Asim Ibn Thabit - Mpiganaji Jihadi Aliepigiwa Mfano na Mtume



Asim Ibn Thabit - Mpiganaji Jihadi Aliepigiwa Mfano na Mtume

Makureshi walitoka wote wakubwa kwa wadogo wenye hadhi na watumwa kwa ajili ya kukutana kivita na Muhammad ibn ‘Abdillah katika uwanja wa Uhud; huku vifua vikiwa ni vyenye kusheheni bughudha na chuki na damu ya kisasi kwa waliouawa katika Badri ilikuwa ikiwachemka.
Hawakutosheka na hayo tu, bali walitoka mpaka na wanawake wa kikureish wakiwa na lengo la kuhamasisha wanaume kupigana na kuzidi kuthibitisha wapiganaji wao na kuwafanya wawe imara kila pale watakaporudi nyuma na kuwa dhaifu.
Jumla ya waliotoka katika wanawake alikuwa ni Hindu bint ‘Utbah, mkewe Abu Sufiani na Raytah bint Munabih mkewe ‘Amrou ibn Al ‘Asi na Sulafa bint Sa’ad pamoja na mumewe Talha na watoto wake watatu; Musafiyu na Al julasi na Kilabu pamoja na kundi kubwa la wanawake.
Makundi mawili yalipokutana katika Uhud na moto wa vita ukazidi kukolea, Hindu ibn ‘Utbah alisimama pamoja na wanawake aliokuwa nao, wakawa wamesimama nyuma ya safu wakiwa wamebeba dufu huku wakizipiga na kusema, “Ikiwa mtasonga mbele tutawakumbatia na kukutandikieni vyema, Ama mkikimbia tutawakimbia mkimbio usio na mahaba”
Ilikuwa wimbo wao huu ni wenye kuzidisha hamasa ya jeshi, na ukawa unawaingizia na uchawi ndani ya nafsi zao.
Baada ya vita kumaliza na makureshi kupata ushindi juu ya waislam, wanawake walisimama wakiwa wamegubikwa kwa furaha ya ushindi, wakaanza ufisadi na kupiga vigelegele hapo kwenye medani ya vita. Pia wakawa ni wenye kukatakata viungo na kupasua matumbo ya (mashahidi wa kiislamu) wakitofua macho wakikata masikio na pua. Hakuwa anahisi mmoja wao amelipiza kisasi chake ila baada ya kukatakata pua na masikio na kutunga mfano wa kidani au bangili na kujivisha yote hayo yakiwa ni kisasi kwa jamii zao baba au ndugu au ami waliouawa katika Badr.
Lakini Sulafa bint Sa’ad hali yake ilikuwa ni kinyume na wengineo katika wanawake wa kikureish. Hofu na wasiwasi vilimzunguka akisubiri kukabiliana na mumewe au mmoja kati ya watoto wake watatu, ili aweze kupata habari na kushiriki na wanawake wengine kusherehekea ushindi.
Lakini bahati mbaya ilikuwa subira yake!. Akawa yuko ndani ya medani ya vita akichunguza nyuso za waliokufa ghafla akajikuta mbele ya uso wa mumewe akiwa amekwisha kufa na amejawa damu.
Akachupa kama simba majeruhi akawa ni mwenye kutupa jicho huku na kule akitafuta wanawe Musafiyu na Kilabu na Al julasi. Mara aliwaona wametawanyika kwenye uwanja wa Uhud, Musafiyu na Kilabu wakiwa wamekwisha kufa, ama Al julasi akiwa yumo akitweta pumzi za mwisho.
Akamkumbatia akiwa akimtuliza na sakarati za mauti na akakiweka kichwa chake mapajani akawa anampangusa pangusa damu usoni na midomoni. Hakika Sulafa machozi yalimkauka machoni mwake kwa kishindo cha msiba.
Akamuelekea mwanawe na kumuuliza: "Nani ulipigana nae?" Akawa anajaribu kusema lakini sakarati ya mauti ilimzuia. Nae akazidi kumuuliza na akapata kauli akasema: “Asim ibn Thabit. Na kaka yangu Musafiyu vile vile amekwishafariki".
Wazimu ulimpanda Sulafa akawa anapaza sauti kwa kilio na akaapa kwa laata na uzzah, kwamba nafsi yake haitotulia wala chozi halitokauka machoni mwake mpaka pale makureshi watakapomlipizia kisasi chake kwa ‘Asim ibn Thabit na watakapomletea bufuru lake la kichwa iwe ni bilauli ya kunywea pombe.
Akaweka nadhiri ya tunzo ya mali aitakayo kwa atakaeweza kukileta kichwa chake. Habari za nadhiri hiyo zikaenea baina ya makureshi na ikawa kila kijana wa Makka anatamani kama atakutana na ‘Asim bin Thabit na kukikata kichwa chake na kukiweka mbele ya Sulafa na kuwa ni mshindi wa zawadi nono.
Waislamu walirudi Madina baada ya vita vya Uhud, wakawa wanawatakia rehema waliokufa mashahidi wakawa pia ni wenye kuwalaki kwa kuwapongeza waliopambana kishujaa akiwemo ‘Asim ibn Thabit, wakawa wanashangaa ni vipi aliweza kuwaangusha watu watatu wote wa familia moja.
Mmoja wao alisema: “kuna ajabu gani katika hilo?” “Hamkumbuki Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) alipotuuliza, kabla ya vita, "Vipi mnapigana?" akasimama ‘Asim ibn Thabit akachukua upinde wake akasema: “Watu wakiwa karibu yangu dhiraa mia basi nitarusha mishale, ama wakiwa karibu yangu zaidi basi ni kuchoma kwa mkuki mpaka ukatike”. Ukikatika tunaweka chini na kutoa panga na hapo ni kupambana kwa upanga”. Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) alisema: "Hivi ndivyo kupigana anaepigana, basi na apigane mfano wa ‘Asim".
Baada ya kupita muda mfupi kumalizika vita vya Uhud, Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) aliwatuma masahaba sita watukufu kwa kazi maalum. Akamchagua ‘Asim ibn Thabit kuwa ni kiongozi wa kikosi hicho.
Wakatoka watukufu hao kutekeleza amri ya Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na walipokuwa katika moja ya njia zisizo mbali na Makka, watu wa kabila la Hudhayl waliwatambua na kuwazingira haraka, ikawa mfano wa kitanzi shingoni mwa ‘Asim na wenzake, wakatoa panga zao na tayari kwa mapambano.
Hudhayl wakawaambia: “Nyinyi ni wachache nasi tunakupendeni ndugu zetu hatutaki kuwadhuru pindipo mtajisalimisha hii ni ahadi na mkataba kwa Allah”. Masahaba wakawa wanatazamana nyusoni kama vile wenye kushauriana.
‘Asim akawageukia wenzake na kusema: “Ama mimi sitakuwa katika mikono ya washirikina". Akakumbuka nadhiri ya Sulafa aliyoitoa kwa ajili yake, akatoa upanga wake katika ala akasema: “Ewe Mola mimi ni mwenye kuilinda dini yako na kuipigania. Ilinde nyama yangu na mifupa yangu wala usiisahilishe kwa adui yeyote wa Allah". 
Hapo akawazungukia Hudhayl yeye pamoja na masahaba wengine wawili wakapambana na kupigana mpaka kufa mmoja baada ya mwengine. Masahaba waliobaki walijisalimisha, lakini hawakusalimika ila waliuawa kikhiyana.
Hudhayl hawakuwa mwanzo wenye kutambua kwamba ‘Asim ibn Thabit ni mmoja wa waliowaua. Walipojua hivyo walifurahi sana na wakajitamanisha zawadi nono.
Jee hajawa Sulafa bint Sa’ad ameweka nadhiri ikiwa atakipata kichwa cha ‘Asim ibn Thabit atakinywelea pombe (kwa kukigeuza bilauli)?
Jee hakuwa ameahidi zawadi kiwango akitakacho mtu atakaemletea ‘Asim hai au amekufa?.
Baada ya muda kupita kwa kufa ‘Asim ibn Thabit.  Makureshi walipata habari kwani Hudhayl walikuwa wanaishi karibu na Makka.
Viongozi wa Makureshi wakatuma mjumbe kwa waliomuuwa ‘Asim na kuwataka walete kichwa chake ili watulize joto la Sulafa bint Sa’ad na wawe wametekeleza kiapo chao, na kupungua huzuni yake ya kuuawa watu wake wote watatu kwenye mikono ya ‘Asim ibn Thabit.
Wajumbe walichukua mali nyingi na wakatakiwa kuitoa kwa Hudhayl wakikipata kichwa chake. Hudhayl wakausogelea mwili wa ‘Asim ibn Thabit ili wakikate na kukitenganisha kichwa na mwili wake. Wakashtushwa na kundi la nyuki wakiwa wamemzunguka kila upande.
Kila walipoukaribia mwili, nyuki waliwashambulia nyusoni mwao na mwilini mwao, waliposhindwa kumfikia baada ya majaribio mengi, wakasema baadhi yao: “mwacheni hadi usiku uingie na kiza kitande kwani wakati huo kikiingia kiza nyuki watahama na kukuachieni mwili kwenu”. Wakakaa mahala sio mbali wakisubiri.
Lakini mchana haukuwa wenye kuzama na usiku kuingia mara kiwingu kizito kikatanda na mameso na mangurumo yakapiga. Mvua nzito ilimwagika ikiwa haina mfano tangu maisha yao yote katika ardhi ile.
Haraka mabonde yakaanza kujaa na mafuriko yakakumba vilivyopo. Asubuhi kupambazuka, Hudhayl, wakaanza kuutafuta mwili wa ‘Asim ibn Thabit kila pembe bila ya mafanikio. Mafuriko yameusafirisha mbali ambapo hawapatambui.
Hakika Allah (Subhaanahu Wata’ala) ameitikia dua ya ‘Asim ibn Thabit na akauhami na kuulinda mwili wake tohara usije kuchezewa na kukatwakatwa. Na amekilinda kichwa chake kitukufu kugeuzwa bilauli ya kunywelewa pombe.
“ Wala hawakujaaliwa washirikina kuwa ni wenye nafasi mbele ya waumini” Quraan
Last Updated on Saturday, 12 September 2009 07:39
 
Administrator