Qaaf: 50

  ق
Qaaf: 50

50. SURAT QAAF

(Imeteremka Makka)


Mwanzo wake Sura hii inasimulia kuthibiti Utume wa Muhammad s.a.w. na wanavyo kanya makafiri kuja Mtume kati yao, na kuona muhali kufufuliwa baada ya kwisha geuka udongo. Na ikaeleza Ishara za uumbaji zinazo onyesha dalili ya kwamba Mwenyezi Mungu hashindwi kuwafufua watu baada ya kufa kwao, na hali Yeye ndiye aliye waumba hapo kwanza, na anajua yanayo wapitikia katika nafsi zao. Na Yeye anavisajili vitendo vyao na maneno yao katika Daftari lenye kuhifadhi hata dogo. Na Sura imebainisha kwamba majaribio ya makafiri Siku ya Kiyama kutaka kuukataa ukafiri walio kuwa nao duniani, ati kwa kusingizia walikuwa ni wafwasi tu wa Mashetani hayatawaletea nafuu yoyote.  Kwani mwisho wa mjadala wao ni kutumbukizwa wote katika Moto, na huku Mwenyezi Mungu anawafadhili Waumini kwa kuwapa neema za milele katika Pepo. Kisha Sura inamalizikia masimulizi yake kwa kumuamrisha Mtume s.a.w. avumilie maudhi ya makafiri ambao hawakuzingatia yaliyo wapata walio kadhibisha katika kaumu zilizo kuwa kabla yao, na kumwelekeza Mtume s.a.w. athibiti juu ya ibada ya Mwenyezi Mungu, na kutilia mkazo hili jambo la kufufuliwa, na kumliwaza Mtume s.a.w. kwa kuwa yeye ni mwenye kuwakumbusha Waumini, wala si mtawala wa makafiri.




بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

ق ۚ وَالْقُرْآنِ الْمَجِيدِ﴿١﴾
1. Qaaf. Naapa kwa Qur-aan Al-Majiyd (adhimu, karimu, yenye kheri, baraka na ilmu tele).


بَلْ عَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ فَقَالَ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا شَيْءٌ عَجِيبٌ﴿٢﴾
2. Bali wamestaajabu kwamba amewajia mwonyaji miongoni mwao, wakasema makafiri: “Hili ni jambo la ajabu.


أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا ۖ ذَٰلِكَ رَجْعٌ بَعِيدٌ﴿٣﴾
3. Je, hivi tukifa na tukawa udongo (tutafufuliwa kuwa hai)? Ni marejeo ya mbali hayo!”


قَدْ عَلِمْنَا مَا تَنقُصُ الْأَرْضُ مِنْهُمْ ۖ وَعِندَنَا كِتَابٌ حَفِيظٌ﴿٤﴾
4. Hakika Sisi Tunajua kinachopunguzwa na ardhi kutokana nao (miili yao iliyokufa) na Tunacho Kitabu kinachohifadhi (Lawhum-Mahfuudhw).


بَلْ كَذَّبُوا بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ فَهُمْ فِي أَمْرٍ مَّرِيجٍ﴿٥﴾
5. Bali wamekadhibisha haki ilipowajia, basi wao wamo katika jambo la mchanganyo.


أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ﴿٦﴾
6. Je, hawatazami mbingu juu yao, vipi Tumezijenga na Tumezipamba, na wala hazina mipasuko yoyote.


وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ بَهِيجٍ﴿٧﴾
7. Na ardhi Tumeikunjua na Tukaitupia humo milima thabiti, na Tukaotesha humo kila aina ya (mimea) ya kupendeza.


تَبْصِرَةً وَذِكْرَىٰ لِكُلِّ عَبْدٍ مُّنِيبٍ﴿٨﴾
8. Ni ufumbuzi macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kurudia rudia kutubu.


وَنَزَّلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً مُّبَارَكًا فَأَنبَتْنَا بِهِ جَنَّاتٍ وَحَبَّ الْحَصِيدِ﴿٩﴾
9. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, kisha Tukaotesha kwayo mabustani na (kila aina za) nafaka za kuvunwa.


وَالنَّخْلَ بَاسِقَاتٍ لَّهَا طَلْعٌ نَّضِيدٌ﴿١٠﴾
10. Na mitende mirefu yenye mashada ya matunda yenye kupangika tabaka tabaka.


رِّزْقًا لِّلْعِبَادِ ۖ وَأَحْيَيْنَا بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا ۚ كَذَٰلِكَ الْخُرُوجُ﴿١١﴾
11. (Ni) Riziki kwa waja; na Tukahuisha kwayo (maji) nchi iliyokufa, hivyo ndivyo kufufuliwa.


كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَأَصْحَابُ الرَّسِّ وَثَمُودُ﴿١٢﴾
12. Wamekadhibisha kabla yao (Maquraysh) kaumu ya Nuwh na watu wa Ar-Rass (kisima) na kina Thamuwd.


وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ وَإِخْوَانُ لُوطٍ﴿١٣﴾
13. Na kina ‘Aad na Fir’awn na ndugu wa Luwtw.


وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ وَقَوْمُ تُبَّعٍ ۚ كُلٌّ كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ وَعِيدِ﴿١٤﴾
14. Na watu wa Al-Aykah (kichakani) na kaumu ya Tubba’, wote walikadhibisha Rasuli. Basi ikahakiki onyo Langu.


أَفَعَيِينَا بِالْخَلْقِ الْأَوَّلِ ۚ بَلْ هُمْ فِي لَبْسٍ مِّنْ خَلْقٍ جَدِيدٍ﴿١٥﴾
15. Je, kwani Tulichoka kwa umbile la kwanza? Bali wao wamo katika kuchanganyikiwa akili na umbile jipya (kufufuliwa).


وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾
16. Na kwa yakini Tumemuumba insani na Tunajua yale yanayomshawishi nafsi yake, na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo.


إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ﴿١٧﴾
17. Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika wanaodhibiti ‘amali) wanaokaa kuliani na kushotoni.


مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾
18. Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi).


وَجَاءَتْ سَكْرَةُ الْمَوْتِ بِالْحَقِّ ۖ ذَٰلِكَ مَا كُنتَ مِنْهُ تَحِيدُ﴿١٩﴾
19. Na sakaratul-mawt (mateso ya kutoka roho) itakapomjia kwa haki. (Itasemwa): “Hayo ndiyo yale uliyokuwa ukiyakimbilia mbali.”


وَنُفِخَ فِي الصُّورِ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْوَعِيدِ﴿٢٠﴾
20. Na itapulizwa katika baragumu.  “Hiyo ndio Siku ya makamio.”


وَجَاءَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّعَهَا سَائِقٌ وَشَهِيدٌ﴿٢١﴾
21. Na kila nafsi itakuja pamoja nayo mwendeshaji na shahidi.


لَّقَدْ كُنتَ فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءَكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ﴿٢٢﴾
22. (Itasemwa): “Kwa yakini ulikuwa katika mghafala na haya! Basi Tumekuondoshea kifuniko chako, basi kuona kwako leo ni kukali.”


وَقَالَ قَرِينُهُ هَـٰذَا مَا لَدَيَّ عَتِيدٌ﴿٢٣﴾
23. Na Qariyn (Malaika) wake atasema: “Hii (rekodi) iliyoko kwangu imeshatayarishwa.”


أَلْقِيَا فِي جَهَنَّمَ كُلَّ كَفَّارٍ عَنِيدٍ﴿٢٤﴾
24. (Allaah Atasema): “Mtupeni katika (Moto wa) Jahannam kila kafiri mno, mkaidi!


مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ مُّرِيبٍ﴿٢٥﴾
25. “Mzuiaji wa kheri, mwenye kutaadi, mtiaji shaka.


الَّذِي جَعَلَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَأَلْقِيَاهُ فِي الْعَذَابِ الشَّدِيدِ﴿٢٦﴾
26. “Ambaye Ameweka mungu mwengine pamoja na Allaah, basi mtupeni katika adhabu shadidi.”


قَالَ قَرِينُهُ رَبَّنَا مَا أَطْغَيْتُهُ وَلَـٰكِن كَانَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ﴿٢٧﴾
27. (Shaytwaan) Mwenzake atasema: “Rabb (Mola) wetu! Sikumvukisha mipaka kuasi lakini alikuwa (mwenyewe) katika upotofu wa mbali”.


قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُم بِالْوَعِيدِ﴿٢٨﴾
28. (Allaah) Atasema: “Msikhasimiane Kwangu, na hali Nilishakukadimishieni onyo Langu!


مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ﴿٢٩﴾
29. “Haibadilishwi kauli Kwangu, Nami si mwenye kudhulumu waja (Wangu).


يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِن مَّزِيدٍ﴿٣٠﴾
30. “Siku Tutakapoambia (Moto wa) Jahannam: “Je, umeshajaa?” Nayo itasema: “Je, kuna ziada yoyote?”


وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ غَيْرَ بَعِيدٍ﴿٣١﴾
31. Na italetwa karibu Jannah kwa wenye taqwa isiwe mbali.


هَـٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِكُلِّ أَوَّابٍ حَفِيظٍ﴿٣٢﴾
32. (Itasemwa): “Haya ndiyo yale mliyoahidiwa kwa kila mwenye kurudia rudia kutubia mwenye kuhifadhi (ahadi ya Allaah سبحانه وتعالى).


مَّنْ خَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ وَجَاءَ بِقَلْبٍ مُّنِيبٍ﴿٣٣﴾
33. “Anayemuogopa Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah) kwa ghayb na akaja na moyo wa kurudia kutubia.”


ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ ۖ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُلُودِ﴿٣٤﴾
34. (Itasemwa): “Iingieni (Jannah) kwa salama.” Hiyo ndio siku yenye kudumu.


لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ﴿٣٥﴾
35. Watapata humo wayatakayo, na Kwetu kuna ziada (kumuona Allaah عز وجل).


وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هُمْ أَشَدُّ مِنْهُم بَطْشًا فَنَقَّبُوا فِي الْبِلَادِ هَلْ مِن مَّحِيصٍ﴿٣٦﴾
36. Na karne ngapi Tumeangamiza kabla yao ambao walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao. Basi walitangatanga sana katika nchi. Je, kuna mahali popote pa kukimbilia?


إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ﴿٣٧﴾
37. Hakika katika hayo, bila shaka ni ukumbusho (na zingatio) kwa aliyekuwa na moyo au akatega sikio naye ni mwenyewe awe hadhiri (kwa moyo wake).


وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ﴿٣٨﴾
38. Na kwa yakini Tumeumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, na wala Haukutugusa uchovu wowote.


فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ﴿٣٩﴾
39. Subiri juu ya yale wanayoyasema, na sabbih kwa Himidi za Rabb (Mola) wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.


وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ﴿٤٠﴾
40.  Na katika usiku Msabbih na baada ya kusujudu.


وَاسْتَمِعْ يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ﴿٤١﴾
41. Na sikiliza kwa makini Siku atakayonadi mwenye kunadi kutoka mahali pa karibu.


يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ﴿٤٢﴾
42. Siku watakayosikia ukelele (wa baragumu) kwa haki. Hiyo ndio Siku ya kutoka (makaburini).


إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَإِلَيْنَا الْمَصِيرُ﴿٤٣﴾
43. Hakika Sisi Tunahuisha na Tunafisha, na Kwetu ni mahali pa kuishia.


يَوْمَ تَشَقَّقُ الْأَرْضُ عَنْهُمْ سِرَاعًا ۚ ذَٰلِكَ حَشْرٌ عَلَيْنَا يَسِيرٌ﴿٤٤﴾
44. Siku itakayowararukia ardhi (watoke) haraka haraka. Huo ndio mkusanyo, Kwetu ni mepesi.


نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ ۖ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِجَبَّارٍ ۖ فَذَكِّرْ بِالْقُرْآنِ مَن يَخَافُ وَعِيدِ﴿٤٥﴾
45. Sisi Tunajua zaidi kwa yale wanayoyasema; na wala wewe si mwenye kuwakandamiza. Basi mkumbushe kwa Qur-aan anayekhofu onyo Langu.




Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com