Khabbab ibn Arraatt- wa mwanzo kudhihirisha imani




Khabbab ibn Arraatt- wa mwanzo kudhihirisha imani 
Bibi mmoja, Umm Ammaar wa kabila za Khuzaa Makka, siku moja alikwenda soko la watumwa. Alitaka kumnunua kijana kwa shughuli za nyumbani.  Alipoangalia waliokuwepo siku ile alimuona kijana mmoja ambaye alionekana hata bado kubaleghe lakini mwenye afya njema na nguvu, hakufikiria mara mbili akatoa pesa na kumnunua.
 
Walipokuwa wanaelekea nyumbani, Umm Ammaar akamuuliza:
  “Nani jina lako, kijana”.
  “Khabbab”, alijibu.
  “Baba yako”, aliendelea kuulizwa.
  Alijibu, “Al-Aratt.”
  “Unatokea wapi?”
  “Najd”
  “Kumbe ni Mwarabu!”
  “Ndio, Banu Tamim”
 
Umm Ammar aliendelea kumuuliza,“Ilikuwaje ukafika kwenye mikono ya wafanya biashara ya utumwa?” :
 
“Mmoja katika makabila ya waarabu walituvamia katika eneo letu, walichukua wanyama wetu na kuwateka wanawake na watoto, mimi ni mmoja wapo mpaka kufikia hapa Makka nimepita katika mikono mingi tu”.
 
Umm Ammar akampeleka kwa mmoja wa wafua vyuma Makka ili ajifunze fani ya kutengeneza panga na jambia.  Alikuwa hodari na muda mchache tu baadaye naye akawa fundi stadi. Alipokuwa mkubwa, Umm Ammaar akamfungulia banda lake lililokuwa na zana zote za kutengeneza mapanga.
 
Aliendelea kuwa kijana maarufu wa kazi yake hii, watu walimpenda kwani alikuwa mkweli na muaminifu.  Umm Ammaar akapata faida nzuri kupitia mgongo wa Khabbab.
 
Tokea utotoni Khabbab alionesha dalili zote za kuwa kijana mwenye akili na busara.  Mara nyingi akimaliza kazi zake huonekana kukaa na kuutazama kwa masikitiko mfumo mzima wa maisha wa waarabu uliojaa rushwa, ubadhirifu, ujahili na ukatili. Akawa anajisemea moyoni, “Baada ya usiku wa kiza basi lazima kuna alfajiri”.  Alikuwa akitaraji kuishi maisha marefu apate kukiona vipi kiza kitakavyotoweka na nuru na mwanga ukatavyoangaza na kumurika.
 
Hakusubiri muda mrefu kwani akiwa mkaazi wa Makka, aliona miale ya mwanzo ya uislamu ikichomoza miale hii ilitoka kinywani mwa Muhammad ibn Abdullah ambaye alitangaza kwamba hakuna anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa muumba ulimwengu.
 
Akawataka watu kuondokana na dhuluma na ukandamizaji na kuwakemea matajiri kujipatia utajiri wao kupitia kwa masikini, alikataza kuwepo tabia ya upendeleo wa kikabila, udugu na ukubwa na kutaka utu wa binadamu lazima uheshimiwe kwa wote na kuwaonea huruma wasiojaaliwa miongoni mwao mayatima, walioishiwa katika safari zao na masikini.
 
Kwa Khabbab, ujumbe huu mzito aliokuja nao Muhammad (SAW) ulikuwa kama mwanga mkubwa uliomulika macho yake na kumtoa katika kiza kinene cha ujahili an ujinga.  Alikwenda mwenyewe kusikiliza mafunzo ya Mtume (SAW) na kusema, “Ash-hadu an laa ilaha Illa llah wa-ana Muhammadan Rasulullah”.  Khabbab ni miongoni mwa watu kumi wa mwanzo kusilimu.
 
Tofauti na wati wengine, hakuficha habari za kusilimu kwake. Lakini habari zilipomfika Umm Ammaar alikasirika sana. Akaenda kwa kaka yake Sibaa ibn Abdul-Uzza naye akakusanya kundi la vijana wa kikhuzaa na wakamfuata kazini kwake. Walimkuta hata habari hana akiendelea na kazi zake.  Sibaa akamuuliza:
 
“Tumesikia habari kuhusu wewe lakini hatuziamini!”
 
Khabbab alijibu, “Habari gani hizo?”.
 
“Kwamba umetoka katika dini yako na sasa unamfuata huyu mtu kutoka Banu Hashim”
 
“Sijatoka katika dini yangu ila nimeamini kwamba kuna Mungu mmoja tu na wala hana mshirika, ninayakataa (kuyaabudu) masanamu na ninaamini kwamba Muhammad ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu (SW) na Mtume wake (SAW).
 
Waliposikia maneno hayo tu, Sibaa na kundi lake likamvamia na kuanza kumpiga kwa ngumi, nondo, vyuma mpaka akazirai huku damu zikimvuja kwa wingi.
 
Habari hizi za Khabbab zikaenea Makka nzima hata watu wakashtushwa na msimamo wake huu. Hakukuwa na mtu yoyote miongoni mwa wafuasi wa dini aliyokuja nayo Muhammad aliethubutu kuonesha imani yake wazi wazi na kwa kujiamini.
 
Wakuu wa kiquraysh ndio walioshtushwa zaidi hawakutaraji huyu mhunzi na mtumwa wa Umm Ammaar ambaye hana hata ukoo Makka wa kumlinda, wala nafasi ya (mtu) wa kumzuia asidhurike, kuwa na moyo wa kumkiuka bwana wake (Umm Ammaar) na kuwakataa miungu na dini ya wazee wake wakahisi kwamba huu ni mwanzo tu lakini………
 
Hawakukosea, msimamo aliounesha Khabbab ulikuwa kama changamoto kwani marafiki zake wengi wakaingia kwenye Uislam na wao pia kujitangaza hadharani.
 
Maquraysh wakaamua kufanya mkutano maalumu na ajenda kuu ilikuwa ni Muhammad. Walikuwepo Abu Sufiyan ibn Harb, Al-Walid ibn Al-Mughira na Abu Jahl ibn Hisham. Waliona jinsi Muhammad anavyopata nguvu siku hadi siku na kupata wafuasi kila kukicha.  Walichokiona na kwamba haya ni kama maradhi na yanaenea kwa kasi kubwa sana hivyo lazima yadhibitiwe kabla hayajaripuka.
 
Wakaamua kwamba kila kabila, kuwakamata na kuwaadhibu wafuasi wote wa Muhammad (SAW) mpaka wakubali kurudi katika dini zao au wafe.
 
Sibaa Ibn Abdul-Uzza na ukoo wake ukawaangukia jukumu la kumwadhibu Khabbab. Wakawa wanamchukua na kumpeleka sehemu za wazi wakati wa jua kali na ardhi kuwa na joto kali.  Hapo humvua nguo zake na kumvisha nguo za chuma na kumlaza chini. Jua kali likimchoma kwa juu, ardhi ikiwa na joto kali likimuunguza kwa chini na huku nguo za chuma zikimuunguza ngozi yake mpaka mwili kufa ganzi. Ilikuwa ni adhabu ilioje na kila wakimuona nguvu kumwishia walimjia na kumuuliza,
 
 “Nini unasema kuhusu Muhammad?”
 
“Ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, amekuja na dini yenye mwongozo wa kweli na kututoa katika kiza kutupeleka kwenye nuru.”
 
Sibaa na wenzake walikasirika sana na kuendelea kumpa mateso zaidi. Wakimuuliza kuhusu Laat na Uzza , Khabbab huwajibu,
 
 “Masanamu mawili viziwi na bubu, hawadhuru wala hawanufaishi”.
 
Kwa jibu hili huzidi kuingiwa na hasira na kumwekea jiwe kubwa lenye joto mgongoni mwake. Maumivu yake yalikuwa hayana mfano wake hata hivyo Khabbab hakutetereka wala kubadili msimamo.
 
Ukatili wa Umm Ammaar ulikuwa mbaya zaidi kupita wa kaka yake. Akimuona Mtume (SAW) akizungumza na Khabbab dukani hujawa na hasira na kwenda mwenyewe dukani na kuanza kumtia adabu.  Huchukua chuma kilichookwa motoni tayari kwa kufundwa, kikiwa chekundu na kumchoma kichwani kwa Khabbab! Ni maumivu yaliyoje, mara zote huzimia.
 
Mateso aliyoyapta Khabbab hayakuwa na mtu yoyote kwa kumsaidia. Kilichomsaidia ilikuwa ni sala na dua tu.  Kila siku aliomba kwa Mwenyezi Mungu aondokane na adhabu za Umm Ammaar  na kaka yake. Nafasi pekee aliyoipata Khabbab ni pale waislam walipofanya Hijra na Umm Ammaar hakuweza kumzuia kwani yeye mwenyewe alisibiwa na maradhi hayajawahi kusikilikana.
 
Kichwa kilikuwa kinamuuma na kumgonga na kuwa kama amechanganyikiwa. Watoto wake wakajitahidi kutafuta dawa bila ya mafanikio yoyote mpaka hatimaye kuambiwa hakuna dawa yoyote itakayomsaidia isipokuwa chuma cha moto kwenye kichwa chake!.   Matibabu haya ilibidi yafanyike na maumivu aliyoyapata bibi huyu yalikuwa machungu mno kuliko hata yale maradhi yenyewe.
 
Alipokuwa Madina, Khabbab alipata utulivu wa nafasi yake ambayo hakuwahi kuupata kipindi chote tokea kutekwa mkononi mwa wazazi wake, kuwa mtumwa kuwa chini ya Umm Ammaar mpaka kusilimu kwake Makka. Hakuwa na khofu wala mashaka ya kubughudhiwa wala kukerwa.
 
Alipigana pamoja na Mtume (SAW) vita vya Badr katika vita vya Uhud, alifurahi pale adui wake mkubwa Sibaa alipouliwa na Hamza ibn Abdul-Muttalib.
 
Alijaaliwa maisha marefu na kuona vipi uislam ukienea ulimwenguni chini ya makhalifa wane waongofu.  Aliwahi kumtembelea Umar enzi za ukhalifa wake.  Umar alipomuona,  hakujali kuwepo kwake kwenye mkutano, alisimama na kumsalimia na kusema, “Hakuna mtu mwengine yeyote zaidi yako na Bilali anayestahiki kuwepo katika majlis hii”
 
Umar alimuuliza Khabbab awasimulie machungu aliyokuwa akiyapata wakati akiteswa.  Khabbab aliwasimulia kwa ufasaha kwani bado yalikuwa kwenye kumbukumbu yake na pale alipovua nguo na kuonesha mgongo wake ulivyojaa makovu, Umar alizidi kusikitishwa.
 
Baadaye Khabbab alijaaliwa utajiri ambao hata yeye mwenye hakuutarajia.  Hata hivyo alisifika kwa ukarimu aliokuwa nao. Inasemekana alikuwa akiweka Dirham na Dinar katika sehemu maalum kwenye nyumba yake ambapo wale wote wenye shida na wahitaji wanapajua na walikuwa wanakuja na kuchukua kiasi wanachohitaji bila ya kuomba ruhusa wala kuuliza.
Licha ya yote hayo alielewa fika kwamba mali na utajiri ni neema na fitna (mitihani), alichelea sana mali yake isije ikamponza na kuchunga wakati wa kuigawa.  Wakati akiugua aliwahi kusema, “Hapa kuna Dirham elfu thamanini, wallahi sijazifungia na sijamzuia mtu yeyote mwenye shida (kuchukua).
 
Baada ya kusema maneno hayo akaanza kulia na kuulizwa, “Kwa nini unalia?
Akajibu, “Nnalia kwa sababu masahaba wenzangu wamefariki bila ya kupata malipo kama haya dunia.  Nimeishi na kupata utajiri huu na nnachelea isije ikawa haya ndio malipo yangu kwa yale yate niliyoyatenda”
 
Alipofariki Khabbab,  enzi za ukhalifa wa Ali ibn Abi-Talib, Khalifa alisimama kaburini kwake na kusema:
 
“Mwenyezi Mungu amrehemu Khabbab, aliukubali uislam kwa moyo mkunjufu, alifanya hijra kwa khiari yake, aliishi mpiganaji jihadi na Mwenyezi Mungu (inshaallah) hatozuia malipo ya wale wanaofanya mambo mema.