15. SURATUL HIJR

الْحِجْر

15. SURATUL HIJR

(Imeteremka Makka)


Suratul Hijr ni Sura ya Makka. Nayo ina Aya 99. Imeanza kwa harufi za kutamkwa zenye kueleza kwamba Qur'ani imejengeka kwa harufi hizi hizi mnazo zitumia katika maneno yenu, na juu ya hivyo ni Muujiza kwenu, hamwezi kuleta kama hii. Kwani aliye iteremsha ni Mwenyezi Mungu, Aliye takasaika, na Akatukuka. Na hizo harufi pia ni kama kuwazindua wale wanao ipuuza Qur'ani, inawalingania, inawaita, waisikilize. Asaa wakanufaika, na wakahidika kumfuata Mwenyezi Mungu.
Sura hii tukufu inabainisha ili watu wazingatie yaliyo wapata kaumu zilizo tangulia, na khabari za  Manabii walio kwisha pita, na yaliyo wapata kutokana na watu wao. Na pia Sura hii inaonyesha ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu, katika mbingu zilizo nyanyuliwa na zenye sayari ziilizo hifadhiwa, na ardhi iliyo tandikwa, na kukunjuliwa, na milima iliyo simama imara, na pepo zenye kubeba maji, na zenye kupandishia miti. Na Sura hii pia inaashiria mpambano wa mwanzo katika maumbile ya asli baina ya maluuni Iblisi na Adam na mkewe, na kuendelea mpambano huo baina ya kheri na shari mpaka imalizike dunia. Kisha tena malipo ya shari Siku ya Kiyama, na malipo ya kheri. Na baada ya hayo Mwenyezi Mungu anasimulia visa vya Manabii wawili, Ibrahim na Luut'i, na watu wa Al Hijr. Na Sura inaeleza cheo cha Qur'ani, na hali ya washirikina katika kuipokea, na impasavyo Nabii kwa mnasaba wa ukafiri wao, navyo ni kufikisha ujumbe wake, na kuutangaza, na kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka ifike amri ya yakini.
 



بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرّحِيمِ

الر ۚ تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ وَقُرْآنٍ مُّبِينٍ ﴿١﴾
1. Alif Laam Raa. Hizo ni Aayaat za Kitabu na Qur-aan iliyo bayana.


رُّبَمَا يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ كَانُوا مُسْلِمِينَ ﴿٢﴾
2. Huenda wakatamani wale waliokufuru lau wangelikuwa Waislamu.


ذَرْهُمْ يَأْكُلُوا وَيَتَمَتَّعُوا وَيُلْهِهِمُ الْأَمَلُ ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٣﴾
3. Waache walena wastarehe na iwaghilibu tumaini (la uongo) basi watakuja kujua.


وَمَا أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ إِلَّا وَلَهَا كِتَابٌ مَّعْلُومٌ ﴿٤﴾
4. Na Hatukuangamiza mji wowote isipokuwa ulikuwa na majaaliwa maalumu.


مَّا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ ﴿٥﴾
5. Ummah wowote (ule) hauwezi kuitangulia muda wake na wala hauwezi kuakhirisha.


وَقَالُوا يَا أَيُّهَا الَّذِي نُزِّلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ إِنَّكَ لَمَجْنُونٌ ﴿٦﴾
6. Na wakasema: “Ee ambaye umeteremshiwa Adh-Dhikru (Qur-aan)! Hakika wewe bila shaka ni majnuni.”


لَّوْ مَا تَأْتِينَا بِالْمَلَائِكَةِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٧﴾
7. “Kwa nini usituletee Malaika ukiwa ni miongoni mwa wakweli?”


مَا نُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ إِلَّا بِالْحَقِّ وَمَا كَانُوا إِذًا مُّنظَرِينَ ﴿٨﴾
8. (Allaah Anawaambia): “Hatuteremshi Malaika isipokuwa kwa haki (kuwaadhibu makafiri) na hawakuwa wenye kupewa muhula.”


إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾
9. Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Tutakaoihifadhi (isibadilishwe kwa vyovyote).


وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ فِي شِيَعِ الْأَوَّلِينَ ﴿١٠﴾
10. Na kwa yakini Tulipeleka (Rasuli) kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika makundi ya awali.


وَمَا يَأْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿١١﴾
11. Na hakuwafikia Rasuli yeyote ila walikuwa wakiwafanyia istihzai.


كَذَٰلِكَ نَسْلُكُهُ فِي قُلُوبِ الْمُجْرِمِينَ ﴿١٢﴾
12. Hivyo ndivyo Tunavyoingiza (kufru) katika nyoyo za wahalifu.


لَا يُؤْمِنُونَ بِهِ ۖ وَقَدْ خَلَتْ سُنَّةُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣﴾
13. Hawaiamini hii (Qur-aan) na hali imekwishapita desturi ya (kuangamzia makafiri wa) awali.


وَلَوْ فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا مِّنَ السَّمَاءِ فَظَلُّوا فِيهِ يَعْرُجُونَ ﴿١٤﴾
14. Na hata kama Tungeliwafungulia mlango wa mbingu (hao makafiri) wakabakia kupanda huko (kutwa).


لَقَالُوا إِنَّمَا سُكِّرَتْ أَبْصَارُنَا بَلْ نَحْنُ قَوْمٌ مَّسْحُورُونَ ﴿١٥﴾
15. Bila shaka wangelisema: “Hakika macho yetu yamelevywa, bali sisi ni watu tumefanyiwa sihiri.”


وَلَقَدْ جَعَلْنَا فِي السَّمَاءِ بُرُوجًا وَزَيَّنَّاهَا لِلنَّاظِرِينَ﴿١٦﴾
16. Na kwa yakini Tumejaalia katika mbingu nyota zilizo kubwa na Tumezipamba kwa wenye kutazama.


وَحَفِظْنَاهَا مِن كُلِّ شَيْطَانٍ رَّجِيمٍ﴿١٧﴾
17. Na Tukazihifadhi na kila shaytwaan aliyefukuzwa mbali (na Rahmah ya Allaah).


إِلَّا مَنِ اسْتَرَقَ السَّمْعَ فَأَتْبَعَهُ شِهَابٌ مُّبِينٌ﴿١٨﴾
18. Isipokuwa (shaytwaan) anayesikiliza kwa wizi, basi humfuatia kimondo bayana.


وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْزُونٍ﴿١٩﴾
19. Na ardhi Tumeitandaza na Tukatupa humo milima iliyosimama thabiti, na Tukaotesha humo kila kitu (wanachohitaji viumbe) kwa uwiano.


وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَايِشَ وَمَن لَّسْتُمْ لَهُ بِرَازِقِينَ﴿٢٠﴾
20. Na Tukakujaalieni humo (vitu) kuendesha maisha (yenu), nanyi si wenye kuruzuku.


وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا عِندَنَا خَزَائِنُهُ وَمَا نُنَزِّلُهُ إِلَّا بِقَدَرٍ مَّعْلُومٍ﴿٢١﴾
21. Na hakuna kitu chochote (kile) isipokuwa Tuna hazina zake, na Hatukiteremshi isipokuwa kwa kadiri maalumu.


وَأَرْسَلْنَا الرِّيَاحَ لَوَاقِحَ فَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَسْقَيْنَاكُمُوهُ وَمَا أَنتُمْ لَهُ بِخَازِنِينَ﴿٢٢﴾
22. Na Tukatuma pepo (za Rahmah) zikibeba umande na Tukateremsha kutoka mbinguni maji na Tukakunywesheni kwayo; nanyi si wenye kuyaweka hazina (kuwapa na kuzuia muwatakao).


وَإِنَّا لَنَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَنَحْنُ الْوَارِثُونَ﴿٢٣﴾
23. Na hakika Sisi Tunahuisha na Tunafisha; na Sisi ni wenye kurithi.


وَلَقَدْ عَلِمْنَا الْمُسْتَقْدِمِينَ مِنكُمْ وَلَقَدْ عَلِمْنَا الْمُسْتَأْخِرِينَ﴿٢٤﴾
24. Na Tumekwishajua (ummah) waliotangulia miongoni mwenu, na Tumekwishajua wenye kutaakhari (wajao baadaye).


وَإِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَحْشُرُهُمْ ۚ إِنَّهُ حَكِيمٌ عَلِيمٌ﴿٢٥﴾
25. Na hakika Rabb (Mola) wako Ndiye Atakayewakusanya. Na hakika Yeye ni Hakiymun-‘Aliym (Mwenye hikmah wa yote - Mjuzi wa yote).


وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٢٦﴾
26. Na kwa yakini Tumemuumba insani kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari (iliyofinyangwa).


وَالْجَانَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ﴿٢٧﴾
27. Na majini Tuliwaumba kabla kutokana na moto ulio mkali mno.


وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِّن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٢٨﴾
28. Na (taja ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Rabb (Mola) wako Alipowaambia Malaika: “Hakika Mimi Namuumba mtu (Aadam) kutokana na udongo mkavu unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari.


فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ﴿٢٩﴾
29. Basi Nitakapomsawazisha na Nikampuliza Roho Niliyomuumbia; basi muangukieni kumsujudia.


فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ﴿٣٠﴾
30. Basi wakasujudu Malaika wote pamoja.


إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ أَن يَكُونَ مَعَ السَّاجِدِينَ﴿٣١﴾
31. Isipokuwa Ibliys alikataa kuwa pamoja na waliosujudu.


قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا لَكَ أَلَّا تَكُونَ مَعَ السَّاجِدِينَ﴿٣٢﴾
32. (Allaah) Akasema (kumuuliza): “Ee Ibliys! Una nini hata hukuwa pamoja na waliosujudu?”


قَالَ لَمْ أَكُن لِّأَسْجُدَ لِبَشَرٍ خَلَقْتَهُ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٣٣﴾
33. (Ibliys) Akasema: “Haiwi mimi nimsujudie mtu Uliyemuumba kutokana na udongo mkavu unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari.”


قَالَ فَاخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ﴿٣٤﴾
34. (Allaah) Akasema: “Basi toka humo, kwani hakika wewe umefukuzwa (mbali na Rahmah ya Allaah).


وَإِنَّ عَلَيْكَ اللَّعْنَةَ إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ﴿٣٥﴾
35. “Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.”


قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴿٣٦﴾
36. (Ibliys) Akasema: “Rabb (Mola) wangu! Nipe muhula mpaka Siku watakayofufuliwa.”


قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ﴿٣٧﴾
37. (Allaah) Akasema: “Basi hakika wewe ni miongoni mwa waliopewa muhula.”


إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ﴿٣٨﴾
38. “Mpaka siku ya wakati maalumu.”



قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٣٩﴾
39. (Ibliys) Akasema: “Rabb (Mola) wangu! Kwa vile Umenihukumia kupotoka basi bila shaka nitawapambia (maasi viumbe Vyako) katika ardhi na nitawapotoa wote.”


إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ﴿٤٠﴾
40. “Isipokuwa (wale) waja Wako miongoni mwao waliochaguliwa.


قَالَ هَـٰذَا صِرَاطٌ عَلَيَّ مُسْتَقِيمٌ﴿٤١﴾
41. (Allaah) Akasema: “Hii ni njia iliyonyooka (ya kurejea) Kwangu.”


إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ إِلَّا مَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْغَاوِينَ﴿٤٢﴾
42. “Hakika waja wangu huna mamlaka nao isipokuwa (yule) atakayekufuata miongoni mwa wapotofu.”


وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمَوْعِدُهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٤٣﴾
43. “Na hakika (Moto wa) Jahannam ni miadi yao wote pamoja.”


لَهَا سَبْعَةُ أَبْوَابٍ لِّكُلِّ بَابٍ مِّنْهُمْ جُزْءٌ مَّقْسُومٌ﴿٤٤﴾
44. “Una milango saba, na kwa kila mlango iko sehemu (khasa) iliyogawanywa.”


إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿٤٥﴾
45. Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu.


ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ آمِنِينَ﴿٤٦﴾
46. (Wataambiwa): “Ingieni humo kwa salama mkiwa katika amani.


وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ إِخْوَانًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ﴿٤٧﴾
47. “Na Tutaondosha katika vifua vyao, mifundo (ya chuki, uhasidi, kinyongo; watakuwa) ndugu (wanaopendana) katika makochi yaliyoinuliwa juu wakikabiliana.


لَا يَمَسُّهُمْ فِيهَا نَصَبٌ وَمَا هُم مِّنْهَا بِمُخْرَجِينَ﴿٤٨﴾
48. “Haitowagusa humo machofu nao humo hawatotolewa.”


نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٤٩﴾
49. (Ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Wajulishe waja Wangu, kwamba: Hakika Mimi ni Al-Ghafuwrur-Rahiym (Mwingi wa kughufuria - Mwenye kurehemu).


وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ﴿٥٠﴾
50. Na kwamba Adhabu Yangu, ndiyo adhabu iumizayo.


وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ﴿٥١﴾
51. Na wajulishe kuhusu wageni wa Ibraahiym (Malaika).


إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ﴿٥٢﴾
52. (Pale) Walipoingia kwake, wakasema: “Salaam!” (Amani!). (Ibraahiym) Akasema: “Hakika sisi tunakuogopeni.”


قَالُوا لَا تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ﴿٥٣﴾
53. (Malaika) Wakasema: “Usiogope! Hakika sisi tunakubashiria ghulamu mjuzi.”


قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِي عَلَىٰ أَن مَّسَّنِيَ الْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ﴿٥٤﴾
54. (Ibraahiym) Akasema: “Je, mnanibashiria (ghulamu) na hali uzee umeshanishika, basi kwa njia gani mnanibashiria?”


قَالُوا بَشَّرْنَاكَ بِالْحَقِّ فَلَا تَكُن مِّنَ الْقَانِطِينَ﴿٥٥﴾
55. (Malaika) Wakasema: “Tunakubashiria kwa haki, basi usiwe miongoni mwa wakatao tamaa.”


قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ﴿٥٦﴾
56. (Ibraahiym) Akasema: “Na nani anayekata tamaa na Rahmah ya Rabb (Mola) wake isipokuwa waliopotea.”


قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ﴿٥٧﴾
57. (Ibraahiym) Akasema: “Basi nini jambo lenu (mlolijia) enyi Wajumbe.”


قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ﴿٥٨﴾
58. (Malaika) Wakasema: “Hakika sisi tumetumwa kwa watu wahalifu.”


إِلَّا آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٥٩﴾
59. “Isipokuwa familia ya Luwtw, hakika Sisi Tutawaokoa wote.”


إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا ۙ إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ﴿٦٠﴾
60. “Isipokuwa mkewe Tumehukumu kwamba yeye bila shaka ni miongoni mwa watakaobakia nyuma (kuangamizwa).”


فَلَمَّا جَاءَ آلَ لُوطٍ الْمُرْسَلُونَ﴿٦١﴾
61. Basi Wajumbe walipokuja kwa familia ya Luwtw.


قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ﴿٦٢﴾
62. (Luwtw) Akasema: “Hakika nyinyi watu msiojulikana.”


قَالُوا بَلْ جِئْنَاكَ بِمَا كَانُوا فِيهِ يَمْتَرُونَ﴿٦٣﴾
63. (Malaika) Wakasema: “Bali tumekujia kwa yale waliyokuwa wanatilia shaka.”


وَأَتَيْنَاكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ﴿٦٤﴾
64. “Na tumekujia kwa haki na hakika sisi ni wakweli.”


فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِّنَ اللَّيْلِ وَاتَّبِعْ أَدْبَارَهُمْ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنكُمْ أَحَدٌ وَامْضُوا حَيْثُ تُؤْمَرُونَ﴿٦٥﴾
65. “Basi toka usiku na ahli wako katika nyakati ya usiku na ufuate nyuma yao wala asigeuke (kutazama) nyuma yeyote miongoni mwenu, na endeleeni kwenda mnakoamrishwa.”


وَقَضَيْنَا إِلَيْهِ ذَٰلِكَ الْأَمْرَ أَنَّ دَابِرَ هَـٰؤُلَاءِ مَقْطُوعٌ مُّصْبِحِينَ﴿٦٦﴾
66. Na Tukamjulisha hukumu ya jambo hilo, kwamba: “Mizizi ya hawa (watendaji uliwati) yatakatwa asubuhi.”


وَجَاءَ أَهْلُ الْمَدِينَةِ يَسْتَبْشِرُونَ﴿٦٧﴾
67. Na wakaja watu wa mji ule wakifurahia.


قَالَ إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ ضَيْفِي فَلَا تَفْضَحُونِ﴿٦٨﴾
68. (Luwtw) Akasema: “Hakika hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe.”



وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَلَا تُخْزُونِ﴿٦٩﴾
69. “Na mcheni Allaah wala msinihizi.”


قَالُوا أَوَلَمْ نَنْهَكَ عَنِ الْعَالَمِينَ﴿٧٠﴾
70. (Watu wa mji) Wakasema (kumwambia Nabiy Luwtw): “Je, hatujakukataza (kukaribisha) watu (wa nje; wageni)?


قَالَ هَـٰؤُلَاءِ بَنَاتِي إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ﴿٧١﴾
71. (Luwtw) Akasema: “Hawa (hapa) mabinti zangu (wa kuwaoa kihalali) ikiwa nyinyi ni wafanyaji.”


لَعَمْرُكَ إِنَّهُمْ لَفِي سَكْرَتِهِمْ يَعْمَهُونَ﴿٧٢﴾
72. “Naapa kwa umri wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم!) Hakika wao walikuwa katika ulevi wao wanatangatanga kwa upofu.”


فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ مُشْرِقِينَ﴿٧٣﴾
73. Basi iliwachukuwa ukelele angamizi walipopambaukiwa jua.


فَجَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ﴿٧٤﴾
74. Tuliufanya (mji huo) juu chini, na Tukainyeshea (mvua ya) mawe ya udongo uliookwa (motoni).


إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْمُتَوَسِّمِينَ﴿٧٥﴾
75. Hakika katika hayo mna Aayaat (ishara, dalili, zingatio, mafunzo) kwa watambuzi.


وَإِنَّهَا لَبِسَبِيلٍ مُّقِيمٍ﴿٧٦﴾
76. Na hakika hiyo (miji) iko katika barabara kuu iliyorasimishwa


إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٧٧﴾
77. Hakika katika hayo ni Aayah (ishara, zingatio n.k) kwa Waumini.


وَإِن كَانَ أَصْحَابُ الْأَيْكَةِ لَظَالِمِينَ﴿٧٨﴾
78. Na hakika watu wa kichakani (Madyan - Nabiy Shu’ayb) bila shaka walikuwa madhalimu.


فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ وَإِنَّهُمَا لَبِإِمَامٍ مُّبِينٍ﴿٧٩﴾
79. Tukawalipiza (kwa kuwaadhibu) na (nchi) zote mbili hizo ziko katika njia kuu bayana.


وَلَقَدْ كَذَّبَ أَصْحَابُ الْحِجْرِ الْمُرْسَلِينَ﴿٨٠﴾
80. Na kwa yakini watu wa Al-Hijr (wa majabalini kina Thamuwd, pia) waliwakadhibisha Rasuli.


وَآتَيْنَاهُمْ آيَاتِنَا فَكَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ﴿٨١﴾
81. Na Tuliwapa Aayaat (ishara, hoja, dalili) Zetuwakawa wenye kuzipuuza.


وَكَانُوا يَنْحِتُونَ مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا آمِنِينَ﴿٨٢﴾
82. Na walikuwa wanachonga majumba katika majabali wakiwa katika amani.


فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ مُصْبِحِينَ﴿٨٣﴾
83. Basi iliwachukua ukelele angamizi walipopambaukiwa asubuhi.


فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿٨٤﴾
84. Basi hayakuwasaidia (chochote) yale waliyokuwa wakichuma.


وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ ۗ وَإِنَّ السَّاعَةَ لَآتِيَةٌ ۖ فَاصْفَحِ الصَّفْحَ الْجَمِيلَ﴿٨٥﴾
85. Na Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake isipokuwa kwa haki. Na hakika Saa (Qiyaamah) bila shaka kitafika. Basi samehe msamaha mzuri.


إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ﴿٨٦﴾
86. Hakika Rabb (Mola) wako Ndiye Al-Khalaaqul-‘Aliym (Mwingi wa kuumba Atakavyo - Mjuzi wa yote).


وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ﴿٨٧﴾
87. Na kwa yakini Tumekupa (Aayaat) Saba (za Suwrat Al-Faatihah) zinazokaririwa (kusomwa) na Qur-aan adhimu.


لَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِلْمُؤْمِنِينَ﴿٨٨﴾
88. Usikodoe macho yako katika Tuliyowasterehesha makundi fulani miongoni mwao (makafiri), na wala usihuzunike juu yao. Na inamisha bawa lako kwa Waumini (kuwahurumia).


وَقُلْ إِنِّي أَنَا النَّذِيرُ الْمُبِينُ﴿٨٩﴾
89. Na sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi ni mwonyaji bayana.”


كَمَا أَنزَلْنَا عَلَى الْمُقْتَسِمِينَ﴿٩٠﴾
90. Kama Tulivyowateremshia (maandikomatukufu) waliojigawanya.


الَّذِينَ جَعَلُوا الْقُرْآنَ عِضِينَ﴿٩١﴾
91. Ambao wameifanya Qur-aan sehemu mbali mbali (waliosema ni sihiri, imetungwa n.k)


فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٩٢﴾
92. Basi Naapa kwa Rabb (Mola) wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), bila shaka Tutawauliza wote.


عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٣﴾
93. Kuhusu yale waliyokuwa wakitenda.


فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ﴿٩٤﴾
94. Basi tangaza wazi yale uliyoamrishwa na jitenge na washirikina.


إِنَّا كَفَيْنَاكَ الْمُسْتَهْزِئِينَ﴿٩٥﴾
95. Hakika sisi Tunakutosheleza dhidi ya wafanyao istihzai.


الَّذِينَ يَجْعَلُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۚ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ﴿٩٦﴾
96. Ambao wanafanya pamoja na Allaah, muabudiwa mwengine basi watakuja kujua.


وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ﴿٩٧﴾
97. Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema.


فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ﴿٩٨﴾
98. Basi Sabbih kwa Himidi za Rabb (Mola) wako, na uwe miongoni mwa wanaosujudu.


وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾
99. Na mwabudu Rabb (Mola) wako mpaka ikufikie yakini (mauti).


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com