003 - Hadiyth Ya 3: Allaah Akimtakia Kheri Mja Humpa Mtihani Duniani

003 - Hadiyth Ya 3: Allaah Akimtakia Kheri Mja Humpa Mtihani Duniani


عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((إِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الْخَيْرَا عَجَّلَ لَهُ الْعُقُوبَةَ فِي الدُّنْيَا وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الشَّرَّ أَمْسَكَ عَنْهُ بِذَنْبِهِ حَتَّى يُوَافِيَ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) وَ قال النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((إِنَّ عِظَمَ الْجَزَاءِ مَعَ عِظَمِ الْبلآءِ وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا أَحَبَّ قَوْمًا ابْتَلاَهُمْ فَمَنْ رَضِيَ فَلَهُ الرِّضَا وَمَنْ سَخِطَ فَلَهُ السَّخَطُ)) رواه الترمذي وقال حديث حسن
Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه)  amesema: Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Allaah Anapompendelea mja Wake kheri, Humharakishia adhabu duniani. Na Allaah Anapomtakia mja Wake shari, Humzuilia dhambi zake mpaka Amlipe Siku ya Qiyaamah)). Na amesema Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtihani mkubwa, na hakika Allaah Anapowapenda watu Huwapa mtihani. Basi atakayeridhika, atapata Radhi [za Allaah] na atakayechukia, atapata hasira. [za Allaah]))[1]
Mafunzo Na Hidaaya: 
  1. Allaah (سبحانه وتعالى) Huwa pamoja na anayesibiwa na mitihani akasubiri, na juu ya hivyo, ni alama ya mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى). [Aal-‘Imraan 3: 146, Al-Baqarah 2: 153, Al-Anfaal 8: 46].
  1. Alama za kufutiwa dhambi Muislamu anapokuwa na subra katika mitihani.
  1. Watu hupewa mitihani kulingana na taqwa na Iymaan zao.
  1. Mwenye kuwa na subra katika mitihani ndiye atakayepata kheri za Siku ya Qiyaamah na malipo mema kabisa, kinyume na atakayeshindwa kuwa na subra: 
إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ
((Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu))[2]
  1.  Muumin inampasa awe radhi kwa mitihani inayomfikia wala asikate tamaa au kuchukia bali ashukuru [Hadiyth: ((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lake ni kheri.  Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin, Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake, na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri, nayo ni kheri kwake))[3]
  1. Pepo si wepesi kuipata ila baada ya kuwa na taqwa, kutenda ‘amali njema na kuwa na subira katika mitihani. [Al-Baqarah 2: 214].
  1. Kuipita mitihani ni thibitisho kuwa mtu huyo yuwapendwa na Allaah (سبحانه وتعالى).


[1]  At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan.
[2]  Az-Zumar (39: 10).
[3]  Muslim.