KUELEKEA QIBLAH – SHARTI YA KUSIHI SALA



KUELEKEA QIBLAH – SHARTI YA KUSIHI SALA


ABU AMMAAR

Moja katika jambo linalowatia mtihani baadhi ya waislamu hasa tunaoishi hapa Uingereza ni upande wa Al Ka’abah Unaweza kufika kwenye nyumba na kuuliza Qiblah kipo wapi na kupatiwa pande mbili au tatu tofauti. Na kwa baadhi ya nyumba ambazo hufahamishwa Qiblah kilipo unapojaribu kuuliza vipi mmefikia kukipata Qiblah; jibu linaweza kuwa ni la kukisia na hakuna jitihada yoyote ya ziada iliyotumika au vigezo sahihi katika jitihada hii.

Tatizo hili pia hutukumba wakati tupo safarini, makazini na sehemu nyengine kuweza kufikia waislamu kusali sala tofauti kwa kila mmoja kujitahidi  kwamba huku nilikoelekea ndio Qiblah.

Tatizo hili linakuwa gumu kwa kuweza pia kukataliwa vipimo vya kisasa - dira (compass) kwamba si sahihi na zinapotosha badala ya kutoa muongozo sahihi na hivyo waislamu kutumia vipimo vya kienyeji zaidi katika jitihada hii. Wenye kauli hii wanatoa ushahidi wa jinsi  dira inavyokuwa na tatizo linalosumbua. Inaweza kukupa mielekeo tofauti kwa kutegemea eneo iliyowekwa na kuathirika na vitu vyengine kama vyumavyuma(metallic objects) na fanicha/samani. Hivyo kuikataa kabisa.

 Ninaamini wengi wetu tumewahi kukutwa na hali hii. Tatizo jengine la Dira ni jinsi ya kuitumia. Licha ya kupewa miongozo (directives) bado wengine  huweza kuitumia kimakosa na hivyo kuweza kupata Qiblah kimakosa.

Kwa uoni wangu mfupi (Wallahu A’alamu) suala hili naona kama halijapewa umuhimu wake unaostahili miongoni mwetu kwani ni suala muhimu na zito la kuweza kuzifanya sala  zisihi au kutosihi. Kwa bahati nzuri tulipotoka (Afrika) hatukuwa na tatizo hili takriban kila muislamu anajua wapi Qiblah na inawezekana kwa wengine kutolichukulia kwa uzito kwa msingi huu. Lakini tulipo(Uingereza) hili limekuwa tatizo na linahitaji kushughulikiwa ipasavyo. Inaweza kushangaza kuona ulimwengu umeendelea kwa kiasi kikubwa na kutuwezesha waislamu kuweza kujua Qiblah chetu kwa urahisi kwa kutumia zana za kisasa kama ramani, dira, kompyuta (maps, compass, computers) n.k. lakini bado tunalo tatizo hili ni jambo kidogo linatia mtihani. Inawezekana hizi ni juhudi za shetani kututia mashaka na wasiwasi kwenye sala zetu ili ziweze kuharibika na yawezekana pia ni kwa kutolipa suala hili umuhimu unaostahili.

Kuelekea Qiblah ni sharti  miongoni mwa  masharti ya  kusihi Sala .

Kwa hivyo ni wajibu kwa kila muislamu anaetaka kusali kuhakikisha kwamba ameelekea Qiblah kabla ya kuanza kwa sala .Na kama ataelekea kwengineko basi sala yake ni batili. Kusihi /kutosihi kwa sala kunategemea kukamilishwa kwa masharti yote na ikiwa mojawapo halijatimizwa, sala huwa haijatimia.
Anasema Allah(Subhaanahu Wata’ala) katika Qur’aan Suuratul Baqarah /144

                فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّواْ وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ

Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo

 روى الترمذي من حديث أبي هريرة أن النبي صلى الله عليه وسلم قال :   
                               ما بين المشرق والمغرب قبلة " .
       تعليقه على "مشكاة المصابيح" وقال : حسن صحيح . وحسنه الألباني في ( 

Imesimuliwa na Attirmidhiy kutokana na Abu Hurayrah Allah amuwie radhi kwamba Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema:

“ Baina ya mashariki na magharibi Qiblah”
  
Hadithi Hasan sahihi na Sh.Albani anasema ni Hasan katika maelezo yake kwenye Mishkaatul Masaabiih

Ikumbukwe kwamba Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) alikuwa akiishi Madina(wakati huo) na riwaya hii iliwahusu zaidi wakaazi wa  mji wa Madina .

Hivyo kwa yule mwenye kuiona Al Ka’abah atatakiwa kusali akiielekea na kwa yule aliekuwepo mbali na Al Ka’abah ataelekea kwa mujibu wa alama zilizowekwa. Na Maulamaa wamejitahidi kutuwekea alama tofauti za kutuwezesha kujua Al Ka’abah. Kwa mtu akitaka kujua mwelekeo itambidi atumie njia mbili kuu. Ima atumie vipimo au kutumia mahesabu.


Utaratibu wa kukitafuta Qiblah

1             Takriban kila nchi ina utaratibu wa kukipata Qiblah basi ni wajibu kwa kila muislamu anaeishi hapa kuutafuta na kuufahamu utaratibu huu. Pia kama kuna msikiti karibu hicho ni kigezo madhubuti cha kukusaidia.
2             Ikishindikana hatua ya pili ni kutumia jitihada na  huanzia kwa kuuliza wenyeji kama wapo na wanaaminika. Na kauli yao ni ya kufuatwa kuliko jitihada  binafsi kwa sababu wao ndio wanaoelewa zaidi mazingira yao.
3             Kama hakuna wenyeji au wapo lakini si wa kuaminika ni kutumia jitihada binafsi kama ifuatavyo:


A.  Njia iliyo rahisi kabisa ni kutumia ramani kwa kuchora mstari ulionyooka kwenye ramani kutoka mji uliopo hadi Makka, Saudi Arabia. Au kwa kuchora mstari ulionyooka  katika mji uliopo kwa kulinganisha na msikiti ulio karibu – angalia ramani kama mfano(kwa bahati nzuri kila mji hapa U.K una ramani yake hivyo inaweza kutumika).

Njia hii ni rahisi kutumika na inaweza kukupa Qiblah kwa urahisi na takriban kiuhakika. Kwa sababu tukiwepo Uingereza, Makkah inakuwa Kusini Mashariki lakini kwa kumili (kuzidi) Mashariki zaidi kuliko Kusini. Tofauti na tukiwepo Tanzania, Makkah huwepo Kaskazini kwa hivyo tukitaka kujua Al Ka’abah   kwa hapa Uingereza ni kuutafuta upande wa Kusini Mashariki.






{mosimage}

Tukiangalia mfano huu wa ramani ya mji wa Northampton, mistari iliyochorwa inaonesha upande wa Al Ka’abah kwa maeneo tofauti  ukichukua vigezo vya misikiti iliyo karibu. Upande wa juu ni Kaskazini, chini kusini, kulia mashariki na kushoto magharibi tunaona mweleko wa Al Ka’abah uko Kusini Mashariki.




 
{mosimage}





B.        Kutumia Dira (Compass)

Dira hizi huwepo kwenye baadhi ya misala , baadhi ya saa na pia kwenye mikebe maalum – angalia  picha. Na zimetengenezwa  kwa ajili ya kujua mwelekeo wa Al Ka’abah. Huwa na mishale miwili, mmoja unaozunguka huonesha Kaskazini mara zote na mwengine huonesha Al Ka’abah ambao hauzunguki, baada ya kutumika kipimo kilichowekwa kwa mujibu wa nchi uliyo. Kwa kila nchi imepewa kipimo cha nambari kwa mujibu wa sehemu ilipo.  

Kwa mfano Uingereza kipimo chake ni 25 au 250 hivyo utatakiwa ule mshale unaozunguka uwepo kwenye namba 25 au 250, kisha kuangalia ule mshale mwengine usiozunguka unakuonesha upande gani. Upande ulipo mshale huu ndio Al Ka’abah (wengine kimakosa huchukua ule upande ulio mshale unaozunguka). Kwa Tanzania ambayo kipimo chake ni 39 au 390 Kwa bahati nzuri mishale hii miwili hukutana hivyo kufanya Al-Ka’abah ni kukutana kwa mishale hii (hili pia limewatatiza baadhi ya waislamu wakitaraji na hapa Uingereza mishale hii ikutane ili kujulikane Qiblah).

Hata hivyo katika matumizi ya dira ni vyema kupima angalau kwa sehemu mbili hadi tatu tofauti ili kuwe na uhakika kwa sababu ya kuathirika na vyumavyuma kama tulivyoeleza hapo juu.

C.        Kwa kutumia mwelekeo wa Dishi/Sahani/Kawa (Dish) la Sky.

Kipimo hiki ni cha kienyeji lakini kama mtu ameshindwa kabisa  kujua mwelekeo wa Al Ka’abah anaweza kuangalia  lilipoelekea Dishi la Sky kwani imethibitika mwelekeo wake unakaribiana na mwelekeo wa Al Ka’abah hivyo kuwa ni moja katika jitihada kwani anaweza kufika muislamu sehemu hana  ramani  wala  dira hivyo kumwia vigumu kujua Al Ka’abah. Kigezo hiki kinaweza kutumika.

Na pia inawezekana kutumia vigezo vyote villivyotajwa hapo juu kwa pamoja ili kupata uhakika zaidi.

Faida

1             Ikiwa mtu atasali baada ya kujitahidi katika kutafuta Qiblah na akategemea vigezo vilivyowekwa kisha ikambainikia kwamba alikosea basi hana wajibu wa kuirudia sala. Sala  itakuwa sahihi kwa mujibu wa makubaliano ya Maulamaa.
2             Na kama muislamu aliposali alielekea Qiblah lakini akazidi  kidogo upande usiokuwa wa Al Ka’abah. Kuzidi huku pia hakubatilishi sala. Kwani kilichotakiwa ni kuelekea Al Ka’abah na kama kumepatikana japo kidogo basi tayari sharti imetekelezwa.Kwani ni vigumu kuitekeleza sharti hii kikamilifu kwa mtu aliekuwepo mbali na Al Kaa’bah.
3             Na Muislamu akisali upande usiokuwa Al Ka’abah lakini kwa jinsi alivyojitahidi kwa vigezo vilivyotajwa kwamba kule alikoelekea ni Al Ka’abah. Pia sala yake itakuwa sahihi ila ikimbainikia kwamba alikosea kwa jitihada hii  basi atakuwa na wajibu na kuachana na jitihada yake ya zamani na kufuata hii mpya.

Wallahu A’alamu