Abdulrahman ibn Awf-alitoa mali yake kwa ajili ya Allah (SW)
Ni mmoja kati ya watu
wanane wa mwanzo kusilimu. Pia ni miongoni mwa watu kumi walibashiriwa pepo
na Mtume (SAW). Alikuwa mmoja kati ya watu sita waliochaguliwa na Umar
kuunda baraza la ‘Shura’ kumchagua Khalifa baada ya kifo chake.
Jina lake enzi za
ujahiliya lilikuwa Abu Amr. Aliposilimu Mtume (SAW) akamwita Abdulrahman
(mja wa mwenye kurehemu). Alisilimu hata kabla Mtume (SAW) hajaanza
kwenda kwa Al-Arqam na inasemekana alisilimu siku mbili tu baada ya kusilimu
Abubakar Siddiq.
Abdulrahman hakukimbia
mateso na adhabu za Maquraysh. Alivumilia madhila na mateso na kubaki na
imani yake thabiti. Pale walipolazimika waislam kufanya Hijira kwenda
Habashah, Abdulrahman naye pia alikwenda. Alirudi Makka baada ya kusikia
uvumi kwamba hali za waislam zimekuwa nzuri na baada ya kuthibitika kwama
zilikuwa ni uzushi tu, alifanya tena Hijra kuelekea Habashah na alihitimisha
kwa hijra ya Madina.
Punde tu, alipowasili
Madina. Mtume (SAW) aliwaunganisha Muhajirin na Ansaar. Lengo la udugu
huu lilikuwa kuweza kuwa na maelewano ya kijamii na pia kuwapunguzia ukiwa
muhajiruun. Abdulrahman akakutanishwa na Saad ibn Ar-Rabiah.
Baada ya kuatambulishwa rasmi, Saad akamwambia Abdulrahman:
“Ndugu yangu, mimi
ndiye mwenye utajiri mkubwa hapa Madina, nina vikataa viwili na wake
wawili. Angalia ni kipi kati ya vikataa hivi viwili utakipenda na
nitakuachia na angalia yupi kati ya wake zangu amekupendeza na nitampa talaka
kwa ajili yako”
Abdulrahman
hakutarajia yote haya kwani alionekana kidogo kuingiwa na aibu na kujibu:
“Inshaallah Mwenyezi
Mungu akurehemu katika familia yako na utajiri wako. Tafadhali kwa hisani
yako nioneshe soko tu liko wapi?”
Abdulrahman alioneshwa
soko na kuanza biashara kwa kile kichache alichokuwa nacho. Akafanya
biashara na kupata faida haraka. Muda mchache tu hali yake ikawa nzuri
sana kibiashara akajitafutia mke na kuoa.
Siku moja, alikwenda
kwa Mtume (SAW) huku akinukia uturi na manukato:
“Maliyam!, ewe Abdulrahman! Akasema Mtume Muhammad (SAW)
kwa mshangao. (maliyam ni neno la asili ya kiyemen linaainisha
mshangao).”
“Nimeoa,” akajibu
Abdulrahman.
“Na mkeo ulimpa kitu gani kama mahari yake?”
“Uzito wa ‘uwat’ wa
dhahabu”
“Lazima ulishe walima
hata kama ni kondoo mmoja na Mwenyezi Mungu (SW) akubariki katika utajiri
wako,” akamalizia Mtume (SAW) huku akitabasamu.
Abdulraham alipigana
vita vya Badr na Uhud kwenye vita vya Uhud alisimama imara licha ya kuwa na
majeraha karibu ishirini mwilini mwake na mengine ya kutisha. Jitihada
yake ya nafsi ilikwenda sambamba na jihadi yake ya mali.
Kuna siku moja, Mtume
(SAW) alikuwa akijiandaa kutuma jeshi vitani na akalihutubia kwa kusema:
“Toeni sadaka kwani ninataka kulituma jeshi.”
Haraka haraka
Abdulrahman alikwenda nyumbani kwake na kurudi, “ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu;
akasema, nina (dinar) elfu nne. Ninatoa elfu mbili kama mkopo kwa mola wangu
na kuiachia familia yangu zilizobaki.”
Mtume (SAW) alipoamua
kutuma jeshi Tabuk ambapo kulikuwa mbali sana. Haja ya msaada wa fedha
ilikuwa kubwa kama ilivyokuwa haja ya wana jihadi. Kwani majeshi yao
yalikuwa yameandamana vyema na kuwa na zana nzito za kivita.
Mwaka huo Madina
kulikuwa na njaa na ukame. Safari ya Tabuk ilikuwa ndefu na zaidi ya
kilomita elfu moja. Chakula hakikutosha na usafiri ulikuwa mchache
mno mpaka Mtume (SAW) kuwarudisha kundi la waislam waliokuwa tayari kwa vita kwa
kukosekana usafiri.
Waislam walioachwa
nyuma walisikitika sana na wakajaeleweka kama ‘Bakkaa-in’ waliokuwa
wakilia. Na jeshi hili likaitwa jeshi la Usrah- ‘taabu’. Hapo Mtume
(SAW) akawahimiza masahaba watoe walichonacho kwa moyo mmoja kulisaidia jeshi
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuwahakikishia malipo makubwa kwa Mwenyezi
Mungu.
Naam! Wito ukaitikiwa
na waislam wakajitolea kwa wingi na miongoni mwao ni Abdulrahman. Alitoa
wakia mia mbili za dhahabu na hapo Umar ibn Khattab alisema:
“Sasa nimemuona
Abdulrahman anafanya kosa, hukuiachia chochote familia yake.”
“Umeiachia chochote
familia yako, Abdulrahman?” Mtume (SAW) alimuuliza.
“Ndio, nilichowaachia
ni kingi kuliko nilichotoa na ni bora,” akajibu Abdulrahman.
Mtume akauliza, “kiasi
gani?”
“Kile ambacho Mwenyezi
Mungu na Mtume wake ameahidi navyo ni rizki, mambo mema na malipo.”
Jeshi la waislam
likaanza safari kuelekea Tabuk. Abdulrahman akabahatika kupata heshima ambayo
kabla yake hajawahi kupewa mtu yoyote. Ulipofika wakati wa sala na Mtume
(SAW) hakuwepo wakamchagua Abdulrahman kuwa Imam. Mtume (SAW) alipodiriki
sala, tayari rakaa ya kwanza ilikwisha malizika na akasali maamuma. Je!
Kuna hadhi imam wa Al-habib Mustafa (SAW), kiumbe kilicho bora zaidi kwa
Mwenyezi Mungu, imam wa Mitume yote Muhammad alayhi ssalaatu wassalam!
Mtume Muhammad (SAW)
alipofariki, Abdulrahman alichukua jukumu la kuihudumia familia yake, Ummahatul
Muuminiin. Aliwashughulikia kwa mahitaji yao na kwenda nao Hija pamoja
ili kuhakikisha mahitaji yao yametimizwa. Huu ni uaminifu ambao alipata
katika familia ya Mtume (SAW).
Aliwahi kuuza sehemu
ya ardhi kwa dinar elfu arubaini na kuzigawa zote kwa Banu Zahrah jamaa wa mama
yake Mtume (SAW), wakeze Mtume (SAW) waliokuwa masikini. Na Bi Aisha (RA)
alipopata mgao wake aliuliza:
“Ni nani aliyeleta
fedha hizi?
Akaambiwa ni,
“Abdulrahman.”
Mtume amesema, “hakuna mtu yoyote atakayewaonea huruma nyinyi
baada ya kufa kwangu isipokuwa wale walio na subira.”
Dua za Mtume (SAW)
zilikubalika kwani Abdulrahman Ibn Awl alikuja kuwa tajiri mkubwa miongoni mwa
masahaba wa Mtume (SAW), makundi yake ya misafara toka na kuja Madina yalizidi
kukua siku hadi siku. Aliwaletea watu wa Madina unga, ngano, samli, nguo,
vyombo vya kupikia, manukato na chochote kitakachohitajika na kuuza nje bidhaa
zilikuwa zikizalishwa.
Siku moja, sauti kubwa
ikasikika ikitokea nje ya mipaka ya mji wa Madina, mji ambao kwa kawaida ni
tulivu sauti ilizidi kuongezeka huku mawingu ya vumbi na michanga yakirushwa
juu angani. Wakagundua kwamba ni kundi kubwa la ngamia takriban mia saba
huku limesheheni mizigo linaingia Madina. Watu wakawa wanaitana kuja
kushuhudia ni bidhaa gani msafara huu wa ngamia wote hawa umeleta:
Bi Aishah, akasikia
zogo lile na akauliza, “nini tena hiki kinachotokea Madina?
Akaambiwa, “ni msafara
wa Abdulrahman ibn Awl unatoka Syria na bidhaa”
“Msafara tu ndio
unaofanya zogo lote hili?” Akauliza huku haamini.
“Naam, Yaa Ummul
Muuminiin, wapo ngamia mia saba”
Bi Aisha akatikisa
kichwa chake na akashika tamaa kama aliyepigwa na butwaa kama kwamba anajaribu
kukumbuka tukio au jambo lililopita kasha akasema:
“Nimemsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu akisema, nimemuona
Abdulrahman Ibn Awl anaingia peponi, huku akitambaa.”
Kwa nini atambae? Kwa
nini haingii mara moja kwa kuruka pamoja na masahaba wa mwanzo wa Mtume (SAW).
Baadhi ya masahaba
wake wakamhadithia Abdulrahamn riwaya hii. Akakumbuka alishawahi kuisikia
hadithi hii zaidi ya mara moja kutoka kwa Al-habib Mustafa (SAW) na akaharakiza
kuelekea kwa Bi Aisha na akamwambia: “Yaa Ammah! Ewe mama yangu! Umeyasikia
haya kutoka kwa Mtume (SAW).
“Ndio,” akajibu.
Abdulrahman akafurahi
sana na akaongezea:
“Kama ningeliweza
ningeliingia peponi huku nimesimama. Nnakuapia yaa Ammah, msafara wote
huu na bidhaa zake zote ninautoa fi Sabiili Llah!
Hilo alilitekeleza kwa
ukarimu huu aliounesha na uadilifu na kuwagawia watu wa Madina na vitongoji
vyake.
Hili ni tukio moja tu
linalomuonesha Abdulrahman kuwa ni mtu wa aina gani? Alipata utajiri
mkubwa lakini haukumvaa wala hakuuvaa.
Aliendelea kutoa kwa
mikono yuke yote miwili kwa siri na kwa dhahiri. Na baadhi ya misaada
aliyoitoa, dirham elfu arubaini, dinar elfu arubaini. Wakia mia mbili za
dhahabu, farasi mia tano kwa mujahidina, dinar mia nne kwa waliopona vita vya Badr
na sehemu kubwa aliyoitoa kwa wake za Mtume (SAW) na bado listi inaendelea……
Na kwa ukarimu wake Bi
Aisha alisema:
“Inshallah Mwenyezi
Mungu (SW) amnywishe kwenye chemchem ya Salsabil.”
Utajiri wote huu
haukumtia jeuri wala kiburi na haukumbadilisha chochote. Alipokuwa na
wafanyakazi na wasaidizi wake hawezi kumtofautisha kabisa. Siku
moja aliletewa chakula kufutari, alikitazama kasha akasema;
“Musab ibn Umayr
aliuwawa, yeye alikuwa bora kuliko mimi. Hatukuwa na hata guo la
kumsitiri tukimfunika kichwani miguu huwa wazi, kisha Mwenyezi Mungu (SW)
akatujaalia rizki hizi za kidunia………nina wasi wasi kwamba malipo yetu tayari
tumeshalipwa mapema duniani.” Akaanza kulia na kushindwa kula.
Na Inshallah Mwenyezi
Mungu amuweke Abdulrahman katika kundi la wale…… Suratul Baqarah 262.