Mus-ab bin 'Umayr: Mwakilishi wa kwanza katika Uislam
Wanahistoria wa
kiislam wanamsimulia Mus’ab kwamba alikuwa kijana mchangamfu mno na
mtanashati. Alizaliwa na kukulia katika utajiri, kudekezwa na wazazi na
kuwa kizungumzaji chao mabinti wa kikuraish wa Makka kwani alikuwa kijana wa
kuvutia na alijaaliwa kuwa na kila kitu ambacho mwanamke yeyote angelihitaji
toka kwa mwanamme.
Kijana huyu katika pitapita
zake mjini Makka alisikia habari za Muhammad alietumwa na Mwenyezi Mungu
kuwabashiria bishara njema na kuwalingania watu kumwabudu Mungu mmoja.
Uvumi huu wa ujio wa Mtume uliukumba mji wa Makka na Mus’ab alikuwa akisikiliza
sana habari zake na ingawa bado alikuwa mdogo lakini tayari alikuwa ni kijana
mwenye hekima na busara.
Baada ya kuifuatilia
vizuri habari hii alijiunga na wenzake usiku mmoja kwenda kwenye nyumba ya al-
Arqam kusikiliza kulikoni hasa! Alimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu akiwafundisha
waislam Quran na kusali na kwa kuwa hekima na busara zilikuwa tayari sifa zake,
alipozisikia aya za Quran zikisomwa moyo wake uliingiwa na utulivu ambao
haujawahi kumfikia na hapo hapo kutamka “Laa Ilaha ill allah, Muhammad rasuulu
llah”
Mama yake Mus’ab,
Khunaas bint Maalik, alikuwa na haiba kubwa mbele ya Maquraysh wa Makka kufika
hadi kuogopewa. Mus’ab alijitahidi kuficha imani yake akichelea ukali wa
mama yake, huku akiendelea kwenda kwa al-Arqam kujifunza zaidi kutoka kwa Mtume
Muhammad (SAW).
Siri hii haikuchukua
muda kwani baadhi ya watu waliokuwa wakimuona Mus’ab akienda nyumba ya al-Arqam
walimwambia mama yake Khunaas ambaye alishtushwa sana kusikia kwamba mwanawe
amesilimu. Zilimshtusha sana habari hizi kwani alichelea ghadhabu zitakazomfikia
yeye na familia yake kutoka kwa miungu yao ya masanamu waliyokuwa wakiabudu,
pia aliangalia nafasi yake mbele ya Maquraish wa Makka kama mwanamke mweye
heshima na haiba sasa itakuwaje na mwanawe tayari ameshamuasi na kuwa muislam.
Alichokifanya ni
kumpiga mwanawe kipigo cha hasira huku akimtaka aachane kabisa na dini ya
Muhammad na kurudi kwa Latta, Uzza na Manat (waungu waliokuwa wakiwaabudu
Maquraysh). Mus’ab hakutetereka na kipigo wala mateso aliyoyapata na
alibaki katika msimamo wake wa haki. Kilichomsaidia ni mama yake
kumhurumia mwanawe kwa kumwona katika hali mbaya. Huruma hii ya mama,
ilichomsaidia ni kuepukana na kipigo tu ila badala yake alifungwa kwa
minyonyoro kwenye chumba kichafu ndani ya nyumba yao na kufungiwa humo.
Katika hali ya
upweke, kifungo na adhabu aliyokuwa akiipata Mus’ab kwa kuamini kwamba hakuna
Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na Muhammad kuwa ni mjumbe
wake, alisikia habari za Hijra ya baadhi ya waislam kuelekea Habashah,
Ethiopia. Kwa uwezo wake Sub-hana aliweza kupenya kwa kuwatoroka walinzi na
kuungana na msafara ulioelekea Habashah katika hijra ya kwanza. Na kwa
ushauri wa Alhabib Mustafa (SAW) alifanya hijra ya mara ya pili kwenda Habashah
pamoja na Waislam.
Hijra mbili hizi
zilizidi kujenga imani ya Mus’ab ya kuwa tayari kuyatoa muhanga maisha yake
aliyokuwa akiishi kwa ajili ya Allah (SW). Siku moja alikuja kwa Bwana
Mtume (SAW) na baadhi ya masahaba walikuwa wamekaa naye, jinsi walivyomuona
hali yake dhaifu na matambara aliyokuwa amevaa, baadhi ya masahaba waliinamisha
nyuso zao na kuanza kutokwa na machozi wakimkumbuka Mus’ab mtanashati mwenye
kuvaa nguo za kifahari. Mtume (SAW) alipomuona Mus’ab alimtazama kwa
jicho la hekima huku akitabasamu na kusema, “Mus’ab hapa na hakuna kijana
yeyote Makka aliekuwa akipendwa na kudekezwa na wazazi wake kushinda yeye,
kisha aliachana nayo yote hayo kwa ajili ya mapenzi ya Allah na Mtume wake”.
Mama yake kuona
mwanawe hajatetereka bali imani yake ilizidi kuimarika kila kukicha, aliamua
kumkatia huduma zote na kumwacha hohe hahe. Na pale alipokusudia
kumfungia kwa mara ya pili aliporudi Habashah, Mus’ab alimwahidi mama yake
kwamba akiwa atathubutu kufanya hivyo basi atamuua kila yule
atakayemkaribia. Mus’ab hakuwa akikaidi amri ya mzazi wake bali alikuwa
akifuatia ile kauli, “Hakuna kumtii muumbwa katika jambo litakalomuasi
muumba” Mama yake alilia sana kuona Mus’ab mwanawe wa kumzaa anamuendea kinyume
na kumuaibisha na kumwambia, “Nenda uendako kuanzia leo mimi si mama yako”.
Alichofanya Mus’ab ni kumkaribia mama yake na kumtaka aingie katika Uislam na
atamke shahada. Mama yake alikasirika na kujibu, “Nnaapa kwa nyota
kamwe sitoingia katika dini yako nisije nikadhalilisha heshima yangu na kukosa
sehemu ya kuweka uso wangu”.
Tokea siku hiyo
aliachana na mama yake na maisha yake kubadilika kwa kuwa katika hali ya ngumu
hata kula yake ilikuwa ya taabu na nguo zake ni matambara ingawa hakuwa kipenzi
tena wa Maquraish kwa hali yake hii lakini alikuwa kipenzi cha Mtume (SAW).
Katika hali yake hii
ndipo pale Mtume (SAW) alipomkabidhi jukumu kubwa katika maisha yake pale
alipomchagua kuwa mwanaharakati na balozi wa kwanza wa Mtume katika mji wa
Madina. Kazi aliyoagizwa kufanya ni kuulingania Uislam na kuwaita watu
wengine kuja katika dini ya Allah (SW), na pia kuiandaa Madina kwa ajili ya
Hijra kubwa itakayofuata.
Miongoni mwa waislamu
waliokuwapo palikuwa na wakubwa wa umri, walio karibu zaidi kwa Mtume. Lakini
Mtume (SAW) alimchagua Mus’ab.
Naam! , Mus’ab
aliitekeleza kazi yake ipasavyo kwani alipofika Madina kulikuwa na waislam kumi
na wawili tu lakini miezi michache baadaye, waislam wa Madina walituma ujumbe
wa watu 70 kike na kiume kwenda kwa Mtume akiwemo Maalim wao Mus’ab .
Fikiria hali halisi ya daawah katika mazingira ya kijahiliya na kazi aliyoweza
kuifanya Mus’ab Madina ilikuwa ni ya kupigiwa mfano na kuthibitisha kwamba
uchaguzi wa Mtume (SAW) haukuwa wa kubahatisha.
Siku, miezi na miaka
ikapita Mtume (SAW) na masahaba wakahamia Madina, Maquraysh bado walikuwa na
hasira za kutisha kwa waislam na vita vya Badr kutokea ambapo makafiri
walishindwa vibaya, na baada ya kushindwa wakapanga mipango yao ya kulipiza
kisasi na hatimaye kupiganwa vita vya Uhud. Katika vita hivi Mtume alimteua
Mus’ab kuwa mshika bendera, Mus’ab alikubali jukumu hili kwa moyo mkunjufu na
kwa heshima kubwa kwani kufikia hadi ya kukabidhiwa bendera imeonesha ni jinsi
gani Mtume (SAW) alivyokuwa na imani naye. Naam! Mus’ab aliongoza jeshi
la waislamu kwa kuhakikisha kwamba bendera ya “Laa Ilaha Ill Allah” inasimama
wakati wote.
Vita viliendelea na
waislam kuwapiga na kuwazidi nguvu makafiri hadi ikabidi warudi nyuma na kuanza
kukimbia. Kuona hivyo wale waislam mastadi wa kurusha mishale waliowekwa
na Mtume (SAW) milimani kuweka kinga kwa maadui wakaanza kuteremka wakidhani
kwamba vita vimekwisha na waislam kushinda.
Tendo hili
walilolifanya bila ya ushauri wa Amiri jeshi mkuu wa waislam, Mtume (SAW) ndilo
lililogeuza ule ushindi uliokuwa ukinukia kwa waislam kuwa kipigo cha ghafla na
kuuwawa kwa waislamu wengi.
Wakati mtafaruku na
vurugu mechi hii inatokea lengo kubwa na makafiri lilikuwa kumuuwa Mtume wa
Allah (SW). Mus’ab aliliona hili na kujua njama yao na hapa alizidi
kuisimamisha bendera juu na kusema “Allahu Akbar” na kama simba aliejeruhiwa,
alinguruma na kuanza kupigana huku na kule, kubwa alilolikusudia Mus’ab ni
kuwashughulisha Makafiri kumfuata yeye badala ya Mtume wa Allah (SW).
Naam! Mus’ab alikuwa peke yake lakini kama ni jeshi zima kwani akiwa na bendera
mkono mmoja na upanga mkono mwengine aliendelea kupambana na makafiri ambayo
tayari walianza kumzidi nguvu.
Mmoja katika Masahaba
waliopigana vita vya Uhudi anasimulia jinsi shujaa Mus’ab alivyoweza kupambana
na maadui wa uislam kwa dhati na nguvu zake zote. Ibn Saad amesema;
Ibrahim bin Muhammad alisimulia kutoka kwa baba yake ambaye alisema, “Mus’ab
alibeba bendera siku ya vita vya Uhud pale ambapo waislamu walipoingiwa na
kiwewe na mtafaruku akapigana mpaka alipokabiliana na kafiri Ibn Qum’uah,
askari farasi na kukatwa mkono wa kulia .
Kuona hivyo
Mus’ab hakuitupa wala kumtoka ile bendera ya kiislam. Ilisimama huku
akiibeba kwa mkono wake wa kushoto huku akisema kwa sauti kubwa kuwaambia
makafiri “Hakuwa Muhammad ila ni Mtume wa Allah, na Mitume walikuja na kupita
kabla yake”. Ibn Qumuah akamkata Mus’ab mkono wake wa kushoto, Mus’ab
akiwa tayari keshakatwa mikono yote miwili aliendelea kukamata bendera kwa ile
sehemu tu ya mkono iliyobakia na kuigandanisha na kifua chake huku damu
zikichuruzika na kuendelea na kauli yake, “Hakuwa Muhammad ila ni Mtume wa
Allah, na Mitume walikuja na kupita kabla yake” . Akaja kafiri mwengine na
kumchoma Mus’ab mkuki uliomwangusha chini akidondoka pamoja na bendera.
Nyota ya
mashujaa imeanguka. Mus’ab alipigana vita hivi kwa ajili ya Allah (SW), vita
ambavyo alipigana vilikuwa mtihani mkubwa kwa waislam, mtihani wa kujitolea
muhanga na mtihani wa imani. Kilichokuwa moyoni mwa Mus’ab ni kwamba
akianguka, basi makafiri watamfikia Mtume (SAW) na kumuuwa, kwani asingekuwa na
kinga wala himaya, akapatwa na woga (kuuwawa kwa Mtume na mapenzi ya Mtume) na
hadi anachomwa mkuki na kudondoka bado alikuwa akirudia ile kauli yake “Hakuwa
Muhammad isipokuwa ni Mtume, na Mitume walikuja na kupita kabla yake”.
Kwa heshima kauli hii
baadaye ilikuja kuteremka kwa Quran kama ilivyo katika Surat Al Imraan/144
“ Na Muhammad
hakuwa ila ni Mtume tu wamekwisha kupita kabla yake mitume. Je akifa au kuuwawa
ndiyo mtageuka mrudi nyuma ?……..”
Baada ya kumalizika
vita masahaba waliuona mwili wa Mus’ab uko kifudifudi labda kwa kuogopa kuona
madhara yatakayompata Mtume wa Allah au kuona haya kufa shahidi kabla ya
kuhakikisha usalama wa Mtume (SAW). Mtume (SAW) pamoja na masahaba wake
walikuwa wakipita kukagua majeruhi na kuwaaga mashahidi na alipofika ulipo
kuwepo mwili wa Mus’ab alisita na kuanza kutokwa na machozi.
Amesema Khabbab
ibn Al-Aratt kwamba, “Tulifanya Hijra pamoja na Mtume kwa ajili ya Allah
(SW). Baadhi tu walifariki hata kabla ya kufaidi matunda ya Hijra na malipo
yake, miongoni mwao ni Mus’ab hakuacha kitu chochote pale alipokufa shahidi
isipokuwa tambara tu alilokuwa akivaa. Wakati tunamkafini kwa tambara
hili lilikuwa halimtoshi kwani tukimfunika kwenye miguu uso wake unakuwa wazi
na tukimfunika usoni miguu inaonekana! Mtume (SAW) akasema , “Mfunikeni
kwenye uso na sehemu itakayobaki muwekeeni majani kwenye miguu”.
Mtume (SAW) alisimama
na kuuangalia mwili wa Mus’ab huku machozi yakimtoka na kusoma,
“Miongoni mwa waumini
wapo watu ambao wametimiza yale waliyoahidiana na Allah (SW) juu yake . Baadhi
yao wamekwisha kufa na baadhi yao wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata
kidogo” Suuratul Ahzaab / 23
Akiangalia
tambara alilopambiwa Mus’ab, Mtume (SAW) alisikitika sana na kusema, “nilikuwa
nikukuona Makka ulikuwa kipenzi na kivutio kuliko vijana wote leo hii uko hapa
na tambara tu!” Kisha Mtume (SAW) akautazama uwanja wa vita jinsi
ulivyojaa mashahidi na kusema “Mtume wa Allah (SW) anashuhudia kwamba nyinyi ni
mashahidi wa Allah siku ya kiama”