Abdul
Abdul Abdullah ibn
Abbass- msomi wa umma huu
Abdullah ibn Abbas bin Abdul
Muttalib ni mtoto wa ami yake Mtume (SAW). Alizaliwa miaka mitatu kabla ya
Hijra. Na Mtume alipofariki, Abdullah alikuwa na umri wa miaka kumi na
mitatu.
Alipofika umri wa kutambua - miaka
saba - alijifunga na kumwambata Mtume (SAW). Alikuwa akimuandalia Mtume
(SAW) maji ya kutawadhia. Husimama nyumba ya Mtume Muhammad (SAW)
anaposali na wanapokuwa safarini, hujaribu kuwa karibu na Mtume (SAW) mpaka
kuambiwa alikuwa kama kivuli cha Mtume, kwani anapokuwepo Mtume na Abdullah
anakuwa karibu naye.
Muda wote huo, Abdullah huwa mtulivu
na kufuatilia kila ambalo Mtume (SAW) hufanya na kusema. Moyo wake umejaa
hamu ya kutaka kuelewa na akili yake kuwa bado changa na safi hivyo kuweza
kuhifadhi maneno ya Mtume (SAW) kwa uhakika kama mfano wa chombo cha kurekodia.
Kwa njia hii pamoja na utafiti wake
baadaye, Abdullah akawa mmoja katika wasomi wakubwa miongoni mwa masahaba na
kuweza kuzihifadhi hadithi za Mtume (SAW) kwa ajili ya kizazi kijacho.
Inasemekana aliweza kuhifadhi hadithi elfu moja mia sita na sitini, ambazo
zimeandikwa na kuhakikiwa katika Bukhari na Muslim.
Mara nyingi Mtume (SAW) alikuwa
akimweka Abdullah karibu naye na kumpiga piga mabegani mwake na kuomba
“Ewe Mola, mjaalie kupata
elimu ya kina ya dini ya kiislam na umuongoze katika kufahamu na utaalam wa
vitu.”
Mtume Muhammad (SAW) pia alimuombea awe
mtu wa hekima pia, mbali na elimu na ufahamu wa mambo Abdullah anasimulia:
“ Mara moja Mtume (SAW) alikuwa
akijiandaa kutia udhu. Niliharakia kumwekea maji. Akafurahishwa na
nilivyofanya. Alipokuwa anataka kuanza kusali, aliashiria nisimame ubavuni mwake.
Hata hivyo, nikasimama nyuma yake. sala ilipokwisha aligeuka na
kusema, ‘Nini kilichokuzuia kutosimama ubavuni mwangu eeh
Abdullah?’
Abdullah akajibu, “wewe ni mwingi wa
haiba na taadhima kubwa nisiyostahili kwa mimi kusimama ubavuni mwako.”
Mtume (SAW) akanyanyua mikono juu na
kuomba, “ewe mola mjaalie hekima,” Dua hii ya Mtume Muhammad (SAW) ilikuja
kuthibitika baadae kwani Abdullah alikuwa mwenye hekima na busara hata kupita
umri wake. Hekima na busara hizi zilikuja kwa ucha Mungu na kutafuta elimu
alikojishughulisha Abdullah enzi za uhai wa Mtume (SAW) na hata baada ya
kufariki kwake.
Enzi za uhai wa Mtume (SAW),
Abdullah hakuwahi kukosa vikao vyote vya Mtume Muhammad (SAW) na kuhifadhi yale
yote atakayoyasema na baada ya kufariki kwake, alijihimu kwenda kwa masahaba
wengi kujifunza yale waliyofundishwa na Mtume (SAW).
Akisikia tu! Kuna mtu anajua hadithi
fulani ambayo yeye haijui atakwenda kwake haraka na kuiandika. Ataihakiki
na kuilinganisha na hadithi nyengine na aliwahi kwenda kwa masahaba karibu
thelathini kuhakiki jambo moja tu.
Abdullah anaeleza nini alichofanya
baada ya kusikia hadithi ambayo hakuijua kabla:
“Nilikwenda kwake wakati wa Qaylula
(baina ya adhuhuri na alasiri watu wanapojipumzisha kwa usingizi) nikatandika
guo langu mbele ya mlango wake. Upepo ukawa unavuma na nikajawa na
mavumbi. Kama ningelitaka ningegonga mlango na kuomba rukhsa na nina
hakika angelinifungulia. Nikaona bora nisubiri ili atakapoamka atakuwa
ameshapumzika. Alipokuwa anatoka na kuniona katika hali yangu akasema,
“ewe bin ami wa Mtume (SAW) una nini? Hata kama ungeagiza nije kwako
ningelikuja.” Abdullah akajibu, mimi ndie ninaepaswa kuja kwako kwani
elimu hufuatwa, haiji. Nikamuuliza kuhusu ile hadithi na kujifunza kutoka
kwake”
Katika njia hii, Abdullah aliendelea
kuuliza na kuuliza na kuendelea kuuliza huku akihakiki na kuchunguza kila
alichokusanya. Abdullah hakuwa mtaalam wa hadithi pekee, alizama pia
katika elimu nyenginezo. Alikuwa akimhusudu sana Zayd ibn Thabit, mkusanyaji
Quran mkuu na mshauri wa sheria Madina, mtaalam wa sheria ya mirathi na kusoma
Quran. Endapo Zayd amekusudia kwenda safari Abdullah humkamatia kipando
chake kwa unyenyekevu kama vile mtumwa mbele ya bwana wake. Zayd
humwambia, “Usifanye hivyo, ewe bin ami wa Mtume (SAW).”
“Hivi ndivyo tulivyoamrishwa
kuwatendea wasomi miongoni mwetu,” Abdullah akajibu.
Zayd naye humwambia, “hebu lete
mkono wako niuone.”
Abdullah naye akiupeleka, Zayd
huubusu na kusema, “Hivi ndivyo tulivyoamrishwa kuwatendea Ahlul bayt (watu wa
nyumbani wa Mtume (SAW).”
Kila kiwango chake cha elimu kikikua
basi na hadhi yake pia ikaongezeka. Masruq ibn al-Ajda anamzungumzia Abdullah,
“Kila nikimuona Abdullah, husema ni kijana mzuri wa kuvutia. Akiongea,
husema ni mzungumzaji fasaha na akisimamia mazungumzo husema “ni msomi wao.”
Khalifa Umar ibn Khattab mara nyingi
husikiliza ushauri wake katika mambo muhimu yanayolihusu dola la kiislam na
kumweleza kama, “kijana aliyekomaa.”
Saad ibn Abi Waqas anamuelezea,
“Sijawahi kumuona mtu anayefahamu kwa haraka, mwingi wa elimu na hekima zaidi
ya Ibn Abbass. Nilimuona Umar akimwita kushauriana naye kwenye mambo
mazito tena mbele ya wakongwe wa Badr miongoni mwa Muhajiriin na Ansaar na
akiongea, Umar hayadharau.”
Kutokana na sifa hizi ndio maana
Abdullah ibn Abbas anafahamika zaidi “Msomi wa umma huu.”
Abdullah hakuwa mtafutaji tu wa
elimu bali alielewa kwamba ana wajibu wa kufundisha umma wa kiislam na wale
wanaotafuta elimu. Akawa maalim na nyumba yake kuwa chuo kikuu.
Naam! Ni chuo kikuu kikitakhassas na elimu ila tu kulikuwa na maalim mmoja tu
jinsi watu walivyomiminika kwenye darasa za Abdullah! Sahaba mmoja anasimulia:
“Niliwaona watu wengi wakielekea
nyumbani kwake mpaka kukawa hakuna nafasi nje. Niliingia ndani na
kumfahamisha kwamba watu wanapigania kuingia ndani na wamejaa mlangoni,
akasema, “nipatie maji nitie udhu.” Alitia udhu na akakaa kitako cha
kudarsisha na kusema, “nenda nje kawaambie, yoyote anaetaka kuuliza juu ya
Quran na lafdhi (matamshi) yake na aingie ndani. Nikafanya kama
nilivyoagizwa, nyumba ikawa bado imejaa na akaelezea na kutoa maelezo ya ziada
kuliko yale yaliyoulizwa.
Kisha akawaambia wanafunzi wake,
“wapisheni wenzenu sasa.”
Akaniagiza tena, “nenda nje
kawaambie, yoyote anayetaka kuuliza juu ya Quran na tafsiri yake na aingie
ndani.”
Nyumba ikajaa tena na kama kawaida
Abdullah akaeleza na kutoa maelezo ya ziada. Ikaendelea hivyo huku
makundi kwa makundi yanakuja kujadiliana na ‘Ustaadh’ kuhusu fiqh, halali,
haramu, mirathi, lugha ya kiarabu na mashairi na kadhalika.
Kwa kutaka kuondoa msongamano,
Abdullah akaweka siku moja kwa somo moja. Kama leo kutasomeshwa fiqh basi
kesho yake ni Quran na tafsiri. Vita vya Mtume, Mashairi, historia ya kiarabu
kabla ya uislam hayo yote yalitengewa siku zao.
Njia yake ya kudarsisha ilikuwa ya
uhakika kwani akisaidiwa na hifadhi yake timamu, hekima na busara, maelezo yake
yalikuwa wadhihi,wazi na ya kimantiki. Hoja zake zilikuwa za nguvu huku
zikishindikizwa na dalili za kimaandiko na matukio ya kihistoria.
Katika tukio moja, nguvu za hoja
zilihitajika kutumika enzi za ukhalifa wa Ali ibn Talib. Kundi kubwa
lililokuwa likimuunga mkono Ali dhidi ya Muawiya likaanza kumtenga.
Abdullah akaenda kwa Ali na kuomba rukhsa azungumze nao.
Kwanza Ali alisita akichelea kwamba
Abdullah ataweza kufikwa na jambo lolote baya akiwaendea. Abdullah
akamhakikishia kwamba hakuna lolote baya litakalotokezea na hivyo kuruhusiwa.
Alikwenda, baadhi yao hawakuwa
tayari kumsikiliza lakini wengine walikubali. Abdullah akaanza:
“Niambieni mna malalamiko gani dhidi
ya bin ami wa Mtume (SAW), mume wa mtoto wake na wa mwanzo kusilimu?
Wakaeleza matatizo yao matatu makuu;
Kwanza, ateue watu kuhukumu mas-ala
ya dini ya Mwenyezi Mungu wakimaanisha Ali alikubali kusuluhishwa na Abu Musa
al-Ash-ari na Amr ibn Aadh dhidi yake na Muawiya.
Pili, alipigana na wala hakuchukua
ngawira wala mateka.
Tatu, hakusisitiza kwenye wa kikao
cha usuluhishi kuitwa Amirul Muuminiin wakati tayari waislam walishaapa kiapo
cha utii kwake na yeye kuwa Khalifa halali.”
Kwa wale waliomuasi Ali, hizi zote
zilikuwa alama za udhaifu na kwamba Ali alikuwa tayari kuingiza alama za
kuuliza katika cheo chake cha Amir.
Abdullah alipoanza kuwajibu
akawaomba ataje aya za Quran na hadithi za Mtume Muhammad (SAW) ambazo hawana
mashaka nazo na zinahusiana na malalamiko yao, iwapo watakuwa tayari
kubadilisha msimamo wao. Walikubali na Abdullah kuendelea:
“Kuhusu maelezo ya kuteua watu kutoa
hukumu katika mas-ala ya dini ya Mwenyezi Mungu (SW).” Mwenyezi Mungu
(SW) anasema, “Enyi mlioamini wala msiuwe wanyama wa kuwinda (kwa mchezo)
wakati mpo ndani ya Hijja. Na mongoni mwenu atakaemuuwa basi malipo yake
yatakuwa sawa na alichokiua, katika mifugo kama wanavyohukumu waadilifu wawili
miongoni mwenu…………..”
“Nnakuombeni mhukumu, wallahi je!
Hii hukumu ya watu hawa kuhusiana na kuenzi maisha yao na kufanya suluhu baina
yao inahitaji kutazamwa zaidi kuliko ile suluhisho la sungura ambaye thamani
yake ni robo dirham?
Bila ya shaka majibu yao yakawa
suluhu ni muhimu zaidi kwa ajili ya kuyaenzi maisha ya watu na kuweka amani
baina yao, kuliko mchezo wa vinyama kwenye baytul haraam:
Akawambia, “tumemalizana kwa hilo?”
Wakajibu, “Allahumma na’am”.
Abdullah akaendelea. Kuhusiana
na maelezo kwamba Ali alipigana na wala hukuchukua mateka wa kivita kama
alivyofanya Mtume (SAW). Hivi kweli mnataka kumchukua ‘mama’ Aisha kama
mateka? Na kumtendea kama wanavyofanyiwa mateka? Ikiwa jibu lenu ni ndio basi
mmeshaingia katika kufuru, na kama mkisema kwamba si ‘mama’ yenu vile vile
mtaingia katika kufuru kwani Mwenyezi Mungu (SW) kasema:
“Mtume yu bora sana na waumini
kuliko hata nafsi zao. Na wakeze ni mama zao.Na jamaa ni karibu wao kwa wao
katika kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko waumini wengine na wahamiaji . Ila muwe
munawafanyia wema marafiki zenu. Ahzaab/6
Abdullah akaendelea, “chagueni
mtakalo, na akamalizia, tumemalizana na hili?”. Na jibu kurudi, “ Allahumma
na’am.”
Na maelezo kwamba Ali amekubali
kutoitwa Amirul Muuminiin (kumbukeni) Mtume (SAW) mwenyewe kwenye suluhu ya
Hudaybiyah, aliwataka makafiri waandike kwenye mkataba “hivi ndivyo Mtume wa
Mwenyezi Mungu mtukufu alivyokubali………”, lakini wakadai “tungelikubali
kama wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (SW) tusingekuzuia kwenda Al kaaba na wala
tusingepigana na wewe. Andika badala yake Muhammad ibn Abdullah.” Mtume
akakubaliana na madai yao huku akisema,
“Wallahi mimi ni mjumbe wa
Mwenyezi Mungu hata kama wananikataa”
Alipofika hapa akawauliza walioasi,
“Je! Na hili tumemalizana nalo?”
Na jibu, “Allahumma na’am.”
Moja katika faida ya nguvu za hoja
kwenye mjadala, sifa aliyeionesha Abdullah ibn Abbass na ile hiba aliyojaaliwa
ya kuifahamu vyema Quran na sira ya Mtume (SAW) na hatimaye kiasi cha watu elfu
ishirini waliokuwa tayari wamemuasi Ali wakarudi kwenye himaya yake. Hata
hivyo, kiasi cha watu elfu nne wakaendelea na msimamao wao wa uasi.
Baadaye wakajafahamika kama Khawarij.
Kwenye tukio hili Abdullah alionesha
msimamo wake wa kupendelea amani kuliko vita na mantiki dhidi ya nguvu na fujo.
Abdullah alikuwa mtu mwenye kuwajali
sana waislam wenzake na aliwahi kusikika akisema:
“Pale ninapoona umuhimu wa aya ya
kitabu cha Mwenyezi Mungu hutamani watu wote wakajua lile linalolijua.”
“Pale ninaposikia kiongozi wa
waislam anaongoza kwa haki na kutawala kwa uadilifu hufurahi na kumuombea
dua…..”
“Pale ninaposikia mvua inanyesha
kwenye ardhi ya waislam, basi na mimi hujawa na furaha.”
Abdullah alikuwa mcha mungu mwenye
kufunga funga za sunna na kusimama usiku, hulia wakati akisoma Quran na akifika
kwenye aya za mauti, kiama na akhera sauti yake huwa nzito na kujawa na kwikwi
kwa khofu.
Alipofariki akiwa na umri wa miaka
sabiini huko Taif.