Kuadhini na Kukimu kwa Mwanamke



Je inajuzu kwa mwanamke kuadhini na kukimu wakati wa kusali sala za fardhi au jambo hili ni kwa wanaume tu?


Jawabu

Kwanza ni vyema tufahamu lengo la adhana ni kutoa taarifa ya kuingia kwa wakati wa sala na lengo la iqamah ni kujuulishwa kuanza kwa sala.

Pili kwamba kila jambo ambalo ameamrishwa mwanamme katika sheria basi na mwanamke nae pia ameamrishwa kama ilivyo haramu ikiharamishwa kwa mwanamme basi ni pia kwa mwanamke isipokuwa kama kutakuwa na dalili iliyo wazi katika Quraan au sunna  inayoelezea kinyume cha hayo

Hivyo katika ufafanuzi wa kina katika suala hili tutaangalia  kauli tofauti za maulamaa wa kizamani na wa karibuni kama ifuatavyo.

Katika Maulamaa wa kizamani:

 Ibn hazm anasema katika kitabu chake cha Al Muhallah 1/167:
 “Si lazima kwa mwenye kusali peke yake kuadhini au kukimu lakini kama ataadhini na kukimu basi ni vizuri”

Anasema Ibn Qudaamah katika kitabu chake cha al- Mughniy 1/438:

“Wala sijawahi kusikia mtu anaesema kinyume cha hayo.(yaani si lazima)”

Ahmed Ibn Hanbal anasema : “wakifanya hakuna kosa na wasipofanya  pia inajuzu”.
Kwa upande wa madhehebu ya kiShaafiy wanasema: “Kukimu kunapendeza kwa wanawake lakini si kuadhini”.

                                                    
Kwenye fataawa za karibuni

Llajnatul Fataawah Daaimah 6/84 :

“Mwanamke hajaamrishwa kuadhini au kukimu kwenye sala ikiwa atasali peke yake au hata wakisali jamaa”.

Majmoo Fataawa wa Maqalaat Mutannawiat 10/356 sh Ibn Baaz  aliwahi kuulizwa suala hili na alisema :

“Wanawake hawajaamrishwa kuadhini au kukimu, jambo hili ni la wanaume hivyo ni bora wasali bila ya adhana wala iqama.”

Sh. Ibn Uthaymin anasema (angalia fatwa –online):

“Wakifanya hivyo hakuna ubaya na wasipofanya pia hakuna ubaya kwa sababu kuadhini na kukimu kumewajibishwa  wanaume tu.”

Sh Albani anasema katika al-Haawee min Fataawa ash-Shaykh al-Albaanee / 184 :

“Hakuna tofauti katika hukumu za kisheria katika sala, funga, udhu, hijja na kadhalika. Hivyo yale yote yaliyowajibishwa kwa mwanamme basi yamewajibishwa kwa mwanamke mpaka kupatikane dalili ya kinyume cha hivyo. Kwa kutumia msingi huu hukumu ya adhana na iqamah itabaki kuwa wajibu kwa wote mpaka kuthibitike vyenginevyo.”

Maulamaa katika kufanya utafiti wa kina wanasema katika suala hili lipo jambo linalolifanya hukmu hii isiwe wajibu kwa mwanamke .  Kuadhini huwa kwa sauti kubwa na wanawake hawatakiwi kunyanyua sauti zao na pia Kuna hadithi iliyopokelewa na Asmaa binti Yazid inayosema:
                                                                                      ليس على النساء أذان ولا إقامة     
          “Wanawake hawana adhana wala iqaama”      


                                                 (al Mughniy 1/438)
Na kuna riwaya iliyosimuliwa na al bayhaqiy inayosema hivyo hivyo kutoka kwa  Abdullah Ibn Umar (Allah awawie radhi yeye na baba yake)

Tuziangalie hali zitazomkuta mwanamke:


Hali
Hukmu
1
Kuadhini na kukimu kwenye kundi la wanaume pekee
Haijuzu
2
Kuadhini na kukimu kwenye mchanganyiko wa wanaume na wanawake 
Haijuzu
3
Kuadhini na kukimu kwenye kundi la wanawake tu
Hakuna ubaya
4
Kuadhini na kukimu akisali peke yake
Hakuna ubaya
5
Kukimu tu bila ya kuadhini kwenye kundi la wanawake tu
mustahab(inapendeza)
6
Kukimu tu bila ya kuadhini akisali peke yake
mustahab(inapendeza)


Hata hivyo wanawake watakapoadhini watatakiwa waadhini kwa sauti itakayotosha kusikilikana kwa wale waliopo miongoni mwa wanawake tu . Pia sala itakuwa sahihi hata kama hapajaadhiniwa au kukimiwa kwa kufuata kauli za Maulamaa takriban wote kwamba jambo hili halijawajibika kwa mwanamke. 

Faida

Adhana zinazoadhiniwa kwenye Computers au T.V au saa zinazoadhini; zote hazina athari kwa muislamu kwamba ndio zimetosheleza . Lengo lake ni kujuulisha kuingia kwa wakati tu .Kwa mtazamo wa kisheria adhana hizi hazichukui nafasi ya adhana ya mwenye kutaka kusali. Muislamu atatakiwa aadhini mwenyewe kwani adhana ni ibada yenye fadhila na ujira mkubwa na wala adhana hii haitokuwa badala ya adhana ya kisheria .

Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) anasema:

و لو يعلم الناس ما في النداء والصف الأول ثم لم يجدوا إلا أن يستهموا عليه لاستهمو عليه
 متفق عليه
“Lau kama watu wangelijua yaliyomo ndani ya adhana na safu ya mwanzo kisha hawakuwa na budi ila kuyapata huku wakipigana vikumbo juu ya hayo basi wangelipigana vikumbo( kuyapata).”  
                                    Imesimuliwa na Bukhari na Muslim.

Na kama mume na mke watasali jamaa nyumbani pamoja, mwenye haki ya kuadhini na kukimu ni mume kwa sababu kwake hili jambo amewajibishwa na mwanamke hakuwajibishwa.

Wallahu Aalamu