Ikrimah ibn Abujahl –Adui mkubwa, mwanajihadi shujaa

Ikrimah alikuwa miongoni mwa maquraysh wanaoheshimika hasa kwa kuwa tajiri na kutoka katika nasaba ya Abu Jahl. Baba yake alikuwa mshirikina mkuu na mmoja katika watukufu wa kiquraysh wa Makka.  Kila nafasi aliyokuwa akiipata huitumia kumfanyia inda na inadi Mtume (SAW) na aliwatesa kupita kiasi waislamu waliotoka katika ujahiliya.
 
Ikrimah naye hakuwa nyuma na aliumuunga mkono baba yake na chuki aliyokuwa nayo kwa Mtume (SAW) na mateso dhidi ya waislamu yalimfanya baba yake Abu-Jahl kuzidi kumpenda na kuwa karibu naye.
 
Katika vita vya Badr, kiongozi wa makafiri wa Makka alikuwa Abu-Jahl na aliapa kwa Laat na Uzza kwamba hatorudi Makka mpaka ahakikishe kwamba amemmaliza Muhammad (SAW).  Kwa uwezo wake Allah (SW) kinyume chake ndicho kilichotokea, kwani katika watu wa mwanzo mwanzo kuuwawa alikuwa yeye Abu-Jahl na mwanawe Ikrimah alikuwa akiona  “live” jinsi mikuki ikipenya mwili wa baba yake huku akilia kwa uchungu hadi kufa. Kitendo cha kuuwawa baba yake mbele ya macho yake kilimsikitisha sana Ikrimah na kilichozidi kumtia simanzi ni kule kushindwa kuuchukua mwili wa baba yake kwenda kuuzika Makka na kuuacha ukioza.
 
Tokea siku hiyo, Ikrimah akawa adui nambari moja wa uislam, alikuwa akimchukia Mtume Muhammad (SAW) na masahaba zake, chuki iliyojaa hasira za kutaka kulipiza kisasi cha kuuwawa kwa baba yake. Na nafasi hiyo ilijitokeza kwenye vita vya Uhud.
 
Katika vita hivi kikosi cha upande wa  kulia cha Makafiri kiliongoozwa na Khalid bin Walid na cha kushoto Ikrimah ibn Abu Jahl.  Makafiri katika vita hivi waliwapiga waislamu na hivyo kuweza kulipiza kisasi cha vita vya Badr.
 
Miaka tisa baada ya Hijra ya Mtume (SAW) pamoja na maelfu ya masahaba walirudi Makka.  Mtume Muhammad (SAW) alikubaliana na Maquraysh kwamba hakutokuwa na vita na hivyo kuruhusiwa kuingia Mji wa Makka, hata hivyo baadhi ya maquraysh hawakukubaliana na uamuzi huu na wakiongozwa na Ikrimah walikwenda kujaribu kuwazuia Waislam wasiingie katika mji wa Makka.
 
Mtume (SAW) alipoingia Makka na maquraysh kusalimu amri alitoa msamaha kwa maquraysh wote watakoingia Masjid Al-Haraam  na wale waliobaki majumbani mwao na wale waliokwenda kwa Abu Sufiyan, kiongozi wa Maquraysh wakati huo.  Hata hivyo alikataa msamaha kwa watu wengine wachache na baadhi yao aliwataja kwa majina.
 
Alitoa amri ya kwamba popote wakionekana wauwawe hata ikiwa wamejificha ndani ya Al-kaaba. Miongoni mwa waliotajwa na Mtume (SAW) alikuwa Ikrimah, naye kusikia hukumu nzito ya Mtume (SAW) dhidi yake aliamua kutoroka kwa kujificha na kuelekea Yemen.
 
Mkewe Ikrimah, Umm Hakim, baadaye aliwenda kumuona Mtume (SAW) akiambatana na Hind bint Utbah, mkewe Abu Sufiyan na mama yake Muawiyah. Walikuwa na akina mama wengine wanaofikia kumi ambao walikwenda kwa ajili ya kiapo cha utii kwa Mtume (SAW).  Mtume Muhammad (SAW) alikuwa pamoja na wakeze wawili, mwanawe Fatma na baadhi ya kina mama wa ukoo wa Abdul-Muttalib.
 
Umm Hakim alitamka Kalimah, “Laa Ilaha ill allah Muhammad Rasuulu Llah” na kusilimu na baadaye alisema kumwambia Mtume (SAW) , “ Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Ikrimah (mume wangu) amekimbia Makka kwa kuhofia kwamba utamuuwa, nakuomba umpe msamaha na Mwenyezi Mungu atakupa hifadhi”. Mtume (SAW) akamjibu , “Amesemehewa”.  Kusikia hivyo Umm Hakim alifarijika na akatoka kuanza safari ya kwenda kumtafuta mumewe alikokimbilia. Katika safari hii alifuatana na mtumwa wake wa kigiriki.
 
Alifanikiwa kumuona Ikrimah kando kando ya bahari nyekundu (Red Sea) katika maeneo ya Tihammah . Akamwambia, “Ewe mume wangu nimekuja kwako kutoka kwa mtu mkarimu kabisa, muadilifu na mbora wa viumbe, Muhammad bin Abdullah, nimemuomba kukusamehe kwa hivyo nnakuomba usijidhuru”.
 
Ikrimah akauliza “Uliongea naye?” Umm Hakima akajibu, “Naam, na amekubali kukusamehe”.  Umm Hakim aliendelea kumhakikishia mumewe kwamba hakuna madhara yoyote atakayoyapata kwani amethibitishiwa hivyo na Mtume wa Allah.  Ikrimah alikubali na wakaanza safari ya kurudi Makka.
 
Walipokuwa njiani Ikrimah akaingiwa na hamu ya kutaka kustarehe na mkewe, lakini mkewe akamkatalia katakata, “La hasha siwezi kufanya hivyo kwani mimi ni muislam na wewe ni kafiri”.
 
Ikrimah alishtushwa sana na kauli hii ya mkewe na kumwambia,“kuishi na wewe bila ya starehe ni jambo lisilowezekana”.
 Wakati Ikrimah akikaribia kuingia katika mji wa Makka Mtume (SAW) aliwaambia Masahaba “Ikrimah ibn Abu Jahl atakuja kwenu kama muislam na muhajir, basi msimtukane baba yake kwani kuwatukana waliokufa ni kuzidi kuwatia huzuni walio hai wala hakuwafikii waliokufa”. 
Walipofika wakapelekwa moja kwa moja kwa Mtume (SAW).  Mtume alipowaona akasimama na kuwapokea na kuwasalimia kwa moyo mkunjufu.
 
“Muhammad!”, akasema Ikrimah,“ameniambia Umm Hakim kwamba umenisamehe”. Mtume (SAW) akajibu,“Ni kweli uko salama”.  Ikrimah akamuuliza Mtume (SAW), “ kitu gani unanilingania?”
 
“Ninachokulingania ni ushuhudie kwamba hakuna mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na mimi ni mjumbe wa Allah na usimamishe sala, utoe zaka, na utekeleze maamrisho yote ya dini” alisema Mtume Muhammad (SAW).
 
“Nnaapa kwa Allah” akasema Ikrimah, “hujalingania isipokuwa jambo la kweli, hujaamrisha (jambo) isipokuwa zuri, uliishi nasi kabla ya kuteremshiwa Wahy ukiwa msema kweli na muaminifu”. Akielekeza mkono wake kwa Mtume (SAW), “Nnashuhudia kwamba hapana Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (SW) na Muhammad ni mjumbe wake”.
 
Baada ya kutamka Shahada, Mtume (SAW) akamtaka atamke maneno haya pia, “ Ninamuomba Mwenyezi Mungu na wote waliokuwepo hapa mshuhudie kwamba mimi ni muislam na ni mujahid (mpiganaji) na muhajir (niliehama)”, Ikrimah akayarudia maneno haya kisha akasema kumwambia Mtume (SAW), “Ninakuomba uniombee msamaha kwa Allah (SW) kwa uadui na uovu nilikuwa nikiufanya na kwa matusi yote niliyokuwa nikiyatamka dhidi yako ulipokuwepo na ulipokuwa hupo.”
 Mtume (SAW) akamuombea dua “Ewe Mola nnakuomba msamehe uadui na uovu wote alionitendea na kwa jitihada yake yote ya kutaka kuizima nuru yako, nnakuomba umsamehe kwa yale yote aliyoyasema au kufanya kunivunjia heshima yangu wenyewe nikiwepo na nikiwa sipo.” 
Uso wa Ikrimah ukajaa bashasha na tabasamu kuona uadui wake wote alioufanya kusamehewa na Mtume na kuhakikishiwa usalama wake na hapo akaahidi mbele ya Mtume (SAW) na masahaba waliokuwepo.
 
“Nnaapa, ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu zile nguvu na juhudi zite nilizokuwa nikizitumia kuzuia njia ya Allah basi nitajitahidi kufanya mara mbili yake kwa ajili ya Allah na vita vyote nilivyopigana dhidi ya dini ya Allah nitapigana mara mbili yake kwa ajili yake”, alisema Ikrimah.
 
Tokea siku hiyo Ikrimah akawa mwenye kuitekeleza ahadi yake na kwa kutumia wakati wake mwingi msikitini na kusoma Quran, mara nyingi alikuwa  akionekana akiweka msahafu kwenye kipaji chake na kusema “Kitabu cha mola wangu, maneno ya mola wangu” na kuanza kutokwa na machozi kwa khofu ya Mwenyezi Mungu.
 
Na katika vita alikuwa safu za mbele kwenye Jihadi kwani alikuwa mpiganaji wa farasi stadi.  Katika vita vya Yarmuk alijitosa kishujaa kupigana na maadui.  Inasimuliwa kwamba wakati fulani waislam walizidiwa sana na hapo Ikrimah akapenya ndani ya ngome ya maadui kupambana nao mpaka Khalid bin Walid kuona hali hii akamkimbilia na kumwambia, “usiende zaidi Ikrimah kifo chako kitakuwa pengo kubwa kwa waislam.”
 
 “Wacha niendelee”, akajibu Ikrimah,“ Ulipata nafasi ya kuwa karibu na Mtume (SAW).Lakini mimi na baba yangu tulikuwa maadui wakubwa.  Hivyo niache nitoe kafara kwa yote niliyoyafanya kabla, kwani nilipigana na waislam katika vita vingi, jee! Leo niwakimbie hawa makafiri?” Akamalizia, “Hilo haliwezekani”.
 
Baada ya maneno haya akanadi kwa sauti kali iliyojaa ushujaa na wala isiyo na chembe ya woga na kusema, “Nani miongoni mwenu anaahidi kupigana hadi kufa?”
 
Waislam wapatao mia nne hivyi waliitikia mwito na kujitosa vitani bila ya kiongozi wao Khalid bin Walid, shambulio hili ndio lililofungua njia ya kushinda vita vya Yarmuk.
 
Baada ya kumalizika vita, kulikuwa na majeruhi takriban mia tatu miongoni mwao Al-Harith Ibn Hisham, Ayyash Ibn Rabiah, na Ikrimah.  Al-Harith aliomba maji na alipoletewa, Ayyash akamtizama jicho la kuyataka maji yale.  Harith akasema , “ mpeni Ayyash ”. Wakati wanamfikia Ayyash kumbe tayari alikuwa keshakata roho na waliporudi kwa Harith na Ikrimah nao pia wakawa tayari wameshafariki.
 
Masahaba wakawasalia mashahidi hawa, Mola amaridhie wote na kuwapa viburudisho kutoka chemchem ya kawthar huko peponi Amin.