Suhayl ibn Amr-mwana diplomasia
Kati kati ya vita vya Badr, Suhayl
(kipindi hicho bado ni kafiri) akajikuta ndani ya mikono ya waislam
mateka. Umar ibn Khattab akamwambia Mtume (SAW):
“Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu!
Niachie mimi nimng’oe meno yake mawili ya mbele ili asiweze tena kusimama na
kuweza kusema chochote dhidi yako baada ya hii leo.”
“Hapana Umar. Sitomfanyia mtu
yoyote ubaya asije Mwenyezi Mungu akanifanyia na mimi hata kama ni Mtume,”
akamtahadharisha. Akamwita Umar karibu yake na kumnong’oneza,
“Umar! Labda
Suhayl atakuja kufanya jambo siku za usoni litakuja kukufurahisha.”
Suhayl ni mtu mmoja maarufu katika
maquraysh. Alikuwa mzungumzaji mzuri na mara nyingi maoni yake hupewa
kipaumbele. Alifahamika zaidi kama ‘Khattaab’ msemaji mkuu wa
maquraysh. Umuhimu wake ulikuja kuonekana zaidi katika kukhitimisha ule
mkataba maarufu wa Hudaybiya.
Mwishoni mwa mwaka wa sita Hijriya,
Mtume (SAW) na kiasi cha masahaba elfu moja na mia tano walitoka Madina
kuelekea Makka kutekeleza ibada ya Umra. Kuonesha kwamba hawakukusudia vita,
waislam hawakuwa na silaha zozote ila panga zao tu viunoni. Pia
walichukua wanyama kwa ajili ya kuchinja kuonesha nia yao ni kuuzuru msikiti
mtukufu wa Makka.
Maquraysh walipopata habari ya
‘ugeni’ huu, haraka wakajiandaa kwa vita. Wakaapa kutowaruhusu waislam
kuingia Makka. Akatumwa Khalid ibn Walid (alikuwa bado kusilimu wakati
huo) na jeshi la farasi kwenda kuwazuia. Jeshi la Makafiri likawasubiri sehemu
moja iitwayo Karral Ghamim.
Mtume Muhammad (SAW) alipata habari
za Khalid mapema kama anawasubiri. Licha ya kuwa na uhasama dhidi yao, muda huu
Mtume (SAW) hakuwa tayari na vita hivyo akauliza:
“Kuna mtu yoyote anayejua njia nyengine
ya kufika Makka ili kuepukana na Maquraysh.
Mtu mmoja wa kabila la Aslam akasema
anaijua na kuwapitisha waislam njia nyengine ya taabu kwenye milima ya Warrah
na hatimaye kuukaribia Makka kutoka upande wa kusini. Khalid alipogundua
kwamba amepigwa chenga akatahayari na kujirudia zake Makka.
Mtume (SAW) akapiga kambi Hudaybiya
na kuwaashiria kwa maquraysh yuko tayari kwa suluhu kama watataka.
Maquraysh wakamtuma Badil ibn Warqa pamoja na watu wengine wa kabila la Khuzaa
kuulizia nini lilikuwa lengo la ujio huu. Alikutana na Mtume (SAW) na
baadaye kurudi kwa Maquraysh na kuwataarifu nia njema ya Mtume (SAW) na
masahaba zake. Hawakumuamini wakisingizia Banu Khuzaa ni masahiba wa
Muhammad wakauliza:
“Hivi anakusudia kuja na jeshi lote
hili kufanya Umra tu? Waarabu watasikia ametujia na kuingia Makka kwa
nguvu wakati hali ya kivita bado ipo baina yetu. Wallahi hilo
halitotokezea bila ya rukhsa yetu.
Maquraysh wakapeleka ujumbe mwengine
chini ya Halis ibn Alqamah, mkuu wa kabila la Ahabish, masahiba na
Maquraysh. Mtume (SAW) alipomwona Halis anakuja akasema, “Huyu mtu
anatoka katika watu wanaothamini kuchinja wanyama. Watangulizeni wanyama wote
ili apate kuwaona. Hilo likafanyika, Halis akapokewa na waislam kwa
talbiya:
“Labbayka llahumma Labbayka” na
alipowajibu akasema kwa mshangao, “Sub-hana Allah watu hawa hawana sababu
ya kuzuiliwa kuingia Makka ikiwa wenye wagonjwa ya ukoma na punda wanaruhusiwa
kuhiji iweje mtoto wa Al Muttalib azuiwe kuizuru nyumba ya Mwenyezi Mungu
(SW)?”
Wallahi, Mola wa Alkaaba waache
Maquraysh wahilikishwe. Hawa watu wamekuja kutekeleza ibada ya Umra.”
Aliporudi na kuwataarifu maquraysh
wakamrudi, “hebu kaa chini wewe ni mbedui tu wa kiarabu, hujui lolote juu ya
mbinu wala njama?”
Akatumwa mjumbe mwengine Urwah ibn
Masoud mkuu wa kabila la Atthaqaf toka Tail. Alipofika akamwambia Mtume
Muhammad (SAW):
“Ewe Muhammad umewakusanya watu wote
hawa na kurudi sehemu uliyozaliwa. Maquraysh wameapa kwa Mungu kwamba
Makka hutoingia kwa nguvu. Nnaapa hawa watu wote watakuasi.” Abubakar
kusikia vile akamwendea Urwah na kumbeza, “Tumuasi Muhammad? Adhabu iwe juu
yako.”
Wakati Urwah akiongea alimgusa Mtume
(SAW) ndevu zake. Mughira ibn Shubah akamkwapua mkono wake, “ondoa mkono wako
hapa!”
Urwah akajibu :”Adhabu iwe juu yako
mtu katili sana wewe, ” Mtume (SAW) akatabasamu. Urwah akauliza, “ni nani
huyu yaa Muhammad?”
“Ni binamu yako Al-Mughira”
“Hana adabu” Urwah akaendelea
kumwagia matusi.”
Urwah akaanza kuwakagua masahaba wa
Mtume (SAW) akagundua wakipewa amri, hutii tena kwa haraka. Akitaka
kutawadha au kuoga, masahaba kushindana kila mtu akitaka kumpelekea maji.
Wakiongea mbele yake, huongea kwa sauti ya chini chini na hata hawamuangalii
usoni kwa kumheshimu.
Naye aliporudi, akaelezea jinsi
alivyovutiwa nao:
“Enyi Maquraysh! Nilikwenda
kumtembelea Chosroes kwenye milki yake, nilimuona Qaysar (Caesar) mtawala
wa kibizantini kwenye kilele cha utawala wake, lakini sijawahi kumuona mfalme
mbele ya watu wake kama Muhammad mbele ya masahaba. Nimewaona watu ambao
hawana hata nia ya kumuasi seuze dhamira ya kumgeuka. Fikirieni sana
msimamo wenu huu amekuleteeni mwongozo wa haki, kubalini alichokuleteeni,
ushauri wangu unatoka ndani ya moyo wangu……….
Sidhani kama mtapata ushindi dhidi
yake milele!”
“Usiseme hivyo,” Maquraysh
wakadakia, “Tutamwambia arudi zake Madina na aje mara nyengine wakati ujao.”
Wakati huo huo, Mtume Muhammad (SAW)
akamtuma Uthman ibn Affan kwa Maquraysh kuwafahamisha lengo na madhumuni ya
safari yake Makka, na pia kuwaomba wawaruhusu kwani wanataka pia kuwakagua
jamaa zao. Uthman pia alikuwa na lengo la kuwashajiisha wale dhaifu wa
Makka waliobaki na kutofanya Hijra na kuwataarifu kwamba fat-h inakuja karibu……
Uthman akafikisha salamu za Mtume
(SAW) kwa Maquraysh na bado wakashikilia msimamo wao wa kutoruhusu kuingia
Makka. Wakamwambia Uthman kwamba anaweza kufanya Tawwaf Al kaabah.
Uthman akawajibu kwamba hilo halitowezekana kwani hatoweza yeye kutufu wakati Mtume
wa Mwenyezi Mungu anakatazwa. Wakamkamata Uthman na kumsweka ndani
mahabusu.
Uvumi ukazuka kwamba tayari
ameuwawa. Mtume aliposikia akabadilika ghafla. Akasema:
“Hatutoondoka mpaka tupigane.”
Akawatolea khutba na kuwataka
wafanye bay-ah- kiapo cha utii cha kuwa tayari kupigana. Wakakusanyika
watu pale Mtume alipokaa na wote kuapa kuwa tayari kwa vita. Muda mfupi
baadaye, Mtume (SAW) akathibitisha kwamba ulikuwa ni uvumi tu.
Kufikia hali hii ndipo Maquraysh
wakamtuma Suhayl ibn Amr. Ujumbe wake ni mfupi tu:
“Mtume arudi Madina.” Uteuzi
wa Suhayl kwa shughuli hii ulikuja kutokana na sifa zake za kuwa msemaji na
mzungumzaji mzuri na mpatanishi wa kutegemewa.
Mtume Muhammad (SAW) alipomuona
Suhayl anakuja akajua kwamba msimamo wa Maqurash unaelekea kubadilika,
“sasa wanataka upatanishi ndio
maana wamemtuma mtu huyu.”
Mazungumzo yalikuwa marefu na
hatimaye wakafikia makubaliano ya kimsingi. Umar na baadhi ya masahaba
hawakufurahishwa na masharti ya makubaliano hayo wakiona kama kwamba
hayatawasaidia waislam na ni ushindi kwa makafiri. Mtume (SAW)
akawahakikishia kwamba hivyo wanavyodhani sivyo, kwani Mtume (SAW) hawezi
kubisa kwenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na Mwenyezi Mungu mtukufu
hatomuacha mkono. Akamwita Ali ibn Talib aandike masharti ya mkataba:
“Andika Bismillahir Rahmanir
Rahiim.”
Suhayl akaruka, “siijui hii.”
“Andika badala yake, Bismika
Llahumma.”
Mtume akakubali, kasha akasema
andika haya yafuatayo:
“Ndivyo walivyokubali
kati ya Muhammad mjumbe wa Mwenyezi Mungu na Suhayl ibn Amr…………..
Suhayl hakukubaliana naye, “kama
nikishuhudia ya kwamba hakika wewe ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu nisingelipigana
nawe. Andika badala yake jina lako na la baba yako.” Na hili pia Mtume
(SAW) akalikubali, na kumuagiza Ali aandike:
“Haya yafuatayo ndivyo
walivyokubaliana kati ya Muhammad ibn Abdullah na Suhayl Ibn Amr………..
Kusimamisha vita kwa muda wa
miaka kumi ambapo watu waishi kwa amani na kujiepusha kudhuriana.
Kwamba, yoyote miongoni mwa
Maquraysh akija kwa Muhammad bila ya idhini ya walii wake, Muhammad amrudishe
na yoyote ambaye yuko na Muhammad akienda kwa Maquraysh wao hawatomrudisha…..
Suhayl aliweza kuwafanya Maquraysh
wawe na pahala pa kuweka uso wao kwani ni dhahiri kwamba alivutia upande wa
Maquraysh huku Mtume (SAW) akimvumilia.
Miaka miwili baada ya mkataba wa
Hudaybiya katika mwaka wa nane Hijiriya Maquraysh wakakiuka masharti .
Waliwaunga mkono Banu Bakr katika umwagaji wa damu dhidi ya Khuzai ambao
walikuwa wakimuunga mkono Mtume (SAW)
Mtume (SAW) akaitumia nafasi hii
kufanya safari ya Makka lakini lengo halikuwa kulipiza kisasi. Waislam
elfu kumi walifanya safari hii na kuingia Makka ndani ya mwezi mtukufu wa
Ramadhani Maquraysh walipoliona jeshi la waislam hawakuwa na ubavu wa kulizuia
na mji wa Makka kusalimu amri kwa Mtume Muhammad (SAW). Mtume (SAW)
akatangaza msamaha na kuwaita viongozi wa Maquraysh:
“Enyi Maqurysh, mnafikiri
nitakufanyeni nini?”
Suhayl ibn Amr akajibu, “Tunafikiria
utatutendea wema.”
Tabasamu likatanda kwenye uso wa
Al-habib Mustafa (SAW) kisha akasema,
“Idh-habuu….wa antum
attulaqaa. ( Nendeni mko huru)”
Kusikia habari hii ya kuachiwa huru
tena bila ya kutarajia, Suhayl ibn Amr akatangaza kusilimu kwake pale
pale. Bila ya shaka imani yake wakati ule haikuwa imani ya mtu
alieshindwa na kukata tamaa bali kama itakavyokuja kuonekana baadaye, ilikuwa
kwa ajili ya uislam na kwa ajili ya upendo kwa Al-habib Mustafa (SAW).
Wale wote waliosilimu siku ya Fat-h
Makka walipewa jina la ‘attulaqaa’ walioachiwa huru. Waliona jinsi
walivyokuwa na bahati na wengi wao wakijitolea kwa hali na mali kwa ajili ya
uislam ambao muda wote walikuwa wakiukandamiza.
Miongoni mwao ni Suhayl Ibn Amr.
Uislam ulimjenga upya. Sifa
zake zote alizokuwa nazo zikapata msukumo mpya na kuwa bora na bora
zaidi. Kwa ufupi tu sifa zake zinaweza kutajwa kama ifuatavyo: mkarimu,
mpole, mtekelezaji sala, mfungaji, msomi wa Quran na kadhalika. Huyu ndie
Suhayl aliekuja fahamika. Licha ya kuchelewa kusilimu, Suhayl alibadilika
na kuwa mcha mungu na mpiganaji jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtukufu.
Habari za kufariki kwa Mtume (SAW)
zilipofika Makka ambapo Suhayl alikuwa akiishi, waislam waliingiwa na mtafaruku
Madina na hata Makka. Abubakar Siddiq alijitahidi kutuliza hali hii
Madina kwa usemi wake maarufu.
“Yoyote aliyekuwa anamuabudu
Muhammad, basi Muhammad amekufa. Na yeyote anaemuabudu Mwenyezi Mungu
basi Mwenyezi Mungu (SW) yuhai na wala hatokufa milele.”
Mjini Makka, Suhayl akawa na jukumu
hilo hilo la kuwatuliza waislam. Akawaita waislam na kuwapo taarifa za
kifo cha Mtume Muhammad (SAW) na kuwahakikishia kwamba Muhammad alikuwa mjumbe
wa Mwenyezi Mungu (SW) na kama amefariki basi atakuwa tayari amekamilisha ile
kazi aliyopewa ya kuwalingania watu na kuitangaza dini ya Mwenyezi Mungu
mtukufu. Na ni wajibu wa waislam kuiendeleza kazi hii baada ya kufa kwake
na kuyachukua maisha yake yote kwa ‘Qudwah’ ruwaza na mfano wa kuiendeleza kazi
hii.
Siku hii ndiyo ile siku aliyoitabiri
Mtume Muhammad (SAW) pale alipomwambia Umar alipotaka kumng’oa jino Suhayl,
“Mwachie, labda kuna siku atakuja kukufurahisha.”
Habari hizi za ‘khutba’ nzito ya
Suhayl kwa waislam wa Makka zilipofika Madina, Umar ibn Khattab akamkumbuka
Mtume (SAW). Ni ile siku ambayo meno mawili ya mbele ya Suhayl yaliyotaka
kutolewa naye yamefaidisha umma wa Mtume Muhammad (SAW).
Aliposilimu Suhayl alijiwekea
nadhiri ifuatayo kwa ufupi:
Kuzidisha juhudi kuutumikia uislam,
kwa uchache basi kama alivyofanya alipokuwa kafiri, alipokuwa akimshirikisha
Mwenyezi Mungu alipoteza muda wake mwingi mbele ya masanamu. Akawa
anatumia muda wake mwingi pamoja na waumini mbele ya Mungu mmoja tu, akisali na
kufunga.
Kabla ya kusilimu, Suhayl alishiriki
kwenye vita vingi dhidi ya Uislam. Sasa akawa dhidi ya ukafiri na
alipigana kwa moyo mmoja dhidi ya waajemi Persia na ukandamizaji uliokuwa
ukifanywa na utawala wa Kibizantini.
Akawa na ari, alitoka kuelekea Syria
pamoja na waislam na kushiriki kikamilifu kwenye vita vya Yarmuk vita
viliyokuwa vikubwa na vya kutisha katika histora ya kiislam.
Suhayl alikuwa akikupenda sana
Makka. Hata hivyo, baada ya ushindi wa waislam Syria akakataa kata kata
kurudi Makka huku akisema:
“Nilimsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu
(SW) akisema,
‘mtu yoyote anaetoka fi sabili Ilah
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa muda wa saa moja tu basi ni bora kwake kuliko
shughuli za maisha yake yote alizojishughulisha akiwa nyumbani kwake.”
Akaahidi, “Nitakuwa ‘muraabit’
(niliyejifunga) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mpaka kufa kwangu na sitorudi tena
Makka.