Abdullah
ibn Masoud- mtaalamu wa Quraan
Tokea utotoni kwake alikuwa ni mtu wa milimani
akichunga wanyama wa mmoja wa watukufu wa kiquraysh Uqbah ibn Muayt. Watu
walikuwa wakimwita Ibn Umm Abd wakimaanisha mtoto wa kijakazi.
Mtoto huyu akasikia habari za Mtume (SAW) ila
hakuzitilia maanani. Habari hizi kwani alikuwa bado mdogo na mara
nyingi kuwa mbali ya jamii ya Makka. Na kawaida yake ilikuwa kutoka mapema
asubuhi na harudi ila pale kiza kimeingia.
Siku moja, huku akiendelea na kuchunga wanyama
wake, akawaona watu wawili kwa mbali wakija upande wake.
Walionekana kuwa watu wazima na wenye heshima zao na kuwa na kila dalili za
uchofu wa safari. Walikuwa na kiu pia kwani koo zao na midomo ilikuwa imekauka.
Walikuja na kumsalimia na kusema:
“Kijana, tukamie mmoja wa hawa kondoo tupate
kuondosha kiu zetu na kurudisha nguvu mwilini.”
“Siwezi, kondoo si wangu mimi nimekabidhiwa
niwachunge tu, aliwajibu.
Wale watu hawakubishana nao na licha ya kuwa
na kiu, walionesha tabasamu kwa ukweli waliousikia.
Hawa watu wawili si wengine bali ni Mtume
(SAW) na Sahiba wake Abubakar (RA). Siku hiyo walikimbilia milimani
kuepukana na mateso na madhila ya maquraysh wa Makka. Kijana naye pia
alivutiwa na Mtume (SAW) pamoja na sahiba wake na akawa karibu nao sana.
Haukupita muda Abdullah alisilimu na kuomba
kumwambata na kumhudumia Mtume (SAW). Mtume akakubali na tokea siku
hiyo akaachana na kuchunga na kuanza kumwambata na kumhudumia Mtume
(SAW).
Abdullah alikuwa karibu sana na Mtume Muhammad
(SAW) na alimshughulikia kwa shida zake ndani na nje ya nyumba yake, alifuatana
naye safari zake za kawaida na vita. Humwamsha anapolala na kumtengenezea
pazia akioga na kumbebea vitu vyake kama mswaki na kadhalika.
Kwa kuwa karibu sana na Mtume (SAW), Abdullah
alibahatika kusoma na kuiga tabia zake Al-Habib na alizifuata zote mpaka
kuambiwa, alikuwa karibu kumfikia Mtume Muhammad (SAW) kitabia.
Abdullah alifundishwa kutoka madrassah ya
Mtume (SAW) mwenyewe alikuwa msomaji mahiri wa Quran miongoni mwa masahaba.
Aliifahamu vizuri zaidi Quran. Moja kwa moja akawa mtaalam wa sheria ya
kiislam. Mfano mzuri ni pale mtu mmoja alipokuja kwa Khalifa Umar ibn Khattab
(RA) huku amesimama kwenye uwanja wa Arafa na kusema:
“Ewe Amirul muuminiin, nimekuja kutoka Kuffah
ambapo nimemuacha mtu anaandika Quran kutoka kwenye hifadhi za watu.”
Umar alikasirika sana na hapo hapo kuuliza kwa
ghadhabu, “ni nani huyo?”
“Abdullah ibn Masoud” akajibu.
Ghafla hasira zote za Umar zikaondoka.
Akaendelea kusema, “wallahi, simjui mtu
mwengine aliebaki mwenye sifa za kuifanya kazi hii zaidi yake.Ngojea
nikuhadithie”, Umar aliendelea:
“Usiku mmoja Mtume Muhammad (SAW) alikuwa na
mazungumzo na Abubakar (RA) kuhusu hali ya waislam, mimi nilikuwepo.
Mtume (SAW) alipoondoka tukafuatana naye na tulipokuwa tunapita msikitini,
kulikuwa na mtu amesimama akiwa katika sala ambaye hatukumwona vizuri.
Mtume (SAW) alisimama na kumsikiliza kisha akatugeukia na kusema, “yoyote
anayetaka kusoma Quran ikiwa safi kama ilivyoteremeshwa basi asome kwa kisomo
cha Ibn Umm Abd.”
Abdullah alipomaliza sala na huku amekaa
akiomba dua, Mtume anasema, “Omba na utapewa”, (akikusudia dua ya Abdullah.)
Umar aliendelea, “Nikajisemea kwenye nafsi
yangu nitakwenda moja kwa moja kwa Abdullah na kumpa habari njema za
kumhakikishia kukubaliwa kwa dua zake. Nilipofika nikamkuta tayari
Abubakar ameshaniwahi!. Wallahi sijawahi kumpiku Abubakar katika kufanya jambo
lolote la kheri.”
Abdullah alijaaliwa elimu na Quran mpaka
mwenyewe kusema, Nnaapa kwa yule ambao hakuna Mungu mwengine isipokuwa yeye,
hakuna aya katika kitabu cha Mwenyezi Mungu (SW) iliyoteremka ila mimi kuijua
wapi imeteremshwa na katika mazingira gani, Wallahi kama mnajua mtu mwengine
anayekijua kitabu cha Allah (SW) zaidi yangu, ningelifanya kila lililo ndani ya
uwezo wangu kuwa karibu naye”
Abdullah hakuwa akitia chumvi wala kujisifu
kwa usemi wake huu, mara moja Umar alikutana na msafara na ilikuwa usiku na ule
msafara haukuonekana vizuri kwa giza nene lililotanda. Umar akaamrisha mmoja
wao kwenda kuwasalimia, Umar akauliza:
“Mnatoka wapi?
“Fajjun Amiiq, (bonde kuu),” akajibiwa.
“Mnaelekea wapi?”
“Baytul Atiq (nyumba ya kale),” akajibiwa.
“Lazima kuna alim -msomi- miongoni mwenu” Umar
akasema.
Umar akamuagiza mmoja katika wale amuulize.
“Ipi ni sehemu adhimu katika Quran?”
“Allah, hakuna mwengine isipokuwa yeye,
aliyehai, na kujitosheleza, halali, wala kuchukuliwa na usingizi….” akajibiwa
na hii ni aayatul kursiy.
“Ni sehemu ipi katika Quran iliyo
wazi kabisa kuhusu uadilifu?”
“Mwenyezi Mungu (SW) anakuamrisheni uadilifu
na kufanya ihsan, na kuwalisha jamaa wa karibu……………..” ,akajibiwa.
“Ni maelezo gani katika Quran yaliyoelezwa kwa
upambanuzi yakinifu?”
“Yoyote
atakayefanya jambo kiasi cha uzito wa chembe ya ngano, likiwa zuri
ataliona na yoyote atakayefanya jambo kiasi cha uzito wa chembe ya ngano,
likiwa la shari ataliona.”
“Sehemu gani ya Quran inaongeza ari ya kuwa
na matarajio makuu?”
“Sema ewe Muhammad, enyi waja wangu mliopoteza
rasilmali zenu, msikate tamaa kwa rehma za Mwenyezi Mungu (SW). Hakika Allah
(SW) anasemehe madhambi yote…………..”
Kufika hapo Umar akauliza:
“Mko na Abdullah ibn Masoud?”
“Wallahi, naam.”
Sifa za Abdullah ibn Masoud hazikuwa katika
usomaji Quran bali alikuwa mchangamfu, pia mpiganaji hodari na shujaa hasa pale
inapohitajika.
Siku moja, masahaba walikuwa pamoja Makka
wakiwa bado wachache na kutokuwa na nguvu yoyote na wakaambizana, “maquraysh
hawajawahi kuisikia Quran ikisomwa hadharani na kwa sauti kubwa, nani
atathubutu kuwasomea?”
Abdullah akajitolea, “mimi nitawasomea”
“Tunakuhofia maisha yako” wakamwambia.
“Tunataka mtu mweye nasaba ya kuweza kumkinga
na ghadhabu zao”
Abdullah bado akawa anasisitiza, “niacheni,
Allah (SW) atanilinda na kuniepusha na yale yote maovu watakayoyakusudia”
Akaenda Al-Kaaba mpaka alipofikia ‘Maqaam
Ibrahim’, Abdullah akaanza kusoma:
“Bismillahi Rrahmanir Rahiim, Ar Rahmaan,
Allamal Quraan. Khalaqal Insaan. Allamahul bayaan………..”
(Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha
neema kubwa kubwa na mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo. Nnaapa kwa mola
mwenye kurehemu. Ambaye amefundisha Quran. Akamuumba
Binadamu. Akafundisha kuweza kubaini ‘haki na batil’ ……..
Aliendelea kusoma huku maquraysh wametulia
wakimsikiliza mpaka baadhi yao kuuliza:
“Nini unasema Ibn Umm Abd?”
Walipokuja kugutuka, “du! anasoma baadhi ya
maneno aliyokuja nayo Muhammad.”
Wakamvamia na kuanza kumpiga usoni huku
akiendelea kusoma. Aliporudi kwa wenzake na kuona jinsi uso wake
ulivyoharibika na kuvuja damu wakamwambia, “haya ndio tuliyokuowa tukiyahofia.”
“Wallahi, maadui wa Mwenyezi Mungu, sasa hivi
hawana raha hata kidogo tena zaidi yangu na kama mkitaka, kesho nitakwenda tena
kuwasomea.” Abdullah aliwaambia.
“Uliyofanya yametosha, tayari umeshawafanya
wasikilize yale wasiyoyapenda Abdullah,”
Abdullah ibn Masoud aliishi hadi enzi za
ukhalifa wa Uthman (RA). Alipougua na kuwa taabani kitandani alitembelewa
na Khalifa:
“Unaumwa na nini?”
“Dhambi zangu,” Abdullah alijibu.
“Na nini unatamani?”
“Rehma za mola wangu”
“Hutaki nikupe ruzuku, ambayo umeikataa kwa
miaka sasa hivi.” Aliulizwa Abdullah.
Abdullah alijibu, “sina haja nayo.”
“Itabaki na kuwasaidia mabinti zako baada
yako”
“Hivi kweli unahofia umasikini wa wanangu,
nimewaamrisha wasome Suratul Waqiah kila usiku kwani nilimsikia Mtume Muhammad
(SAW) akisema, “atakae soma Suratul waqiah kila siku usiku, hatopatwa na balaa la
umasikini maishani kwake.”
Usiku huo Abdullah, aliiaga dunia kuelekea kwa
Mola wake, ulimi wake ukiwa bado na unyenyekevu kwa kumkumbuka Allah (SW) na
kwa kukisoma kitabu chake Quraan.