Waliwahi
kusema wema waliotutangulia – Salafun Saalih – kwamba: “Ikiwa
Allah Subhaanahu Wata’ala anamtakia kheri mja wake basi humfungulia mlango wa
vitendo na humfungia mlango wa mijadala na mabishano. Hivyo kila ukimuona
muislamu anaeitekeleza dini yake kivitendo na kutekeleza sunnah za Mtume Salla
Allahu ‘Alayhi Wasallam basi ujue hiyo ni moja katika alama za kheri”.
Tatizo
la umma wetu wa leo kubwa ni utekelezaji. Tunaweza kubahatika kupata maarifa ya
dini yetu lakini yakabaki kwenye bongo zetu kama nadharia tu – theory lakini
hakuna vitendo au kuyatekeleza hata yale kidogo tuliyojaaliwa kuyapata.
Tuangalie
mfano mizuri walituachia masahaba katika kutekeleza kwa vitendo yale
waliyobahatika kujifunza kutoka kwa mwalimu wetu, kigezo chetu na ruwaza njema,
al habib Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kama ilivyopokelewa kwamba:
أُمّ
حبيبة رضي الله عنها أنها قالت: قال النبي صلى الله عليه وسلم : ((من صلّى لله في
يوم وليلة ثنتي عشر ركعة تطوّعاً غير الفريضة إلا بُني له بهنّ بيتٌ في الجنة))
أخرجه أحمد وابن ماجة
Ummul Muuminiyn, Ummu Habibah, Allah amuwie radhi, alisema:
Amesema Mtume: Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam:
“Mwenye kusali katika siku moja na usiku wake rakaa kumi na mbili za
sunnah zisizokuwa za fardhi basi hujengewa kwa ajili yake nyumba peponi”.
Ahmad na ibnu Majah
Anasema
Ummu Habibah, Allah amuwie radhi, ambae alikuwa mke wa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam: “Sikuziwacha tena
tokea siku nilipomsikia Mtume Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam. Anasema Anbasa ambae aliipokea hadithi hii kutoka kwa Ummu Habibah:
“Nami sikuziwacha hata siku moja tokea siku nilipomsikia Ummu Habibah”. Anasema
Annu’umaan bin Salim, ambae aliipokea hadithi hii kutoka kwa Anbasa: “Hata na
mimi sikuziwacha tena tokea siku nilipomsikia Anbasa.”
Huu ndio mfano unaoonesha utekelezaji baada ya kujifunza jambo
lolote la dini.
Tusitosheke nalo tu kwamba tayari tumeshalijua bali likiwa jambo
hilo linahitaji utekelezaji basi tokea wakati huo tutakuwa na dhimma la
kulifanyia kazi na kulitenda kama walivyotuwekea kigezo masahaba, taabiina na
wema waliotutangulia inshaAllah.
Aliwahi kunukuliwa Abdullah ibn Mas’ud, Allah amuwie radhi,
akisema:
“Elimu ya kweli si ile iliyohifadhiwa kisha kunukuliwa tu bali elimu
ya kweli ni ile itakayodhihirishwa kwa kuwepo taqwa (kumuogopa Allah). Jifunze
na kisha tekeleza kwa vitendo yale uliyobahatika kujifunza”