Al-Jinn (72)

سُورَةُ  الْجِنّ
Al-Jinn (72)
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

قُلْ أُوحِيَ إِلَيَّ أَنَّهُ اسْتَمَعَ نَفَرٌ مِّنَ الْجِنِّ فَقَالُوا إِنَّا سَمِعْنَا قُرْآنًا عَجَبًا ﴿١﴾

1. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Nimeletewa Wahy kwamba kundi la majini lilisikiliza; likasema: ‘Hakika sisi tumeisikia Qur-aan ya ajabu.

يَهْدِي إِلَى الرُّشْدِ فَآمَنَّا بِهِ ۖ وَلَن نُّشْرِكَ بِرَبِّنَا أَحَدًا ﴿٢﴾

2. ‘Inaongoza kwenye uongofu, basi tukaiamini, na wala hatutomshirikisha Rabb (Mola) wetu na yeyote.

وَأَنَّهُ تَعَالَىٰ جَدُّ رَبِّنَا مَا اتَّخَذَ صَاحِبَةً وَلَا وَلَدًا ﴿٣﴾

3. ‘Na (inafunza) kwamba umetukuka kabisa Utukufu wa Rabb (Mola) wetu, Hakujifanyia mke wala waladi.

وَأَنَّهُ كَانَ يَقُولُ سَفِيهُنَا عَلَى اللَّـهِ شَطَطًا ﴿٤﴾

4. ‘Na kwamba safihi miongoni mwetu alikuwa akisema juu ya Allaah uongo uliopinduka mipaka.

وَأَنَّا ظَنَنَّا أَن لَّن تَقُولَ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا ﴿٥﴾

5. ‘Na kwamba sisi tulidhania wanadamu na majini hawatosema uongo juu ya Allaah.

وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا ﴿٦﴾

6. ‘Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wanadamu wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia mzigo (wa madhambi na kufru).

وَأَنَّهُمْ ظَنُّوا كَمَا ظَنَنتُمْ أَن لَّن يَبْعَثَ اللَّـهُ أَحَدًا ﴿٧﴾

7. ‘Na kwamba wao (pia) walidhania kama mlivyodhani kwamba Allaah Hatomtuma yeyote (kuwa Rasuli).

وَأَنَّا لَمَسْنَا السَّمَاءَ فَوَجَدْنَاهَا مُلِئَتْ حَرَسًا شَدِيدًا وَشُهُبًا ﴿٨﴾

8. ‘Na kwamba sisi (tulitafuta kuzifikia na) kuzigusa mbingu, basi tukazikuta zimejaa walinzi wakali na vimondo.

وَأَنَّا كُنَّا نَقْعُدُ مِنْهَا مَقَاعِدَ لِلسَّمْعِ ۖ فَمَن يَسْتَمِعِ الْآنَ يَجِدْ لَهُ شِهَابًا رَّصَدًا ﴿٩﴾

9. ‘Na kwamba sisi tulikuwa tukikaa huko vikao kwa ajili ya kusikiliza, basi atakayesikiliza sasa atakuta kimondo kinamvizia.

وَأَنَّا لَا نَدْرِي أَشَرٌّ أُرِيدَ بِمَن فِي الْأَرْضِ أَمْ أَرَادَ بِهِمْ رَبُّهُمْ رَشَدًا ﴿١٠﴾

10. ‘Na kwamba sisi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanaokaa ardhini, au Rabb (Mola) wao Anawatakia uongofu.

وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ كُنَّا طَرَائِقَ قِدَدًا ﴿١١﴾

11. ‘Na kwamba miongoni mwetu (wako walio) wema, na miongoni mwetu (wako walio) kinyume chake; tumekuwa njia za mbali mbali.

وَأَنَّا ظَنَنَّا أَن لَّن نُّعْجِزَ اللَّـهَ فِي الْأَرْضِ وَلَن نُّعْجِزَهُ هَرَبًا ﴿١٢﴾

12. ‘Na kwamba tulikuwa na yakini kwamba hatutoweza kumshinda Allaah ardhini, na wala hatutoweza kumkwepa (adhabu Yake kwa) kutoroka.

وَأَنَّا لَمَّا سَمِعْنَا الْهُدَىٰ آمَنَّا بِهِ ۖ فَمَن يُؤْمِن بِرَبِّهِ فَلَا يَخَافُ بَخْسًا وَلَا رَهَقًا ﴿١٣﴾

13. ‘Na kwamba sisi tuliposikia mwongozo tukaiamini; basi atakayemuamini Rabb (Mola) wake hatoogopa kupunjwa (mazuri yake) na wala kuzidishiwa (dhambi).

وَأَنَّا مِنَّا الْمُسْلِمُونَ وَمِنَّا الْقَاسِطُونَ ۖ فَمَنْ أَسْلَمَ فَأُولَـٰئِكَ تَحَرَّوْا رَشَدًا ﴿١٤﴾

14. ‘Na kwamba miongoni mwetu (wako walio) Waislamu, na miongoni mwetu (wako walio) wanaopotoa haki; hivyo atakayesilimu, hao ndio waliofuata uongofu.”

وَأَمَّا الْقَاسِطُونَ فَكَانُوا لِجَهَنَّمَ حَطَبًا ﴿١٥﴾

15. Ama (wale) waliopotoa haki, watakuwa kuni za Jahannam.

وَأَن لَّوِ اسْتَقَامُوا عَلَى الطَّرِيقَةِ لَأَسْقَيْنَاهُم مَّاءً غَدَقًا ﴿١٦﴾

16. Na kwamba lau wangelinyooka kwenye njia, bila shaka Tungeliwanywesha maji kwa wingi.

لِّنَفْتِنَهُمْ فِيهِ ۚ وَمَن يُعْرِضْ عَن ذِكْرِ رَبِّهِ يَسْلُكْهُ عَذَابًا صَعَدًا ﴿١٧﴾

17. Ili tuwatie katika mtihani kwayo. Na anayepuuza dhikri (ukumbusho, mawaidha na Qur aan) ya Rabb (Mola) wake, Atamsukuma kwenye adhabu (kali) inayozidi.

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا ﴿١٨﴾

18. Na kwamba Misikiti ni (kwa ajili) ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.

وَأَنَّهُ لَمَّا قَامَ عَبْدُ اللَّـهِ يَدْعُوهُ كَادُوا يَكُونُونَ عَلَيْهِ لِبَدًا ﴿١٩﴾

19. Na kwamba mja wa Allaah (Nabii Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) aliposimama kumwomba (Rabb wake), walikaribia kumzonga.

قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا ﴿٢٠﴾

20. Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi namuomba Rabb (Mola) wangu (Pekee), na wala simshirikishi na yeyote.”

قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا ﴿٢١﴾

21. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu.”

قُلْ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ اللَّـهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا ﴿٢٢﴾

22. Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika hakuna yeyote awezaye kunilinda na Allaah (ikiwa nitamuasi), na wala sitoweza kupata  mahali pa kukimbilia.

إِلَّا بَلَاغًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِسَالَاتِهِ ۚ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ﴿٢٣﴾

23. “Isipokuwa (linalonipasa kwenu ni) ubalighisho kutoka kwa Allaah, na Risala Zake.” Na yeyote yule atakayemwasi Allaah na Rasuli Wake, basi hakika atapata Moto wa Jahannam ni wenye kudumu humo abadi.”

حَتَّىٰ إِذَا رَأَوْا مَا يُوعَدُونَ فَسَيَعْلَمُونَ مَنْ أَضْعَفُ نَاصِرًا وَأَقَلُّ عَدَدًا ﴿٢٤﴾

24. (Makafiri wataendelea na kufuru zao) Mpaka watakapoona yale waliyoahidiwa, basi watajua ni nani msaidizi dhaifu, na mchache zaidi kwa idadi.

قُلْ إِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ مَّا تُوعَدُونَ أَمْ يَجْعَلُ لَهُ رَبِّي أَمَدًا ﴿٢٥﴾

25. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم):  “Mimi sijui kama yapo karibu hayo mnayoahidiwa, au Rabb (Mola) wangu Atayaweka muda mrefu.”

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾

26. Aalimu (Mjuzi) wa ghayb na wala Hamdhihirishii yeyote ghayb Yake.

إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ فَإِنَّهُ يَسْلُكُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ رَصَدًا ﴿٢٧﴾

27. “Isipokuwa yule Aliyemridhia miongoni mwa Rasuli basi hakika Yeye Anamwekea mlinzi mbele yake na nyuma yake.


لِّيَعْلَمَ أَن قَدْ أَبْلَغُوا رِسَالَاتِ رَبِّهِمْ وَأَحَاطَ بِمَا لَدَيْهِمْ وَأَحْصَىٰ كُلَّ شَيْءٍ عَدَدًا ﴿٢٨﴾

28. Ili Ajue kwamba (wao) wamekwishafikisha Risala za Rabb (Mola) wao; na Ameyazunguka (kwa ujuzi Wake) yale waliyo nayo, na Amedhibiti barabara idadi ya kila kitu.





Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com