Alikuwa
na umbo la kuvutia, mwembamba na mrefu uso wake mwingi huwa na tabasamu na kuwa
na ndevu ziliachana achana. Alikuwa mkarimu sana mpole na mwenye
haya. Hata hivyo, katika mazingira magumu huwa mkakamavu na mkali mfano
wa upanga.
Jina
lake kamili ni Amr ibn Abdullah ibn Al-Jarraah.
Abdullah
ibn Umar anasimulia:
“Watu
watatu katika kabila la maquraysh walikuwa wanajulikana sana kuwa na tabia
nzuri na wapole. Wakiongea nawe hawakughilibu na ukiongea nao
hawakusingizii uongo: Abubakar Siddiq, Uthman ibn Affan na Abu Ubaydah
ibn Al-Jarraah.”
Abu
Ubaydah ni miongoni mwa watu wa mwanzo kusilimu. Yeye na Abubakar
wamepishana kwa siku moja tu. Na kupitia kwa Abubakar ndiko kulikomfanya
kusilimu. Abubakar aliwachukua yeye, Abdurrahmaan ibn Awf, Uthman ibn
Madh-uun na
Al-arqam
ibn Abil Arqam kwenda kwa Mtume (SAW)
ambapo wote kwa pamoja wakakubali ukweli na dini ya haki. Hawa
wanahesabika kuwa mihimili ambayo uislam ulikuja kujengewa baadae.
Kama
walivyokuwa waislam wa Makka, Abu Ubaydah pia alipata taabu sana kwani alikuwa
ni miongoni mwa waislam wa mwanzo. Taabu, shida, matusi, vipigo na huzuni
vyote hivi vilikuwa ni majaribu yaliyowapata na ni imani thabiti kwa Mwenyezi
Mungu (SW) ndiyo iliyomsaidia. Na katika mtihani mkubwa uliomfika ni majaribu
aliyoyapata katika vita vita vya Badr.
Alikuwa
ni miongoni wa wapiganaji wa jeshi la kiislam na alipigana kwa ari moja kama
mtu asiyegopa kabisa kifo. Majeshi ya kiquraysh yalimfahamu vyema na mara
nyingi yalimwepuka, lakini kulikuwa na mtu mmoja alikuwa akimfuata kila aendako
naye akajitahidi wasikutane.
Hata
hivyo, yule mtu akawa anamrandia na alipopata nafasi akaanza
kumshambulia. Abu Ubaydah bado hakuwa tayari kupigana naye, aliendelea
kujihami tu. Lakini yule mtu akawa kikwazo kwake kuendelea kupigana kwani
kila akijaribu kumuepuka humkalia mbele yake mpaka wakawa uso kwa uso.
Abu Ubaydah hakustahamili tena akampiga pigo moja la nguvu na kumuua.
Mwenyewe
utaweza kufahamu ni nani kwani ulikuwa ni mtihani wa aina yake kati ya uislam
na ukafiri na ubaba ua umwana. Alikuwa ni baba yake mzazi Abdullah ibn
Al-Jarraah!
Abu
Ubaydah hakutaka kumuua baba yake lakini kwenye vita kati ya uislam na ukafiri
chaguo lilikuwa moja tu. Chaguo lenyewe ni majaribu makubwa na ya kuzingatia
sana mpaka baadhi wakasema hakumuua baba yake bali alichoua ni ukafiri uliomo
kwenye mwili wa baba yake.
Na
kuhusu tukio hilo aya ya Suratul Mujaadalah/22 iliteremka
“Huwakuti
watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga
Mwenyezi Mungu na Mtume wake hata wakiwa ni baba zao,au watoto wao ,au ndugu
zao,au jamaa zao.Hao ameandika katika nyoyo zao imani na amewapa nguvu kwa roho
itokayo kwake. Na atawaingiza katika mabustani ipitayo mito kati yake.Humo
watakaa daima.Mwenyezi Mungu awe radhi nao na wao wawe radhi nae.Hao ndio kundi
la Mwenyezi Mungu.Hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa”
Na
athari za kukutana na baba yake vitani zilimfanya awe na imani zaidi kwa
Mwenyezi Mungu na uchamungu wa hali ya juu kwa ajili yake.
Imehadithiwa
na Muhammad ibn Jaafar (RA) kwamba ujumbe wa wakristo ulikuja kwa Mtume (SAW)
na kusema, “Ewe Abul Qasim, (wakimaanisha Mtume) tunamtaka mmoja wa masahaba
wako aje pamoja nasi, mtu ambaye wewe mwenyewe uko radhi naye, ili atahukumie
baadhi ya mas-ala yetu kuhusu vitu ambavyo sisi wenyewe tumekhtalifiana. Kwani
nyinyi waislam tunakuheshimuni sana.”
“Njooni
jioni, nitakupeni mtu mmoja ambaye ni thabit na mkweli” akajibu Mtume
(SAW)
Umar
ibn Khattab aliyasikia haya na baadaye kusema:
“Nilikwenda
mapema kusali nikitaraji labda mimi ndiye niliyesadifu yule mtu aliesifiwa na
Mtume (SAW).
Mtume
(SAW) alipomaliza kusali akaanza kutazama kulia na kushoto, nikajiinua kidogo
na kujishughulisha ili Mtume (SAW) apate kuniona. Mtume (SAW) aliendelea
kutafuta mpaka alipomuona Abu Ubaydah akamwita na kumwambia, “Nenda nao na
wahukumie kwa haki yale wanayotofautiana.” Hivyo ndivyo alivyochaguliwa
Abu Ubaydah.
Sifa
hii ya uadilifu ya Abu Ubaydah, aliweza kuitekeleza kwa amana katika kutekeleza
majukumu yake na hayo kuthibitishwa na matukio tofauti.
Siku
moja, Mtume (SAW) alipeleka kundi la masahaba kwenda kukutana na msafara wa
maquraysh. Alimteua Abu Ubaydah kuwa Amir (kiongozi) na kuwapa kigunia
cha tende kama chakula chao. Abu Ubaydah akawa anampa kila sahaba mmoja
tende moja kila siku. Alikuwa akiila ile tende na kuinyonya kama mtoto mchanga
anavyonya ziwa la mama yake. Kisha akanywa maji na hii kumtosheleza kwa
siku nzima.
Siku
ya vita vya Uhud, pale waislam walipokuwa wanapigwa, mmoja katika makafiri
alikuwa akisema kwa sauti kubwa, “ Nionesheni Muhammad, nionesheni Muhammad”
Abu Ubaydah alikuwa miongoni mwa waislam kumi waliomzunguka Muhammad kumkinga
na makafiri.
Vita
vilipomalizika, ilibainika moja ya jino lake Mtume (SAW) la gego limevunjika,
kipaji chake kimejeruhiwa na vipande vya vyuma viwili vya ngao yake kupenya
kidogo kwenye mashavu yake. Abubakar akataka kumtoa Mtume (SAW) lakini
Abu Ubaydah akamwambia:
“Niachieni
mie”
Aliogopa
kuvivuta vile vipande vya nyuma kwa mkono kuchelea kumzidishia maumivu Mtume
(SAW). Hivyo akaamua kuvitoa kwa meno, akavibana na akavivuta kwa nguvu
kwa bahati mbaya jino lake la nabu likatoka akimshughulikia Mtume
(SAW). Ikabidi kile kipande cha chuma chengine akitoe kwa kwa jino
lake jengine la nabu nalo pia likatoka, Abubakar akasema kwa mzaha;
“Abu
Ubaydah ni mtaalam wa kun’goa jino la nabu!”
Baada
ya Mtume (SAW) kufariki, waislam walikutana ili kumchagua Khalifa.
Mkutano huu ulifanyika Saqifa sehemu ya mkutano ya Banu Saadah siku hii
inajulikana katika historia kama siku ya Saqifa. Umar ibn Khattab
akamwambia Abu Ubaydah, “Lete mkono ili niape kiapo cha utii kwako kwani
nilimsikia Mtume (SAW) akisema, Kila umma una Amir (msimamizi) na wewe ni Amir
wa umma huu”
“Wala
sitofanya, kujitanguliza mbele ya mtu ambaye Mtume (SAW) aliamrisha atuongoze
kwenye sala naye akatuongoza mpaka kufa kwa Mtume (SAW)” akajibu Abu Ubaydah
akimaanisha Abubakar Siddiq.
Alikuwa
mshauri wa karibu wa Abubakar enzi za ukhalifa wake na kufanya hivyo hivyo kwa
Umar. Hakuwahi kutofautiana kwa lolote lile isipokuwa jambo moja ambalo
alitofautiana na Umar ibn Khattab.
Tukio
hilo lilitokea wakati Abu Ubaydah yupo Syria akiongoza jeshi la waislam mpaka
kuweza kuikamata Syria yote na kuwa chini ya himaya ya kiislam.
Yakaja
kuingia maradhi ya mlipuko (kuambukiza). Mlipuko ambao haujawahi katokea na
watu wengi kuathirika. Umar akamtuma mjumbe kumpelekea salamu Abu Ubaydah
akiwa na barua isemayo:
“Nina
shida na wewe muhimu sana.Ukiipata tu barua hii hata kama usiku, nnakushauri
kuanza safari hata kabla ya alfajiri haijaingia na kama utaipata mchana,
haraka fanya safari hata kabla ya jioni haijaingia.”
Alipoipata
barua, Abu Ubaydah akasema, “nnajua kwa nini Amirul Muumiinin
ananihitaji. Anataka kuhakikisha uhai wa mtu na hata hivyo utamalizika.”
Hivyo
akajibu,
“Ninajua
kama unanihitaji. Lakini nipo ndani ya jeshi la waislam na wala sina hamu
yoyote ya kujiokoa nafsi yangu na haya majanga yanayotupata. Sitopendelea
kutengana nao mpaka pale Mwenyezi Mungu atakapotaka. Hivyo ikikufika
barua hii (ukubali udhuru wangu) niachie kutoka kwenye amri yako na uniruhusu
niendelee kubaki.”
Umar
alipoipata barua na kuisoma alitokwa na machozi mpaka wale waliokuwepoo
wakauliza;
“Vipi
Amirul Muuminiin, Abu Ubaydah amefariki?”
Umar
akajibu, “Hapana, lakini kifo kipo karibu naye.”
Na
kama alivyosema Umar haukupita muda maradhi yakamkumba Abu Ubaydah na kabla ya
kufariki alitoa wasia kwa jeshi lake na kusema:
“Ngojeni
nikupeni wasia ambao utakufanyeni muwepo katika njia ya kheri:”
“Simamisheni
Sala, fungeni Ramadhani, toeni sadaqa, tekelezeni ibada ya Hijja na Umrah, na
kuweni pamoja. Msiiruhusu dunia ikuharibuni kwani mtu hata akiishi miaka elfu
mwishowe atafikia kama hapa ambapo mimi nipo.”
“Amani
iwe kwenu na rehema za Mwenyezi Mungu.”
Abu
Ubayadah akamgeukia Muadh ibn Jabal na kumwambia, “ewe Muadh, wasalishe watu”
na hapo hapo roho kumtoka.