Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu)

Aliy bin Abi Twaalib  (Radhiya Llaahu ‘anhu)
Khalifa wa nne aliyeongoka

Babu Yake


Abdul Muttalib bin Hashim alikuwa mkuu wa kabila la Kikureshi, mbora wao na kiongozi wao wanayemtii. Sifa zake zilienea katika eneo lote la jangwa la (Bara ya) Arabuni kuanzia Kaskazini mpaka Kusini yake. Wote walikuwa wakimheshimu na wakijua kuwa yeye ndiye aliyekichimba kisima cha maji ya Zamzam kwa mikono yake. Kisima kinachoendelea kutowa maji yenye baraka mpaka wakati wetu huu.
Majeshi ya Abraha Mhabeshi yalipotaka kuibomoa Al Kaaba, Abdul Muttalib alitambua kuwa hana uwezo wa kupambana nayo. Aliwataka watu wake wauhame mji na kupanda juu ya majabali. Akawakusanya kondoo zake na kuondoka nao huku akimuomba Mola wake Mtukufu ailinde nyumba Yake hiyo ya Al Kaaba.
Alipoulizwa kwa nini anakimbia pamoja na wanyama wake na kuiacha Al Kaaba bila ulinzi, Abdul Muttalib alijibu:
"Lilbayti rabbun yah-miyhi", maana yake; "Nyumba ina Mola wake mlezi mwenye kuilinda".
Alifurahi kupita kiasi alipoletewa bishara njema ya kuzaliwa kwa mjukuu wake Muhammad bin Abdillahi bin Abdul Muttalib (Swalla Llahu alayhi wa sallam). Akambeba kwa mikono yake miwili na kukimbia naye mpaka ndani ya msikiti wa Al Kaaba huku akimuomba Mwenyezi Mungu na kumshukuru akisema;
"Alhamdulillahi aliyenipa mtoto huyu mwema na mzuri".
Akampa jina la Muhammad, na kabla ya kufariki kwake alimuusia sana mwanawe Abu Talib juu ya mtoto huyo na kumtaka amlee vizuri, akamwambia;
"Mwanangu huyu atakuwa na shani kubwa, kwa hivyo umtunze vizuri, asije akafikiwa na dhara yoyote".
Abdullahi, baba yake Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alifariki dunia kabla ya kuzaliwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam). Kwa hivyo Abu Talib akachukuwa jukumu la kumlea mtoto huyo kama alivyousiwa na baba yake Abdul Muttalib, na hata pale Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipoanza kufunuliwa Wahyi na kuilingania dini ya Mola wake, Abu Talib alimsaidia sana, akamlinda yeye pamoja na ujumbe aliokuja nao juu ya kuwa yeye mwenyewe (Abu Talib) hakuingia katika dini hii tukufu.

Abu Talib alikuwa na heba na heshima kubwa mbele ya waarabu kama aliyokuwa nayo baba yake. Pia alirithi sifa na tabia njema za baba yake, akaweza kujulikana na kuheshimiwa na Waarabu wote kama alivyokuwa akiheshimiwa baba yake Abul Muttalib..
Alikuwa shujaa na mwenye uwezo wa kuongoza, na kwa vile alikuwa mkubwa wa kabila la Makureshi aliweza kumlinda Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) asidhuriwe na Makureshi.

Katika ukoo huu uliokuwa ukiwaongoza Makureshi na waarabu wote kwa hekima na heshima na utukufu mkubwa kupitia karne nyingi sana, alitokea Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) mwana wa Abu Talib bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdu Manaf, aliyerithi kutoka kwa baba yake Abu Talib kila sifa njema za ukarimu, ushujaa na ukweli.
Katika kitabu chake kiitwacho 'Abqariyat Imam Ali', na maana yake (Kipaji cha hekima cha Imam Ali), anasema Abbas al Aqqad;
"Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) anajulikana kuwa ni mtu wa mwanzo katika kabila la Bani Hashim aliyezaliwa kutokana na baba na mama wote wakiwa wanatoka katika ukoo wa Al Hashimiy. Baba yake Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), jina lake ni Abu Talib bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdi Manaf na mama yake pia jina lake ni Fatima bint Asad bin Hashim bin Abdi Manaf.
Inasemekana kuwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipewa na mamake jina la 'Haidarah', (na maana yake ni 'Simba'), sawa na jina la babu yake (babake mamake) ambaye jina lake lilikuwa 'Asad', na maana yake pia ni Simba, lakini baba yake akalibadilisha na kumpa jina la Ali."
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mdogo wa ndugu zake, na mkubwa wake alikuwa Jaafar kisha Aqiyl kisha Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu).  Inasemekana kuwa Aqiyl alikuwa kipenzi cha baba yake, na hii ndiyo sababu pale Abu Talib alipokuwa katika shida na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akifuatana na Hamza na Al Abbas walipomwendea Abu Talib kwa ajili ya kumsaidia ulezi wa watoto wake, akawaambia;
"Niachieni mimi Aqil na wachukuweni muwatakao".
Al Abbas akamchukua Talib, Hamza akamchukua Jaafar, na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamchukuwa Aliy (Radhiya Llahu anhum).

Wake zake


Vitabu vya historia vinasema kuwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) hajawahi kuoa mke mwengine wakati alipokuwa akiishi na bibi Fatima (Radhiya Llaahu ‘anha) binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), lakini baada kufariki, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alioa wake wafuatao:
1.   Umama bint Abul Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) binti yake bibi Zainab (Radhiya Llaahu ‘anha) mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na Abul Aas mume wa bibi Zainab alikuwa mtoto wa dada yake bibi Khadija binti Khuwaylid (Radhiya Llaahu ‘anha).
2.   Asmaa binti Umais (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa mke wa Jaafar bin Abu Talib na alipofariki Jaafar bibi Asmaa aliolewa na Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu), na alipofariki Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaolewa na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu).
3.   Fatima Ummul Baniyn.
4.   Ummu Said binti Urwa bin Masaud Al Thaqafiy
5.   Khaula binti Jaafar bin Qays
6.   Al Suhabaa binti Rabia
7.   Laila binti Masaud
8.   Muhyaat binti Mruul Qays

Inasemekana pia kuwa alioa wake wengine zaidi ya hawa.

Ewe Dunia Mtafute Mwengine!


Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipomtaka Dhirar bin Dhamira Al Kanaaniy azungumze juu ya sifa za Aliy bin Abu Talib (RAnhum), Dhirar akasema;
"Ali bin Abu Talib alikuwa Wallahi mtu mwenye kuona mbali, mwenye nguvu nyingi, anasema kwa utulivu na anahukumu kwa uadilifu, elimu inabubujika kutoka katika kila sehemu yake, na hekima inazungumza kutoka katika kila kitendo chake, hakuipa thamani yoyote dunia wala mapambo yake.
Alikuwa akistarehe nyakati za usiku (pale anaposali) ndani ya kiza chake. Aikuwa Wallahi mwingi wa mafunzo, mwingi wa kufikiri, akipenda kupindua pindua viganja vya mikono yake pale anapofikiri, akipenda kuvaa nguo zisizokuwa ndefu sana (hakuwa akipenda kuvaa maguo mengi na makubwa yanayoburura), na alikuwa akipenda chakula kisichokuwa laini (hakuwa akipenda vyakula vya fakhari), Alikuwa Wallahi akijiweka kama mmoja wetu, tukimwendea anatusogelea na tunapomwita anatujia, na juu ya kujikurubisha nasi kwake, hatukuwa tukimsemesha sana kwa sababu ya haiba aliyokuwa nayo.
Alikuwa akiwatukuza wachaMungu na akiwapenda maskini. Mbele yake, mwenye nguvu muovu hawi na tamaa ya kuitimiza batili yake, na aliye dhaifu hakati tamaa ya kupata haki yake - Nashuhudia mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa nilikuwa nikimuona wakati unapoingia usiku akiuendea msala wake huku akizishika ndevu zake na kulia kwa huzuni kubwa sana huku akisema;
"Ya Rabbana ya Rabbana" - huku akimnyenyekea Mola wake, kisha anasema kuiambia dunia;
"Hay-haata hay-haata (hayawi hayawi).  Ewe dunia mhadae mwingine, nimekwisha kukuacha talaka tatu wala sitokurejea tena. Umri wako mdogo, kukaa nawe ni hatari, na hatari zako zinakuja kwa wepesi, Aah! Aah! (nasikitika) kwa machache niliyojitayarishia, na safari ni ndefu na njia ni ya hatari."
Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa analia huku akijifuta machozi kwa kitambaa, na wote waliohudhuria hapo siku hiyo wakawa wanalia.

Sali Ubavuni Mwa Bin Ami Yako


Siku moja Abu Talib alimuona mwanawe Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akisali nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na hii ilikuwa katika siku za mwanzo za Uislamu, na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuogopa wala kubabaika, na baada ya kumaliza kusali akamwendea baba yake na kumwambia kwa ufasaha;
"Ewe baba yangu, nimemuamini Mwenyezi Mungu na kumfuata Mtume wake (Swalla Llahu alayhi wa sallam)".
Baba yake akamwambia;
"Yeye hakuiti isipokuwa ndani ya jambo la kheri. Kuwa pamoja naye".
Na siku ile Abu Talib alipomuona Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akisali nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kuliani kwake huku mwanawe Jaafar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akiwa amesimama kwa mbali kidogo akiwatazama, Abu Talib akamwita Jaafar (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Kamilisha ubawa wa Bin ammi yako, nenda kasali upande wake wa kushoto".

Wa Mwanzo Kusilimu Katika Watoto


Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa miaka minne wakati alipochukuliwa kulelewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na alikuwa kesha timia miaka kumi pale wahyi ulipoanza kuteremka. Na siku ile alipomuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akisali, alimuuliza;
"Unafanya nini?"
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia;
"Ninasali".
"Unamsalia nani?"
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
"Mola wa ulimwengu wote".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza;
"Nani huyu Mola wa ulimwengu wote?"
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
"Ni Mungu mmoja asiye na mshirika, aliyeumba, na mikononi mwake imo amri ya kila kitu, Naye ni Mweza wa kila kitu".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akazitamka shahada mbili na kuwa mtoto wa mwanzo kusilimu. Lakini juu ya udogo wa umri wake, alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakihudhuria darsi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) katika nyumba ya Al Arqam bin Abul Arqam pamoja na masahaba wenye umri mkubwa kupita yeye kama vile Abubakar na Uthmaan na Al Zubair na Twalha na Abdul Rahman bin Ouf na Saad bin Abi Waqqaas na wengine (RAnhum) tokea siku za mwanzo za Uislamu.

Niulizeni Kisha Niulizeni


Hakuwa akisema uwongo siku ile alipowaambia watu;
"Niulizeni, kisha niulizeni kisha niulizeni mtakacho juu ya kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwani Wallahi hapana hata aya moja katika aya zake ila ninaijua iwapo imeteremshwa usiku au mchana".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alilelewa katika nyumba ya Qurani, au tunaweza kusema kuwa alilelewa na yule aliyekabidhiwa Qurani, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam). Akawa anaipokea kutoka katika kinywa chake kitukufu ikiwa bado mbichi na mpya, Qurani ambayo daima ni mbichi na mpya, maneno  yake yasiyokonga wala kuchosha.
Alikuwa akiwatangulia wenzake katika kuisikia Qurani pamoja na siri zake, ikimtakasa huku ikibubujika kutoka katika kinywa cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) wakati akikumbana na taathira zake. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) awe mtiifu wa Qurani maisha yake yote.
Hakusema uwongo siku ile alipomuandikia Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Mtume Muhammad ni ndugu yangu na mkwe wangu
Na Hamza bwana wa mashahidi pia ni ami yangu
Jaafar ambaye usiku na mchana anaruka na Malaika ni mtoto wa mama yangu
Na binti wa Muhammad ni mke wangu na utulivu wangu
Tumechanganya pamoja naye damu yangu na nyama yangu
Wajukuu wawili wa Mtume kutoka kwake, nao pia ni wanangu
Yupi kati yenu mwenye sehemu kubwa kuliko yangu?
Nimetangulia katika Uislamu kabla kubalighi kwangu.

Uadilifu Wake (Radhiya Llaahu ‘anhu)


Siku moja aliipoteza ngao yake, naye wakati huo alikuwa Khalifa wa Waislamu. Alipokuwa akipita sokoni akaiona ikiwa mikononi mwa Myahudi aliyekuwa akitaka kuiuza.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimwendea Myahudi huyo na kumwambia;
"Ngao hii ni yangu imenianguka usiku wa siku fulani mahali fulani."
Myahudi akasema;
"Bali hii ni ngao yangu na imo mikononi mwangu ewe Amiri wa Waumini".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Hii ni ngano yangu na mimi sikuwahi kumuuzia mtu yeyote wala kumpa zawadi mtu yeyote hata ikaweza kukufikia wewe".
Myahudi akasema;
"Atakayehukumu baina yetu ni kadhi wa Kiislamu".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Sawa! twende kwa kadhi".
Wakaondoka pamoja na kuelekea kwa kadhi Shuraih, anayejulikana kwa uadilifu wake na kwamba ni mtu asiyemuogopa yeyote mbele ya haki.
Shureih akasema;
"Unasemaje ewe Amiri wa Waislamu?"
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Nimeiona ngao yangu hii kwa mtu huyu, na mimi ilinianguka usiku kadha na mahali kadha (akapataja mahala ilipomuanguka). Nashangaa vipi imekuwa yake wakati mimi sikupata kumuuzia mtu wala kuigawa".
Shureih akasema kumuuliza Myahudi;
"Unasemaje na wewe?"
Akajibu;
"Ngao ni yangu na imo mikononi mwangu na mimi simtuhumu Amiri wa Waumini kuwa anasema uongo".
Shureih akamgeukia Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Mimi sina shaka yoyote kuwa maneno yako ni kweli tupu ewe Amiri wa Waumini, na kwamba ngao hii ni yako kama ulivyosema, lakini huna budi kuleta mashahidi wawili watakaoshuhudia juu ya madai yako".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Ndiyo nitawaleta, nitamleta aliyekuwa mtumwa wangu niliyemuacha huru Qambar na mwanangu Al Hassan, nao watashuhudia juu ya ukweli wa madai yangu".
Kadhi Shureih akasema:
"Lakini ushahidi wa mwana kwa ajili ya babake haukubaliwi ewe Amiri wa Waisalmu".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Subhanallah! Mtu katika watu wa Peponi ushahidi wake haukubaliwi! Kwani hukumsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akisema;
"Al Hassan na Al Hussein ni mabwana wa vijana wa Peponi?".
Shureih akasema;
"Naam! nimemsikia ewe Amiri wa Waislamu, isipokuwa mimi siukubali ushahidi wa mwana kwa ajili ya babake".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamgeukia Myahudi yule na kumwambia;
"Ichukue! kwani sina mashahidi wengine isipokuwa hao'.
Myahudi akasema;
"Lakini mimi nashuhudia kuwa ngao hii ni yako ewe Amiri wa Waislamu".
Kisha akaongeza kusema;
"Ya Allah! Amiri wa Waislamu anahukumiwa na kadhi wake, na kadhi huyo anahukumu dhidi yake? Nashuhudia kwamba hapana Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah, na kwamba Muhammad ni Mtume wake. Nakujulisha ewe kadhi kuwa ngao hii ni ya Amiri wa Waumini na kwamba mimi nilikuwa nikimfuata alipokuwa akenda na jeshi lake mpaka alipofika mji wa Siffiyn na hapo ndipo ngao hiyo ilipomuanguka kutoka juu ya ngamia wake na mimi nikaiokota".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
"Kwa vile umesilimu, basi nakupa wewe ngao hii kama ni zawadi yako na pia nakupa zawadi farasi wangu huyu".

Anayependwa na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake


Kutoka kwa Abul Abbas Sahal bin Saad Al Saidiy (Radhiya Llaahu ‘anhu), amesema kwamba siku ya vita vya Khaibar, Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alisema;
"Kesho nitampa bendera mtu ambaye kwa mikono yake Mwenyezi Mungu atatupa ushindi. Mtu huyo anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake".
Anaendelea kusema Sahal (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Usiku kucha watu walikuwa wakiwaza kwa kutaka kujua ni nani huyo mwenye kupendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake atakayepewa bendera hiyo. Asubuhi yake watu wote wakaamkia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam). Kila mmoja akitamani apewe yeye bendera siku hiyo".
Imepokelewa kuwa; Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alisema;
"Hakuna siku niliyotamani kupewa bendera kuliko siku hiyo".
Baada ya watu kujikusanya mbele yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akauliza;
"Yuwapi Aliy bin Abu Talib?"
Akajibiwa;
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Aliy anaumwa macho".
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akasema;
"Niitieni"
Akaitwa, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamtemea mate machoni pake huku akimpangusa na kuomba dua. Hapo hapo Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akapona na kukabidhiwa yeye bendera hiyo.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza;
"Nipigane nao mpaka wawe kama sisi?"
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia;
"Nenda mpaka utakapofika katika mji wao. Kisha waite katika Uislamu na uwajulishe juu ya yale Mwenyezi Mungu anayotaka kutoka kwao…."
Imeelezwa kuwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipoufikia mlango wa Khaibar (mji wa Mayahudi), alipiga ukelele na kusema;
"Mimi Aliy Bin Abu Talib".
Anasema Khalid Muhammed Khaled katika kitabu cha 'Khulafaa Rrasuul';
"Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akielewa namna gani jina hilo linavyoingiza khofu ndani ya nyoyo za makafiri, kwani mara baada ya kulitaja jina lake, kwa ghafla alishambuliwa na kupigwa pigo la nguvu mpaka ngao yake ikamuanguka, na mbele yake akawaona walinzi wa mlango huo waliokuwa wakimshambulia wakijitayarisha kummaliza, na yeye akiwa amelala chini bila ya kuwa na hata ngao ya kujikinga.
Akasema moyoni mwake;
"Leo ama nitaonja yale yaliyomkuta Hamza au Mwenyezi Mungu atanipa ushindi".
Akainuka na kuwaendea walinzi hao na kuanza kuwasukuma huku na kule kwa nguvu zake zote. Ikisha akauendea mlango wa ngome hiyo ya Khaibar na kuung'oa kwa mikono yake".
Anaendelea kusema Dr. Khaled;
"Watu kabla hawakujua nini kinachotendeka walistukia Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akitoa takbir kwa sauti kali; "Allahu Akbar", na kumuona keshaubeba mlango huo kwa mikono yake miwili.
Anasema Abu Raafi-a (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye alikuwa katika kikosi cha Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Tulijaribu mimi na wenzangu saba kuubeba mlango huo tukashindwa".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) pamoja na majeshi yake wakawa wanashambulia huku wakiingia ndani ya mji wa Khaibar. Haukupita muda mrefu wakafanikiwa kuuteka mji huo.
Alipoletewa habari za kutekwa kwa mji huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akasema; "Allahu Akbar! ishaangamia Khaibar – Hakika sisi tunaposhuka uwanja wa watu itakuwa asubuhi mbaya kwa wale walioonywa (wasionyeke)".
Bukhari na Muslim

Askari Mwenye Adabu


Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa askari mwenye wingi wa adabu na heshima. Na kwanini asiwe hivyo wakati amelelewa katika nyumba ya mwalimu wa adabu Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliyefundishwa adabu na Mola wake Subhanahu wa Taala.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema;
"Amenifundisha Mola wangu na amenifundisha vizuri".
Katika vita vya Uhud, Abu Saad bin Abi Twalha aliyekuwa msitari wa mbele katika majeshi ya makafiri alipaza sauti yake juu akimwita Aliy bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu) kumtaka apambane naye. Aliy akauitikia mwito huo kwa kujisogeza mbele mpaka wakawa uso kwa uso na mapambano makali yakaanza baina yao.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alifanikiwa kumpiga Abu Saad pigo la nguvu na kumuangusha chini huku akilia kutokana na maumivu makali, lakini alipounyanyua upanga wake juu tayari kumuuwa, nguo ya Abu Saad ikafunuka na utupu wake ukawa unaonekana.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akafumba macho huku akigeuka na kurudi nyuma kuelekea msitari wa mbele wa jeshi la Waislamu akimwacha adui yake huyo amelala chini.
Alipoulizwa;
"Kwa nini hujamuua?"
Akajibu;
"Alinikabili kwa utupu wake nikamuonea huruma".
Si hivyo tu, bali hata baada ya majeshi ya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kushinda katika vita vya Al Jamal, na kabla ya vita vya Siffiyn kuanza, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipata habari kuwa watu wawili katika jeshi lake na majina yao ni Hajar bin Uday na Umar bin Al Hamaq walikuwa wakimtukana Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa dhahiri, jambo lililomkasirisha sana Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyewaita na kuwataka waache matusi yao.
Wakamuuliza;
"Ewe Amiri wa waumini, kwani sisi si tupo katika haki?"
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu;
"Ndiyo, naapa kwa Mungu wa Al Kaaba (kuwa sisi tupo katika haki)".
Wakamuuliza;
"Sasa kwa nini basi unatukataza tusiwatukane?"
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawaambia;
"Sipendi muwe watukanaji wanaopenda kulaani watu. Bora mseme;
"Mola wetu zuwia damu yetu na damu yao isimwagike na utupatanishe, na uwatowe kutoka katika makosa yao mpaka waijuwe haki na batil ili wasijiingize ndani yake (batili hiyo)".
Anasema Dr. Khalid Muhammad Khalid;
"Huyu ni mpiganaji mwenye heshima ya hali ya juu, na huu ni ushujaa wa hali ya juu usiopatikana isipokuwa kwa mwanamume wa kweli, na unaofaa kuigwa na wanaume wa kweli".

Abu Sufyan


Abu Sufyan alitumwa na makafiri wa Makka kwenda Madina kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kumuomba msamaha baada ya wao Makureshi kuvunja baadhi ya masharti ya mkataba wa Hudaibia. Alipowasili Madina hapana hata Muislamu mmoja aliyekubali kukaa au kuzungumza naye.
Alipoamua kwenda nyumbani kwa binti yake Umm Habiba Ramlah bint Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye ni mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), binti yake huyo alikataa kumuacha baba yake akae hata juu ya tandiko la mumewe, akalikunja na kumuacha baba yake akae chini.
Alipomuuliza binti yake:
"Kwa nini hutaki nilikalie tandiko hili?"
Akamwambia;
"Kwa sababu wewe ni mshirikina na kwa ajili hiyo hustahiki kulikalia tandiko la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam)".
Aliporudi Makka Abu Sufyan akawahadithia Makureshi yaliyomkuta Madina, akasema;
"Nikamwendea mwana wa Abi Quhafa (Abubakar Al Siddiq (Radhiya Llaahu ‘anhu)) lakini sikupata msaada wowote kutoka kwake. Kisha nikamwendea Ibni l Khattab (Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu)) nikamuona amegeuka kuwa adui mkubwa., akanambia;
"Unataka mimi nikakuombeeni msamaha kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu? Wallahi lau kama sitapata kitu cha kukupigeni isipokuwa punje ndogo ndogo basi nitapigana nanyi jihadi kwa punje hizo", kisha nikamwendea Ali, nikamuona ni mwenye huruma kupita wote".

Vita Vya Al Ahzab (Khandaq)


Makabila mbali mbali ya washirikina yaliungana na kuunda jeshi kubwa la watu wapatao elfu kumi kwa ajili ya kuwapiga vita Waislamu hapo Madina, na hii ilikuwa baada ya washirikina hao kuchochewa na Mayahudi wa mji huo.
Riwaya nyingine zinasema kuwa jeshi hilo lilikuwa la watu wapatao elfu ishirini na nne, na idadi hii ilikuwa kubwa kuliko idadi ya watu wote wanaoishi Madina wakijumuishwa na wanawake na watoto wa mji huo.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliitisha baraza la ushauri kuzungumzia mpango wa kuuhami mji wao kutokana na uadui huo, na baada ya mashauriano na rai mbali mbali, wakakubaliana juu ya rai ya Salman Al Farsiy (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyesema:
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, katika ardhi ya Wafursi tulikuwa pale tunapozungukwa tukichimba handaki lenye kuuzunguka mji wetu".
Anasema Al Mubarak Furriy katika kitabu cha 'Al Rahiyq al Makhtum;
"Haya yalikuwa maarifa mazuri ambayo Waarabu kabla ya hapo hawakuwa wakiyajua".
Wachache sana miongoni mwa makafiri akiwemo Amr bin Abd Wud Al Amry aliyekuwa mpiganaji mwenye nguvu nyingi anayejulikana kwa ujabari na ukhabithi wake waliweza kuvuka na kuwafikia Waislamu waliokuwa upande wa pili wa handanki hilo kwa kupitia njia ndogo iliyojibana.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipambana na Amr na akaweza kumuuwa, na Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipambana na Nofel bin Abdullahi al Mughiyra al Makhzumiy naye pia akafanikiwa kumuua.
Fathul Bari (Sharhi ya Sahih al Bukhari).

Imepokelwa katika Mustadrak ya Al Hakim hadithi iliyo sahihi kwa shuruti zilizowekwa na Maimam Bukhari na Muslim inayosema kuwa;
"Miongoni mwa walioweza kulivuka handaki hilo kupitia njia iliyojibana alikuwa Amr bin Abdu Wud Al Amry aliyewahi kupigana katika vita vya Badr akaumizwa mguu, na hakuwahi kupigana vita vya Uhud.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamtokea na kumwambia;
"Ewe Amr, niliwahi kukusikia pale penye Al Kaaba ukisema kuwa mtu akikuita katika mambo mawili utakubali moja wapo".
Akasema;
"Ndiyo"
Akamwambia;
"Basi mimi nakwita utoe shahada ya 'Laa ilaaha illa Llah wa anna Muhammadan rasuulu Llah' na nakwita katika Uislamu".
Amr akasema;
"Sina haja na yoyote katika mawili hayo".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia;
"Basi nakwita tupambane mimi na wewe".
Akasema;
"Mimi sitaki kukuua".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Lakini mimi nataka kukuua".
Wakapambana na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuua Amr."

Msitari wa Mbele


Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa msitari wa mbele katika kila anachowaamrisha au kuwanasihi Waislamu.
Alikuwa msitari wa mbele katika ucha Mungu, katika kupigana jihadi, katika mwenendo na tabia njema, katika kutoa, katika ustahamilivu, katika kuikinai dunia na katika kila nyanja ya maamrisho ya Kiislamu.
Siku moja alipokuwa katika mji wa Al Kufa na baada ya kuwasalisha Waislamu Sala ya Alfajiri, alikaa kimya muda kidogo huku uso wake ukionesha dalili ya huzuni nyingi.
Aliendela kukaa akiwa katika hali hiyo huku watu wakimuangalia na kuuheshimu ukimya wake huo mpaka jua lilipochomoza vizuri na miale yake kuenea katika kuta za msikiti, kisha akainuka na kusali raka-a mbili kisha akatikisa kichwa chake kwa masikitiko na kuvipindua pindua viganja vya mikono yake huku akisema;
"Wallahi nimewaona Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na wala simuoni kati yenu yeyote anayefanana nao. Walikuwa wakati wa asubuhi zinaonekana juu ya nyuso zao dalili ya kukesha kwao huku wakifanya ibada na kusoma Qurani na kurukuu na kusujudu. Na wanapokuwa wakimdhukuru Mwenyezi Mungu, utaviona vichwa vyao vimeinama kwa unyenyekevu mfano wa miti inavyoinama siku za upepo mkali huku macho yao yakibubujika machozi mpaka nguo zao kuroa".
Anasema Khalid Muhammed Khalid katika kitabu chake  'Khulafaa Rrasuul';
"Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) anatujulisha hapa juu ya hali ilivyokuwa katika zama tukufu kupita zote, siku za Wahyi na utume, siku ambazo nafsi ya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ingali inaishi ndani yake na akawa anaendelea kuishi ndani yake katika maisha yake yote. Hata wakati ukisonga mbele namna gani, hawezi kuusahau utukufu ule na mapenzi yake juu ya Masahaba wa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ambao pia ni Sahibu zake. Hawezi kuiondoa heshima yake juu yao, wala kuwasahau, na hawezi pia kuuondoa utukufu na mapenzi yake juu ya siku hizo ndani ya moyo wake, ndani ya dhati yake, kwa sababu huo ndio mwenendo wake na hayo ndiyo makimbizi yake".

Maneno ya Hekima


Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mwingi wa hekima, na zifuatazo ni baadhi ya kauli zilizonukuliwa kutoka kwake;
"Jifunzeni ilimu ili muwe watu wake. Jueni kuwa dunia tunaiacha nyuma na akhera tunaikabili, na kila moja kati ya nyumba mbili hizo ina watu wake. Basi kuweni watu wa akhera na wala msiwe watu wa dunia.
Wale waloikinai dunia, wameijaalia ardhi yake kuwa busati lao, udongo kuwa tandiko lao, na maji kuwa pambo lao.
Mwenye kuipenda akhera lazima ajiweke mbali na matamanio, na mwenye kuuogopa moto ajiweke mbali na yaliyoharamishwa.
Mwenye kuitaka Pepo akimbilie kumtii Mwenyezi Mungu, na aliyeikinai dunia hayapi umuhimu wowote masaibu yake.
Jueni kuwa Mwenyezi Mungu ana waja wake, amewahifadhi wasifanye shari, nyoyo zao za huzuni, nafsi zao zimekinai, matakwa yao machache, wamesubiri siku chache ili wapata raha za milele".

Anapomsikia mtu akiitukana dunia alikuwa akimwambia;
"Dunia ni nyumba ya ukweli, mahali panapoteremka Wahyi, msikiti wa Mitume, mahala pa kufanya biashara (na Mwenyezi Mungu) kwa wanaomjua (Mwenyezi Mungu). Kwa hivyo ndani ya dunia chumeni rehema za Mwenyezi Mungu ili muipate Pepo Yake".

Hakubadilika hata kidogo (Radhiya Llaahu ‘anhu) tokea utoto wake mpaka ukubwani. Na hata katika zama za hatari, zama za vita, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akiuweka mbele ucha Mungu wake. Hakuwa akiongoza watu kwa akili zake, na hekima yake ya hali ya juu peke yake, bali kwa ucha Mungu wake pia. Hakuwa akitaka chochote kutoka kwao isipokuwa wawe wacha Mungu, kwa sababu anayemuogopa Mola wake, ndiye askari wa kuaminika.
Na siku ile ya mapamabano baina yake na Muawiya (Radhiyallahu Anhuma), alipoambiwa na bin ammi yake Abdullahi bin Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu), ambaye naye pia ni mcha Mungu;
"Tumia hadaa, kwa sababu vita ni hadaa".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu;
"Abadan, sitoiuza dini yangu kwa dunia".
Anasema Khalid Muhammed Khalid;
"Mtu adhimu aliyekuwa akiufundisha ulimwengu uaminifu, utakatifu, na utiifu kwa Mola wake".

Hotuba yake ya mwanzo alipowasili mji wa Al Kufa


Katika hutoba yake ya Ijumaa ya mwanzo aliyowahutubia Waislamu mara baada ya kuwasili mji wa Al Kufa, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alianza hotuba yake kwa kuwausia Waislamu katika kumcha Mwenyezi Mungu, akasema;
"Nakuusieni waja wa Allah kumuogopa Allah, kwani Taqwa ni jambo bora la kunasihiana baina ya waja wa Allah, na ndiyo amali anayoridhika nayo Mwenyezi Mungu kutoka kwa waja wake.
Mumeamrishwa kumcha Mungu na kwa ajili ya wema mumeumbwa, kwa hivyo ogopeni yale Allah aliyokutahadharisheni nayo, kwa sababu amekutahadharisheni na adhabu kali kabisa.
Muogopeni Mwenyezi Mungu kuogopa kwa kweli na tendeni matendo yenu bila ya kujionesha kwa watu wala kutaka sifa au umaarufu, kwani mwenye kufanya amali yoyote ile kwa ajili ya kujipendekeza kwa mwengine asiyekuwa Allah, basi Mwenyezi Mungu humsukumiza nazo amali zake kwa huyo aliyemfanyia amali hiyo.
Ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu hajakuumbeni kwa upuuzi, na wala hakuacha chochote kiende ovyo. Keshataja athari zenu na keshajua siri zenu na kuzihesabu amali zenu na kuziandika ajali zenu. Kwa hivyo dunia isikubabaisheni kwani inawaghururisha watu wake, na ameghurika yule atakayebabaishwa nayo.
Na jueni ya kuwa Akhera ndiyo makazi ya milele".

Siku moja kabla majeshi yake na majeshi ya Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) kupambana katika vita vya Siffiyn, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwahutubia majeshi yake kwa maneno ya hamasa, bali aliwahutubia kwa kuwaambia maneno yanayohitalifiana kabisa na maneno yanayosemwa na majemadari katika hali kama hiyo.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alisema;
"Kesho mtapambana na kaumu, kwa hivyo usiku wenu ufanyeni uwe mrefu kwa kusali na zidisheni katika kusoma Qurani na muombeni Mwenyezi Mungu akupeni subira, maghufira na afya."
Katika wakati wa amani au katika wakati wa vita, anapokuwa ameshinda au anapokuwa katika shida yoyote ile, hapana kinachomshughulisha isipokuwa kumcha Mola wake Subhanahu wa Taala.

Isipokuwa vita vya Tabuk


Huo ndio msimamo wake, na namna hii ndivyo alivyokuwa akivikabili vita vyote alivyoshiriki.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alishiriki katika vita vyote vilivyopiganwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) isipokuwa vita vya Tabuk, wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipomuamrisha abaki Madina kwa ajili ya kuwalinda watu wa nyumba yake. Jambo hilo lilimhuzunisha sana Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), kwa sababu katika vita hivi hapana aliyebaki Madina isipokuwa wanawake, wazee, watoto wadogo, na wanafiki waliokuwa wakijulikana kwa unafiki wao, na walibaki pia Wale Watatu Waliongojeshwa ambao kisa chao kimetajwa katika Suratu al Tawba.aya ya 18 na kuendelea mbele.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam);
"Unaniweka mlinzi juu ya wanawake na watoto?"
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamjibu mbele ya Masahaba wake wote (RAnhum) kwa kumwambia;
"Haikuridhishi kuwa wewe kwangu mfano wa Harun alivyokuwa kwa Musa, isipokuwa hapana tena Mtume baada yangu?"

Khalifa na mfano mwema


Mwenyezi Mungu amejaalia Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) awe Khalifa katika wakati mgumu sana, wakati ambao hapana mwengine katika wakati wake angeliweza kuumudu, na Waislamu walikuwa na haja kubwa sana ya uongozi wa mcha Mungu mfano wake, muadilifu pamoja na hekima yake, kwa sababu wakati wa utawala wake yalizuka masaibu na matatizo mengi magumu sana pamoja na fitna nyingi baina ya Waislamu, lakini mwanafunzi huyu ambaye ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alisimama imara mbele ya kimbunga hicho kilichomkabili yeye, pamoja na umma wa Kiislamu.
Katika maamuzi yake alikuwa daima akikumbuka jinsi Ustadhi wake Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alivyokuwa akiyakabili kwa hekima kubwa mitihani mingi iliyokuwa ikimkuta, alikuwa akikumbuka maneno aliyowahi kumsikia akimuambia Ammi yake Abu Talib pale alipomshauri kuacha kuulingania Uislamu kutokana na mateso na maudhi aliyokuwa akiyapata kutoka kwa Makureshi, na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamjibu;
"Wallahi lau kama wataliweka jua katika mkono wangu wa kulia na mwezi mkono wangu wa kushoto, basi sitoicha amri hii mpaka Mwenyezi Mungu atakapoidhihirisha au nife kwa ajili yake".
Hakuisahau pia siku ile ya 'Fat'hi Makka', siku Waislamu walipouteka mji wa Makka, na hakuzisahau zile nyuso za makafiri wa Makka waliokuwa kabla ya hapo wakiwatesa na kuwauwa Waislamu, wakiwadhulumu na kuwadhulumu kila walichokimiliki. Na pia katika vita vya Uhud namna walivyomuuwa ami yake, Hamza (Radhiya Llaahu ‘anhu) bwana wa Mashahidi.
Siku hiyo Makureshi waligeuka wao kuwa mateka wa majeshi ya Kiislamu, wakakusanywa upande mmoja wakingojea hukumu kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) itakayoamua mustakbali wao; hukumu kwa walivyokuwa wakitaraji kuwa hawatosalimika.
Akakumbuka pia namna gani siku ile Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alivyosimama mbele ya mateka hao na kuwahutubia akiwauliza;
"Mnadhani nitakufanyeni nini?"
Wakajibu;
"Kheri, ewe ndugu mkarimu na mwana wa ndugu mkarimu".
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akawaambia;
"Nendeni, nyote mko huru".

Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuisahau pia siku ile ami yake Al Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipomwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na kumuomba ampe ugavana katika mojawapo ya wilaya za Kiislamu. Juu ya kuwa Al Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni ami yake Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) tena ni mtu muadilifu, mcha Mungu na shujaa, lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alimjibu kwa kumuambia;
"Sisi Wallahi ewe ammi yangu, hatumpi kazi hii mwenye kuiomba wala hatumpi mwenye kuichunga ".
Alikuwa akipenda kujikumbusha maneno na maamuzi ya hekima pamoja na uvumilivu na ushujaa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na kuyafanya kuwa dira yake na mfano wake bora wa kuufuata.

Mwanzo wa kuhukumu kwake


Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mwingi wa hekima na hodari wa kutoa hukumu. Mara nyingi Abu Bakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokuwa khalifa wa Waislamu alikuwa akimwendea kutaka msaada wake huku akimwambia;
"Tupe fatwa juu ya jambo hili ewe Abal Hassan (baba wa Hassan)".
Umar bin Khattab (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye pia mara nyingi alikuwa akimwendea Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kutaka ushauri wake, na aliwahi kumwambia;
"Lau kama si Ali, basi Umar angeangamia".
Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokuwa khalifa naye pia mara nyingi alikuwa akimwita Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumtaka ushauri wake katika matatizo mbali mbali,na hili si jambo la kushangaza kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliwahi kusema;
"Mbora wenu katika kutoa hukumu ni Ali."
Ibni Majah – Sehemu ya (1) mlango wa fadhila za Masahaba
Abu Yaala
Sayuty katika Jameal Saghiyr -mlango wa herufi ya hamza, na wengine

Jukumu lake la kuhukumu lilianza pale waasi waliokuwa wameizunguka nyumba ya Uthmaan bin Affan (Radhiya Llaahu ‘anhu) waliporudi mara ya pili baada ya kukubali ushauri wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) hapo mwanzo wa kuondoka kuelekea makwao.
Waasi hao walirudi baada ya kuikamata barua inayowataka magavana wa Misri na AlKufa kuwauwa waasi hao wote mara watakapowasili huko.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alijaribu tena kuwataka waasi hao waondoke na kurudi makwao, lakini mara hii walikataa. Juu ya kuwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikanusha, na sisi tunaamini kuwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema kweli alipokanusha, kwani huyu ni mtu ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema juu yake kuwa hata Malaika wanamsitahi.
Kwa hivyo ikajulikana kuwa waasi hao hawakurudi mara hii isipokuwa kwa sababu ile ile iliyowaleta hapo mwanzo nayo ni kumuuwa Khalifa wa Waislamu Uthmaan bin Affan (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Katika riwaya iliyopokelewa na Shaddad bin Aus (Radhiya Llaahu ‘anhu) anasema;
"Baada ya kutambua hayo, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoka nyumbani kwake akiwa amevaa kilemba cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na kuubeba upanga wake akielekea moja kwa moja nyumbani kwa Khalifa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), akiwa amefuatana na mwanawe Al Hassan na Abdullahi bin Umar bin Khattab pamoja na baadhi ya Masahaba watu wa Makka na wa Madina (RAnhum). Akaingia nyumbani kwa Khalifa na kumsalimia kisha akamwambia;
"Naona watu hawa hawataridhika isipokuwa kukuuwa, kwa hivyo tuamrishe tupigane nao".
Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Nakuombeni kwa jina la Mwenyezi Mungu ikiwa yupo kati yenu anayemshuhudia Mwenyezi Mungu kikweli na akaelewa kuwa mimi nina haki yoyote ile juu yake, basi arudishe upanga ndani ya ala yake na aondoke na isimwagike damu kwa ajili yangu".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akarudia tena na tena kumwambia maneno hayo, lakini Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaendelea kukataa., kwa hivyo Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoka na kuelekea msikitini, na Sala iliposimamishwa watu wakamtaka Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) awasalishe, wakamwambia;
"Ewe Abul Hasan, tangulia usalishe watu".
Akawajibu;
"Sitakusalisheni wakati nyumba ya Khalifa wa Waislamu imezungukwa, nitasali peke yangu".
Akasali peke yake. Kisha akatoka na kuelekea nyumbani kwake akiwaacha wanawe wawili pamoja na baadhi ya Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu) waulinde mlango wa nyumba ya Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu).

Waasi walielewa kuwa kila wakikawia kuutimiza uadui wao, mambo hayatakuwa mazuri upande wao. Yakatokea yaliyotokea, na Khalifa wa Waislamu Uthmaan bin Affan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliwa kwa njia ya kikhabithi, na mkewe Bibi Naila (Radhiya Llaahu ‘anha) alipokuwa akijaribu kumkinga akakatwa vidole vya mkono wake pamoja na sehemu ya kiganja, na hapo ndipo uti wa mgongo wa mwanzo wa Waislamu ulipovunjika.

Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) anaukataa Ukhalifa mara tatu


Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa ameketi msikitini pamoja na watu wapatao kumi zilipomfikia habari za kuuliwa kwa Khalifa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), akaondoka haraka kuelekea nyumba ya Khalifa na alipowasili akaanza kwa kuwapiga wanawe Al Hassan na Al Hussein huku akiwaambia;
"'Tabban lakum' (Mtaangamia), vipi anauliwa Khalifa wa Waumini na nyinyi mpo mlangoni pake?".

Mji wa Madina ulibaki bila ya khalifa muda wa siku tano, na katika siku zote hizo aliyekuwa akitamba mjini hapo na kutoa amri alikuwa Al Ghafiqiy bin Harb mtu aliyemuuwa Khalifa wa Waislamu Uthmaan bin Affan (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Wamisri waliokuwa wengi wa waasi hao walimuendea Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) mara mbili wakimtaka awe Khalifa wa Waislamu lakini Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikataa. Wakamwendea Twalha (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye pia akakataa, kisha wakatoka na kumwendea Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye pia akakataa, kisha wakamwendea Abdillahi bin Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), naye akakataa na mwisho wakamwendea Saad bin Abi Waqaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye pia alikataa, na walipomrudia tena Aliy bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu) akakataa tena .
Hapana aliyethubutu kubeba jukumu la ukhalifa wakati umma umekabiliwa na tatizo kubwa kama hilo, na nani atakayethubutu ikiwa Aliy mwenyewe (Radhiya Llaahu ‘anhu) ameukataa?
Wote walioukataa walikuwa wakihofia yale yatakayotokea baadaye, kwani atakayeshika uongozi itambidi awahukumu wauaji wa khalifa wa tatu wa Waislamu Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa kifo kwa ajili ya kitendo kiovu hicho.
Lakini wakati huo huo lazima ajitokeze mtu wa kuiongoza dola ya Kiislamu. Lazima achaguliwe Khalifa kwa sababu kila wakati unaposogea na nchi kuwa bila ya Khalifa, hatari inayotokana na wenye tamaa inaongezeka. Hatari inayoweza kuiparaganya dola ya Kiislamu, kuutawanya umma na kuupotezea mustakbali wake.
Anasema Dr.Khalid Mohammad Khalid;
"Watu waliitambua hatari hiyo, pamoja na hatari ya waasi ambao baada ya kumuuwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakawa wanaeneza chuki, bughudha pamoja na uongo mwingi juu ya Khalifa huyo mtukufu (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Wote waliitambua hatari ambayo mfano wake ilikuwa kama kimbunga kitakachouangamiza umma wote. Wakatambua kuwa lazima awepo kiongozi madhubuti atakayezishika hatamu na kuuongoza umma na kuwavusha nje ya bahari hii iliyochafuka.
Wakakusanyika watu wema katika watu wa Makka na wa Madina na kumwendea Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), na baada ya mazungumzo ya hekima kupita baina yao, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akakubali kufungamana ili awe Khalifa wao.
Hapakuwa katika Masahaba wa Mtume (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakati ule aliyestahiki kuwa Khalifa kupita Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), na hapakuwa na mtu aliye na kipaji, uwezo, hekima na ushujaa kupita yeye. Wakati huo ukhalifa wenyewe haukuwa kitu chenye manufaa yoyote ya kidunia, bali ulikuwa ni mzigo mkubwa kwa yule atakayeubeba na ulikuwa ni hatari kubwa kwa mwenye kumuogopa Mola wake".
(Mwisho wa maneno ya Dr. Khalid).

Wa mwanzo kufungamana naye


Wa mwanzo kufungamana naye, aliyeuingiza mkono wake ndani ya mkono wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) siku hiyo alikuwa ni Twalha bin Ubaidullah (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyefungamana naye kwa mkono wake wa kulia uliokatika katika vita vya Uhud pale alipokuwa akipigana kwa ajili ya kumkinga Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliyekuwa amezungukwa na maadui .
Anasema Ibn Kathir katika 'Al Bidaya wal Nihaya;
"Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoka moja kwa moja na kuelekea msikitini. Akapanda juu ya membari akiwa amevaa nguo zake pamoja na kilemba huku akiwa amekamata bakora yake. Akasimama akiwa ameiegemea bakora hiyo, na watu wote wakafungamana naye hapo. Hiyo ilikuwa ni siku ya Jumamosi tarehe kumi na tisa mwezi wa Dhul Hijjah.
Wa mwanzo kufungamana naye alikuwa Twalha (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa mkono wake uliokatwa siku ya vita vya Uhud, na yule aliyemuuwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipoona vile akasema (kwa kejeli); "Inna lillahai wa inna ilayhi raajiun". Na wa pili kufungamana naye alikuwa Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) kisha wakafuatilia Waislamu wote kufungamana naye mmoja baada ya mmoja".
Anaendelea kusema Ibni Kathir;
"Na katika hotuba yake ya mwanzo siku hiyo, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimshukuru Mwenyezi Mungu akampwekesha, kisha akasema;
"Hakika Mwenyezi Mungu ameteremsha kitabu kinachotujulisha nini kheri na nini shari. Kwa hivyo ifuateni kheri na epukaneni na shari. Mwenyezi Mungu ameharamisha mengi, akaitukuza heshima ya Muislamu na kuifadhilisha kupita kila kitu".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawataka Waislamu waheshimiane na wawe na ikhlasi katika amali zao na katika Tauhid pamoja na kuhurumiana na kupendana, na akawajulisha kuwa Mwislamu mwema ni yule ambaye Waislamu wenzake watasalimika na ulimi wake pamoja na mkono wake na kwamba si halali kwa Muislamu kumuudhi Muislamu mwenzake.
Akasema; "Kumbukeni kuwa watu wapo mbele yenu na akhera ipo nyuma yenu (inakuja). Mnapoiona kheri, ifuateni, na mnapiona shari, iepukeni, na kumbukeni pale mlipokuwa wachache madhaifu mlipokuwa mkionewa juu ya ardhi".
(Mwisho wa maneno ya Ibni Kathir).

Kuwalani wauaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu)


Atakayechunguza maisha ya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ataona kuwa yale matatizo na mapambano mbali mbali aliyokuwa akikabiliana nayo tokea utotoni mwake, pamoja na hekima na busara kubwa iliyojificha ndani ya dhati yake, ilikuwa muda wote huo ikimlea Khalifa huyu mtukufu kwa ajili ya kumtayarisha na mitihani mbali mbali atakayopambana nayo katika wakati huu mgumu kupita nyakati zote katika historia ya Waislamu.
Kuanzia siku ya mwanzo ya utawala wake baadhi ya Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu) walimwendea nyumbani kwake wakimtaka awakamate wauaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kuwahukumu, lakini Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwaambia;
"Wakati bado haujafika, kwani waasi hawa ni wengi sana na idadi yao inapindukia watu elfu kumi. Kwa hivyo itakuwa bora kama tutasubiri mpaka pale nitakapojimakinisha barabara."
Maneno hayo yaliwakasirisha masahaba hao (Radhiya Llaahu ‘anhu), wakatoka kwa ghadhabu huku wakimtuhumu Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa hataki kuwakamata waasi.
Miongoni mwa waliochukuwa msimamo mkali sana katika jambo hili walikuwa Twalha, Al Zubair na Muawiya bin Abu Sufyan (Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote).
Anasema Ibni Jariyr;
"Mara baada ya watu kufungamana na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), Naila, mke wa Uthmaan bin Affan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimwita Al Noaman bin Bashir (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumpa nguo ya Uthmaan iliyojaa damu aliyokuwa ameivaa siku aliyouliwa, pamoja na vidole vyake (Bibi Naila) kikiwemo kiganja chake kilichokatwa na waasi pale alipokuwa akimkinga mumewe, na kumtaka Al Noaman avipeleke nchi ya Sham kwa Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Muawiya alilia sana alipoviona vitu hivyo, akavichukuwa na kuvipeleka moja kwa moja mpaka ndani ya msikiti wa Damascus na kuvitundika juu ya membari ya msikiti ili kila mtu aweze kuviona na kuhamasika katika kudai kisasi cha kuuliwa Khalifa huyo wa tatu wa Waislamu .
Akapanda juu ya membari na kuwahutubia watu waliokuwa wakilizana kwa uchungu mkubwa sana na kwikwi kila anapovinyanyua vitu hivyo ili wavione, na akaendela na kazi hii ya kuhamasisha watu muda wa karibu mwaka mzima.

Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye aliwahi kumuomba Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ampe ugavana wa mji wa Al Kufa, na Twalha (Radhiya Llaahu ‘anhu) akataka apewe ugavana wa Basra ili waweze kukusanya watu wengi na kutayarisha jeshi kubwa la kupambana na wauaji wa Khalifa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), lakini Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawataka msamaha na kuwaambia;
"Mtanisamehe sana, lakini kwa wakati huu jambo hili haliwezekani kutendeka".
Masahaba hao hawakuridhika na msimamo huo. Wakaondoka kwa ghadhabu, jambo lililosababisha kuvunjika kwa mfupa wa pili wa mgongo wa Kiislamu.

Chanzo cha tukio la ngamia (Waqa'at al Jamal)


Kilichozidi kuharibu mambo na kuyafanya yawe magumu zaidi kwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), ni kule kujiunga kwa Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) pamoja na wale wanaodai kisasi cha kuuliwa kwa Khalifa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Wakati Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipouliwa, Bibi Aisha pamoja na wake wenzake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) walikuwa Makka kwa ajili ya kufanya Umra, na pia kwa ajili ya kuwa mbali na uasi ulioanza kudhihiri wakati ule dhidi ya Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) alipata msituko mkubwa aliposikia habari za mauaji hayo.
Al Zubair bin Al Awaam na Twalha (RAnhum) waliondoka Madina baada ya kuruhusiwa na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), ingawaje baadhi ya Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu) walimshauri Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) asiwaruhusu kuondoka wakihofia wasije kuungana na Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kusababisha upinzani mkubwa dhidi yake.
Masahaba wawili hao (Radhiya Llaahu ‘anhu) pamoja na maelfu ya watu waliokuwa nao waliungana na Bibi Aisha (Radhiyallahu anha), na wote kwa pamoja wakaondoka kuelekea mji wa Basra kwa ajili ya kujaribu kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye aliondoka Madina kuelekea Al Kufa akiwa na kundi kubwa la watu, na katika kila mji aloupitia watu wengi wa miji hiyo waliungana naye, isipokuwa alistushwa sana alipopata habari za kujiunga kwa Bibi Aisha (Radhiyallahu anha) na kundi la wanaotaka kisasi cha damu ya Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kilipwe kwa haraka.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa na uhakika kuwa Bibi Aisha, Al Zubair na Twalha (Radhiya Llaahu ‘anhum), wote hao wanaelewa vizuri kuwa yeye hawaungi mkono wauwaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na kwamba wakati utakapofika atawakamata na kuwahukumu, lakini kilichomhuzunisha ni ule uamuzi wao wa kutoka na makundi makubwa ya watu kwa ajili ya kuharakisha kukamatwa kwa wauaji hao. Habari zilizomfikia zilisema kuwa kundi hilo linaelekea Basra kwa nia ya kuwajumuisha watu wema wa mji huo, pamoja na wa nchi yote ya Iraq na kukusanya jeshi kubwa kwa ajili ya mapamabano.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa vile yeye ndiye kiongozi na mtu wa mwanzo kulibeba jukumu la kulipa kisasi hicho, bila shaka hatokubali dhulma kubwa kama hiyo ipite bila ya yule aliyedhulumu kutiwa adabu. Lakini kilichomhuzunisha ni kule kutoachwa yeye kama ni mkuu wa dola hiyo ya Kiislamu kutumia hekima zake na uwezo wake katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.

Baadhi ya Masahaba wakubwa kama vile Abdullahi bin Omar, Osama bin Zaid, Saad bin Abi Waqqaas, Muhammad bin Muslamah na wengineo (RAnhum) walikataa kujiunga na kundi lolote katika hayo mawili wakihofia visitokee vita vya wenyewe kwa wenyewe, na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokuwa akiondoka kuelekea Basra walikataa kuungana naye, wakamwambia;
"Mwenyezi Mungu ametuamrisha kupigana vita na washirikina, ama vita hivi vikitokea baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe, sisi hatupendezewi kuitia mikono yetu ndani yake."
Hata hivyo walimjulisha Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa wao wanatambua kuwa yeye yupo upande wa haki, lakini hawakutaka kunyanyua panga zao na kuzielekeza katika vifua vya Waislamu wenzao.
Hakika kuuliwa kwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kulisababisha fitna kubwa sana baina ya Waislamu.
Katika kambi ya pili, Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) aliwahutubia watu na kuwajulisha ubaya wa waasi hao waliomuuwa Khalifa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) tena ndani ya mwezi ulioharamishwa umwagaji wa damu ndani yake na katika mji ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliharamisha kupigana vita ndani yake, kisha wakakikata kiganja cha mkono wa Bibi Naila (Radhiya Llaahu ‘anha) mke wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kuvikata vidole vyake pamoja na kuiba mali yao.
Watu wengi wakaungana na Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha), huku wakimwambia;
"Popote utakapokwenda sisi tuko nyuma yako".
Kabla ya Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) kuondoka Makka, hitilafu ilitokea kati ya wake za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam). Wapo miongoni mwao waliotaka kwenda moja kwa moja mpaka Madina kumtaka Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) awakamate wauaji hao na kuwahukumu, na wengine wakataka wende Basra kukusanya jeshi kubwa kwa ajili ya kupambana na wauaji hao.
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) aliunga mkono rai ya kwenda Basra, na walipokuwa njiani, wao pia wakaungwa mkono na baadhi ya watu, na idadi yao ikafika kiasi cha watu wapatao elfu tatu. Wakaondoka huku Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) akiwa amebebwa ndani ya hema linalofungwa juu ya ngamia (Hawdaj).

Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye alipowasili mji wa Al Kufa alipata wafuasi wengi waliokuwa na hamasa kubwa ya kutaka kupigana vita kwa ajili ya kumnusuru Khalifa wao mpya ambaye ni mtoto wa ammi yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).
Alipoona hamasa zao zinaongezeka, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwatuliza kwa kuwaambia kuwa; haki haipatikani kwa mapambano peke yake, bali hupatikana kwa njia nyingi na kwamba kupigana vita kuwe ni jambo la mwisho la kulitegemea.
Akamwita Al Qaa qaa (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumtaka ende Basra kwa Mama wa Waislamu Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) na kuzungumza naye ili mambo haya yamalizike kwa amani.

Mazungumzo baina ya makundi mawili


Alipowasili mji wa Basra, Al Qaa qaa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikwenda moja kwa moja kuonana na Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta amani akamwambia:
"Ewe Mama wa Waislamu, kipi kilichokuleta mji huu?
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) akasema;
"Kupatanisha baina ya watu".
Al Qaa qaa (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Na wewe Twalha na Zubeir, kipi kilichokuleteni?"
Nao pia wakasema;
"Kupatanisha baina ya watu".
Al Qaa qaa (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Hebu niambieni, mtu vipi anaweza kusuluhisha baina ya watu?"
Twalha na Al Zubeir wakasema;
"Kwa kulipa kisasi cha kuuliwa kwa Uthmaan kwa kuwauwa waliomuuwa, kwa sababu tukiwaacha tutakuwa tumekwenda kinyume na mafundisho ya Qurani."
Al Qaa qaa (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Kwanini hamuukubali udhuru wa Aliy wa kuchelewesha kuwakamata wauaji hao, wakati mnaelewa kuwa waliomuuwa wanao wafuasi wengi sana, tena kwa maelfu, na kwamba kitendo cha kuwauwa wauaji hao hivi sasa kitasababisha umwagaji mkubwa wa damu. Nyinyi wenyewe huko mlikotoka mliwauwa (baadhi ya) wauwaji wa Ali, na mkajikuta mnapambana na watu wapatao elfu sita wenye silaha, hatimaye mkaamuwa kuwaacha. Isitoshe, Aliy hakuwasamehe wauaji hao, isipokuwa anasubiri mpaka pale fursa nzuri itakapopatikana, hapo atawakamata na kuwahukumu. Lakini wakati huu umma upo katika hali mbaya, watu wanakhitalifiana, na maelfu ya watu wamejikusanya ili waanzishe vita vikali baina yao. Msitupoteze!, umma utaangamia!"
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) akasema;
"Nini rai yako ewe Qaa qaa?"
Al Qaa qaa (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Mimi naona kuwa bora tuyatulize mambo hivi sasa, na nyinyi mfungamane na Ali, kwani kufungamana kwenu naye ni dalili ya kheri. Lakini mkikataa na mkaendelea kufanya upinzani, hii itakuwa ni dalili ya shari na kutoweka kwa ufalme, na mimi naogopa ikiwa mtashikilia kuifuata njia hii ya shari mtakuja dhurika nyinyi pamoja na sisi. Naogopa Mwenyezi Mungu asije akatuteremshia ghadhabu yake. Kwa hivyo kuweni funguo za kheri kama ilivyo kawaida yenu, na tusijiingize katika balaa mpaka ikatusibu. Bora tuyatulize mambo".
Mazungumzo yakaishia hapo na wakakubaliana kuwa Al Qaa qaa atakuja pamoja na Aliy (RAnhum) mpaka Basra ili wote wafungamane naye.

Al Qaa qaa akarudi kwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumpa habari hizi njema zilizoingiza furaha isiyo na kifani ndani ya kifua chake, kwa kuweza kuikinga damu ya Waislamu isimwagike.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akainuka na kuwahutubia watu na kuwakumbusha wakati wa ujahilia (kabla ya Uislamu) na upotovu wake na matendo yake, kisha akazungumza juu ya Uislamu na uongofu wake pamoja na kuongoka kwa watu wake kwa kuweza kuwafanya wawe kitu kimoja.
Akasema;
"Mwenyezi Mungu ametujumuisha baada ya kufa kwa Mtume wake (Swalla Llahu alayhi wa sallam) chini ya uongozi wa Khalifa Abubakar, kisha baada yake chini ya uongozi wa Khalifa Umar bin Khattab, kisha chini ya Khalifa Uthmaan, kisha yakatokea haya yaliyotokea ndani ya mwili wa umma.
Watu wanaikimbilia dunia na kuwaonea husda wale Mwenyezi Mungu aliowaneemesha na kuwapa fadhila alizowapa.Wakataka kuturudisha nyuma, lakini Mwenyezi Mungu lazima atalifanikisha lile alitakalo".
Kisha akasema;
"Mimi kesho naondoka na sitaki anifuate yeyote kati ya wale waliosaidia kuuwawa kwa Uthmaan".

Ilipoingia asubuhi, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaondoka pamoja na maaskari wake kuelekea Basra kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo ya amani. Wakawasili wakati wa usiku, na kila mtu alilala katika kambi yake kwa furaha wakiingoja siku ya pili yake kwa hamu kubwa.

Tukio la ngamia


Kambi zote mbili, (kambi ya upande wa Aliy na upande wa Twalha na Al Zubair wakiongozwa na Bibi Aisha (Radhiya Llahu anhum)) walilala wakiwa na furaha kubwa sana usiku huo. Lakini waovu wenye nia mbaya wakiongozwa na Abdillahi bin Sab-a myahudi, wao hawakuweza kupata usingizi, na usiku kucha walikuwa wakipanga hila za kuuvunja mkataba huo wa amani ambao ungekamilika wangepata  hasara kubwa sana.
Abdillahi bin Saba-a akasema kuwaambia wenzake walioshiriki katika mauaji ya Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Makubaliano gani haya? Wallahi Aliy anakijua vizuri zaidi kitabu cha Mwenyezi Mungu kupita hawa wanaodai kuuliwa kwa wauwaji wa Uthmaan. Keshasema mliyoyasikia, na kesho atakuja kuwajumuisha wote chini ya neno moja na wote watakuwa dhidi yenu. Mkae mkijua kuwa watu wote hawataki jengine isipokuwa wanakutakeni nyinyi. Mtakuwa katika hali gani wakati idadi yenu ni ndogo sana mbele yao?"
Al Ashtar akasema;
"Tulikuwa tukiijua rai ya Twalha na Al Zubair juu yetu tokea mwanzo. Kilichoaki ilikuwa ni kuijua rai ya Aliy juu yetu. Ama leo baada ya kuijua rai yake juu yetu, tumehakikisha kuwa mapatano yote haya ni kwa ajili ya kuimwaga damu yetu. Kwa vile mambo yenyewe yashakuwa hivyo, basi bora tumsukumize Aliy kule kule tulikomsukumiza Uthmaan".
Abdillahi bin Saba-a akasema;
"Maneno gani uyasemayo? Tukimuuwa Aliy nasi tutauliwa, kwani sisi idadi yetu hapa tulipo ni watu elfu mbili na mia tano tu, wakati watu wa Twalha na Al Zubair pamoja na wenzao, idadi yao ni watu elfu thelathini.  Hamna uwezo wa kupambana nao".
Mmoja wao aitwae Ghulab al Haytham akasema;
"Bora tuachane nao na tuondoke twende tukajikalie katika nchi yoyote ile na tujitowe katika balaa hili".
Abdillahi bin Saba-a myahudi akasema;
"Maneno gani haya usemayo na wewe. Wallahi tukifanya hivyo watu watatunyakuwa. Enyi watu! Tumaini letu la pekee ikiwa mnataka kuishi ni katika kuwagombanisha watu hawa wenyewe kwa wenyewe. Watakapokusanyika usiku wakati wa kulala, sisi tufanye kila hila ili tuanzishe vita baina yao na wala tusiwape fursa ya kupatana".
Kabla ya kuingia alfajiri ya siku ile iliyopangiwa kufanya sulhu, watu wapatao elfu moja kutoka katika kambi ya waasi waliomuuwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakiongozwa na Abdillahi bin Saba-a Myahudi wakazivamia kambi za jeshi la Basra iliyokuwa ikongozwa na Twalha na Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu), na wengine wakaivamia kambi ya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) na  kuwauwa watu wakiwa wamelala.
Watu wa kambi mbili hizo wakaamka na kukimbilia panga zao na kuingia vitani moja kwa moja baina yao wenyewe kwa wenyewe. Kila mmoja akidhania kuwa mwenzake amefanya khiana na kwamba yale mazungumzo ya kusuluhisha baina yao yalikuwa ni hadaa ya kuwaingilia na kuwauwa wakiwa wamelala.
Na hivi ndivyo majeshi mawili yalivyokutana katika uwanja wa vita katika mapambano yaliyokuja kujulikana kwa jina la Mapambano ya ngamia, au Tukio la ngamia.
Vita vikali sana vilipiganwa na maelfu ya watu walikufa siku hiyo.
Anasema Dr. Khalid;
"Kila kichwa kinapoanguka au kiungo cha mwili kinapokatwa, bali kila tone ya damu inapomwagika, moyo wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ulikuwa ukiungua na kuyeyuka. Ingawa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa shujaa na akipenda kupigana vita, hasa pale anapopambana na majeshi ya makafiri na ya washirikina huku akirudi nyuma na kusonga mbele ndani ya zahma, timko la vumbi na zogo la sauti za panga na mikuki huku vichwa vya makafiri na washirikina vikikatwa na kupeperuka huku na kule. Llakini leo hii anayeuwa na kuuliwa ni wana wa dini moja. Na yeye ndiye Khalifa wao kiongozi wao na mwenye jukumu juu yao pamoja na jukumu la damu yote inayomwagika na roho zao zinazotoka mahala hapo. Nani atakayemliwaza kwa haya yanayotokea? Na nani atakayemsaidia?"
Mwisho wa maneno ya Dr. Khalid
Mapambano baina ya jeshi la upande wa Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) lililokuwa na watu wasiopungua elfu thelathini, na jeshi la Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) lililokuwa na watu wasiopungua elfu ishirini, yaliendelea kwa nguvu sana, na kwa kasi kubwa sana, na maelfu ya watu waliuliwa na kujeruhiwa siku hiyo.
Sayiduna Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa anapiga kelele;
"Basi jamani! Basi jamani! Inatosha!"
Lakini hapana aliyekuwa akimsikia.
Kadhi wa Basra aitwaye Kaab bin Suwaar akasema kumwambia Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha);
"Ewe mama wa Waislamu wadiriki watu! Yaingilie mambo haya. Huenda Mwenyezi Mungu akajaalia ikapatikana sulhu baina yao kupitia kwako".
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) akainuka na kukaa juu ya hema lililofungwa juu ya ngamia wake, na watu wake wakalizungushia hema hilo ngao. Kisha akainuka na kutizama huku na kule ili ajaribu kutafuta njia ya kuvisimamisha vita.
Kwa mbali akamuona Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) akiwa keshamuangusha chini Ammar (Radhiya Llaahu ‘anhu), na Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) huku akiwa ameushika mkuki wake akimuelekezea Ammar (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Ammar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa anamuuliza;
"Ndiyo kweli utaniuwa ewe "Aba Yaqadhan' (umaarufu wa Al Zubair)?
Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu;
"La ewe Aba Abdullah (umaarufu wa Ammar), sitokuuwa".
Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mpiganaji bora na mwenye nguvu kuliko Ammar (Radhiya Llaahu ‘anhu), lakini alimuacha bila kumuuwa kwa sababu siku hiyo mtu yeyote asiyekuwa na silaha wala kinga aliachwa bila kuuliwa, na anayeondoka vitani bila kupigana, naye pia aliachwa aondoke.
Na sababu nyingine ya Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) kumuacha Ammar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni kwa sababu Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliwahi kusema kumwambia Ammar (Radhiya Llaahu ‘anhu);
"Utakuja kuuliwa na upande wenye makosa".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipoona watu wengi sana wanakufa akamshika mwanawe Al Hassan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamsogeza kifuani pake na akamkumbatia kwa nguvu sana huku akimwambia;
"Ewe mwanangu, laiti babako angekufa miaka ishirini iliyopita, kabla hakuiona siku hii ya leo".
Al Hassan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia babake;
"Ewe babangu, si nilikukataza mimi juu ya jambo hili".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu;
"Ewe mwanangu, sikutegemea mimi kama mambo yangefikia kiasi hiki".

Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipowaona Twalha na Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa mbali, akawaita kwa sauti kali sana, na walipomkaribia akawaambia;
"Nakuoneni mmejitayarisha kwa jeshi lenu kubwa sana na farasi wengi sana. Jee mmekwishautayarisha udhuru wenu pia siku ya kiama? Muogopeni Mola wenu"
Kisha Aliy akamgeukia Twalha na kumwambia;
"Ewe Twalha! umemuacha mkeo nyumbani kwako na umekuja na mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ili upigane pamoja naye?"
Kisha akamgeukia Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumwambia;
"Na wewe Al Zubair, unaikumbuka siku ile ulipopita wewe na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na mimi nilikuwa nimesimama katika mtaa wa Bani Saqifa, Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akacheka na wewe ukacheka pamoja naye, kisha Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akakuuliza;
"Unampenda Aliy ewe Al Zubair?"
Na wewe ukamjibu;
"Bila shaka mimi nampenda".
Kisha Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akakwambia;
"Itakuwaje siku hiyo utakapopigana naye vita ukiwa unamdhulumu ewe Zubair".
Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) akapiga ukelele huku akisema;
"Kweli, lo! ndiyo kwanza hivi sasa nimeyakumbuka maneno haya".
Akautupa upanga wake chini na kuondoka katika uwanja wa vita huku akilia. Alipokuwa akiondoka huku amemshika farasi wake, alikutana na mwanawe Abdillahi bin Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyemuuliza;
"Mbona unaondoka ewe babangu?"
Al Zubair akamwambia;
"Naondoka kwa sababu Aliy amenikumbusha maneno aliyowahi kuniambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kuwa siku moja nitakuja kupigana vita na Aliy huku nikiwa namdhulumu".
Mwanawe akamwambia;
"Lakini baba, wewe hukuja kwa nia ya kutaka kupigana vita, bali umekuja kwa nia ya kupatanisha".
Akasema;
"Nishaapa kuwa sitapigana naye vita".
Twalha na Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakaondoka katika uwanja wa vita baada ya kusikia waliyoyasikia kutoka kwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) na baada ya kujua kuwa Ammar (Radhiya Llaahu ‘anhu) anapigana upande wake.
Anasema Ibni Kathiyr;
"Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliuliwa na mtu mmoja aitwaye Amr bin Jarmouz aliyemnyemelea wakati wa usiku alipokuwa amelala katika bonde liitwalo Wadi al Sibaa na kumuuwa. Ama Twalha aliuliwa kwa mshale usiojulikana umerushwa na nani wakati alipokuwa akiondoka katika uwanja wa vita. Ingawaje zipo baadhi ya riwaya zinazosema kuwa mshale huo ulirushwa na Marwan bin Al Hakam (Wallahu aalam)".
Mwisho wa maneno ya Ibni Kathiyr.

Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) alipoona vita vinazidi kuwa vikali, na Al Zubair keshaondoka uwanjani na Twalha keshauliwa, akajikuta amebaki na jeshi bila ya viongozi, akainuka akiwa juu ya ngamia wake na kumwita Kaab bin Siwaar - kadhi wa mji wa Basra na kumtaka abebe msahafu na kuwaita watu wakusanyike chini yake.
Lakini wale waliomuuwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), akiwemo Abdillahi bin Saba-a, ambao wengi wao walikuwa msitari wa mbele katika jeshi la Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), walipomuona Kaab bin Siwaar ameunyanyua msahafu wakaogopa watu wasije kukusanyika chini yake na hatimaye ikapatikana sulhu kisha wote wawe dhidi yao. Wakaanza kumrushia mishale wote kwa pamoja mpaka wakamuuwa.
Na hili si jambo la ajabu kwani tokea mwanzo waasi hawa walikwisha kubaliana kuwa wasiwape watu fursa ya kupatana.
Baada ya kumuuwa Kaab, wakawa wanaendelea kuivurumisha mishale yao mahali alipo yule ngamia aliyembeba Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) kwa matumaini kuwa ngamia akianguka, wao watawahi kupavamia mahali hapo na kumteka Mama wa Waislamu na kwa njia hiyo vita vitamalizika kama wanavyotaka wao.
Lakini Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimtaka mwanawe Mohammad bin Al Hanafiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa amebeba bendera, asonge mbele kwa nguvu na kutangulia ili awahi kumfikia mama wa Waislamu kabla ya waovu hao kumfikia. Naye akaichukua bendera hiyo ya babake na kutangulia nayo mbele huku akitoa amri kwa watu wake kuwa mara watakapomuona ngamia huyo ameanguka wawahi wao kulifikia hema hilo na kumhami Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) kabla ya waasi kumfikia na kumsibu.
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) akawa ananyanyua sauti yake juu huku akiomba dua na kuwalani wauwaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na watu wake walikuwa wakiitikia – 'Aamin', huku wauwaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakiwa wanaendelea kumtupia mishale ngamia wake.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliposikia kelele akauliza;
"Nini hicho?"
Akaambiwa;
"Huyo ni Bibi Aisha anawalani wauaji wa Uthmaan na watu wake wanaitikia - Amin".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye akanyanyua sauti yake juu huku akisema;
"Allahuma walaani wauwaji wa Uthmaan ardhini na baharini".
Vita vikaendela kwa ukali sana, mara kundi hili linatangulia na mara nyengine linatangulia kundi la pili. Watu wengi wakauliwa, hasa pale penye ngamia, mpaka majeshi ya upande wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) yalipofanikiwa kumfikia ngamia huyo ndipo vita vilipomalizikia.

Baada ya kumalizika kwa vita vya Ngamia


Baada ya vita kumalizika, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaomba ruhusa ya kumuona Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha), akamwendea na kumsalimia, kisha akamwambia;
"Mwenyezi Mungu akughufirie".
Kisha akamtaka ndugu yake Bibi Aisha, Muhammed bin Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa upande wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) afuatane naye mpaka mjini Basra na kumweka katika nyumba maalum iliyotayarishwa kwa ajili yake.
Kisha Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawageukia watu na kuwahutubia akiwaambia;
"Atakayekimbia msimfuate, aliyejeruhiwa msimuuwe, mali zao msizifanye kuwa ngawira, atakayeweka silaha yake chini yu katika amani na atakayeufunga mlango wake kesha pata amani."
Huyu ndiye Jemadari muungwana wa hali ya juu na mwalimu anayewafunza watu khulqa njema zinazopasa kuwa baina ya Waislamu katika nyakati za vita na pia katika nyakati za amani.

Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwasili Basra siku ya Jumatatu tarehe kumi mwezi wa Rajab, mwaka wa Thelathini na sita. Siku hiyo hiyo watu wote wa mji huo wa Basra wakafungamana naye.
Siku ya pili Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akataka ruhusa ya kuonana tena na Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha), akaomba ruhusa ya kuingia na baada ya kuingia akamsalimia, kisha Bibi Aisha akasema;
"Hakika juu ya yote haya yaliyotokea, lakini hapakuwa na chochote na wala hapana chochote baina yangu na baina ya mwanangu huyu Ali, au sivyo?'
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajibu;
"Ndivyo ewe mama yetu".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamwambia bibi Aisha  (Radhiya Llaahu ‘anha) kuwa anaweza kuondoka na kurudi nyumbani kwake Madina wakati wowote apendapo, na akamtaka ndugu yake Mohammad bin Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa upande wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) afuatane naye mpaka Madina.

Kilichomridhisha Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni kuwa viongozi wote wa kambi ya pili walikiri kuwa yeye Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ndiye aliyekuwa upande wa haki.
Twalha, Al Zubair na hata Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha), wote walikubali kuwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ndiye aliyekuwa upande wa haki. Na hili ndilo jambo analolipenda Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), kwani yeye daima alikuwa akipenda awe upande wa haki. Na kauli hii aliitamka pia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) siku ile alipomuambia Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu):
"Utakuja kutokea mgogoro baina yako na baina ya Aisha ".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza;
“Mimi?”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia;
“Ndiyo wewe”.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
“Kwa hivyo mimi ndiye mwenye makosa.”
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia;
“Sivyo, lakini yatakapotokea hayo, basi umrudishe kwake kwa amani”.
Ahmed na Al Bazzar na Al Tabarani

Ama wewe uliyemuuwa mwana wa Safia, nakubashiria Moto


Baada ya vita kumalizika, Amr bin Jarmouz, yule aliyemuuwa Al Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokuwa amelala, alitaka ruhusa ya kuonana na Aliy bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu), na alipoingia akamkabidhi upanga wa Al Zubeir kwa kutafakhari akidhani kuwa Khalifa huyo wa Waislamu atampokea mapokezi ya heshima kama wanavyopokewa wapiganaji mahodari.
Lakini mara baada ya kuingia, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuuliza kwa sauti kali kabisa;
"Huu upanga ulioubeba ni upanga wa Al Zubair?"
Amr akajibu;
"Ndiwo, nimeuteka baada ya kumuuwa".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauchukuwa upanga kwa mkono wake wa kulia, kisha akaushika kwa mikono yake yote miwili, akaunyanyua kwa khushuu mpaka akufikisha mdomoni pake, akaubusu kwa huzuni nyingi sana huku machozi yakimtiririka, akasema;
"Upanga huu Wallahi mara ngapi mwenyewe ameutumia katika kumuondolea dhiki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam)."
Kisha akasema kumwambia Amr;
"Ama wewe, ewe uliyemuuwa mwana wa Safia (Al Zubeir), nakubashiria Moto".
Amr bin Jarmouz akatoka akiwa amekasirika huku akisema;
"Ama nyinyi ni watu wa ajabu kabisa. Namuuwa adui yenu, kisha mnanibashiria Moto?"
Huo ndio utukufu na uadilifu wa yule aliyelelewa katika nyumba ya Wahyi, haikubali dhulma hata kama imetendwa na mtu aliyesimama pamoja naye katika vita.

Vita vya Siffiyn


Vita vya Siffiyn vilivyopiganwa baina ya watu wa Iraqi wakiongozwa na Sayiduna Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), na upande mwingine watu wa Sham (Syria) chini ya uongozi wa Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) vilikuwa vita vikali sana.. Waislamu waliuwana wenyewe kwa wenyewe, na athari yake inaendelea mpaka hii leo.
Anasema Ibni Kathiyr katika Al Bidaya wal Nihaaya;
"Hadithi sahihi iliyopokelewa kutoka kwa Imam Ahmed bin Hanbal inasema kuwa; Ingawaje maelfu kwa maelfu ya Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu) walikuwa bado wahai wakati vita hivyo vilivyopiganwa, lakini wengi wao walikataa kushiriki isipokuwa wachache sana na idadi yao haizidi watu thelathini.
Hawakushriki katika vita hivi wale Masahaba waliopigana katika vita vya Badr isipokuwa wawili tu, nao ni Khuzayma bin Thabit na Sahal bin Hanif (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Hata hivyo wengi wa Masahaba juu ya kutoshiriki kwao lakini walikiri kuwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ndiye aliyekuwa upande wa haki. Wakamwendea na kumjulisha hayo, lakini walimtaka msamaha kuwa wao hawatoweza kushiriki katika vita hivyo vya baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe.
Ingawaje zipo baadhi ya riwaya zinazoelezea juu ya mamia ya Masahaba walioshiriki katika vita hivyo, lakini kutokana na tahakiki niliyoifanya nimegundua kuwa nyingi ya hadithi hizo si sahihi".
(Mwisho wa maneno ya Ibni Kathiyr).

Kanzu ya Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu)


Baada ya kuuliwa kwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na ile kanzu yake iliyojaa damu pamoja na kiganja na vidole vya mkewe Bibi Naila (Radhiya Llaahu ‘anha) vilivyokatwa na wauwaji hao kuchukuliwa kutoka Madina na kupelekwa Sham aliko Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuviingiza ndani ya msikiti mkuu wa Damascus na kuvitundika juu ya membari ya msikiti huo na kuwahutubia watu akiwaelezea juu ya ubaya wa kitendo hicho cha kumuua Khalifa wa Waislamu, huku akilia na watu wakilizana kwa kwikwi na kuwalani wauaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), watu wakawa wanamiminika kwa maelfu kila siku msikitini hapo huku wakilizana na kudai kisasi kilipwe kwa haraka sana.
Kwa njia hiyo Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliweza kukusanya watu wapatao elfu hamsini waliokuwa tayari wakati wowote kuingia vitani.
Tusisahau kuwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwa akiwaunga mkono wauaji hao na alikuwa akiwalani, isipokuwa yeye alikuwa na rai nyingine juu ya jambo hilo, na huko nyuma Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwatuma wanawe wawili pamoja na baadhi ya Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwenda kumlinda Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakati nyumba yake ilipozungukwa na waasi hao.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) pia hakuwa na nia ya kuwahami wauaji hao, bali yeye sawa na Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa na nia ya kuwakamata waasi hao na kuwahukumu kwa uovu wao huo, kwani kuachwa waasi hao huru bila ya kuhukumiwa ni kwenda kinyume na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume wake (Swalla Llahu alayhi wa sallam). Kutokuchukuliwa hatua sahihi kutapunguza heba ya dola ya kiislamu ikiongozwa na Khalifa huyo mpya. Lakini yeye aliiona kuwa wakati mzuri bado haujafika wa kuweza kupambana na waasi hao, na kwamba ni bora asubiri mpaka wakati huo utakapowadia.
Moja katika sababu kubwa ya kutochukuwa mapema hatua ya kuwakamata, ni ile idadi kubwa ya waasi hao iliyopindukia elfu sita, na wengi wao walikuwa wamejipenyeza ndani ya jeshi lake.
Hata wakati mmoja, pale ulipokuja ujumbe kutoka kwa Muawiya kwa ajili ya kukutana na Aliy kuzungumzia namna ya kulitatua tatizo hilo kwa amani na namna ya kuwakamata waasi hao, watu wapatao elfu sita na katika riwaya nyingine, idadi yao ilifika watu elfu kumi, walikusanyika nje ya nyumba ambayo ndani yake mkutano huo ulikuwa ukifanyika, huku wakipiga kelele wakisema;
"Sisi sote ni wauaji wa Uthmaan, kama mnaweza basi tuuweni sote !!!".
Isitoshe, Khalifa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuuliwa kwa njia ya kuviziwa, bali aliuliwa na watu waliouteka mji wa Madina na kuizunguka nyumba yake kwa muda unaokaribia miezi minne, na wauaji hao hata wakati huo walikuwa bado wakitamba na kubeba silaha zao.
Ali na Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu), kila mmoja kati yao aliliona tatizo hilo kwa jicho lake, na alikuwa na fikra zake katika kulitata tatizo hilo.

Wakati Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokuwa akitayarisha jeshi kubwa kwa ajili ya kupambana na wauaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), watu wengi walikuwa wakiwasili mji wa Al Kufa kwa ajili ya kufungamana na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Watu wa Makka na Madina, Misri, Basra na Al Kufa, watu wa Al Hijaz, Yemen, Oman na watu wa Bahrain na Yamama, wote hao walifungamana na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) isipokuwa Muawiya aliyekuwa Gavana wa Sham (Syria) ndiye aliyebaki nje ya mfungamano huo akidai kuwa lazima wauaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambao wengi wao wamo ndani ya jeshi la Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakamatwe kwanza na kuhukumiwa, kabla ya kukubali kufungamana naye.
Ikumbukwe kuwa wakati wa uhai wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakupata kudai haki ya kuwa Khalifa na wala hakutamka hata mara moja kuwa yeye ndiye anayeustahiki ukhalifa kuliko Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), bali tatizo lao lilikuwa ni namna ya 'Kulipa kisasi cha wauaji wa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu)'.

Barua ya Aliy kwa Muawiya


Ili kuepukana na vita vyengine, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimtuma mjumbe wake aitwaye Jariyr bin Abdullah (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumpa barua aipeleke kwa Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na kusudi la barua hiyo ni kumtaka Muawiya aingie katika kufungamana na Khalifa wa Waislamu kama walivyofanya magavana wenzake wote, na kuirudisha dola ya Kiislamu kuwa dola moja kubwa na pia kuuepusha umma na vita vyengine vya wenyewe kwa wenyewe.
Zipo hadithi nyingi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) zinazokataza mtu kujitoa nje ya mwili wa umma wa Kiislamu. Hii ni kwa sababu katika umoja umma unakuwa na nguvu, na kwa mfarakano unakuwa dhaifu unaomegeka kwa urahisi, na kugeuka kuwa tonge jepesi kwa adui.
Alipowasili Sham, Jariyr alikutana na Muawiya bin Abu Sufyan na kumkabidhi barua hiyo iliyoandikwa yafuatayo;
"Bisimillahi Rahmani Rahiym,
Amma baad, kwa vile watu wote wamefungamana nami katika mji wa Madina, basi nawe pia uliyeko huko Sham unalazimika kufungamana nami. Na hii ni kwa sababu watu waliofungamana nami ni wale wale waliofungamana na Abubakar na Umar na Uthmaan, kwa hivyo aliyehudhuria fungamanao hilo hana haki ya kulikataa na asiyehudhuria hana haki ya kulipinga. Kwani kwa hakika Ushauri ni wa Muhajirin na Ansar (Watu wa Makka na wa Madina), wakikubaliana wote juu ya mtu na kumchagua kuwa ni Imamu wao. Na Mwenyezi Mungu anaridhika na uchaguzi huo.
Na yeyote atakayejitenga kwa ajili ya maslahi yake ya kibinafsi, basi watu watamrudisha kule alikotoka na kumweka juu ya njia iliyo sawa. Na kama akikataa, basi watu watampiga vita kwa sababu ya kufuata kwake njia nyengine isiyokuwa ya wenzake.
Twalha na Zubair, hapo mwanzo wote walifungamana nami, kisha wakajitoa, na kwa ajili hiyo ikanibidi nipambane nao mpaka haki iliporudi na amri ya Mwenyezi Mungu ikadhihiri. Kwa hivyo nawe ingia na uwe pamoja na Waislamu, kwani mimi nakupendelea zaidi usalimike, ila kama wewe mwenyewe unataka upambane na mitihani. Na ikiwa hivyo ndivyo utakavyo, basi itanibidi nipambane nawe na kumuomba Mwenyezi Mungu anipe ushindi juu yako.
Umepindukia mipaka katika kuwataka wauaji wa Uthmaan wakamatwe. Kwa hivyo ingia katika yale waliyoingia Waislamu wenzako ndani yake, kisha nitakupa wewe jukumu la kuwahukumu wauaji hao kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Ama hayo unayoyataka wewe ni mfano wa kumhadaa mtoto mdogo ili akubali kunywa maziwa. Wallahi kama utachunguza kwa akili yako utaona kuwa mimi niko mbali kabisa na damu ya Uthmaan.
Jua kuwa wewe ni katika Tulaqaa, (Tulaqaa ni wale walioinga katika Uislamu baada ya kutekwa mji wa Makka na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akawaacha huru, kisha wao wenyewe wakaingia katika Uislamu), na kwa ajili hiyo huna haki ya kudai ukhalifa, na wala huna haki ya kutakiwa ushauri wowote.
Nimemtuma kwako Jariyr, naye ni katika watu wa Imani na watu waliohajir, kwa hivyo fungamana nami - Walaa quwwata illa billaah!!".

Hii ndiyo barua aliyoituma Aliy kwa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) akimtaka afungamane naye na wakati huo huo akimpa Muawiya fursa ya kuwa Mwanasheria mkuu na kuisimamia kesi hiyo ya waasi waliomuuwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) ikiwa anataka.
Baada ya kuisoma barua hiyo, Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimwita Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) pamoja na viongozi wa watu wa Sham na kuwataka ushauri juu ya jambo hilo, na wote wakakataa na kusema;
"Sisi hatufungamani na Aliy mpaka kwanza awauwe wauaji wa Uthmaan au awakamate au atupe sisi tuwauwe wauaji hao. Ama sivyo, sisi tuko tayari kupambana naye mpaka tutakapowauwa wauaji hao".

Mapambano


Baada ya majibu hayo makali, Muawiya bin Abu Sufiyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) akatoka na jeshi lake kubwa na kuelekea nalo mahali panapoitwa Siffiyn katika nchi ya Syria, akipitia kando kando ya mto wa Euphrates, kwa sababu alielewa kuwa hapakuwa na njia nyingine ambayo Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) angeweza kuitumia ili kumfikia isipokuwa hiyo. Na hapo ndipo mahali mapambano makali yalipotokea baina yao.
Kwa upande mwingine Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye akatoka na jeshi lake kubwa kutoka mji wa Al Kufa - Iraq, na kuelekea nalo nchi ya Sham - Syria,  lakini yeye alirudi nyuma na kulitaka jeshi lake litangulie, na akawa anawaambia watu wake;
"Msianzishe vita mpaka waanze wao, na msiwakaribie sana ili kujiepusha na mapambano. Wakati huo huo msiwe mbali nao sana hata wakadhani kuwa mnawaogopa, na hata kama vita vitapiganwa basi kila mara muwaite katika kufungamana".
Jeshi la Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) liliwahi kupafikia mahali penye chemchem ya maji na kupazunguka, na Majeshi ya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) yalipowasili na Aliy mwenyewe akiwa bado hajafika, yakajaribu kuyasogelea maji hayo lakini watu wa Muawiya hawakuwaruhusu kuyakaribia.
Watu wa upande wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakasema;
"Vipi nyinyi, mnatunyima maji na sisi Waislamu wenzenu?"
Wakajibu;
"Tunakunyimeni ili mupate na nyinyi kuonja utamu wake kama mlivyomnyima Uthmaan maji na kuizunguka nyumba yake kwa muda wa siku arubaini".

Baada ya majadiliano marefu na mapambano makali kidogo baina yao, wakakubaliana kuwa majeshi yote yaondoke mahali hapo na yapige kambi mbali na maji hayo na kwamba kila upande uruhusiwe kuyachota".
Ali bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwasili mahali hapo asubuhi ya siku ya tatu baada ya tukio hilo, na mara baada ya kuwasili alisimama katika msitari wa mbele wa jeshi lake, na Muawiya bin Abu Sufyan (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipomuona, naye pia akasogea na kusimama mbele ya jeshi lake.
Kwa muda mrefu walikabiliana, kisha wakakumbushana kuwa huo ulikuwa ni mwezi wa Dhul Hijjah, mwezi ambao umeharamishwa kupiganwa vita ndani yake, na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akarudisha jeshi lake na kungoja mwezi mzima.
Baada ya mwezi kumalizika, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimtuma tena Bashir (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) ili azungumze naye na kujaribu kumfanya akubali sulhu na afungamane naye, na alipokabiliana naye, Bashir akasema kumwambia Muawiya;
"Ewe Muawiya, dunia inakwenda zake hii, na akhera inakuja, na Mwenyezi Mungu atakuhesabia amali zako, atakulipa jaza njema kwa yale mema utakayojitangulizia kwa mikono yako. Mimi nakuomba usimamishe umwagaji wa damu katika umma huu".
Muawiya akasema;
"Na huyo sahibu yenu umempa usia huu pia?"
Bashir akajibu;
"Sahibu yangu ni kiumbe aliye na haki kupita wote katika jambo hili. Na hii inatokana na fadhila zake, uchamungu wake, na pia kutokana na kutangulia kwake kuingia katika dini hii, na kutokana na kuhusiana kwake na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na yeye anakuita katika kufungamana naye ili upate usalama katika dini yako".
Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Na damu ya Uthmaan iwe imemwagika bure? La wallahi sikubali kamwe".
Mmoja kati ya watu wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akajaribu kumtolea ujeuri Muawiya, na Muawiya akawafukuza wote na kuwataka waondoke na kurudi walikotoka.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipoona kuwa milango yote ya amani imekwishafungika na kwamba kwa wakati huu hapana tamaa ya kupatikana masikilizano. Akaanza kuyapanga majeshi yake na kuwagawa watu wake makundi mbali mbali na kumweka kiongozi katika kila kundi.
Vita vikaanza kama kawaida kwa mapambano ya mtu mmoja mmoja na mara nyingine vita vikali vilipiganwa baina yao kisha vikasita na mara nyingine vilipiganwa vita mara mbili kwa siku kisha vikanyamaza.

Watu wa Sham wanyanyua misahafu


Kabla ya vita hivyo vikali kuanza, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kama kawaida yake alitoa amri ifuatayo kwa watu wake;
"Mnapopigana nao mkawashinda msije mkamuuwa yeyote anayerudi nyuma wala aliyejeruhiwa. Msimkashifu aliyekufa wala msiwakatekate maiti, na mtakapoingia mjini msije mkaingia nyumba ya mtu bila ya idhini ya mwenye nyumba wala msichukuwe chochote katika mali yake".
Majeshi hayo yakakutana mahali hapo panapoitwa Siffiyn, na kuingia katika mapambano makali na marefu sana, na damu nyingi sana ilimwagika hata ardhi yake ikawa haionekani kwa wingi wa maiti na majeruhi.
Anasema Ibni Kathiyr katika Al Bidaya wal Nihaya;
"Ingawaje wanahistoria wamehitalifiana juu ya siku ngapi vita hivyo vilipiganwa, lakini katika tahakiki yangu, nimeona kuwa siku zote za Siffiyn ni sabini na saba, Wallahu aalam".
(Ibni Kathiyr hapa anazungumza juu ya siku zote za Siffiyn – yaani tokea majeshi yalipoanza kujikusanya kabla ya mapambano kuanza hadi kumalizika kwa mapambano na hatimaye kuanza mazungumzo ya kupatanisha mpaka kumalizika kwa mazungumzo na majeshi kuanza kutawanyika na kurudi makwao.)
Zipo riwaya zinazosema kuwa vita hivyo vilipiganwa muda wa siku tatu – mchana na usiku.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akitazama na kuona namna gani watu walivyokuwa wakianguka baina ya wanaokufa na majeruhi, na mara kasi ya vita ikiongezeka na mara nyingine kupungua, mpaka alipoamua kumuanidikia tena barua Muawiya aliyoandika ndani yake maneno yafuatayo;
"Ewe Muawiya, kwa nini unasababisha kuuliwa kwa watu wote hawa kwa ajili yangu mimi na wewe? Toka tupambane sisi wawili tu! na atakayeshinda ndiye atakayetawala".
Lakini Muawiya baada ya kushauriana na sahibu yake Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikataa.

Vita vilipokuwa vinapamba moto na watu wa Sham (upande wa jeshi la Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu)) walipoona namna maelfu ya watu wanavyopukutika baina ya wanaokufa na wanaojeruhiwa wakakubaliana kuinyanyua misahafu na kuitundika juu ya panga zao ikiwa ni ishara kuwa vita visimamishwe na wahukumiane kwa Qurani.
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipoona hivyo akasema kuwaambia watu wake;
"Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, endeleeni kupigana mpaka haki ipatikane, na wala msihadaike, maana mimi nawajua vizuri Muawiya na Amr bin al Aaas. Wao hawakufanya hivi isipokuwa baada ya kuhisi kuwa majeshi yao yanakaribia kushindwa. Hii ni mojawapo ya hadaa zao na mbinu zao za kivita tu. Kwani mimi napigana nao kwa ajili gani nyingine gheri ya kuwa wao wamekwenda kinyume na kitabu cha Mwenyezi Mungu?".
Lakini baadhi ya watu wake hawakuwa tayari kumtii, wakamwambia;
"Ewe Ali, unapoitwa katika kitabu cha Mwenyezi Mungu itikia, ama sivyo tutakufanyia yale yale tuliyomfanyia Uthmaan bin Affan, kwa sababu yeye pia alikataa kuitikia alipotakiwa ahukumu kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na sisi tukamuuwa".

Kisa cha kuhukumu


Vita vikasimamishwa na makubaliano yakafikiwa kuwa wachaguliwe watu watakaohukumu baina yao, na kwamba kila upande umchague mtu mmoja atakayeuwakilisha upande wake, na pande zote mbili utalazimika kuukubali uamuzi utakaofikiwa, na kwamba mazungumzo hayo yahudhuriwe na wakubwa wa Masahaba waliokuwepo wakati huo.
Upande wa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakamchagua Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) na upande wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) walimchagua Abu Musa Al Ash ary (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliyejitoa katika vita hivyo tokea mwanzo baada ya kuwakataza sana watu wasiingie katika mapambano hayo ya wenyewe kwa wenyewe ambayo mwisho wake utaleta mtengano baina ya Waislamu. Kwa vile hawakutaka kumsikiliza, akajiuzulu hata ugavana waliompa na kuuhama mji.
Ali bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuridhika kuchaguliwa kwa Abu Musa (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwani yeye alipendekeza Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) auwakilishe upande wake, na hii si kwa sababu Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwa akimuamini, bali alikuwa akielewa vizuri kuwa Abu Musa (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni mtu mwema na mchaMungu sana, na alikuwa akijua kuwa alikuwa akimpenda sana Ali, isipokuwa kwa vile upande wa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) unawakilishwa na Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) anayejulikana sana kwa umahiri wake katika kujadiliana, na uhodari wake wa kupanga maneno na wepesi wake wa kufikiri na kutoa uamuzi unaosibu. Kwa hivyo Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye akataka upande wake pia uwakilishwe na mtu wa kadiri yake. Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akijulikana kuwa ni kufu yake Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Lakini Al Ash'ath bin Qais aliyekuwa upande wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipinga sana jambo hilo na kushikilia kuwa lazima upande wao uwakilishwe na Abu Musa (Radhiya Llaahu ‘anhu), ama sivyo watajitenga naye, na Sayiduna Aliy  (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa ajili ya kuogopa mfarakano akakubali ushauri huo.

Kisa kisichokuwa sahihi


Kuna kisa maarufu ambacho kimezushwa na wasimulizi waongo wa historia. Uongo huo ni kuhusu mazungumzo yaliyokuwa baina ya Amr bin Al Aas na Abu Musa Al Ash ary (R.Anhuma).
Kwa sababu mbali mbali kisa hiki kimeweza kupenya na kuandikwa katika vitabu maarufu vya wanavyuoni wanaojulikana kwa uchaMungu wao kama vile Ibni Kathiyr na wengineo, lakini wamefanya hivyo bila kukifanyia tahakiki.
Kisa chenyewe kinasema hivi;
"Baada ya Masahaba wawili hao kukubaliana kuwaondoa wote wawili Aliy na Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) katika ukhalifa, Amr alifanya khiana aliposimama na kumthibitisha mtu wake ambaye ni Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu)."
Kisa kinaendelea kusema kuwa:
"Baada ya majadilianao marefu, Amr bin Al Aas na Abu Musa al Ash'ary walikubaliana wawaondoe Aliy na Muawiya katika uongozi kisha Waislamu washauriwe na wamchaguwe kiongozi mwingine. Baada ya kukubaliana, watu wakakusanywa wapate kujulishwa juu ya makubaliano hayo, na Amr akamtaka Abu Musa (Radhiya Llaahu ‘anhu) aanze yeye kusema na Abu Musa (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaanza kwa kusema;
"Mimi namvua Aliy Ukhalifa kama ninavyoivua pete yangu hii". Kisha akaivua pete yake, na baada ya hapo Amr bin al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akainuka na kusema;
"Na mimi pia namvua Aliy ukhalifa kama alivyomvua Abu Musa na kama ninavyoivua pete yangu hii, lakini mimi namthibitisha Muawiya kuwa ni Amiri wa Waislamu kama ninavyoithibitisha pete yangu hii".
Kwa vile Amr alikwenda kinyume na makubaliano - kisa hicho cha uongo kinasema kuwa Abu Musa akaondoka hapo akiwa ameghadhibika na kurudi Makka badala ya kwenda Al Kufa kwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), na Amr akarudi Sham."
Tarekh ya Al Tabari 4/51, Al Bidaya wal Nihaya Juz.7 mlango 'Ulipoingia mwaka wa 37 na Al Kamil fil Tarikh3/168

Ukweli


Kwanza kabisa lazima ieleweke kuwa sehemu kubwa ya historia ya Kiislamu imeandikwa mara baada ya kuanguka kwa dola ya Bani Umayya. Na kwa vile wakati huo yalikuwepo makundi mbali mbali yanayowaunga mkono na mengine yanayowachukia, pamoja na kundi lengine lililojihusisha na kuandika Historia bila ya kuchukua jukumu ya kuifanyia tahakiki.
Kwa hivyo, vitabu vya historia ya kiislamu vikajaa mchanganyiko wa hadithi sahihi na zisizokuwa sahihi, ikawa vigumu sana kuweza kuupata ukweli mtupu juu ya yale yaliyotokea wakati wa misukosuko hiyo iliyoukumba umma huu.
Hata hivyo baadhi ya maulamaa wameweza kufanya jitihada kubwa sana na kufanikiwa kiasi kikubwa katika kuzichambua hadithi hizo na kuzibainisha zile za kweli na kuziweka mbali na hadithi zisizo za kweli.
Katika kuzifanyia tahakiki riwaya zinazohusiana na kisa hiki 'Kisa cha kuhukumu', maulamaa wa elimu ya hadithi wamegundua kuwa asili yake kinatokana na mtu anayejulikana kwa jina la Abu Makhnaf na jina lake hasa ni Luut bin Yahya ambaye riwaya zake za uongo mia tano na themanini na saba zimenukuliwa na Al Tabari katika kitabu chake cha Tarikh, na riwaya hizi zinazungumzia juu ya ule wakati mgumu sana kwa Waislamu, kuanzia siku ile alipofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na kumalizikia wakati wa ukhalifa wa Yazid bin Muawiya, na huu ndio wakati mgogoro wa Saqifat Bani Saaida ulipoanza, kisha mgogoro wa Shuura, kisha sababu zilizowafanya Khawarij wasimame msimamo wao dhidi ya Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na hatimaye kuuliwa kwake. Hadithi hizo zinazungumzia pia juu ya ukhalifa wa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), vita vya ‘Al Jamal’, vita vya ‘Siffin’, kisa hiki cha kuhukumu, (Tahkiym), vita vya Naharawan, ukhalifa wa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu), na kuuliwa kwa Al Hussein (Radhiya Llaahu ‘anhu). Kote huko utazikuta riwaya zilizosimuliwa na Abi Makhnaf huyu, na wazushi wanazishikilia sana riwaya hizi na wanazitegemea sana katika kuineza batili yao.

Bila shaka khiyana kama hii haiwezi kutendwa na mtu kama Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye ni sahibu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na vitendo kama hivi havitendeki isipokuwa katika vikao vya watu waongo na wenye kupenda kuhadaa watu.
Pili, inajulikana kuwa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwa akipigania ukhalifa wala hakupata kuudai ukhalifa, na wakati huo yeye hakuwa khalifa wa Waislamu hata aondoshwe au kuthibitishwa kama inavyothibitishwa pete kidoleni, kama ilivyoelezwa katika riwaya hiyo. Bali tokea mwanzo matakwa yake yalikuwa wazi kabisa, nayo ni kulipa kisasi cha kuuwawa kwa Khalifa wa Waislamu Uthmaan bin Affan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na kwamba hatofungamana na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) mpaka pale atakapochukua hatua ya kuwakamata waasi hao na kuwafikisha mbele ya mahakama na kuhukumiwa kwa uovu wao huo.
Katika hadithi sahihi iliyosimuliwa na Addaraqutni pamoja na Khalifa bin Khayyat (huyu ni mwalimu wa Imam Bukhari) juu ya kisa hiki, wanasema;
"Katika mkutano ule Abu Musa alipendekeza Aliy na Muawiya wasimamishwe na achaguliwe Abdillahi bin Umar bin Khattab (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa Khalifa wa Waislamu kwa ajili ya heshima aliyonayo mbele ya Waislamu, pamoja na elimu yake na ucha Mungu wake, na hasa kwa vile tokea mwanzo alikataa kujiingiza katika mgogoro huu.
Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Kwa nini hatumchaguwi Muawiya?".
Baada ya kukataliwa pendekezo lake hilo, Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akampendekeza Abdillahi bin Amr (mwanawe) aliyekuwa mcha Mungu na akiheshimiwa sana na Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) pamoja na Waislamu wengine.
Abu Musa akamwambia;
"Mwanao ni mwanamume kweli kweli na mcha Mungu, lakini kwa vile wewe umo ndani ya mgogoro huu, haitawezekana kumchagua yeye akakubalika. Sikiliza ewe Amr! Waislamu wametubebesha sisi jukumu hili baada ya kushindwa kulimaliza kwa panga zao na mikuki, kwa hivyo usizidi kuwaingiza katika mitihani mingine".
Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Sasa wewe unaonaje?"
Abu Musa akasema;
'Mimi naona bora tuwaondoe wote wawili na tuwaachie uamuzi Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) wamchaguwe wanayemuona kuwa anafaa katika jambo hili".
Amr (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza;
'Mimi na Muawiya tutakuwa na msimamo gani?'
Abu Musa akasema;
"Mkihitajiwa mtaitwa, la ikiwa hamkuhitajiwa nyinyi hamtakuwa watu wa mwanzo wasiohitajiwa".
Wakakubaliana kuwaachia uamuzi Masahaba wakubwa kulitatua tatizo hili kwa kumchagua yule wanayemuona kuwa ndiye anayefaa.
Walikubaliana pia kuwa, kwa wakati ule mambo yabaki kama yalivyo, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye alichaguliwa kuwa Khalifa baada ya watu wote kufungamana naye abaki katika utawala wake, na Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) abaki na ugavana wake huko Sham mpaka pale Masahaba waliochaguliwa na wajumbe hao wawili watakapofikia uamuzi juu ya Khalifa mpya wa Waislamu.
Abu Musa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mtu mwenye hekima kubwa sana, kwani aliona kuwa mambo yamekwishapindukia mpaka, na kwamba maelfu ya Waislamu wanakufa kila siku katika vita hivi. Alikuwa akielewa kuwa si sawa kuiangusha haki iliyochaguliwa kisheria kwa ajili ya kuwaridhisha watu wanaopigana, lakini wakati huo huo aliona kuwa hitilafu baina ya Aliy na Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) na mapambano baina ya watu wa Iraq na watu wa Sham yalifikia daraja mbaya kiasi ambacho hapana budi watu wabadilishe fikra zao katika kulitatua tatizo hili.
Abu Musa (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliona pia kuwa madai ya Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) hayakuwa madai ya kawaida, na hitilafu iliyopo baina ya Waislamu haikuwa hitilafu ya kawaida, bali yote yaligeuka kuwa ni vita vikali sana vya wenyewe kwa wenyewe vilivyopoteza maelfu ya roho za Waislamu na wakati huo huo hatari ya kuweza kupotea kwa maelfu ya roho nyengine za Wasilam ingalipo.
Akaona kuwa njia ya pekee inayoweza kusimamisha vita hivyo kwa wakati huo ni kuwaondoa wale waliohusika na mgogoro huo katika mamlaka yao ikiwa kama ni chanzo bora cha kusimamisha vita hivyo.
Ikiwa uamuzi wake wa pili wa kuwataka Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu) wamchaguwe yule wanayemwona kuwa atafaa kuwaongoza Waislamu katika wakati huo mgumu haukutimizwa, na hii ni kwa sababu ya mabadiliko ya haraka sana yaliyotokea, basi wa kulaumiwa si Amr wala si Abu Musa (Radhiya Llahu anhum).
Walihudhuria mazungumzo hayo pia Masahaba wakubwa kama vile, Abdillahi bin Omar, Abdillahi bin Abbas, Abdillahi bin Zubair, Al Mughiyra bin Shuuba na wengineo (RAnhum).
Kisa kama hiki pia kimeelezwa katika Tarikh ya Bukhari kama alivyoelezea Sheikh Uthmaan Al Khamis katika 'Huqbah mina Tariykh – uk.84'.

Baada ya makubaliano


Haujapita muda mrefu baada ya makubaliano hayo baina ya Abu Musa na Amr (Radhiya Llaahu ‘anhu), zikasikika sauti kutoka kwenye kambi ya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) zikisema;
"Tulikosea tulipokubali kuhukumiwa na watu, na sasa tunarudia tena makosa yetu yale yale. Hatukubali kuhukumiwa isipokuwa kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye tokea mwanzo alikwishawaonya watu wake kuwa madai ya upande wa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) ya kutaka kuhukumu kwa Qurani yalikuwa ni katika hadaa na mbinu za kivita akawajibu watu wake kwa kuwaambia;
"Sasa hivi tena baada ya kutoa ahadi zetu na baada ya makubaliano ndiyo mnasema maneno haya?".
Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliondoka hapo akiwa pamoja na watu wachache aliobaki nao na kuelekea mje wa Al Kufa.
Wengi kati ya wafuasi wake walijitenga naye kwa hoja kuwa eti alikubali kuhukumiwa na watu badala ya kuhukumiwa na kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wengine waliamua kujitenga kwa kuchoshwa tu na vita virefu visivyokwisha
Inasemekana kuwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alijikuta amebakiwa na watu wasiozidi elfu kumi na sita, na riwaya nyingine zinasema kuwa alibakiwa na watu wapatao elfu kumi na mbili na nyengine zinasema kuwa waliobaki walikuwa wachache zaidi kuliko idadi hiyo.
Kuanzia hapo Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa anakabiliwa na makundi mawili - Moja lipo Sham likidai kisasi cha kuuliwa kwa Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu), na kundi la pili lipo Iraq, limepiga kambi katika mji unaoitwa Naharawan, ulio kando kando ya mto Tigris. Kundi hili lilipewa jina la Khawarij, na kundi hilo lilikuwa likimlaumu Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa kukubali kwake kuhukumiwa na watu badala ya kuhukumiwa kwa sheria ya Mwenyezi Mungu
Walikuwa wakisema;
"Hapana hukmu isipokuwa ile ya Mwenyezi Mungu".
Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimuomba Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) amkubalie ende kujadiliana na watu hao, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Mimi nakuogopea."
Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Hapana hofu yoyote Inshaallah".
Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipowaendea akawakuta kuwa ni watu wenye kufanya ibada sana, na walipomuona wakamwambia;
"Karibu ewe Ibni Abbas, kipi kilichokuleta?"
Akasema;
"Nimekuja kuzungumza nanyi".
Wengine kati yao wakasema;
"Msizungumze naye".
Wengine wakamwambia;
"Sema tutakusikiliza".
Akasema;
"Hebu niambieni, mnamlaumu kwa makosa gani Aliy bin Ammi yake Mtume wa Mwenyezi Mungu, mume wa mwanawe na wa mwanzo kumuamini?"
Wakasema;
"Mambo matatu".
"Yepi hayo?"
Wakasema;
"La mwanzo ni kukubali kwake kufuata hukmu ya wanadamu katika dini ya Mwenyezi Mungu. La pili, amepigana vita na Aisha na Muawiya bila kuchukuwa ngawira wala kuwateka, na la tatu amekubali kujiondolea mwenyewe cheo chake cha Ukhalifa juu ya kuwa Waislamu wamefungamana naye na kumkubali kuwa yeye ni Khalifa wao".
Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawauliza;
"Mnaonaje nikikupeni dalili kutoka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na kutoka katika mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) juu ya haya mnayomlaumu, mtarudi kwake na kuyaacha haya mliyo ndani yake?"
Wakasema;
"Ndiyo".
Akasema;
"Ama ile kauli yenu katika kumlaumu kukubali kwake kuhukumiwa na watu katika dini ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu anasema;
"Enyi mlioamini! Msiuwe mawindo na hali mumo katika Hija au Umra. Na miongoni mwenu atakayemuua kwa kusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa (kuchinja) kilicho sawa na alichokiuwa katika wanyama wanaofugwa, kama watakavyohukumu waadilifu wawili miongoni mwenu."
Al Maidah - 95
Semeni ukweli wenu, hivyo kuhukumiwa na wanadamu katika kusimamisha umwagaji wa damu na kupoteza nafsi zenu na kupatanisha baina yenu ni bora au kuhukumiwa na wanadamu juu ya sungura (aliyeuliwa na mtu anayehiji) ambaye thamani yake ni sawa na robo dirham?"
Wakasema;
"Bali katika kusimamisha umwagaji wa damu na kupatanisha baina ya watu".
Akasema;
"Hilo tushalimaliza?'
Wakasema;
"Ndiyo".
Akasema;
"Ama ile kauli yenu kuwa Aliy alipigana vita na hakuwateka ngawira wanawake kama vile Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alivyofanya. Kweni nyinyi mlikuwa mkitaka amteke ngawira Mama yenu Bibi Aisha na awe halali kwenu kama wanavyohalalishwa wanawake wanaotekwa katika vita? Mkijibu 'ndiyo', mtakuwa mumekufuru, na mkisema kuwa yeye si mama yenu, pia mtakuwa mumekufuru, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema;
"Na wakeze ni mama zao"
Ahzab - 6
Kwa hivyo jichagulieni mnachotaka".
Wakasema;
"Na hili pia tushalimaliza".
Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema;
"Ama kauli yenu kuwa Aliy alijifutia mwenyewe cheo chake cha Ukhalifa, hata Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alifanya hivyo siku ya mapatano ya Hudaibia, pale washirikina walipomtaka aandike mkataba, na yeye akaandika; "Haya ni makubaliano baina ya Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu." Na makafiri wakasema; "Tungelikuwa tunaamini kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, tusingelikuzuwia kwenda kutufu Al Kaaba, na wala tusingekupiga vita, lakini andika;
"Muhammd bin Abdillah". Na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akalikubali sharti lao huku akisema;
"Wallahi mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu hata mkinikadhibisha".
Wakasema;
"Na hili pia nalo tushalimaliza.
Ikawa katika matunda ya majadiliano hayo yenye hoja zilizo wazi, watu wapatao elfu tano walirudi katika kambi ya Aliy bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu) na riwaya nyingine zinasema kuwa idadi kubwa kuliko hiyo walirudi.

Vita vya Nahrawan


Baada ya wengi kati ya wale waliojitenga na jeshi la Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kutambua makosa yao na kurudi katika kambi ya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), waliobaki katika kundi la Khawarij wakaondoka na kupiga kambi mahali panapoitwa Nahrawan, mji uliopo kando kando ya mto Tigris, na huko wakawa wanafanya zogo na kuingia misikitini huku wakipiga kelele wakisema; "Hatukubali kuhukumiwa isipokuwa na Mwenyezi Mungu."
Aliposikia kauli hiyo Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alisema; "Ni kauli ya haki hiyo lakini (wanaitamka) kwa ajili ya kutaka kuipitisha batili yao."
Anasema Imam Ahmed bin Hanbal:
Nimehadithiwa na Is'haq bin Issa al Taba'a aliyehadithiwa na Yahya bin Suleyam kutoka kwa Abdullah bin Uthmaan bin Khaytham kutoka kwa Ubeidullah bin Iyadh bin Amr al Qariy kuwa amesema; "Abdullahi bin Shaddad alikuja kwa Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) wakati sisi tupo kwake tumekaa na wakati huo alikuwa anarudi kutoka Iraq katika siku za kuuliwa kwa Ali, na bibi Aisha akamwambia; "Ewe Abdullah bin Shaddad utanielezea ukweli kwa nitakayokuuliza? Nihadithie juu ya hawa waliomuua Ali" Abdulah akasema; "Na kwa nini nisikuelezee ukweli." Akasema; "Haya nihadithie juu ya kisa chao."
Akasema; "Hakika Aliy alipokubali mkataba na Muawiya na waamuzi wawili walipotoa uamuzi wao, wakajitoa kutoka katika jeshi lake watu elfu nane miongoni mwa wasomi na kuelekea mahali panapoitwa Hururaa pembezoni mwa mji wa Al Kufa huku wakimwambia; "Umejivua nguo aliyokuvisha Mwenyezi Mungu na (umelikataa) jina alilokupa Mwenyezi Mungu  kisha ukakubali hukmu ya watu katika dini ya Mwenyezi Mungu wakati hapana hukmu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu."
Zilipomfikia habari hizo Aliy akaamrisha patangazwe kuwa kila mtu aje kwake akiwa amebeba msahafu. Na nyumba ilipojaa watu wenye elimu zao Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akataka aletewe msahafu. Akauweka mbele yake na kuushika huku akiuambia; "Ew msahafu! Zungumza na watu!"
Watu wakamwambia; "Ewe Amiri wa Waislamu unazungumza na nani? Hizi ni karatasi na uwino tu, sisi ndio tunaozungumza kama kitabu kinavyotutaka, unataka nini?"
Akasema; "Sahibu zenu hawa waliojitenga, baina yangu na wao kitabu cha Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu katika kitabu chake anasema;
"Na kama mkijua kuwa kuna ugomvi baina ya mke na mume basi pelekeni mwamuzi mmoja katika jamaa za mwanamume na mmoja katika jamaa za mwanamke. Kama wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu atawawezesha."
Annisaa 35
Na damu ya umati wa Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ni adhimu zaidi na tukufu zaidi kupita ugomvi baina ya mume na mke. Kisha wananilaumu kuwa nimekubali kama alivyotaka Muawiya kuliandika jina langu Aliy bin Abu Talib (bila kuandika kuwa mimi ni Khalifa wa Waislamu), wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikubali katika sulhu ya Hudaibia kuliandika jina lake Muhammad bin Abdillah bila ya kuandika Muhammad Rasulullah kwa ajili ya kutaka sulhu."
Na hapo ndipo Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokubali Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) awaendee waliojitenga naye na wakatubu waliotubu na kurudi katika jeshi la Ali."
Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha) akaendelea kumuuliza Abdulla bin Shaddad; "Kisha Aliy akapigana vita nao?"
Akasema;"Ndiyo wallahi, na Aliy akawashinda, na ndani ya kundi hilo alikuwemo Dhu Thadiy, na ikawa kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kuwa; wakati Waislamu watakapokhitalifiana (wakawa makundi mawili) litatokea kundi la tatu litakalopigwa vita na kundi la haki baina ya mawili hayo, na ndani ya kundi hilo (la tatu) atakuwemo Dhu Thadiy. Na vita vilipomalizika Aliy akawa anatafuta baina ya waliouliwa mpaka alipomuona Thu Thadiy ndipo aliposujudu kumshukuru Mwenyezi Mungu maana alielewa kuwa yupo upande wa haki."
Muslim -  mlango wa Zaka juu ya kundi hilo.  Imam Ahmed -  katika Musnad ya Aliy bin Abu Talib, na hadithi hii imefanyiwa tahakiki na Ahmed Shakir na akasema kuwa ni hadithi sahihi.

Vita vilianza baada ya habari nyingi kumfikia Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) juu ya mauaji ya kila siku yanayofanywa na watu hao na Aliy bin Abu Talib (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaamua kuwafuata huko na kuwapiga vita.
Walimuuwa sahaba mcha Mungu aitwaye Abdullahi bin Khubab (Radhiya Llaahu ‘anhu), kisha wakamuua mkewe na kumkatakata tumbo lake na wakati huo alikuwa na mimba, na Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipotuma ujumbe kutaka kujua nani aliyemuuwa wakajibu;
"Sote tumemuua!"
Hapo ndipo Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipoamua kupeleka majeshi yake na kuwashambulia watu hao na kuwashinda katika vita hivyo vilivyokuja kujulikana kwa jina la 'Vita vya Naharawan'.
Hata hivyo uasi na mapambano marefu ya chini kwa chini baina yao yaliendelea muda mrefu sana na hatimaye Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliwa.

Kuuliwa kwa Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu)


Ali (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliuliwa wakati wa alfajiri baada ya kupita kiasi cha miaka miwili tokea vita vya Nahrawan kumalizika alipokuwa katika jukumu lake la kila siku la kuwaamsha watu Sala ya alfajiri. Akastukia akishambuliwa na mtu aliyekuwa katika kundi la Khawarij aitwaye Abdurahman bin Muljim al Muradiy huku akimchoma kwa panga na visu vilivyojazwa sumu.
Aliuliwa alipokuwa akisema kwa sauti kubwa;
"Assalaatu enyi watu, amkeni Mungu akurehemuni".
Muuaji huyo alikuwa keshapangana na wenzake wawili, Breik bin Abdullah Al Tamimi na Amr bin Bakar Al Tamimi. Mmoja aende Sham na kumuuwa Muawiya na mwengine aende Misri na kumuuwa Amr bin Al Aas (RAnhum) kwa mpigo mmoja katika siku moja na wakati mmoja waliokubaliana baina yao, ili wawapumzishe watu na matatizo yao.
Wakakubaliana wote kuwa watimize ukatili wao huo siku ya Ijumaa, Ramadhani ya kumi na saba, mwaka wa arubaini baada ya Hijra

Sayiduna Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa na kawaida ya kutoka peke yake bila ya ulinzi kabla ya Sala ya alfajiri kwa ajili ya  kuwaamsha watu, na kwa ajili hiyo ilikuwa rahisi kwa muuaji wake kumshambulia kwa upanga wake alioulaza ndani ya sumu kwa muda wa mwezi mzima.

Ama Breik, aliyekwenda kumuuwa Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu), alimkosea na kumjeruhi pajani, na watu wa Muawiya waliwahi kumkamata mtu huyo, na alipokamatwa alisema;
"Usuniuwe ewe Muawiya, maana nataka kukupa habari njema".
Muawiya akamuuliza;
"Habari gani hizo?"
Akasema;
"Mwenzangu tuliyepangana naye keshamuuwa Aliy bin Abu Talib siku hii ya leo".
Muawiya akamuuliza;
"Unajuaje pengine naye pia hakufanikiwa?"
Akasema;
"Lazima atafanikiwa kwa sababu Aliy hatoki na walinzi kama wewe".
Muawiya (Radhiya Llaahu ‘anhu) akaamrisha auliwe, akauliwa.

Amr bin Al Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) naye siku hiyo kwa bahati alishikwa na tumbo la kuharisha akachelewa kutoka, na badala yake akatoka mmoja katika majemadari wa jeshi lake aitwaye Kharija bin Abi Hubaibah, na yule aliyepewa jukumu la kumuuwa Amr ambaye jina lake pia ni Amr bin Bakar alimshambulia Kharija na kumuuwa akidhania kuwa ndiye aliyemkusudia.

Maziko yake


Alipokuwa akianguka baada ya kupigwa panga na visu, Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alisema;
"Mkamateni na msimuache. Nikifa naye auliwe bila ya kukatwa katwa, ama nikiishi basi mimi mwenyewe nitaamuwa ikiwa nimuuwe au nimsamehe".
Baada ya kufariki dunia, watoto wake wakamuuwa Abdurahman bin Muljim.

Maiti ya Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ilisaliwa na mwanawe mkubwa Al Hassan (Radhiya Llaahu ‘anhu) kisha akazikwa katika nyumba iitwayo Dar al Imara katika mji huo huo wa Al Kufa.
Ama ile hadithi mashuhuri isemayo kuwa eti maiti yake ilipakiwa juu ya mnyama na kuachwa iende isikojulikana, hadithi hiyo si sahihi, na jambo hilo haliwezekani kufanywa na Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) waliofundishwa na Mtume wao  namna ya kuzika maiti wao.