(Kutoka katika kitabu صور من حياة الصحابة
cha Muandishi Dr, Abdurrahman Raafat Al-basha)
Kimefasiriwa na Ustaadh Talib Juma Ali
A
|
likuwa Abu
Al-‘Asi ibn Alrabiy Alabshamy kijana mzuri aliye mrembo mwenye mvuto kwa mwenye
kumuangalia, aliyezungukwa na neema, na mwenye nasaba iliyo bora. Hivyo
alielekea kuwa ni miongoni mwa mashujaa wa kiarabu kwa kila maana iliyoibeba
neno hili, akiwa ni mwenye murua na ahadi, na mwenye kila alama ya kujivunia
urathi wa wazee na mababu.
Alirithi Abu
al- ‘Asi kutoka kwa wazee, mapenzi ya biashara yaliyomo katika misafara miwili
ya “miongo ya kiangazi na kipupwe”.
Havikuwa
vipando vyake vyenye kukosekana au kuchoka kuwemo katika safari ya kwenda au
kurudi baina ya Makka na Sham. Msafara wake ulikuwa ni wenye kukusanya baina ya
watu wafikao mia mbili. Watu walikuwa ni wenye kumpa mali zao kufanyia
biashara, ziada ya mali yake, nayo ni kwa sababu ya uzoefu wake, ukweli na
uaminifu aliokuwa nao.
Khala
(Shangazi) yake, bibi Khadija mkewe Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam )
alimfanya mfano wa mwanawe ndani ya nafsi yake na aliwacha nyumba yake kuwa
wazi na kumkaribisha kwa furaha na mapenzi.Na hayakuwa mapenzi ya Mtume
(Salallahu ‘Alayhi Wasallam ) kwa Abu Al ‘Asi ni madogo kuliko ya bibi Khadija.
Siku zikawa ni
zenye kwenda haraka na kupita katika nyumba ya Muhammad ibn Abdillah na mtoto
wake mkubwa Zainab akawa tayari ameingia katika utu uzima na uwa la uzuri
kuchanua na kupelekea nafsi za watoto wa nyumba bora za Makka kuvutiwa nae. Kwa
nini isiwe hivyo?, wakati yeye ni mtoto bora wa nasaba miongoni mwa watoto wa
kike wa kikureish na mwenye baba na mama watukufu na ni mwenye adabu na tabia
njema? Lakini watampataje? Wakati Khala yake (Abu-al ‘Asi) amesimama mbele yao
kuwa ni kizuizi naye ni Abu Al‘Asi ibn Al rabiy kijana miongoni mwa vijana wa
Makka.
Haukupita muda
baada ya ndoa ya wawili hawa Zainab bint Muhammad na Al-‘Asi isipokuwa nuru ya
imani ya Allah Subhaanahu Wata’ala ikaangaza Mji wa Makka na Allah
Subhaanahu Wata’ala akamtuma Mtume wake Muhammad (Salallahu ‘Alayhi Wasallam )
na dini ya uongozi na ya haki na akamuamrisha kuwahadharisha jamaa zake wa
karibu na akawa wa mwanzo kuamini miongoni mwa wanawake ni mkewe bibi Khadija bint
Khuwaylid na watoto wake Ruqayyah, Ummukulthum na Faatimah licha ya kwamba
Faatimah alikuwa ni mdogo.
Bahati mbaya
mkwewe Abu al ‘Asi alichukia kuacha dini ya mababa na mababu zake. Hivyo
akapinga kuingia (dini) aliyoingia mkewe, bibi Zainab, licha ya kwamba alikuwa
ni mwenye kumpenda sana, mapenzi yaliyo safi na ya kweli.
Mivutano
ilipozidi baina ya Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam) na makureshi walisema
baadhi yao wakiambizana: “kwa nini mnamsaidia Muhammad kwa kukubali vijana wenu
wa kiume kuwaowa watoto wa Muhammad, laiti mngeliwaacha na kumrejeshea mwenyewe
angekuwa ni mwenye kuwashughulikia wao baada yenu”.
Wakasema Hakika
ni rai bora hiyo mliyoiyona wakamwendea Abu al ‘Asi na kumwambia: “muache mkeo
ewe Abu al-‘Asi na mrejeshe nyumbani kwa baba yake. Nasi tutakuozesha mwanamke
yeyote umtakae katika watoto wazuri wa kikureish”. Akawajibu; "hapana
wallahi; mimi simwachi, mke wangu na mimi sina nimpendae katika wanawake wote
wa dunia zaidi yake”.Ruqayyah na Ummukulthum wao wakaachwa na kurejeshwa kwake
Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam ) alifurahishwa kwa hilo, na alitamani laiti
Abu al-‘Asi nae angefanya walivyofanya rafiki zake. Na hakuwa na nguvu za
kumlazimisha kumuacha kwani ilikuwa bado hakujateremka amri ya kuharamisha ndoa
baina ya muislam mwanamke na mshirikina.
Alipohama Mtume
(Salallahu ‘Alayhi Wasallam ) kwenda Madina na shauku kumzidi juu ya mtoto
wake, na makureshi wakatoka kwa ajili ya kupambana na Mtume katika Badri, Abu
al-asi alilazimika kutoka nao, sio kwa lengo wala hamu ya kupambana na waislamu
au kwa kutaka chochote kile, bali ni kutokana na nafasi na cheo chake katika
kaumu yake ndiyo iliyompelekea kuwa ndani ya msafara huo.
Vita vya Badr
vilimalizika kwa kushindwa makureshi vibaya sana, vita ambavyo vilivunja kiburi
vya shirki na kuvunja ufedhuli wao. Miongoni mwao wakauwawa na wengine kutekwa
na wengine wakatoroka.
Miongoni mwa
waliotekwa ni Abu-al ‘Asi mume wa Zainab bint Muhammad (Salallahu ‘Alayhi
Wasallam). Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam), aliwawekea mateka wa vita hao fidya
kwa ajili ya kuzikomboa nafsi zao. Fidya hiyo ilikuwa ni baina ya dirham elfu
hadi elfu nne kulingana na hali na utajiri wa mateka huyo katika familia yake.
Ujumbe ukawa ni
wenye kuja na kurudi baina ya Makka na Madina, ukiwa umebeba mali za kukombolea
mateka wao. Bibi Zainab alituma nae mjumbe wake Madina akiwa amebeba fidya ya
kumkombolea mumewe Abu-alasi. Nayo ilikuwa ni mkufu aliopewa zawadi na mama
yake Bibi Khadija siku aliyoolewa.
Mtume
(Salallahu ‘Alayhi Wasallam) alipouona mkufu ule, vazi la huzuni liliugubika
uso wake mtukufu na akamtamani na kumhurumia sana mwanawe, hapo hapo aliwaambia
masahaba wake;
“Hakika Zainab
ametuma mali hii ili kuwa ni kikombolea cha Abu al‘Asi mkihisi kumwachia huru
Abu al ‘Asi na mkamrejeshea Zainab mali yake basi fanyeni". Masahaba
wakajibu papo hapo: "Hakika hilo ni ombi bora kutoka kwako Mtume wa
Allah".
Lakini Mtume
(Salallahu ‘Alayhi Wasallam) alimshurutishia Abu al ‘Asi kuachiliwa kwake.
Lazima kuambatane na kumrejeshea mtoto wake haraka haraka bila ya kuchelewa.
Abu al-‘Asi hakuingia Makka isipokuwa alianza kutekeleza ahadi yake. Akaamrisha
bibi Zainab ajitayarishe kwa safari na akamwambia msafara wa wajumbe wa Mtume
hawapo mbali na Makka wanamsubiri akamtayarishia mizigo na mnyama wake na
akamwakilisha ndugu yake ‘Amru ibn Al-rabiy kufuatana nae na kumfikisha kwa
wajumbe hao mkono kwa mkono. ‘Amru bin Al-rabiy akaitia pinde, mishale
alani, na kuvaa mabegani mwake na kumpandisha bibi Zainab ndani ya khawdaj[1]
tayari kwa safari na alitoka mchana mchana mbele ya macho ya makureshi, watu
wakaja juu na kumfuata na kuanza kumtisha na kumtia hofu.
Hapo ‘Amru
alitoa upinde wake na kutia mshale wake, akasema: “yeyote atakayejaribu
kumsogelea Zainab basi nitauachia mshale shingoni mwake”. Na ‘Amru alikuwa
mwenye shabaha asiekosea.
Abu Sufiyan
alikuwa ndio kwanza anafika alisema kumwambia ‘Amru: “Ewe mtoto wa ami yangu
rejesha mshale dhidi yetu tuzungumze na akarejesha" na Abu Sufiyan
akasema:
“Hakika
hujafanya jema kwa tendo lako hili kwani umetoka na Zainab mbele ya macho ya
watu, wakati waarabu wote wanajua kushindwa kwetu na yaliyotufika kwenye mikono
ya Muhammad. Ikiwa utatoka na mwanawe mbele ya macho ya watu kama ulivyofanya
makabila yatatusema kwa woga na watatushusha hadhi na kutukebehi na kutudharau.
Basi rejea nae na mwache kwa mumewe siku mbili tatu watu wakianza kusema kwamba
tumemzuia kutoka, hapo toka nae kifichoficho (kwa kujificha?) na mpeleke kwa
baba yake. Hakika sisi hatuna haja nae.”
‘Amru alikubali
hayo na kurudi nae Makka. Baada ya siku kupita akatoka nae usiku na kumfikisha
kwa wajumbe wa Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam) mkono kwa mkono kama
alivyousiwa na kaka yake. Abu al-‘Asi alikaa Makka baada ya kufarakana na mkewe
hadi ilipokaribia Fat-h (kukombolewa) Makka kwa muda mchache. Alitoka kwenda
Sham kwa ajili ya biashara. Alipokuwa akirejea Makka akiwa na wanyama (ngamia)
wafikao mia na watu wasiopungua mia na sabini walitokewa na kikosi miongoni mwa
vikosi vya Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam) kikiwa karibu ya Madina vikateka
wanyama na watu wake lakini Abu al‘Asi aliwahi kukimbia bila ya kutekwa.
Kiza kilipoingia
Abu al ‘Asi alijificha na kuingia Madina kinyemela mpaka akafika alipo
Zainab na akaomba himaya na akampa.
Alipotoka Mtume
(Salallahu ‘Alayhi Wasallam) wakati wa alfajiri kwa sala na akawa tayari
mihrabuni na analeta takbira ya kuhirimia na watu wakaleta takbira, sauti kali
ya Zainab iliita toka safu za wanawake ikisema:“Enyi watu mimi ni Zainab bint
Muhammad na nimempa himaya Abu al ‘Asi hivyo mlindeni.”
Baada ya Mtume
(Salallahu ‘Alayhi Wasallam ) kusali alisema: “Mmeyasikia niliyoyasikia"
wakasema: “ndiyo ewe Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam)”. Akasema: “Naapa na
yule ambae nafsi yangu imo mikononi mwake (Allah) hakika sikuwa na habari
yoyote ya haya mpaka pale niliposikia mliyoyasikia. Hakika muislamu anamlinda
yule aliye chini yake”.
Kisha akaondoka
kuelekea nyumbani kwake na akamwambia mwanawe:
“Mkirimu Abu
al‘Asi lakini tambua hakika wewe sio halali yako akawaita walioteka mali yake
na kuwaambia: “Hakika ni miongoni mwetu kama mjuavyo nanyi mmechukua mali yake.
Mkimtendea wema na kumrejeshea mali yake itakuwa ni katika tuyapendayo ama
ikiwa hamkurejesha itakuwa ni jumla ya - ngawira- ambayo Allah Subhaanahu
Wata’ala ameruhusu kwenu na mtakuwa ni wenye haki".
Wakasema: “Bali
tutamrejeshea mali ewe Mtume wa Allah” . Alipokuja kuchukua mali yake walimwambia:
“Ewe Abu al ‘Asi hakika wewe ni mbora katika makureshi na ni mtoto wa ami yake
Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam). na mkwewe jee huoni bora usilimu nasi
tutakurejeshea mali zako zote upate kutononeka na neema na mali za watu wote wa
Makka halafu wewe ubakie nasi Madina?" Akajibu: “Hakika ni wazo baya
mlilonipa kuanza dini mpya kwa woga.
Abu al ‘Asi
alitoka na wanyama wake na mali zake kuelekea Makka na alipofika alimpa kila
mwenye haki, haki yake na akasema: "Enyi makureshi jee yuko aliebaki na haki
yake kwangu hajaichukua?"
Wakasema:
“Hapana Mungu akujaze kheri na kila wema hakika wewe ni muaminifu na
mkarimu". Akasema: “Ama maadam nimetekeleza amana zenu na haki zenu, basi
nashuhudia kwamba hakuna anaestahiki kuabudiwa kwa haki ila Allah na Muhammad
ni Mtume wake. Wallahi hakuna kilichonizuia na uislamu kwa Muhammad Madina
isipokuwa ni hofu yangu kwamba mtanidhania kuwa nilitaka kula mali zenu. Ama
Allah Subhaanahu Wata’ala alipozirejesha kwenu na kujitakasa basi sasa
nimesilimu".
Kisha akatoka na
kuelekea hadi kufika kwa Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam) na akakirimiwa na
kurejeshewa mkewe akawa anasema Mtume (Salallahu ‘Alayhi Wasallam):
"Amesema akawa mkweli, akaniahidi akanitekelezea ahadi yangu".