013 - Hadiyth Ya 13: Atakayepitiwa Na Usingizi Bila Ya Kusoma Nyiradi Zake Alipize Kabla Ya Adhuhuri

013 - Hadiyth Ya 13: Atakayepitiwa Na Usingizi Bila Ya Kusoma Nyiradi Zake Alipize Kabla Ya Adhuhuri


عَنْ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه)  يَقُولُ:  قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((مَنْ نَامَ عَنْ حِزْبِهِ أَوْ عَنْ شَيْءٍ مِنْهُ فَقَرَأَهُ فِيمَا بَيْنَ صَلاَةِ الْفَجْرِ وَصَلاَةِ الظُّهْرِ كُتِبَ لَهُ كَأَنَّمَا قَرَأَهُ مِنْ اللَّيْلِ)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab(رضي الله عنه)  amesema: Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Atakayelala na kupitiwa na hizbu yake [nyiradi zake] au chochote kutoka humo kisha akaisoma baina ya Swalaah ya Alfajiri na Swalaah ya Adhuhuri, ataandikiwa kama kwamba ameisoma usiku)).[1]
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Umuhimu wa Muislamu kuhifadhi na kuendeleza nyiradi zake kila siku.
 
  1. Anayepitwa na nyiradi zake, akimbilie kuzisoma nyakati zilotajwa katika Hadiyth ili apate fadhila zake kamilifu [Al-Furqaan 25: 62].
 
 
وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ خِلْفَةً لِّمَنْ أَرَادَ أَن يَذَّكَّرَ أَوْ أَرَادَ شُكُورًا
Naye Ndiye Aliyejaalia usiku na mchana ufuatane (kubadilika usiku kuingia mchana, na mchana kuingia usiku) kwa atakaye kudhukuru (kumkumbuka na kumtaja Allaah) au atakaye kushukuru[2]
 
  1. Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja Wake kuwalipa thawabu wakati wanaposhindwa kupata wasaa au wanapokalifika na jambo kama ugonjwa n.k. [Al-Baqarah 2: 286] [Hadiyth: Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه)  kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Allaah Akimjaribu mja Muislamu kwa kumpa mtihani katika mwili wake, Humwambia Malaika: ‘Mwandikie ‘amali zake njema alizokuwa akizitenda’. Akimpa shifaa [Akimponyesha] Humwosha na kumtoharisha, na Akichukua roho yake, Humghufuria na Akamrehemu)).[3]
 
  1. Asiitegemee mtu Hadiyth hii kwa kutokujihimiza kuamka usiku kufanya ‘Ibaadah, bali ajitahidi kila njia kujiwezesha kuamka kupata fadhila za Tahajjud pia (Kuamka usiku kwa ajili ya kuswali). [As-Sajdah 32: 16-17, Al-Israa 17: 79, Adh-Dhaariyaat 51: 15-18, Al-Muzzammil 73: 2-8].
 
  1. Kuna fadhila tukufu za nyiradi na ‘amali za usiku, hivyo inatakiwa mja ajipinde katika kuzitekeleza.
 
  1. Kuchuma fadhila za nyakati baina ya Alfajiri na Adhuhuri kwa kuleta nyiradi alizokosa mja yeyote yule.
 
 



[1]  Muslim.
[2]  Al-Furqaan (26: 62).
[3]  Ahmad katika Musnad na amesema Al-Albaaniy: Hasan Swahiyh.