Al-Fajr (89)


سُورَةُ  الْفَجْر
Al-Fajr  (89) 

(Imeteremka Makka)

Imeanza Sura hii kwa viapo vya mambo yanayo onekana namna mbali mbali, yanayo pelekea kuangalia athari ya kudra kwamba wanao mkanya Mwenyezi Mungu na kukanya kufufuliwa watakuja adhibiwa, kama walivyo kwisha adhibiwa walio kadhibisha kabla yao. Na Sura ikaingia kuthibitisha mwendo wa Mwenyezi Mungu wa kuwajaribu waja wake kwa kheri na shari, na kwamba kupa kwake na kunyima kwake sio dalili ya kuridhika kwake au kukasirika kwake. Tena mazungumzo yakawaelekea wanao semezwa ya kwamba hali zao zinafichua wingi wa pupa yao na choyo chao. Kisha inakhitimisha kwa kuashiria majuto ya wanao pindukia kiasi na kutamani kwao kwamba laiti wangeli tanguliza mema ya kuwaokoa na hayo wanayo teseka nayo ya vitisho vya Siku ya Kiyama, na yanayo kuwa ya kuiliwaza nafsi iliyo tua iliyo tanguliza mema wala isikiuke mipaka, na itavyo itwa iingie pamoja na walio kirimiwa miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu katika Pepo ya Mwenyezi Mungu.


بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

وَالْفَجْرِ ﴿١﴾

1. Naapa kwa Alfajiri.

وَلَيَالٍ عَشْرٍ ﴿٢﴾

2. Na (Naapa kwa) masiku kumi.

وَالشَّفْعِ وَالْوَتْرِ ﴿٣﴾

3. Na (Naapa kwa) shufwa na witri

وَاللَّيْلِ إِذَا يَسْرِ ﴿٤﴾

4. Na (Naapa kwa) usiku unapopita.

هَلْ فِي ذَٰلِكَ قَسَمٌ لِّذِي حِجْرٍ ﴿٥﴾

5. Je, hakuna katika hayo kiapo cha mwelekevu (akawa na taqwa)?

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِعَادٍ ﴿٦﴾

6. Je, hukuona vipi Rabb (Mola) wako Alivyowafanya kina ‘Aad?

إِرَمَ ذَاتِ الْعِمَادِ ﴿٧﴾

7. Wa Iram (waliokuwa warefu) wenye majumba marefu (kama) nguzo?

الَّتِي لَمْ يُخْلَقْ مِثْلُهَا فِي الْبِلَادِ ﴿٨﴾

8. Ambao hawakuumbwa mfano wao katika nchi.

وَثَمُودَ الَّذِينَ جَابُوا الصَّخْرَ بِالْوَادِ ﴿٩﴾

9. Na kina Thamuwd ambao wamechonga majabali (miamba) mabondeni.

وَفِرْعَوْنَ ذِي الْأَوْتَادِ ﴿١٠﴾

10. Na Fir’awn wenye vigingi.

الَّذِينَ طَغَوْا فِي الْبِلَادِ ﴿١١﴾

11. Ambao wamevuka mipaka (kumuasi Allaah) katika nchi.

فَأَكْثَرُوا فِيهَا الْفَسَادَ ﴿١٢﴾

12. Wakakithirisha humo ufisadi.

فَصَبَّ عَلَيْهِمْ رَبُّكَ سَوْطَ عَذَابٍ ﴿١٣﴾

13. Rabb (Mola) wako Akawamwagia mjeledi wa adhabu.

إِنَّ رَبَّكَ لَبِالْمِرْصَادِ ﴿١٤﴾

14. Hakika Rabb (Mola) wako bila shaka Yuko katika kuchunga (na kuwavizia).

فَأَمَّا الْإِنسَانُ إِذَا مَا ابْتَلَاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَنِ ﴿١٥﴾

15. Basi insani pale Rabb (Mola) wake Anapomtia mtihanini, Akamkirimisha na Akamneemesha, husema: “Rabb wangu Amenikirimu.”

وَأَمَّا إِذَا مَا ابْتَلَاهُ فَقَدَرَ عَلَيْهِ رِزْقَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَهَانَنِ ﴿١٦﴾

16. Ama Anapomtia mtihanini, Akamkadiria (Akamdhikishia) riziki yake, husema: “Rabb (Mola) wangu Amenidhalilisha.”

كَلَّا ۖ بَل لَّا تُكْرِمُونَ الْيَتِيمَ ﴿١٧﴾

17. Sivyo hivyo! Bali hamuwakirimu mayatima.

وَلَا تَحَاضُّونَ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ ﴿١٨﴾

18. Na wala hamuhimizani kulisha maskini.

وَتَأْكُلُونَ التُّرَاثَ أَكْلًا لَّمًّا ﴿١٩﴾

19. Na mnakula urithi kwa ulaji kamilifu.

وَتُحِبُّونَ الْمَالَ حُبًّا جَمًّا ﴿٢٠﴾

20. Na mnapenda mali mapenzi makuuu mno.


كَلَّا إِذَا دُكَّتِ الْأَرْضُ دَكًّا دَكًّا ﴿٢١﴾

21. Sivyo hivyo! (Kumbukeni pale) Ardhi itakapovunjwavunjwa.

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا ﴿٢٢﴾

22. Na Atakapokuja Rabb (Mola) wako, na Malaika safusafu.

وَجِيءَ يَوْمَئِذٍ بِجَهَنَّمَ ۚ يَوْمَئِذٍ يَتَذَكَّرُ الْإِنسَانُ وَأَنَّىٰ لَهُ الذِّكْرَىٰ ﴿٢٣﴾

23. Na utaletwa siku hiyo (Moto wa) Jahannam; siku hiyo insani atakumbuka, lakini wapi atapata ukumbusho?

يَقُولُ يَا لَيْتَنِي قَدَّمْتُ لِحَيَاتِي ﴿٢٤﴾

24. Atasema: “Laiti ningelikadimisha (mazuri) kwa ajili ya uhai wangu (nilipokuwa duniani)”. 

فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُعَذِّبُ عَذَابَهُ أَحَدٌ ﴿٢٥﴾

25. Basi siku hiyo hakuna yeyote atakayeadhibu kama adhabu Yake.

وَلَا يُوثِقُ وَثَاقَهُ أَحَدٌ ﴿٢٦﴾

26. Na wala hakuna yeyote atakayefungisha kama kufungisha Kwake.

يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ ﴿٢٧﴾

27. (Itasemwa) “Ee nafsi iliyotua.

ارْجِعِي إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً ﴿٢٨﴾

28. “Rejea kwa Rabb (Mola) wako (hali) umeridhika na umemridhisha.

فَادْخُلِي فِي عِبَادِي ﴿٢٩﴾

29. “Basi ingia katika (kundi la) waja Wangu.

وَادْخُلِي جَنَّتِي ﴿٣٠﴾

30. “Na ingia (kwenye) Jannah Yangu.”





Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com