Barakah-mama mlezi wa Mtume Muhammad (SAW)
Hatuna data za uhakika kuweza kujua
vipi huyu binti wa kihabashah aliishia Makka kuuzwa. Hatumjui asili yake,
wazazi na nasaba yake. Kama walivyokuwa watoto wengi wa kike na kiume,
waarabu na wasiokuwa waarabu walikamatwa na kuletwa kwenye soko la watumwa
Makka.
Baadhi yao yaliwakumba mambo mengi
tu kuishia kuwa chini ya wakubwa na ‘mabibi’ wakatili na kutumika kama punda
bila ya kujali watu wakarimu na wanaojali.
Barakah, binti wa Kihabashah,
alibahatika . Alifika nyumba ya Abdullah ibn AbdulMuttalib.
Alikuwa mtumishi pekee nyumbani kwake na Abdullah alipomuoa bibi Aminah
aliendelea pia kumhudumia.
Kwa mujibu wa Barakah, wiki mbili tu
baada ya ndoa ya Abdullah na Amina, baba yake Abdullah, Bwana Abdul Muttalib
alikuja nyumbani na kumtaka mwanawe aambatane na msafara wa biashara uliokuwa
ukielekea Syria. Bi Amina alisikitika sana na kuanza kulia:
“Mambo gani haya! Mambo gani haya!
Vipi mume wangu aondoke na mimi ndio kwanza bi harusi na hata hina bado
haijatoka mikononi mwangu?”
Kuondoka kwake kulikuwa pigo kubwa
kwa Bi Amina, hakuweza kulistahamilia kwani hapo hapo alipoteza fahamu.
Barakah anaendelea:
“Nilipomuona bi Amina hana fahamu,
nikalia kwa sauti kubwa na ya kusikitika; Ewe bibi yangu! Bi Amina akafungua
macho huku akitokwa na machozi na kusema, nipeleke kitandani”
Bi Amina alibaki kitandani kwa muda
mrefu na hakutaka kuzungumza na mtu yoyote, hakutaka kumuona mtu yoyote
anayetembelea isipokuwa Abul Muttalib mkwewe. Miezi miwili baada ya
safari ya Abdullah, Bi Aminah akaniita siku moja alfajiri huku uso wake umejaa
tabasamu na kuniambia:
“Barakah! Nimeota ndoto ya ajabu.”
“Kuna jambo zuri, bibi yangu.”
Aliendelea “Nimeona nuru imetoka
tumboni mwangu ikamurika milima, majabali na mabonde yanayoizunguka Makka.”
“Ni mja mzito nini bibi yangu.”
“Naam, Barakah! Lakini sijihisi
kuumwa umwa kama wanavyokuwa wanawake wengine.”
“Utazaa mtoto ambaye ataleta kheri”
akamalizia Barakah
Muda wote ambao Abdullah alikuwa
safarini Bi Aminah alikuwa mnyonge sana. Muda wote Barakah alikuwa
naye na kumliwaza huku akimchangamsha kwa riwaya na hadithi.
Bi Amina alisikitishwa zaidi pale
mkwewe, Bwana Abdul Muttalib alipokuja siku moja na kumtaka aondoke nyumbani na
kwenda milimani kama watu wote wa Makka wanavyofanya kwani mtawala wa Yemen
alikuwa akijiandaa kuivamia Makka.
Amina alilalamika hali yake ya uja
uzito na hana nguvu za kuelekea huko milimani. Abdul Muattalib alikasirika
sana lakini Bi Amina wala hakuwa na woga wowote.
Usiku na mchana, Barakah alikaa na
Bi Amina. Barakah anasema:
“Nilikuwa nikilala chini ubavuni mwa
kitanda cha Bi Aminah na husikia kuugua kwake usiku huku akimtaja mumewe.
Akiugua hunifanya niamke na hujaribu kumliwaza na kumpa moyo.”
Kundi la kwanza, likarudi kutoka
Syria na kupokelewa kwa hoi hoi na vifijo na familia za wafanya biashara
Makka. Barakah alikwenda kwa kujificha hadi nyumbani kwa Bwana Abdul
Muttalib kujua habari za Abdullah. Hakukuwa na habari zozote.
Akarudi kimya hadi nyumbani na wala hakumwambia lolote Bi Aminah asijea kazidi
kuchanganyikiwa. Baada ya kundi zima likarudi bila ya Abdullah.
Zilipofika habari za kufariki kwa
Abdullah, Madina. Barakah alikuwepo kwa Bwana Abdul Muttalib na
anasimulia:
Nilipiga ukelele huo niliposikia na
sikujijua tena nikatoka mbio hadi nyumbani kwa Bi Amina nikipiga kelele na
kulalama kwa kuwa hatunae tena duniani. Kulalama kwa kuwa kipenzi chetu
ambaye tulikuwa tukimsubiri kwa muda mrefu, na kulalama kwa mmoja katika vijana
watanashati wa Makka keshatutoka.
“Bi Amina alipopata habari akapoteza
fahamu na nikakaa karibu naye akiwa katika hali ambayo si hai na wala si
maiti. Hakukuwa na mtu mwengine zaidi yetu. Nikamuuguza usiku na
mchana mpaka alipojifungua mtoto wake.
Alipozaliwa, Barakah ndiye
aliempokea na kuwa mtu wa kwanza kumpokea mtoto. Na alipokuja babu yake
Abdul Muttalib akampa jina la Muhammad na akamchukua hadi Al-kaabah na wakaazi
wote wa Makka wakafurahi kuzaliwa kwa Muhmmad.
Barakah akaendelea kukaa na Bi Amina
pale Muhammad alipopelekwa ‘Badiyyah’ jangwani kulelewa na Bi Halima.
Aliporudishwa akiwa na umri wa miaka kama mitano hivi. Mama yake
alimpokea kwa furaha na upendo na Barakah kumkaribisha kwa hamu.
Muhammad alipokuwa na miaka sita
mama yake akaamua kuzuru kaburi la mumewe Yathrib. Barakah na Bwana Abdul
Muttalib walijaribu kumshawishi asifanye safari hii. Bi Amina hakukubali
ushauri wao. Siku moja asubuhi wakatoka Bi Amina, Muhammad na Barakah
wakapanda ngamia, wakiwa ni miongoni mwa msafara mkubwa wa biashara ukielekea
Syria.
Msafara ulichukua siku kumi kufika
Yathrib. Muhammad akabaki kwa wajomba zake wa Banu Najjar wakati Bi
Aminah akifanya ziara kila siku katika siku chache alizokuwepo Madina, Bi Aminah
alitembelea kaburi la mumewe huku akiwa na huzuni.
Na walipokuwa njiani kurudi Makka,
Bi Aminah akapatwa na homa kali. Walipofika Al-Abwa, mji uliopo kati kati
ya Makka na Yathrib, walisimama. Hali ya Bi Aminah ilizidi kuwa mbaya na
joto lake kupanda. Homa ikapanda kichwani, akamwita Barakah kwa sauti ya
kukohoa kohoa. Barakah anasimulia:
Akanieleza kwa sauti ya chini, “Ewe
Barakah, ninaona kama karibu nitaondoka duniani. Ninamuaacha mwanangu
umlee. Baba yake alikufa wakati yuko tumboni. Hivi sasa hapa
anampoteza mama yake mbele ya macho yake. Uwe kama mama yake na usimwache
kabisa!”
“Moyo wangu ukaishiwa na nguvu na
nikaanza kulia kwa kwikwi mpaka mtoto akashtuka na yeye kuanza kulia.
Akajirusha na kumkumbatia mama yake kwa nguvu huku mama anakata roho.”
Barakah akarudi Makka na mtoto
yatima, hana baba wala mama na kumpeleka kwa babu yake Bwana Abdul
Muttalib. Alikaa hapo kwa ajili ya kumlea na miaka miwili baadaye
alipokufa babu yake alikwenda naye pamoja kwa ami yake Abu Talib.
Aliendelea kumshughulikia mpaka
akawa mkubwa na kuoa. Barakah naye akamfuata Muhammad kwenye nyumba ya Bi
Khadija. “Sijawahi kumuacha na wala yeye hajawahi kuniacha,”
alisema.
Siku moja alikuja Muhammad (SAW) na
kumwita
“Ya, Ummah! (siku zote alimwita
mama). Mimi nimeshaoa na wewe bado hajaolewa. Unaonaje akija mtu
kukuposa.?”
Barakah akamwangalia Muhammad na
kusema, “Sitokuacha hata kidogo, hivi mama anamtupa mwanawe?”
Muhammad akatabasamu na kumbusu
kwenye kichwa chake na akamtizama mkewe Bi Khadija na kumwambia.
“Huyu ndiye
Barakah. Huyu ni mama yangu baada ya mama yangu. Ni sehemu ya ukoo
wangu.”
Bi Khadija akamwambia Barakah,
“Barakah! Umeupoteza ujana wako kwa ajili ya Muhammad naye sasa anataka
kukulipa baadhi ya fadhila zako, kwa ajili yangu na yake, kubali uolewe kabla
ya uzee kukufika.”
“Niolewe na nani mie?” Akauliza
Barakah.
“Kuna Ubayd ibn Zayd wa kabila la
Khazraj kutoka Yathrib amekuja kukuposa. Tafadhali usikatae.”
Barakah alikubali na akaolewa na
kwenda Yathrib kwa mumewe. Akajaaliwa mtoto wa kiume na kumwita
Ayman. Tokea hapo watu wakamwita ‘Umm Ayman.”
Kwa bahati mbaya ndoa yake haikudumu
kwani mumewe alifariki na yeye kujirudia zake Makka kwa ‘mwanawe’ Muhammad
nyumbani kwa Bi Khadijah. Katika nyumba hiyo pia walikuwepo Ali ibn
Talib, Hindi (mtoto wa Bi Khadija kwa mumewe wa kwanza na Zayd ibn Harith.
Zayd ni mwarabu wa kabila la
Kalb. Alikamatwa alipokuwa mdogo na kuletwa Makka kuuzwa soko la
watumwa. Alinunuliwa na jamaa yake Bi Khadija. Zayd akajikuta yupo
karibu mno kwa Muhammad mpaka uhusiano wao ukawa kama wa baba na mwana.
Na pale baba yake Zayd alipokuja Makka kumtafuta mwanawe, Zayd alipewa jukumu
la kuchagua kama kukaa na Muhammad au kwenda kwa baba yake. Majibu yake
yalikuwa ni haya:
“Katu sitomwacha mtu huyu. Yale
mambo aliyomtendea ni sawa na baba anavyomtendea mtoto wake. Hakuna hata siku
moja niliyojihisi kama mtumwa. Na amenishughulikia vizuri tu, ni mpole na
mwenye upendo na kuhakikisha kwamba nipo katika furaha. Ni mtu mmoja
mpole wa ajabu na mbarikiwa katika viumbe. Vipi nimwache ili niende na
wewe?……..katu sitomwacha.
Baadae, Muhammad akamwambia uko
huru. Hata hivyo, Zayd aliendelea kuishi naye na kuwa sehemu ya
familia.
Wakati Mtume (SAW) alipoteremshiwa
wahy. Barakah na Zayd walikuwa ni miongoni mwa watu wa mwanzo
kusilimu. Walipata pia mikiki na mateso ya Maquraysh kama walivyokuwa
waislam wa mwanzo.
Barakah na Zayd walikuwa na umuhimu
wao mkubwa enzi hizo. Walikuwa kama mashushushu kwani walijitolea
kustahamili mateso na adhabu za Maquraysh ili kupata habari za mkakati na mbinu
za Makafiri.
Siku moja, Makafiri wakafunga njia
zote zinazoelekea kwa Al-Arqam ambapo Mtume Muhammad (SAW) huwakusanya masahaba
na kuwafundisha dini ya kiislam. Bi Khadija akawa na ujumbe muhimu kwenda
kwa Mtume (SAW). Akamtuma Barakah, Barakah akayahatarisha maisha yake kwa
kuweza kupenya mtego huu wa Maquraysh na kufika kwa Mtume Muhammad (SAW) na
kumfikisha ujumbe Mtume (SAW), Mtume akatabasamu na kumwambia:
“Umerehemewa, Umm Ayman.
Bila ya shaka una pahala pako peponi.”
Alipoondoka Mtume (SAW) akawauliza
masahaba,
“Ikiwa mtu anataka kuoa
mwanamke katika watu wa peponi basi na amuoe Umm Ayman.”
Masahaba wote wakanyamaza kimya na
hakuna yoyote aliyesema kitu, Umm Ayman hakuwa mzuri wa sura wala
hakuvutia. Umri wake ulikuwa ni miaka Khamsini na keshaanza
kuzeeka. Licha ya hivyo Zayd ibn Harithah akajitokeza na kusema:
“Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu mini
nitamuoa Umm Ayman, ni bora yeye kuliko wanawake walio na uzuri na hadhi.”
Wakaoana na kujaaliwa mtoto wa kiume
na wakamwita Usamah. Mtume (SAW) alimpenda sana Usamah na alikuwa
akicheza naye, akimbusu na kumlisha. Tokea utotoni kwake Usamah
alijitolea nafsi yake kwa ajili ya Uislam na baadaye akaja kupewa majukumu makubwa
na Mtume (SAW).
Pale Mtume (SAW) alipohamia Yathrib
ambayo ikaja kujulikana kama Madina, alimwacha Umm Ayman Makka kwenye nyumba
yake kwa shughuli fulani. Baadaye Umm Ayman akaifanya safari hii peke
yake. Ilikuwa safari ya taabu na mashaka akikata majagwa, majabali na
milima. Joto lilikuwa kali, mchanga unaunguza, vumbi linatimka na
alistahamili yote hayo mpaka kuwasili Madina. Alipofika miguu yake
ilikuwa imevimba, uso wake hatuamaniki kwa vumbi na michanga.
“Ya Umm Ayman! Ya Umm Ayman! (Oo Umm
Ayman, oo mama yangu) Bila ya shaka una pahala peponi.”
Alitamka Mtume (SAW) pale alipomuona
Mtume (SAW) akamfuta uso wake na kumkanda miguuu na mabega.
Ummm Ayman alishiriki kikamilifu
katika kuushughulikia Uislam Madina. Katika vita vya Uhud, aliwashughulikia
majeruhi na kuwagawia maji. Alishiriki kwenye vita vya Khaybar na Hunayn
pamoja na Mtume (SAW).
Mwanawe Ayman alikufa shahidi kwenye
vita vya Hunayn. Mumewe Zayd alikufa shahidi kwenye vita vya Mut a huko
Syria. Kipindi hicho Barakah alikuwa na miaka sabini na muda mwingi
alikuwepo nyumbani. Mtume (SAW) akifuatana na Abubakar na Umar humtembelea mara
nyingi na humuuliza, “vipi hali yako hujambo?”
Naye hujibu, “sijambo, ewe mjumbe wa
Mwenyezi Mungu maadam uislam upo na unaendelea!
Alipofariki Mtume (SAW), Barakah
alikuwa akionekana mara nyingi kutokwa na machozi na anapoulizwa kwa nini unali
hujibu; “Wallahi, nilijua kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu atakufa lakini ninalia
kwa sababu (kifo chake) ndio mwisho wa kuteremshiwa Wahy kwetu.”
Barakah alikuwa mtu mmoja muhimu
sana kwani ni mtu pekee aliekuwa karibu na Mtume (SAW) katika maisha yake yote
tokea kuzaliwa kwake mpaka kufariki. Alifariki enzi za Ukhalifa wa
Uthman.
Ndio, asili yake haikujulikana
lakini mahala pake peponi tayari amethibitishiwa.