Abu Ammaar
Heshima ambayo Allah Subhaanahu
Wata’ala amempa mume katika ndoa ni kumkabidhi haki ya talaka kuwa mikononi
mwake pekee bila ya kumshirikisha mke ambae wameoana katika ndoa halali ambapo
kila mmoja angekuwa na haki sawa.
Heshima hii ingawa amepewa mume
pekee lakini na mke pia ana haki ya kuitekeleza endapo mume atakubali katika
masharti ya ziada katika ndoa (prenuptials) kwamba na mke nae anayo haki ya
kumuacha mumewe kwa kutumia talaka. Vyenginevyo mke hupaswa kutumia njia
nyengine kama kuomba kuachwa, Khul’u au kupitia kwa Kadhi.
Sababu za kimsingi kupewa mume
heshima hii ni kama zifuatazo:
1
Mke mara nyingi hukosa uvumilivu na
subira kuliko mume na hivyo kuweza kuitumia haki hii pasi na sababu za
kimsingi.
2
Athari za talaka humfunga zaidi mume
kama kulipa mahari (ikiwa hayakukamilishwa) kumhudumia mke muda wote wa eda.
Heshima hii hakupewa mume tu kama ni
silaha au kuitumia kwa jinsi atakavyo,aonavyo au apendavyo bali amewekewa
mipaka na taratibu maalum zinazohusiana na suala zima la ndoa ikiwa ni mkataba
wa pande mbili zenye haki sawa na huku akitakiwa kuchunga mipaka ya Allah
Subhaanahu Wata’ala.
Allah Subhaanahu Wata’ala
alipoifanya ndoa kuwa ni moja katika mipangilio ya muendelezo wa maisha ya
binadamu katika ardhi anataka kuhakikisha kwamba malengo ya ndoa yanakuwepo na
kutimizwa kama kuwepo mapenzi, kuoneana huruma, kuweza kuenziana na kuwepo maelewano
ya hali ya juu kati ya mume na mke.
Endapo kutatokea moja katika misingi
na mihimili ya ndoa kushindwa kufikiwa kwa kutokea mabadiliko ya tabia, mapenzi
kuondoka na kushindikana kwa waliopewa jukumu la kuleta maelewano kati ya
wanandoa basi hakuna busara yoyote kuendeleza maisha ya ndoa katika mazingira
ambayo ni kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Jamii ya kiislamu imepoteza mweleko
katika masuala ya ndoa kwa ujumla na hasa katika masuala ya talaka ndiyo kuna
mtihani mkubwa. Bado kuna miongoni mwa waume waislamu mawazo yao makubwa
wanapoingia katika chuo hiki muhimu ni kustarehe na mke na wengine kufikia
kuwaita mabinti wa kike kama ni bidhaa mbovu na huku ni kuwadhalilisha
akinamama kijinsia.
Mtazamo huu ndio unaowafanya baadhi
ya waume wasifahamu ya kujifunza maana na makusudio halisi ya ndoa katika dini
yetu ya kiislamu. Wengine hata hawafahamu hekima ya kuletwa na kuruhusiwa
talaka na kuitumia kwa istihzai na inda kama ni silaha, kitisho na mkwala
kumtishia mke wa ndoa. Mke aliekabidhiwa kwa neno lake Allah Subhaanahu
Wata’ala na kwa Sunnah za Mtume wake Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam.
Hekima hii ambayo Allah Subhaanahu
Wata’ala ameitolea ufafanuzi kwa kuwepo aya tofauti ndani ya Quraan zinazofafanua
utaratibu wa kufuatwa mpaka kufikia kutumika. Kama anavyosema Annisaa/35
وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ
بَيْنِهِمَا فَابْعَثُواْ حَكَماً مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَماً مِّنْ أَهْلِهَا إِن
يُرِيدَا إِصْلاَحاً يُوَفِّقِ اللّهُ بَيْنَهُمَا إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيماً
خَبِيراً).
Na mkichelea kutakuwepo
mfarakano (Kutokuelewana) baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana
na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allah
atawawezesha. Hakika Allah ni Mjuzi Mwenye khabari
Kabla ya kufikiwa kutolewa hupitiwa
na taratibu za kutafutwa suluhu baina ya Wanandoa kwa mawaidha, nasaha,
miongozi hadi kupelekea wawakilishi wa kila upande kukutana kwani suluhu ina
kheri kubwa kuliko talaka kama anavyothibitisha Allah katika Quraan Annisaa/128
وَإِنِ امْرَأَةٌ خَـفَتْ
مِن بَعْلِهَا نُشُوزاً أَوْ إِعْرَاضاً فَلاَ جُنَاْحَ عَلَيْهِمَآ أَن يُصْلِحَا
بَيْنَهُمَا صُلْحاً وَالصُّلْحُ خَيْر
Na mwanamke akichelea kutupwa
au kutojaliwa na mumewe, basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu
ni bora
Hata hivyo ikifika hali ya
kutoelewana kwa wanandoa kufikia sura ya kushindikana kupatika suluhisho licha
ya jitihada zote kupita hakuna budi ila talaka kutumika ikiwa ni hatua ya
mwisho na wala si ya mwanzo kama wengi wanavyoitumia kimakosa, kwa kutokujua au
kwa kufanya inda. Suluhisho hili ni kwa dharura iliopo tu – malengo
yaliyokusudiwa kuwepo ndoa kuondoka.
Allah Subhaanahu Wata’ala
anafahamisha utaratibu wa kutengua mkataba wa ndoa kama ifuatavyo Suuratul
Baqarah /229
(الطَّلاَقُ مَرَّتَانِ
فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ
بِإِحْسَانٍ
Talaka ni mara mbili.
Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri.
Na pia kusema katika Suuratu
Talaaq/2
(فَإِذَا بَلَغْنَ
أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ)
Basi wanapofikia muda wao,
ima warejeeni mkae nao kwa wema, au farikianeni (achaneni) nao kwa wema.
Hapa zimetajwa hali mbili tu nazo
ni:
1
Kukaa na mke kwa wema
2
Kuachana nao kwa vizuri
kwa daraja ya Ihsaani
Allah Subhaanahu Wata’ala ndiye
aliyetuumba na kutujua hali zetu na undani wetu anaejua yaliyojificha na ya
dhahiri. Ni yeye aliyetupa moja ya machaguo haya mawili aliyoyataja ndani ya
kitabu chake Quraan – kitabu kisicho na shaka wala dosari na kilichokamilika.
Kumomonyoka maadili na misingi
sahihi aliyetuachia Mtume wetu Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam pamoja na watangu
wema kumewafanya baadhi ya waislamu kuongeza jambo la tatu nalo ni kumtundika
mke kwa kumuacha katika hali ya kuwa hajaachika na wala haishi na mume maisha
ya kindoa. Annisaa /129
وَلَن تَسْتَطِيعُواْ أَن
تَعْدِلُواْ بَيْنَ النِّسَآءِ وَلَوْ حَرَصْتُمْ فَلاَ تَمِيلُواْ كُلَّ
الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَة
Wala
hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata mkikakamia. Kwa hivyo msimili
moja kwa moja mkamwacha (mmojawapo) kama aliyetundikwa.
Anasema Ibn ‘Abbaas, Allah awawie
radhi yeye na baba yake, kwamba neno “Mu’allaqah” maana yake ni mwanamke ambae
hana mume na wala hajaachika - ametundikwa.
Baya zaidi wanaowafanyia wake zao
uovu huu, huwa hawajioni kama wanamuasi Allah Subhaanahu Wata’ala pamoja na
Mtume wake Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam bali hujiona na kujilabu kwa kitendo
chao hiki. Na kila wakimuona mke akiatilika huchekelea ndani ya nafsi zao huku
wakiisahau kauli ya Allah Subhaanahu Wata’ala Al Baqarah/231
وَلاَ تُمْسِكُوهُنَّ ضِرَاراً لَّتَعْتَدُواْ
وَمَن يَفْعَلْ ذَلِكَ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ وَلاَ تَتَّخِذُوَاْ آيَاتِ اللّهِ
هُزُواً
Wala msiwarejee kwa
kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakayefanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake. Wala
msizichukulie Aya za Allah kwa utani.
Aya hii, anasema Ibnu ‘Abbaas Allah
awawie radhi yeye na baba yake, ilikuwa wanaume wakiwaacha wake zao na
wakikaribia kumaliza eda zao huwarudia si kwa wema bali kuwa kuwazuia ili
wasiweze kuolewa na watu wengine na baada ya muda huwaacha tena na kisha
kusubiri mpaka karibu na kumalizika kwa eda na kisha kuwarudia. Allah Subhaanahu
Wata’ala akateremsha aya hii kuwakataza kwa kitendo chao hiki.
Na pia katika tafsiri ya Ibn Kathiyr
anaifafanua aya hii kwa kusema:
"هذا أمر من الله عز
وجل للرجال، إذا طلق أحدهم المرأة طلاقاً له عليها فيه رجعة أن يحسن في أمرها إذا
انقضت عدتها ولم يبقى منها إلا مقدار ما يمكنه فيه رجعتها، فإما أن يمسكها، أي
يرتجعها إلى عصمة نكاحه بمعروف، وهو أن يشهد على رجعتها وينوي عشرتها بالمعروف، أو
يسرحها، أي يتركها حتى تنقضي عدتها ويخرجها من منزله بالتي هي أحسن، من غير شقاق،
ولا مخاصمة، ولا تقابح"
Hii ni amri ya Allah
Subhaanahu Wata’ala kwa wanaume. Akiacha mmoja wenu mkewe talaka(moja) basi ana
haki ya kumrudia na kumfanyia wema katika mambo yake ikikaribia kumalizika eda
yake na haikubaki isipokuwa muda mchache ambao utamuwezesha kumrudia mke ima
amrudie katika ndoa kwa wema nako ni kushuhudia kumrudia na kunuia kukaa nae
kwa wema au amuache yaani mpaka amalize eda yake na kisha kumfahamisha kuondoka
katika nyumba katika hali nzuri ya masikilizano bila ya kuwepo chuki, ugomvi au
kufanyiana ubaya.
Mke anaweza kutundikwa katika hali
kama zifuatazo kwa kupigia mifano:
1
Aliedai talaka akiwa na sababu
zinazokubalika kisheria na mume kumkatalia na kugoma kuitoa kwa vikwazo na
visingizio tofauti.
2
Mke mwenza ambae ametelekezwa na
mumewe bila ya huduma ya aina yoyote wala kupata haki zake za kimsingi na
akidai kuachwa hukataliwa na wala hatimiziwi majukumu yake.
3
Alie mbali na mumewe kwa sababu
tofauti na kutokuwa na mawasiliano kwa muda mrefu kupita muda mrefu huku akiwa
hapati huduma ya aina yoyote.
4
Aliefukuzwa katika nyumba ya
mke(mfano huu kwa waliodanganya kama hawana waume huku wameolewa kihalali kama
ilivyo baadhi ya familia Uingereza kwa ajili ya kupata unafuu wa kimaisha)
kisha akagoma kutoa talaka akidai mpaka warudi kule waliopooana.
5
Mume anaekataa kutoa talaka akidai
lazima apewe haki ya kuwa na watoto na kadhalika.
Wake nao kwa upande wao huchangia
hali hizi kutokana na mazingira kuwa dhidi yao kama
1
Kuwa na khofu na woga ya
kunyang’anywa watoto.
2
Kukosa mtu wa kuweza kumsaidia na
kumsimamia kudai haki zake.
3
Kuwa dhaifu na kutoweza kukabiliana
na waume kuweza kudai haki zao za kimsingi kwa kuogopa vitisho na mbinu za
waume.
4
Kufungika na vikwazo vyengine kama
waliooana katika nchi za Ulaya na kusajili ndoa kwa msajili (registrar)
na hivyo kuweza kuachana kiislamu na kujikuta bado ni wanandoa kiserikali na
kadhalika.
Inawezekana wake kwa upande wao
wakadai talaka kwa sababu zisizokuwa za msingi na hapa ni vyema pakaeleweka
maapizo ya Allah Subhaanahu Wata’ala kama hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam
أيما
امرأة سألت زوجها الطلاق من غير ما بأس فحرام عليها رائحة الجنة رواه أحمد
Mwanamke yeyote
atakaedai talaka kutoka kwa mumewe pasi na kuwa na sababu za kimsingi ni haramu
kwake harufu ya peponi
Ahmad
Hakuna kitu ambacho mume atafaidika
kwa kumuacha mke katika hali ya kumtundika hajijui cheo chake kwa kuwepo tu si
mke wa ndoa yenye kutambulika na wala si mtalaka bali ni kuasi na kukiuka
mipaka ya Allah Subhaanahu Wata’ala. Mipaka ambayo Mtume wetu Salla Allahu
‘Alayhi Wasallam anatuhadharisha nayo kwa makaripio makali kwa kusema:
إِنَّ اللهَ حَدَّ
حُدُودًا فَلَا تَعْتَدُوهَا، وفَرَضَ فَرَائِضَ فَلَا تُضَيِّعُوهَا، وحَرَّمَ
مَحَارِمَ فَلَا تَنْتَهِكُوهَا،
وَسَكَتَ عَنْ أَشْيَاءَ رَحْمَةً لَكُمْ مِنْ غَيْرِ نِسْيَانٍ فَلَا
تَسْأَلُوا عَنْهَا
Hakika Allah ameweka
mipaka yake basi msiivuke na amefaridhisha fardhi zake na wala msizipuuze na
ameharamisha maharamisho yake na wala msiyafanye na amenyamaza katika baadhi ya
vitu ikiwa ni rehma kwenu bila ya kughafilika basi msiviulizie na kuvidadisi.
Addaylamiy na wengineo
Kadhia hii haina budi kupigwa vita
na waislamu hasa kwa waume waliojijengea tabia ya kuwatelekeza na kuwatundika
wake bila ya kuzingatia taratibu za kimsingi na kisheria kama anavyosema Allah
katika Suuratul Baqarah/231
وَاذْكُرُواْ نِعْمَتَ
اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَمَآ أَنزَلَ عَلَيْكُم مِّنَ الْكِتَـبِ وَالْحِكْمَةِ
يَعِظُكُم بِهِ وَاتَّقُواْ اللَّهَ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَىْءٍ
عَلِيم
Na kumbukeni neema ya
Allah juu yenu, na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na hikima anacho kuonyeni
kwacho. Na mcheni Allah, na jueni kwamba hakika Allah ni Mjuzi wa kila kitu
Juu ya yote haya kwanini turuhusu
hali ifikie katika daraja hii ya chuki mpaka kufikia kukomoana wakati Allah
Subhaanahu Wata’ala anatuusia kwa maneno yenye hekima kwa kusema - Al
Baqarah/237
وَأَن تَعْفُواْ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى وَلاَ تَنسَوُاْ الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ إِنَّ
اللّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ
Na kusameheana ndiko kulio
karibu zaidi na uchamungu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allah
anayaona mnayo yatenda.
Ukaribu huu kwa uchamungu anauonesha
Allah kwa kutuweza kutuonesha njia kama anavyosema a Attalaaq /2
وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ
يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا
Na anaye
mcha Allah humtengezea njia ya kutokea
Tujitahidi kurudi kwa
mola wetu na kuheshimu mipaka yake katika kila tulifanyalo. Tumuombe Rahmaani
atuondoshee uovu katika nafsi zetu na kuzingatia pamoja na kuheshimu mipaka
yake bila ya kuikiuka.
Wabillahi Ttawfiyq.