Ammaar bin YaasirPepo Ilikuwa na Hamu Naye |
Alitoka baba yake
Ammaar, Mzee Yaasir Yemen kuja Makkah
kumtafuta kaka yake. Na baadae akapafanya Makkah ndiyo makaazi yake akiwa chini
ya Hudhyafah Ibn Mughiyrah. Na ni Hudhayfah
aliemshauri Yaasir kumuoa mmoja wa wajane aliokuwa nao Sumayyah
bin Khiyaat. Na katika ndoa hii alizaliwa ‘Ammaar.
Familia hii ilikuwa
ni miongoni mwa familia za mwanzoni kusilimu pale alipowalingania Mtume Salla
Allahu ‘Alayhi Wasallam dini na kuongoka katika kufuata dini ya haki.
Tatizo lililokuwepo
Makkah wakati huo ni kuangaliwa aliesilimu anatoka katika ukoo wa aina gani.
Wakiwa miongoni mwa koo zenye nguvu na zinazoheshimika hutumia njia ya kuwaonya
na kuwatisha kama alivyokuwa akisema Abu Jahl:
تركت دين آبائك وهم خير منك.. لنسفّهنّ حلمك، ولنضعنّ شرفك، ولنكسدنّ تجارتك، ولنهلكنّ مالك"
“Umeacha
dini ya baba zako ambayo ni bora kwako na tutaivunja ndoto yako na kuiondoa
hadhi yako na kuzigomea biashara zako na kuangamiza mali zako”
Na kama walitoka
katika ukoo usiokuwa na hadhi pamoja na maskini na wasiokuwa na uwezo
hawa ndio walichokiona cha moto. Familia ya Yaasir ilikuwa ni miongoni mwao
Kabila la Bani Makhzuum ndilo
lillilopewa jukumu la kuiadhibu familia hii yote Yaasir,Sumayyah na mtoto wao ‘Ammaar.
Na adhabu waliyokuwa wakiipata si rahisi kuisimulia kwani kipindi hichi uislamu
ulikuwa bado hauna nguvu.
Adhabu waliyoipata
ilifikia hadi ya kushindwa kuvumilia huku wakisema kumwambia Mtume Salla Allah
‘Alayhi Wasallam:
يا رسول الله.. لقد بلغ منا العذاب كل مبلغ"..
“Yaa Rasuulu Llah ! Adhabu tunayopewa imetufikia
kikomo(hatuwezi kuvumilia tena)”
Mpaka
kumfanya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kila siku kutoka kwenda kuwapa
pole na kuwausia kwa kusema:
" صبرا آل ياسر ان موعدكم الجنة
Vumilieni
Aali Yaasir kwani hakika mmeahidiwa pepo
Adhabu waliyokuwa
wakiipata inasimuliwa katika hadithi tofauti kutoka kwa masahaba kama
anavyosema Amr bin Haakim : “ Ammaar alikuwa akiadhibiwa mpaka akawa hajui
anachokisema”
Yaasir baba yake
‘Ammaar – Allah awawie radhi wote – alikuwa akiwa matesoni. Mkewe, Sumayyah
mama yake Ammaar akamtolea maneno ya ukali Abu Jahal, maneno haya
yalimkera na kumchoma Abu Jahal. Akaamua kumchoma mkuki mbeleni na kumuua mbele
ya mwanawe. Historia ya Uislamu haiandikiki bila ya kumtaja bibi huyu, kwani
yeye ndiye mtu wa kwanza kuuawa shahidi katika Uislamu. Baada ya kifo cha baba
na mama yake, Ammaar alizidishiwa adhabu maradufu. Wakati walimuadhibu kwa
kumlaza katika mchanga wa jangwani na kumuwekea jiwe kubwa kifuani, mara
nyingine wakimuunguza kwa moto na huku wakimuambia : Hatutakuachilia mpaka
umtukane Muhammad na uwataje kwa wema lata na uzzah (Waungu wa kisanamu wa
Maquraish wakati huo). Akafanya kama wanavvotaka kutokana na adhabu kali. Na
‘Ammaar, bila ya kujijua, akawa akiyakariri haya maneno anayoambiwa
Adhabu ilifikia
hadi mpaka ‘Ammaar alikuwa akipoteza fahamu na wakati mmoja walimuadhibu mpaka
hakujijua . Alipozinduka na kukumbuka aliyokuwa akiyasema aliingiwa na majuto
huku akijua ni kosa kubwa kuyatamka na alipokutana na Mtume alikuwa akilia kwa
majuto na Mtume alikuwa akimfuta machozi na kumwambia usiwe na wasiwasi. Wakija
tena na kukutaka utamke wanayokutaka uyatamke wakubalie kisha akamsomea aya ya
Quraan Annahl /106
إِلاَّ مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالإِيمَانِ
Isipokuwa
aliye lazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetulia juu ya Imani
Tokea wakati huo
‘Ammaar hakuhuzunishwa wala kujutia kwani alijua kwamba Allah Subhaanahu
Wata’ala amemhakikishia kwamba ataziangalia nyoyo na si matamshi yanayotoka
vinywani wakati moyo unayasuta.
Baada ya waislamu
kuhamia Madina na dola la kiislamu kuasisiwa , ‘Ammaar alikuwa ni miongoni mwa
masahaba waliokuwa na hadhi kubwa kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kwani
alikuwa akipendwa na Mtume huku Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam hukaa na kumsifia
juu ya imani yake na uongofu wake. Mpaka siku moja palipotokea kutoelewana kati
yake na Khalid ibn Waliyd, Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akasema :
من عادى عمارا، عاداه الله، ومن أبغض عمارا أبغضه الله"
Yeyote
mwenye kumfanyia uadui ‘Ammaar basi Allah atamfanyia uadui na
yeyote mwenye kumbughudhi ‘Ammaar basi Allah atambughudhi.
Ilimbidi Khalid
kwenda kumuomba radhi ‘Ammaar.
Mapenzi haya ya
Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kwa ‘Ammaar hayakuja kwa bahati bali ni
jinsi imani yake,uongofu wake , mateso aliyoyapata kwa ajili ya dini, mitihani
aliyoipata ya kujaribiwa katika imani yake ni mambo yaliyoifanya itikadi yake
kuwa thabiti isyo na shaka wa kutetereka. Uongofu huu alikuwa akiuusia Mtume
Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kwa kusema :
" اقتدوا بالذين من بعدي أبي بكر وعمر... واهتدوا بهدي عمّار
“Wafuateni
baada yangu kina Abu Bakr na ‘Umar…. Na igeni uongofu wa ‘Ammaar”
Imani ya ‘Ammaar
haikumalizika kwa kufariki kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam bali
alikuiwa mstari wa mbele katika kupigana vita vya Jihadi na kuzidi kulitangaza
kalima yake Allah Subahaahu Wata’ala kuwa juu. Alikuwa ni mwanajihadi shujaa,
asiyeogopa wala kubadilisha msimamo.
Enzi za Ukhalifa wa
‘Umar Ibnul Khattaab aliteuliwa kuwa Amiri katika mji wa Kufa na ‘Abdullah ibn
Masoud kuwa waziri wake na mwalimu wa kuwafundisha waislamu dini
yao. Wakati watu wakiteuliwa Maamiri huzidi kuwa na nguvu au kuzidiwa na kibri
lakini kwa ’Ammaar ilikuwa kinyume chake kwani alikuwa dhalili mpaka watu
wakashangazwa na Amiri walieletewa. Anasema Ibn Abu
Huzayl ambae alikuwepo Kufa wakati ‘Ammaar ni Amiri:
رأيت عمّار بن ياسر وهو أمير الكوفة يشتري من قثائها، ثم يربطها بحبل ويحملها فوق ظهره، ويمضي بها الى داره"..!
“Nilikuwa nikumuona ‘Ammaar bin Yaasir wakati akiwa
Amir wa Kufa akinunua vitu vyake akivifunga kwa kamba na kisha kuibeba mgongoni
mwake akielekea nyumbani kwake”
Hakuwa mtu mwenye
mambo makubwa kwani hata siku moja alijiwa na mmoja katika wenye hadhi na jina
katika mji wa Kufa ili kuomba jambo kwa Amiri na kutokana na nafasi yake
alikuwa na hakika kwamba Amiri angelimkubalia. Hata hivyo ‘Ammaar alimkatalia
na kukasirika mpaka kudiriki kumrushia shutuma na matusi Amiri kwa kumwambia:
:" يا أجدع الأذن
“Mtizame
aliekatika sikio!”
Sikio moja la
‘Ammaar lilikuwa limekatika alipopigana vita vya Yamaamah
ambavyo ushujaa wake ulikuwa ni changamoto ya kuweza kuwatia morali
waislamu na hatimaye kushinda. Mpaka ilifikia kusimama wakati tayari
ameshakatwa sikio na kusema kwa sauti ya ukali “Mnaikimbia pepo? Niangalieni
mimi ni ‘Ammaar bin Yaasir nifuateni nifuateni”
Amiri
hakukasirishwa na kauli ile bali alijibu tu kwa kusema:
خير أذنيّ سببت.. لقد أصيبت في سبيل الله
“Umelitukana sikio langu lililo bora kwani lilikatwa
(wakati nnapigana) kwa ajili ya Allah”
Uadilifu wa ‘Ammar
ulikuja dhihirika zaidi wakati ilipokuja fitna kubwa katika Uislamu na huku
tayari akiwa ni mzee wa miaka zaidi ya tisini. Naam mzee wa miaka tisini
aliweza kuikamata na kuibeba bendera ya vita ambavyo viliwagawa waislamu
wasijue nani aliye kwenye haki kati ya Sayyidna ‘Ali bin Abi Talib akiwa kama
ni khalifa na Mu’awiyah ibn Abu Sufyaan. Siku hiyo alisimama na bendera na
kusema :
" والذي نفسي بيده.. لقد قاتلت بهذه الراية مع رسول الله صلى الله عليه وسلم، وهأنذا أقاتل بها اليوم..
والذي نفسي بيده. لو هزمونا، لعلمت أننا على الحق، وأنهم على الباطل". .
“Kwa Yule ambae nafsi yangu iko kwenye mikono yake
Nilipigana kwa ajili ya bendera hii pamoja na Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi
Wasallam na hivi leo nnapigana tena kwa ajili ya bendera hii.
Kwa
Yule ambae nafsi yangu iko kwenye mikono yake hata kama wakitushinda basi bado
nnnajua kwamba sisi ndio tuliokuwa katika haki na wao wako kwenye batili.”
Hii ndiyo siku
aliyopigana ‘Ammaar kwa ajili ya haki na watu kumfuata mpaka akauwawa shahidi
kama walivyokufa mashahidi wazazi wake wawili ambao walisiimamia haki.
Mzee wa miaka zaidi ya tisini anauwawa shahidi
katika kuisimamia haki ambayo ndiyo msimamo wa kila muislamu. Alizikwa katika
eneo pamoja na mashahidi katika nguo zake alizozivaa huku Khalifa Ali bin Abi
Talib akiuchukua mwili wake na kuuhifadhi huku Pepo ikiwa tayari ikimsubiri na
kama alivyowahi kusimulia Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam katika moja ya
hadithi zake kwamba pepo ilikuwa na hamu sana na ’Ammaar.