Asmaa bint Abubakar- dhaati annitaqayn





Asmaa bint Abubakar- dhaati annitaqayn
Asma alikuwa akitoka kwenye ukoo unaoheshimika, Baba yake Abu Bakar alikuwa rafiki wa karibu sana wa Mtume (SAW) na Khalifa wa kwanza baada ya kifo chake. Dada yake Aisha alikuwa mke wa Mtume (SAW).  Mumewe Zubeir ibn Awwam alikuwa mmoja kati ya washauri wakuu wa Mtume Muhammad (SAW). Mwanawe Abdullah bin Zubayr akaja kuwa Sahaba aliesifika kwa ukweli na uaminifu.
 
Asma ni miongoni mwa watu wa mwanzo kusilimu.  Alikuwa ni mtu wa kumi na nane kusilimu na baadaye alipewa jina la utani “Dhati annitaqayn” , likimaanisha mwenye mikanda miwili kwa sababu baba yake na Mtume (SAW) walifanya hijra pamoja. Alikuwa ni miongoni mwa watu wachache waliojua mpango wa Hijra kwenda Madina, mpango huu ulikuwa siri kubwa kwani tayari Maquraysh walishaazimia kumuua Mtume (SAW).  Siku ya safari yao, ni yeye aliyewaandalia chakula chao cha safari pamoja na maji kwa kuwa hakuwa na kitu cha kufungia mikebe ya chakula na maji aliamua kutumia mkanda wake wa kiunoni na hapo baba yake akamshauri aukate mara mbili na kupatikana jina maarufu la (dhati annitaqayn).
 
Asma alikuwa miongoni mwa watu wa mwisho mwisho kufanya Hijra na alifanya safari hii akiwa mja mzito. Hata hivyo safari hii ngumu pamoja na hali yake ya uja uzito havikumzuia kutekeleza wajibu wake.  Walipokaribia Madina katika kijiji cha Quba alijifungua mtoto wa kiume (Abdallah), waislam walifurahi na tukio hilo na kusema “Allah Akbar, Laa Ilaha Ill allah”  Alikuwa mtoto wa kwanza kuzaliwa na waliohajiri katika mji wa Madina.
 
Asma alikuwa mkarimu na mweye busara kufikia hadi mwanawe Abdullah kusema “Sijawahi kuona wanawake wawili walio wakarimu kushinda shangazi yangu (Aisha) na mama yangu (Asma).  Ukarimu wao ulikuwa tofauti, shangazi hukusanya vitu mpaka akiona vinatosha kisha huvitoa kuwasaidia wanaohitaji.  Mama yangu yeye haweki kitu ndani hata cha kutumia kesho”.
 
Licha ya baba yake kuwa tajiri, Asma alikuja kupata taabu baba yake alipohamia Madina kwani hakuacha chochote kwa aila yake .Babu yake Abu Quhafah (hakuwahi kusilimu) kusikia habari hii alikwenda nyumbani kwao na kuwasikiliza, “Nasikia mwanangu hajaacha pesa yoyote  ya matumizi na amekukimbieni”.  “Hapana babu” alijibu Asma, “mbona ametuachia pesa nyingi tu” alimchukua babu yake (alikuwa kipofu) akampeleka pahala wanapoweka pesa ambapo kwa ujanja aliweka changarawe na kuzifunika akamgusisha babu yake, “ona kiasi gani baba ametuachia”  Hakukubali kuchukua msaada kutoka kwa kafiri hata akiwa ni damu yake mwenyewe.
 
Msimamo huu pia aliouonesha kwa mama yake Qutaylah pale alipokuja kumtembelea Madina mama yake hakuwa muislamu na waliachana na baba yake enzi za ujahiliya, alimletea mwanawe zawadi chungu nzima zikiwemo ngano, samli na kadhalika.  Asma alikataa kuzipokea na wala kumruhusu mama yake kukanyaga nyumba yake, alimtumia mtu kwenda kwa bibi Aisha ili amuulize kuhusu msimamo wake huu. Mtume akaagiza ampokee mama yake na apokee zawadi na katika hali hii ndipo pale ilipoteremka aya ya nane na tisa Suuratul Mumtahinah:
 
“Mwenyezi Mungu hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita wala hawakukutoeni makwenu . Hakika M/Mungu huwapenda wanaofanya uadilifu.Hakika M/Mungu anakukatazeni kufanya urafiki na wale waliokupigeni vita na wakakutoeni makwenu na wakasaidia katika kufukuzwa kwenu. Na wanaofanya hao marafiki basi hao ndio madhalimu”
 
Kama ilivyokuwa kwa waislamu waliohamia Madina maisha yalikuwa ya taabu sana mwanzoni na hali hiyo alikuwa nayo bibi Asma na mumewe, mali waliyokuwa nayo ni farasi mmoja waliyenunua, Bi Asma anasimulia.
 
“Nilikuwa nikimlisha farasi majani na maji na kumpuna, nikisaga ngano kutengeneza unga lakini sikuwa mzuri katika kuoka mikate, wanawake wa Kiansari walinipikia mikate, walikuwa wazuri sana.  Nilikuwa nikibeba ngano kutoka kwenye kikataa cha mume wangu alichopewa na Mutme kulima kilikuwa na umbali wa farsakh tatu (kama kilometa nane hivi) kutoka mjini.  Siku moja wakati nnarudi huku nimebeba kizigo changu nikakutana na Mtume (SAW) akiwa na masahaba, aliniita na kunitaka nipande kwenye ngamia wake, sikujisikia vizuri kufuatana na Mtume hasa nikikumbuka kwamba mume wangu ana wivu sana.  Mtume (SAW) alilifahamu hilo na akaendelea na safari yake”  
 
Alipofika nyumbani akamhadithia mumewe na Zubeir akajibu, “Nnaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kiachonikera na kunibughudhi ni wewe kubeba ngano kuliko kupanda ngamia na Mtume Muhammad (SAW).”
 
Bi Asma na mumewe waliishi na kujituma mpaka hali yao ya maisha ikainuka, waliishi kwa maelewano mazuri ingawa baadhi ya wakati mumewe alikuwa mkali.  Hivyo alikwenda kwa baba yake Abubakar kumlalamikia na jibu lake, “Mwanangu jitahidi uwe na subira ikiwa mke atapata mume muadilifu na (mume huyo) kufa bila ya mwanamke kuolewa na mume mwengine basi watakuwa pamoja peponi”
 
Bwana Zubeir baadaye akabahatika na kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa miongoni mwa Masahaba, hata hivyo Bi Asma alihakikisha utajiri haumuathiri na kutoka katika mstari na hata pale mwanawe mwengine Al-Mundhir alipomletea zawadi ya kanzu ya gharama kutoka Iraq, wakati huo tayari ameshakuwa kipofu basi aliishika shika kitambaa na kusema “Mrudishieni mwenyewe” . Al-Mundhir hakufurahishwa na kauli hii na kumwambia mama yake ,“lakini mama si nyepesi hii inayoonyesha maungo.”
Bi Asma akajibu, “Inawezekena si nyepesi lakini inabana na kuonesha (mpangilio wa) mwili”.  Kuona hivyo Al-Mundhir akamnunulia kanzu nyengine inayolingana na mahitaji yake.
 
Tukio la kihistoria ambalo halitokuwa rahisi kusahauliwa ni pale Bi Asma alipokutana na mwanawe Abdullah kwa mara ya mwisho.
 
Abdullah alikuwa miongoni mwa waislam waliokuwa mstari wa mbele kuchaguliwa Khalifa baada ya kufariki Yazid Bin Muawiya. Nchi za Misri, Iraq, Hijaz (Saudia) na sehemu kubwa ya Syria zilimuunga mkono.  Kabila la Banu Ummayya, hawakuafiki uchaguzi huu na wakaanzisha vita wakiongozwa na Hajjaj bin Yussuf Athaqafiy kuhakikisha ukhalifa unabaki kwao.  Vita vilipiganwa huku Abdullah ibn Zubair  akipigana  kwa ushujaa hata hivyo wafuasi wake wengi walishindwa kuendelea na vita na kidogo kidogo walianza kumwacha mkono. Kuona hivyo ikambidi akimbilie Al-kaaba kutafuta himaya. 
 
Wakati huo ndipo alipokwenda kwa mama yake ambaye tayari ni mtu mzima na macho yake kutokuwa tena na nuru na kumwamkia, “Assalam Alaykum warahamatullah wabarakatu mama” . Akajibiwa “Waalaykumu ssalaamu Abdallah” na kumuuliza :
“Nini kimekuleta hapa huku vimondo vinateremka kama mvua kwenye nyumba zetu, na majeshi ya Hajjaj yamewazunguka wanajeshi wako kwenye Al-Kaaba?”  Abdulla akasema, “Nimekuja kuomba ushauri”
Mama yake alishtushwa na kushangaa, “Ushauri wangu? Ehee ! kuhusu nini tena?” akauliza.  Abdullah akasema “Watu tayari wamenitenga kwa kumwogopa Hajjaj au kwa kudanganyika na ahadi alizowapa.  Hata watoto na familia yangu wamenikimbia, tuko kikundi kidogo cha watu ambao wapo pamoja na mimi na hata wakisimama kidete kupigana labda wataweza kufanya hivyo kwa saa au masaa mawili tu.
 
Wajumbe wa Banu Ummayya wanajaribu kuzungumza na mimi wakiahidi kunipa chochote nikitakacho katika ulimwengu huu alimradi niweke silaha chini na kumkubali Abdul-Malik ibn Marwan (Khalifa wanaemtaka Banu Ummayya), “wewe unasemaje”.
 
Mama yake akamjibu, mwanangu! “Haya ni mambo yako, na wewe mwenyewe unaelewa vizuri.  Hata hivyo ikiwa unafikiri haya unayoyafanya kwamba upo katika haki na unasimama kidhati kuusimamia ukweli, basi kakamaa na endelea kupigana kama walivyopigana wafuasi wako na wakauwawa la kama unaitaka dunia, utajiharibia mwenyewe pamoja na kuwaharibia wafuasi wako”.
 
Abdullah akamfahamisha mama yake, “hakuna shaka yoyote ila leo mimi nitauwawa tu”.  “Hilo ni bora zaidi kuliko kusalimu amri kwa Hajjaj binafsi yako na kuwafanya madhalili wa Banu Ummayya wacheze na kichwa chako (baada ya kuuwawa)” mama yake akamjibu.
“Mimi siogopi kufa ninachoogopa ni kuukata kata mwili wangu”.
 
“Hakuna kitu cha kuogopa mwanangu baada mauti, kumchuna ngozi, hakumletei maumivu yoyote kondoo aliechinjwa ”.
 
Kusikia hivyo, Abdullah akawa na furaha na kumwambia mama yake “Mama aliyerehemewa na kuwa na rehema busara zako, nimekuja kwako wakati huu kusikiliza hayo niliyoyasikia, MwenyeziMungu ndiye atakuwa shahidi kwamba si kusimama huku kwa kupata mambo ya kidunia na raha zake isipokuwa nikiwa na hasira kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, mipaka yake imevukwa.  Na Inshaallah ninakwenda kufanya lile litakalokuridhisha hivyo kama nikiuwawa usihuzunike wala kusikitika bali niombee dua kwa Mwenyezi Mungu.”
 
“Nitasikikitia pale tu utakapouwawa pasipokuwa na haki”, alisema mama yake.
 
“Ninakuhakikishia mama yangu, mwanao hakuwahi kuunga mkono udhalimu kwa muislam na   waliopata hifadhi ya waislam na kuishi katika nchi za kiislam ilhali wao wenyewe si waislamu, wala kuunga mkono jambo lolote lisilokua la haki, na ninasema haya si kwa kujitakasa, Mwenyezi Mungu anajua kwamba nnasema haya kwa kuupa nguvu moyo wangu kuweza kusimama kidete.”
 
“Alhamdulillah, ambaye amekupa moyo wa kuyafanya yale ambayo ameyaridhia na yale ambayo nimeyaridhia mimi, njoo karibu yangu mwanangu nisikie harufu ya mwili wako na kuugusa kwani buriani sidhani kama tutakutana tena”
 
Abdullah akainama na kukumbatiana na mama yake akimiminiwa mabusu, mikono ya mama yake ikaanza kumbana ghafla kuachia “nini umevaa?”
 
“Nguo zangu za chuma” alijibu Abdullah.
 
Mama yake akamwambia “Hizi mwanangu si nguo za mwenye kutaka kufa shahidi zivue na uvae suruali kwani ukija kuuwawa utupu wako usije kuonekana.”
 
Abdullah akavua zile nguo zake za kivita na kuvaa suruali na kuanza kurudi Haram kuungana na wapiganaji wenzake haku akimsisitiza mama, “Usinisahau kwa dua mama”
 
Akinyanyua mikono yake kuelekea mbinguni akaomba “Ewe Mola wangu nnakuomba umrehemu na kumpa uwezo wa kusimama kwa muda mrefu na umpe uwezo wa kuwa na kilio kikubwa usiku wakati watu wamelala.”
 
“Ewe Mola wangu nnakuomba umrehemu kwa njaa na kiu yake aliyokuwa akiikabili katika safari zake za Makka na Madina ilhali amefunga”
 
“Ewe Mola wangu mpe rehma katika uadilifu wake kwa mama na baba yake”
 
“Ewe Mola, ninamkabidhi katika kupigania dini yako na niko radhi naye kwa lolote utakalomjaalia na umlipe kwa ajili yake, malipo ya wale waliokuwa na subira na stahamala”
 
Ilipofika jioni, Abdullah alikwisha fariki na kufuatiwa na mama yake aliyekufa siku kumi baada yake. Uzee haukumondolea hata kidogo busara na hekima alizokuwa nazo.