Al-Munaafiquwn (63)

سُورَةُ  الْمُنَافِقُون
Al-Munaafiquwn (63)

(Imeteremka Madina)


Sura hii imekusanya kikundi cha sifa za wanaafiki; ikataja kwamba hao hutangaza imani yao kwa ndimi zao bila ya kuwa wanasema kweli.  Na ikabainisha kwamba wanafanya yamini zao za uwongo kuwa ni kinga wasiambiwe kuwa ni makafiri, ambao kwa hakika ndivyo walivyo na ndivyo watakavyo lipwa hivyo. Pia imebainisha kuwa hao wanaafiki wana umbo zuri la kumpendeza anao waona, na wana ufasihi mzuri wa kusikilizwa. Na juu ya hivyo, nyoyo zao zi tupu, hazina Imani ndani yake. Wao ni kama magogo yaliyo egemezwa, yasiyo na uhai.
Na Sura inaelezea kuwa wakiitwa ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee maghfira, hali yao hubainika kwa kuwa hutakabari, na hudhihirisha kukataa kwao kuitikia,  nao wanajivuna.
Kisha Sura ikaingia kutaja madai ya wanaafiki kwamba wao ati ndio watukufu wenye nguvu, na Waumini ni madhalili; na ahadi walio waahidi Waumini kuwa watawatoa mji wakisha rejea Madina. Sura imebainisha wepi katika makundi mawili hayo walio watukufu na wenye nguvu.
Na khatimaye Sura inaelekeza kuwasemeza Waumini watoe kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, wafanye haraka kwa hayo kabla mauti hayajamfikia mmoja wao, akajuta, na akatamani laiti inge akhirishwa ajali yake. Na wala Mwenyezi Mungu hamuakhirishi yeyote ikisha fika ajali yake.

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ ﴿١﴾

1. Watakapokujia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Rasuli wa Allaah.” Na Allaah Anajua (vyema) kuwa hakika wewe ni Rasuli Wake, na Allaah Anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo.

اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢﴾

2. Wamefanya viapo vyao (vya uongo) kuwa ni kinga (ya ‘amali zao ovu). Hivyo wakazuia (watu) njia ya Allaah, hakika ni uovu mbaya mno waliokuwa wakitenda.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا فَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ ﴿٣﴾

3. Hiyo ni kwa kuwa wao waliamini, kisha wakakufuru, basi ikapigwa chapa juu ya nyoyo zao kwa hiyo hawafahamu.

وَإِذَا رَأَيْتَهُمْ تُعْجِبُكَ أَجْسَامُهُمْ ۖ وَإِن يَقُولُوا تَسْمَعْ لِقَوْلِهِمْ ۖ كَأَنَّهُمْ خُشُبٌ مُّسَنَّدَةٌ ۖ يَحْسَبُونَ كُلَّ صَيْحَةٍ عَلَيْهِمْ ۚ هُمُ الْعَدُوُّ فَاحْذَرْهُمْ ۚ قَاتَلَهُمُ اللَّـهُ ۖ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٤﴾

4. Na unapowaona, inakupendezesha miili yao, na wanaposema, unasikiliza kauli yao, kama kwamba magogo yaliyoegemezwa; wanadhania kuwa kila ukelele unaopigwa ni dhidi yao. Wao ndio maadui, basi tahadhari nao, Allaah Awaangamize! Namna gani wanavyogeuzwa?

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا يَسْتَغْفِرْ لَكُمْ رَسُولُ اللَّـهِ لَوَّوْا رُءُوسَهُمْ وَرَأَيْتَهُمْ يَصُدُّونَ وَهُم مُّسْتَكْبِرُونَ ﴿٥﴾

5. Wanapoambiwa: “Njooni (ili) Rasuli wa Allaah akuombeeni maghfirah.” Hupindisha vichwa vyao, na utawaona wanakwepa nao ni wenye kutakabari.

سَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَسْتَغْفَرْتَ لَهُمْ أَمْ لَمْ تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ لَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ ﴿٦﴾

6. Ni sawasawa juu yao, ukiwaombea maghfirah au usiwaombee, Allaah Hatowaghufuria kamwe. Hakika Allaah Haongoi watu mafasiki.

هُمُ الَّذِينَ يَقُولُونَ لَا تُنفِقُوا عَلَىٰ مَنْ عِندَ رَسُولِ اللَّـهِ حَتَّىٰ يَنفَضُّوا ۗ وَلِلَّـهِ خَزَائِنُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَفْقَهُونَ ﴿٧﴾

7. Wao ndio wale wasemao: “Msitoe (mali) kwa ajii ya walioko kwa Rasuli wa Allaah mpaka watoweke.”  Na ni za Allaah Pekee hazina za mbingu na ardhi, lakini wanafiki hawafahamu.

يَقُولُونَ لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الْأَعَزُّ مِنْهَا الْأَذَلَّ ۚ وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٨﴾

8. Wanasema: “Tutakaporudi Madiynah, mwenye utukufu (yaani ‘Abdullaah bin Ubayy bin Saluwl kichwa cha wanafiki) atamfukuza humo aliye dhalili (yaani Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم)” Na hali utukufu ni wa Allaah na wa Rasuli Wake na wa Waumini, lakini wanafiki hawaelewi.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُلْهِكُمْ أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٩﴾

9. Enyi mlioamini! Yasikushughulisheni mali zenu na wala auladi wenu na dhikri[4] ya Allaah. Na yeyote (yule) atakayefanya hivyo basi hao ndio waliokhasirika.

وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠﴾

10. Na toeni katika yale Tuliyokuruzukuni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti akasema: “Rabb (Mola) wangu! Lau Ungeliniakhirisha mpaka muda wa karibu hivi, basi ningetoa swadaqah na ningelikuwa miongoni mwa (watu) wema.”


وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّـهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا ۚ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١١﴾

11. Lakini Allaah Haiakhirishi kamwe nafsi yeyote inapokuja ajali yake (ya kufa) na Allaah ni Khabiyr (Mjuzi wa vilivyodhahiri na vilivyofichikana) kwa mnayoyatenda.


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com