Saad ibn Abi Waqaas - Shujaa wa Qadisiyyah
Alikuwa kijana mfupi na aliyejengeka
kimwili na nywele nyingi. Watu wa Makka walimfananisha na simba mtoto. Nae pia
anatoka katika ukoo wa kitajiri na kuheshimika. Ni mtu wa karibu sana kwa
wazazi wake na alimpenda sana mama yake. Muda wake mwingi aliupoteza
kutengeneza mishale na pinde na kufanya sana mazoezi ya kurusha mishare kama
kwamba anajiandaa na vita vikubwa.
Saad hakuwa na furaha katika mfumo mzima wa
maisha ya Maquraysh wa Makka. Alihisi kwamba imani zao na miungu wanayoiabudu
ina upungufu aina fulani bila ya kuujua hasa ni upi. Tabia za Maquraysh
nazo pia hazikumpendeza wala kumridhisha.
Siku moja alitembelewa na Abubakar Siddiq
na kuzungumza naye. Abubakar alimfahamisha kuhusu Muhammad ibn Abdullah
mtoto wa marehemu dada yake kwa mjomba na shangazi, Amina bint Wahab kwamba
ameteremshiwa Wahy na kutumwa kutangaza dini ya haki na uongofu.
Baadae Abubakar alienda naye kwa Muhammad
(SAW). Ilikuwa ni jioni na Mtume ndio kwanza amemaliza kusali. Baada ya
kusikia wito na yeye mwenyewe tangu mwanzo kuwa na wasi wasi na imani ya
kiquraysh alikubali hapo hapo na kutamka shahada.
Mtume alifurahishwa sana na kusilimu kwa
Saad kwani tokea utotoni wake alama za kuwa mtu wa busara tayari zilijitokeza.
Vile vile kusilimu kwake kungepelekea vijana wengine pia nao kuja katika
uislamu.
Ingawa Mtume (SAW) alifurahishwa sana na
kitendo cha Saad kuingia katika uislamu, kuna watu wengine walichukizwa sana na
tendo hilo akiwemo mama yake Saad. Saad anasimulia:
“Wakati mama yangu alipopata habari
kwamba nimesilimu aliingiwa na hasira na alikuja kwangu huku ameghadhibika na
kunikaripia, ‘Ewe Saad mwanangu, nini kimekusibu kuacha dini ya baba na mama
yako na kufuata dini gani hii…..? Naapa ima uachane na dini yako hii mpya au
nitajifungia kula na kunywa mpaka nife. Moyo wako utaemewa kwa huzuni na
majuto kukukumba na watu kukuapiza milele kwa jinsi ulivyomtendea mama yako.’
Saad akajibu, “usifanye hivyo, ewe mama
yangu, hakuna kitu chochote kitakachonifanya niachane na dini yangu.”
Hata hivyo, mama yake hakumsikiliza na
kuanza mgomo wake wa kutokula wala kunywa. Akaanza kudhoofika na Saad
alijitahidi kumbembeleza na kumsihi mama yake huku akimletea chakula.
Mama yake alikataa kata kata na kurudia usemi wake ule ule, “achana na dini
yako na mimi nitakula, ila hivyo, niache nife.”
Saad akamwambia, “ewe mama yangu nina
mapenzi makubwa kwako kama mama yangu ulienizaa, lakini mapenzi yangu kwa
Mwenyezi Mungu (SW) na Mtume wake ni makubwa zaidi, Wallahi, lau hata roho elfu
moja na moja zitaondoka (kwa kunitaka nirudi dini yangu ya zamani) kamwe
sitorudi dini yangu.” Mama yake kuona msimamo wa mwanawe haujatetereka
wala kuyumba licha ya kitisho kizito alichomtisha akaona hakuna haja tena ya
kuendelea na mgomo na kuanza kula.
Ni kwa tukio hili adhimu la msimamo wa Saad
kwa mama yake; aya za 14-15 za Surat Luqman ziliteremka:
“Na tumemuusia mtu kwa (kuwatendea wema)
wazazi wao wawili, mama yake alibeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu na
kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia) Nishukuru mimi na wazazi
wako. Ni kwangu mimi ndio marudio. Na pindi wakikushikilia
kunishirikisha na ambayo huna elimu nayo basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema
duniani. Na ishike njia ya anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu na
mimi nitakuambieni mliokuwa mkiyatenda”
Katika siku za mwanzo wa Uislam, Mtume
(SAW) aliwaasa waislam kuwa na tahadhari sana na Maquraysh wasije wakakasirika
kwani bado Uislam haukuwa na nguvu za kuweza kuhimili vishindo vyao.
Wakati huo walikuwa wakitoka kwa vikundi kwenda kando kando ya mji wa Makka
kufanya ibada. Siku moja baadhi ya makafiri waliwaona waislam wakisali na
wakawabughudhi na kuwafanyia inda.
Subira ya waislam ilifika kikomo na
wakavamiana nao na kuanza kupigana. Saad alikamata bufuru la ngamia na
kumpiga mmoja wao na kumjeruhi. Ilikuwa ni damu ya kwanza kumwagika kati ya
vita vya waislam na makafiri vita ambavyo ilikuja kuwa kubwa na kujaribu imani
za waumini na kuwatia katika mitihani.
Hata hivyo, baada ya tukio hili, Mtume
(SAW) bado alisisitiza pale pale kuwa na subira na uvumilivu na kuwakumbusha
kuwa hiyo ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu mtukufu na wakati bado haujawa
muafaka. Suratul Muzamil /10-11
“Basi kuweni na subira na yale
wanayoyasema na jitengeni nao kwa vizuri. Na niacheni mimi peke yangu
niwashughulikie wale wanaokadhibisha , walioneemeka, basi wastahamilie kidogo”
Miaka ilipita na rukhsa ya kupigana Jihadi
ilipotoka Saad alikuwa na umuhimu mkubwa hasa katika vita vilivyotokea wakati
wa Mtume (SAW) na baada ya kufariki kwake.
Alipigana vita vya Badr pamoja na mdogo
wake Umayr ambaye aliomba aruhusiwe kuungana na jeshi japokuwa alikuwa na umri
mdogo. Saad alirudi peke yake Madina kwani Umayr ni mmoja katika
mashahidi kumi na wane waliouwawa.
Katika vita vya Uhud, Saad alichaguliwa
pamoja na Zayd, Saib ibn Othman bin Maazun kwani walikuwa warusha mishale
stadi. Alipigana kwa moyo na nguvu zake zote katika kumlinda Mtume (SAW)
hasa pale baadhi ya waislam waliopangwa milimani kuondoka sehemu zao.
Mtume (SAW) alikuwa akimpa moyo huku
akimwambia, “rusha, rusha yaa Saad… Fidaaka Abi wa Umm.”
Ali ibn Abitalib anasema hajawahi kumsikia
Mtume Muhammad (SAW) akiahidi kulipa kwa mtu yoyote isipokuwa Saad.
Katika historia ya kiislam Saad atakumbukwa
kuwa sahaba wa kwanza kurusha mishale kwa ajili ya kuuhami Uislam na Mtume
(SAW) akamuombea dua:
“Ewe Mola uongoze mshale wake na
umkubalie dua zake”
Naam! Saad alijaaliwa utajiri na hakuwa
maarufu kwa ushujaa tu bali pia alikuwa mkarimu. Wakati wa Hijjatul Widaa
– Hijja ya kuaga- akiwa pamoja na Mtume Muhammad (SAW) aliugua. Mtume (SAW)
akaja kumkagua na Saad akasema, “Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nimejaaliwa mali
na nimebahatika kuwa na mtoto mmoja tu wa kike atayenirithi, Je! Niitoe
thuluthi mbili ya mali yangu kama sadaqa?
Mtume (SAW) akasema, “Hapana”
Akauliza tena, “nusu je?”
Mtume akamkatalia tena, “hapana.”
“Je! Thuluthi?”
“Naam na bado thuluthi ni nyingi kwani
kuwaacha warithi wako katika hali nzuri ni bora kuliko kuwaacha masikini
wakiomba watu…….” Mtume alimjibu.
Saad alijaaliwa kupona ugonjwa na
kubarikiwa na watoto wengine wengi tu.
Alikuwa maarufu zaidi kama kamanda wa jeshi
la kiislam lililotumwa na Khalifa Umar ibn Khattab kwenda kupigana na waajemi
(Persians) katika vita vya Qadisiyya. Khalifa alitaka kuung’oa
utawala wa Sasania (Ctesphon) uliokuwa ukitawala kwa karne nyingi.
Kazi hii haikuwa rahisi kwani waajemi
walikuwa wapiganaji stadi na wenye nidhamu ya hali ya juu. Hivyo
lilihitajika jeshi lililotimia katika maeneo yote. Khalifa akatuma wajumbe
katika miji ya waislam iliyokombolewa kutangaza wito wa Jihadi na kukusanya
wale wote wenye uwezo, utaalam, mbinu na mikakati kujiandaa na vita hivi
adhimu.
Naam! Wanajihadi wakaitikia wito na
kukusanyika Madina kutoka ila kona ya miji ya waislam. Kutokana na ukubwa wa
jeshi la kiislam na uzito wa kazi yenyewe, Khalifa ikambidi afanye shura kuhusu
nani atakuwa kiongozi wa jeshi. Ushauri wake Khalifa ulikuwa kuliongoza yeye
mwenyewe kwani kazi ilikuwa nzito na kama ni Amirul Muuminin ni wajibu wake
kuwaongoza waislam. Sayyidina Ali hakuunga mkono wazo hilo na kumfahamisha
Khalifa kwamba waislam walikuwa wanamuhitaji sana Khalifa kubaki Madina kuliko
kwenda kuhatarisha maisha yake vitani.
Baada ya kupita shura, Saad akachaguliwa.
Mmoja katika masahaba wakongwe Abdulrahman ibn Awl akampongeza Khalifa na
kusema, “umejua kuchagua! nani mwengine zaidi ya Saad?”
Sayyidina Umar akasimama na kulitakia kila
la kheri jeshi la kiislam na kumpa nasaha Saad kwa kumwambia:
“Ewe Saad! Usikubali maneno yoyote
yatakayosemwa kwamba (umechaguliwa kwa sababu) ni mjomba wa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (SW) au ni sahaba wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu (SW), Mwenyezi Mungu (SW)
haondoshi jambo baya kwa ubaya bali huondosha baya kwa jambo jema”
“Ewe Saad! Hakuna mahusiano yoyote kati ya
Mwenyezi Mungu (SW) na mtu yoyote isipokuwa kwa kumtii yeye Allah (SW).
Kwa mtazamo wa Mwenyezi Mungu watu wote ikiwa ni mheshimiwa au mtu wa kawaida,
ni sawa sawa. Mwenyezi Mungu ni Mola wao, wote ni waja wake wanaotafuta
kunyanyuliwa kwa taqwa na kutii. Mkumbuke mjumbe wa Mwenyezi Mungu
alivyokuwa akiwafanyia waislam na wewe ufanye hivyo hivyo!”
Amirul Muuminiin aliweka bayana kwamba vita
hivi si kwa ajili ya mtu kupata umaarufu wala kutawala bali ni kulifanya neno
la Mwenyezi Mungu “Laa Ilaha Ill allah” kuwa juu.
Watu elfu thelathini wakaanza safari kuelekea Qadisiyya wakiwemo tisini na tisa waliopigana Badr na zaidi ya mia tatu walioshuhudia suluhu ya
Hudaybiya, pia wakiwemo takriban mia tatu wengine waliokuwamo katika jeshi la
kuifungua Makka. Wakiwemo watoto wa masahaba na wanawake waliokwenda
kuwashajiisha na kama wauguzi.
Walipiga kambi Qadisiyya
katika mji wa Hira, Waajemi walijiandaa na
vita hivi na jeshi la watu laki moja na ishirini elfu wakiongozwa na kamanda
wao shujaa Rustum.
Amirul Muuminiin alimuagiza Saad kumpelekea
habari kwa kila kitakachotokea kwa waislam na makafiri. Saad akamwandikia Amirul
Muuminiin juu ya ukubwa wa jeshi lao na zana walizonazo.
Amirul Muuminiin akajibu, “Usitishike wala
kushtushwa na utakayoyasikia kuhusu jeshi lao na mbinu watakazozitumia dhidi
yenu. Omba msaada kwa Mwenyezi Mungu na uwe na imani. Peleka ujumbe wa
watu wenye busara, hekima na walio madhubuti wamlinganie kuingia Uislam na
jitahidi kuniandikia kila siku.”
Saad alifanya kama alivyoagizwa na kutuma
ujumbe mzito kwanza kwa Yazdaqird na baadaye
kwa Rustum, wote kuwataka kuingia katika
uislam na kulipa jizya (ushuru) ili wahakikishiwe usalama wao na kuishi kwa
amani vyenginevyo wachague vita baina yao.
Ujumbe wa mwanzo wa waislam ulibezwa na
kudharauliwa na kiongozi wa Waajemi, Yazdaqird.
Uliongozwa na Bin Nuum ibn Muqarrin. Ujumbe
wa pili ukiongozwa na Rubiiy ibn Aamir kwa Rustum, ulikwenda moja kwa moja kambi ya Rustum.
Huku akiwa na mkuki mkononi, Rubiiy akampa ujumbe na Rustum akauliza:
“Rubiiy! Nini unataka kutoka kwetu?” ukiwa
unataka utajiri, tutakupeni, mkitaka chakula tutakulisheni mpaka mkinai. “
Aliendelea kusema,
“Tutakupeni nguo na kukufanyeni muwe
matajiri na wenye furaha, tazama Rubriiy! Nini unaona kwenye majlis yangu hii,?
Hapana shaka huoni alama za utajiri, mazulia ya fahari, mapazia ya kupepea, kuta
zilizonakishiwa dhahabu, huna hata hamu basi tukikutunukia vyote hivi
tulivyonavyo!”
Rubiiy alitulia na kumsikiliza Rustum
akijifaharisha na kumwambia, “Sikiliza, Mwenyezi Mungu ametuchagua sisi na
kutoka kwetu sisi kizazi chake ambacho mwenyewe Mwenyezi Mungu (SW) amemtaka
ili kututoa kutoka kuabudu masanamu kwenda kwenye Tauhid (kumpwekesha Mwenyezi
Mungu) na kututoa kutoka kwenye wale wote wanaojishughulisha na dunia (kusahau
akhera), na kututoa kutoka watawala dhalimu dhidi ya uislam.” Aliendelea kusema,
“Na yeyote atakayetukubalia wito wetu tuko
tayari kumkaribisha kwa mikono miwili na yoyote atakayeamua kupigana nasi, sisi
tutapigana na mpaka ahadi ya Mwenyezi Mungu (SW) itakapotimia.
Rustum akauliza,
“Kitu gani amekuahidini Mungu wenu?”
“Pepo kwa wataokufa shahidi na ushindi kwa
watakaoishi.” Alijibu Rubiiy.
Hata hivyo, Rustum kwa kujiona wo ni bora
zaidi hakuwa tayari kuzingatia maneno haya hasa kwa mtu mwenyewe anayesema
kuonekana dhalili na kwa kuwa karne nyingi, watu hawa walikuwa wakiwatawala na
kuwajua kama walikuwa katili na wajinga.
Vita hivyo vikawa vinanukia, Saad alitokwa
na machozi kwani kupindi hiki alikuwa mgonjwa hata kushindwa kusimama sawa
sawa. Aliona dalili zote kwamba vita hivi vitakuwa vikubwa, hatari na
damu nyingi itamwagika. Akawa akisema moyoni Lau………….. Lakini hapo hapo
akaikumbusha nafsi yake kwamba Mtume (SAW) amefundisha waislam kutosema Lau…
kwani humaanisha ukosefu wa dhati na azma ya kufanya na kuona kwamba lau hali
ingelikuwa tofauti si tabia ya kiislam.
Akajikongoja na kusimama mbele na kuanza
kuwahutubia wanajihadi. Alianza kwa aya ya 105 katika Quraan Suratul
Anbiyaa,
“ Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya kumbukumbu,ya kwamba ncha watarithi waja wangu walio wema”
Baada ya kumaliza khutba ya kuhuisha nyoyo
na kuwatia mori wanajihadi, wakasali sala ya adhuhuri jamaa na kuwageukia tena
baada ya sala na kuwapa amri ya kupigana kwa kutamka kilio cha kivita,
“Allah Akbar, Allah Akbar, Allah Akbar,
Allah Akbar” mara nne na kuamrisha washambulie huku akiwatia moyo kwa
kusema, “Hayya ala barakatillah”, (haya wavamieni kwa baraka za Mwenyezi Mungu)
Kwa siku nne mfulululizo vita vilipigwana
huku Saad akiwa kwenye hema lake akiongoza mashambulizi na kupanga mikakati na
kuwatia mori wanajihadi,
“Allahu Akbar, Laa haula walaa Quwwata
illaa Billahi.”
Waislam walipigana kwa moyo wao wote na
ufundi wakijua ima ni ushindi au shahada tu. Baadhi ya wanajihadi
mashujaa walitafuta mbinu mpaka kuweza kumfikia kamanda Rustum kwenye ngome
yake. Hapo ikazuka piga nikupige ya aina yake kwani ni vumbi tu lililokuwa
likitimka ndilo lililoonekana na paa la ngome ya Rustum kutupwa ndani ya mto.
Kuona patashika hiyo Rustum alijaribu kukimbia lakini hakufika mbali na
alikamatwa na kuuwawa.
Baada ya kuuwawa kwa kamanda wao majeshi ya
Kiajemi yalianza kusambaratika na kukimbia huku na kule wasijue la kufanya na
huku wanajihadi wa kiislam wakiwashambulia.
Vita hivi viliweka historia ya damu nyingi
sana kumwagika kwani kwa siku nne tu zilizopiganwa vita hivi takriban
watu elfu
thelathini waliuwawa, na katika siku moja tu waislam
elfu mbili walikufa shahidi na makafiri elfu
kumi kupoteza maisha yao.
Vita vya Qadisiyyah vilileta ushindi
muhimu sana kwa waislam. Vilimaliza kabisa na kuondoa utawala wa
kisasania kama vilivyokuwa vita vita vya Yarmuk kuumaliza utawala wa kibizantini.
Miaka miwili baadaye na kuwa na hali nzuri
ya kiafya Saad alikwenda kuutwaa mji mkuu wa Sasan – Ctesiphon,
waliweza kuutwaa mji huu baada ya kuuvuka mto Tigris
wakati wa mafuriko.