Fayruz
Ad-Daylami-muuaji wa al-Aswad mkadhibishaji
Mtume Muhammad (SW) aliporudi Madina baada ya kutekeleza
Hijjatul Widaai (hija ya kuaga) alianza kuugua, habari za kuugua kwake
zikaenea bara arabu yote na waislam wa kweli kusikitishwa sana na kwa wengine
wakaiona hii kama ni fursa ya kuonesha misimamo yao halisi dhidi ya Uislam na
Mtume. Kwani lile chaka la unafiki walilojivika nalo halikuwa na haja
tena.
Huko, Al-yamama Musaylamah mnafiki na muongo akuaukana
uislam. Katika mji wa Asad, Tulayhah al-Asadiy akartadi na Yemen Al
aswad al Ansi nae pia akartadi. Wazandiki hawa watatu hawakuishia hapo bali
nao wakadai kwamba ni mitume wametumwa na Mwenyezi Mungu kwa kaumu zao kama
alivyokuwa Muhammad (SAW) alivyotumwa kwa maquraysh.
Al-Asad alikuwa mwana mazingaombwe Hata hivyo, alijaaliwa kuwa
na kipaji cha kusema na kuweza kuwadanganya watu kwa yote ayakayoyasema.
Alikuwa na uwezo na nafasi katika jamii yake aliweza kuwavuta watu wa aina
zote matajiri, masikini, wakubwa, wadogo, wanawake na wanaume. Na
alikuwa na kawaida ya kuvaa “niqaab” kizoro kuficha uso wake na kuwazidishia
watu kumshangaa na kupumbaa.
Katika mji wa Yemen siku hizo, ukoo wa Abna ulikuwa ni moja
katika koo maarufu na kutajika sana. Abna ni mchanganyiko wa waajemi
waliokuwa wakitawala Yemen ambao waliwaowa waarab wa kiyemen na kuchanganyika
nao. Feyruz Ad-Daylam alikuwa ni mmoja wa hawa waabna.
Wakati wa kuja Uislam, Yemen ilitawaliwa na Wa-abna na Badhan
alitawala Yemen kwa niaba ya Waajem1 wa kichosroes. Badhan aliposikia habari
za Uislam zilimuingia vyema na kuzikubali pamoja na kumkubali Mtume (SAW) na
risala yake.
Alijitenga na Wachosroes na kuingia Uislam na wafuasi wake wakamfuata
na kuingia Uislam kwa wingi. Mtume (SAW) akampa heshima ya kuendelea
kutawala Yemen mpaka kufariki kwake muda mfupi kabla ya kuibuka kwa al-Aswad
al-Ansi.
Ukoo wa Al-Aswad-Banu Mudh-hij- walikuwa wa kwanza kuukubali
“utume”wa al-Aswad. Akiungwa mkono na kabila lake lililokuwa na nguvu
al Aswad alianza kuvamia miji ya karibu na kuanzia Sanaa ambako akamuua
mtawala wake, Shah ibn Badhan na kumtwaa mkewe kwa nguvu. Akaendelea kuvamia
miji mengine mpaka maeneo kutoka Hadhramawt mpaka Taif na kutoka Al-Ahsa
mpaka Aden yakawa chini yake.
Al-Aswad alikuwa mjanja na mwerevu sana kuweza kuwadanganya
watu na kuwatapeli kwa mbinu aina kwa aina. Alidai kwamba alitembelewa
na Malaika na kumteremshia wahy na kumpa bishara ya kuweza kuwajua watu na
mambo yao. Kilichomsaidia ni mashushushu aliokuwa nao kila pembe ambao
humletea habari zao, matatizo, siri, matarajio na wasi wasi wao.
Kwa mbinu hii akija mtu kwake na kuelezwa yale aliyokuwa nayo
vile vile yalivyo hushangazwa sana na kuzidi kuchanganyikiwa na kumkubali.
Alipata wafuasi wengi kwa ujanja wake huu.
Habari za al-Aswad, kurtadi na kudai utume zilipomfikia Mtume
Muhammad (SAW), alituma ujumbe wa masahaba kumi wakiwa na barua rasmi, kwa
masahaba wa Yemen ambao alikuwa akiwaamini. Akawahimiza kuikabili fitna hii
ya Al-Aswad na kuzidisha imani. Pia akawaamrisha wamuondoshe Al-Aswad
kwa njia yoyote ile.
Wote waliobahatika kupata barua za Mtume (SAW) walianza mara
moja kupanga mbinu za kuikabili fitna. Mmoja wapo wa watu hawa ni
Fayruz. Fayruz mwenyewe anaeleza:
“Mimi na wa-Abna waliokuwa pamoja na mimi hatukuwa na shaka
hata mara moja kwa dini ya Mwenyezi Mungu. Hakuna imani yoyote katika
maadui wa Mwenyezi Mungu iliyoweza kutuingia katika nyoyo zetu bali
tulisubiri na kutafuta wakati mwafaka wa kumkamata Al-Aswad na kumpoteza kwa
njia yoyote”. Aliendelea kusema, “Na tulipopata barua kutoka kwa Mtume
Muhammad (SAW) ilituzidishia imani yetu na kutupa nguvu zaidi na kila mmoja
wetu akawa na ari kwa lile atakalolifanya.”
Baada ya kupata mafanikio katika mpango wake, jeuri na kiburi
vikamuingia Al- Aswad mpaka akawa anaanza kumuonea choyo kamanda wake
mwenyewe wa majeshi, Qays ibn Yaghuth na aliwahi kumwambia anaonekana kuwa na
nguvu sana. Qays alihisi moja kwa moja kwamba usalama wake uko hatarini
hasa baada ya kuona mahusiano yake na Al-Aswad hayakuwa mazuri.
Anaendelea kusimulia Fayruz, “tukatoka mimi na bin ami yangu
Dadhaway na kwenda kwa Qays. Tulimfahamisha kuhusu ujumbe wa Mtume (SAW) na
tukamuomba ajumuike nasi tumfanye ‘asusa’ al-Aswad kabla ya al-Aswad
hajamfanya yeye Qays ‘asusa’. Alitukubalia na kuanza kutupa baadhi ya
siri za al-Aswad.
Sote watatu tulikubaliana kukabiliana nae chini kwa chini
kwani tulikuwa karibu naye na wenzake wengine kukabiliana nae kwa njia
nyengine, tukielewa kwamba Dadha (Al-Aswad alimchukua kwa nguvu na baadaye
kumuua mume wake) bin ami yetu nae pia angelituunga mkono. Tulikwenda kwake
na Fayruz kumwambia Dadha, “ewe bin ami, umeona madhara na ubaya wa huyu mtu
aliyoyafanya kwako na kwetu. Amemuua mumeo na kuwadhalilisha wanawake wote wa
ukoo wako, amewauwa waume zao na kuwanyang’anya madaraka.”
“Hii ni barua kutoka kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu (SW), kwetu
sisi hasa na kwa watu wa Yemen kwe ujumla katutaka tuiondoe fitna hii.
Je! uko tayari kutusaidia?”Akauliza, “vipi nnaweza kusaidia?”Feyruz akajibu,
“kumfanya aukimbie mji……….au hata kumuua.”
“Wallahi”, akasema Dadha, “mawazo yangu yote yako huko
kumuua”. Aliendelea, “ila niliogopa kushauri hilo. Sijawahi kumuona mtu mbaya
na mkatili kuliko huyu (al-Aswad), na Mwenyezi Mungu (SW) hajamuumba mtu
mwengine anayechukiza zaidi yake isipokuwa shetani na nnaahidi kwa Mwenyezi
Mungu (SW) aliyemtuma Mtume Muhammad (SAW) kutuamrisha mema na kutukataza
mabaya, mimi sikuwa na shaka hata kidogo katika dini yangu”
Fayruz akauliza, “sasa vipi tutammaliza?” Baada ya kufikiri,
akasema Dadha, “huyu mtu ana ulinzi wa hali ya juu. Hakuna hata sehemu
moja katika kasri yake hapajazungukwa na walinzi, ila kuna chumba kimoja
kibovu na kimeelekea nje siku ya tatu tokea leo usiku, nendeni kwenye chumba
hicho mtakuta silaha na mimi nitawasubiri…….”
Lakini Fayruz akalalama na kusema, “kupita kwenye kasri lenye
ulinzi mkali mpaka kufika kwenye hicho chumba bila ya kuonekana na walinzi
haitokuwa kazi rahisi.”
Dadha akajibu, “ni kweli lakini nina wazo”. Aliendelea,
“mtumeni mtu kesho ambaye mnamuamini aje kama mfanyakazi, nitamfahamisha
atengeneze njia kwenye chumba ya kuweza nyinyi kupita kwa urahisi” “Sasa
umesema, hilo ni wazo zuri”, akamalizia Fayruz.
Tukaenda kujiandaa na kuwafahamisha waumini wengine waliokubali kutusaidia
nao pia wajiandae kwa ajili ya vita na tukawapa aina ya ishara tutakayotumia
kuashiria kuanza kuvamia. Ulipoingia usiku na wakati kufika tulienda mimi na
wenzangu wawili mpaka kwenye chumba tulichofahamishwa na kuingia ndani ya
kasri. Tukakuta silaha na kuzichukua tukielekea chumba cha adui wa
Mwenyezi Mungu. Tulimkuta bin ami yetu Dadha akitusubiri na kutuonesha chumba
alicholala Al-Aswad na tukaingia. Tulimkuta amelala fofofo huku
akikoroma. Fayruz akatoa upanga na kumkata shingo yake kwa pigo mmoja tu na Al-Aswad
kutoa mayowe kama fahali la ng’ombe linapochinjwa.
Walinzi waliposikia mayowe yale wakakimbilia chumba cha
Al-Aswad na kumkuta Dadha mlangoni na walipomuuliza, “ kulikoni”, aliwajibu,
“msiwe na wasi wasi, mnaweza kwenda, mtume wa Mwenyezi Mungu anapokea Wahy”.
Kusikia kauli hii kutoka kwa mkewe walinzi hawakushughulika na wakaondoka
kuendelea na lindo.
Ilipofika alfajiri, Fayruz akasimama kwenye ukuta wa kasri na
kuanza kuadhini, “Allah Akbar, Allah Akbar na kuendelea mpaka alipofika
Ash-hadu anna Muhammad Rasul Lllah! Kisha akaongeza Wa ash-hadu annal Aswad
al Ans kadhaab!” na nnashuhudia kwamba Al-Aswaad ni muongo!
Hii ndiyo ilikuwa ishara waliyokuwa wakiisubiri wapiganaji
jihadi wa kiislam waliokuwa nje wakisubiri. Wakaanza kulivamia kasri kila
pembe na kuwapiga walinzi. Kwanza walinzi walishtushwa na adhana ndani ya
kasri, halafu wakasikia takbira ‘Allah Akbar’ za waislam zikitokea kila
kona.Wakaanza kukimbia wasijue la kufanya huku wanajihadi wakiwavamia.
Kulipopambazuka vita vilikwishamalizika na asubuhi yake tu
Fayruz na masahaba wengine wakaandika barua yenye habari njema kwenda kwa
Mtume (SAW) Madina, habari ya kuuwawa kwa mkadhibishaji na muongo mkubwa
al-Aswad.
Kwa bahati mbaya ujumbe ulipofika Madina wa barua, wakakuta
tayari Mtume Muhammad (SAW) amefarika usiku wake tu! Hata hivyo
walifahamishwa kwamba Mtume (SAW) aliteremeshiwa wahy kufahamishwa kuuwawa
kwa Al-Aswad siku ya tukio lilipotokea.
Miaka ikapita na Khalifa Umar ibn Al Khattab alimuandikia
barua Fayruz, “nimepata habari kwamba umeshughulika na kula mkate na asali
(akimaanisha hakuwa na harakati zozote). Itakapokufika barua hii
tafadhali uje na kwa rehema zake Mola, kujumuika nasi katika njia ya Mwenyezi
Mungu.
Fayruz akatekeleza amri ya Amirul muuminiin na kwenda Madina.
Alipofika akaomba kuonana na Umar na kuruhusiwa. Kulikuwa na watu
wengine pia wakitaka kumwona. Akatokea kijana wa kikuraysh na kumsukuma
Fayruz na kutaka kuingia ndani. Fayruz akampiga yule kijana na
kumuumiza kwenye pua. Kijana alipofika kwa Khalifa na alipomuona tu
akamuuliza:
“Ni nani aliyekupiga?” Akajibu kijana “ Fayruz, yuko mlangoni”
Fayruz akaingia na Umar akamuuliza, “Fayruz nini tena hiki?” Akajibu, “Yaa
Amirul Muuminiin uliniandikia barua na wala huyu kijana hukumuandikia, uliniruhusu
niingie na wala hukumruhusu na alitaka kuingia kabla yangu, kisha nikafanya
kama ulivyoambiwa.”
Umar akatoa hukumu pale pale, “kisasi!” akimaanisha maadam
Fayruz amempiga yule kijana basi na yeye apigwe. Fayruz akauliza, “kwani ni
lazima hicho kisasi?” Umar akajibu, “ni lazima”
Fayruzi akainama na kuweka magoti yake chini na kijana
akajiandaa kurudisha lile pigo alilopigwa pale puani. Wakati
akijitayarisha kupiga, Umar akamwambia, “hebu subiri kidogo kijana!
Ngojea nikwambie kitu ambacho nilisikia kwa Mtume (SAW). Nilimsikia
jioni moja akisema,” “usiku huu al-Aswad al-Ans aliedai kuwa ni mtume
ameuwawa. Fayruz Ad-daylami muungwana na muadilifu amemuua” Kisha Umar
akamuuliza yule kijana, “bado unajihisi kulipiza kisasi baada ya kusikia yale
niyoyasikia kwa Bwana Mtume Muhammad (SAW)? Kijana akasema, basi nimemsamehe
baada ya kuniambia haya maneno, kutoka kwa Mtume wa Allah (SW).
Fayruz hakuridhika bado na kumuuliza khalifa, “hivi unafikiri,
kusalimika kwangu huku ni kwa mimi kukiri kosa na kwamba msamaha wake haukuja
kwa kurubuniwa?”
“Naam”, Umar akajibu
“Nnakuzawadia upanga wangu, farasi wangu na elfu thelathini
katika fedha zangu kama zawadi kwako”,akamwambia yule kijana.
Amirul muuminiin akapendezwa sana na tukio hili la Fayruz,
ghafla kuwa hasira na papo papo kuwa takrima na kumwambia yule kijana wa
kiquraysh, “unaona msamaha wako umezaa matunda, tayari uko tajiri sasa hivi.”
|
Fayruz Ad-Daylami-muuaji wa al-Aswad mkadhibishaji
Subscribe to:
Posts (Atom)