Muaadh bin Jabal - Mjuzi wa Mambo ya Halali na Haramu



Muaadh bin Jabal - Mjuzi wa Mambo ya Halali na Haramu


Kimefasiriwa na Ustaadh Talib Juma Ali
Ilipoanza kun’gara Jaziyrat Al-Arab kwa nuru ya uongofu ya Uislamu na haki, alikuwa kijana wa kimadina Mu’aadh bin Jabal bado ni mdogo na alikuwa akitofautiana na wacheza wenzake kwa uhodari wake, ufasaha na hima ya juu.  Zaidi ya hayo alikuwa mwenye sura jamili (nzuri), macho ya wanja kichwa kilichojaa nywele, meno yang'arayo yanayovutia kwa mwenye kumtazama na kumvutia moyoni mwake
Alisilimu kijana huyu kwenye mikono ya mlinganiaji wa Makka Mus’ab bin ‘Umayr. Na usiku wa Al-Aqaba alinyoosha mkono wake kukamatana na wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wassalam) na kumfanyia bay-at (kiapo cha utii). Alikuwa Mu’aadh pamoja na watu wengine sabini na mbili waliokusudia kwenda Makka wakiwa na shauku ya kukutana na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) wawe na hadhi ya kumfanyia bay-‘at na kuweza kuandika ukurasa bora katika tarekhe.
Mara baada ya kurudi Makka na kufika Madina, yeye na vijana wenzake walianzisha kikundi cha kuvunja masanamu na kuyatoa nje ya majumba ya washirikina wa Madina kwa siri na kwa dhahiri. Ilikuwa athari ya harakati za vijana hawa, kusilimu mzee miongoni mwa wazee wa Madina, nae ni ‘Amru bin Aljamouh ni bwana katika mabwana wa Bani Salamah na ni mtukufu miongoni mwa watukufu wao.
Na alikuwa na sanamu lake alilolifanya kwa ubao wa mti wenye thamani kama ilivyokuwa ada kwa watu wa juu. Alikuwa mzee huyu, akilitukuza na kulishughulikia sana sanamu lake na kulipamba kwa hariri na kulitia manukato bora kila asubuhi. Vijana hawa wakalivamia sanamu hilo ndani ya kiza cha usiku na kulibeba kutoka mahala lilipowekwa na kulipeleka hadi nje ya viambo vya Bani Salama na kulitupa ndani ya shimo la taka.
Asubuhi alipoamka Amour bin Aljamouh aliliendea sanamu lakini hakulikuta akaanza kulitafuta kila mahala na mwisho akalikuta limetupwa kifudifudi na kujaa uchafu. Akasema; "Ole wenu ni nani aliyemfanyia mungu uadui usiku?". Akalitoa na kulikosha na kulipaka manukato na kulirejesha mahala pake. Akasema “Ewe manata, laiti ningelimjua aliyekufanyia hivi basi ningemuadhibisha".
Usiku ulipoingia na Amrou bin Aljamouh akaingia ndani kulala, vijana walilinyemelea tena sanamu na wakalifanyia kama walivyolifanyia usiku uliopita. Akawa ni mwenye kuendelea kulitafuta mpaka akalikuta ndani ya shimo la taka akalitoa na kulikosha na kulitoharisha na kulitia manukato, na akatoa ahadi dhidi ya adui wake.
Hali ilipozidi kuendelea alilitoa shimoni lilimotupwa halafu akaja na upanga akautundika kwenye sanamu, akalihutubia kwa kusema; “Wallahi hakika mimi simjui anaekufanyia haya kama unavyoona ikiwa iko kheri kwako ewe manata basi jilinde nafsi yako na huu upanga unao".
Usiku ulipoingia tena na kulala, walirudi tena vijana kwenye sanamu na upanga unanin’ginia shingoni mwake, na kulichukua na wakalifunga pamoja na mbwa aliyekufa na kwa pamoja wakawatumbukiza ndani ya shimo la taka.
Asubuhi ilipochomoza Amrou bin Aljamouh alitoka kwa hima na kuanza kulitafuta sanamu lake, mpaka akalikuta limetumbukizwa shimoni likiwa limezongwa na mbwa aliyekufa na kutupwa kichwa chini.Hapo alilitazama na kusema; “Naapa laiti ungelikuwa ni mungu usingalikuwa ndani ya shimo pamoja na mbwa umezongwa.”
Alisilimu na akawa mbora katika Uislamu wake.
 Alipofika Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) Madina akiwa ni mwenye kuhama (Makka), kijana Mu’aadh aliambatana na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) mfano wa kivuli na mwenyewe. Akachukua kutoka kwake Qur an na akapata kwake masuala ya sheria ya kiislamu akawa ni msomaji mkubwa wa kitabu cha Allah na mjuzi wa masuala ya kisheria.  
Anasimulia Yazid bin Qutayb; “Niliingia ndani ya msikiti wa mji wa Himsi nikamkuta kijana amezungukwa na watu, anaposema ni kama vile nuru na lulu zinatoka kinywani mwake.”
Nikauliza; “Ni nani huyo?”
Wakaniambia ni Mu’aadh bin Jabal.
Amepokea Abu Muslim Al-Khawlaniy na kusema; "Niliingia ndani ya msikiti wa Damascus na nikakutia darsa iliyojumuisha wazee masahaba wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) baina yao kijana mwenye macho ya wanja, meno yenye mn’garo, kila walipokuwa wakihitilafiana katika jambo hulirejesha kwake. Nikawauliza wale waliopo baina yake ni nani huyo wakasema  ni Mu’aadh bin Jabal.
Hakuna shaka hakika Mu’aadh amelelewa katika madrasa ya Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) tangu kucha zake zinaanza kuchomoza na akamaliza kutoka madrasa hiyo akiwa na elimu aliyoichota moja kwa moja katika chemchem yake na akapata maarifa katika asili yake.
Unamtosha Mu’aadh ushahidi wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) aliposema; “Mjuzi katika umma wangu wa mambo ya halali na haramu ni Mu’aadh bun Jabal." Inatosheleza fadhila juu ya umma wa Muhammad kwamba alikuwa ni mmoja ya watu sita waliokusanya Qur an wakati wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam). Hivyo ilikuwa masahaba wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) wanapozungumza na baina yao Mu’aadh bin Jabal, humuangalia kwa haiba yake na kumtukuza na kumheshimu kwa elimu yake. Aliweka Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) Masahaba wake wenye nguvu katika huduma ya Waislamu na Uislamu.
Huyu hapa Nabii (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) wakati anawaona makureshi wanaingia katika dini ya Allah makundi kwa makundi baada ya Fat-hi Makka. Na anahisi haja ya Waislamu wapya ya kupatiwa mwalimu mzuri wa kuwafundisha Uislamu na kuwafunza fiqh, basi anamchagua Attab bin Useyd kuwa ni Khalifa wake wa Makka na kumwacha pamoja na Mu’aadh bin Jabal kuwafundisha watu Qur an na kuwapa fiqh ya dini yao.
Ulipokuja ujumbe wa watawala wa Yemen Madina kwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na kutangaza kusilimu kwao na wanaowafuata, wakaomba kupatiwa mwalimu wa kuwafundisha dini yao. Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam)  alichagua kwa kutekeleza wajibu huu kundi la madu’aati (walinganiaji) waongofu katika masahaba wake na akamchagua Mu’aadh bin Jabal kuwa ni Amiri wao.
Na alitoka Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) kuliaga kundi la uongofu na nuru akawa anatembea pembeni ya mnyama wa Mu’aadh, na Mu’aadh akiwa amepanda juu ya mnyama akatoka nae mbali akiwa na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) kama kwamba anataka kumwambia jambo Mu’aadh.
Halafu akamuusia na kumwambia; “Ewe Mu’aadh pengine hutanikuta tena baada ya mwaka wangu huu, na pengine upite kwenye msikiti wangu na kaburi langu.” Mu’aadh akalia sana kilio cha huzuni ya kumkosa kipenzi Muhammad (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na wakalia pamoja nae Waislamu.
Na ilikuwa ni kauli ya kweli ya Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) kwani jicho la Mu’aadh halikupata tena kumuona Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) baada ya muda ule.
Baada ya kurudi Yemen hapana shaka, Mu’aadh alilia alipofika Madina. Kwani Madina ilikuwa imejiinamia kwa huzuni ya kukosekana kipenzi wake Alhabib Mustafa (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam). Alipochukua ukhalifa Sayyidina ‘Umar bin Al Khattaab, alimtuma Mu’aadh kwenda kwenye kabila la Bani kilabi kwa ajili ya kuwagawia malipo yao, na kuwagawia mafukara wake sadaka kutoka kwa matajiri wao na akatekeleza kama alivyoamrishwa.
Aliporudi safarini, alikuja kwake na alipokewa na mkewe akiwa na mfano wa ukanda ambao hufungiwa farasi kwenye soji lake, ameuzungusha shingoni mwake. Mkewe alimuuliza; “Ziko wapi zawadi ambazo viongozi huletea wake zao?” Akamwambia; “Nilikuwa na mlinzi aliye macho ananiangalia kwa kila jambo” Akasema; “Hakika wewe ulikuwa ni mwaminifu wakati wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na Abubakar halafu amekuja ‘Umar ndiyo anakuwekea mlinzi kukufuatilia?”
Habari hizo alizieneza kwa wakeze ‘Umar nao wakamshitakia ‘Umar. ‘Umar zikamfika habari na akamwita Mu’aadh na kumwambia; “Je mimi nimekutumia mtu kukufuatiliya?” Akasema Mu’aadh; “Siyo. Ewe Amiirul Muuminina lakini sikuwa na hila ya kuombea msamaha ila hiyo".’Umar akacheka na akampa kitu, na kumwambia; “Nenda ukamridhishe nacho",
Na wakati huo huo wa Al-farouq, alitumiwa na liwali wake wa Sham Yazid bin Abi Sufiyan ujumbe na kumwambia; “Ewe Amir Al - Muuminina. Hakika watu wa Sham wamekuwa wengi na kuenea miji kadhaa, na nahitajia mwalimu wa kuwafundisha Qur an kuwafunza fiqhi ya dini yao hebu nisaidie ewe Amiirul Muuminina watu wakusomesha"
‘Umar akawaita watu watano waliokusanya Qur an zama za Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) nao ni Mu'aadh bin Jabal na 'Ubaadah bin Saamit na Abu Ayyub Al-ansaariy, Ubay bin Ka’ab na Abu  Ddardaai," Akawaambia wote; "Hakika ndugu zenu wa Sham wanaomba msaada wa wenye kuweza kuwasomesha Qur an na fiqh ya dini basi fanyeni hivyo Allah akurehemeni watatu wenu na mkipenda chagueni watatu wenu au nichague mimi"
Wakasema; “Kwa nini tufanye kura? Abu Ayyub ni mtu mzima sana na Ubay ni mgonjwa. Tuliobaki ni sisi watatu” Akasema Umar: “Anzeni kwenye mji wa Himsi mkiridhishwa na hali ya watu wake mwacheni mmoja wenu hapo na mwengine atoke kwenda Damascus na wa mwisho aelekee Palestina.”
Wakasimama Masahaba hawa wa Mtume watatu na wakatekeleza amri waliyopewa na Alfarouq kuanzia miji wa Himsi na wakamuacha hapo 'Ubaadah bin Saamit na Abu Ddardaai akaelekea Damascus na Mu'aadh bin Jabal akaelekea Palestina.
Na huko Mu’aadh akasibiwa na maradhi na mauti yalipomkabili alielekea kibla akawa anasema.
-                      Karibu ewe mauti karibu.
-                      Mgeni amewadia baada kuondoka kitambo
-                      Na mpenzi ametujia katika shauku.
Akanyanyua macho na kuangalia mbinguni na kusema; “Ewe Mola!, hakika wewe ni mwenye kujua kwamba hakika mimi sikuwa mwenye kupenda dunia wala mwenye kupenda kubakia humo kupanda milima na kuvuka mito lakini ni kiu tu itokanayo na joto na shida za wakati na kufuatilia wanachuoni kwa kukaa kwenye vikao vya dhikri.
Ewe Mola ipokee nafsi yangu kwa kheri vile unavyoipokea nafsi ya Muislamu Muumini".
Hapo roho yake ikatoka akiwa mbali na jamaa zake akiwa ni mlinganiaji - Daa'iy- katika njia ya Allah Subhaanahu Wata’ala akiwa ni Muhajir katika njia ya Allah Subhaanahu Wata’ala.