Hakim ibn Hazm- rafiki
wa Mtume (SAW)
Historia
inanukuu kwamba Hakim ni mtu pekee aliyezaliwa ndani ya Al-Kaabah!
Mama
yake, akiwa pamoja na marafiki zake, siku hiyo waliitembelea Al –Kaaba
ilikuwa wazi kwani kulikuwa na sherehe enzi za Ujahiliya. Akapatwa na
uchungu na hata kushindwa kwenda wala kusogea pahala pengine. Likaletwa
busati na kujifungua Hakim hapo hapo. Baba yake ni Hazm ibn Khuwaylid,
ndugu yake aliekuwa mke wa Mtume (SAW) bi Khadija bint Khuwaylid (RA).
Alikuwa
katika utajiri na neema hasa kutokana na nasaba yake kuwa yenye hadhi na
heshima. Alikuwa mstaarabu na mwenye khulka nzuri mpaka kuweza kuheshimiwa na
watu wa rika tofauti. Alikabidhiwa jukumu la ‘rifada’ kitengo maalum
cha kuwasaidia wenye shida na waliopoteza mali zao msimu wa Hijja.
Alifanya kazi hii kwa uadilifu na ikhlaas mpaka wakati mwengine alikuwa
akitoa katoka mfuko wake mwenyewe.
Hakim
alikuwa rafiki wa karibu wa Mtume (SAW) kabla ya kupewa utume. Ingawa
alimzidi umri Mtume (SAW) kwa takriban miaka mitano, alikuwa akitumia muda
wake mwingi pamoja na Muhammad ibn Abdullah. Uhusiano wao huu ulikuja
pata nguvu zaidi pale Mtume (SAW) alipomuoa shangazi yake, Bi Khadija bint
Khuwaylid.
Kilichoshangaza
zaidi, licha ya kuwa na urafiki wa karibu na Mtume (SAW), lakini hakusilimu
mpaka Makka ilipofunguliwa, ikiwa ni zaidi ya miaka ishirini baadaye.
Mtu kama Hakim mstaarabu na mwenye busara na kuwa na karibu sana na Mtume
(SAW) angelihesabika katika miongoni mwa watu wa awali kusilimu, lakini hali
haikuwa hivyo.
Kama
waislam walivyoshangaa Hakim kuchelewa kuingia uislam, Hakim mwenyewe naye
pia alijishangaa hasa baada ya kuonja tamu ya imani, akajuta kwa kila muda
katika maisha yake alioupoteza akimshirikisha Allah (SW) na kumkataa Mtume
Muhammad (SAW).
Siku
moja, mwanawe alimuona baba yake akilia na kumuuliza, “kwanini unalia
baba?”
“Vitu
vingi tu mwanangu mpenzi” alijibu Hakim huku akindelea:
“Zaidi
ni kuchukua muda mrefu mpaka kusilimu kwangu, ningeliwahi kungelinisaidia
kupata wasaa wa kufanya mambo mengi mema ambayo nimeyakosa hata kama
ningelipewa dhahabu kuitumia kwenye ardhi. Nilinusurika vita vya Badr
na pia vita vya Uhud, baada ya vita vya Uhud nikajisemea sitowasaidia tena
maquraysh dhidi ya Muhammad (SAW) na sitoondoka tena Makka.”
Aliendelea,
“Ikinijia kutaka kusilimu, huwaangalia watu wengine miongoni mwa maquraysh,
watu waliokuwa na nguvu na upeo wa mambo na kusimama kidete kwenye hadhara na
vitendo vya kijahiliya. Basi hurudi nyuma na kuungana nao na majirani
zao….. Allah! (SW) najuta kwa nini sikusilimu, na kufuata wazee na mababu
zetu tu bila ya kuwa nadhari; kwanini nisilie mwanangu?”
Hata
Mtume Muhammad (SAW) alishindwa kumwelewa Hakim ilikuwa kuwaje mpaka uislam
ukawa umejificha kwake? Mtu mwenye hekima, busara na haiba kubwa kama
Hakim nini chengine anahitaji kuuona ukweli na haki?
Kwa
muda mrefu Mtume(SAW) alikuwa akitamani kundi la watu fulani kuingia
uislam. Siku ya kukombolewa Makka, Mtume Muhamad (SAW) alisema
kuwaambia Masahaba:
“Kuna
watu wane Makka ambao ninawachukulia kutojishughulisha na shirk, na
ningependelea kama wangesilimu.”
Masahaba
wakauliza, “Ni nani hao, ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu?.
Ibn
Usayd, Jubayr ibn Mutim, Hakim ibn Hazm na Suhayl ibn Amr”
Kwa
rehma zake Mwenyezi Mungu wote hawa walikuja kusilimu pale Muhammad (SAW)
alipoingia Makka na kuikomboa kutoka katika ukafiri, ujinga na ujahili na
alitoa kinga kwa kusema:
“Yoyote
atakayetamka ‘Ash-hadu ana-laa ilaha ill allah wahdahuu laa sharika
lahu wa ana Muhamaad Abuduhu warasuuluhu” basi yuko salama.” “Yoyote
atakayebaki Al kaaba na kuweka silaha chini basi yuko salama. Yoyote
atakayekwenda nyumba ya Abu Sufiyan, basi yuko salama. Na yoyote
atakayekwenda nyumba ya Hakim ibn Hazm, yuko salama……..
Hakim
alitamka ‘kalima’ bila ya kinyongo na kuapa kwamba zile juhudi zote alizokuwa
akizitumia kuupiga vita uislam sasa atazitumia kwa ajili ya uislam.
Hakim
alimiliki ‘Darun nadwa’ lililokuwa jengo la kihistoria Makka kwani lilikuwa ‘
jengo la bunge’ ambapo maquraysh hukutana zama za ujahiliya kupanga njama za
kumpiga vita Mtume (SAW).
Aliamua
kuachana nalo kabisa jengo hilo na kukata mawasiliano yake yote nalo na
hatimaye kuliuza kwa Dirham laki moja, mpaka kijana mmoja wa kiquraysh
akamhoji, ‘umeuza’ kitu cha thamani na hadhi na historia ya waquraysh!”
“Njoo
mwanangu; hadhi na utukufu wote umekwisha na chote kilichobaki cha thamani ni
taqwa. Mimi nimeuza jumba hili ili nikapate nyengine peponi. Wallahi fedha
yote niliyoipata kwa kuliuza nimezitoa zitumike kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
(SW)” akamjibu Hakim.
Hakim
alitekeleza ibada ya Hijja na alikwenda na ngamia mia walio bora na wote
kuwachinja ili apate kuwa karibu na Mwenyezi Mungu na Hijja iliyofatia alisimama
Arafa akiwa pamoja na watumwa wapatao mia, kila mmoja akampatia nishani ya
fedha ambayo imeandikwa ‘Uko huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kutoka kwa
Hakim ibn Hazm’
Ilipokuja
Hijja ya tatu, alikwenda na kondoo elfu moja na na akawachinja wote Mina ili
kuwalisha maskini na yote hayo alifanya ili apate kuwa karibu na Allah (SW).
Ingawa
alikuwa mkarimu mno na kutumia mali zake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
(SW). Hata hivyo, alipenda na yeye kuwa na kingi. Baada ya
vita vya Hunayn, alimuomba Mtume (SAW) ngawira aliyokuwa akiigawa na akapewa,
akaomba aongezwe, akaongezwa. Kwa kuwa Hakim alikuwa mwanagenzi katika
uislam, Mtume (SAW) alikuwa mkarimu zaidi kwa wanagenzi ili kuwazoea nyoyo
zao. Hakim akapata ngawira nyingi sana lakini Mtume (SAW) akamwambia
kwa kumkumbusha; “Ewe Hakim! Hakika utajiri ni mtamu na unapendeza.
Yoyote atakaeuchukua kwa uchu hatorehemewa nao, itakuwa kama mtu anakula bila
ya kutosheka, mkono ulio juu bora kuliko mkono ulio chini (ni bora kutoa
kuliko kupokea).
Maneno
haya ya hekima na busara kutoka kwa Mtume (SAW) yalimwingia Hakim vizuri sana
akilini mwake na hapo kumwambia Mtume (SAW);
“Ewe
mjumbe wa Mwenyezi Mungu ambaye amekutuma kwa haki sitoomba tena baada
yako kitu chochote.”
Enzi
za Ukhalifa wa Abubakar, Hakim aliitwa mara kwa mara kwenda kuchukua ruzuku
yake kutoka Baytul-Mal lakini alikataa na enzi za Umar pia akaendelea na
msimamo wale mpaka Umar akawahutubia waislam:
“Nnashuhudia
kwenu enyi waislam kwamba nimemwita Hakim kuchukua ruzuku yake lakini
anakataa.”
Hakim
akawa mkweli kwa ahadi yake kwani hakuchukua kitu chochote, alipata funzo
kubwa kutoka kwa Mtume (SAW) kwamba kukinai ni utajiri usiokuwa na mfano!
|
Hakim ibn Hazm- rafiki wa Mtume (SAW)
Subscribe to:
Posts (Atom)