13. SURAT AR-RAA'D

  الرَّعْد

13. SURAT AR-RAA'D

(Imeteremka Madina)


"Surat Ar Raa'd" ni Sura ya Madina, na imeitwa "Raa'd" kwa kusimuliwa kwamba Radi (inamsabihi) inamtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hisabu za Aya zake ni arubaini na tatu. Imeanza Sura hii kwa kubainisha cheo cha Qur'ani Tukufu, na kwamba imeteremshwa kwa Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kisha ikabainisha uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ulimwengu wote, na ikazindua kueleza mambo yaliyo umbwa na yenye manufaa. Kisha ikatoka kubainisha uwezo wake Mwenyezi Mungu wa kuumba, ikaingia kubainisha uwezo wake kurejesha tena na kufufua, na ujuzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu wa kila kitu, na kubainisha kudra yake ya kuadhibu duniani, na kwa hivyo yaweza kukisiwa adhabu ya Akhera. Kisha Sura hii ikaelekeza nadhari zizingatie maajabu ya ulimwengu yaliyo zagaa. Baada ya hayo Mwenyezi Mungu Mtukufu amezieleza hali za watu katika kupokea kwao uwongofu wa Qur'ani. Kisha akataja sifa za Waumini katika makhusiano yao ya kibinaadamu, na tabia za makafiri na karaha yao kushikilia kutaka miujiza isiyo kuwa hii Qur'ani juu ya ubora wake wa cheo, na ikataja kejeli zao kwa Mtume wao. Na ikamueleza Mtume kuwa Mitume wa kabla yake pia walifanyiwa kejeli! Na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kusimamia vitu vyote na nafsi zote, na kwamba Yeye ni Mwenye kumlipa kila mtu kwa anavyo stahiki, na kwamba Qur'ani ndio muujiza mkubwa  kabisa utakao baki mpaka Siku ya Kiyama, na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye anaye wapa nguvu Mitume wake kwa miujiza aitakayo. Na ikiwa hao washirikina wanakanya Utume wa Nabii huyu, basi Mwenyezi Mungu Mwenyewe anashuhudia ukweli wake, na Yeye ni Mwenye kutosheleza kwa hayo.
 



بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ


المر ۚ تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ ۗ وَالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ﴿١﴾
1. Alif Laam Miym Raa. Hizo ni Aayaat za Kitabu. Na yale yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka kwa Rabb (Mola) wako ni haki; lakini watu wengi hawaamini.


اللَّـهُ الَّذِي رَفَعَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُم بِلِقَاءِ رَبِّكُمْ تُوقِنُونَ ﴿٢﴾
2. Allaah Ambaye Ameinua mbingu bila ya nguzo mnaziona; kisha Istawaa (Yuko juu kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah) juu ya ‘Arsh.  Na Akavitiisha jua na mwezi, vyote vinakwenda (na kuendelea kuzunguka) kwa muda maalumu uliokadiriwa. Anadabiri mambo, Anazifasili Aayaat (za Qur-aan, ishara za kilimwengu) ili mpate kuwa na yakini (kuhusu) kukutana na Rabb (Mola) wenu.


وَهُوَ الَّذِي مَدَّ الْأَرْضَ وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنْهَارًا ۖ وَمِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ جَعَلَ فِيهَا زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ ۖ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٣﴾
3. Na Yeye Ndiye Yule Aliyetandaza ardhi na Akajaalia humo milima na mito, na katika kila (aina ya) mazao Amejaalia humo jozi mbili (dume na jike). Anafunika usiku juu ya mchana. Hakika katika hayo kuna Aayaat (dalili, zingatio, ishara n.k) kwa watu wanaotafakari.


وَفِي الْأَرْضِ قِطَعٌ مُّتَجَاوِرَاتٌ وَجَنَّاتٌ مِّنْ أَعْنَابٍ وَزَرْعٌ وَنَخِيلٌ صِنْوَانٌ وَغَيْرُ صِنْوَانٍ يُسْقَىٰ بِمَاءٍ وَاحِدٍ وَنُفَضِّلُ بَعْضَهَا عَلَىٰ بَعْضٍ فِي الْأُكُلِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٤﴾
4. Na katika ardhi kuna vipande vinavyoungana na mabustani ya mizabibu na mimea (mingineyo) na mitende inayochipuka katika shina moja na isiyochipuka katika shina moja, (vyote hivyo) vinanyweshezwa kwa maji ya aina moja; na Tunafadhilisha baadhi yake juu ya vinginevyo katika ulaji (ladha, manufaa, rangi n.k). Hakika katika hayo kuna Aayaat (dalili, ishara, zingatio n.k) kwa watu wanaotia akilini.


وَإِن تَعْجَبْ فَعَجَبٌ قَوْلُهُمْ أَإِذَا كُنَّا تُرَابًا أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ ۖ وَأُولَـٰئِكَ الْأَغْلَالُ فِي أَعْنَاقِهِمْ ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٥﴾
5. Na ukistaajabu (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi (cha) ajabu ni kauli yao (makafiri): “Je, (sisi) tukiwa mchanga, hivi kweli sisi (tutafufuliwa) katika umbo jipya?” Hao ni wale waliomkufuru Rabb (Mola) wao. Hao watafungwa minyororo katika shingo zao. Na hao ndio watu wa Motoni, wao humo ni wenye kudumu.


وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ وَقَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِمُ الْمَثُلَاتُ ۗ وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ لِّلنَّاسِ عَلَىٰ ظُلْمِهِمْ ۖ وَإِنَّ رَبَّكَ لَشَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٦﴾
6. Na wanakuhimiza kwa maovu kabla ya mazuri, na hali imekwishapita kabla yao adhabu za mifano (kama waziombazo). Na hakika Rabb (Mola) wako ni Mwenye maghfirah kwa watu juu ya dhulma zao, na hakika Rabb wako ni Mkali wa kuakibu.


وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ ۗ إِنَّمَا أَنتَ مُنذِرٌ ۖ وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ ﴿٧﴾
7. Na wanasema wale waliokufuru: “Kwa nini hakuteremshiwa Aayah (muujiza, ishara) kutoka kwa Rabb (Mola) wake?” Hakika wewe ni mwonyaji (tu) na kwa kila kaumu ina mwongozi wake.


اللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَحْمِلُ كُلُّ أُنثَىٰ وَمَا تَغِيضُ الْأَرْحَامُ وَمَا تَزْدَادُ ۖ وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾
8. Allaah Anajua abebacho kila mwanamke (katika mimba) na kinachopunguza fuko la uzazi (kuzaa kabla ya wakati wake) na kinachozidisha (kupitisha muda au idadi). Na kila kitu Kwake ni kwa kipimo.


عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ ﴿٩﴾
9. ‘Aalimu (Mjuzi) wa ghayb na dhahiri Al-Kabiyrul-Muta’aal (Mkubwa wa dhati vitendo na sifa – Mwenye Uluwa Aliyejitukuza kabisa).



سَوَاءٌ مِّنكُم مَّنْ أَسَرَّ الْقَوْلَ وَمَن جَهَرَ بِهِ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍ بِاللَّيْلِ وَسَارِبٌ بِالنَّهَارِ ﴿١٠﴾
10. Ni sawasawa kwenu anayefanya siri kauli (yake), au anayeisema kwa jahara, na anayenyemelea usiku na anayatembea huru (waziwazi) mchana.


لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ ۚ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ ﴿١١﴾
11. (Kila mtu) Ana (Malaika) wanaofuatana mfululizo mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa amri ya Allaah. Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao (wenyewe) wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. Na Allaah Akiwatakia watu uovu (adhabu, balaa), basi hakuna wa kuurudisha. Na hawana wao pasi Naye waliyy (mtawalia, mlinzi) yeyote.


هُوَ الَّذِي يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنشِئُ السَّحَابَ الثِّقَالَ ﴿١٢﴾
12.  Yeye Ndiye Anayekuonyesheni umeme (unaosababisha) khofu na matumaini na Anaanzisha mawingu mazito (yanayoleta mvua).


وَيُسَبِّحُ الرَّعْدُ بِحَمْدِهِ وَالْمَلَائِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِ وَيُرْسِلُ الصَّوَاعِقَ فَيُصِيبُ بِهَا مَن يَشَاءُ وَهُمْ يُجَادِلُونَ فِي اللَّـهِ وَهُوَ شَدِيدُ الْمِحَالِ ﴿١٣﴾
13. Na radi inamsabbih (Allaah) kwa Himidi Zake na Malaika (pia humsabbih) kwa kumkhofu, na Anatuma mingurumo ya radi, humsibu kwayo Amtakaye nao huku (makafiri) wakiwa wanabishana kuhusu Allaah Naye ni Mkali na Mwenye nguvu za kuhujumu. 



لَهُ دَعْوَةُ الْحَقِّ ۖ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُم بِشَيْءٍ إِلَّا كَبَاسِطِ كَفَّيْهِ إِلَى الْمَاءِ لِيَبْلُغَ فَاهُ وَمَا هُوَ بِبَالِغِهِ ۚ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ ﴿١٤﴾
14.  Kwake Anayo maombi ya haki. Na wale wanaoomba pasi Naye (masanamu, walioko kaburini, mizimu n.k.) hawawaitikii kwa chochote isipokuwa kama anayenyosha viganja vyake viwili vya mikono kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, wala hayafikii.  Na du’aa za makafiri hazipo ila katika upotofu. 


وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ۩﴿١٥﴾
15. Na kwa Allaah Pekee Humsujudia vilivyomo katika mbingu na ardhi (kwa) khiyari na kuchukia na vivuli vyao (pia vinamsujudia) asubuhi na jioni. 


قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ ۚ قُلْ أَفَاتَّخَذْتُم مِّن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ ۗ أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚ قُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿١٦﴾
16.  Sema: “Ni nani Rabb (Mola) wa mbingu na ardhi?” Sema: “Ni Allaah.” Sema: “Je, mnawafanya wengineo badala Yake kuwa walinzi, wasaidizi na hali hawamiliki kwa ajili ya nafsi zao manufaa wala dhara?”  Sema: “Je,   kipofu analingana sawa na mwenye kuona, au je, viza vinalingana sawa na nuru?” Au wamemfanyia Allaah washirika wameumba kama uumbaji Wake, kisha (kama kwamba) yakafanana maumbile kwao?  Sema: “Allaah (Ndiye) Muumbaji wa kila kitu, Naye ni Al-Waahidul-Qahhaar (Mmoja Pekee - Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Mshindi, Asiyepingika).”


أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌ بِقَدَرِهَا فَاحْتَمَلَ السَّيْلُ زَبَدًا رَّابِيًا ۚ وَمِمَّا يُوقِدُونَ عَلَيْهِ فِي النَّارِ ابْتِغَاءَ حِلْيَةٍ أَوْ مَتَاعٍ زَبَدٌ مِّثْلُهُ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْحَقَّ وَالْبَاطِلَ ۚ فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَاءً ۖ وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ ﴿١٧﴾
17. (Allaah) Ameteremsha kutoka mbinguni maji (mvua) na mabonde yakatiririka (maji) kwa kadiri yake, kisha mbubujiko ukabeba mapovu (na takataka) yanayopanda juu (ya maji). Na katika vile wanavyoviunguza katika moto (kuyayusha) kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Hivyo ndivyo Anavyopiga Allaah (mfano wa) haki na ubatilifu. Basi povu linapita kama takataka (halifai chochote). Lakini vile vinavyowafaa watu hubakia ardhini. Hivyo ndivyo Allaah Anavyopiga mifano.


لِلَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَالَّذِينَ لَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُ لَوْ أَنَّ لَهُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ سُوءُ الْحِسَابِ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمِهَادُ﴿١٨﴾
18. Kwa wale wanaomuitikia Rabb (Mola) wao watapata Al-Husnaa (Jannah). Na wale wasiomuitikia hata kama wangelikuwa wana vyote viliomo ardhini na mfano wa kama hivyo pamoja, bila shaka wangelivitoa kujikombolea navyo (kuepuka adhabu). Hao watapa hesabu mbaya, na makazi yao ni (Moto wa) Jahannam. Na mahali pabaya mno pa kupumzikia.


أَفَمَن يَعْلَمُ أَنَّمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰ ۚ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٩﴾
19. Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka kwa Rabb (Mola) wako ni haki (akayafuata, je) ni sawa ambaye yeye ni kipofu? Hakika wanakumbuka (na kuzingatia) wenye akili (tu)


الَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَلَا يَنقُضُونَ الْمِيثَاقَ ﴿٢٠﴾
20.  Ambao wanatimiza ahadi ya Allaah, na wala hawavunji fungamano.


وَالَّذِينَ يَصِلُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوءَ الْحِسَابِ ﴿٢١﴾
21. Na ambao wanaunga yale Aliyoamrisha Allaah kuungwa na wanamkhofu Rabb (Mola) wao, na wanakhofu hesabu mbaya.


وَالَّذِينَ صَبَرُوا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٢﴾
22. Na ambao wamesubiri kutaka Wajihi wa Rabb (Mola) wao, na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa katika yale Tuliyowaruzuku (kwa) siri na (kwa) dhahiri, na wanaepusha ovu kwa zuri, hao watapata matokeo (mazuri) ya nyumba (ya Aakhirah)


جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ﴿٢٣﴾
23. Jannaat  za ‘Adn wataingia pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao na wake zao na dhuria zao. Na Malaika wanawaingilia katika kila milango.


سَلَامٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٤﴾
24. (Wanasema) “Salaamun ‘Alaykum” (Amani iwe juu yenu) kwa yale mliyosubiri. Basi uzuri ulioje hatima (nzuri) ya nyumba (ya Aakhirah).



وَالَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ ۙ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ ﴿٢٥﴾
25.  Na wale wanaovunja ahadi ya Allaah baada ya kufungamana kwake na wanakata yale Aliyoyaamrisha Allaah kuwa yaungwe na wanafanya ufisadi katika ardhi, hao watapata laana na watapata nyumba mbaya (Motoni).


اللَّـهُ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ وَفَرِحُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا مَتَاعٌ ﴿٢٦﴾
26. Allaah Hukunjua riziki kwa Amtakaye, na Humzuilia (Amtakaye). Na wamefurahia uhai wa dunia. Na uhai wa dunia kulingana na Aakhirah si chochote ila ni starehe ya muda tu.


وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ ۗ قُلْ إِنَّ اللَّـهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَنْ أَنَابَ ﴿٢٧﴾
27. Na wanasema wale waliokufuru: “Kwanini hakuteremshiwa Aayah (muujiza, ishara) kutoka kwa Rabb (Mola) wake?” Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Hakika Allaah Anampotoa Amtakaye na Anamuongoza kuelekea Kwake anayerudi kutubuia


الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾
28. Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah. Tanabahi!  Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia!


الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ طُوبَىٰ لَهُمْ وَحُسْنُ مَآبٍ ﴿٢٩﴾
29. Wale walioamini na wakatenda mema watapata ‘twuwbaa’ (hali nzuri) na marejeo mazuri (Jannah).


كَذَٰلِكَ أَرْسَلْنَاكَ فِي أُمَّةٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهَا أُمَمٌ لِّتَتْلُوَ عَلَيْهِمُ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَـٰنِ ۚ قُلْ هُوَ رَبِّي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ مَتَابِ ﴿٣٠﴾
30.  Hivyo ndivyo Tumekutuma katika Ummah uliokwishapita kabla yake umati nyingine ili uwasomee yale Tuliyokufunulia Wahy; nao wanamkufuru Ar-Rahmaan. Sema: “Yeye Ndiye Rabb (Mola) wangu, hapana ilaah (muabudiwa wa haki) ila Yeye, Kwake natawakali na Kwake ni marejeo yangu.”



وَلَوْ أَنَّ قُرْآنًا سُيِّرَتْ بِهِ الْجِبَالُ أَوْ قُطِّعَتْ بِهِ الْأَرْضُ أَوْ كُلِّمَ بِهِ الْمَوْتَىٰ ۗ بَل لِّلَّـهِ الْأَمْرُ جَمِيعًا ۗ أَفَلَمْ يَيْأَسِ الَّذِينَ آمَنُوا أَن لَّوْ يَشَاءُ اللَّـهُ لَهَدَى النَّاسَ جَمِيعًا ۗ وَلَا يَزَالُ الَّذِينَ كَفَرُوا تُصِيبُهُم بِمَا صَنَعُوا قَارِعَةٌ أَوْ تَحُلُّ قَرِيبًا مِّن دَارِهِمْ حَتَّىٰ يَأْتِيَ وَعْدُ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿٣١﴾
31. Na kama ingelikuweko Qur-aan ambayo kwayo majabali ingeliondoshwa (sehemu yake), au kwayo ardhi ingelipasuliwa au kwayo wafu wangelisemeshwa (basi ingelikuwa ni Qur-aan hii hii). Lakini kwa Allaah (Pekee) amri (na mambo) yote. Je, hawakujua wale walioamini kwamba kama Angetaka Allaah bila shaka Angeliwaongoa watu wote. Na hayatoacha kuwasibu wale waliokufuru maafa kwa yale waliyoyatenda, au yakawateremkia karibu na nyumba zao, mpaka ifike ahadi ya Allaah. Hakika Allaah Hakhalifu miadi (Yake).


وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِّن قَبْلِكَ فَأَمْلَيْتُ لِلَّذِينَ كَفَرُوا ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ عِقَابِ ﴿٣٢﴾
32. Na kwa yakini walifanyiwa istihzai Rasuli kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi Nikawapa muhula wale waliokufuru, kisha Nikawachukua (kuwaangamiza). Basi vipi ilikuwa (kali) malipo ya ikabu Yangu.


أَفَمَنْ هُوَ قَائِمٌ عَلَىٰ كُلِّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۗ وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ قُلْ سَمُّوهُمْ ۚ أَمْ تُنَبِّئُونَهُ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي الْأَرْضِ أَم بِظَاهِرٍ مِّنَ الْقَوْلِ ۗ بَلْ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا مَكْرُهُمْ وَصُدُّوا عَنِ السَّبِيلِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٣٣﴾
33. Je, basi Anayeisimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, (Anastahiki kuabudiwa au miungu ya uongo?). Wanamfanyia Allaah washirika. Sema: “Watajeni!” Au, mnampa habari kwa yale Asiyoyajua katika ardhi, au ni maneno matupu tu?” Bali waliokufuru wamepambiwa mbinu zao na wamezuiliwa na njia (ya haki). Na ambaye Allaah Amempotoa, basi hana wa kumuongoa.



لَّهُمْ عَذَابٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَقُّ ۖ وَمَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مِن وَاقٍ ﴿٣٤﴾
34. Watapata adhabu katika uhai wa dunia, na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni ya mashaka zaidi. Na hawatopata mbele ya Allaah wa kuwahami.



مَّثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ أُكُلُهَا دَائِمٌ وَظِلُّهَا ۚ تِلْكَ عُقْبَى الَّذِينَ اتَّقَوا ۖ وَّعُقْبَى الْكَافِرِينَ النَّارُ ﴿٣٥﴾
35. Mfano wa Jannah ambayo wameahidiwa wenye taqwa, inapita chini yake mito. Makulaji yake ya kudumu, na (pia) kivuli chake. Hiyo ndiyo hatima ya wale waliokuwa na taqwa. Na hatima ya makafiri ni Moto.



وَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَفْرَحُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ ۖ وَمِنَ الْأَحْزَابِ مَن يُنكِرُ بَعْضَهُ ۚ قُلْ إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّـهَ وَلَا أُشْرِكَ بِهِ ۚ إِلَيْهِ أَدْعُو وَإِلَيْهِ مَآبِ ﴿٣٦﴾
36. Na wale Tuliowapa Kitabu (wakaamini) wanafurahia kwa yale yaliyoteremshwa kwako (Qur-aan). Na katika makundi (ya makafiri) wako wanaoyakanusha baadhi yake. Sema: “Hakika mimi nimeamrishwa nimwabudu Allaah, na nisimshirikishe. Kwake nalingania na Kwake ni marejeo yangu.”



وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ حُكْمًا عَرَبِيًّا ۚ وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُم بَعْدَ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ مَا لَكَ مِنَ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا وَاقٍ ﴿٣٧﴾
37.  Na hivyo ndivyo Tumeiteremsha (Qur-aan) kuwa ni hukumu (shariy’ah) kwa Kiarabu. Na kama utafuata hawaa zao baada ya kukujia elimu, basi hutokuwa na waliyy (mlinzi, msimamizi) yeyote wala mwenye kukuhami mbele ya Allaah. 


وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً ۚ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ لِكُلِّ أَجَلٍ كِتَابٌ﴿٣٨﴾
38. Na kwa yakini Tulituma Rasuli kabla yako, na Tukawajaalia wawe na wake na dhuria. Na haiwi kwa Rasuli yeyote (yule) kuleta Aayah (muujiza) isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Kwa kila kipindi kina hukmu.


يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ﴿٣٩﴾
39. Allaah Anafuta yale Ayatakayo na Anathibitisha (Ayatakayo pia), na Kwake kiko Mama wa Kitabu (Lawhum Mahfuwdhw).


وَإِن مَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ ﴿٤٠﴾
40. Na kama Tutakuonyesha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) baadhi ya yale Tunayowaahidi (ya adhabu), au Tukikufisha; basi hakika juu yako ni kubalighisha (tu ujumbe), na juu Yetu ni hesabu.


أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَأْتِي الْأَرْضَ نَنقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَا ۚ وَاللَّـهُ يَحْكُمُ لَا مُعَقِّبَ لِحُكْمِهِ ۚ وَهُوَ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴿٤١﴾
41. Je, hawaoni kwamba Tunaifikia ardhi, Tunaipunguza katika mipaka yake? Na Allaah Anahukumu na hakuna wa kupinga hukumu Yake. Naye ni Mwepesi wa kuhesabu.


وَقَدْ مَكَرَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلِلَّـهِ الْمَكْرُ جَمِيعًا ۖ يَعْلَمُ مَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ ۗ وَسَيَعْلَمُ الْكُفَّارُ لِمَنْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٤٢﴾
42. Na kwa yakini walifanya njama wale wa kabla yao, basi ni kwa Allaah mipango yote (ya kupindua njama zao). Allaah Anajua yale yote yanayochumwa na kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani itakuwa hatima (nzuri) ya nyumba (ya Aakhirah).


وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَسْتَ مُرْسَلًا ۚ قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَمَنْ عِندَهُ عِلْمُ الْكِتَابِ﴿٤٣﴾
43.  Na wanasema waliokufuru: “Wewe si Rasuli.” Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Anatosheleza Allaah kuwa ni Shahiyd (Mwenye kushuhudia yote) baina yangu na baina yenu, na pia (shahidi) yule mwenye elimu ya Kitabu.”


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com