014 - Hadiyth Ya 14: Kuzishikilia Sunnah Kwa Magego Ili Kubakia Imara Na Kujiepusha Na Ikhtilaaf


عن أبي نَجِيح الْعِرْبَاضُ  بن سارية (رضي الله عنه) قال: وَعَظَنَا رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم) مَوْعِظَةً بَلِيغَةً وَجِلَتْ مِنْهَا الْقُلُوبُ  وَذَرَفَتْ مِنْهَا الْعُيُونُ. فَقُلْنَا:  يَا رَسُولَ اللَّهِ كَأَنَّها مَوْعِظَةُ مُوَدِّعٍ فأوْصِنا. فَقَالَ: ((أُوصِيكُمْ بِتَقْوَى اللَّهِ وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وَإِنْ تأَمَّرَ عَلَيْكُم عَبْدٌ حَبَشِيّ, وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيَرَى اخْتِلاَفًا كَثِيرًا, فَعَلَيْكُمْ بِسُنَّتِي وَسُنَّةِ الْخُلَفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ, عَضُّوا عَلَيْهَا بِالنَّوَاجِذِ وَإِيَّاكُمْ وَمُحْدَثَاتِ الأُُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٌ ضَلاَلَةٌ)) رواه أبو داوود والترمذي وقال حديث حسن صحيح
Imepokelewa kutoka kwa Abu Najiyh Al-‘Irbaadhw bin Saariyah (رضي الله عنه) amesema: Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alitupa mawaidha mazito (yenye maana kubwa), nyoyo zikaogopa na macho yakabubujikwa machozi. Tukasema: Ee Mjumbe wa Allaah! Yanaonekana kama kwamba mawaidha ya kutuaga, basi tuusie.  Akasema: ((Nakuusieni kuwa na taqwa ya Allaah na kusikiliza na kutii japokuwa mtaongozwa na mtumwa Mhabashi. Hakika atakayeishi umri mrefu miongoni mwenu ataona ikhtilaaf nyingi. Kwa hiyo, shikamaneni na mwenendo wangu na mwenendo wa Makhalifa waongofu, yashikilieni kwa magego [mambo yao]. Na tahadharini na mambo yenye kuzushwa, kwani kila uzushi ni upotovu)).[1]
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Wajibu wa kumcha Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kufuata maamrisho na makatazo Yake. [Al-Anfaal 8: 46, Al-Ahzaab 33: 70, At-Tawbah 9: 119, An-Nuwr 24: 54, Muhammad 47: 33]. Na jambo hilo limepatiwa kipaumbele kwa kutajwa mwanzo kwa kuwa umuhimu wake ni mkubwa sana.
 
  1. Wajibu wa kumtii kiongozi anayeongoza kwa kufuata Shari’ah japokuwa ni mtu anayeonekana kuwa duni mbele yenu, na inapotokea ikhtilaaf, arudie mtu katika Qur-aan na Sunnah.
 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا
Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni (njia) bora na matokeo mazuri zaidi.[2]
 
  1. Hadiyth hii ni miongoni mwa miujiza ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kubashiria yatakayotokea, kwani zimeshadhihirika ikhtilaaf nyingi baina ya Waislamu.
 
  1. Kufuata amri za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) ni dalili ya mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى) na tahadharisho la kumkhalifu [Aal-‘Imraan 3: 31, An-Nuwr 24: 63].
 
  1. Umuhimu wa kufuata Sunnah za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuzishikilia bila ya kutoka nje ya mipaka na njia iliyonyooka ikapeleka kufarikiana Waislamu na kujitokeza makundi makundi. [Al-An’aam 6: 153].
 
  1. Kufuata Sunnah za Makhalifa Waongofu na kuamini kauli ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu Sunnah zao khaswa pale inapokuwa ni jambo walilolitenda wao bila ya kutendwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).
 
  1. Kujiepusha kabisa na Bid’ah (Uzushi), kwani hatari yake ni upotofu na motoni. [Hadiyth: ((Na kila upotofu unapeleka motoni)).[3]
 
  1. Vitendo vya bid’ah havina thamani wala havitapokelewa. [Rejea Hadiyth namba 15].
 
  1. Kuonyesha usawa ulioletwa na Uislamu baina ya waja bila kujali tofauti ya ukoo, kabila, utaifa na mwengineo. Ndio tukaamrishwa kumfuata kiongozi mchaji Allaah hata kama ni mtumwa.
 
  1. Utiifu kwa Amiri ni wajibu, maadamu hajakuamrisha jambo la kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى) na Mtume Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).
 
  1.  Fadhila za Maswahaba wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) waliopata hadhi ya kuwa Makhalifa baada ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).


[1]  Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh.
[2]  An-Nisaa (4: 59).
[3]  Muslim.