Salamah bin Qays Al-Ashjaiy - Alieifungua Kurdistan

 Salamah bin Qays Al-Ashjaiy - Alieifungua Kurdistan


Alipitisha Al-farouq usiku wake akiwa macho akikagua vichochoro vya Madina ili watu walale wakiwa katika hali ya amani na salama. Ilikuwa wakati wa doria yake baina ya majumba na masoko akihesabu akilini mwake watu wa kheri na muruwa na mashujaa miongoni mwa masahaba wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam); ili mmoja wao ampe bendera kuongoza kikosi cha kwenda kufungua mji wa Al-Ahwazi.
Haukupita muda na akasema: “Nimempata naam. Nimempata Inshaallah”.  Asubuhi ilipochomoza akamwita Salamah bin Qays Al-Ashaja’iy akamwambia; “Mimi ninakukabidhi uongozi wa kikosi kinachoelekea Al-Ahwazi. Nenda kwa jina la Allah na pigana kwenye njia ya Allah kwa kila aliemkufuru Allah. Na mkikutana na adui wenu katika washirikina, basi walinganieni Uislamu. Wakisilimu na kuamua kubakia katika miji yao na wala wasishiriki nanyi kumpiga vita yeyote yule, na hawana jukumu ila kutoa zake, na wala wasipewe chochote katika ngawira. Ama wakiamua kushiriki nanyi watashiriki mfano wenu. Ama wakipinga kuingia katika Uislamu basi walinganieni kutoa jizya na waacheni na mambo yao na muwalinde dhidi ya maadui wao na wala usiwakalifishe juu ya nguvu zao. Ama wakipinga hapo wapigeni vita na hakika Allah ni mwenye kukunusuruni. Ama wakijiimarisha kwenye ngome halafu wakataka kwenu mufuate hukumu ya Allah na Mtume wake basi hilo msilikubali kwani hamjui ni ipi hukumu ya Allah na Mtume wake. Ama wakitaka wateremshwe kwenye dhima ya Allah na Mtume wake, basi wapeni dhima yenu nyinyi.  Mkienda kupigana msifanye israfu (msichupe mipaka) wala msifanye khiyana, wala msichinjechinje kwa kukata viungo na wala msiuwe watoto".
Akasema Salamah; “Tunasikia na kutii ewe Amiirul Muuminina"
Amiirul  Muuminina akamuaga kwa hamasa  na kuushika kwa nguvu mkono wake na kumuaga kwa du’aa. Alikuwa anatambua Khalifa uzito wa jukumu alilojibebesha na kubebesha jeshi lake kwani mji wa Al-Ahwazi ulikuwa ni mji wa milima, wenye njia ngumu na una ngome imara uliopo baina ya Basra na milima ya Fursi (Persia)
Wakaazi wake walikuwa ni wakurdi, watu wa vita na ilikuwa hakuna budi kwa Waislamu ila kuukomboa ili wajizuilie na mashambulizi ya wafursi dhidi ya mji wa Basra na kuwazuilia kuufanya kambi ya askari wao, na ikawa Iraq katika hatari daima.
Alitoka Salamah bin Qays akiongoza jeshi la ufunguzi katika Al-Ahwazi lakini muda mfupi tu baadae walianza kupambana na maumbile magumu ya ardhi hiyo. Kikosi kikaanza kupata shida ya kupanda na kushuka majabali marefu na kupita kwenye mwitu wake mnene na kupambana na nyoka wake na nge wenye sumu, katika hali ya kulala au kuwa macho. Lakini roho ya Salamah iliyojawa imani na mapenzi ilikuwa ni yenye kupepea kwa mbawa zake askari wake. Hakika shida ni laini na huzuni ni nyepesi.
Alikuwa mara kwa mara akiwaliwaza kwa mawaidha yaliyozitikisa nyoyo zao, na akawachombeza usiku wao kwa raha na ladha ya Qur’aan. Wakawa wamegubikwa kwa nuru yake wakimsabihi Allah na kuanza kusahau shida zilizowafika. Salamah alitekeleza wasia wa Amiirul Muuminina.
Na alipokutana tu na watu wa Al-Ahwazi alianza kuwalingania kuingia katika Uislamu lakini walipinga na kukataa. Akawalingania kutoa jizya pia walipinga na kufanya kiburi na hapakuwa na chaguo ila panga kugongana.
Wakapigana mujahidina katika njia ya Allah wakitamani kwake malipo yaliyo mazuri vita vikapamba moto, na makundi mawili yakakutana kila mmoja kwa ushujaa na nguvu zake hali ambayo haikupata kuonekana ila katika vita vichache tu.
Vita vikaendelea vikiashiria ushindi mkubwa wa jeshi la mujahidina waumini wenye kunyanyua neno la Allah, na kushindwa kubaya kwa washirikina maadui wa Allah. Vita vilipomalizika Salamah bin Qays alianza kugawa ngawira baina ya askari wake. Akakutia miongoni mwa ngawira hizo mapambo mazuri sana akawaambia Mujahidina: “Je zitaridhika nafsi zenu kama tutampelekea haya Amiirul Muuminina?” Wakasema; “Ndio.” Akayatia mapambo hayo ndani ya kisanduku na akamtuma mtu katika watu wake wa Bani al ashja’iy na kumwambia; “Nendeni wewe na kijana wako Madina na mumbashirie Amiirul Muuminina ushindi na umkabidhi mzigo (mapambo haya)”.
Ilikuwa baina ya mtu huyu na Amiirul  Muuminina habari yenye mazingatio na mawaidha.  Hebu na tumwambie huyu mtu atusimulie habari hiyo yeye mwenyewe. Anasema kijana huyu wa kiashja’iy:
“Nilitoka mimi na kijana wangu mpaka Basra na kununua farasi wawili kwa gharama alizotupa Salamah bin Qays na tukawabebeshea mizigo yetu ya safari. Tukatoka baada ya hapo kuelekea Madina, tulipofika na kuanza kumtafuta Amiirul Muuminina tulimkuta amesimama akiwagaia chakula Waislamu  na huku  ameegemea bakora yake mfano wa mchungaji, alikuwa akizungukia sinia akisema; “Ewe Yarfaa waongeze hawa nyama. Ewe Yarfaa waongeze hawa mkate. Ewe Yarfaa waongeze hawa mchuzi” Nilipokaribiana nae akasema; "Kaa kitako" Nikakaa mwisho walipo watu, akanisogezea chakula nikala.
Baada ya watu kumaliza kula alisema; “Ewe Yarfaa ondosha sinia". Kisha akaondoka nami nikamfuata alipoingia nyumbani kwake niliomba ruhusa kuingia. Alikuwa amekaa kwenye busati ameegemea mito miwili ya ngozi iliyojazwa majani ya mtende (makuti), akanisogezea mmoja nikakalia, nyuma yake palikuwa na paziya, na aliita kupitia kwenye pazia; “Ewe Ummu kulthum tuletee chakula chetu” Nikasema ndani ya nafsi yangu; “Pengine ni chakula cha Amiirul Muuminina alichowekewa maalum kwa ajili yake. Pakaletwa mkate na mafuta na vidonge vya chumvi bado havijasagwa. Akanielekea akasema; "Kula". Nikala kidogo nae  pia akala.
Sijapata kumuona mtu bora katika kula kama yeye. Baadae akasema; "lete kinywaji". Kikaletwa kinywaji kilichotengenezwa kwa ngano (sha’iyr) Akasema; "mpe huyu mtu mgeni kwanza" Nikachukua bilauli nikanywa kidogo na kilikuwa ni kinywaji kizuri kitamu. Akachukuwa yeye na kunywa mpaka akatosheka na halafu akasema; "Ninamshukuru Allah alietulisha tukashiba na kutunywesha na kukata kiu zetu"
Tukazungumza baada ya hapo na kumuambia kuhusu ujumbe wake “Ewe Amiirul Muuminina nina ujumbe wako”
Akasema; “kutoka wapi?”
Nikasema; “Kutoka kwa Salamah bin Qays”
Akasema; “Karibu Salamah bin Qays karibu mjumbe wa Salamah bin Qays”
“Hebu nisimulie habari za jeshi la Waislamu”
 Nikamwambia; “Kama unavyopenda ewe Amiirul Muuminina kheri na ushindi dhidi ya adui wako na maadui wa Allah”
Nikampa habari njema ya ushindi kwa ukamilifu akasema “Alhamdulillah aliyetoa na kufadhilisha na akaneemesha na kuzidisha.”
Akasema; "Ulipita Basra?"
Nikasema; "Ndiyo ewe Amiirul Muuminina"
Akasema; “Vipi hali ya Waislamu huko?”
Nikamwambia; “nzuri"
Akasema “Vipi bei za bidhaa?”
Nikamwambia; “Bei zao ni rahisi sana” 
Akasema;  “Vipi nyama? Kwani nyama ni chakula cha msingi kwa waarabu na bila hicho maisha hayawi”
Nikasema; “Imejaa tele”.
Mara akakitazama kile kisanduku nilichokuja nacho akasema; “Ni kitu gani hicho mkononi mwako?”
Nikamwambia; “Allah alipotupa ushindi dhidi ya adui yetu tulikusanya ngawira nyingi, Salamah bin Qays akakutia mapambo mazuri akawaambia askari wake hakika mapambo haya yakigaiwa kwenu hayatatosheleza jee itawafurahisha ikiwa nitampelekea Amiirul Muuminina? Nao wakasema “Ndio"
Hapo nikamkabidhi kisanduku alipokifungua na kuona vilivyomo.  Yalikuwa mapambo rangi mbali mbali nyekundu, kijani, manjano. Alisimama ghafla pale alipokaa na kukirembea kisanduku na kutawanyika vilivyomo ardhini kuliani na kushotoni mwake. Wanawake waliopo walichungulia mapaziani wakidhani labda anataka kumdhuru na akaniambia; “Viokote! Vikusanye!”
Akamwambia kijana wake Yarfaa; ‘”Mtie adabu kali huyo”   Huku nikiwa nakusanya mabaki ya mapambo na huku ananipiga akaniambia; "Wewe na rafiki yako nyote sio watu wema"
Nikamuomba aniruhusu niondoke mimi na kijana wangu na tuelekee Al Ahwazi kwani farasi wangu amechukuliwa na Yarfaa akasema; “Yarfaa wape farasi katika farasi wa sadaka yeye na kijana wake” Kisha akamwambia; “Mkimaliza shughuli zenu juu ya wanyama hao basi wapeni wale ambao mtaona ni wahitaji zaidi” Nikasema; “Nitafanya hivyo ewe Amiirul Muuminina” Akanielekea na kusema; “Wallahi ikiwa askari wataondoka na kutawanyika na hamjawagawia mapambo haya basi wewe na mwenzio nyote mtapata adhabu kali”
Nikaondoka hapo haraka haraka mpaka kwa Salamah bin Qays. Nikamwambia; “Haikuwa njema kazi uliyonituma hivyo haraka haraka yagawe mapambo haya kabla msiba haujatufika mimi na wewe".
Nikamueleza habari yote, na hakuondoka Salamah kwenye majlis yake ila baada ya kuyagawa yale mapambo yote.