Fatwa kwa Mchache wa Elimu


ABU AMMAAR

Kadhia ya fatwa kwa siku za karibuni limekuwa suala tata hasa kwa kupatikana rai, maoni na hukumu tofauti kwa mas-ala yanayolingana.

Pia kumejitokeza utitiri wa mufti na tunaona fataawa na majibu ya masuala takriban katika maredio,T.V, magazeti na kwenye mitandao ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuelimisha waislamu na kupata majibu ya mas-ala yanayowatatiza. Hatuna budi kuwapongeza mamufti na wanazuoni wanaojitahidi kufutu mas-ala katika hukumu za kisheria. Hata hivyo na kwa sababu hii hii pia kukithiri kwa fatawa tofauti kumewatatiza waislamu wengine kujiona wana majibu yanayotofautiana katika masail yanayolingana na kutopata maelekezo mazuri ya fatwa ipi kuifuata na ipi kuiacha.

Tatizo hili la kuwepo fataawa tofauti ni la kihistoria na  limejitokeza kutokana na kuwa na madhehebu tofauti, kuwepo katika mazingira yanayofanya baadhi ya fatwa kubadilika, masheikh kufutu mas-ala kwa kutegemea na jinsi ya muulizaji na pia wakati mwengine pasina kufanyiwa utafiti  wa kina kwa mas-ala kabla ya kupatiwa hukmu yake. Na sababu nyengine ni kuandikwa kwa fatwa.Tutakuja kulifafanua hili kwa kirefu.
Maana ya karibu ya neno Fatwa ni maoni ya kielimu ya Ulamaa katika kutoa hukumu ya kisheria katika jambo la kidini.Na wengine huitafsiri kama kupiga muhuri kwa hukumu ya jambo ambalo Allah Subhaanahu Wataala alipaswa alitolee hukmu. Imam Ibnul Qayyim anasema katika kitabu chake cha I’ilaamul Muwaqi’iyn kwamba: “Kila muislamu atakaebebeshwa jukumu hili awe na hadhari na nadhari na aelewe uzito wa jukumu lenyewe na wala kusiwe na  chochote moyoni mwake kitakachomzuia kutosema ukweli na kuuusimamia, kwani Allah Subhaanahu Wataala pekee ndie atakaemlinda na kumuongoa……..”
Moja katika jambo zuri la kuandikwa fatwa ni kwamba tunaweza kuzitumia kama ni rai au hukmu katika mas-ala yatakayojitokeza na pia kuitumia kama dira katika kutupa mwanga wa kulitolea hukmu ya jambo kama litakuwa linalingana katika baadhi ya sehemu zake.Hapa tuna mfano mzuri wa kitabu maarufu cha Fataawa za Sheikhul Islam Ibnu Taymiyah ambacho kina hazina ya faida ya kielimu na vipi mufti anaweza kufikia kulipatia jambo hukmu ya kisheria.

Mfano mzuri kwa upande wa kimataifa ni hukumu ya kuwaunga /kutowaunga mkono Hizbullah katika mapambano yao na adui mkubwa wa kiislamu - mayahudi. Masheikh na mamufti wameonesha tofauti zao kuhusu kadhia hii wengine wakijuzisha kuwaunga mkono mashia kwa hili tu kwa sababu ya kigezo cha kuondosha uovu - Dar-ul Mafaasid. Wengine wamekataa katakata kuunga mkono kwa sababu tayari mashia ni kundi potofu lililokengeuka kiitikadi hivyo haipaswi kwa muislamu kushirikana nalo kwa chochote. Na kauli nyengine ni kuwaunga mkono moja kwa moja kwani ni waislamu na wametamka Shahada na tofauti zilizopo haziathiri kutowaunga mkono.

Katika masaail ya kifiqhi pia tunaona masaail mengi sana kuwa na rai na miono tofauti kati ya Maulamaa. Kama suala la kuandama kwa mwezi ambalo kila mwaka hukutana nalo na waislamu kutafuta njia za kuweza kutafuta njia za kuondosha tofauti hizi bila ya mafanikio. Kwani katika nchi moja inawezekana waislamu wakaanza kufunga Ramadhan katika siku tatu tofauti huku kila mmoja akiona kwamba rai yake ni sahihi na nyengine si sahihi kwa jinsi ya vigezo na dalili zinazotumika.

Pia katika ibada ya Hijja kupatikana rai na maoni tofauti kwenye vipengele vya Hijja na ‘Umrah, kama kujuzu/kutojuzu kufanya Tawaaful Widaa’i kwa wenye kufanya ‘Umrah. Au kuweza kufanya ibada ya ‘Umrah zaida ya mara moja katika safari moja na kadhalika.

Na hata kwenye vyakula pia hukutana na rai tofauti kuhusu uhalali na uharamu wa chakula. Kama siki – vinegar ambayo uhalali/uharamu wake hutegemea na jinsi ilivyotengenezwa.Na masuala mengi kuulizwa kuhusu uhalali/uharamu wake.

Tunaweza kuona baadhi ya mifano tofauti ya kuweza kubadilika fatwa kutokana na mazingira au hali kama ilivyotokea kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam

أنه جاءه شيخ كبير فقال له: أيقبّل الصائم؟ قال : (نعم)،ثم جاءه شاب فتيّ فأعاد عليه
                                                        ((.(السؤال، فقال له : (لا))                                         

Alijiwa na mtu mzima na kumuuliza “Je mwenye kufunga anaweza kubusu?” Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akamjibu: “ndiyo”. Kisha akajiwa na mtoto wa kiume baleghe akauliza suala hili hili na akajibiwa ; “hapana”

Pia Abdullah ibn ‘Abbass – Allah awawie radhi -

 أنّه جاءه رجل محمرّ العينين، منتفخ الودجين، تلوح عليه علامات الانتقام؛ فقال له: يا ابن عبّاس، هل للقاتل من توبة؟، قال له: لا... ثمّ جاءه رجل آخر خافض الطرْف، منكّس الرأس، قد بدت عليه علامات الحزن والندم، فقال: يا ابن عبّاس، هل للقاتل من توبة ؟   قال: نعم
                                                                                                                  

Alikuja mtu huku macho yake yamewiva na huku akionesha kuvinjari kulipa kisasi na kusema Ewe Ibnu ‘Abbaas ? mwenye kuua anaweza kutubu? Ibnu ‘Abbaas akamjibu;“hapana”. Kisha akajiwa na mtu mwengine ambae anaonekana mnyonge huku amejiinamia kichwa chake na anaonesha alama za majuto na huzuni na kusema Ewe Ibnu Abbaas Mwenye kuua anaweza kutubu? Ibnu ‘Abbaas akajibu ;”ndiyo”

Katika matukio haya mawili la kwanza kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kumkubalia mtu mzima na kumkatalia mtoto ni kutokana na hali kwani mtu mzima anaweza kuimiliki nafsi yake, tofauti na mtoto ambaye ndio kwanza baleghe - haimudu nafsi yake na matamanio.

La pili ni mazingira aliyekuja nayo muulizaji wa kwanza moja kwa moja yalimfanya Ibnu ‘Abbaas  kumkatalia kuwepo tawba kwa mwenye kuua kwani lengo lake lilionekana ni kutaka kulipiza kisasi kisha kutumia mlango wa toba kama njia . Wa pili alionekana kujuta na tendo lake lile hivyo amekuja kwa Ibnu ‘Abbaas kutaka kujua kwamba anaweza kutubu kwa kosa lake.

Sasa tuangalie athari za fatwa kama hizi kama zitaandikwa. Alhamdulillah enzi za Mtume  Salla Alahu ‘Alayhi Wasallam na masahaba –Allah awawie radhi – hili halikuwa tatizo kwani kupata ufafanuzi wa jambo lolote haikuwa taabu kwani Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alikuwepo  na masahaba walikuwa karibu.  Pia tunaona vipi Khalifa ‘Umar ibnul Khattaab, Allah amuwie radhi, alivyobadilisha hukumu baada ya kupata kauli kinyume na jinsi alvyohukumu kutoka kwa sahaba kama pale alipotaka kuzuia ughali wa mahari na ikatoka sauti ya mwanamke ikimkumbusha aya ya Qur’aan inayoruhusu hivyo. Hali hii iliendelea mpaka kwa watangu wema – salafun saalih.

 Ieleweke kwamba hukumu yoyote ya kisheria huwa ni thabiti na wala haibadiliki ikiwa hali na mazingira yatakuwa yanalingana. Hubadilika kwa kubadilika hali na mazingira kulingana na jinsi matukio yanavyojitokeza. Na wenye uwezo wa kuyaona mabadiliko haya ni wanazuoni na maulamaa walio na upeo katika elimu ya dini kwa kuzingatia misingi mikuu ya dini yetu kama ilivyokuja katika Quraan na Sunna za Mtume wetu Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam

Katika athari za kuandikwa fatwa:

1             Inaweza kutumiwa katika mazingira yasiyolingana

Ingawa ni fatwa sahihi isiyo na kosa lolote.  Mazingira itakayotumiwa itaweza kuleta madhara zaidi kuliko manufaa. Kwani kwa muislamu atakaenukuu fatwa ya Mufti inawezekana hakuangalia kwa undani mazingira ya fatwa ya awali ilipotolewa. Aliangalia zaidi natija ya fatwa.

Hapa tutachukua mfano wa hukumu ya kuvuta sigara:

Masheikh waliopita walifutu kwamba kuvuta sigara ni makruhu. Hukumu hii iliendelea kwa muda mrefu na baadhi ya waislamu kuitumia hadi hii leo kwamba ndiyo hukumu sahihi. Mamufti wa karibuni wamefutu kwamba kuvuta sigara ni haramu kwa sababu ya madhara makubwa yanayosababisha upotevu wa mali, maradhi ya saratani (cancer) kuudhi watu wengine na kadhalika.

Masheikh waliofutu kwamba sigara ni makruhu si kwamba walikosea bali mazingira ya wakati ule ambapo sayansi na teknolojia ilikuwa duni hawakuweza kuyaona madhara haya yaliyokuja kuonekana baada ya kuendelea kwa sayansi na teknolojia. Hivyo fatwa ilienda sambamba na mazingira ya wakati wao. Sasa kwa muislamu kubaki na kusisitiza fatwa ile ni sahihi na hii ya sigara kuwa ni haramu ni batili ni moja katika athari za kuandikwa fatwa hii na wengine kuitumia kama hadidu rejea.

Sasa tukitumia fatwa kwamba sigara ni makruhu tunaona hapa madhara makubwa yatayowapata waislamu kuliko manufaa kwa kigezo tu kwamba tayari fatwa hii ipo na imeshatolewa.
 
2          Inaweza kutumika katika wakati na pahala pasipolingana.           

Kwa kuandikwa fatwa, kama tulivyosema, huangalia zaidi natija ya fatwa bila ya kuangalia hali halisi iliyofanya kutolewa kwa fatwa hii. Hivyo Mufti anaweza kufutu mas –ala na kwa kuwa yamendikwa muislamu mwengine kuja kuichukua hukumu ile bila ya kuangalia kwa undani kwamba si mahala pake kutumika.

Mfano

Katika nchi za joto imewahi kutoka Fatwa kwa wanaofunga Ramadhan kufunga siku moja na kuacha siku moja kwa sababu ya joto kali linalofanywa waislamu wakifunga kuwa hatarini katika afya zao.

Muislamu mwengine anaweza kuathirika na kutumia fatwa hii kama kigezo lakini pahala alipo si sehemu ya joto kali wala waislamu kutokuwa hatarini kwa afya zao. Kwa kigezo tu kwamba fatwa hii tayari imeshatolewa na ipo.

3          Inaweza kuwa ni ya muda tu lakini ikachukuliwa kama ndio hukmu ya kudumu.

Hapa kama kuna jambo limejitokeza ambalo lingehitaji Fatwa kwa wakati ule tu kwa dharura iliyojitokeza na kuondoka kwa dharura pia humaanisha kufutika kwa Fatwa.

Mfano.

Hukmu aliyoitoa Khalifa - Amiirul Muuminiin - Umar ibnul Khattaab, Allah amuwie radhi, alipokataza wezi kukatwa mikono kipindi kilichozuka njaa katika mji wa Madina. Fatwa hii ilitolewa kwa dharura ya njaa tu na pale dharura ilipomalizika hukmu ikarudi palepale.

Hata hivyo muislamu ambae maarifa ya dini yake bado machache anaweza kuikuta fatwa hii na kuichukua kama ni hukmu huku akimnukuu Khalifa wa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kwamba alifanya jambo hili.

Au mfano wa baadhi ya Mamufti kuruhusu kuweka pesa katika mabenki yanayoendeshwa kwa riba ikiwa pahala hapana kabisa Benki inayoendeshwa kiislamu. Mfano kama Uingereza ya enzi hizo. Ila fatwa hii tayari imefutwa kwa sababu ya tayari kuwepo Benki za kiislamu au Benki zinazoruhusu kuweka pesa pasina kuwepo riba.

4          Muislamu anaweza kujiamulia kufuata fatwa “poa”

Hii ni pia ni athari mojawapo ambapo muislamu wa kawaida anaweza akautumia uchochoro huu kutafuta fatwa inayolingana na shida na mahitaji yake na kuifuata. Kwani amejikuta katika hali ya kuwa na fatwa tofauti huku uwezo wake wa kielimu ni mdogo kuweza kuzichambua dalili zilizotumika kufikia hukmu. Si kila muislamu ana uwezo wa kielimu kuweza kuzichambua na kuzihakiki dalili na hoja zilizotumika hivyo kuamua kufuata fatwa “poa” katika zilizopo kwa kukosa vigezo vya kutumia tatizo hili lkijitokeza.

5          Inawezekana Mufti hakupata ufafanuzi wa kutosha kwa aliyeuliza au kutofanywa utafiti wa kina kabla ya kutolewa Fatwa.

Katika masharti ya ziada ya Mufti ni kwamba atatakiwa awe na uwezo wa kuona mbali , mwenye busara na kuwafahamu vizuri watu  janja , hila na mbinu zao , awe na msimamo madhubuti katika dini yake na asikubali lawama , asiathirike na khofu wa vitisho vitakavyoelekezwa dhidi yake, asitetereke na awe ni mtu asiyependa makuu na amuogope Allah (Subhaanahu Wata’ala) kwa kila jambo alifanyalo

Hivyo yawezekana Mufti kutopata maelezo ya kutosha hasa katika masuala yanayofikishwa kwa maandishi- kwa mfano- ambayo huwa si rahisi kwa Mufti kupata hali halisi ya suala lenyewe. Na hivyo utafiti kuwa si wa kina katika kujibu suala alilopelekewa.

Ikumbukwe hapa kwamba fatwa mara nyingi huwa ni rai au uoni wa sheikh au mufti kwa jinsi alivyolifahamu jambo alilopelekewa na inawezekana ikawa sahihi au ikawa si sahihi. Hivyo tunaona nyengine hukubaliwa na baadhi ya fatwa zikihojiwa na kutiwa alama za kuuliza na nyengine kukataliwa moja kwa moja. Nyengine huzusha mjadala ndani yake. Na mara nyingi huwekwa mwisho wa maelezo “Allah ndie ajuae zaidi” ikiwa ni hatua ya tahadhari ikiwa mufti ameteleza katika fatwa yake.

Nini cha kufanya kwa muislamu wa kawaida atakapoona mas- ala lina fatwa zinazotofautiana?

Muislamu wa kawaida, tunaemkusudia, ni yule asie na uwezo wa kielimu ya dini ya kuweza kuzichambua na kuzihakiki dalili na hoja zilitumika hadi kupatikana hukmu ya mas-ala. Kwani kinachozingatiwa zaidi kwenye fatwa ni dalili na jinsi zilivyotumika kama ni Qur’aan, Sunna, Ijmaa au Qiyaas. Inawezekana kutumika kwa dalili vilivyo lakini jinsi ilivyotumika ikawa kidogo kuna mtihani.

Kwa kuwa fatwa ni maoni ya mwanachuoni kwa mujibu wa alivyofahamu na kuzitafsiri hukumu katika sheria ya dini ya kiislamu; kukubalika kwa fatwa kutategemea zaidi jinsi ya uwezo alionao katika kuzichambua na kuzihakiki dalili na kuzitumia vilivyo.Hivyo elimu ya mwanachuoni au ‘Alim ni kigezo muhimu cha kukiangalia kabla ya kuikubali au kuikataa fatwa yake.

Maulamaa wametofautiana kwa muislamu mchache wa elimu katika kuzitumia fatwa katika katika kauli tatu zifuatazo:
1             Achague atakayoona inafaa katika hizo.
2             Afanye jitihada na hatimae kuchagua kauli ya mwenye elimu zaidi miongoni mwa waliotoa fatwa.
3             Achague rai iliyokuwa na nguvu miongoni mwa rai zilizotolewa.

Ukiziangalia kauli zote tatu unazikuta zina udhaifu kidogo katika matumizi.

Kwani kumuachia mchache wa elimu kuchagua rai atakayoona inafaa anaweza kuathirika na rai au hoja atakayoiona ni rahisi au yenye mvuto kwa jinsi ilivyopangwa au inalingana na jinsi atakavyo kwa sababu hana sifa  na uwezo wa kuweza kuzichambua hoja zilizotolewa wala dalili zilizotumika.

Jitihada ya kuchagua rai ya mwenye elimu miongoni mwao angalau inaweza kuwa ni rai nzuri iwapo mchache huyu wa elimu ataweza kupata C.V za wanazuoni wote au kupitia watu wengine wanaowafahamu na kuweza kusema huyu anaonekana ni mwenye elimu zaidi. Na pia katika utoaji fatwa zake huonekana kuzingatia zaidi dalili za kimsingi Qura’an na Sunnah. Lakini pia inaweza kujenga dhana kwamba kila asemalo mwanazuoni huyu litakuwa ni sahihi na mengineyo si sahihi. ‘Alim huyu ni mujtahid (mwenye kujitahidi) na kisheria atalipwa ujira mara mbili akipatia hukmu ya jambo na kulipwa ujira mara moja akikosea.Pia inawezekana ikaendeleza ile dhana ya Taqlid- kufuata tu – ambako nako pia kunakuwa na mtihani wake.

Kuweza kuitambua rai yenye nguvu miongoni mwa rai zilizotolewa pia ni mtihani kwa mchache wa elimu kwani kila mufti anaweza kudai kwamba rai yake ndio yenye nguvu au karibu na sahihi kwa jinsi ya alivyotumia vigezo anavyowafikiana navyo. Hivyo daraja hii itahitaji muislamu mwenye upeo katika kuijua dini yake na kuweza kuzijua na kuzihakiki vilivyo dalili na vigezo alivyotumia mufti kama vinaweza kukubalika na hivyo rai yake kuwa na nguvu kuliko nyenginezo.

Kwa muono wangu, wallahu a’alamu, rai ya kuchagua mwenye elimu miongoni mwao,licha ya kuwa na udhaifu kidogo katika matumizi, ni rai nzuri na muwafaka katika kutafuta fatwa ipi ataweza kuitumia muislamu mchache wa elimu kwa sababu zifuatazo:

1             Kwa kutokuwa na uwezo wa kielimu moja kwa moja daraja yake huwa ya ittiba’a - mwenye kufuata na kuelekea daraja ya chini ya taqleed - mwenye kuiga na kila mwenye kufuata taqleed hupaswa kuwafuata walio na elimu. Suuratu Nnahl/43

                             فَاسْأَلُواْ أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ
     "Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui"
2             Elimu ni kigezo muhimu kwani ikiwa elimu ya mufti ina walakini ,fatwa yake pia inaweza kuwa na walakini ingawa si lazima.
3             Uwezo wa kuzichambua dalili unahitaji elimu katika nyanja tofauti za dini hivyo kwa aliebobea ataweza kuwa na nafasi nzuri ya kutumia elimu yake kuzichambua dalili kwa kituo na ushuhuda.
4             Upeo na uelevu wa mambo ukichangiwa na elimu sahihi ya dini humfanya mufti kuweza kutoa rai madhubuti katika mas-ala kwani kutalenga katika kuangalia vigezo anavyotumia kama ni sahihi au vyenginevyo.
5             Matumizi ya dalili za kisheria ni kigezo cha kufuata hata kama kuna ugumu au wepesi. Na ikiwa jambo lenyewe lina rai tofauti basi mwenye elimu ataweza kutupa picha halisi ya jinsi vigezo alivyotumia kufikia hukmu na jinsi vilivyotumika kwani tumeagizwa tuangalie zaidi dalili katika hukmu na si vyenginevyo.

Wallahu A’alamu – Allah ndie ajuae zaidi.