Ash-Shuwraa: 42

الشُّورى
Ash-Shuwraa: 42

(Imeteremka Makka)


Hii ni Sura ya Makka, na idadi ya Aya zake ni 53, na imeitwa Ash-shuura, yaani "Kushauriana" kwa sababu inavyo waongoza Waumini waendeshe mambo ya jamii zao kwa kushauriana, ili ipatikane Haki, na uthibiti uadilifu. Na Sura hii imekusanya mambo mengi ya Dini na hoja za itikadi.
Imefungua Sura kwa kuisifu Qur'ani yenyewe kwa kuwa ni Wahyi (Ufunuo) ulio toka kwa Mwenyezi Mungu, ikayarudisha matusi ya makafiri, na ikashughulikia kumpoza Mtume s.a.w., na tena baada ya hayo ikaingilia kuthibitisha uweza wa Mwenyezi Mungu aliye iteremsha Qur'ani na ukatukuka utawala wake, na ikaeleza kukanya kwa baadhi ya watu juu ya kuwa hoja zake ziwazi zinazo onyesha kuwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kubainisha khitilafu zao katika kufahamu Haki. Na baada yake Sura hii ikatilia mkazo uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya kila kitu. Kisha ikathibitisha kuwa msingi wa sharia ni mmoja, na ikaashiria kuwa wapo wanao kufuru juu ya hivyo. Hali kadhaalika imeashiria kuwa Vitabu vyote vya mbinguni vinaongoza kwendea Haki. Na Sura imelaani shirki ya washirikina, na kukhitalifiana kwao katika Haki kwa udhalimu tu. Na pia imelaani kule kuhimiza kwao, wanao kadhibisha,  kuhimiza Kiyama kwa maskhara. Na ikatoa uwongozi kwa wafuasi wake wawalinganie watu kwenye Dini, kama ilivyo eleza ubora wa upole wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na Sura hii imehadharisha kuzama katika kuiwania dunia tu peke yake. Na ikabainisha uovu wa hali ya makafiri na wema wa hali ya Waumini katika Akhera. Na Sura ikawalaumu wale walio mkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. kwa kumwambia kaizua Qur'ani, hali wao wameshindwa hata kuleta Sura moja tu mfano wake. Kisha ikatangaza kuwa Mwenyezi Mungu ameikubali toba ya Waumini, na ikatangaza hikima ya kuzigawa riziki kwa watu kwa mpango wa hikima. Hawakuwa wote matajiri, kwa kuchelea wasipande jeuri, wala wasiwe wote mafakiri wakateketea. Bali amewakunjulia baadhi na amewadhikisha wengine.
Na akadhihirisha baraka za mvua, na dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kwa jambo hili, na kwamba masaibu ya dunia ni kwa sababu ya maasi. Kisha Subhanahu akakariri kwa njia nyingine hali za Waumini na wanao kadhibisha huko Akhera, na madhila yatayo wapata wanao kadhibisha. Na akataka wafanye haraka kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu kabla uhai haujakata fursa ya kutenda. Kadhaalika Sura imeshughulika kumpoza  Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. na kubainisha uweza wake Subhanahu kumtunukia amtakaye watoto wa kike, na wa kiume mwenginewe, na mchanganyiko kwa wa tatu, na kumnyima kabisa wa nne. Kisha Sura ikataja njia za Mwenyezi Mungu kusema na Manabii wake, na ikakhitimisha kwa kubainisha Njia ya Haki Iliyo Nyooka ambayo inayo pasa kuifuata.



بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيم

حم﴿١﴾
1. Haa Miym.


عسق﴿٢﴾
2. ‘Ayn Siyn Qaaaf.


كَذَٰلِكَ يُوحِي إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ اللَّـهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٣﴾
3. Hivyo ndivyo Anavyokufunulia Wahy na kwa wale walio kabla yako, Allaah Al-’Aziyzul-Hakiym (Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika – Mwenye hikmah wa yote).


لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ﴿٤﴾
4. Ni Vyake (Pekee) vilivyomo mbinguni na ardhini, Naye ni Al-‘Aliyyul –‘Adhwiym (Mwenye ‘Uluwa, Ametukuka - Mwenye Taadhima, Mkuu kabisa).


تَكَادُ السَّمَاوَاتُ يَتَفَطَّرْنَ مِن فَوْقِهِنَّ ۚ وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥﴾
5. Zinakaribia mbingu kuraruka kutoka juu yake, na Malaika wanasabbih kwa Himidi za Rabb (Mola) wao, na wanawaombea maghfirah walioko ardhini. Tanabahi! Hakika Allaah Ndiye Al-Ghafuwrur-Rahiym (Mwingi wa kughufuria - Mwenye kurehemu).


وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ اللَّـهُ حَفِيظٌ عَلَيْهِمْ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِوَكِيلٍ﴿٦﴾
6. Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi; Allaah ni Hafiydhw (Mhifadhi) wao, nawe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) si mdhamini wao.


وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِّتُنذِرَ أُمَّ الْقُرَىٰ وَمَنْ حَوْلَهَا وَتُنذِرَ يَوْمَ الْجَمْعِ لَا رَيْبَ فِيهِ ۚ فَرِيقٌ فِي الْجَنَّةِ وَفَرِيقٌ فِي السَّعِيرِ﴿٧﴾
7. Na hivyo ndivyo Tulivyokufunulia Wahy wa Qur-aan ya Kiarabu ili uonye mama wa miji (Makkah), na wale waliozunguka pembezoni mwake, na uonye Siku ya kujumuika isiyokuwa na shaka ndani yake. Kundi (litakuwa) katika Jannah, na kundi katika (Moto wa) As-Sa’iyr.”


وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَجَعَلَهُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلَـٰكِن يُدْخِلُ مَن يَشَاءُ فِي رَحْمَتِهِ ۚ وَالظَّالِمُونَ مَا لَهُم مِّن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ﴿٨﴾
8. Na lau Angelitaka Allaah Angeliwafanya ummah mmoja, lakini Anamuingiza Amtakaye katika Rahmah Yake. Na madhalimu hawana mlinzi yeyote wala mwenye kunusuru.


أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۖ فَاللَّـهُ هُوَ الْوَلِيُّ وَهُوَ يُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٩﴾
9. Je, wamejichukulia badala Yake walinzi, wasaidi? Basi Allaah Yeye Ndiye Al-Waliyy (Mlinzi, Msaidizi) Naye Ndiye Anayehuisha wafu, Naye Ndiye juu ya kila kitu ni Qadiyr (Muweza).


وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ﴿١٠﴾
10. Na katika lolote lile mlilokhitilafiana, basi hukumu yake ni kwa Allaah. Huyo Ndiye Allaah Rabb (Mola) wangu, Kwake nimetawakali na Kwake narudi kutubia.


فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾
11. Muanzilishi wa mbingu na ardhi. Amekujaalieni kutokana na nafsi zenu wenzi na katika wanyama wa mifugo wenzi. Anakusambazeni humo. Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye As-Samiy’ul-Baswiyr (Mwenye kusikia yote - Mwenye kuona yote).


لَهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٢﴾
12. Ni Zake (Pekee) funguo za mbingu na ardhi, Anamkunjulia riziki Amtakaye na Anadhikisha. Hakika Yeye kwa kila kitu ni ‘Aliym (Mjuzi).


شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ ۚ كَبُرَ عَلَى الْمُشْرِكِينَ مَا تَدْعُوهُمْ إِلَيْهِ ۚ اللَّـهُ يَجْتَبِي إِلَيْهِ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَن يُنِيبُ ﴿١٣﴾
13. “Amekuamuruni katika Dini yale Aliyomuusia kwayo Nuwh, na ambayo Tumekufunulia Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na Tuliyomuusia kwayo Ibraahiym, na Muwsaa na ‘Iysaa kwamba: “Simamisheni Dini na wala msifarikiane humo. Yamekuwa makubwa kwa washirikina yale unayowalingania. Allaah Anamteua Kwake Amtakaye, na Anamuongoza Kwake anayerudia rudia kutubia.


وَمَا تَفَرَّقُوا إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى لَّقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۚ وَإِنَّ الَّذِينَ أُورِثُوا الْكِتَابَ مِن بَعْدِهِمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ ﴿١٤﴾
14. Na hawakufarikiana isipokuwa baada ya kuwajia elimu kwa uhusuda baina yao. Na kama si neno lilotangulia (kuakhirisha adhabu) kutoka kwa Rabb (Mola) wako mpaka muda maalumu uliokadiriwa, bila shaka ingelikidhiwa baina yao. Na hakika wale waliorithishwa Kitabu baada yao bila shaka wamo katika shaka na wasiwasi nayo.



فَلِذَٰلِكَ فَادْعُ ۖ وَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ ۖ وَقُلْ آمَنتُ بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِن كِتَابٍ ۖ وَأُمِرْتُ لِأَعْدِلَ بَيْنَكُمُ ۖ اللَّـهُ رَبُّنَا وَرَبُّكُمْ ۖ لَنَا أَعْمَالُنَا وَلَكُمْ أَعْمَالُكُمْ ۖ لَا حُجَّةَ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ ۖ اللَّـهُ يَجْمَعُ بَيْنَنَا ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿١٥﴾
15. Basi kwa hiyo (Dini ya Allaah) walinganie (ee Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم, na thibitika imara kama ulivyoamrishwa, na wala usifuate hawaa zao. Na sema: “Nimeamini yale Aliyoyateremsha Allaah katika Kitaab (Qur-aan na vinginevyo) na nimeamrishwa niadilishe baina yenu. Allaah ni Rabb (Mola) wetu na Rabb wenu; sisi tuna ‘amali zetu, nanyi mna ‘amali zenu. Hakuna kubishana baina yetu na baina yenu; Allaah Atatujumuisha baina yetu, na Kwake ndio mahali pa kuishia.


وَالَّذِينَ يُحَاجُّونَ فِي اللَّـهِ مِن بَعْدِ مَا اسْتُجِيبَ لَهُ حُجَّتُهُمْ دَاحِضَةٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ وَلَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ﴿١٦﴾
16. Na wale wanaobishana kuhusu (Dini ya) Allaah baada ya kuitikiwa (wakasilmu watu) - hoja yao ni batilifu mbele ya Rabb (Mola) wao na juu yao iko ghadhabu (Yake) na watapata adhabu shadidi.


اللَّـهُ الَّذِي أَنزَلَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ وَالْمِيزَانَ ۗ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ قَرِيبٌ﴿١٧﴾
17. Allaah Ambaye Ameteremsha Kitabu (hiki) kwa haki na mizani. Na nini kitakachokujulisha pengine Saa (Qiyaamah) iko karibu?


يَسْتَعْجِلُ بِهَا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِهَا ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا مُشْفِقُونَ مِنْهَا وَيَعْلَمُونَ أَنَّهَا الْحَقُّ ۗ أَلَا إِنَّ الَّذِينَ يُمَارُونَ فِي السَّاعَةِ لَفِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ﴿١٨﴾
18. Wanaihimiza wale wasioiamini; na wale walioamini wanaiogopa na wanaitambua kwamba hiyo ni haki. Tanabahi!  Hakika wale wanaotilia shaka kuhusu Saa (Qiyaamah); bila shaka wamo katika upotofu wa mbali.


اللَّـهُ لَطِيفٌ بِعِبَادِهِ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ﴿١٩﴾
19. Allaah ni Latwiyfun (Latifu) kwa waja Wake, Anamruzuku Amtakaye, Naye Ndiye Al-Qawiyyul-‘Aziyz (Mwenye nguvu zote - Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika).


مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ﴿٢٠﴾
20. Yeyote yule aliyekuwa anataka (kwa ‘amali zake) mavuno ya Aakhirah Tunamzidishia katika mavuno yake; na yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya dunia, Tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote.


أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةُ الْفَصْلِ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٢١﴾
21. Je, wanao washirika waliowaamuru Dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea idhini? Na lau si neno la uamuzi (ulokwishapita), bila shaka ingelikidhiwa baina yao; na hakika madhalimu watapata adhabu iumizayo.


تَرَى الظَّالِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا كَسَبُوا وَهُوَ وَاقِعٌ بِهِمْ ۗ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فِي رَوْضَاتِ الْجَنَّاتِ ۖ لَهُم مَّا يَشَاءُونَ عِندَ رَبِّهِمْ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ﴿٢٢﴾
22. Utawaona madhalimu ni wenye kuogopa kwa yale waliyoyachuma, nao (adhabu ya Allaah) itawaangukia tu. Na wale walioamini na wakatenda mema (watakuwa) katika mabustani yaliyositawi ya Jannaat, watapata wayatakayo kwa Rabb (Mola) wao, hiyo ndio fadhila kubwa.


ذَٰلِكَ الَّذِي يُبَشِّرُ اللَّـهُ عِبَادَهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ ۗ قُل لَّا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلَّا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَىٰ ۗ وَمَن يَقْتَرِفْ حَسَنَةً نَّزِدْ لَهُ فِيهَا حُسْنًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ شَكُورٌ﴿٢٣﴾
23. Hayo ndiyo Aliyowabashiria Allaah waja Wake wale walioamini na wakatenda mema. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Sikuombeni ujira wowote juu yake (ujumbe wa Allaah) isipokuwa mapenzi kwa ajili ya ujamaa wa karibu.” Na yeyote yule anayechuma mazuri, Tutamzidishia humo zuri. Hakika Allaah ni Ghafuwrun-Shakuwr (Mwingi wa kughufuria - Mwingi wa kupokea shukurani).


أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا ۖ فَإِن يَشَإِ اللَّـهُ يَخْتِمْ عَلَىٰ قَلْبِكَ ۗ وَيَمْحُ اللَّـهُ الْبَاطِلَ وَيُحِقُّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿٢٤﴾
24. Je, wanasema: “Amemtungia Allaah uongo?” Basi Allaah Akitaka Atapiga mhuri juu ya moyo wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na Allaah Anaufuta ubatilifu, na Ataihakiki haki kwa maneno Yake. Hakika Yeye ni ‘Aliymun (Mjuzi) wa yaliyomo vifuani.


وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ وَيَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ﴿٢٥﴾
25. Naye Ndiye Ambaye Anapokea tawbah kutoka kwa waja Wake, na Anasamehe maovu, na Anayajua mnayoyafanya.


وَيَسْتَجِيبُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَيَزِيدُهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ وَالْكَافِرُونَ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ﴿٢٦﴾
26. Na Anawaitika (du’aa) wale walioamini na wakatenda mema, na Anawazidishia kutoka fadhila Zake. Na makafiri watapata adhabu kali.


وَلَوْ بَسَطَ اللَّـهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَـٰكِن يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَّا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ﴿٢٧﴾
27. Na lau kama Allaah Angelikunjua (mno) riziki kwa waja Wake, bila shaka wangefanya ufidhuli katika ardhi; lakini Anateremsha kwa kiasi Akitakacho. Hakika Yeye kwa waje Wake ni Khabiyrun-Baswiyr (Mjuzi wa yaliyodhahiri na yaliyofichikana - Mwenye kuona yote).


وَهُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ الْغَيْثَ مِن بَعْدِ مَا قَنَطُوا وَيَنشُرُ رَحْمَتَهُ ۚ وَهُوَ الْوَلِيُّ الْحَمِيدُ﴿٢٨﴾
28. Naye Ndiye Anayeteremsha mvua baada ya kuwa wamekata tamaa, na Anaeneza Rahmah Yake. Naye Ndiye Al-Waliyyul-Hamiyd (Mlinzi, Msaidizi - Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote).


وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَثَّ فِيهِمَا مِن دَابَّةٍ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ جَمْعِهِمْ إِذَا يَشَاءُ قَدِيرٌ﴿٢٩﴾
29. Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake; ni uumbaji wa mbingu na ardhi, na Aliowatawanya humo kati ya viumbe vinavyotembea, Naye kwa kuwakusanya Atakapo ni Qadiyr (Muweza).


وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ﴿٣٠﴾
30. Na haukusibuni katika msiba wowote basi ni kwa sababu ya yale yaliyochuma mikono yenu, na Anasamehe mengi.


وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ ۖ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ﴿٣١﴾
31. Nanyi si wenye kushinda kuepuka (adhabu ya Allaah) ardhini, na wala hamna badala Yake mlinzi yeyote na wala mwenye kunusuru.


وَمِنْ آيَاتِهِ الْجَوَارِ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ﴿٣٢﴾
32. Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni merikebu zinazotembea baharini kama milima.


إِن يَشَأْ يُسْكِنِ الرِّيحَ فَيَظْلَلْنَ رَوَاكِدَ عَلَىٰ ظَهْرِهِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ﴿٣٣﴾
33. Akitaka Anautuliza upepo mkali (ili merikebu) zisimame tutwe juu ya mgongo wake (wa bahari). Hakika pana katika hayo Aayaat (zingatio, ishara) kwa kila mwenye kusubiri, mwenye kushukuru.


أَوْ يُوبِقْهُنَّ بِمَا كَسَبُوا وَيَعْفُ عَن كَثِيرٍ﴿٣٤﴾
34. Au Aziangamize kwa sababu ya (maovu) waliyoyachuma, na Anasamehe mengi.


وَيَعْلَمَ الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِنَا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ﴿٣٥﴾
35. Na watajua wale wanaobishana kuhusu Aayaat, (ishara, dalili) Zetu; kwamba hawana mahali popote pa kukimbilia.


فَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٣٦﴾
36. Basi chochote mlichopewa katika kitu ni starehe ndogo za uhai wa dunia.  Na yale yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi na ni ya kudumu kwa wale walioamini na kwa Rabb (Mola) wao wanatawakali.


وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ﴿٣٧﴾
37. Na wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu na wanapoghadhibika wao wanasamehe.


وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣٨﴾
38. Na wale waliomuitikia Rabb (Mola) wao, wakasimamisha Swalaah, na jambo lao hushauriana baina yao, na kutokana na vile Tulivyowaruzuku wanatoa.


وَالَّذِينَ إِذَا أَصَابَهُمُ الْبَغْيُ هُمْ يَنتَصِرُونَ﴿٣٩﴾
39. Na wale inapowasibu ukandamizaji, wao wanajitetea.


وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ﴿٤٠﴾
40. Na jazaa ya uovu ni uovu mfano wake. Lakini atakayesamehe na akasuluhisha, basi ujira wake uko kwa Allaah, hakika Yeye Hapendi madhalimu.


وَلَمَنِ انتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَـٰئِكَ مَا عَلَيْهِم مِّن سَبِيلٍ﴿٤١﴾
41. Na bila shaka anayelipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, basi hao hawana sababu (ya kulaumiwa).


إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٤٢﴾
42. Hakika sababu (ya kulaumiwa) ni juu ya wale wanaodhulumu watu na wanakandamiza katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iumizayo.


وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ﴿٤٣﴾
43. Na atakayevuta subira na akasamehe, hakika hilo bila shaka ni katika mambo ya kuazimiwa.


وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن وَلِيٍّ مِّن بَعْدِهِ ۗ وَتَرَى الظَّالِمِينَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ يَقُولُونَ هَلْ إِلَىٰ مَرَدٍّ مِّن سَبِيلٍ﴿٤٤﴾
44. Na aliyepotolewa na Allaah basi hatopata mlinzi baada Yake. Na utawaona madhalimu watakapoiona adhabu, wakisema: “Je, ipo njia yoyote ya kurudi (duniani)?”


وَتَرَاهُمْ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا خَاشِعِينَ مِنَ الذُّلِّ يَنظُرُونَ مِن طَرْفٍ خَفِيٍّ ۗ وَقَالَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا إِنَّ الظَّالِمِينَ فِي عَذَابٍ مُّقِيمٍ﴿٤٥﴾
45. Na utawaona wanahudhurishwa (kwenye Moto) wakiwa wanyenyekevu kutokana na udhalilifu, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na watasema wale walioamini: “Hakika wenye kukhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na ahli zao Siku ya Qiyaamah. Tanabahi!  Hakika madhalimu wamo katika adhabu ya kudumu.


وَمَا كَانَ لَهُم مِّنْ أَوْلِيَاءَ يَنصُرُونَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن سَبِيلٍ﴿٤٦﴾
46. Na wala hawatokuwa na walinzi wowote wa kuwanusuru badala ya Allaah. Na ambaye Allaah Amempotoa basi hatopata njia (ya kuongoka).


اسْتَجِيبُوا لِرَبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّـهِ ۚ مَا لَكُم مِّن مَّلْجَإٍ يَوْمَئِذٍ وَمَا لَكُم مِّن نَّكِيرٍ﴿٤٧﴾
47. Muitikieni Rabb (Mola) wenu kabla haijafika Siku isiyo rudishwa nyuma kutoka kwa Allaah. Hamtokuwa na mahali popote pa kukimbilia Siku hiyo na wala hamtopata kupinza (maovu).


فَإِنْ أَعْرَضُوا فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ۖ إِنْ عَلَيْكَ إِلَّا الْبَلَاغُ ۗ وَإِنَّا إِذَا أَذَقْنَا الْإِنسَانَ مِنَّا رَحْمَةً فَرِحَ بِهَا ۖ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ فَإِنَّ الْإِنسَانَ كَفُورٌ﴿٤٨﴾
48. Wakikengeuka, basi Hatukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uwe mlinzi wao. Si juu yako isipokuwa ubalighisho (wa ujumbe). Na hakika Sisi Tunapomwonjesha insani Rahmah kutoka Kwetu, huifurahia. Na linapowasibu ovu kwa sababu ya yaliyotanguliza mikono yao, basi hakika insani ni mwingi wa kukufuru.


لِّلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ يَهَبُ لِمَن يَشَاءُ إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَن يَشَاءُ الذُّكُورَ﴿٤٩﴾
49. Ni wa Allaah Pekee ufalme wa mbingu na ardhi. Anaumba Atakavyo. Humtunukia Amtakaye wana wa kike, na Humtunukia Amtakaye wana wa kiume.


أَوْ يُزَوِّجُهُمْ ذُكْرَانًا وَإِنَاثًا ۖ وَيَجْعَلُ مَن يَشَاءُ عَقِيمًا ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ قَدِيرٌ﴿٥٠﴾
50. Au Huwachanganya (wana wa) kiume na (wana wa) kike, na Humjaalia Amtakaye kuwa ni tasa, hakika Yeye ni ‘Aliymun-Qadiyr (Mjuzi wa yote – Muweza wa yote).


وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ﴿٥١﴾
51. Na wala haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Allaah Amsemeze isipokuwa kwa (njia ya) Wahy au kutoka nyuma ya kizuizi, au Hutuma Mjumbe, kisha Anamfunulia Wahy kwa idhini Yake Ayatakayo; hakika Yeye ni ‘Aliyyun-Hakiym (Mwenye ‘Uluwa, Ametukuka - Mwenye hikmah wa yote).


وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا ۚ مَا كُنتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلَا الْإِيمَانُ وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴿٥٢﴾
52. Na hivyo ndivyo Tulivyokuletea Ruwh (Qur-aan) kutoka amri Yetu. Hukuwa unajua nini Kitabu wala iymaan, lakini Tumeifanya ni Nuru, Tunaongoa kwayo Tumtakaye miongoni mwa waja Wetu. Na hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka.


صِرَاطِ اللَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِلَى اللَّـهِ تَصِيرُ الْأُمُورُ﴿٥٣﴾
53. Njia ya Allaah Ambaye ni Vyake Pekee vyote vilivyomo mbinguni na vyote vilivyomo ardhini. Tanabahi! Kwa Allaah Pekee yanaishia mambo (yote).




Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com