Atw-Twalaaq (65)


سُورَةُ  الطَّلاق
Atw-Twalaaq (65)

(Imeteremka Madina)


Sura hii inaeleza baadhi ya hukumu za talaka, na eda, na namna zake, na hukumu zake - tangu kubaki mwenye eda katika nyumba aliyo pewa talaka ndani yake, na waajibu wa kumtazama kwa matumizi, na maskani. Na kati ya hukumu hizi, kama ilivyo mwendo wa Qur'ani, ipo ahadi kwa mwenye kufuata amri za Mwenyezi Mungu, na onyo kwa mwenye kukiuka mipaka yake. Kisha Sura imeashiria malipo ya wenye kutakabari wakakataa kutimiza amri za Mwenyezi Mungu na Watume wake. Na ikakhitimisha Sura kwa kuwahimiza Waumini wamche Mwenyezi Mungu, na kuwakumbusha neema za kuwapelekea Mtume anaye wasomea Aya za Mwenyezi Mungu, ili awatoe kwenye giza wende kwenye mwangaza, na kwa uweza wake Mwenyezi Mungu kuziumba mbingu saba, na katika ardhi mfano wa hizo.
 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ


يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ رَبَّكُمْ ۖ لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِن بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ ۚ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّـهِ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ ۚ لَا تَدْرِي لَعَلَّ اللَّـهَ يُحْدِثُ بَعْدَ ذَٰلِكَ أَمْرًا ﴿١﴾

1. “Ee Nabii!  Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda (twahara na si katika hedhi) zao, na hesabuni (barabara siku za) eda; na mcheni Rabb (Mola) wenu. (Wakati huo wa eda ya talaka) Msiwatowe (hao mliowataliki) katika nyumba zao, na wala wao (wenyewe) wasitoke isipokuwa wakileta uchafu ulio bayana. Na hiyo ndio mipaka ya Allaah. Na yeyote (yule) atakayevuka mipaka ya Allaah basi kwa yakini amedhulumu nafsi yake. Hujui; huenda Allaah Atatokezesha jambo jingine (mapatano) baada ya haya. 

فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ وَأَقِيمُوا الشَّهَادَةَ لِلَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمْ يُوعَظُ بِهِ مَن كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا ﴿٢﴾

2. Na watakapokaribia kufikia muda wao, basi (ima) wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema, na mshuhudishe mashahidi wawili wenye uadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa (ajili ya) Allaah.  Hivyo ndivyo anavyowaidhiwa (yule) anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na yeyote (yule) anayemcha Allaah; (basi Allaah) Atamjaalia njia (ya kutoka katika matatizo).

وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا ﴿٣﴾

3. Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii. Na yeyote (yule) anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza amri Yake. Allaah Amejaalia kwa kila kitu kipimo chake.


وَاللَّائِي يَئِسْنَ مِنَ الْمَحِيضِ مِن نِّسَائِكُمْ إِنِ ارْتَبْتُمْ فَعِدَّتُهُنَّ ثَلَاثَةُ أَشْهُرٍ وَاللَّائِي لَمْ يَحِضْنَ ۚ وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ ۚ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا ﴿٤﴾

4. Na wale wanawake wanaokata tamaa (wanaokoma) hedhi miongoni mwa wanawake wenu, mkiwa na shaka (katika muda wao wa eda), basi eda yao ni miezi mitatu, na (hiyo pia ni eda ya) wale wanawake wasiopata hedhi. Na wenye mimba muda wao (wa eda) watakapozaa mimba zao. Na yeyote (yule) anayemcha Allaah; (basi Allaah) Atamjaalia wepesi katika jambo lake

ذَٰلِكَ أَمْرُ اللَّـهِ أَنزَلَهُ إِلَيْكُمْ ۚ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يُكَفِّرْ عَنْهُ سَيِّئَاتِهِ وَيُعْظِمْ لَهُ أَجْرًا ﴿٥﴾

5. Hiyo ni Amri ya Allaah Amekuteremshieni; na yeyote (yule) anayemcha Allaah, (Allaah) Atamfutia maovu yake na Atamuadhimishia ujira.

أَسْكِنُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ سَكَنتُم مِّن وُجْدِكُمْ وَلَا تُضَارُّوهُنَّ لِتُضَيِّقُوا عَلَيْهِنَّ ۚ وَإِن كُنَّ أُولَاتِ حَمْلٍ فَأَنفِقُوا عَلَيْهِنَّ حَتَّىٰ يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ ۚ فَإِنْ أَرْضَعْنَ لَكُمْ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ ۖ وَأْتَمِرُوا بَيْنَكُم بِمَعْرُوفٍ ۖ وَإِن تَعَاسَرْتُمْ فَسَتُرْضِعُ لَهُ أُخْرَىٰ ﴿٦﴾

6. Wawekeni (hao mliowataliki) kwenye majumbani mnayokaa nyinyi kwa kadiri ya kipato chenu, na wala msiwadhuru ili muwatie dhiki. Na wakiwa ni wenye mimba, basi wagharamieni (matumizi yao) mpaka wazae mimba zao. Na wakikunyonyesheeni, basi wapeni ujira wao. Na shaurianeni baina yenu kwa wema. Na mkiona uzito, basi amnyonyeshee mwanamke mwengine.

لِيُنفِقْ ذُو سَعَةٍ مِّن سَعَتِهِ ۖ وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ فَلْيُنفِقْ مِمَّا آتَاهُ اللَّـهُ ۚ لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا مَا آتَاهَا ۚ سَيَجْعَلُ اللَّـهُ بَعْدَ عُسْرٍ يُسْرًا ﴿٧﴾

7. Ili mwenye wasaa agharimu kwa wasaa wake, na aliyebaniwa riziki yake, basi agharimie katika kile Alichompa Allaah. Allaah Haikalifishi nafsi yeyote ile isipokuwa kwa kile Alichoipa. Allaah Atajaalia baada ya dhiki faraji.

وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ عَتَتْ عَنْ أَمْرِ رَبِّهَا وَرُسُلِهِ فَحَاسَبْنَاهَا حِسَابًا شَدِيدًا وَعَذَّبْنَاهَا عَذَابًا نُّكْرًا ﴿٨﴾

8. Na miji mingapi imeasi amri ya Rabb (Mola) wake na (pia ikaasi amri ya) Rasuli Wake, basi Tukaihisabia hesabu shadidi, na Tukaiadhibu adhabu inayochukiza.

فَذَاقَتْ وَبَالَ أَمْرِهَا وَكَانَ عَاقِبَةُ أَمْرِهَا خُسْرًا ﴿٩﴾

9. Ikaonja maovu ya mambo yake, na ikawa matokeo ya mambo yake kuwa ni khasara.

أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا ۖ فَاتَّقُوا اللَّـهَ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ الَّذِينَ آمَنُوا ۚ قَدْ أَنزَلَ اللَّـهُ إِلَيْكُمْ ذِكْرًا ﴿١٠﴾
10. Allaah Amewaandalia adhabu kali, basi mcheni Allaah enyi wenye akili mlioamini! Allaah Amekwishakuteremshieni dhikri (ukumbusho, mawaidha na Qur-aan).


رَّسُولًا يَتْلُو عَلَيْكُمْ آيَاتِ اللَّـهِ مُبَيِّنَاتٍ لِّيُخْرِجَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ وَيَعْمَلْ صَالِحًا يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ قَدْ أَحْسَنَ اللَّـهُ لَهُ رِزْقًا ﴿١١﴾

11. Ni Rasuli anakusomeeni Aayaat za Allaah zinazobainisha; ili (Allaah) Awatoe wale walioamini na wakatenda mazuri kutoka kwenye viza (na kuwaingiza) kwenye Nuru. Na yeyote (yule) anayemwamini Allaah na akatenda (‘amali) nzuri, (basi Allaah) Atamuingiza Jannaat zipitazo chini yake mito ni wenye kudumu humo abadi. Allaah Amekwishampa riziki nzuri.


اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ وَمِنَ الْأَرْضِ مِثْلَهُنَّ يَتَنَزَّلُ الْأَمْرُ بَيْنَهُنَّ لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا ﴿١٢﴾

12. Allaah ni Yule Aliyeumba mbingu saba na katika ardhi mfano wake (mfano wa mbingu), inateremka Amri baina yake, ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Qadiyr (Muweza), na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi (Wake).



Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com