006 - Hadiyth Ya 6: Kutawakali Kwa Allaah Na Kuwa Na Moyo Laini

006 - Hadiyth Ya 6: Kutawakali Kwa Allaah Na Kuwa Na Moyo Laini


عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ: ((يَدْخُلُ الْجَنَّةَ أَقْوَامٌ أَفْئِدَتُهُمْ مِثْلُ أَفْئِدَةِ الطَّيْرِ)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Wataingia Peponi watu ambao nyoyo zao ni mithali ya nyoyo za ndege)).[1] Kwa maana: Wenye kutawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na nyoyo zao zikiwa laini.
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Waumini ni wenye nyoyo laini, kinyume na makafiri na wanafiki. [Al-Maaidah 5: 13].
 
  1. Umuhimu wa kutawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na kuwa na moyo mlaini (wenye yaqini), kwani ni sababu ya kumuingiza Muislamu Peponi.
 
فَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ
Basi chochote mlichopewa katika kitu ni starehe (fupi ipitayo ya) maisha ya dunia.  Na yale yaliyoko kwa Allaah ni bora na ni ya kudumu zaidi kwa wale walioamini na kwa Mola wao wanatawakali.[2]
 
  1. Muumin anapaswa asishughulishwe hadi kujiangamiza au kuingia katika chumo la haramu katika kutafuta maisha na rizki yake, kwani rizki inakutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Anayemruzuku ndege anayekutoka asubuhi bila ya kujua rizki yake, akarudi jioni akiwa amepata mahitajio yake. [Huud 11: 6, Al-An’aam 6: 38]. Na kughushi ni miongoni mwa chumo la haramu. [Rejea Hadiyth namba 101 kuhusu kughushi].
 
  1. Kutawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى), kuwa na yakini na moyo laini ni miongoni mwa sifa kuu za Muumin. [Al-Anfaal 8: 2-4, Al-Ahzaab 33: 22, Aal-‘Imraan 3: 173-174].
 



[1]  Muslim.
[2]  Ash-Shuwraa (42: 36).