikasisitiza, “hapana baba
dini yao ni bora kuliko yetu.”
Baba hakufurahishwa na mtazamo wangu na
akaingiwa na khofu kwamba nitaacha dini yangu. Kuona hivyo akaamua kunifungia
na kunitia minyonyoro miguuni. Niliwahi siku moja kupenyeza ujumbe kuwambia
wakristo wanipe habari za msafara wowote utakaoendea Syria. Ilipokuwa
tayari wakanipa habari niliweza kujifungua ile minyororo niliyofungwa na
kutoroka kwa kujificha mpaka nikajiunga na msafara. Na niliulizia kiongozi wao
nikelekezwa kwa Askofu mmoja, nikenda kumuona na kusema:
“Ninataka kuwa mkristo na nitapenda kujifunga
na kanisa na nijifunze kutoka kwako na kusali pamoja na wewe.”
Askofu akanikubalia. Muda mchache tu baadae
nikagundua kwamba Askofu huyu hakuwa mkweli wala hakuwa na uadilifu
kwani alikuwa akiwaamrisha wafuasi watoe sadaka huku akiwaahidi
kurehemewa. Watu wanapotoa sadaka, Askofu badala ya kuzitumia kwa njia ya
kheri kama kuwapa masikini na wanaohitaji, alikuwa akizitia mfukoni
mwake. Aliweza kujikusanyia fedha na dhahabu nyingi kwa njia hii.
Alipokufa na walipotaka kumzika nikawaeleza wale wafuasi tabia mbaya ya Askofu
wao .
Waliniomba niwaoneshe alipoficha sadaka hizo.
Niliwaonesha na walipoona machupa yaliyojaa dhahabu waliingiwa na ghadhabu na
kusema, “Hatukuziki tena na badala yake wakamsulubu na kumpiga mawe.”
Niliendelea kumtumikia mrithi wake na alikuwa
tofauti na wa kabla yake kwani alikuwa mtu wa dini na mwenye kuitafuta
akhera. Alikuwa akiabudu mchana na usiku. Nilipendezwa nae sana na
kutumia muda mwingi pamoja naye. Alipokufa, nikajifunga na watumishi tofauti wa
kanisa katika miji mbali mbali baada yake. Wa mwisho kukutana naye akanieleza
kuja kwa Mtume Muhammad (SAW) katika ardhi ya waarabu ambao alikuwa mkweli na
kukubali zawadi lakini kukataa kuitumia sadaka, Salman aliendelea.
Kundi la viongozi wa kiarabu wa kabila la Kalb
lilipita Ammuriyah, niliwaomba wanipeleke ardhi ya waarabu na kuwalipa kiasi
cha pesa nilichonacho. Walikubali na tulipofikia Wadil Qura (mji katikati ya
Madina na Syria) walivunja ahadi yetu na wakaniuza kwa myahudi. Nikawa mtumwa
wa kumfanyia kazi bwana wangu huyu ambaye naye akaniuza kwa jamaa yake kutoka Banu
Quraydha, akanichukua Yathrib.
Kipindi hicho, Mtume (SAW) alikuwa
akiwalingania watu dini ya kiislam Makka. Siku moja nilikuwa juu ya
mtende, wakati bwana wangu alitembelewa na jamaa yake akasema:
“Mungu awaapize na kuwapiga vita Aws na
Khazraj (makabila mawili makubwa ya madina). Wanakusanyika Quba leo
hii wakijiandaa kumpokea mtu mmoja kutoka Makka anaedai kuwa ni Mtume”
Niliposikia maneno haya niliingiwa na baridi
ya ghafla na kuanza kutetemeka kwa nguvu mpaka niliogopa huenda nikamuangukia
bwana wangu nikashuka na kumuuliza tena, “unasema nini?, Hebu rudia!
Bwana alikasirika na kunibamiza kibao na
kuniambia, “inakuhusu nini wewe rudi nenda ukafanye uliyotumwa.”
Jioni yake nikakusanya tende kidogo na kwenda
sehemu Mtume amefikia na kumwambia,
“Nimesikia wewe ni mtu mkweli na muadilifu na
kwamba una masahaba ambao ni wageni na wanahitaji msaada hii basi ni sadaka
yangu, nnahisi lakini wewe utahitajia zaidi kuliko wengine.
Mtume (SAW) akawapa masahaba na yeye hakula
hata kidogo. Sifa ya uadilifu na yale maneno aliyoambiwa na maaskofu wa
kikristo kuyathibisha mwenyewe Salman kwa Mtume (SAW) ni moja katika sababu
zilizomfanya asilimu. Mtume (SAW) alimkomboa pamoja na Salman mwenyewe
kuingia mkataba na bwana wake kwamba akimpa cha kiasi fulani cha mitende
angekuwa huru.
Mara nyingi akiulizwa yeye ni mtoto wa nani,
hujibu “ni Salman mtoto wa kiislam kutokana na kizazi cha Adam”
Salman alikuwa na nafasi muhimu sana katika
harakati za kupanuka kwa uislam. Katika vita vya Khandaq ni yeye aliyekuja na
rai ya kuchimbwa Khandaq kuizunguka Madina. Hata Abu Sufiyan alipoona
mbinu hii alisema “waarabu hawajawahi kutumia mbinu hii kabla”
Alipokuwa Amir wa Al-Madain (Ctesiphon) karibu
na Baghdad, Salman alikuwa akipata ruzuku ya Dirham 5000. Zote hii
huzitoa sadaka. Alijikimu mwenyewe kwa kilimo chake cha mitende mpaka baadhi ya
watu wakasema, “wewe ni Amir na rizki yako ni ya uhakika kutoka baytul maal na
bado unafanya kazi hii.”
“Ninapenda kujilisha kwa mikono yangu
mwenyewe”, Salman aliwajibu.
Inasemekana siku moja alimtembelea Abu Dardaa
na kumkuta mkewe katika hali mbaya sana na akamuuliza “una kitu gani?”
“Ndugu yako hana habari kabisa na hii dunia
akajibu, alipokuja Abu Dardaa alimkaribisha Salman chakula alipomwomba haya na
tule basi, Abu Dardaa akasema, mimi nimefunga!”
“Wallahi na mimi sili mpaka na wewe ule.”
Salman alikaa siku hiyo hadi usiku na Abu
Dardaa alipotaka kuamka kwa ajili ya ibada, Salman akamzuia na kumwambia:
“Ewe Abu Dardaa mola wako ana haki juu yako, Aila
(Familia) yako ina haki juu yako na mwili wako una haki juu yako, kipe kila
kimoja haki yake.”
Asubuhi yake walisali pamoja na baadaye kwenda
kwa Mtume (SAW). Mtume alimuunga mkono Salman.
Salman alibahatika kuwa mtu mwenye elimu,
hekima na busara. Ali ibn AbiTalib aliwahi kumfananisha Salman na
Luqman. Kaab Al-Ahbaar naye anasimulia: “Salman alikuwa na elimu na
busara kama mfano wa bahari isiyokauka.”
Alikuwa na elimu ya vitabu vya ukristo, Quran
na pia majusi na aliwahi kutafsiri baadhi ya sura za Quran kwa lugha ya kifarsi
wakati wa Mtume (SAW). Anahesabika kama ni mtu wa kwanza kuifasiri Quran
katika lugha isiyokuwa ya kiarabu.
Kwa mujibu wa riwaya za uhakika alifariki
mwaka 35 Hijiria enzi za Ukhalifa wa Uthman huko Madain (Ctesiphon).