Katika
vigezo vya kuviangalia katika kujifunza elimu ya dini.
1
Kutokuwa na pupa.
Muislamu hujifunza na kufundishwa
pole pole na kwa ya uwezo wake na hali yake. Anasema Ali ibnu Abi Talib Allah
amuwie radhi katika Hadithi mauquuf (ambayo haikutajwa Mtume Salla Allahu
‘Alayhi wasallam imesita kwa sahaba tu) ilivyopokewa na Bukhari katika mlango
wa kubagua katika elimu nani wa kumsomesha na wa kutomsomesha kuogopea kutofahamu
kwamba:
حدثوا الناس بما يعرفون،
أتحبون أن يكذب الله ورسوله
Zungumzeni(elimisheni) na watu kwa yale wanayoyajua kwani
mnapendelea kukadhibishwa Allah na Mtume wake?
Kujifunza
pole pole na kwa mpangilio humsaidia mwenye kutafuta elimu kufahamu
aliyofundishwa kwanza kabla ya kupata maelezo ya kina. Vyenginevyo athari zake
zinaweza kuwa kama alivyosema mmoja katika mataabi’i Azzuhriy pale aliposema:
جُمْلَةً فَاتَهُ جُمْلَةً
مَنْ طَلَبَ الحَدِيثَ
Mwenye kuitafuta hadithi zote kwa mpigo basi hupitwa na zote kwa
mpigo.
Kwanza
ni vizuri kupata msingi kwa kusoma vitabu vidogo vidogo kabla ya kuendelea na
vitabu vikubwa.
2
Kutazama unapoitafuta na kuichukua
elimu
Mwenye kuitafuta elimu anapaswa
kuangalia vizuri wapi anaipata elimu hii. Hili limekuwa suala muhimu katika
ulimwengu wetu wa leo kwa jinsi elimu ilivyoenea. Si kila linaloandikwa au
kuzungumzwa kuhusu uislamu ni elimu na pia kuwa na tahadhari kama alivyosema
Imaam Muhammad ibn Sireen Allah amrehemu:
"Hii ni elimu ya Dini, kwa
hivyo kuwa muangalifu ni kutoka kwa nani unaichukua Dini yako."
3
Kuitafuta kutoka vyanzo vilivyo na uhakika
Elimu
tuliyonayo inakuja katika hali tofauti. Enzi za zamani tulikuwa tukimtegemea
sana Ustaadh au Mwalimu kutufundisha. Enzi hizi nafasi ya kusoma kutoka kwa
walimu imekuwa ndogo sana na hivyo kutegema elimu kutoka katika vyanzo ambavyo
vinahitaji utafiti kwanza kujua uhakika wake kama mitandao,tovuti, televisheni,
kaseti, Dvds na kadhalika.
Walimu
wamegawika aina mbili walimu wadarisishaji na na walimu watendaji. Mdarisishaji
ni mwenye kuelimisha bila ya yeye mwenyewe kuathirika nayo na hivyo
kutoyatekeleza yale anayoyafundisha. Mwalimu mtekelezaji ni mwenye kufundisha
na kuonekana athari ya elimu yake katika mwenendo na murua wake,vitendo na
tabia zake, kauli na matamshi yake. Walimu wa aina hii hujulikana kama
Rabbaaniyiin – walimu walezi. Kwani tukichukua elimu kutoka kwa walimu wa aina
hii hufaidika kinadharia na kivitendo. Tofauti na mwalimu mdarisishaji ambae
husomesha bila ya kuathiri. Kigezo hichi alikuwa nacho Mtume wetu kama pale
bibi Aishah Allah amuwie radhi alipowahi kuulizwa kuhusu tabia ya Mtume صلى الله عليه وسلم
akasema
tabia yake ilikuwa (kama) Qur’aan.
Kutegemea
nyenzo za kisasa katika kujielimisha pia tunatakiwa tuwe na uhakika na nyenzo
hizo kama ni za kutegemewa au laa. Makala yaweza kuonekana ni nzuri lakini
kumbe chanzo chake si cha uhakika. Dvd yawezekana kuwa ni maridadi na mhadhiri anazungumza
kimahiri lakini kauli zinazotoka kwake zina mushkeli.
4
Kujiepusha na tofauti za Maulamaa
Kwa
mwenye kuanza kutafuta elimu lengo ni kuwa na maarifa na si kujua Sheikh fulani
kasema kitu gani na sheikh huyu mbona kasema hivi. Daraja hii si kwa wanaoanza
na wale ambao bado msingi wao wa elimu ni mdogo. Ikiwa msingi wa kuanzia ndio
huu basi lengo hapa huwa si kutafuta elimu bali ni kujitapa mbele ya Maulamaa
na kushindana nao au kujilabu mbele ya wasiokuwa na elimu na kuwabeza. Mwenye kutafuta
elimu hujifunga katika fani moja au mbili mpaka aielewe vilivyo na si busara
katika hali – mustawaa – huu kujaribu kupitia vitabu tofauti kwani si wakati
wake. Au kuanza kutafuta tofauti kati ya Maulamaa na kuanza kuwatia dosari na
makosa na kuwapongeza wengine.
Elimu yetu ya dini imegawika sehemu mbili. Kwanza ni elimu
wanayopaswa kusomeshwa waislamu wote kwa ujumla kwani hakutokuwa na madhara
yoyote endapo itasomeshwa. Na kila mtu ataipokea atasikiliza na kunufaika nayo.
Na elimu nyengine ni maalum kwa waliokuwa na upeo miongoni mwa waislamu. Elimu
hii kufundishwa kwake huenda kukaleta madhara zaidi kuliko faida mpaka mwenye
kuitafuta afikie sifa za kuweza kuifahamu vyema na kuweza kujua wapi pa
kuitumia na wapi isitumike..
Kuna baadhi ya mas-ala katika elimu yetu ya dini
huwa si busara kuwekwa wazi au kujadiliwa kwa mapana na marefu kwani
kufanyika hivyo kunaweza kuleta madhara na fitna kuliko
faida.