Khalifa wa pili aliyeongoka
Jina na nasaba yake
Jina lake
ni
Umar bin Al Khatwaab bin Nufail bin Abdul Uzza bin Riyah bin Abdullah bin Qarat
bin Razah bin Uday bin Kaab bin Luay bin Ghalib Al Qurashi Al Adawi, aliyekuwa
pia akijulikana kwa jina la Abu Hafs.
Jina la mama yake ni
Hantamah binti Hashim bin Al Mughiyrah bin Abdullah bin Umar bin Makhzum.
Imepokelewa kuwa Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu) alisema;
"Nilizaliwa miaka minne kabla ya
vita vikubwa vya Al Fujaar.", na vita hivi
vilipiganwa kabla ya kupewa utume Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kwa
miaka 30.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
ananasibiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) upande
wa baba katika babu yao wa saba, na upande wa mama wanakutana katika babu yao
wa sita.
Wanawe na wakeze
Watoto wa Umar
(Radhiya Llaahu ‘anhu) walikuwa Abdullah na Abdul Rahman (mkubwa) na Hafsa,
wote hawa alizaa na mkewe wa mwanzo Zeinab binti Madhaun bin Habib bin Wahab
bin Hudhafa bin Jumah.
Alikuwa na
binti mwengine Ruqayah aliyezaa na mkewe mwingine ambaye ni Ummu Kulthum binti
wa Ali bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu) na Bibi Fatima binti wa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).
Na alikuwa pia na
watoto wengine wawili Zeid na Ubeidullah, na mama yao
alikuwa Ummu Kulthum binti Jarwal bin Malik, na wawili hao walipigana katika
vita vya Siffin wakiwa upande wa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Alikuwa pia na mtoto mwengine aliyempa
jina la Asim pamoja na Abdul Rahman (wa
kati), na mama yao alikuwa Jamila binti Thabit na alikuwa na Abdul Rahman
(mdogo) na mama yake akiitwa 'Um Walad',
na alikuwa pia na mtoto aliyempa jina la Fatima, na mama yake ni Hakim binti al
Harith bin Hisham na alikuwa na binti mwengine aliyempa jina la Zeinab na huyu
ni mdogo wa watoto wote wa Umar na mama yake ni Fakiha na alikuwa pia na Iyadh
bin Umar na mama yake ni Atika binti Zeid bin Amr bin Nufeil.
Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alilibadilisha jina la mamake Asim
aliyekuwa akiitwa 'Aasiya' na maana yake ni (mwenye kufanya maasi). Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia;
"Hapana, bali
wewe ni Jamila."
Umbo lake
Umar bin Khatab (Radhiya Llaahu ‘anhu)
alikuwa mrefu, unapomuona kwa mbali utadhani amepanda mnyama, na alikuwa na kipara
sehemu ya mbele ya kichwa chake, na rangi ya ngozi yake ilikuwa nyekundu kupita
kiasi, mwenye ndevu nyingi, na alikuwa mtumiaji wa mkono wa kushoto (mashoto)
na alikuwa akitembea kwa haraka sana.
Maisha yake
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliishi
miaka 65. Miaka 30 katika ukafiri na miaka 35 katika Uislamu, na kabla ya kusilimu kwake
alikuwa akifanya kazi ya kuchunga kondoo na ngamia wa baba yake Al Khatab bin
Nofeil.
Mara baada ya kusilimu, Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) alibadilika akawa mmoja katika watu adhimu walioushangaza
ulimwengu kwa kipaji cha uhodari wake, hekima ya hali
ya juu, pamoja na elimu iliyochimbuka ghafla katika kifua chake.
Aliposhika ukhalifa aliweza kuziangusha dola
kubwa za Kirumi na Fursi zilizokuwa na nguvu nyingi
wakati ule, akaweza kuikomboa Baytul Maqdis na kuwafukuza Mayahudi nje ya bara
ya Arabuni, na nchi nyingi moja baada ya nyingine zilikuwa zikisalimu amri
mbele ya majeshi yake.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni katika watu wanaokushangaza kila unaposoma sira yake na
kukufanya uihisi haiba yake na kujiona kama
unaishi naye katika wakati wake, katika uadilifu wake, katika ushujaa wake,
katika uaminifu wake, katika hekima aliyokuwa nayo na katika ukali wake. Ukali
ulomfanya mwalimu wake na mwalimu wa ulimwengu
Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aseme;
"Mkali wenu katika Uislam Umar bin
Khatab".
Imam Ahmad na Ibni Hibban
Yupo mtumishi kuliko mimi?
Siku moja katika siku za joto kali sana
Othman bin Affan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akichungulia dirishani pake,
akamuona Umar bin Khatwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) anakwenda mbio nyuma ya
ngamia aliyekata kamba, akamuuliza;
'Kuna nini ewe Umar?"
Akamwambia;
"Ngamia wa zaka amekata
kamba."
Othman (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
"Umar, si ungetuma watumishi
tu wamfuatilie?"
Umar akajibu:
"Kuna mtumishi kuliko mimi?"
Kuwa Khalifa wa
Waislamu, kwake yeye maana yake ni kuwa mtumishi wa Waislam, kuwatumikia
Waislamu, kuwahurumia Waislam, kulinda haki za Waislam, kuwalinda Waislam na
kuulinda Uislam.
Kila mtu huko anakula chakula hiki?
Siku moja Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
aliletewa zawadi ya halwa nzuri sana kutoka kwa mmoja wa magavana
wake katika nchi ya Azerbijan, akamuuliza mjumbe aliyepewa haluwa ile;
"Kwani kila mtu huko anakula
chakula hiki?"
Mjumbe akajibu:
"La, sivyo ewe Khalifa wa Waislamu, hiki ni chakula cha watu wakubwa tu".
Umar akaghadhibika sana, akamuuliza;
"Yu wapi ngamia wako? Chukua chakula
hiki umrudishie aliyekupa, kisha umwambie;
"Umar anakuamrisha;
Usijishibishe chakula mpaka washibe kwanza Waislamu wote chakula hicho".
Waislamu wanazistahiki zaidi
Siku moja mkewe alitamani halwa, Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akamuuliza;
"Ziwapi pesa za kununulia
halwa?"
Mkewe akamjibu;
"Mimi ninazo, nimeweza
kudunduliza katika pesa zetu za chakula zinazozidi".
Umar akamwambia;
"Kama
katika pesa zetu za chakula zipo zinazoweza kuzidi, basi wapo Waislamu
wanaozistahikia, kwa hivyo nenda kazirudishe katika
hazina ya Waislam."
Umehukumu ukafanya uadilifu ukaweza kulala
Siku moja aliwasili Madina mjumbe wa Kaisar mfalme wa Warumi aliyetumwa kuonana na Umar.
Akauliza;
"Yuko wapi Umar?"
Akaambiwa;
"Yule pale Umar aliyelala
chini ya mti ule."
Akamtizama Umar aliyekuwa amelala chini ya
mti, kisha akawatazama Waislam waliokuwa wakipita mbele yake bila kujali, kila
mmoja anakwenda katika shughuli zake, akakumbuka alikotoka namna wafalme wao
wanavyoishi ndani ya ngome zinazolindwa na maaskari
kila mahala, Mrumi yule akatamka kauli yake maarufu akasema;
‘Umehukumu, ukafanya uadilifu,
ukaweza kulala ewe Umar’.
Mwenyezi Mungu ametutukuza kwa Uislamu
Siku ile majeshi ya Kiislamu yalipoingia
Palestina na kuuteka mji wa Jerusalem
pamoja na msikiti wa Baytul Maqdis kutoka mikononi mwa manasara, maaskofu wa
kanisa kuu walikataa kuzitoa funguo na kuwapa wafunguzi hao, wakataka ahudhurie
Khalifa wa Waislamu mwenye sifa maalumu zilizoandikwa ndani ya vitabu vyao ili
wamkabidhi funguo hizo.
Akafikishiwa habari hizo Umar bin Khatwaab (Radhiya
Llaahu ‘anhu) aliyefunga safari ndefu kutoka Madina hadi Palestina akifuatana na mtumishi wake. Ngamia wa mtumishi alikufa njiani akabaki
ngamia mmoja waliyekuwa wakimpanda kwa zamu, mara mtumishi na mara anampanda
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na mara anakwenda bila kupandwa, na walipowasili
Baytul Maqdis ilikuwa zamu ya mtumishi kupanda ngamia, na Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akaingia akiwa anatembea kwa miguu wakati mtumishi wake yupo juu ya
ngamia.
Wakuu wa majeshi ya
Kiislam waliokuwepo Jerusalem
walipomuona Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akiwasili akiwa katika hali ile,
wakamzunguka na kumtaka yeye ampande ngamia huyo badala ya mtumishi wake, maana
haitokuwa vizuri kuwakabili wakubwa wa manasara akiwa anatembea kwa miguu.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawaambia;
“Mwenyezi Mungu ametutukuza kwa Uislam, na iwapo tutautafuta utukufu kwengine na sio
katika Uislam, basi Mwenyezi Mungu atatudhalilisha”.
Huyu ndiye Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
aliyewashangaza waandishi wa historia na kuushangaza
ulimwengu mzima kwa hekima na busara yake, uadilifu wake, ujasiri na ushujaa
wake.
Huyu ndiye Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa
akikesha wakati Waislam wamelala, aliyejinyima ili Waislam wapate, aliyebaki na
njaa ili Waislam washibe, aliyejitolea maisha yake pamoja na maisha ya Masahaba
wenzake (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa ni mhanga ili neno la Mwenyezi Mungu liwe
juu na neno la wale waliokufuru liwe chini.
Mwenyezi Mungu utie nguvu Uislamu kwa kumsilimisha Umar bin Khatwaab
Wakati wa ujahilia
(kabla ya Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kuanza kuteremshiwa Wahyi) Umar
(Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mpiganaji mieleka maarufu katika Soko la Ukadh,
mahali walipokuwa wakikutana Waarabu kila mwaka kwa ajili ya kufanya biashara
na kufanya michezo mbali mbali na mashindano ya mashairi na mengine.
Miongoni mwa mashindano hayo yalikuwa ni mieleka, na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa bingwa wa
kupigana mieleka. Alikuwa akitumia mkono wake wa
kushoto na alikuwa 'akipiga anaumiza', kama
walivyokuwa wakimsifia.
Alikuwa akijulikana kwa
sifa zifuatazo:
'Akisema anasikilizwa, akitembea
anakazana na akipiga anaumiza.'
Hakuwa akimuogopa mtu yeyote, na alikuwa anapoanzisha jambo hupenda kulikamilisha. Hapendi
kufanya mambo nusu nusu kisha akaacha na kurukia
mengine. Hakuwa akiyachukulia mambo kwa wepesi. Kila
kitu alikuwa akikipa umuhimu wake, na yaliyomo moyoni
mwake huyadhihirisha katika ulimi wake. Hajuwi kuficha wala
kujificha.
Kwa sababu hizi ndiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamuomba
Mwenyezi Mungu kwa kusema:
"Mwenyezi Mungu utie nguvu Uislamu kwa
(kumsilimisha) Umar bin Khatab".
Al Hakim
Anasema Abdillahi bin Masaood (Radhiya Llaahu
‘anhu):
"Tuliendelea kuwa na nguvu
tokea aliposilimu Umar. Kusilimu kwake kulikuwa ufunguzi, kuhama
kwake (kwenda Madina) kulikuwa ushindi, na Ukhalifa
wake ulikuwa huruma. Tulikuwa hatuwezi kusali panapo nyumba
(ya Al Kaaba) mpaka aliposilimu Umar".
Namna Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alivyosilimu
Siku moja wakati wa adhuhuri Umar bin Khatwaab
(Radhiya Llaahu ‘anhu) alitoka nyumbani kwake panga mkononi akielekea nyumba ya
Al Arqam bin Abil Arqam, ambayo ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llahu alayhi wa sallam) pamoja na Sahaba zake (Radhiya Llaahu ‘anhu) walikuwa
wakikutana na kujifunza Qurani tukufu.
Alipokuwa njiani, Umar alikutana na mtu aitwaye Naeem bin Abdullah, aliyemuuliza;
"Unaelekea wapi ewe Umar?"
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu;
"Nakwenda kwa
huyu anayewabadilisha watu na kuwatenganisha Makureshi na kuitukana dini yao
pamoja na miungu yao.
Nakwenda kumuua".
Yule mtu akamwambia;
"Uelekeaji mbaya unaoelekea
na mwendo mbaya unaokwenda".
Umar akadhani kuwa huyu naye keshasilimu,
akamuuliza;
"Isiwe na wewe
washakubadilisha? Ikiwa ni hivyo basi bora nikuanze wewe".
Kwa uwoga mkubwa yule mtu akamwambia;
"Umar, Jua ya kuwa dada yako keshasilimu
pamoja na mumewe Said bin Zeyd na wamekwisha iacha
dini yako".
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akageuza njia na kuelekea nyumbani kwa dada yake Fatima
bint Al Khatab (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa wakati huo yuko pamoja na
mumewe na Sahaba mwengine aitwae Khabbab bin Al Arat (Radhiyallahu anhum), na
wote walikuwa wakisoma na kuidurusu Qurani tukufu.
Alipowasili aligonga mlango kwa kishindo kikubwa.
"Nani?"
"Mimi Umar!"
Khabbab (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliruka na kujificha chini ya kitanda huku akimuomba Mwenyezi Mungu amsalimishe.
Ama Fatima dada yake Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu), yeye aliwahi kuzificha kwa kuzishindilia
kifuani pake zile karatasi zilizoandikwa Qurani tukufu.
Wakamfungulia mlango na
kumkaribisha huku nyuso zao zikionesha dalili ya uoga.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawauliza;
"Ni yepi haya maneno
niliyoyasikia mkiyasoma nilipokuwa nje kabla ya kuingia humu?"
Wakajibu ;
"Si kitu ni
mazungumzo na hadithi tu."
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Nasikia nanyi pia
mumebadilisha dini yenu?"
Said (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu;
"Umar! unaonaje ikiwa ukweli upo katika dini nyingine….?"
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakumuacha
amalize maneno yake, akamrukia kwa nguvu za ajabu na
kumwangusha chini kwa kishindo kisha akamkalia juu ya kifua chake, na dada yake
alipojaribu kuja kumsaidia mumewe alipigwa kofi la nguvu usoni na damu zikaanza
kumtoka, jambo lililomfanya apige ukelele mfano wa baragumu au radi huku
akimkabili Umar na kumwambia:
"Ewe adui wa
Mwenyezi Mungu! Unanipiga kwa sababu nimemuamini
Mwenyezi Mungu mmoja? Basi fanya utakavyo mimi natamka;
"Ash hadu an
laa ilaaha illa Llah wa anna Muhammadan Rasuulu Llah".
Ndani ya sauti kali na
ushupavu wa dada yake, Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaiona nuru ya Uislamu.
Hajapata hata siku moja kumsikia dada yake akimkabili na kumjibu, kwani Fatima
alikuwa akimuogopa sana
Umar, lakini
leo dada yake huyu anamnyanyulia sauti na kumjibu kwa ukali na kwa ushupavu
bila uoga? Bila shaka pana jambo tukufu sana lililombadilisha na kumgeuza na
kuuingiza ushujaa ule moyoni mwake.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwa akipenda
kuzitumia nguvu zake kwa ajili ya inda tu, bali alikuwa mtu anayependa kuyaweka mambo sawa.
Hapo mwanzo alidhani kuwa dada yake anapotea, akataka kumuongoza katika haki, lakini alipogundua
kuwa dada yake yupo katika haki, na yeye ndiye aliyepotea, akaikubali haki na
kuifuata.
Akainuka kutoka juu ya kifua cha Said (Radhiya
Llaahu ‘anhu), na alipoziona zile karatasi alozificha
dada yake kifuani pake zikijitokeza, akamwambia;
"Nipe hizo karatasi."
Dada yake akamwambia;
"Sikupi kwani hawazigusi
hizi isipokuwa waliotahirikia. Nenda kaoge kwanza ili ujitahirishe."
Umar(Radhiya Llaahu
‘anhu) akenda kuoga kisha akarudi haraka huku ndevu zake zikiwa bado
zinatiririka maji, akazichukua karatasi zile kutoka kwa dada yake na kuanza
kuzisoma, na ndani yake ilikuwa imeandikwa Surat Twaha - kuanzia aya ya mwanzo
hadi ya kumi na sita:
"TWAHA! .
Hatukukuteremshia Qur'ani ili
upate mashaka.
Bali
ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea.
Materemsho yatokayo kwa
aliye umba ardhi na mbingu zilizo juu.
Arrahmani, Mwingi wa
Rehema, aliyetawala juu ya Kiti cha Enzi.
Ni vyake vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, na vilivyomo baina yao,
na vilivyomo chini ya ardhi.
Na ukinyanyua sauti kwa
kusema...basi hakika Yeye anajua siri na duni kuliko siri.
Mwenyezi Mungu! Hapana
Mungu isipokuwa Yeye.
Yeye ana majina mazuri kabisa.
Na jee! Imekufikia hadithi
ya Musa?
Alipouona moto, akawaambia watu wake:
Ngojeni! Mimi nimeuona moto, huenda nikakuleteeni kijinga
kutoka huo moto, au nikapata uongofu kwenye moto.
Basi alipoufikia akaitwa: Ewe Musa!
Hakika Mimi ndiye Mola wako Mlezi! Basi vua viatu vyako.
Kwani upo katika bonde takatifu
la T'uwa.
Nami nimekuteua wewe; basi
sikiliza unayo funuliwa.
Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana Mungu ila Mimi tu.
Basi niabudu Mimi, na
ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.
Hakika Saa itakuja bila ya shaka. Nimekaribia
kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyoyafanya.
Basi wasikuzuwie na
(kuyaamini) hayo wale wasio yaamini na wafuatao matamanio ya nafsi zao.Usije
ukaangamia."
Kwa moyo mkunjufu, Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akazikumbatia karatasi hizo na kuzibusu huku
akisema;
"Haipaswi kwa mwenye aya kama
hizi kuwa na mshirika anayeabudiwa pamoja naye, - Nipelekeni kwa Muhammad!".
Hapo ndipo Khabbab (Radhiya Llaahu ‘anhu)
aliyekuwa amejificha chini ya kitanda alipojitokeza na
kusema;
"Bishara njema ewe Umar, Wallahi Mwenyezi
Mungu ameikubali dua ya Mtume wake".
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoka na kuelekea nyumba ya Al Arqam (Radhiya Llaahu ‘anhu)
iliyopo karibu na mlima Safaa, na Hamza (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa pamoja
na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipomuona Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akija na uso mkunjufu, akasema;
"Huyo anakuja, iwapo Mwenyezi Mungu
anamtakia kheri basi atasilimu, ama iwapo hamtakii hivyo, basi kifo chake
kitakuwa mikononi mwetu leo".
Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akatoka na kumuendea Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu), akamkabili kwa kumshika na kumkunjakunja nguo zake pamoja na ala ya
panga yake huku akimwambia;
"Hivyo utangoja ewe Umar mpaka Mwenyezi
Mungu atakapoteremsha aya juu yako zikikulani kama alivyoteremshiwa Al Walid bin Mughiyra? -
Mola wangu, huyu Umar bin Khatab! Mwenyezi Mungu ipe nguvu dini kwa kumuingiza
Umar katika dini yako"
Hapo ndipo Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
aliposilimu na kuzitamka shahada mbili;
"Ash- hadu an
Laa ilaaha illa Llah wa ash - hadu annaka Rasulu llah."
Alisilimu akiwa na
umri wa miaka ishirini na sita na wakati huo walikuwa wamekwisha kusilimu watu
thelathini na tisa na yeye akawa wa arubaini kusilimu.
Kwa kauli hii, Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
alibadilika na kutoka katika ushirikina wa kuabudu masanamu na kuingia katika
ibada ya Mwenyezi Mungu mmoja asiye na mshirika, na kutoka katika uadui mkubwa
dhidi ya Uislamu na kugeuka kuwa mlinzi mkubwa wa Uislamu, na kutoka katika
nguvu na ushujaa usio na mwongozo na kuingia katika nguvu na ushujaa ulio na
mwongozo wenye nuru inayoongozwa na kitabu kinachon'gara, kitabu cha Mwenyezi
Mungu Subhanahu wa Taala.
Ushujaa na nguvu
zake alizokuwa akizitumia dhidi ya Uislamu akavigeuza na kuvitumia katika
kuulinda na kuuendeleza mbele Uislamu.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa na tabia ya kuipenda haki na kuitetea mara anapoiona na
kuijua, na mara baada ya kusilimu kwake alimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llahu alayhi wa sallam) na kumuuliza;
"Sisi si tuko katika haki katika kuishi
kwetu na kufa kwetu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa
sallam) akamjibu:
"Ndiyo ewe Umar. Naapa kwa Yule ambaye nafsi zetu zimo mikononi mwake, nyinyi mumo
katika haki katika maisha yenu na katika kufa kwenu".
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema:
"Kwa nini basi tunajificha? Naapa kwa Yule aliyekuleta kwa haki, utoke, na sisi tutoke pamoja
na wewe."
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa
sallam) akakubali kutoka pamoja na Waislamu, wakawa wanatembea katika barabara
za Makkah mistari miwili, msitari mmoja ukiongozwa na Umar na mwengine
ukiongozwa na Hamza (Radhiya llahu anhum)
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa
hastarehe bila ya kukamilisha kile alichokianzisha, akaapa akisema:
"Wallahi kila mahali
nilipokaa nikiutetea ukafiri lazima nikakae tena kuutetea Uislamu".
Akafanya kama
alivyokula kiapo, kisha akamwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi
wa sallam) na kumwambia:
"Ewe Mtume wa Mwenyezi
Mungu, nini kinachotufunga ndani tu? Wallahi mimi
nishakwenda kila mahali nilipokuwa nikikaa kuutetea ukafiri na badala yake
nikawa nautetea Uislamu bila ya kuwaogopa, na kutoka sasa ewe Mtume wa Mwenyezi
Mungu tusimwabudu tena Mwenyezi Mungu kwa kificho".
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam)
akalikubali pendekezo lake.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye anatamani apigwe kama ndugu zake
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa mtu wa ajabu sana
alikuwa akiona uchungu kila anapowaona Waislamu wenzake wakipigwa wakati yeye
hapana anayethubutu kumsogelea. Akaamua kumuendea Abu Jahal nyumbani kwake na kumgongea mlango. Alipoufungua na
kumuona Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesimama mbele yake akamwambia;
"Wewe!?" Kisha
akaufunga mlango mbele ya uso wake.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaondoka na kuziendea nyumba nyingine za washirikina, akawa
anawagongea milango moja baada ya nyingine, lakini hapana aliyethubutu kumtokea.
Akaamua kuwaendea panapo Al Kaaba mahali
wanapokusanyika, huku akijua kuwa itakuwa vigumu kwao kumuacha atambe mahali
hapo, na itawabidi wapigane nae.
Hebu tumsikilize Umar mwenyewe
akituhadithia yaliyomkuta siku hiyo. Anasema Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu):
"Watu wakaanza kunizunguka na kupigana na mimi, wakawa wananipiga na mimi nawapiga,
mpaka alipokuja mjomba wangu na kusimama panapo Hijr Ismail na kusema:
'Umar mtoto wa dada
yangu yumo ndani ya himaya yangu,'
Kwa kauli yake hiyo watu wakaacha kunipiga,
lakini nilipowatazama ndugu zangu na kuwaona
wakiendelea kupigwa wakati mimi hapana anayethubutu kunigusa, nikamwendea
mjomba wangu na kumwambia:
"Himaya yako nakurudishia mwenyewe"
Akaniambia:
"Usifanye hivyo ewe mwana wa dada yangu"
Nikamwambia:
"Bali
nairudisha fanya utakavyofanya "
Nikawa naendelea kupambana nao mpaka Mwenyezi
Mungu alipotutukuza kwa Uislamu".
Anasema Khalid Muhammad Khaled katika kitabu
chake kiitwacho 'Khulafaa Rasuul':
"Mwanamume aliyefanya yote haya mara tu
baada ya kusilimu kwake, tutakutana naye tena akiwa Khalifa wa Waislamu, huku
majeshi yake yakibomoa makasri ya Kisra, mfalme wa Wafursi na Kaisar mfalme wa
Warumi, lakini juu ya ushindi mkubwa aliokuwa akiupata pamoja na nguvu zake
zote hizo, mtu huyu huyu tutamuona akipanda juu ya membari baada ya kuwaita
Waislamu ili akutane nao, kisha anawambia:
"Enyi watu, mimi kazi yangu ilikuwa
kuchunga kondoo wa shangazi zangu katika kabila la Bani Makhzum na malipo yangu
yalikuwa gao la tende au zabibu", na baada ya kusema maneno hayo anateremka akiwa amewashangaza
watu, na Abdurahman bin Auf (Radhiya Llaahu ‘anhu) anapotangulia na kumuuliza:
"Kwa nini ukafanya hivyo ewe Amiri wa Waumini?"
Akajibu:
"Ole wako ewe mwana wa Auf, nilikaa peke
yangu nikitafakari na
kujiuliza;
'Wewe ndiyo ushakuwa Khalifa wa Waislamu, na hapana aliye juu yako isipokuwa Mwenyezi
Mungu, NANI ALIYE BORA KULIKO WEWE? Nikaona bora niijulishe nafsi yangu kadiri yake
(nikivunje kiburi changu)".
Hijra yake
Anasema Sayiduna Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu);
“Wote waliohama kutoka Makka kwenda Madina
walihama kwa kificho isipokuwa Umar bin Khatab. Yeye alipotaka kuhama aliuvaa
upanga wake kiunoni na kubeba ngao yake, akachukua
mikuki mkononi mwake kisha akenda moja kwa moja mpaka mbele ya Al Kaaba mahali
wanapojikusanya washirikina, akatufu mara saba mbele yao
kisha akaelekea Maqamu Ibrahim na kusali rakaa mbili, kisha akaanza kuyaendea
makundi yaliyojikusanya hapo moja baada ya moja huku akiwaambia;
‘Zimedhalilika nyuso zenu. Yeyote kati
yenu anayetaka mamake amkose na wanawe wawe mayatima
na mkewe awe kizuka, basi na akutane nami nyuma ya bonde hili”.
Anasema Sayiduna Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu);
“Hapana hata mmoja aliyethubutu
kumfuata isipokuwa wanyonge wachache waliokuwa wakionewa, hao ndio waliomfuata. Akawafundisha na kuwaongoza kisha akaendela na safari yake”.
Alipowasili Madina, Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu) alipokelewa na wenzake waliotangulia kabla yake
nao ni Masa ab bin Umair na Ibni Ummi Maktoum (R Anhum) na wengine.
Waislam waliobaki Makkah wakaendelea kuhamia
Madina makundi kwa makundi na hatimaye akahamia Mtume (Swalla
Llahu alayhi wa sallam), na dola ya Kiislam ikaanzishwa hapo Madina chini ya
misingi iliyo thabit na yenye nguvu. Mapambano mengi yakatokea na vita vingi baina ya nuru ya haki na viza vya batil.
Baadhi ya nishani alizopewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam)
Zifuatazo ni baadhi tu ya sifa nzuri nzuri
alizopewa Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na Mtume Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa
sallam) zilizonukuliwa kutoka katika hadithi sahihi:
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi
wa sallam) amesema;
"Mwenyezi Mungu ameijaalia haki katika
ulimi wa Umar na katika moyo wake. Miongoni
mwa waliokuja kabla yenu walikuwepo watu wenye kufunuliwa bila ya wao kuwa
mitume. Ikiwa katika umma wangu wapo wenye mfano wao,
basi huyo atakuwa Umar".
Bukhari- Muslim na
Attarmidhiy
Na akasema;
"Niliota nimo Peponi, nikamwona mwanamke
anatawadha karibu na kasri, nikauliza ;
'Kasri ya nani hii?'
Nikajibiwa;
'Kasri ya Umar'
Nilipokumbuka wivu wa
Umar nikarudi haraka kule kule nilikotoka."
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliposikia
maneno hayo, alilia sana na kusema;
"Nikuonee wivu wewe ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Bukhari na Muslim
Na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akasema;
"Nilipokuwa nimelala nikaota nimeletewa
mbele yangu watu wakiwa wamevaa kanzu, wamo miongoni mwao waliovaa kanzu (fupi)
zinazowafika vifuani pao, wengine (fupi) juu zaidi kuliko hapo, kisha
nikaletewa Umar akiwa amevaa kanzu inayoburura"
Akaulizwa ;
"Nini tafsiri ya ndoto hiyo ?"
Akajibu;
"Dini"
Bukhari na Muslim
Na akasema;
"Nilipokuwa nimelala niliota
nimeletewa birika la maziwa, nikanywa na kumpa Umar yaliyobaki".
Akaulizwa :
"Nini tafsiri yake?"
Akajibu;
"Elimu"
Bukhari
Myahudi mmoja anayeitwa Zeyd bin Sana
alitaka kusilimu, na hii ni baada ya kuzijua alama
zote za Utume alizokuwa nazo Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) isipokuwa
mbili, nazo ni ‘Upole wake’ na ‘Ustahamilivu wake’.Akataka kujihakikishia juu
ya alama mbili hizo.
Tumwache Zeyd mwenyewe atuhadithie;
"Nilipoipata fursa nilimwendea Mtume
alipokuwa akenda mazikoni pamoja na sahaba zake na kumkunja nguo zake huku
nikimkunjia uso wangu na kumwambia;
"Wallahi sikujua kama nyinyi wana wa Abdul Muttalib mnachelewesha
kulipa madeni ya watu namna hii."
'Umar akawa ananitazama huku macho yake
yanamzunguka kama
nyota, akaniambia';
"Wewe adui wa Mwenyezi Mungu, unamwambia
Mtume wa Mwenyezi Mungu haya ninayosikia na kutenda haya ninayoyaona? Wallahi ingekuwa siilindi
heshima yake, basi ningeikata shingo yako kwa panga langu".
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa
sallam) akawa anamwangalia Umar kwa utulivu uliojaa mapenzi, kisha akatabasam
na kusema;
"Mimi na huyu
mtu tunahitajia yaliyo bora kuliko hayo ewe Umar, ilikuwa uninasihi mimi niwe
mlipaji mzuri wa deni lake
na umnasihi yeye adai kwa
njia bora kuliko hii. Nenda ewe Umar kamlipe deni lake
na mwongezee pishi
ishirini za tende".
Zeyd akasilimu.
Al Hakim
Siku moja baada ya kugonga mlango na kupewa idhini ya kuingia nyumbani kwa Mtume (Swalla Llahu
alayhi wa sallam), Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaingia na kumkuta Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akicheka.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
"Mwenyezi Mungu akujaalie uwe na furaha siku zote ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu."
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa
sallam) akamwambia:
"Nimeshangazwa na hawa
wanawake waliokuwa pamoja nami, walikuwa wakizungumza, na mara ulipoingia
wakanyamaza na kujifunika gubi gubi (kwa kukuogopa)".
Umar(Radhiya Llaahu
‘anhu) akamwambia;
"Wewe ndiye unayestahiki wakuogope zaidi
ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu".
Kisha akawageukia wale wanawake na kuwaambia;
"Enyi maadui wa
nafsi zenu, mnaniogopa mimi na hamumwogopi Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Wakamwambia;
"Ndiyo! Wewe ni mkali kuliko Mtume wa Mwenyezi Mungu".
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa
sallam) akasema;
"Eeh! Mwana wa L Khataab we, naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo
mikononi mwake; Lau kama shetani atakuona unatembea katika njia yake, basi
atageuza njia na kukukimbia".
Bukhari – Muslim - Ahmad
Utamwambia nini kesho Mola wako ewe Umar?
Anasema Dr. Khaled Mohd Khaled;
“Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) angelikuwa mtu
mwenye ghururi basi ingejitokeza ghururi hiyo mara baada ya kusilimu kwake au
baada ya kuwa Khalifa wa Waislamu, maana mara tu baada ya kusilimu kwake,
Uislamu ulipata nguvu, na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alielewa vizuri kiasi
gani Waislamu walivyokuwa wanyonge na wenye kuogopa kabla ya hapo, alikuwa
akiona namna walivyoanza kupata nguvu mara tu baada ya kusilimu kwake, wakawa
wanasali panapo Al Kaaba bila uwoga. Na alikuwa akiona pia namna walivyokuwa
wakitembea na kupiga kelele za Takbir katika mji wa
Makka bila ya uwoga.
Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akimsikiliza rai zake, na mara
nyingi akimkubalia, bali mara nyingine Mwenyezi Mungu huteremsha aya zinazounga
mkono rai zake.
Kwa mfano katika hadithi iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim, anasema Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu);
“Mwenyezi Mungu amenikubalia mara matatu;
Niliposema ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu
ungefanya mahali alipokuwa akisimama Ibrahim pawe panasaliwa; Ikateremshwa aya;
“Na mahali alipokuwa akisimama
Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia”.
Al Baqarah – 125
Na aya ya Hijabu, nilimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam); ‘Ewe
Mtume wa Mwenyezi Mungu, ungeliwaamrisha wakezo wajifunike, kwa sababu miongoni
mwa wanaozungumza nao wamo wema na wamo waovu’. Ikateremshwa aya ya Hijabu;
“Nanyi mnapowauliza (wakeze)
waulizeni nyuma ya pazia. Kufanya haya
kutasafisha nyoyo zenu na nyoyo zao.”
Al Ahzab – 53
Na pale wake wa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa
sallam) waliposhirikiana kwa wivu wao dhidi ya Mtume (Swalla Llahu alayhi wa
sallam), Nikawaambia (akiwemo Bi Hafsa(Radhiya Llaahu ‘anhu) – mwanawe ambaye
pia ni mke wa Mtume(Swalla Llahu alayhi wa sallam)), ‘Akikupeni talaka, Mola wake atampa badala
yenu wake wengine walio bora kuliko nyinyi’; Ikateremshwa aya;
“(Mtume) akikupeni talaka, Mola wake atampa
badala yenu wake wengine walio bora kuliko nyinyi; wanaofuata nguzo za Imani,
watii, watubiao wanapokosa, wafanyao ibada, wafanyao mambo mengi ya kheri,
waliopata kuolewa na wasiopata kuolewa.’
At Tahriym – 5
Bukhari na Muslim
Na baada ya kufariki Abubakar Al Siddiq (Radhiya
Llaahu ‘anhu), Khalifa wa mwanzo wa Waislamu, akapewa
ukhalifa Umar bin Khatwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyejaaliwa kupata ushindi
mkubwa dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu.
Yote haya yanaweza kumfanya mtu wa kawaida awe na kiburi pamoja na majivuno, lakini Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) alikuwa akijulikana kwa kutojivuna kwake hata baada kupata
mafanikio yote hayo.
Juu ya nguvu na
ushujaa na ukali wake, Umar alikuwa mtu ambaye ukitaka kumtisha umwambie:
"Utasema nini kwa Mola wako
kesho Ewe Umar."
Utamwona anavyolia kama mtoto mdogo.”
Sidai wala sidaiwi
Siku moja Umar bin Khatwaab (Radhiya Llaahu
‘anhu), alimuuliza Abu Musa Al Ash- ariy (Radhiya Llaahu ‘anhu) :
"Ewe Aba Musa, utafurahi ikiwa kule kusilimu kwetu pamoja na
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na kuhama kwetu pamoja naye, na shahada
yetu pamoja na matendo yetu mema, vyote turudishiwe wenyewe na badala yake
tufutiwe dhambi zetu tuwe hatudai wala hatudaiwi?"
Abi
Musa AL Ash ary (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu:
"La Wallahi, ewe Umar, kwani sisi
tumepigana Jihadi, tukasali, tukafunga, tumefanya mema mengi na wamesilimu mikononi
mwetu watu wengi kwa hivyo sisi tunategemea thawabu za amali hizo."
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu huku
machozi yakimlenga:
"Ama mimi naapa kwa yule
ambaye nafsi yangu ipo mikononi mwake, natamani nirudishiwe yote hayo, kisha
nisalimike nisidai wala nisidaiwe".
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) mara nyingi
alinukuliwa akisema;
‘Iwapo nitaambiwa kuwa watu wote wataingia
Peponi isipokuwa mtu mmoja tu, basi ningeogopa mtu huyo asiwe mimi’.
Haya ni mafundisho aliyoyapata kutoka kwa
mwalimu wake na mwalimu wa ulimwengu mzima, Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa
sallam), kwani siku moja Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) alipomuona akisali
mpaka miguu yake ikivimba alimuuliza:
"Kwa nini unafanya yote hayo
wakati wewe umeshasamehewa madhambi yako yote yaliyotangulia na yanayokuja?"
Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamjibu:
"Basi nisiwe mja mwenye
kushukuru?"
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akijinyima vyakula vizuri
akiogopa siku ya Kiama asije akaambiwa kuwa amekwishajifurahisha navyo hapa
duniani.
Imepokelewa kuwa siku moja Hafs bin Abil Aas (Radhiya
Llaahu ‘anhu) alikuja kumtembelea Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamkuta anakula,
na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamkaribisha, lakini Hafs (Radhiya Llaahu
‘anhu) alipouona mkate mkavu alokuwa akila Umar huku akichovya ndani ya mafuta,
akakataa kulipa taabu tumbo lake, akamshukuru Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
lakini hakukikaribia chakula hicho.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuuliza;
“Kwa nini hutaki kula na
mimi?”
Hafs (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
“Chakula unachokula ni
kikavu na kigumu wakati mimi sasa hivi nitarudi nyumbani na kula chakula laini
nilichokwishatayarishiwa.”
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia:
“Unadhani mimi
nashindwa kuamrisha nikachinjiwa kijibuzi kidogo kikachunwa ngozi yake kisha
nikaamrisha iletwe ngano nyepesi nipate kupikiwa mikate laini, kisha niamrishe
ziletwe zabibu zitupwe juu ya samli inayokaangiwa nyama hiyo, kisha yamiminwe
maji juu yake mpaka yageuke rangi yake na kuwa nyekundu mfano wa damu ya paa,
kisha nikala hii (mikate na nyama) na kunywa ile (supu)?”
Hafs (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu:
“Wewe ni mjuzi wa
vyakula vizuri ewe Amiri wa Waumini”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaendelea;
“Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko
mikononi mwake; Ingelikuwa siogopi kupunguza thawabu zangu, ningekula kama
mnavyokula nyinyi, na kama ningetaka ningeishi maisha bora kuliko mnayoishi,
lakini kila nikiikumbuka Siku ambayo kila anayenyonesha atamsahau
anayemnyonesha na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake, nikaamua kuvibakiza
vizuri vyangu mpaka siku hiyo, kwani nimemsikia Mwenyezi Mungu akisema;
“Mlipoteza vitu vyenu vizuri katika maisha
yenu ya dunia (basi hamtavipata leo hapa) nyinyi mlijifurahisha navyo (huko)..”
Al Ahqaf – 20
Juu ya kuwa si haramu kula vyakula vizuri,
lakini huyu ni Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye hata
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alisema juu yake;
"Mkali katika dini ya Mwenyezi Mungu
kupita wote ni Umar."
Attirmidhy - Ibni Majah na
wengine
Ukhalifa
Katika tukio la Saqifa, siku aliyofariki
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa
sallam), Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikaribia kuwa Khalifa wa Waislamu wakati
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipomwambia;
“Lete mkono wako tufungamane nawe
ewe Umar”.
Lakini Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikataa
akauvuta mkono wake nyuma kwa nguvu na kusema;
“Bali wewe
ndiye tutakayefungamana naye, kwani wewe ni bora
kuliko mimi, haiwezekani mimi kuwa Khalifa wa watu, Abubakar akiwa ndani yao.’
Abubakar(Radhiya Llaahu
‘anhu) akasema;
“Wewe una nguvu kuliko mimi
ewe Umar”
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu;
“Ama Nguvu zangu ziko chini ya amri yako kwa ajili ya ubora wako”.
Akaunyanyua mkono wa
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kufungamana naye na Waislam wote mmoja baada
ya mwengine wakafungamana naye mahali hapo. Lakini Abubakar (Radhiya Llaahu
‘anhu) alipokuwa akifariki dunia, alimchaguwa Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) awe
Khalifa wa Waislamu baada yake, na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akakubali kwa
sababu Waislamu walikuwa na haja ya uongozi wa mtu wa nguvu zake na hekima
yake.
Mali hiyo si ya Umar wala si ya watu wa nyumba ya Umar
Siku moja uliwasili Madina msafara uliopitia
nchi mbali mbali, na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawauliza
watu wa msafara huo juu ya yale waliyokumbana nayo na kuyasikia wakiwa njiani,
wakamwambia;
“Ama katika mji fulani watu wanakuogopa sana
kwa ukali wako, na katika mji mwingine tumewaona watu wakikusanya mali
nyingi na kujitayarisha kuja hapa kukuletea, lakini katika mji fulani tumewaona
watu wacha Mungu wanakuombea dua wakisema ;
“Mola wetu tunakuomba umghufirie
Umar madhambi yake na umnyanyue daraja yake”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Ama wale wanaoniogopa, ingelikuwa
wananitakia kheri basi wasingeniogopa, na mali
hiyo inayokusanywa si ya Umar wala si ya watu wa nyumba ya Umar, bali ya baitul
maal ya Waislamu, na mimi sina chochote ndani yake, ama wale mlowasikia
wakiniombea dua bila mwenyewe kuwajua, hayo ndiyo ninayotarajia".
Alikuwa anapomuona mtoto mdogo njiani
humshika na kumwambia;
‘Niombee dua kwa
Mwenyezi Mungu, kwani wewe ni mdogo na bado huna dhambi, na dua yako
inakubaliwa’.
Kifo cha mnafiki
Abdullahi bin Ubey bin Salul, alikuwa
kiongozi wa wanafiki pale Madina, na aya nyingi
ziliteremshwa kuwajulisha Waislamu juu ya unafiki wake. Lakini Abdillahi huyu
alikuwa na mwanawe aitwae Abdillahi bin Abdillahi bin
Ubey bin Salul (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliyekuwa kipenzi cha Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), kinyume na babake.
Hebu tumsikilize Umar bin Khatwaab (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akituhadithia namna ilivyokuwa siku aliyofariki mnafiki huyo;
‘Alipokufa Abdullahi bin Ubey, Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliwaita watu waje kumsalia na
yeye alisimama mbele yetu, na alipotaka kuanza kumsalia nikasimama mbele yake
na kumwambia;
‘Unamsalia adui wa Mwenyezi
Mungu?' Nikawa namkumbusha kila ubaya aliomtendea, huku Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam)
akitabasamu. Na aliponiona nazidi kusema, akaniambia;
‘Nipishe ewe Umar, mimi nimehiyarishwa na
nikachagua, Mwenyezi Mungu ameniambia;
‘Ewe Mtume! Waombee msamaha (hao wanafiki) au usiwaombee; (yote sawa sawa) Hata
ukiwaombea msamaha mara sabini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe.’
At Tawba –80
Na kama
nikijua kuwa nikiongeza zaidi ya mara sabini atasamehewa, basi
ningeongeza".
Kisha Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamsalia na akalifuata jeneza lake
na kusimama kaburini pake.
‘Nikashangazwa kwa
kumwendea kwangu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam),
lakini Wallahi haujapita muda ikateremka aya ifuatayo;
‘Wala usimsalie kamwe mmoja wao
yoyote yule akifa, wala usisimame kaburini kwake (kumuombea dua).’
At Tawba -84
Hii ndiyo tabia ya Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu), ambaye anapohisi pana makosa hujaribu kuyasahihisha, lakini Mtume (Swalla
Llahu alayhi wa sallam) mwingi wa huruma alimhurumia
Abdillahi bin Ubay akamsalia na kumwombea dua huenda Mola wake akamsamehe. Umar
(Radhiya Llaahu ‘anhu) alijaribu kusema, lakini alinyamaza akatii na kusali nyuma yake baada ya Mtume (Swalla Llahu alayhi wa
sallam) kushikilia kuwa lazima amsalie.
Mwaka wa Ramada
Siku moja katika mwaka wa Ramada, mwaka
maarufu wa ukame na njaa kali iliyouwa watu wengi pale Madina, waliletwa ngamia
kutoka nchi ya Sham, na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaamrisha wachinjwe na
kugawiwa nyama yake.
Baada ya kumaliza kusimamia uchinjaji na
ugawaji wa nyama hiyo, na kurudi nyumbani kwake, Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
akaletewa na mtumishi wake vipande vizuri vya nyama vilivyochaguliwa kwa ajili
yake.
Umar akauliza;
‘Imetokea wapi nyama hii?’
Akaambiwa;
‘Katika wanyama waliochinjwa’
Akasema, huku akiisogeza upande nyama hiyo;
‘Ole wangu! Nitakuwa amiri gani mimi ikiwa nitakula vipande vizuri vya nyama
vilivyochaguliwa na kuwaachia watu kula mabaki yake?’
Akamwita mtumishi wake Aslam na kumwambia;
‘Ewe Aslam, ondoa chakula hiki na uniletee mkate wangu na mafuta ya kutolea’.
Baada ya juhudi kubwa aliyoifanya ya
kusimamia uchinjaji na ugawaji wa nyama siku ile, Umar
alistahiki kula vipande vizuri vya nyama ile, lakini yeye hakuona hivyo, bali
aliona kuwa Waislam ndio wenye kustahiki.
Alikuwa mkali zaidi kwa watu wa nyumba yake
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mkali
zaidi kwa watu wa nyumba yake kuliko kwa wengine kwa
kuhofia watu wasije wakasema kuwa Umar anawapendelea jamaa zake.
Alikuwa anapoweka kanuni mpya akiwakusanya
watu wake wa nyumbani na jamaa zake na kuwaambia;
‘Mimi nimewakataza watu kufanya
hivi au vile, na watu wanakutazameni mfano wa ndege wanavyoitazama nyama. Mkianguka na wao wanaanguka na mkinyanyuka wananyanyuka. Na mimi Wallahi nikiambiwa kuwa mmoja wenu ametenda katika yale
niliyoyakataza, basi nitamtia adabu mara mbili zaidi kuliko watu wengine. Kwa hivyo atakaye na afanye na atakaye na aache.”
Kwa hivyo kuwa jamaa yake Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) hakukuwa na maana kuwa mtu anaweza kufanya atakalo kisha
akasalimika, bali kinyume cha hivyo Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa
akiwanyima jamaa zake baadhi ya haki wanazopata watu wengine kama
ilivyokuwa katika kisa cha Abdillahi bin Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa
akijulikana kwa ucha Mungu wake.
Siku moja Umar(Radhiya
Llaahu ‘anhu), alipokuwa akitembea akaona ngamia wanene, waliohitilafiana na
wengine kwa uzuri wao.
Akauliza;
‘Ngamia wa nani hawa?”
Akaambiwa;
‘Ngamia wa Abdillahi bin Umar’.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alitetemeka huku
akishangaa, akasema;
‘Ole wako ewe mwana wa
Amiri wa Waislamu’.
Akatuma watu wamwitie Abdillahi (Radhiya
Llaahu ‘anhu), na alipowasili akamwambia;
‘Vipi ngamia hawa ewe Abdillahi’
Mwanawe akajibu;
‘Hawa ni ngamia
wangu, nimewanunua kwa pesa zangu mwenyewe na kuwapeleka malishoni ili wanenepe
na ili nipate kuwauza kama wanavyofanya
biashara Waislam wengine’.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu kwa ukali;
‘Ndiyo! Na watu
watasema ngamia hawa wa mtoto wa Amiri wa Waislamu kwa hivyo wachungeni vizuri
na walisheni majani mazuri, na kwa njia hii ngamia wako watanenepa na ngamia wa
wenzio watakonda, na wewe utapata faida kubwa kuliko wenzio’.
Kisha akasema;
‘Abdullahi, chukua ngamia wako nenda kawauze na uchukuwe rasilmali yako tu uliyonunulia ngamia hawa na
pesa zilizobaki zirudishe katika Baytul mal ya Waislam’.
Huyu ndiye Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
aliyekuwa akimuogopa Mwenyezi Mungu asije akamhesabia siku ya Kiama kuwa
aliwapendelea wanawe au jamaa zake na kwamba walikuwa
wakiitumilia fursa ile kwa kujineemesha wakati wenzao hawakuwa wakiipata fursa kama
ile.
Huyu ndiye Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye
siku moja alipokuwa akipokea mali kutoka katika miji
mbali mbali ya Kiislamu, binti yake Hafsa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimtania kwa
kumwambia;
‘Usitusahau watu wako, maana Mwenyezi
Mungu ameusia juu ya nasaba’.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu;
‘Mwanangu, haki ya nasaba katika mali yangu, ama hii ni mali
ya Waislamu, inuka nenda nyumbani kwako’.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alijifunza haya
kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu
alayhi wa sallam), aliyemuona mara nyingi akimwambia kipenzi chake, Fatima
l Batool (Radhiya Llaahu ‘anhu);
‘La ewe Fatima,
wapo Waislam wanaohitajia zaidi mali
hii.’
Hotuba yake ya mwanzo
Baada ya Waislam kufungamana naye na kumkubali kuwa Khalifa wao, Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
alipanda juu ya membari na kutoa hotuba yake ya mwanzo akasema;
“Ninasikia kuwa kuna watu
wanauogopa ukali wangu na ugumu wangu. Wanasema; 'Umar alikuwa mkali
wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu alipokuwa nasi, kisha akawa mkali zaidi wakati
Abubakar alipokuwa
Khalifa wetu. Atakuwaje leo wakati amri
yote ipo mikononi mwake?'
Anayesema hayo amesema kweli, kwani mimi nilikuwa msaidizi na mtumishi wa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ambaye hapana anayeweza kuufikia upole
wake na huruma zake na alikuwa kama
alivyosema Mwenyezi Mungu;
‘Kwa walioamini ni mpole na mwenye huruma’
Na mimi nilikuwa
kwake mfano wa upanga ulionolewa nikingoja amri zake. Nikaendelea kuwa naye
katika hali hiyo mpaka Mola wake alipomchukua akiwa ameridhika nami. Namshukuru
sana
Mwenyezi Mungu kwa ajili hiyo, na nina furaha sana
kwa ajili hiyo.
Kisha Abubakar akapewa Ukhalifa, na alikuwa
kama mnavyomjuwa ukarimu wake na upole wake, na mimi nilikuwa mtumishi wake na
msaidizi wake nikichanganya ukali wangu kwa upole wake na nilikuwa mfano wa
upanga wake ulionolewa nikingoja amri zake, na nikaendelea kuwa naye katika
hali hiyo, mpaka Mola wake alipomchukua akiwa ameridhika nami. Namshukuru
Mwenyezi Mungu na nina furaha sana
kwa ajili hiyo.
Kisha nikakabidhiwa mimi
Ukhalifa, basi mjue kuwa ukali ule umeongezeka, lakini utakuwa kwa wale
madhalimu na wanaokiuka mipaka. Ama wale watu wa
usalama na dini na mwenendo mwema, mimi nitakuwa laini kwao kuliko ulaini wao
baina yao, na
sitomuacha mtu amdhulumu mwenzake au apindukie mipaka katika kuwaudhi wenzake.
Na atakayefanya hivyo nitauchukua uso wake na kuuweka
juu ya ardhi mpaka aikubali haki, kisha baada ya ukali wangu huo nitauweka uso
wangu mimi juu ya ardhi kwa wale walio wapole na wasiopindukia mipaka.
Na kwangu mimi kuna
haki zenu zisikilizeni vizuri;
Juu yangu nisikuchukulieni chochote katika
haki zenu ila kwa haki yake. Na ni
juu yangu kila kinachoingia mkononi mwangu, kisitoke isipokuwa pale
panapostahiki. Ni juu yangu kujitahidi ili mapato yenu
yaongezeke Inshaallah, ni juu yangu kuziba pengo zenu (kuondoa shida zenu). Na ni juu yangu nisikutieni katika maangamizo, na mnapokuwa
vitani basi mimi ni baba wa watoto wenu mpaka mtakaporudi…..
Kwa hivyo mcheni Mungu na
munisaidie katika nafsi zenu na munisaidie katika nafsi yangu katika kuamrisha
mema na kukataza maovu na kuninasihi katika yale aliyonipa Mwenyezi Mungu
katika kukuongozeni.”
Nitamlipia kisasi chake
Katika kila msimu wa
Hija, Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), alikuwa akiwatangazia mahujaji wanaokuja
kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu, kwa kuwaambia;
"Enyi watu! Mimi siwatumi
magavana kwenu kwa ajili ya kukupigeni wala siwaleti
ili wachukue mali
zenu, bali nawaleta wakufunzeni dini yenu na mafundisho ya Mtume wenu (Swalla
Llahu alayhi wa sallam). Kwa hivyo yeyote aliyetendewa kinyume na hayo alete malalamiko yake kwangu. Na
mimi Wallahi nitamlipia kisasi chake".
Mmoja katika Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu)
akamuuliza;
"Iwapo mmoja katika magavana
uliowaweka kampiga mtu, ndiyo kweli utalipa kisasi cha aliyepigwa?"
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu;
‘Ndiyo! Nitafanya
hivyo, kwani mimi nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llahu alayhi wa sallam) akisema;
"Kama
yupo kati yenu niliyempiga mgongoni pake, basi mgongo wangu huu hapa na aje
kulipa kisasi chake."
Na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) huwa
anakusudia yale anayoyasema, kwa sababu siku moja
alipotembelewa na watu kutoka mji wa Hims – Syria,
aliwauliza juu ya gavana wao huko aitwaye Abdullah bin Qurt (Radhiya Llaahu
‘anhu), wakasema;
‘Ni mtu mwema isipokuwa amejijengea jumba la
fahari’
Jumba la fahari! anajifaharisha
mbele ya watu kwa kujijengea jumba la fahari wakati Waislam wanatafuta tonge ya
kuzuwia njaa?
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamtuma mjumbe
kwenda mji wa Hums na kumwambia;
"Kahakikishe juu ya jambo hili, na ikiwa ni kweli basi ianze hiyo nyumba, choma moto mlango
wake, kisha njoo naye Amiri huyo".
Mjumbe akaifunga safari mpaka mji wa Hums na
kurudi na Abdillahi bin Qurt (Radhiya Llaahu ‘anhu) mpaka kwa Umar bin Khatwaab
(Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekataa kumkabili gavana huyo muda wa siku tatu,
kisha akamtaka akutane naye panapo zizi la ngamia na kondoo wa sadaka.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamtaka Amiri
huyo avue nguo za thamani alizovaa na badala yake avae
nguo za wachungaji, kisha akampa bakora na kumwambia;
‘Nguo hizi ni bora kuliko
alizokuwa akivaa baba yako na fimbo hii ni bora kuliko ile ulokuwa ukiichungia
kondoo. Wafuate ngamia hawa na wachunge ewe Abdullah’.
Baada ya kupita siku tatu akamwita na kumuuliza;
"Kwani mimi
nilikupa ugavana na kukupeleka huko kwa ajili ya kujijengea majumba na
kujiimarisha? Rudi katika kazi yako lakini usirudie tena
uliyofanya".
Alimetendea haya gavana ambaye watu wake
walishuhudia kuwa ni mtu mwema isipokuwa tu
alijijengea jumba zuri la fahari kwa ajili ya nafsi yake.
Mimi ni bora kuliko wewe
Huyu ndiye Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye
siku moja alipopata mashtaka kutoka kwa kijana wa
Kimisri aliyekuwa katika dini ya Kinasara kuwa alipigwa bakora na Muhammad
mwana wa Amru bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) gavana wa Misri kwa sababu
alimshinda katika mashindano ya mbio, na baada ya kumtandika bakora akamwambia;
‘Mimi ni bora kuliko wewe’.
Amr bin Al Aas huyu (Radhiya Llaahu ‘anhu),
ndiye aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Kiislam yaliyoiteka
nchi ya Misri na hatimaye akapewa yeye ugavana wa nchi hiyo.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamtaka Amr bin
Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) aje Madina, yeye pamoja na
mwanawe Muhammad.
Hebu tumsikilize Anas bin Malik (Radhiya
Llaahu ‘anhu), akituhadithia jinsi mambo yalivyokuwa siku hiyo. Anasema Anas (Radhiya
Llaahu ‘anhu);
‘Wallahi tulikuwa tumekaa kwa
Umar, mara Amru bin Aas akatokea akiwa amevaa saruni na nguo ya juu, na Umar
akawa anageuka huku na kule kumtafuta mwanawe Muhammad aliyekuwa nyuma ya baba
yake.
Umar akauliza;
‘Yuko wapi Mmisri?’
Mmisri akasema;
“Mimi niko hapa ewe Amiri wa
Waislamu.”
Umar akamwambia;
“Chukua bakora hii umtandike huyo ‘Aliye bora'
Akamtandika bakora huku Umar akimwambia;
“Endelea kumpiga huyo ‘Aliye bora”
Kisha Umar akamwambia yule kijana wa Misri;
“Sasa mtandike bakora baba yake,
kwa sababu mwanawe asingekupiga isipokuwa kwa kuwa anaendekezwa na baba yake”.
Yule Mtu wa Misri
akasema;
“Ewe Amiri wa Waumini, nimekwisha
piga na kulipiza kisasi changu kiasi cha kutosha kwa kumpiga yule aliyenipiga”.
Umar akamgeukia Amru na
kumwambia;
“Ewe Amru, tokea lini mnawageuza
watu kuwa watumwa na hali wamezaliwa na wazee wao wakiwa huru?”
Huyu ni Amru bin Al Aas mkuu wa jimbo kubwa
kabisa katika majimbo yanayohukumiwa na dola ya Kiislamu, na mwanawe hajaweza
kuepukana na uadilifu wa Umar bin Khatwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu), bali hata yeye
mwenyewe aliponea chupu chupu kutandikwa bakora, na hii ni kwa sababu ya
kusamehewa na yule aliyeonewa.
Matumizi yake
Anasema Abdullahi bin Amer bin Rabia (Radhiya
Llaahu ‘anhu);
Nilifuatana na Umar
bin Khatwaab kutoka Madina hadi Makka katika safari ya Hija kisha nikarudi
naye. Wallahi sikumwona akipigiwa hema la fahari wala akikaa ndani ya jengo, bali alikuwa akijikinga na jua kwa kutandaza kitambaa juu ya
mti na kulala chini yake.
Ama Bashaar bin Namir (Radhiya Llaahu ‘anhu)
yeye anasema;
“……Kisha Umar akaniuliza;
‘Kiasi gani tulichotumia katika
Haji yetu?’
Nikamjibu;
‘Dinari kumi na tano’
Akasema;
‘Tumefanya israfu katika mali
hii’
Walipotambua kuwa inambidi Umar akope ili
aweze kuendesha maisha yake vizuri, masahaba wakubwa kama
Othman, Ali, Talha na Al Zubeir (RAnhum) wakakutana na kuamua kumtuma binti
yake Hafsa (Radhiya Llaahu ‘anhu) amshauri na kumkinaisha baba yake akubali
kuongeza mshahara wake kutoka nyumba ya mali
ya Waislam.
Umar akamuuliza binti yake;
‘Nani aliyekutuma?’
Bibi Hafsa akamwambia;
‘Mimi naona hivyo.’
Umar akamwambia;
‘Bali
kuna watu waliokutuma.’
Kisha akamuuliza mwanawe;
‘Mwanangu wewe ulikuwa mke wa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), nyumbani kwake alikuwa akivaa
nini?.
Akasema;
‘Nguo mbili tu alikuwa nazo’
Akasema;
‘Na kipi katika vyakula vizuri
mlichokuwa mkila?’
Akajibu;
‘Mkate wa ngano
tukiivuruga ndani ya mafuta au samli."
Akamuuliza tena;
‘Kitambaa gani cha thamani alichokuwa nacho
nyumbani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi
wa sallam)?
Akajibu;
‘Nguo moja nzito, tulikuwa
tukiitandika chini siku za joto na katika siku za baridi tukiigawa kwa
kuitandika nusu chini na nusu nyingine tukijifunikia’.
Kisha akasema;
‘Ewe Hafsa, waambie waliokutuma kuwa; mfano
wangu na mfano wa sahibu zangu wawili Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu), ni mfano wa watu watatu waliotembea njia moja,
wa kwanza amewasili pamoja na zawadi alizotakiwa achukuwe, na wapili akapita
njia hiyo hiyo na akawasili pamoja na zawadi inayotakikana, kwa hivyo wa tatu
wao akiifuata njia ya wawili hao na kuridhika na zawadi kama yao basi atakutana
nao. Ama akifuata njia nyengne isiyokuwa yao
hatokutana nao’.
Mashauriano (Shura)
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akipenda
kushauriana na kusikiliza rai za wengine katika kila
dogo na kubwa, wala hakuwa akipenda kuwahukumu watu kwa mabavu.
Alikuwa akitumia hekima ya hali ya juu na kusikiliza ushauri wao katika mambo yote ya kimaisha,
isipokuwa katika mambo mengine hasa yale aliyokuwa akimuona Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akiyatenda. Hayo alikuwa akiyafuata bila
kurudi nyuma hata kama
alikuwa haijui hekima iliyo ndani yake.
Alikuwa kwa mfano akilibusu
jiwe jeusi la Al Kaaba huku akiliambia;
‘Najua wewe ni jiwe
tu, hudhuru wala hunufaishi, na lau kama
nisingemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akikubusu
basi nisingekubusu’.
Anapotufu alikuwa akienda mbio huku akiliacha
wazi bega lake la upande wa kulia huku akisema;
‘Sisi tulikuwa tukikimbia na
hatukuwa tukiyafunika mabega haya wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llahu alayhi wa sallam) aliyetutaka tufanye hivyo kwa ajili ya kuwaonesha
makafiri kuwa hatuna maradhi waliyokuwa wakitusingizia, na kuwaonesha kuwa sisi
tuna nguvu za kutosha. Lakini sasa Uislamu ushaenea na
ukafiri ushaondoka, juu ya hayo siwezi kuacha jambo tuliokuwa tukilitenda
wakati wa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam).”
Alikuwa anapoisoma kauli ya Mwenyezi Mungu;
‘Wa dhaariati dharwa falhaamilati wiqra,’
akisema;
"Wadhaariati dharwa, maana yake ni Upepo, na kama
nisingemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akisema
hivyo basi nisingesema. Falhaamilati wiqra, maana yake ni
Mawingu, na kama nisingemsikia Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akisema hivyo basi nisingesema.”
Alikuwa akihuzunika anapoona watu
wanaogopa kumtoa makosa anapokosea au kumnasihi pale anapohitajia nasaha.
Siku moja Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa
akimsikitikia sahaba Hudhaifa (Radhiya Llaahu ‘anhu) juu ya uamuzi alioutowa wa kutowapa ardhi za kilimo wapiganaji Jihadi, hasa zile
ardhi za kilimo zilizotekwa na Waislam katika nchi ya Fursi (Iran)
baada ya kutekwa kwa nchi hiyo. Alitaka zibaki vile vile zikimilikiwa na wenye ardhi zao watakaokuwa wakitoa malipo maalumu
yatakayokwenda katika Nyumba ya mali
ya Waislam, na kwa njia hiyo watu watafaidika zaidi.
Alikuwa akiona pia kuwa kuwagawia ardhi
wanaopigana Jihadi kutawafanya waiache kazi hiyo muhimu na
kujishughulisha na mambo ya kidunia.
Baadhi ya watu hawakuridhika na rai hiyo, na
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipotaka ushauri wa watu wanaojulikana kwa hekima,
wote wakamuunga mkono Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) katika uamuzi wake.
Jambo hilo
lilimhuzunisha Umar(Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyedhani kuwa watu wanaogopa kutoa
rai zao, ndipo alipomwita Hudhaifa (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumsikitikia, na
Hudhaifa (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu;
“Wallahi kama tukikuona umeiacha
haki na kwenda upande, basi sisi tutakurudisha tena katika haki ewe Umar”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alifurahi sana kwa kauli hiyo akasema;
“Namshukuru Mungu kuwa nina
marafiki watakaonirejesha katika haki iwapo nitaiendea kombo.”
Siku moja alipanda juu ya membari na kuhutubia watu akisema;
“Enyi Waislam, mtasema nini iwapo
nitakigeuzia dunia kichwa changu hivi?" Mtu mmoja akainuka na kutangulia mbele huku akiunyosha upanga wake na kuutikisa
huku akimuambia;
“Ukifanya hivyo, basi na sisi
tutakwambia kwa panga zetu hivi”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
‘Unanikusudia mimi
maneno hayo?’
Yule mtu akasema;
“Naam ni wewe niliyekukusidia”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema:
“Mwenyezi Mungu akurehemu,
Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyejaalia miongoni mwenu atakayeniweka sawa pindipo
nikienda upande”.
Umar(Radhiya Llaahu ‘anhu), hakuwa akitamka
haya kwa ajili ya kujionesha tu, kwani alikuwa na nguvu pamoja na kuaminika
kiasi ambacho hakuwa na haja ya kufanya mambo kwa kutaka kujionesha, bali huu
ulikuwa ni mwenendo wake wa kweli, na tabia yake ya kweli ya kuipenda haki.
Alikuwa pale anapokosolewa, hupenda kuitamka
kauli maarufu ifuatayo;
‘Mwenyezi Mungu amrehemu mja aliyenipa zawadi
makosa yangu’
Kwake yeye, anapotolewa makosa huona kama amepewa zawadi, na kwa ajili hiyo
humshukuru yule aliyemkosoa na kumuombea rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Siku moja alipanda juu ya membari, na baada ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume wake (Swalla
Llahu alayhi wa sallam), akaanza kuhutubia kwa kusema;
“Sikilizeni, Mwenyezi Mungu awarehemu”
Mmoja katika Waislam waliohudhuria akainuka na kusema:
“Wallahi hatukusikilizi Wallahi
hatukusikilizi”
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuuliza;
“Kwa nini hunisikilizi ewe
Suleiman?”
Suleiman (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Kwa sababu umejipendelea nafsi
yako, umetugawia kila mmoja wetu kitambaa kimoja na wewe umejichukulia viwili”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), akawa anatafuta
baina ya watu, kisha akauliza:
“Yu wapi Abdullahi bin Umar”
(mwanawe).
Abdillahi bin Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
akainuka na kusema;
“Ni mimi hapa ewe
Amiri wa Waislam”.
Umar, akasema:
“Mimi kama mjuavyo ni mrefu, na
kitambaa nilichopata hakijanitosha, na Abdullahi mwanangu akanipa kitambaa
chake nikakiunganisha na changu”.
Suleiman (Radhiya Llaahu ‘anhu), akasema huku
machozi yakimlenga:
“Alhamdulillah, sasa tutakusikiliza ewe Amiri
wa Waumini”.
Hapana mfalme wala kiongozi yeyote duniani
aliyewapa watu uhuru kama huu, akaruhusu kuhojiwa hata juu ya nguo aliyovaa
mbele ya umma kama ule na kwa lugha kali kama ile juu ya kuwa Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) wakati huo hakuwa akiitawala Bara ya Arabu peke yake, bali
alikuwa Khalifa wa Dola ya Kiislamu inayotawala Bara ya Arabu yote na sehemu
kubwa ya Asia na Afrika.
Na kwa nini asifanye
hivyo wakati yeye ni mwanafunzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi
wa sallam) aliyemuona siku moja akiambiwa na mbedui;
“Nipe, kwani mali
hii si mali
yako na ufalme huu si wako”
Na Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alitabasamu kisha akamwambia mbedui yule:
“Umesema kweli, kwa
hakika mali
hii ni ya Mwenyezi Mungu”.
Na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipotaka
kumvamia mbedui yule, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llahu alayhi wa sallam) akamzuwia na kumwambia;
“Mwache ewe Umar, mwenye haki
yake ana haki ya kusema”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliupenda na kuufuata mwenendo huu wa kipenzi chake, mbora wa viumbe
vyote, Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam).
Aliupenda na
kuufuata, na akawajulisha umma kuwa kushauriana ndiyo njia ya kunyanyuka kwa
Umma.
Na wao walifahamu vizuri kuwa kiongozi wao
alikuwa akikusudia kuwapa uhuru wa kutoa rai zao, na
kwamba hilo
halikuwa jambo la mzaha au la kupita njia.
Huyu ndiye Khaula bint al Hakim
Siku moja Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
alipokuwa akitembea akiwa amefuatana na Al Jaarod,
alitokea bibi mmoja aliyemwita Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa sauti kubwa huku
akisema;
“Tembea taratibu ewe Umar ili
niweze kukufikia na kukuambia maneno machache”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akageuka
kumtazama bibi huyo, na alipomuona alisimama na
kumsubiri huku akitabasamu.
Bibi akasema;
“Umar, mimi nakujua
wewe tokea ulipokuwa ukiitwa Umayr (kwa kulidogosha jina la Umar), ulipokuwa
ukipigana mieleka katika soko la Ukhadh, hazikupita siku ukawa unaitwa Umar,
kisha hazikupita siku nyingi ukawa unaitwa Amiri wa Waislamu, kwa hivyo Muogope
Mwenyezi Mungu katika raia zako…..”
Al Jarood aliyekuwa amefuatana na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia yule bibi;
“Umevuka mpaka katika maneno yako na Amiri wa Waislamu.”
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), akamwambia;
“Muache aseme, kwani wewe humjuwi
nani huyu? Huyu ndiye Khaula bint Al Hakim ambaye Mwenyezi Mungu ameyasikia maneno
yake akiwa juu ya mbingu Zake saba alipokuwa
akijadiliana na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) juu ya mumewe, Basi Umar
ni nani hata akatae kusikiliza kauli yake?”
(Kwa ajili ya bibi huyu Mwenyezi Mungu hapo
mwanzo aliteremsha aya nne za mwanzo za Suratu l
Mujadilah “Qad samia”).
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliupa umma kila
tumaini, kila nafasi na kila haki ili watu wajue kuwa wanao
uhuru na kwamba kila mmoja anayo haki ya kusema na ya kutoa ushauri na kumkosoa
yeyote katika viongozi, hata kama kiongozi
huyo ni Amiri wa Waislamu. Hii ni kwa sababu uhuru ni
jambo jepesi kabisa; nalo ni kila mtu kuipata haki yake na awe na uhuru wa
kuidai haki hiyo popote alipo.
Na kwa vile haki
haimilikiwi na mtu mmoja au kundi fulani, au haijulikani na mtu mmoja tu au na
kundi Fulani, kila mmoja alikuwa na haki ya kuifuata njia hiyo.
Siku moja mtu mmoja alikuwa akijadiliana na Umar huku akiwa ameshikilia hoja yake kuwa ni sawa na
kwamba hoja ya Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) haikuwa sawa. Akawa anamwambia:
“Ittaqi llah yaa Umar – (Muogope
Mwenyezi Mungu ewe Umar).” Akawa anayakariri maneno hayo,
huku wenzake wakimwambia;
“Basi inatosha, unazidisha tena kubishana na Amiri wa Waislamu”.
Umar akasema;
“Mwacheni aseme. Hamtakuwa na kheri iwapo hamtosema, na hatutakuwa na kheri iwapo
hatutasikiliza”.
Na hii ni kauli ya
haki kabisa, kwani watu hawatakuwa na kheri ikiwa wataogopa kusema ukweli, na
viongozi hawatakuwa na kheri ikiwa watakataa kusikiliza.
Kuupanua msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam)
Siku moja Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
alimwendea Al Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) ami yake Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia;
“Niliwahi kumsikia Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akisema kuwa anataka kuupanua
msikiti, na kwa vile nyumba yako ipo karibu zaidi na msikiti basi naona bora
ujitolee ili tuweze kuifanya kazi hii, na badala yake tutakupa ardhi kubwa
zaidi”.
Al Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Sitofanya hivyo”
Umar akamwambia;
“Kwa hivyo itanibidi
nikulazimishe.”
Al Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Huna haki ya kunilazimisha. Tumtafute mtu ahukumu baina yetu kwa haki”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuuliza;
“Unamchagua nani atuhukumie baina yetu?”.
Al Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Hudhaifa bin Al Yamani”.
Umar na Al Abbas (R Anhum), wakamwendea Hudhaifa
nyumbani kwake ili ahukumu baina yao, na kwa ajili hiyo ufalme wa Hudhaifa (Radhiya
Llaahu ‘anhu) utakuwa mkubwa zaidi kupita ule wa Amiri wa Waislamu kwa sababu
watalazimika yeye na Al Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuukubali uamuzi wowote
atakaouamua.
Kwa msemo wa kisasa
tutasema; Hudhaifa atakuwa kadhi baina ya mtu anayeiwakilisha Serikali ambaye
ni Umar, dhidi ya mmoja kati ya wananchi ambaye ni Al Abbas (Radhiyallahu
anhum).
Baada ya kuwakaribisha na
kusikiliza maneno ya pande zote mbili Hudhaifa (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Nilisikia kuwa Nabii Daud (AS) alitaka
kuupanua msikiti wa Baytul Maqdis na kulikuwa na
nyumba ya yatima karibu na msikiti huo. Nabii Daud (AS) akataka kuichukua
nyumba hiyo kwa nguvu ili aibomoe na kuiunganisha na
msikiti, lakini Mwenyezi Mungu akamfunulia wahyi kuwa;
'Nyumba iliyotakasika na dhulma
ni nyumba yangu,' Nabii Daud (AS), akaamua kumrudishia yatima huyo nyumba yake."
Al Abbas akamtazama Umar na
kumuuliza;
‘Bado unataka kuichukua nyumba
yangu?’
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“La, sitaki tena.”
Al Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
“Sasa kwa hiari
yangu nakupa nyumba yangu ili uweze kuupanua msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llahu alayhi wa sallam)."
Mwenye kipaji na hekima
Mwenye kupewa hekima basi amepata kheri
nyingi sana,
na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema;
"Miongoni mwa waliokuja kabla yenu
walikuwepo watu wenye kufunuliwa bila ya wao kuwa ni
mitume. Ikiwa katika umma wangu wapo wenye mfano wao, basi
atakuwa Umar".
Bukhari- Muslim na
Attarmidhiy
Katika kauli zake za hekima, ni pale alipomsikia mtu akimsifia mwenzake kuwa ni madhubuti
na mwaminifu, na Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuuliza;
“Ushawahi kusafiri naye?”
Akasema;
“La, sijawahi”
“Uliwahi kugombana naye?”
“La, sijawahi”
“Uliwahi kumwaminisha mali?”
“La”
"Basi usimpe mtu sifa ya umadhubuti ikiwa hukumshuhudia
akipapambana na mitihani."
Usiku umekuwa mrefu
Inajulikana kuwa Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akipenda kutoka
nyakati za usiku kwa ajili ya kuchunguza hali za raia
wake, na usiku mmoja alipokuwa katika hali hiyo alimsikia mwanamke akiwa
nyumbani kwake akihuzunika huku akisema kwa sauti kubwa;
“Usiku umekuwa mrefu na mume wangu hayupo, Wallahi
ningekuwa simuogopi Mwenyezi Mungu ningekitingisha kitanda changu hiki kila
pembe. Lakini kumuogopa
Mola wangu na wingi haya zangu pamoja na kuilinda
heshima ya mume wangu kunanizuwia nisifanye hivyo”.
Kisha mwanamke huyo akaendelea kusema;
“Hivyo Umar anaona ni jambo jepesi kunifarikisha na mume
wangu?”
Asubuhi iliyofuata Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa binti yake Hafsa (Radhiya Llaahu
‘anhu), akamuuliza;
“Ewe Hafsa, mwanamke anaweza kustahamili kuwa mbali na
mumewe kiasi cha muda gani?”
Hafsa (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
“Mwezi, miezi miwili, mitatu, mwezi wa nne
subira inaanza kutoweka”.
Kuanzia siku hiyo Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaweka kanuni ya kuwa
askari yeyote aliyekuwa mbali na nchi yake kwa ajili
ya kupigana jihadi, aruhusiwe kurudi nyumbani kwake kila baada ya miezi mine.
Na alipomsikia mtu mzima mmoja akisikitika kuwa siku nyingi zishapita
hajamuona mwanawe wa pekee aliyekwenda kupigana Jihadi, Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu) akaamrisha mwanawe huyo arudishwe haraka kwa mzee wake, na akaweka
kanuni kuwa asiruhusiwe mtu yeyote kwenda kupigana Jihadi iwapo ana wazee
wawili watu wazima, au hata mmoja, isipokuwa baada ya idhini yao.
Umar ni kipaji cha
hekima kinachofanya kazi kimaumbile na kinachoweka kanuni zinazonasibiana na
hali za watu.
Namna ya kuhukumu baina ya watu
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimuandikia Abu
Musa Al Ash ary (Radhiya Llaahu ‘anhu) yafuatayo akimfundisha hekima za
kuhukumu baina ya watu kwa uadilifu;
“Kutoka kwa Mja wa
Mwenyezi Mungu Amiri wa Waislamu, kwa Abdullahi bin Qays, kwa hakika kuhukumu
baina ya watu ni fardhi iliyo wazi na mwenendo unaowajibika kufuatwa. Sikiliza
vizuri na ufahamu pale unapotolewa ushahidi, na uamue
unapokubainikia ukweli, kwani uamuzi bila ya haki hauna faida. Wapoze watu katika vikao vyako. Mwenye kudai anawajibika
kutoa ushahidi, na mwenye kukanusha anawajibika kula
kiapo.
Suluhu ni bora baina
ya Waislamu, lakini isiwe suluhu inayohalalisha haramu na kuharamisha halali.
Usije ukakuzuwia uamuzi uliouamua jana, kisha Mwenyezi Mungu akakuongoza ukatambua kuwa
ulikosea katika uamuzi ule, ukakufanya uogope kuiweka sawa haki, kwani haki ni
haki na haibatilishwi na chochote. Na kuirudisha haki kwa
wenyewe ni bora kwako kuliko kuendelea kuinyamazia batili.
Ushahidi wa Waislamu
baina yao ni
haki, isipokuwa yule aliyewahi kuhukumiwa kupigwa mjeledi kwa kosa kubwa au
aliyewahi kutoa ushahidi wa uwongo au anayetiliwa shaka kwa sababu ya
kumpendelea mshitaki au mshitakiwa kwa ajili ya undugu wa nasaba, (hawa
ushahidi wao haukubaliwi). Mwenyezi Mungu ndiye ajuwaye siri
za moyoni.
Usiwatishe watu au kuingiza uoga nyoyoni
mwao, kwani yule anayeihusisha nia kwa ajili ya
kumridhisha Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu anamtosheleza. Ama mwenye kuamua
kinyume na haki kwa ajili ya kutaka kujipendekeza kwa
watu, Mwenyezi Mungu humuacha alivyo, na iko siku atamfedhehesha. Unaonaje si
bora mtu azikimbilie thawabu za Mola wake na Rehema
Zake?
Wassalaam”.
Mtu wa aina hii,
muadilifu, mcha Mungu, mwaminifu, mwenye kipaji cha hekima na nguvu pamoja na
kuwa yeye ni khalifa wa Waislamu anayehukumu Mashariki ya ardhi na Magharibi
yake, asiyechaguwa pa kukaa, bali hukaa popote inapomalizika safari yake,
analala popote, ikiwa ni juu ya mchanga, chini ya mti au juu ya rundu la
majani. Anakula anachokipata, ikiwa ni kipande cha
mkate kwa nyama au mara nyingine hutolea mafuta au samli.
Huwa na furaha
anapomsikia mtoto au mtu yeyote akimwita kwa jina lake;’Ewe Umar’.
Hufurahi pale anapomuona mzee akijaribu
kubeba mzigo mzito kisha akatangulia yeye na kumbebea
mzigo ule mpaka nyumbani kwake kisha mzee yule akasema;
“Mwenyezi Mungu akujaze kheri ewe
mwanangu, wewe unastahiki kuwa Khalifa kuliko Umar”.
Jambo ambalo wafalme
wangelilisikia basi wangemuonea husuda.
Mpe habari sahibu yako kuwa amepata mtoto wa kiume
Usiku mmoja alipokuwa katika matembezi yake
ya kusikiliza shida za raia alifika sehemu za nje ya mji wanapoishi mabedui, na akawa anasikia sauti ya mwanamke akilia kwa maumivu.
Alipoelewa kuwa kinachomliza ni uchungu wa uzazi na
kwamba hana mtu wa kumsaidia isipokuwa mumewe, Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
akarudi nyumbani kwake na kumwambia mkewe Ummu Kulthum binti wa Imam Ali bin
Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu);
“Tuna chochote nyumbani mwetu?”
Mkewe (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza;
“Kuna nini?”
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
“Mwanamke mbedui anazaa na hana
wa kumsaidia”.
Ummu Kulthum (Radhiya Llaahu ‘anhu)
akamwambia;
“Naam tunacho ukitaka.”
Umar na mkewe (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakaanza
kukusanya unga, samli, sukari na baadhi ya mahitaji, kisha wakaondoka na
kufuatana mpaka penye hema la mzazi, na Ummu Kulthum (Radhiya Llaahu ‘anhu)
akaingia ndani ya hema na Umar akabaki nje pamoja na mume wa mzazi, akawasha
moto kwa ajili ya kuwapikia kitakachoweza kumsaidia mzazi huku mume wa mzazi
akimshukuru.
Bada ya mzazi kujifungua, Ummu Kulthum (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akachungulia nje na kumwambia Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu);
“Ewe Amiri wa Waislamu, mpe
habari sahibu yako kuwa amepata mtoto wa kiume.”
Kauli hii ilimsitua mbedui aliyeinuka kwa mshangao huku akionesha kuona haya huku akijaribu
kutamka neno lolote lile baada ya kujua kuwa Khalifa wa Waislamu pamoja na
mkewe ndio waliokuwa wakiwatumikia usiku kucha.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
“Baki hapo hapo ulipo wala
usisituke."
Kisha Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akinyanyua
chungu kilichokuwa na chakula na kukisogeza mlangoni
na kumwita mkewe;
“Ewe Ummu Kulthum nipokee chungu
hiki ili umlishe mama na mwache ashibe sawa sawa”.
Ummu Kulthum (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamlisha
mama yule na baada ya kushiba akakirudisha chungu kile
kwa Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliyekiweka mbele ya baba na kumwambia;
“Kula, maana wewe umekesha usiku
kucha na bila shaka una njaa”.
Kisha akaondoka yeye na
mkewe kurudi nyumbani huku akimwambia yule mtu;
“Kesho njoo mjini ili
niamrishe upewe katika mali
kiasi cha kukusaidia wewe, na ili mtoto mchanga awe analipwa haki yake”.
Kifo chake
Ilikuwa siku ya Ijumaa wakati Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu) alipopanda juu ya membari akampwekesha Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume wake (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kisha
akasema;
“Nimeota ndoto, na sioni tafsiri
nyengine isipokuwa ajali yangu imeshakaribia. Nimeota jogoo mwekundu ananidokoa mara mbili kichwani pangu.”
Kisha akazungumza juu ya Khalifa atakayekuja
baada yake, akasema;
“Watu wananitaka nimchague Khalifa, na Mwenyezi Mungu hataipoteza dini yake wala Ukhalifa wake
kwa kuondoka kwangu mimi duniani, Ushauriano juu ya nani atakayekuwa Khalifa
baada yangu uwe kati ya watu hawa sita ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llahu alayhi wa sallam) alipokufa alikuwa radhi nao. Na yeyote kati yao mtakayefungamana naye basi lazima
mumsikilize na kumtii, nami najua kuwa wapo watakaonilaumu juu ya uamuzi wangu
huu, watu hao mimi nilipambana nao kwa upanga wangu huu hata wakaingia katika
Uislamu”.
Hotuba hiyo ilikuwa siku ya Ijumaa na aliuliwa siku ya Jumatano na mmajusi mmoja (mwenye
kuabudu moto) aitwaye Abu Luu lua Al Majusiy, wakati alipokuwa akisalisha watu
Sala ya Alfajiri.
Abu Luu lua huyu aliyekuwa na jambia
alilolipaka sumu, aliingia msikitini akijificha kwa kiza wakati wa Sala ya
Alfajiri na wakati ule hakukuwa na taa za kutosha kama ilivyo hivi sasa, na
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakati huo alikuwa kesha funga Sala na kuanza
kusoma baadhi ya Sura, na Abu Luu lua akamsogelea na kumpiga jambia mara tatu,
moja wapo chini ya kitovu, na hiyo ndiyo iliyomuuwa Simba huyu wa Waislamu (Radhiya
Llaahu ‘anhu) katika uwanja wake wa Ibada.
Abu Luu lua akafanikiwa kuwauwa masahaba
wengine saba na kuwajeruhi sita walipojaribu kumkamata na hatimaye mmoja katika
Masahaba aitwaye Huttan Al Tamimi (Radhiya Llaahu ‘anhu) alifanikiwa kumrushia
guo lake usoni na kumfunika nalo, na alipoona kuwa kesha wezwa akajiuwa
mwenyewe kwa kujipiga na jambia lake aliyolipaka sumu.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokuwa
akianguka alimvuta nguo Abdulrahman bin Auf (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa
nyuma yake na kumtaka akamilishe Sala.
Anasema mwanawe Abdillahi bin Umar (Radhiya
Llaahu ‘anhu);
“Kabla ya kufariki kwake, kichwa cha babangu
kilikuwa juu ya paja langu, akaniambia;
‘Abdullah! kiweke kichwa changu juu ya ardhi huenda Mola wangu akikiona
juu ya ardhi akanionea huruma’.
Kiongozi mfano wa
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyeweza kuzivunja vunja nguvu za Warumi na
Wafursi, dola mbili kubwa za wakati huo, pamoja na kuweza kuwatoa Mayahudi nje
ya Bara ya Arabu. Kwa sababu hizi mamilioni ya watu wakaingia
katika dini hii ya Mwenyezi Mungu. Mtu wa aina
hii hakosi kuwa na maadui katika kila pembe ya ulimwengu wanaochukizwa na
mafanikio yake.
Hakukuwa na jeshi
lolote lililoweza kusimama mbele ya majeshi yake, lakini makhabithi waliweza
kuwachomeka watu wao katika sehemu mbali mbali ili kuizuwia nguvu hiyo, na juu
ya hayo, juu ya kifo cha Shahada alichotunukiwa na Mola wake, Makhalifa
waongofu waliokuja baada yake waliweza kuiendeleza kazi hiyo na kuinyanyua
bendera ya Laa ilaaha illa Llah.
Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye ni bin ammi yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi
wa sallam) alikuwepo alipokuwa Umar akikata roho akamwambia;
“Mwenyezi Mungu akurehemu ewe Abu Hafs (Umar
bin Khatwaab) kwani Wallahi ulikuwa Mlinzi wa dini ya
Kiislamu, makimbilio ya mayatima, mahali pa imani, mlinzi wa madhaifu.
Ukiwasaidia watu na kuisimamia haki, mfunguzi wa miji,
na kwa hivyo ukafanikiwa akawa anatajwa Mwenyezi Mungu kila wakati katika kila
pembe ya dunia”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuuliza;
"Utashuhudia hayo mbele ya
Mwenyezi Mungu?"
Ali bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu)
aliyekuwa karibu yake akamshika mkono Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Shuhudia, na
mimi nitakuwa shahidi wako."
Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia Umar;
"Nitashuhudia."
Maziko yake
Alipotambua kuwa wakati wa kuonana na Mola
wake umeshafika, alimtuma mwanawe Abdillahi (Radhiya Llaahu ‘anhu) ende kwa
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) na kumuomba akubali azikwe karibu na Sahibu
zake wawili ambao ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na
Abubakar Al Siddiq (Radhiya Llaahu ‘anhu) waliozikwa ndani ya chumba cha Mtume
wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kwa Bibi Aisha (Radhiya
Llaahu ‘anha).
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) akasema;
“Wallahi mahali hapa baina ya Mume wangu na Baba yangu nilijiwekea mwenyewe, lakini kwa vile Umar
ameniomba, basi sitomkatalia ombi lake. Mmwambie nimekubali”.
Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alifurahi sana kusikia hayo, lakini alimwambia
na kumsisitiza mwanawe kuwa;
“Kabla sijazikwa nenda kamtake tena ruhusa
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha), na iwapo atakubali ndiyo munizike hapo, kwa
sababu huenda ikawa amenikubalia hivi sasa bado ningali hai kwa kunionea haya
au kwa kuniheshimu nikiwa Khalifa wa Waislamu, lakini huenda akataka
kubadilisha nia yake baada ya kufa kwangu.”
Mwenyezi Mungu akurehemu ewe Umar. Hata unapokuwa
baina ya uhai na mauti, kipaji chako kina fanya kazi
yake sawa sawa. Nguvu zako zinafanya kazi sawa sawa, na
hekima yako inafanya kazi yake na UchaMungu wako unafanya kazi yake bali hata
kuwapenda kwako Sahibu zako kunafanya kazi yake.
Mwenyezi Mungu amswalie Mtume wetu Muhammad (Swalla
Llahu alayhi wa sallam) na awe radhi nao Sahaba zake
pamoja na Umma wote wa Kiislamu - Aamin.